Rudi nyuma Yaliyomo endelea

Kwa upande mwingine nimekuta kwamba Ahlus-Sunna Wal-Jamaa, Maimamu wao ni Wafursi, kwa kuwa idadi kubwa ya Maimam wao ni Wafursi kama vile Abu Hanifa, Imamun-Nasai, Tirmidhi, Bukhari, Muslim, Ibn Majah, Razi, Imam Ghazali, Ibn Sina na Al-Faarabi na wengineo wengi ambao nafasi haitoshi kuwataja wote. Sasa basi ikiwa Mashia Wafursi wanampinga Umar ibn Khatab eti kwa sababu aliwabomoa wakubwa wao, ni kwa nini basi Mashia Waarabu na wengine wasiokuwa Wafursi nao wanampinga Umar? Madai haya hayana msingi, bali kilichopo ni kwamba upinzani wa Mashia kwa Umar unatokana na jinsi Umar mwenyewe alivyoshiriki kumtenga mbali Amirul-Muuminina na Bwana wa mawasii Ali ibn Abi Talib kutoka kwenye nafasi ya Ukhalifa baada ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu jambo ambalo lilisababisha fitina na mitihani na kulegalega na hatimaye kuporomoka kwa umma huu. Inatosha kabisa kwa yeyote yule anayefanya utafiti kwa uhuru kumuondoshea utata na kumfunulia ukweli wa mambo kiasi kwamba atakuwa mpinzani wa Umar bila ya kuwepo uadui

204

hapo kabla baina yake na Umar.

Na ukweli ni kuwa, Mashia wakiwa ni Wafursi au Waarabu au wasiokuwa mataifa haya mawili, bila shaka ni wanyenyekevu na wenye kufuata maandiko ya Qur'an na maandiko ya hadithi za Mtume, na wamemfuata kiongozi wa uongofu na wanawe ambao ni taa zinazoondosha giza, na hawakumridhia mwingine asiyekuwa hawa, licha ya ile siasa ya Banu Umayyah iliyoambata na vivutio na vitisho, (siasa ambayo pia) ilifuatwa na watawala wa kibani Abbas kwa muda wa karne saba na ndani ya kipindi hiki chote (watawala) hawa waliwafuatilia Mashia katika kila kona na kila mji wakawauwa na kuwatawanya, wakawanyima haki yao na kufuta athari zao. Kisha wakaeneza kila upande uzushi na madai ya uongo (dhidi ya Mashia) ambayo yatawafanya watu wawatenge na hali hii imeendelea kubaki hadi leo.

Lakini Mashia wamekuwa madhubuti na imara kabisa, na wenye subira, wameshikamana na haki, haiwaogopeshi lawama ya mwenye kulaumu (kwa kila walitendalo) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na mpaka leo hii wanatetea msimamo huu, nami kwa upande wangu natoa changamoto kwa Mwanachuoni yeyote miongoni mwa wanachuoni wetu kwamba afanye kikao na mwanachuoni wa Mashia ajadiliane naye, basi kamwe hatatoka kwenye kikao hicho isipokuwa atauona uongofu walionao (Mashia).

Naam nimepata badala (ya kile nilichokuwa nacho) namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba ameniongoza kwenye uongofu huu, kwani nisingeongoka lau yeye Mwenyezi Mungu asingeniongoa.

Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu na ninamshukum kwa kunionesha lile kundi lenye kuokoka ambalo nilikuwa nalitafuta kwa hamu kubwa na hapakubakia shaka yoyote kwangu kwamba, yeyote mwenye kushikamana na Imam Ali

205

na watu wa nyumba ya Mtume, huwa ameshika kishiko chenye nguvu kisichovunjika, na maneno ya Mtume juu ya hilo (la kushikamana na watu wa nyumba yake) ni mengi, ambapo Waislamu wote wamekubaliana, na akili peke yake ni dalili iliyobora kwa mwenye kutega sikio hali yakuwa yuhadhiri. Ali alikuwa ni mjuzi mno kuliko Sahaba wote na alikuwa shujaa wao bila kupingwa na hili nalo ni kwa makubaliano ya umma (wa Kiislamu), na hili peke yake linatosha kuwa dalili ya kustahiki kwake Ukhalifa kuliko mtu mwingine.

Mwenyezi Mungu amesema: "Nabii wao akawaambia, hakika Mwenyezi Mungu amekuleteeni Talut awe Mfalme (wenu) wao wakasema, itakuwaje awe mfalme wetu wakati sisi ni wenye haki mno kwa ufalme kuliko yeye na hakupewa wasaa wa mali. (Yule Nabii) akasema, bila shaka Mwenyezi Mungu amemchagua juu yenu na akamzidishia wasaa wa elimu na mwili, naye Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake yule

amtakaye na Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa na ni mjuzi". (Qur. 2:247)

Naye Mjumbe wa Mwenyezi Mungu amesema "Hapana shaka Ali anatokana nami, na mimi natokana naye, na yeye ndiye msimamizi wa mambo ya kila Muumini baada yangu".

