Rudi nyuma Yaliyomo endelea

Tulifika kwenye Maqam, na wakati rafiki yangu anasoma idhini ya kuingia mimi nilikuwa nauangalia mlango na nilikuwa nastaajabia dhahabu na nakshi ambazo zimeenea mlango wote na zote zilikuwa ni (nakshi za) aya za Qur'an.

Rafiki yangu aliingia nami nikaingia baada yake hali ya kuwa ni mwenye tahadhari, akilini mwangu nafikiria namna

40

mbali mbali ya uzushi niliousoma ndani ya baadhi ya vitabu vinavyowakufurisha Mashia. Na ndani ya Maqam niliona nakshi na mapambo ambayo sikuwahi kuyaona hapo kabla, nilishangazwa na mambo niliyoyaona na nikajihisi kwamba niko katika ulimwengu usio wa kawaida na usio fahamika na kila wakati nilikuwa nikiwaangalia kwa chuki watu hawa waliokuwa wakitufu wakizunguka pembeni ya kaburi huku wakilia na kubusu nguzo zake na kona zake na wengine wanasali karibu na kaburi. Basi hapo niliikumbuka hadithi ya Mtume (s.a.w.) isemayo "Mwenyezi Mungu amewalaani Mayahudi na Wakristo walioyafanya makaburi ya Mawalii wao kuwa misikiti".

Nilijitenga na rafiki yangu ambaye alipoingia tu alianza kulia kisha nilimwacha anaswali na nikausogelea ubao ulioandikwa na kutundikwa kwenye kaburi kwa ajili ya ziyara.

Nikausoma na sikuyafahamu mambo mengi yaliyomo kutokana na kuwa na majina mengi ambayo kwangu ni mageni na siyajui.

Nilielekea kwenye kona na nikasoma fatiha kwa ajili ya kumrehemu mwenye kaburi hilo nikasema, "Ewe Mwenyezi Mungu ikiwa maiti huyu ni miongni mwa Waislam basi umrehemu kwani wewe ni mjuzi mno kuliko mimi". Rafiki yangu alinisogelea na akaninong'oneza sikioni akasema: "Kama una haja yoyote ile muombe Mwenyezi Mungu mahala hapa kwani sisi tunapaita kuwa ni mlango wa maombi." Mimi sikujali maneno yake (Mwenyezi Mungu anisamehe) bali nilikuwa nikiwaangalia wazee wenye umri mkubwa na vichwani mwao wamevaa vilemba vyeupe na vyeusi na katika nyuso zao kuna alama ya sijida, haiba yao ilikuwa ikiongezewa na ndevu zilizokuwa zikinukia uzuri na wanao mvuto wenye haiba.

Hapana yeyote aliyeingia mahala hapo miongoni mwao isipokuwa alikuwa akilia nami nikajiuliza moyoni, je inawezekana machozi haya yakawa ni ya uongo? hivi

41

inawezekana wazee hawa wenye umri mkubwa wakawa wanakosea?

Nilitoka hali ya kuwa nimechanganyikiwa na kushangaa kutokana na mambo niliyoyaona na wakati huo rafiki yangu alikuwa akirudi kinyume nyume kwa heshima ili asije akaipa mgongo Maqam ile.

Nilimuuliza ni nani huyu mwenye Maqam hii? Akasema, "Ni Imam Musa Al-Kadhim". Nikasema, "Huyu Imam Musa Al-Kadhim ni nani?"

Akasema, "Subhanallah! ninyi ndugu zetu Masunni mumewacha kiini na mumeshikamana na maganda".

Nilisema kwa hasira, "Vipi tumeshikamana na maganda na tumeacha kiini?" Basi alinituliza na akasema:

"Ndugu yangu, wewe tangu ulipoingia Iraq huachi kumkumbuka Abdul-Qadir Al-Jailan huyu aliyewajibisha hima yako yote ni nani?"

Nikajibu kwa haraka tena kwa fahari kubwa, "Yeye ni katika watu wa kizazi cha Mtume na lau kungekuwa na Nabii baada ya Muhammad basi angekuwa Abdul-Qadir Jailan (r.a.)".

Akasema, "Ewe ndugu yangu Al-Samawi unaifahamu historiayaUislam?" Nilijibu bila kusita kwamba, "Ndiyo" lakini kwa kweli sikuwa nafahamu katika historia ya Uislamu isipokuwa sehemu ndogo na siyo nyingi, kwani waalimu wetu walikuwa wakitukataza jambo hili (la kujifunza historia ya Uislamu) wakidai kwamba hiyo ni historia iliyochafuliwa hakuna

faida kuisoma.

