rudi nyuma Yaliyomo endelea

Mtume s.a.w.w. pia anaripotiwa kwa kusema: "Ikamateni elimu." Na alipoulizwa ni nini alichokuwa akimaanisha, alielezea kuwa yeye alikuwa akimaanisha uandishi.

Umma Salma R.A. ameripotiwa akiwa amesema: "Mtume s.a.w.w. aliulizia adim ya kondoo iliyotiwa dawa ili isioze iletwe mbele yake. Imam Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa pamoja naye. Baadaye aliyazungumza mambo mengi mno kwa Imam Ali ibn Abi Talib a.s. hadi kukaandikwa sehemu zote mbili za ngozi hiyo na vile vile kingo zake pia zilijaa maandishi."

Hadith zote hizi zinathibitisha wazi kuwa Mtume s.a.w.w. aliruhusu uandishi wa Hadith. Wapo Wanzuonini wengi ambao wanashikilia kwamba Mtume s.a.w.w. alikuwa ameharamisha hapo mwanzoni na kuruhusu hapo baadaye. Iwapo ndiyo hali ilivyo, je, ilikuwa ni kwa misingi gani ambapo baadhi ya Makhalifa waliharamisha uandishi wake na baada ya Hadith nyingi mno kuandikwa, tukamsingizia ati kuwa ni Mtume s.a.w.w. ndiye aliyeharamisha uandishi wa Hadith?

Rashid Ridha amezichambua Hadith zinazoharamisha na zenye kuruhusu kuandika Hadith.Yeye anajaribu kuthibitisha kuwa Hadith zinazopiga marufuku zinashinda zile zenye kuruhusu, hivyo Hadith zinazoelezea kuharamishwa kwa kuandika Hadith ni lazima zichukuliwe kuwa ni halisi na kweli. Yeye anaandika:

"Iwapo tutachukulia kuwapo kwa mgogoro baina ya Hadith zenye kupiga marufuku na zile zenye kuruhusu, basi mtu anaweza kusema kuwa mojawapo baina yao imetengua (batilisha) nyenzio kwa kuthibitisha kuwa Hadith zinazoharamisha zinashinda zile zenye kuruhusu, kwa sababu mbili: Kwanza, Sahaba walisimulia Hadith zinazoharamisha hata baada ya Mtume s.a.w.w. Pili, Sahaba hawa kuziandika Hadith; kwani iwapo wao wangalikuwa wameziandika, basi zingalikuwa zimetufikia sisi."

Sisi hatuwezi kukubaliana na maelezo hayo kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, Sahaba ndio waliosimulia Hadith zenye kuruhusu uandikaji wa Hadith pamoja na zile zinazoharamisha, na kama vile tulivyokwisha ona hapo juu, baadhi ya Sahaba waliendelea na kuziandika hizo Hadith.

Pili, sababu ya Sahaba kutojishughulisha na ukusanyaji wa Hadith kulitokana na kutolewa kwa amri ya kuharamishwa na Makhalifa wa kwanza na pili, na wala si kuwa ni Mtume s.a.w.w. aliyeharamisha.

Tatu, kwa kuwa haiwezekani sisi tukadai kuwa aina moja ya Hadith hizi zinashinda aina ya pili yake, sisi twaweza kusema kuwa ugomvi wao unazifanya zote ziwe zimebatilika na wala si kwamba mojawapo inaishinda ya pili yake.

Kuhusiana na kukubali kwa Abu Hurayrah kuwa Abd Allah ibn Amr alizoea kuandika Hadith, Rashid Ridha anasema: "Hakuna sababu ya kwamba sisi tuchukulie hivyo kama uthibitisho wa ruhusa ya kuandika Hadith, kwa sababu haijaelezwa katika Hadith kuwa Abdallah aliandika Hadith kwa kuruhusiwa na Mtume s.a.w.w.

Sisi tulikwishawaonyesha hapo juu riwaya zinazoonyesha kuwa Abd Allah ibn Amr kwa hakika alikuwa amepatiwa ruhusa kama hiyo. Zipo riwayat nyingi ambazo zimeshuhudia hayo, na mojawapo hapo juu Abu Hurayrah kwa kusisitiza anasema kuwa Abd Allah ibn Amr alikuwa amepatiwa ruhusa na Mtume s.a.w.w. kama hiyo.