Taz: (1) Sahih Tirmidh Juz. 5 uk. 296

(2) Khasaisun-Nasai uk. 87

(3) Mustad-rak Al-Hakim Juz. 2 uk. 110

Naye Imam Zamakhshari amesema ndani ya beti zake:-

Mashaka na khitilafu vimezidi, na kila mmoja anadai yeye ndiye njia ya sawa, basi mimi (nilipoona hivyo) nikashikamana na Lailaha Illallah, napendo langu nikampa Ahmad na Ali. Mbwa alifuzu kwa kuwapenda watu wa pangoni (As-habu

Kahfi) vipi nitakuwa muovu kwa kuwapenda watu wa (kizazi cha) Mtume?

206

Naam, nimekwishapata badala (ya kile nilichokiamini zamani) namshukuru Mwenyezi Mungu na sasa baada ya Mtume ninamfuata Amirul-Muuminina na Bwana wa Mawasii na kiongozi wa watu wateule, simba wa Mwenyezi Mungu aliyemshindi Imam Ali Ibn Abi Talib, na kitulizo cha nafsi ya Mtume katika umma huu Imam Abu Muhammad Hasan Az-Zaki na Imam Abu Abdillah Husein na sehemu ya mwili wa Mustapha ambaye Mola Mtukufu hughadhibika pindi anapoghadhibika (naye) ni mwanamke bora kuliko wote Fatmah Az-Zahra.

Nimembadilisha Imam Malik kwa (kuwa pamoja na) Mwalimu wa Ummah Imam Jaafar As-Sadiq.

Na nikashikamana na Maimamu tisa wenye Isma wanaotokana na kizazi cha Husein (a.s.), hao ni Maimamu wa Waislamu na ni Mawalii wema wa Mwenyezi Mungu.

Nikabadili Masahaba (kutoka kwa wale) waliorudi nyuma kwa visigino vyao kama vile Muawiyah, Amr ibn Al-As, Abuhurairah, Ikrimah na Kaab Al-Ahbar na wengine, (nimewabadili hawa nikashikamana na) Masahaba wenye shukurani ambao hawakutengua ahadi waliyomuahidi Mtume (Masahaba hao ni) kama Ammar ibn Yasir, Sal-man Al-Farisi, Abud-Dhari Al-Ghifari, Miqdad ibn Al-As-wad, Khuzaimah ibn Thabit Dhus-Shahadatain, Ubay Ibn Kaab na wengineo. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa huku kuzindukana.

Nimebadilisha wanachuoni wa watu wangu arnbao walizigandisha akili zetu, na wengi wao wamekuwa wafuasi wa masultani na watawala wakati wote (nimebadilisha hawa) kwa (kushikamana na) wanachuoni wa Kishia waliowema ambao hawakuufunga mlango wa Ij-Tihadi na wala hawakudhalilika na kuwa wanyonge kwa watawala madhalimu.

Naam, nimebadilisha fikra zilizogandamana zenye upinzani usiyo na hoja madhubuti, fikra zinazoamini mambo

207

yanayopingana (nimebadilisha fikra hizi) kwa fikra zenye nuru na uhuru, zilizo wazi na zenye kuamini dalili, hoja na Bur-han.

Kama isemwavyo katika zama zetu hizi kwamba:

"Nimeukosha ubongo wangu" kutokana na uchafu ulioufunika (kwa kipindi cha miaka thelathini) na upotovu wa kibanu Umayyah, nikautakasa kwa itikadi ya (watu) wenye Ismah ambao Mwenyezi Mungu amewaondoshea uchafu na amewatakasa kwa tahara iliyokamilika na (nitabaki katika Aqida hii) katika uhai wangu uliobakia.

Ewe Mwenyezi Mungu tuweke hai ndani ya mila yao na utufishe katika Sunna yao, na utufufue pamoja nao, bila shaka Mtume wako (s.a.w.) amesema, "Mtu atafufuliwa pamoja na ampendaye".

Kwa yote haya ninakuwa nimerejea kwenye asili yangu, kwani baba yangu na ami zangu walikuwa wakitusimulia juu ya asili yao wanayoifahamu ya kuwa wanatokana na ukoo wa masharifu waliokimbia kutoka Iraq chini ya ukandamizaji wa utawala wa Banu Abbas na wakakimbilia Afrika ya Kaskazini wakaja hadi Tunis na athari zao zimebakia hadi leo.

Na huko Afrika ya Kaskazini wako watu wengi mfano wetu ambao wanaitwa masharifu kwa kuwa wanatokana na kizazi kitukufu (cha Mtume) lakini wamepotea ndani ya upotovu wa Banu Umayyah na Banu Abbas, hakuna uhakika wowote waliobakia nao isipokuwa hiyo heshima na cheo wanachovishwa na watu. Mimi namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uongofu wake (alionipa), namshukuru Mwenyezi Mungu kwa utambuzi (niliotambua) na kunifungua macho yangu na kuiona haki,

208

SABABU ZA UTAMBUZI

Ama sababu zilizonifanya kuubaini ukweli ni nyingi mno wala haiwezekani katika muda huu mfupi isipokuwa kutaja baadhi tu ya mifano miongoni mwake.