Kwa mfano nakumbuka kwamba Mwalimu aliyekuwa akihusika kutusomesha somo la Balagha alikuwa akitusomesha khutba ya Shaqshaqiyyah iliyoko ndani ya Nahjul-Balaghah ya

42

Imam Ali, nilishangaa kama walivyoshangaa wanafunzi wengi wakati wa kuisoma khutba hiyo, nami nilijasirika kumuuliza Mwalimu kama kweli haya ni katika maneno ya Imam Ali, basi alijibu, "Bila shaka nani mwingine mwenye balagha kama hii (hakuna) ila yeye na kama yasingekuwa ni maneno yake Ali Karrama Llahu Waj-hahu, basi wanachuoni wa Kiislam mfano wa Sheikh Muhammad Abdou ambaye ni Mufti wa Misri wasingejishughulisha kuyasherehesha".

Hapo mimi nilisema: "Kwa hakika Imam Ali katika hotuba hii anawatuhumu Abubakar na Omar kwamba wao wamempokonya haki yake ya Ukhalifa."

Basi Mwalimu alifura na kunikemea kwa ukali na kunionya kwamba atanifukuza iwapo nitarudia kuuliza swali kama hili, na akaongeza kusema sisi tunasoma Balaghah wala hatusomi historia hakuna umuhimu wowote wa historia ambayo matukio yake yamejaa fitna na vita vya kumwaga damu baina ya Waislamu basi kama ambavyo Mwenyezi Mungu amezitakasa panga zetu kwa damu zao, nasi tuzitakase ndimi zetu tusiwashutumu.

Sikutosheka na sababu hii (aliyoitoa mwalimu) bali nilibakia nimemkasirikia Mwalimu yule ambaye alikuwa akitufundisha Balaghah bila ya maana (zilizomo) na nilijaribu mara nyingi kusoma historia ya Uislamu lakini sikupata rejea za kutosha na pia uwezo wa kununua vitabu ulikuwa mdogo, na sikumpata Sheikh yeyote miongoni mwa masheikh wetu na wanachuoni wetu anayeipakipa umbele historia, kama kwamba wao wamekubaliana kuisahau na kutoichunguza, na huwezi kumpata yeyote anamiliki kitabu kamili cha historia.

Basi rafiki yangu aliponiuliza kuhusu kuifahamu historia nilitaka kumpinga tu ndipo nilipojibu kuwa "Ndiyo" wakati hali halisi inasema kwamba "Nikijuacho ni kuwa hiyo ni historia iliyovurugwa hakuna faida ndani yake isipokuwa kuna fitna na

43

chuki na mambo yanayopingana.

(Rafikiyangu) alisema: "Je unafahamu ni lini na ni zama zipi Abdul-Qadir alizaliwa?" Mimi nilisema, "Kiasi amezaliwa katika karne ya sita au ya saba"

Basi kuna miaka mingapi kati yak na mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Nikasema, "Karne sita" yeye akasema, "Basi karne moja kuna vizazi viwili kwa makadirio madogo, itakuwa nasaba ya Abdul-Qadir Al-Jaylani kwa Mtume iko baada ya babu wa kumi na mbili nikasema ndiyo".

Akasema huyu Musa Ibn Jaafar Ibn Muhammad Ibn Ali Ibn Hussein Ibn Fatmah Al-Zahra, nasaba yake inafika kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu baada ya mababu wanne tu au yafaa kusema kuwa yeye ni kizazi cha karne ya pili ya hijriyah, basi ni yupi kati ya wawili hawa ambaye yuko karibu kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Musa na Abdul-Qadir? Bila ya kufikiria nilisema! "Bila shaka huyu yuko karibu, lakini ni kwanini basi sisi hatumfahamu na wala hatusikii kutajwa kwake?" Akasema, "Hapa ndipo kwenye lengo na ndiyo maana nilisema kwamba (samahani niruhusu nirudie) mumeacha kiini na mumeng'ang'ania maganda na usinielewe vibaya natarajia utaniwia radhi".

Tulikuwa tukizungumza huku tunakwenda na mara nyingine tunasimama mpakatukafika mahala panaposomeshwa elimu na hapo wanafunzi na waalimu walikuwa wamekaa wakibadilishana maoni na nadharia za kielimu na tulikaa huko na rafiki yangu alikuwa akimtafuta mtu maalum miongoni mwa walioketi kama kwamba anayo ahadi na mmoja wao.

Hatimaye alikuja mtu na akatusalimia na nilifahamu kuwa ni mwenziwe chuoni hapo, na alimuuliza kuhusu mtu fulani, kutokana na majibizano nilimfahamu kuwa mtu huyo ni Daktari na atafika hivi karibuni, basi wakati huo rafiki yangu

44

aliniambia kuwa nimekuleta mahala hapa ili nikutambulishe kwa msomi anayehusika na uchambuzi wa mambo ya historia, naye ni Profesa wa historia katika chuo kikuu cha Baghadad na alipata shahada ya uprofesa kutokana na utafiti wake aliouandika kuhusu Abdul-Qadir Al-Jailan, na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu atakunufaisha, kwani mimi si bingwa wa somo la historia.