Ama kwa upande wa upinzani, wengineo, kama Abu Zuhra, wenye mawazo ya kusema kuwa Mtume s.a.w.w. aliruhusu uandishi wa Hadith kufikia mwishoni mwa Utume wake ambapo hapakuwapo na hatari ya kuzichanganya Hadith pamoja na Aya za Quran. Iwapo sisi tutachukulia kusema kuwa matendo ya baadhi ya Sahaba, hasa yale ya Makhalifa, sisi hatuwezi kuikubalia hivyo, ama kwa upande wa pili, iwapo tutakubalia, basi itatubidi kuwalaumu baadhi ya Makhalifa kwa mienendo yao. Sisi hatujui iwapo Bwana Abu Zuhrah ataupendelea uelekeo upi.

  • MAONI YA BAADHI YA SAHABA KUHUSIANA NA UANDIKAJI WA HADITH
  • Mbali na imani ya baadhi ya Sahaba kuwa Hadith zisiandikwe, kikundi miongoni mwao kiliendelea kufanya hivyo. Ukweli huu ni dalili yenyewe inayoelezea kuwa kuharamishwa kwa uandishi wa Hadith ulitokana na Makhalifa na wala si Mtume s.a.w.w. kama inavyodaiwa. Miongoni mwa Sahaba waliokuwa wakiamini ruhusa ya uandishi wa Hadith walikuwa Amir al-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s. na mwana wake al-Hasan a.s. ambao si tu kwamba waliziandika Hadith, bali walitilia mkazo juu ya uandikaji wake pia.

    Abdallah ibn al-Abbass, imeripotiwa kuwa alizoea kusema, "Ikamateni (kuitia mahabusi) 'ilim kwa njia ya kuiandika." Harun ibn Antarah anaripoti kutokea baba yake kuwa abd Allah ibn al-Abbass baada ya kuitamka hiyo Hadith aliyomwomba aiandike.

    Salami anaripoti kuwa yeye aliona vipande vya maandishi kwa Ibn abbass ambamo alikuwa ameandika matendo ya Mtume s.a.w.w. kama vile ilivyokuwa imesimuliwa na Abu Rafi. Imeripoti kuwa Anas ibn Malik alizoea kumwambia mwanae:

    “Ikamateni ilim kwa kuiandika." Al-Kattani anaripoti kuwa Ayadh alizoea kusimulia ruhusa ya kuziandika Hadith kutokea Sahaba na Tabi'un. Hata hivyo, wengi wa Sahaba, inavyoonekana, ama walikuwa hawana uhakika katika yale waliyoyaandika kuhusu kuruhusiwa kwa kuziandika Hadith au hawakuwa na ari ya kuyazingatia na kuyasisitiza hayo kimatendo; uthibitisho huo ni kule kujiepusha kwao katika ukusanyaji wa Hadith.

    Zaazan anaripoti: "Mimi nilichukua baadhi ya maandishi (tasabih) kutoka Umm Ya'fur na kumwendea Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Naye alinifundisha hayo na baadaye aliniambia nikayarudishe kwa Umm Ya'fur."

    Imenakiliwa pia kwamba Ibn Abbass alizoea kuziandika Sunan za Mtume s.a.w.w. juu ya vibao vya kuandikia, ambazo alizichukua mwenyewe hadi pale palipokuwapo na mkusanyiko wa Wanazuoni. Pia imeanakiliwa kwa wingi (mutawatir) kuwa alipofariki aliacha vitabu vingi mno vinavyoweza kupakiwa juu ya ngamia mmoja.

    Kwa mujibu wa ripoti kuwa Abu Bakr aliandika baadhi ya Hadith baada ya Mtume s.a.w.w. na baadaye alizichoma moto, nayo pia inadalilisha kuwa uandishi wa Hadith ulikuwa ni desturi iliyokuwa inakubaliwa miongoni mwa Sahaba.

    Riwaya iliyonakiliwa kutoka Imam Ali ibn Abi Talib a.s. ambamo alisema kuwa yeyote aandikaye Hadith basi aandike pamoja na sanad yake navyo pia inaungana na mawazo hayo. Vianzio vyote vyote ni dhahiri kuwa idadi ya Sahaba walikubaliana kuwa uandishi wa Hadith ulikuwa umeruhusiwa. Ripoti kuhusu Sahifah ya Ja'abir ibn Abd Allah ambayo ilikuwanayo Hadith za Mtume s.a.w.w. pia inaunga mkono juu ya tabia na mazoea ya Sahaba katika uandishi wa Hadith zilikuwapo miongoni mwa Sahaba. Katika misingi hiyo, tunaweza kumalizia kuwa uandishi wa Hadith ulikuwa umekubaliwa na vikundi vya Sahaba na upinzani wa Mahalifa juu ya uandishi wa Hadith haukutokana na kukatazwa na Mtume s.a.w.w. kama inavyodaiwa, bali ulitokana na uamuzi wao wenyewe.