1. Maandiko yanayohusu Ukhalifa.

Bila shaka niliapa, wakati naingia ndani ya utafiti huu kwamba sitategemea isipokuwa kile kitu ambacho kimethibitishwa katika pande mbili na kukitupa kile ambacho upande mmoja umepwekeka, na kwa msingi huu nitatafiti ile fikra ya ubora uliopo baina ya Abubakr na Ali ibn Abi Talib na kwamba Ukhalifa lilikuwa ni tamko (la Mtume) lililomuashiria Ali kama wanavyodai Mashia, au (Ukhalifa) ulikuwa ni kwa misingi ya uchaguzi na mashauriano kama wanavyodai Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa.

Mtu yeyote anayefanya uchunguzi kuhusu maudhui hii atakapoweka juhudi zake kwa lengo la kupata ukweli, basi bila shaka atakuta maandiko yaliyowazi juu ya (Ukhalifa wa) Ali ibn Abi Talib, kama vile kauli ya Mtume (s.a.w.), "Yeyote ambaye mimi nilikuwa mtawala wa mambo yake, basi huyu hapa Ali ni mtawala wa mambo yake." Maneno haya aliyasema baada ya kutoka katika hija ya kuaga hadi yakafanywa maandamano ya watu kwenda kumpongeza Ali ibn Abi Talib na mpaka Abubakr mwenyewe na Umar walikuwa miongoni mwa watu waliompongeza Imam Ali wakasema, "Hongera ewe

209

mwana wa Abu Talib leo umekuwa mtawalia mambo kwa kila muumini wa kike na wa kiume". Taz: Musnad Imam Ahmad Ibn Hambal J. 4 uk. 281, Sirul-Alamimina cha Imam Ghazal uk. 12, Tadh-Kiratul-Khawas cha Ibn Al-Jauzi, Ar-Riyaz-Un-Nazrah cha Tabor i J. 2 uk. 169, Kanzul-Ummal J. 6 uk. 397, Al-Bidayah Wan-Nihayah cha Ibn Kathir J. 5 uk. 212, Tarikh IbnAsakirJ. 2uk. 50, Tafsir Ar-Razi J. 3 uk. 63, Al-Hawi Lil-Fatawi cha Suyut J. 1 uk. 112.

Tamko hili wamekubaliana Mashia na Masunni, nami sikuandika rejea yoyote ile kuhusu utafiti huu isipokuwa ni za Kisunni, pamoja na hayo sikuzitaja rejea zote kwani ni nyingi mno kuliko idadi niliyoitaja, lakini ili kuchunguza kwa undani zaidi na kwa ufafanuzi namuomba msomaji asome kitabu kiitwacho Al-Ghadir cha Mwanachuoni mkubwa aitwaye Al-Amini na kimechapishwa mijaladi kumi na tatu, ambapo mwandishi amekusanya ndani yake wapokezi wa hadithi hii kwa njia za Kisunni.

Amma ile ijmai (makubaliano) inayodaiwa (kufanyika na) kumchagua Abubakar siku ile ya Saqifa, kisha kumpa baia Msikitini bila shaka madai hayo hayana dalili kwani itakuwaje iwe ijmai wakati ambapo baia yake ilipingwa na Ali, Abbas na Banu Hashim wengine, kama ambavyo Usamah ibn Zaid, Zubair, Sal-man Al-Farisi, Abudhari Al-Ghifari, Miqdad ibn Al-As-wad, Ammar ibn Yasir, Hudhaifa ibn Yaman, Khuzaimah ibn Thabit, Abu Buraidah Al-Aslam, Al-Barraa ibn Azib, Ubay ibn Kaab, Sahl ibn Hunaif, Saad ibn Ubadah, Qays ibn Saad, Abu Ayyub Al-Ansari, Jabir ibn Abdillah, Khalid ibn Said, na wengineo, (wote hawa) waliipinga baia hiyo. Taz: Tarikh Tabari, Tarikh ibn Al-Athir, Tarikh Al-Khulafa, Tarikh Al-Khamis, Al-Istiiabu na kila Aliyeitaja baia ya Abubakar.

Basi iko wapi hiyo ijmai isemwayo enyi waja wa Mwenyezi Mungu? Kwani lau Ali ibn Abi Talib peke yake

210

angekuwa ndiye aliyepinga baia hiyo ingetosha kabisa kuituhumu hiyo ijmai, kwani ni yeye pekee ndiye aliyekuwa ameandaliwa na Mtume (s.a.w.) ili awe Khalifa hata kama tukikadiria kutokuwepo kwa tamko linalomgusa moja kwa moja (lakini yapo matamko wazi ya mwenyewe Mtume s.a.w.).