Tulikunywa juice ya baridi mpaka alipokuja yule profesa, na rafiki yangu alinyanyuka kumsalimia na akanitambulisha kwake na akamtaka anidokezee kwa ufupi historia ya Abdul-Qadir Al-Jailan, na aliniomba tumruhusu aende kwa ajili ya baadhi ya shughuli zake.

Yule profesa aliniagizia kinywaji baridi na akaanza kuniuliza jina langu, nchi yangu na kazi yangu kama ambavyo alinitaka nimsimulie umashuhuri wa Abdul-Qadir Al-Jailan huko Tunisia.

Nilimsimulia mengi juu ya jambo hili kiasi kwamba kwetu sisi watu wanaitakidi kwamba Sheikh Abdul-Qadir alikuwa akimbeba mjumbe wa Mwenyezi Mungu mabegani kwake katika usiku wa Miiraj wakati Jibril alipochelea kuungua, na mjumbe wa Mwenyezi Mungu akamwambia unyayo wangu uko juu ya mabega yako na unyayo wako uko juu ya bega la kila walii mpaka siku ya Qiyamah.

Yule Profesa akacheka sana alipoyasikia maneno yangu lakini mimi sikufahamu je kucheka kwake kulitokana na riwaya nilizomsimulia au alikuwa akimcheka mwalimu wa kitunisia aliyeko mbele yake? Baada ya majadiliano mafupi kuhusu mawalii na watu wachamungu alisema kwamba, yeye ametafiti kwa muda wa miaka saba, katika kipindi hicho alisafiri hadi Lahorre nchini Pakistani na alikwenda Uturuki, Misri na Uingereza na kila mahali yaliko maandiko (au kumbu kumbu zinazonasibishwa kwa Abdul-Qadir Al-Jailan, aliyachunguza

45

na kuyapiga picha, na hakuna ndani ya kumbu kumbu hizo   kitu chochote kinachothibitisha kwamba Abdul-Qadir  Al-.jailani  anatokana na kizazi cha Mtume, bali kilichopo ni ubeti wa shairi unaonasibishwa kwa mmoja wa wajukuu zake anasema  katika beti hiyo "Na babu yangu ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu" Na hilo laweza likachukuliwa kuwa ni tafsiri ya hadithi  ya Mtume (s.a.w.) isemayo kuwa "Mimi ni babu wa kila mchamungu."

Aliongeza kunieleza kwamba, historia sahihi inathibitisha kuwa Abdul-Qadir asili yake ni Mfursi (Muirani) na siyo Muarabu kamwe, na amezaliwa katika mji mmoja huko Iran uitwao Giilani na ndiyo anaonasibishwa kwao, na alihama kutoka huko na kwenda Baghdad, akasoma na kuishi huko huko na kufundisha katika kipindi ambacho maadili yalikuwa yameharibika.

Mtu huyu alikuwa mchamungu na watu walimpenda na baada ya kufa kwake waliasisi Tariqa ya Qadiriyah kwa munasaba wake kama wanavyofanya siku zote wafuasi wa kila mwana Tasawafi. Aliendelea akasema "Kwa kweli hali ya Waarabu kwa upande huu inahuzunisha".

Hamasa ya Kiwahabi ilifura kichwani mwangu nikamwambia yule mtaalam wa historia, "Kwa hiyo mheshimiwa Profesa wewe fikra zako ni za Kiwahabi, kwani wao wanasema kama usemavyo wewe kwamba hakuna mawalii".

Akasema; "Hapana mimi siko katika misingi ya mtazamo wa Kiwahabi, jambo la kuhuzunisha kwa Waislamu ni kwamba imma watamsifu mtu zaidi ya anavyostahiki kusifiwa, au kukebehi kila kitu au huamini na kusadiki kila aina ya uzushi ambao hautegemei dalili na haukubaliki kiakili wala kisheria na imma watapinga kila kitu hata miujiza ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.) na hadithi zake kwa kuwa tu havikubaliani na matamanio na itikadi yao wanayoitakidi na

46

kwa ajili hiyo kundi fulani (la Waislamu) limeelekea Mashariki najingine Magharibi, Masufi kwa mfano wanasema kuwa kuna uwezekano wa Sheikh Abdul-Qadir Al-Jailan kuwepo Baghdad na wakati huo huo akawa Tunisia, na huenda akamponya mgonjwa huko Tunisia na pia kumuokoa mtu anayezama katika mto Tigris kwa wakati huo huo. Basi huku ni kuvuka mipaka ya kumsifia mtu (Ifrat). Nao Mawahabi kwa kuwapinga masufi wakakanusha kila kitu mpaka wamesema kuwa, ni shirki kutawassal kwa Mtume (s.a.w.) na hii ni kupuuza (haki inayomstahiki mtu) yaani "Tafrit", sivyo hivyo ndugu yangu bali sisi ni kama alivyosema Mwenyezi Mungu mtukuru ndani ya kitabu chake kitukufu "Namna hivyo, tumekufanyeni kuwa ni ummati wa kati na kati ili muwe mashahidi juu ya watu". (2:143).