    9. AL-QURAN NA UANDISHI:

    Al-Khatib al-Baghdadi, ili kuunga mkono maelezo yake juu ya ruhusa ya uandikaji wa Hadith, anaelezea uthibitisho kutokea aya za Qurani.Katika misingi ya Quran inayotuamrisha kuandika vyote vile ambavyo vina hatari ya kuweza kusahaulika, yeye anaelezea kuwa Hadith, ambayo pia ipo hatarini kupotea, basi ni lazima ziandikwe. Katika uhusiano huu yeye anaelezea aya zifuatazo za Quran 2:282, 6:91 na 31:157

    Al-Tahawi, pia anaelezea akitoa Aya:

    "Wala msipuuze kuandika, mapatano yawe ni madogo au makubwa mpaka muda wake" (2:282) kuhusu uandishi wa madeni, anasema kuwa pale Mwenyezi Mungu anapotuamrisha kuandika madeni ili kuepukana na kutokezea mashaka na mizogo, na uhakika wa elimu ambavyo pia kuuchunga kwake ni vigumu kabisa na muhimu mno kuliko kurikodi madeni basi inasimama pamoja na umuhimu mno katika kuandikwa ili kuepukana na mashaka yaliyoelezwa hapo juu. Abu Hanifa, Abu Yusuf na Muhammad ibn al-Hassan al-Shaybani pia ni watu waliokuwa na msimamo kama huo.

    10. MTUME S.A.W.W. KUHARAMISHA UANDISHI WA HADITH NA SABABU ZA KWELI

    Uchambuzi wetu wa hapo mwanzoni unatuonyesha kuwa lawama zozote katika ucheleweshwaji wa uandishi wa Hadith hauwezi kamwe kutupiwa Mtume s.a.w.w. kwani riwaya zote zilizozuliwa juu yake haziwezi kamwe kukubaliwa kwa sababu mbali mbali. Katika jaribio hili, sisi tutakuwa tukitegemea mno juu ya riwaya zitegemewazo na Ahl al-Sunnah na penginepo tutatumia riwaya za Mashia. Ni mategemeo yetu kuwa msomaji ataweza kukadiria usahihi na ukweli wa uchambuzi huu kwa makini.

    Aisha anaripotiwa kusema: "Baba yangu alikuwa amezikusanya Hadith mia tano za Mtume s.a.w.w. . Asubuhi moja, alinijia na kusema, 'Lete Hadith zote zilizopo, kwako.' Nami nilizileta mbele yake. Yeye aliziunguza zote kwa moto na kusema, 'Nisije mimi nikafa huku nimekuachia vyote hivi.'''

    Imeripotiwa kwa mamlaka ya al-Zuhri kuwa: Umar alikuwa akitaka kuandika Sunan ya Mtume s.a.w.w. Yeye alikuwa akilifikiria kwa muda wa mwezi mmoja, alitarajia mwongozo kutokea kwa Allah swt katika swala hili. Siku moja asubuhi, alichukua uamuzi na kubainisha: "Mimi niliwakumbuka watu wote wale waliokwisha nitangulia, ambao waliandika na wakawa wamevutiwa mno katika yale waliyokuwa wameyaandika na ambao hatimaye walikiacha kitabu cha allah (yaani Quran)."

    Abd al-'Ala ansema: "Qasim ibn Muhammad ibn Bakr alizoea kutamka Hadith mbele yangu. alisema kuwa kulikuwapo na ongezeko katika Hadith katika zama za Umar. Naye Umar aliamrisha Ahadith zote zikusanywe, na zilipokusanywa, alizichoma moto zote kwa pamoja, akibainisha: Kama muthnat ya Ahl al-Kitab 'Mathnat' kama inavyoonekana kilikuwa ni kitabu ambacho Mayahudi walikiandika wao wenyewe na ambacho kilikuwa ni tofauti na Taurati. Hapa Umar alikilinganisha kitabu hicho pamoja na Hadith za Mtume s.a.w.w. , ambavyo alikuwa hataki ziwepo pamoja na Kitabu cha Allah (yaani Quran). Yahya ibn Ju'dah naye pia ameripoti kuwa 'Umar alidhamiriwa kuandika hadith na Sunan. Lakini alibadilisha dhamira yake na kutuma ujumbe wake katika miji yote, ikibainisha:

    "Yeyote yule aliyenacho chochote kutokana na hayo, ayateketeze yote."