Kilichotokea ni kwamba baia ya Abubakar ilipatikana bila ya mashauriano, bali ilipatikana bila kutegemewa kwani wahusika na wakata shauri kama wanavyoitwa na wanachuoni wa Kiislamu hawakuwepo walikuwa wameshughulika kumuandaa Mtume kwa mazishi. Nao watu wa Madina waliokuwa wamegubikwa na kifo cha Mtume wao walishitukizwa na kulazimishwa kufanya baia kwa nguvu baada ya tukio hilo kama ambavyo onyo lao (hao walioandaa baia hii) kwamba wangeiunguza nyumba ya Fatmah iwapo wapinzani wa baia hawatatoka nje. Basi ni vipi itafaa kwetu sisi baada ya (mambo kama) haya tuseme (eti) baia (ya Abubakr) ilipatikana kwa mashauriano na ijmai!!? Taz: Tarikh Al-Khulafa.

Hapana shaka Umar ibn Al-Khatab mwenyewe alishuhudia ya kwamba baia ile ilikuwa (ni jambo la) ghafla, Mwenyezi Mungu aliwakinga Waislamu na shari yake, na akaendelea kusema, "Yeyote atakayerudia kufanya baia kama hiyo muuweni, au alisema "Yeyote mwenye kufanya kampeni kama hiyo asipewe baia wala yule aliyembai." Taz: Sahih Bukhar, J. 4 uk. 127.

Naye Imam Ali anasema juu ya baia hiyo: "Ama namuapa Mwenyezi Mungu, hapana shaka mwana wa Abu Quhafah (Abubakr) alijivalisha Ukhalifa, hali ya kuwa anajua kwamba daraja yangu na Ukhalifa ni sawa na mhimili najiwe la kusagia, kwangu mimi mamriko huporomoka na wala ndege hafiki juu yangu.

Naye Saad ibn Ubbadah Bwana wa Maansari ambaye aliwahujumu Abubakr na Umar siku ile ya Saqifah na alijaribu

211

juhudi zake zote kuwazuwia na kuwaweka mbali na Ukhalifa, lakini-akashindwa kwa sababu alikuwa mgonjwa asiyeweza hata kusimama, na baada ya Ansari kumpa baia Abubakr yeye alisema:- "Wallahi kamwe sitakupeni baia mpaka nimalize mishale yangu kukurushieni kutoka kwenye ala yangu ya mishale, na niuloweshe damu mkuki wangu nikupigeni kwa upanga wangu kadiri mkono wangu utakavyoweza kuumiliki, na nitakupigeni pamoja na watu nilionao miongoni mwa watu wangu najamaa zangu. Hapana kabisa (siwaungi mkono) lau hata kama majini na watu wote wangekusanyika kwa ajili yenu nisingewapeni baia hadi nifike kwa Mola wangu."

Saad ibn Ubbadah alikuwa hasali pamoja nao au nyuma yao wala hasali nao sala ya ljumaa na wala hamiminiki nao kwenye mmiminiko wao (kutoka Arafah).

Lau kuna mtu angemuunga mkono Saad kuwapiga vita, angeliwapiga vita na alibakia hivyo mpaka alipokufa huko Shamu katika kipindi cha Ukhalifa wa Umar. Taz: Tarikhul-KhulafaJ. 1 uk. 17

Basi iwapo baia hii ilikuwa ya ghafla, ambayo Mwenyezi Mungu aliikinga shari yake kama alivyoeleza Umar ambaye ndiye aliyeimarisha nguzo zake na unafahamu matokeo ya mambo ya Waislamu yaliyosababishwa na baia hiyo. Na iwapo Ukhalifa huu ulikuwa ni wa kujivalisha (kama kanzu) na Abubakr kama alivyoueleza Imam Ali kwani yeye (Imam All) ndiye mstahiki wake kisheria. Na iwapo baia hii ilikuwa ni dhulma kama alivyoizingatia Saad ibn Ubbadah, Bwana wa Maansari ambaye alijitenga na jamaa kwa sababu ya baia hiyo. Na kama baia hii siyo ya kisheria kwa sababu ya kupingwa na Masahaba wakubwa pamoja na Abbas ambaye ni ammi yake Mtume. Ni ipi hoja (inayohalalisha) kusihi Ukhalifa wa Abubakar? Jawabu ni kwamba, hapana hoja yoyote waliyonayo Masunni.

212

Kwa hiyo kauli ya Mashia ndiyo sahihi ndani ya maudhui hii, kwani imethibiti kupatikana kwa maandiko juu ya Ukhalifa wa Ali kwa Masunni wenyewe, na wameyafanyia taawili (tafsiri) ili kulinda heshima ya Masahaba, lakini kwa mtu muadilifu hana njia ya kukwepa, isipokuwa kukubali maandiko hayo, na khasa pindi atakapofahamu utata uliyomo ndani yajambo hili. Taz:

Saqifah Wal-Khilafah cha Abdul-Fatah Abdul-Maqsood na As-Saqifa cha Sheikh Muhammad Ridhaa Mudhafar.