Maneno yake yalinipendeza sana na kimsingi nilimshukuru na nikaonesha kukinaika kwangu kwa maneno aliyoyasema. Alifungua mkoba wake na akatoa kitabu kinachohusu Abdul Qadir Al-Jailan na akanizawadia, vile vile alinialika nyumbani kwake lakini nilitoa udhuru na tukabakia tunazungumzia juu ya Tunisia, na Afrika kaskazini mpaka alipokuja rafiki yangu na tulirudi nyumbani usiku baada ya kuwa siku nzima tumeimaliza katika ziyara na majadiliano. Nilihisi kuchoka basi nikaenda kulala.

Niliamka mapema nikaswali na nikakaa nikisoma kile kitabu chenye utafiti wa maisha ya Abdul-Qadir basi rafiki yangu alipoamka nilikuwa nimekwisha kimaliza nusu yake na alikuwa akija mara kwa mara kuniita kwa ajili ya kifungua kinywa lakini sikukubali mpaka nilipokimaliza kitabu chote. Kilinivutia na kunitia mashaka ambayo hayakudumu bali yalitoweka kabla sijaondoka nchini Iraq.

47

MASHAKA NA KUJIULIZA

Nilibakia nyumbani kwa rafiki yangu kwa muda wa siku tatu na nilipumzika katika siku hizo huku nikiyafikiria kwa makini mambo yote niliyoyasikia toka kwa watu hawa ambao nimewagunduwa na ni kama kwamba wao walikuwa waishi  juu ya mwezi, basi ni kwa nini hakutusimulia mtu  yeyote kuhusu habari zao isipokuwa zile ambazo ni za kudharaulika   na mbaya, ni kwa nini mimi nawachukia bila ya kuwalfahamu, huenda jambo hilo ni matokeo ya uvumi tunao usikia dhidi yao kwamba wao wanamuabudu Ali na kwamba wao wanawaweka Maimamu wao katika daraja ya Mungu na kwamba wao wanaitakidi kuwa Mungu huingia ndani ya mwili wa kiumbe. Na kwamba wao wanasujudia jiwe kinyume cha Mwenyezi Mungu na wao (kama alivyotusimulia) baba yangu baada ya kurejea toka hija huwa wanakwenda kwenye kaburi la Mtume (s.a.w.) na kutia uchafu na najisi, na polisi wa Saudia waliwakamata na kuwahukumu wauliwe, na mengine mengi ya uzushi dhidi yao..... na eleza lolote kuwahusu watu hawa si vibaya!!

Itakuwaje Waislamu wayasikie haya wasiwachukie watu hawa na kuwabughudhi? Bali vipi wataacha kuwaua, lakini pia ni vipi nitaamini uvumi huu hali ya kuwa nimeona kwa macho yangu mambo niliyoyaona, na nimesikia kwa masikio yangu niliyoyasikia na hapo sasa nimemaliza zaidi yawiki moja nikiwa miongi mwao na sikuona wala kusikia toka kwao isipokuwa maneno yanayokubalika akilini, ambayo yanaingia akilini bila

48

kupingwa bali nilivutiwa na ibada zao, dua zao, tabia yao na heshima yao kwa wanachuoni wao mpaka nilitamani niwe kama walivyo wao.

Nilibakia najiuliza "Je, hivi ni kweli kwmba wao wanamchukia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na kila nikimtaja (Mtume) na mara nyingi nilikuwa namtaja ili kuwajaribu nijue msimamo wao, basi wao husema kwa viungo vyao vyote "Ewe Mwenyezi Mungu msalie Muhammad na Aali zake Muhammad." Nilidhani kwamba wanafanya unafiki lakini dhana yangu hii iliondoka baada ya kuangalia vitabu vyao ambavyo nilisoma sehemu fulani ya vitabu hivyo nikakuta jinsi wanavyoiheshimu na kuitukuza na kuitakasa dhati ya Mtume (s.a.w.), jambo ambalo sikulizoea katika vitabu vyetu, kwani wao wanasema kuwa, "Mtume ni maasum katika kila hali, kabla ya kupewa Utume na baada ya kupewa Utume." Wakati sisi Masunni tunasema kuwa," Yeye ni maasum katika kufikisha Qur'an tu, na lisilokuwa hilo yeye anakosea kama wengine." Mara nyingi tunatolea ushahidi jambo hilo kwa kumkosoa Mtume (s.a.w.) na kuziona kuwa rai za baadhi ya masahaba ni sahihi ukilinganisha na rai ya Mtume, na tunayo mifano mingi kuhusiana na jambo hilo, wakati ambapo Mashia wanapinga(usemi usemao) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu hukosea na watu wengine kupatia, hivyo basi baada ya yote haya ni vipi nitaamini kwamba wao wanamchukia Mtume wa Mwenyezi Mungu? Vipi itakuwa hali hii?