    Imeripotiwa kutoka 'Urwah ibn al-Zubayr kuwa, "Umar ibn al-Khattaab alikuwa akitaka kuandika Sunan ya Mtume s.a.w.w.Kuhusiana na swala hili, alishauriana na Sahaba wengineo. Sahaba wote waliafikiana kuwa Hadith zote ziandikwe.Lakini Umar alikuwa akizingatia swala hilo hadi ikafika asubuhi moja alipochukua uamuzi wake wa kughairi hivyo, na akasema, 'mimi nilitaka kuandika sunan. Lakini baadaye nilijikumbusha watu walionitangulia ambao waliandika vitabu na kukiacha kitabu cha Allah (yaani Quran). Kwa kiapo cha Allah swt mimi sitakifunika Kitabu cha Allah kwa kitu chochote kile."

    Riwaya hii inatuonyesha kuwa Sahaba wote au angalu wale waliokuwa wameshauriwa walikubali juu ya uandishi wa Hadith. Lakini Khalifa, baada ya kufikiri kwa muda wa mwezi mmoja hivi, aliharamisha uandikaji wa Hadith katika misingi aliyoelezea yeye mwenyewe, jambo ambalo, bila shaka, halikuwepo pamoja na Sunnah za Mtume s.a.w.w..

    1. UPINZANI WA BAADHI YA SAHABA NA TABIUN KATIKA UANDISHI WA HADITH:

    Baada ya Khalifa kukataza uandishi wa Hadith, kwani mienendo yao ilichukuliwa na watu kama ni Sunnah, basi kikundi cha Sahaba na Tabiun pia walijiepusha na uandishi wa Hadith na walikuwa wakitegemea mno juu ya kile kimehifadhiwa akilini mwao.Wao walieneza Hadith kwa midomo tu na walichukia wazo la kuziandika. Kwao ilikuwa sivyo sahihi katika kuziandika Hadith za Mtume s.a.w.w. ambapo Quran na Mtume s.a.w.w. vyote vimeweka msisitizo mkubwa juu ya uandishi kwa ujumla.

    Abu Burdah anaripotiwa akisema kuwa baba yake alimwambia Abu Musa al-Ash’ari amletee chochote kile alichokuwa amekiandika kutokana na riwaya za baba yake.Na yote yalipoletwa, aliyaangamiza yote na alisema, "Wewe nae pia, kama sisi, lazima ukariri tu bila ya kuandika chochote."

    Abd al-Rahman ibn Salamah al-Jamhi anaripoti: "Mimi nilisikia Hadith ya Mtume s.a.w.w. kutoka kwa Abd Allah ibn Amr na niliiandika. Na baada ya kuhifadhi (kuikariri) akilini mwangu, nilikiteketeza kile nilichokiandika."

    Asim alisema: "Mimi nilitaka kumwachia Ibn Sirin kitabu, lakini yeye alikataa kukiweka, akisema kuwa yeye hakutaka kuwa na kitabu chochote karibu yake."

    Abu Nadhrah asema: "Mimi nilimwambia Abu Sa'id awe akituandikia sisi, yeye alijibu, 'mimi sitawaandikieni na mimi siwezi kuwafanyieni chochote kama Quran kwa ajili yenu. Wewe uichukue (Hadith) kutoka sisi vile tulivyopokea kutoka Mtume s.a.w.w. ' Abu Sa'id alizoea kusema, Simulieni Hadith miongoni mwenu, kwani mmoja wenu anamkumbusha mwingine vile kujali."

    Imeripotiwa kuwa mamlaka ya Ibn Abi Tamin kuwa Ibn Sirin na wenzake wasingeliziandika Hadith.

    Al-Harawi anaandika kuwa Sahaba na Tabiun walikuwa hawaziandiki Hadith na walikuwa wakizihifadhi akilini mwao, isipokuwa kitabu cha Sadaqa.