2. Kuhitilafiana kwa Fatmah na Abubakr

Maudhui hii pia wamekubaliana Masunni na Mashia kuwa ni sahihi, haimpi nafasi mtu muadilifu isipokuwa kutoa maamuzi ya kwamba Abubakr alikosea, hata kama hakukiri juu ya dhulma aliyoifanya dhidi ya (Fatumah ambaye) ni mwanamke bora kuliko wote, kwani yeyote mwenye kufuatilia tukio hili la huzuni na kulichunguza kila upande atafahamu kwa yakini kabisa kwamba, Abubakr alikusudia kumuudhi Fatumah na kumkanusha ili asijetoa hoja dhidi yake kuhusu yale maagizo ya Mtume katika siku ya Ghadir na mengineyo yanayohusu Ukhalifa wa mumewe na ibn ammi yake Ali (a.s.), na tunakuta (dalili) nyingi kuhusu jambo hilo.

Miongoni mwake ziko zile ambazo wanahistoria wameziandika ya kwamba Bibi Fatumah (a.s.) alitoka akiuzunguka (mji wa Madina) kwenye vikao vya Maansari akiwataka msaada wa kumpa baia ibn ammi yake basi wao husema "Ewe binti wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kwa hakika baia yetu tumekwisha mpa bwana huyu, na lau mumeo na ibn ammi yako angelitangulia kwetu kabla ya Abubakr kamwe tusingemkiuka". Basi Imam Ali (ambaye) Mwenyezi Mungu ameutukuza uso wake husema: "Hivi kweli (ilikuwa Busara nimuache Mjumbe wa Mwenyezi Mungu nyumbani mwake bila kumzika ili tu nitoke kuja kugombana na watu juu ya cheo chake"? Hivyo basi Fatumah naye husema, "Alichofanya

213

Abul-Hasan ndicho kilichompasa kukifanya, na wao wamefanya jambo ambalo Mwenyezi Mungu atawauliza na atawalipa (kwa tendo hilo). Taz: Tarikh AI-Khulafaa cha ibn Qutaibah Juz. 1

uk. 19, Sharh Nahjul-Balagha cha ibn Abil-Hadid (Baiatu Abubakar.)

Na lau Abubakar angelikuwa kakosea akiwa na nia njema, au kwa misingi ya Ish-tibahi basi Fatumah (a.s.) angelimkinaisha (kwa kumfahamisha) lakini sivyo bali (Fatumah) alimkasirikia (Abubakr) na hakumsemesha hadi kifo chake, kwa kuwa yeye Abubakr aliyakanusha madai yake na hakuukubali ushahidi wake na ushahidi wa mumewe na kwa yote haya ghadhabu yake dhidi ya Abubakar ilizidi kiasi kwamba hakumruhusu kuhudhuria mazishi yake kwa mujibu wa usia wake kwa mumewe ambaye alimzika usiku tena kwa siri. Taz: Sahih Bukhar Juz. 3 uk. 36, Sahih Muslim Juz. 2 uk. 72 mlango usemao La-mirath ma Taraknahu Sadaqah.

Na katika kueleza mazishi yake Bibi Fatumah kwamba yalikuwa usiku tena kwa siri, mimi wakati wa utafiti wangu huu nilisafiri kwenda Madina yenye nuru ili nipate kuchunguza mwenyewe binafsi juu ya baadhi ya uhakika (wa mambo) na nimegundua ya kwamba: -

Kwanza: Kaburi la Bibi Fatumah halijulikani lilipo hapana ajuwaye, wako wasemao kwamba limo ndani ya chumba cha Mtume, na wengine wanasema kwamba limo ndani ya nyumba yake muqabala na chumba cha Mtume, na kauli ya tatu ni kwamba limo ndani ya (uwanja wa) Jannatul-Baqii katikati ya

makaburi ya watu wa nyumba ya Mtume, bila ya kuwepo ufafanuzi.

Huu ni uhakika wa mwanzo niliougundua ya kwamba Bibi Fatumah alitaka hapo baadaye Waislamu wajiulize ni sababu zipi zilizomfanya amtake mumewe amzike kwa siri tena usiku na asiwepo miongoni mwao yeyote aliyehudhuria mazishi

214

yake!!! na kwa ajili hiyo itawezekana kwa kila Muislamu kupata baadhi ya ukweli wa mambo yanayozindua (fikra), wakati wa kurejea historia.