Siku moja nilipokuwa nazungumza na rafiki yangu nilimtaka anijibu wazi wazi na mazungumzo yetu yalikuwa kama ifuatavyo: "Ninyi Mashia munamuweka Ali (r.a.) katika daraja ya Manabii kwani mimi mara nyingi kila nimsikiapo mtu miongoni mwenu anamtaja Ali basi husema "Alaihi-Salaam".

Alinijibu na akasema, "Bila shaka sisi tunapomtaja Amirul-Muuminina (Ali) au mmoja wa Maimamu huwa

49

tunasema "Alaihi Salam" hali hii haimaanishi kwamba wao ni Manabii, bali wao ni familia ya Mtume na ni watu wa kizazi chake ambao Mwenyezi Mungu ametuamrisha kuwatakia rehma katika kitabu chake kitukufu na kwa msingi huu inajuzu pia kusema alaihimus-salatu  Was-salaam."

Hapana ndugu yangu, sisi hatutambui "Salat na Salaam" isipokuwa kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu na Manabii waliomtangulia na wala Ali na wanawe hawahusiki katika jambo hilo,

Yeye akasema; "Nakuomba na ninakutarajia usome zaidi mpaka ufahamu ukweli."

Nikasema, "Nitasoma vitabu gani ewe ndugu yangu, je siyo wewe uliyeniambia kuwa vitabu vya Ahmad Amin siyo hoja dhidi ya Shia? Vile vile vitabu vya Shia siyo hoja dhidi yetu na wala hatuvitegemei, huoni ya kwamba vitabu vya Wakristo wanavyo vitegemea vinasemakuwa Isa (a.s.) amesema kwamba "Mimi ni mtoto wa Mungu" wakati ambapo Qur'an tukufu ambayo ndiyo msema kweli inasema ikimnukuu Issa mwana wa Mariam kwamba, "Sikuwaambia ila yale uliyoniamrisha, mwabuduni Mwenyezi Mungu Molawangu na ni Mola wenu".

Akasema, "Vema kwa hakika hivyo ndivyo, nilivyosema, nikitakacho kwako ni hiki, yaani utumie akili, mantiki na dalili kwa kutumia Qur'an tukufu na Sunnah sahihi kwa kuwa sisi ni Waislamu, na lau mazungumzo hayo yangekuwa yanawahusu Wayahudi na Wakristo basi (tungetumia) dalili zisizokuwa hizi.

Mimi nikasema, "Kwa hiyo ukweli nitaufahamu kutoka katika kitabu gani kwani kila mwandishi, kila kundi na kila. madh-hebu yanadai kuwa yako katika haki."

Akaniambia, "Sasa hivi nitakupa dalili thabiti ambayo

50

Waislamu pamoja na Madh-hebu zao na vikundi vyao mbali mbali hawatofautiani japokuwa wewe huitambui (nayo ni hii ifuatayo) Waambie, Ewe Mola wangu nizidishie Elimu.

Akasema, "Je umepata kusoma tafsiri ya aya tukufu isemayo "Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamsalia Mtume, Enyi mulioamini msalieni na mumpe salamu bilakusita." (Qur'an, 33:52)

Wanachuoni wote wa tafsiri wameafikiana, Masunni na Mashia ya kwamba, Masahaba ambao aya hii ilishuka kwao walikuja kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu wakasema "Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, sisi tumekwisha fahamu ni vipi tutakusalimia na hatujafahamu ni vipi tutakusalia" Mtume akasema; "Semeni Ewe Mwenyezi Mungu mrehemu Muhammad na Aali zake Muhammad kama ulivyomrehemu Ibrahim na aali zake Ibrahimu katika walimwengu kwa hakika wewe ni mwenye sifa njema tena mtukufu na wala musinisalie sala iliyokatika". Wakasema, "Ni ipi hiyo sala iliyokatika ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu?" Akasema, "Mtasema, Ewe Mwenyezi Mungu msalie Muhammad na kisha mtanyamaza, na fahamuni kwamba Mwenyezi Mungu ni mkamilifu hakubali ila kitu kilichokamilika".

Masahaba waliyafahamu yote hayo na pia waliokuja baada yao walifuata amri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, basi walikuwa wakimsalia sala iliyokamilika, kiasi kwamba Imam Shafii alisema kuhusu haki yao yaani (kizazi cha Muhammad) kama ifuatavyo:

"Enyi kizazi cha nyumba ya mjumbe wa Mwenyezi Mungu, mapenzi yenu ni faradhi (wajibu) kutoka kwa Mwenyezi Mungu ameyateremsha ndani ya Qur'an, yakutosheni ninyi heshima tukufu ya kwamba yeyote asiyekusalieni hana sala (sala yoke ni batili). "

51

Maneno yake yalikuwa yakitwanga masikio yangu na kupenya hadi moyoni na kuikuta nafsi yangu inakubali, na kwa kweli hapo kabla nilipata kusoma maneno kama haya ndani ya baadhi ya vitabu, lakini sikumbuki vema ni rejea gani.