    Al-Nuwawi anaandika: "Mwelekeo wote wa Sahabah ulikuwa juu ya jihad, harakati dhidi ya matamanio ya mwili, na vile vile juu ya ibadah. Kwa hivyo wao hawakuwa na muda wa kunakili na kuandika (!). Kwa sababu kama hizo, Tabiun pia hawakuweza kuleta chochote kile kilichoandikwa (tasnif)."

    Abu Kathir al-Ghubri anamnakili Abu Hurayrah akiwa amesema:"Ahadith zisifichwe wala zisiandikwe."

    Abd Allah ibn Muslim anaripoti kuwa Sa'id ibn Jubayr alikuwa anachukizwa na uandishi.Vivyo hivyo, Ibrahim al-Nakhai alibainisha kuwa yeye kamwe alikuwa hajawahi kuandika chochote. Wakati alipoulizwa sababu ya kutoandika, yeye alijibu, "Wakati mtu anapoandika kitu chochote, basi huja kutegemea juu ya yale aliyoyaandika."

    Habib ibn Abi Thabit anaripotiwa kusema: "Mimi sina kitabu chochote ulimwenguni kote, isipokuwa kwa ajili ya Hadith ambayo ni kwa ajili ya sanda yangu."

    Al-Hassan ibn Abi al-Hassan wakati wa kifo chake alimwamrisha mfanyakazi wake aliwashe tanuru na kuvitupa vitabu vyote alivyokuwa navyo isipokuwa kimoja tu. Ibn Sirin alikuwa akisema: "Iwapo mimi nitahitaji kuandika kitabu basi nitaandika kitabu juu ya barua za Mtume s.a.w.w." Yahya ibn Sa'id anasema: "Mimi niliwaona Wanzuonini katika hali ambayo wanapingana juu ya kunakili na kuandika." Suleyman ibn Harb anaripoti: "Yahya ibn Sa'id alitujia na alikuwa akisema Hadith. Mwanzoni mwenzi wetu walikuwa hawaziandiki Hadith alizokuwa akizisimulia, lakini baada ya muda kupita, wao walianza kuziandika."

    Qasim ibn Muhammad ibn Abi Bakr alikuwa akimwambia Abd Allah ibn 'Ala asiwe akiandika Hadith. Sufyan ameripoti kuwa, pale alipoambiwa Amr ibn Dinar kuwa yeye alikuwa akiziandika Hadith za Amr, 'Amr alisimama na kusema, "Yeyote yule anayeziandika Hadith basi atoke hapa kwangu." Sufyan anasema kuwa kuanzia hapo hakuandika chochote kile alichokisikia kutoka Amr isipokuwa alikuwa akihifadhi tu.

    Imeripotiwa kutoka Ibn Tawus kuwa baba yake alisema:"mtu mmoja alimwuliza Abd Allah ibn Abbass, swali ambalo lilimfurahisha mno. Huyo mtu alimwomba Ibn Abbass amwandikie jibu lake.Lakini Ibn Abbass alisema kuwa wao kamwe hawaandiki chochote kile kilicho cha 'ilim' Riwaya hii ipo katika mzozano pamoja na riwaya zinginezo zilizotangulia za Ibn Abbass.

    Malik ibn Anas anaripoti kuwa Ibn Musayyab alipofariki, hakuacha hata kitabu kimoja. Vivyo hivyo ndivyo ulivyokuwa ukweli wa Qasim ibn Muhammad, Urwah ibn al-Zubayr na Ibn Shihab al-Zuhri.Mansur ibn Mu'tamir ameripotiwa akiwa amesema: "Mimi sijaandika chochote hadi leo."Na taarifa kama hiyo hiyo ipo imeripotiwa kutokaYunus ibn Ubayd.Imeripotiwa kuhusu Ibn Abi Dhu'ayb kuwa yeye alikuwa akikariri tu Hadith. Yeye alitokana na tabaka la tano na aliishi katikati ya karne ya 2 A.H./8 A.D. Imesemwa kuhusu Sa'id ibn Abd al-Aziz alikuwa haandiki chochote.

    Ismail ibn Ayyash, aliyetokana na tabaka la sita alikuwa amehifadhi akilini mwake kiasi cha Hadith elfu kumi lakini hakuandika hata moja. Abu Hatim anaripoti kuwa yeye kamwe hakuona chochote kilichoandikwa mikononi mwa Abd al-Walid al-Tayalisi.Wote hao walikuwamo katika tabaka la saba na walichukia mno uandishi wa Hadith. Pia imesemwa kuwa al-Nufayli kamwe hakuonekana pamoja na kitabu chochote. Vile vile Sahib al-Basri inasemekana alichukia mno uandikaji.