Pili: Nimegundua kwamba yeyote anayetaka kuzuru kaburi la Uthman Ibn Affan atatembea masafa marefu mpaka afike mwisho wa Baqii, atamkuta chini ya ukuta wakati wengi wa Masahaba atawakuta wamezikwa mwanzoni tu mwa Baqii karibu na mlangoni, hata Malik Ibn Anas muasisi wa madh-hebu ya Malik, ambaye ni Tabiit-Tabiina (siyo Sahaba) amezikwa karibu na wakeze Mtume (s.a.w.), na imenithibitikia kwamba, Uthman amezikwa Hash Kaukab ambalo lilikuwa eneo la Mayahudi. Ni kweli kwani Waislamu walizuwia kumzika Baqii ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Muawiyah ibn Abi Sufiyan alipotawalia Ukhalifa aliinunua ardhi hiyo na kuingiza ndani ya eneo la Baqii ili apate kuliingiza ndani yake kaburi la ibn ammi yake Uthman. Na yeyote atakayezuru Baqii hata leo hii atauona ukweli huu wazi wazi.

Na mimi nastaajabu sana ninapofahamu kwamba Fatumah Zahra (a.s.) ndiye mtu wa kwanza kumfuatia Baba yake (kwa kufariki) kwani kuna miezi sita tu kwa makadirio makubwa baina ya kifo cha Mtume na Bibi Fatmah, kisha ni kwanini hakuzikwa pembezoni mwa baba yake?

Sasa iwapo Fatumah Zahra mwenyewe ndiye aliyeusia kuwa azikwe siri na hakuzikwa karibu na kaburi la baba yake kama nilivyoeleza, basi nini kilichotokea kwenye mwili wa mwanawe Hasan ambaye naye hakuzikwa karibu na kaburi la Babu yake? Jambo hili alilizuwia Ummul-Muuminina Aisha na alifanya jambo hilo pindi Husein (a.s.) alipouleta mwili wa nduguye Hasan ili auzike pembeni mwa Babu yake mjumbe wa Mwenyezi Mungu.

Mama Aisha alipanda nyumbu akatoka akinadi na kusema "Msimzike nyumbani mwangu mtu nisiyempenda."

215

Banu Umayyah na Banu Hashim wakajipanga kwa ajili ya vita, lakini Imam Husein (a.s.) akamwambia mama Aisha kwamba yeye atatufu kaburi ya babu yake akiwa na mwili wa nduguye kisha amzike Baqii kwa sababu Imam Hasan alimuusia ya kuwa wasije mwaga damu japo kidogo kwa ajili yake.

Na kwa sababu hii Ibn Abbas alimwambia Bibi Aisha katika beti mashuhuri kama ifuatavyo:-

Ulipanda ngamia ukapanda nyumbu, lau utaishi zaidi utapanda tembo, wewe unayo sehemu moja katika tisa lakini thumni yote umeitumia.

Na huu ni ukweli mwingine miongoni mwa mambo yanayotisha, itakuwaje kwa Bibi Aisha (peke yake) miongoni mwa wakeze Mtume wengi ambao ni tisa airithi nyumba yote kama alivyosema ibn Abbas?

Na ikiwa Mtume harithiwi kama alivyodai Abubaki mwenyewe na kwa sababu hiyo akazuwia urithi wa Fatumah" kwa baba yake, basi ni vipi Bibi Aisha alirithi? Je, hivi ndani ya kitabu cha Mwenyezi Mungu iko aya inayompa mke haki ya kurithi na kumnyima haki hiyo Binti? Au tuseme hizo ni sias ambazo ndizo zilizobadilisha kila kitu zikamnyima Binti kila kitu na kumpa mke kila kitu?

Na kwa mnasaba huu naeleza kisa cha ajabu ambacho baadhi ya wanahistoria wamekieleza, na kinauhusiano na maudhui hii ya urithi.

Amesema Ibn Abil-Hadid Al-Muutazili ndani ya Shark Nahjil-Balagha: -

Mabibi Aisha na Hafsa walimwendea Uthman katika

zama za Ukhalifa wake, wakamtaka awagawie urithi wao kutoka kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Uthmani alikuwa kajiegemeza akakaa sawa na kumwambia Bibi Aisha

216

"Wewe na huyu mwanamke aliyeketi mlimleta bedui ambaye hujitahirisha kwa mkojo wake na hali ya kuwa ninyi mnashuhudia kwamba Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kasema, "Sisi Mitume haturithiwi", ikiwa kweli Mtume harithiwi, basi ninyi mnataka nini baada ya hayo, na iwapo Mtume anarithiwa ni kwanini basi mlimnyima Fatumah haki yake"? Bibi Aisha akaondoka mbele ya Uthman hali ya kuwa amekasirika na akasema "Muuweni Naathal hakika amekufuru". Taz: Shark Nahjil-Balagha cha ibn Abil-Hadid Juz. 16 uk. 220-223.

3. Ali ndiye anayestahiki kufuatwa

Miongoni mwa mambo yaliyonifanya nizindukane na kuacha mwenendo wa wazazi na mababu ni kipimo cha kiakili na maandiko yanayowahusu, Ali ibn Abi Talib na Abubakr.