Nilikiri kwamba sisi tunapomsalia Mtume tunawasalia na Aali zake na Masahaba wake wote lakini hatumpwekeshi Ali (r.a.) kwa salamu kama wasemavyo Mashia (Ali alaihis-salam).

Akasema: "Nini mtazamo wako kuhusu Bukhari, je yeye ni Shia?"

Nikasema "Ni Imam mtukufu miongoni mwaMaimamu wa Kisunni na kitabu chake ni sahih mno baada ya kitabu cha Mwenyezi  mungu".

Basi pale pale alisimama akatoa Sahih Bukhari ndani ya maktaba yake, akaifungua na kuutafuta ukurasa aliokuwa akiutaka kisha akanipa nisome. "Ametusimulia fulani toka kwa fulani naye toka kwa Ali Alaihis-Salaam, sikuyaamini macho yangu na nilishangaa mpaka nikaitilia mashaka kuwa hiyo ni sahihi Bukhari yenyewe?

Nilichanganyikiwa nikarudia kuangalia ndani ya kurasa na juu ya jalada, rafiki yangu alipohisi shaka yangu alikichukua kitabu na kunionyesha ukurasa mwingine ambao ndani yake kuna (riwaya) isemayo "Ametusimulia Ali Ibn Hussein (Alayhi s-salaaamu). Sikuwa na jibu baada ya hapo isipokuwa nilisema "Subhanallah" na kwa jibu hili rafiki yangu alitosheka aliniacha na akatoka. Nilibaki nafikiri na kurudia kuzisoma zile kurasa na kuthibitisha chapa ya kitabu nikaikuta ni miongoni mwa chapa za shirika la Al-Halabi na wanawe lililoko Misri.

Ewe Mungu wangu ni kwa nini ninampinga na kumkanusha (mtu huyu), kwa hakika amenipa hoja thabiti kutoka ndani ya kitabu sahihi mno kwetu sisi, na huyu Bukhari

52

siyo Shia kamwe, naye ni miongoni mwa Maimam wa Kisunni na mwanachuoni wao wa hadithi, je niukubali ukweli huu ambao ni hii kauli yao ya kusema Ali "Alaihi s-salaam". Lakini nachelea juu ya ukweli huu kwamba huenda ukafuatiwa na ukweli mwingine ambao sipendi kuukubali, nami nimeshindwa mara mbili mbele ya rafiki yangu, nimekwisha kiporomosha cheo cha Abdul-Qadir Al-Jailan na nimekubali kwamba Musa Al-Kadhim ni bora kuliko yeye na nimekubali pia kwamba Ali "Alaihis-Salaam" anastahiki hivyo, lakini sitaki kushindwa kwa mara nyingine, nami ndiye yule ambaye kabla ya siku kadhaa nilikuwa mwanachuoni nchini Misri na nikajionea fahari nafsi yangu na wanachuoni wa Azhar walinitukuza, leo najikuta mwenye kushindwa na kuhemewa, na nani hasa (anishindaye) je ni wale watu ambao nilikuwa bado naamini kwamba wao wako katika makosa kwa hakika nimelizowea tamko la "Shia" kuwa ni tusi.

Bila shaka hiki ni kiburi nakujiona, hakika ni ubinafsi na ubishi na chuki, ewe Mungu wangu niongoze na unisaidie kuukubali ukweli japokuwa una uchungu.

Ewe Mwenyezi Mungu nifungue macho yangu na moyo wangu nauniongoze kwenye njia yako iliyonyooka na unijaalie kuwa miongoni mwa wanaosikiliza kauli na kufuata iliyo njema mno, Ewe Mwenyezi Mungu tuoneshe haki kuwa ni haki na uturuzuku kuifuata na utuoneshe batili kuwa ni batili na uturuzuku kuiepuka.

Rafiki yangu alirudi nyumbani nami nikiwa katika hali ya kurudia rudia maombi haya, basi alisema hali ya kuwa anatabasam "Mwenyezi Mungu atuongoe sisi na ninyi na Waislamu wote na amesema ndani ya kitabu chake kitukufu "Na wale wanaopigana Jihadi katika njia yetu tutawaongoa (tuwaoneshe) njia yetu na Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema." (Qur'an, 29:69)

53

Na tamko la jihadi ndani ya aya hii linafasiriwa kwa maana ya utafiti wa kielimu ili kuufikia ukweli, na Mwenyezi Murmu anamuongoza kwenye ukweli kila anaye utafuta ukweli.