    12. KITABU KINGINECHO MBALI NA QURAN:

    Kama itakavyoonekana kutokana na riwayah zinazotokana na wale wote waliokuwa wakizingatia kuharamishwa kwa Hadith kuandikwa, kwamba madai yao yote ya hasa kuficha ukweli yalikuwa ni khofu ya kutokezea kwa 'kitabu kinginecho mbali na Quran', na kwamba matokeo yake yatakuwa ni kutumika vitabu vingine na kuachwa kwa Quran. Hapa sisi tutajaribu kuchambua uhakika wa khofu kama hiyo na itaonekana wazi kuwa hayo yalikuwa ni hoja za kutaka kuuficha ukweli na wala hapakuwapo na makusudio mengineyo. Al-Quran na Sunnah vinakamilishana, na kama vile Waislamu wote wanavyoelewa kuwa kimoja hakikamiliki bila ya kingine - isipokuwa tu labda wale wenye kusema kuwa: "Kitabu cha Allah kinatutosha."

    Jambo ambalo linahitaji kuzingatiwa hapa ni kuwa wale mabingwa wote wa kuharamisha uandishi wa Hadith iwapo wao walikuwa ni Makhalifa au wale waliofuata katika swala hili na waliweza kutumia hivyo kwa kuhalalisha tendo lao- walikuwa wakijua kauli ya Mtume s.a.w.w. kuhusu "Kitabu ubavuni mwa Kitabu cha Allah swt." Hata hivyo kimakosa au kimakusudi wao waliitumia visivyo hivyo kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.

    Ni kweli kuwa katika zama za uhai wa Mtume s.a.w.w. baadhi ya Sahaba waliweza kujipatia vitabu vya Taurati na vitabu vinginevyo vya Mayahudi. Na Mtume s.a.w.w. alipokuja kupata habari kuhusu hayo, aliwaambia wasivilinganishe sambamba na Kitabu cha Al-lah, al-Quran. Katika uhusiano huu itatubidi kuzingatia riwaya ifuatayo iliyonakiliwa na Jaabir. Jaabir anaripoti kuwa Umar al-Khattab alileta nakala moja ya Tawrati mbele ya Mtume s.a.w.w. na kusema: "Hii ni nakala ya Tawrati ambayo mimi huwa ninaisoma." Mtume s.a.w.w. alikaa kimya lakini rangi ya uso wake ulibadilika. Abu Bakr aliiona hali hiyo, na alimwambia Umar, "Mama yako alie katika kilio chako, je, hauoni uso wa Mtume s.a.w.w.! Umar alipouona uso wa Mtume s.a.w.w. . akasema, "Mimi najikinga na Mungu kwa ghadhabu za Mtume s.a.w.w. Mimi namkubalia Allah kama mmiliki wa vyote, Islam kama Dini na Muhammad kama Mtume." Juu ya hayo Mtume s.a.w.w. alisema: "Kwa kiapo cha Mungu, iwapo Musa angalitokea hapa na wewe umfuate yeye kwa kuniacha mimi, basi ungalikuwa umepotoka njia ya haki. Iwapo Musa angalikuwa hai na kuniona mimi, angalikuwa akinifuata mimi."

    Mapokezi haya yanatuonyesha Mtume s.a.w.w. alivyokuwa amekasirishwa kwa sababu Umar alikuwa amekichukulia kitabu kingine sambamba na Quran. Katika mapokezi mengine kama haya, mtu kutoka Ansaar anachukua nafasi ya Abu Bakr. Inawezekana kuwa mapokezi hayo mawili yanatuelezea matukio mawili tofauti na kwamba tunaweza kuelewa kuwa matukio hayo mawili yametokea katika nyakati mbalimbali.