Kama nilivyoeleza ndani ya milango iliyotangulia katika uchunguzi huu, kwa hakika mimi nategemea Ijmai wanayo afikiana Masunni na Mashia, na hapana shaka nimechunguza ndani ya vitabu vya makundi haya mawili kuhusu maelezo yaliyokuja miongoni mwa maandiko yaliyothibitishwa na rejea za pande mbili sijakuta isipokuwa Ijimai iliyopo ni kwa Ali ibn Abi Talib, kwani wamekubaliana kuhusu Uimamuwake Mashia na Masunni, ndani ya maandiko yaliyokuja na kuthibitishwa na rejea za pande mbili. Wakati huo huo hakuna anayedai Uimamu wa Abubakr isipokuwa kundi moja miongoni mwa Waislamu, na hapo kabla tumeeleza maneno aliyoyasema Umar kuhusu baia ya Abubakr, vile vile ubora na sifa wanazozieleza Mashia juu ya Ali ibn Abi Talib zinazo sanadi zinazopatikana na kuthibitishwa ndani ya vitabu vya Ahlus-Sunnah wanavyovitegemea, tena zimekuja kwa njia nyingi ambazo hazina shaka.

Idadi kubwa ya Masahaba wamesimulia hadithi juu ya ubora wa Imam Ali kiasi cha kumfanya Imam Ahmad ibn Hambal aseme:-

217

"Hapakuja hadithi nyingi kwa Sahaba yeyote miongoni mwa Masahaba wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kuhusu ubora kama zilivyokuja kwa Ali ibn Abi Talib. Taz: Musfad-rak As-Sahihain cha Al-Hakim Juz. 3 uk. 107, Al-Manaqib cha Khawar-Zami uk. 3 na 19, Tarikh Al-Khulafa cha Suyut uk. 168, As-Sawaiqu Al-Muh-riqah cha ibn Hajar Al-Haithami uk. 72, Tarikh ibn Asakir Juz. 3 uk. 63, Shawahiduf-Tamil cha Al-Haskani Al-Hanafi Juz. 1 uk. 19.

Naye Qadhi Ismail na An-Nasai na Abu Ali Nishapuri wamesema:- "Hapakuja kuhusu haki ya yeyote miongoni mwa Masahaba kwa Sanaa ya Hasan kama ilivyokuja kwa Ali.

Kwa hiyo, pamoja na kutupiajicho hali ya Banu Umayyah ambao waliwalazimisha watu mashariki na magharib ya ulimwengu wamtukane Imam Ali na wasitaje ubora wake, mpaka walizuwia mtu yoyote asiitwe kwa jina la Ali, lakini pamoja na yote haya sifa zake na fadhila zake zilichomoza licha ya upinzani huo. Anasema Imam Shafii kuhusu jambo hili:-"Nastaajabu, mtu ambaye maadui zake wameficha fadhila zake kwa sababu ya husuda, na wampendao wakazificha kwa sababu ya khofu, lakini sifa zake zimechomoza baina ya wawili hawa na kuenea ulimwengu mzima".

Ama kuhusu Abubakar, pia nimechunguza ndani ya vitabu vya pande hizi mbili sijakuta ndani ya vitabu vya Ah-lus-Sunna Wal-Jamaa walioandika sifa za Abubakar kwamba ana sifa ambazo zinaweza kulinganishwa au kuzidi zile fadhila za Imam Ali, kwa msingi kwamba ubora wa Abubakar unaotajwa ndani ya vitabu vya historia imma utakuwa umesimuliwa na Binti yake Aisha ambaye tumekwishafahamu msimamo wake dhidi ya Imam Ali, kwani Bibi Aisha amejaribu kwa juhudi zake zote kumjenga baba yake japokuwa kwa kutumia hadithi maudhui (za kubuni) au zilizopokelewa toka kwa Abdallah ibn Umar ambaye naye ni miongoni mwa watu waliokuwa wamejitenga

218

mbali na Imam Ali, na alikataa kumpa baia Imam Ali pindi watu walipokubaliana juu ya hilo na alikuwa akisimulia kwamba, "Mtu bora baada ya Mtume ni Abubakar kisha Umar kisha Uthman kisha haboreshwi mtu mwingine na baada ya hao, basi watu wengine ni sawa sawa." Hadithi hii ina maana kwamba, Abdallah ibn Umar, alimfanya Imam Ali kuwa ni miongoni mwa watu wa kuongozwa kama walivyo watu wa kawaida hana aina yoyote ya daraja ya ubora. Yu wapi basi Abdallah ibn Omar na ule ukweli walioutaja wanachuoni wa umma (wa Kiislamu) ya kwamba hapakuja kwa Sahaba yeyote sanadi (za hadithi) zenye daraja ya Hasan kama zile zilizokuja (kutaja ubora wa) Ali ibn Abi Talib. Je hivi ni kweli Abdallah ibn Omar hakupata kusikia kutoka kwa Mtume japokuwa fadhila moja ya Ali?