54

SAFARI YA KWENDA NAJAF

Katika usiku mmoja rafiki yangu alinijulisha kwamba. kesho Mwenyezi Mungu apendapo tutasafiri kwenda Najaf, nikamuuliza, "Najaf ni nini? akasema: "Huo ni mji wa kielimu na katika mji huo ndimo yalimo malazi ya Imam Ali Ibn Abitalib." Nilistaajabu, itakuwaje Imam Ali  awe na kaburi linalofahamika hiyo ni kwa sababu Masheikh wetu wanasema kwamba hakuna kaburi la Sayyidna Ali linalofahamika.

Tulisafiri ndani ya Gari la abiria mpaka tukafika Al-Kufah na huko tuliteremka ili kuuzuru Msikiti wa Al-Kufah, nao ni miongoni mwa kumbukumbu za kale za Kiislam. Rafiki yangu alikuwa akinionesha maeneo ya kumbukumbu na akanitembeza kwenye Msikiti wa Muslim Ibn Aqil na Hani Ibn Ur-wah na akanisimulia namna walivyouawa (mashahidi) vile vile aliniingiza kwenye Mihrab ambayo Imam Ali aliuawa.

Na baada ya hapo tuliitembelea nyumba aliyokuwa akiishi Imam Ali na wanawe Hasan na Husein na ndani ya nyumba hiyo kuna kisima ambacho walikitumia kwa maji ya kunywa na kutawadha, kipindi hiki nilijikuta nikiishi maisha ya kiroho na kuisahau dunia na yaliyomo ili niogelee ndani ya bahari ya utawa wa Imamu Ali na maisha yake yasiopenda makuu, hali akiwa mtawala wa waumini na ni katika makhalifa waongofu. Sitaacha kueleza ukarimu na unyenyekevu ambao niliuona huko Al-Kufah, kwani hatukupita kwenye kundi la watu isipokuwa walisimama kwa heshima yetu na kutusalimia

55

na ni kama kwamba rafiki yangu alikuwa akiwafahamu wengi miongoni mwao, mmoja wao ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Al-Kufah alitualika nyumbani kwake ambako tulikutana na wanawe na tukalala kwao usiku mtulivu, nami nilijihisi kama kwamba niko miongoni mwa ndugu zangu na jamaa zangu. Walikuwa kila wanapozungumza kuhusu Massunni husema "Ndugu zetu Masunni" hivyo niliyapenda mazungumzo yao na nikawauliza baadhi ya maswali ya kuwajaribu ili niyakinishe ukweli wa maneno yao.

Tulielekea Najafu ambako ni umbali wa kilomita kama kumi kutoka Al-Kufah, na mara tulipofika niliukumbuka Msikiti wa AI-Kadhmiyyah ulioko Baghdad, minara ya dhahabu ilijitokeza iliyozunguka Quba la dhahabu tupu, na tukaingia kwenye Haram ya Imam Ali baada ya kusoma idhini ya kuingia kama kawaida ya Mashia wanaozuru. Niliona mambo ya ajabu kuliko yale niliyoyaona kule kwenye Msikiti wa Musa Al-Kadhim, na kama kawaida nilisimama nikasoma fatiha hali ya kuwa nina mashaka kwamba hili ndilo kaburi ambalo limehifadhi mwili wa Imam Ali, na kwa kiasi falani nilikinaika na ile nyumba ndogo ya kawaida aliyokuwa akiishi Imam huko Al-Kufah, na nikasema moyoni, "Haiwezekani kwa Imam Ali kuridhia mapambo haya ya dhahabu na fedha wakati ambapo kuna Waislamu wanaokufa njaa sehemu mbali mbali duniani, na hasa kwa kuwa niliwaona masikini njiani wakinyoosha mikono yao kwa wapita njia wakiomba sadaka, kwa hiyo moyoni nilikuwa nasema:- "Enyi Mashia ninyi ni wenye makosa, kubalini angalau kidogo kosa hili, Imam Ali ndiye ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu alimtuma kwenda kuyasawazisha makaburi, ni ya nini basi makaburi yaliyojengwa kwa dhahabu na fedha, kwa hakika kama siyo kumshirikisha Mwenyezi Mungu basi kwa namna fulani ni kosa kubwa ambalo Uislamu haulisamehi.

Rafiki yangu aliniuliza hali ya kuwa akinipa kipande cha udongo mkavu akaniuliza "Je unataka kuswali?" nilimjibu

56

kwa ukali, "Sisi hatusali pembeni ya makaburi" akasema "Basi nisubiri kidogo niswali rakaa mbili". Wakati namsubiri nilikuwa nasoma ubao uliotundikwa kwenye dharih na nilikuwa natazama ndani yake kupitia nguzo za dhahabu mara nikaona kuwa (ndani ya dharih) kumejaa sarafu na noti za kila rangi, dir-ham na Rial mpaKa dinar na Lira (zimo) na zote hizo zikitupwa (humo) na watu wanao uzuru ili kupata baraka kwa ajili ya kuchangia kazi za kheri zinazohusika na Maqam hayo, na nilidhani kwamba kutokana na wingi wake labda zina miezi kadhaa lakini rafiki yangu alinijulisha kuwa wahusika wa kusafisha Maqm ile huzichukua kila siku usiku baada ya sala ya Isha.