Hapana kabisa, wallahi amesikia na kuzidhibiti (fadhila za Ali) lakini siasa ilimzuga na kipi kitakacho kujulisha hiyo siasa ni kitu gani, hapana shaka hiyo siasa (iliyopita) ilikuwa ni kuugeuza ukweli na kufanya maajabu.

Hali kadhalika yataka ufahamu ya kwamba, watu kama amri Ibn Al-as, Abuhurairah, Urwa na Ikhrimah wamesimulia fadhila za Abubakar na wote hawa walikuwa dhidi ya Imam Ali na walimpiga vita ima kwa silaha au kwa kumsingizia na kuunda fadhila nyingi za maadui wa Imam Ali (a.s.).

Imam Ahmad ibn Hambal amesema: "Hapana shaka kwamba Imam Ali (a.s.) alikuwa na maadui wengi, maadui zake hao walitafuta jambo ambalo lingemuaibisha lakini hawakupata, hivyo basi wakamuendea mtu ambaye alikuwa akimpiga vita Imamu Ali (a.s.) wakamsifu sana kwa nia ya kumfanyia vitimbi Imam Ali.

Lakini Mwenyezi Mungu anasema, "Bila shaka wao wanafanya hila, nami nazipindulia mbali hila zao, basi wape muda makafiri wape muda kidogo" (Qur.86:15-17)

219

Kwa hakika ni miongoni mwa miujiza ya Mwenyezi Mungu tu kutokeza na kutambulikana kwa fadhila na ubora wa Imam Ali (a. s.) baada ya kupita karne sita za utawala dhalimu na wa mabavu dhidi ya Imam Ali na watu wa nyumba yake, kwani watawala wa Banu Abbas hawakupunguza kero, chuki, vitimbi na kuwanyanyasa watu wa nyumba ya Mtume kama walivyofanya watawala waliowatangulia wa Kibanu Umayyah.

Pamoja na kwamba Abubakar ndiye aliyekuwa Khalifa wa kwanza na alikuwa na madaraka kama tulivyokwishakufahamu, na kwamba dola ya Banu Umayya ilikuwa ikitoa zawadi maalum na rushwa kwa kila mwenye kusimulia (hadithi) zinazowahusu Abubakar, Umar na Uthman pia zilitengenezwa hadithi nyingi zinazohusu ubora na sifa za Abubakar ambazo zimejaa ndani ya vitabu. Basi pamoja na yote hay a, hazikuweza kufikia sehemu moja ya kumi ya daraja za Imam Ali na fadhila zake. Zaidi ya hayo ni kwamba iwapo wewe utazichambua hadithi zilizosimuliwa juu ya fadhila za Abubakar utazikuta haziafikiani na jinsi historia ilivyoyasajili baadhi ya matendo yake yanavyopingana na yaliyosemwa kumuhusu Abubakar, na wala akili haiwezi kuyakubali wala sheria. Hapo kabla umetangulia ufafanuzi wa ile hadithi isemayo "Lau itapimwa imani ya Abubakar na imani ya umati wangu basi imani ya Abubakar itakuwa nzito" Na lau Mjumbe wa Mwenyezi Mungu angelifahamu ya kwamba Abubakar anayo daraja (kubwa) kama hii, basi asingemfanya Usamah ibn Zaid kuwa amiri na wala asingekataa kumshuhudia wema na mafanikio kama alivyowashuhudia mashahidi wa Uhdi na isitoshe Mtume alimwambia (Abubakar) "Hakika mimi sijui ni mambo gani mutayazua baada yangu" hali iliyomfanya Abubakr alie. Taz:

Muwatta ya Imam Malik juz. luk. 307, Maghazi ya Al-Waqidi uk. 310.

Pia Mtume asingemtuma Ali ibn Abi Talib kumfuata Abubakar ili aichukue kutoka kwake Sura ya Baraa na

220

kumzuwia kuifikisha. Taz: Sahih Tirmidhi Juz. 4 uk. 339 Musnad Ahmad ibn Hambal Juz. 2 uk. 319, Mvstadrak Al-Hakim Juz. 3 uk. 51

Na wala Mtume alipokabidhi bendera siku ya Khaibar asingesema kuwa "Kesho nitampa bendera yangu mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda mtu huyo, ni madhubuti kwenye mapambano harudi nyuma, Mwenyezi Mungu ameufanyia mtihani moyo wake kwa imani." Baada ya usemi huo akampa bendera Ali (a.s.) na hakumpa Abubakr. Taz: Sahih Muslim, Babu Fadhail Ali Ibn Abi Talib.

Na lau Mwenyezi Mungu angelitambua ya kwamba Abubakari anayo daraja hii ya imani na kwamba imani yake inashinda imani ya ummati Muhammad wote, basi Mwenyezi Mungu asingelimuonya kuwa mema yake yataporomoka pale aliponyanyua sauti yake juu ya sauti ya Mtume. Taz: Sahih Bukhari Juz. 4 uk. 184.

Rudi nyuma Yaliyomo endelea