Nilitoka nikimfuata hali ya kuwa nimeshangazwa, nikitamani wanipe mimi sehemu yake au wazigawe kwa mafakiri na masikini ambao huko ni wengi mno.

Nilikuwa nikiiangalia kila upande ndani ya ukuta mkubwa unaozunguka Maqam, watu wengi walikuwa wakisali huku na huko na wengine wakiwasikiliza makhatibu waliokuwa juu ya mimbar, nilisikia vilio vya baadhi yao wakiomboleza kwa sauti za huzuni.

Niliona kundi la watu wakilia na kupiga vifua vyao na nikataka kumuuliza rafiki yangu kuwa wana nini watu hawa mbona wanalia na kujipiga, mara lilipitajeneza karibu yetu na nikawaona baadhi yao wanaondoa "marumaru " (kifuniko cha kaburi) katikati ya ukumbi unaozunguka Maqam na kumteremsha maiti hamo, basi nilidhania kuwa kilio chao hawa jamaa ni kwa ajili ya maiti huyu ambaye ni mtu muhimu kwao.

57

KUKUTANA NA WANACHUONI

Rafiki yangu aliniingiza ndani ya msikiti ulioko pembeni ya Haram umetandikwa wote kwa miswala, na kwenye mihrab yake kuna aya nyingi za Qur'an zilizonakshiwa kwa hati nzuri, niliwaona vijana wadogo wadogo wenye vilemba wamekaa karibu ya Mihrab wakisoma na kila mmoja wao mkononi mwake anacho kitabu. Basi mandhari hii nzuri ilinistajaabisha kwani hapo kabla sijawahi kuwaona Masheikh wenye umri huu, umri wao ulikuwa kati ya miaka kumi na tatu na kumi na sita na kilichowazidisha uzuri ni hilo vazi kwa kuwa wamekuwa kama miezi kutokana na kung'ara.

Rafiki yangu aliwauliza juu ya "Sayyid" wakamwambia kwamba anasalisha watu sala ya jamaa, nami sikutambua huyo "Sayyid" ambaye aliwauliza ni nani isipokuwa niliamini kuwa ni mmoja wa wanachuoni.

Baadaye nilitambua kwamba ni Sayyid Al-Khui ambaye ni kiongozi wa Chuo cha Elimu cha Kishia pia nilifahamu kwamba Laqabu ya "Sayyid" kwa Mashia ni jina la kila yule ambaye anatokana na kizazi cha Mtume (s.a.w.). Na Sayyid ambaye ni mwanachuoni au mwanafunzi huvaakilemba cheusi, amma wanachuoni wengine huvaa kilemba cheupe na Laqabu yao ni ya "Sheikh" na kuna watu wengine mashuhuri ambao siyo wanachuoni wanavilemba vya kijani.

Rafiki yangu aliwataka nikae nao wakati

58

atakapokwenda kukutana na Sayyid, walinikaribisha na kunizunguka nusu duara nami nikiwa naziangalia nyuso zao na nikahisi hawana dhambi na ni wasafi wa tabia zao, akilini mwangu nikawa naikumbuka hadithi ya Mtume (s.a.w.) "Mtu huzaliwa katika mila y a Kiislamu bali wazazi wake humfanya awe na mila ya Kiyahudi au Kikristo au Majusi na nikasema moyoni au humfanya awe Shia.

Waliniuliza kuwa mimi ninatoka nchi gani nikasema "Tunisia" wakasema "Je kwenu kuna vyuo vya elimu?" Nikawajibu, "Kwetu tunavyo vyuo vikuu na shule" Basi yalinimiminikia maswali toka kila upande na yote ni maswali makali na yenye kutatiza, sasa niwaambie nini maskini hawa ambao wanaamini kwamba katika ulimwengu wa Kiislamu wote kuna vyuo vya elimu ambavyo ndani yake munasomeshwa-Fiqhi Usuhid-din, Sheria na Tafsiri, na hawafahamu kwamba sisi katika ulimwengu wetu wa Kiislamu na katika nchi zetu ambazo zimeendelea na zimebadilika, tumezigeuza madrasa za Qur'an na kuwa shule za malezi ya watoto zinazosimamiwa na watawa wa Kikristo, je niwaambie kwamba wao bado wako nyuma kimaendeleo ukilinganisha nasisi?

Rudi nyuma Yaliyomo endelea