    Imepokelewa kutoka Abu Qalabah kuwa mara moja Umar ibn al-Khattab alipita karibu na mtu aliyekuwa akisoma kitabu. Baada ya kumsikiliza kwa muda mfupi, Umar alipendezewa na kile alichokisikia. Basi alimwomba mtu yule amwandikie kutoka kitabu hicho. Mtu huyo alikubali kumwandikia hivyo. Hapo Umar alilinunua jani na kumletea huyo mtu, ambamo mtu yule aliandika kwa kujaza sehemu zote mbili. Baadaye Umar alifika mbele ya Mtume s.a.w.w. na kumsomea yaliyokuwa yameandikwa. Papo hapo rangi ya Mtume s.a.w.w. ilibadilika kwa ghadhabu. Basi hapo mtu aliyetokana na Ansaar alimwambia Umar: "Mama yako alilie kilio chako! Je, hauoni uso wa Mtume s.a.w.w. ?" Kwa hayo Mtume s.a.w.w. alisema: "Mimi nimetokezea kama Mtume, kama mfunguzi (fatih) na kama mfungaji (khatim), na mimi nimeleta kila kitu ambacho ilinibidi kujanacho (hivyo hakuna kilichobakia hadi nyinyi) kwenda kuvitafuta kutoka kwa watu wengineo."

    Imeripotiwa kwa mamlaka ya al-Zuhri kuwa Hafsah binti yake Umar, alikileta kitabu chenye Hadith (masimulizi za Mtume Yusuf a.s. mbele ya Mtume s.a.w.w.. Yeye alianza kukisoma huku Mtume s.a.w.w. akiwa akisikiliza na uso wake kubadilika rangi kuwa mwekundu. Hapo ndipo Mtume s.a.w.w. aliposema, "kwa haki ya Mungu, iwapo Yusuf mwenyewe angalikuja hapa na iwapo wewe ungalimfuata yeye na kuniacha mimi basi wewe ungalikuwa umepotoka."

    Riwaya hizi zote zinatuonyesha kile alichokuwa akikichukia Mtume s.a.w.w. kilikuwa ni maandishi mapotofu ambayo athari zake zilikuwa ni kueneza imani potofu za Mayahudi ambazo zilikuwa zikiitwa Israilayyat - miongoni mwa Waislamu. Mtume s.a.w.w. alikuwa hataki vile vitabu vya Mayahudi viwe sambamba na Quran Tukufu, maneno yote ambayo yalikuwa ni maneno ya Allah swt; katika vitabu vya Mayahudi kulikuwamo na visa na Hadithi za uwongo na zenye imani za ushirikina na kuamini uchawi, vinaweza kumfanya mtu apotoke na njia iliyo na mafundisho halisi ya Quran ambayo yameelezwa mbele yao.

    Riwaya zilizoelezwa hapo juu pia zinaonyesha kuwa Khalifa na binti yake walikuwa wakipendezewa mno na usomaji wa vitabu kama hivyo na mara nyingine ilitokea kuchunguzwa na Mtume s.a.w.w. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, tunaona kuwa baadaye ambapo Ka'aba al-Ahbar, Myahudi aliyesilimu kidhahiri tu, alipomwijia Umar na kumwomba ruhusa ya kuisoma Tawrati, Umar alimwambia: "Iwapo wewe unajua kuwa hiyo ndiyo Tawrati aliyokuwa ameteremshiwa Musa a.s. huko katika Milima ya Sinai, basi uisome usiku na mchana."Na haya ndiyo yaliyokuwa majibu ya Umar baada ya Mtume s.a.w.w. kumkataza yeye mwenyewe kutoisoma Tawrati wala mambo yoyote kama hayo.

    Zipo riwaya zingine ambazo zinathibitisha fikara zetu kuwa Mtume s.a.w.w. alichokuwa akiharamisha kuwapo kwa kitabu sambamba na Quran yalikuwa ni maandiko ya Mayahudi yaliyokuwa yakitumiwa na Waislamu. Ipo imeripotiwa kuwa Abdallah ibn Mas'ud aliposikia kuwa watu walikuwanacho kitabu ambacho walistaajabishwa na yale yaliyokuwemo,basi alikichukua na kuki teketeza, akisema:"Watu wa vitabu (Ahl al-Kitaab) waliangamia kwa sababu wao walikuwa wakitegemea mno maandiko ya Wanazuoni wao (ulamaa) na walikuwa wamepuuzia Kitabu cha Allah (yaani Tawrati)" Neno ulamaa katika Waarabu wa zama hizo ilikuwa ikimaanisha Wanazuoni wa Kiyahudi na Kikiristo na vitabu vinavyozungumzwa katika riwaya hizi ni maandishi ya Kiyahudi.

    Riwaya ifuatayo inaelezea vizuri zaidi swala hili. Murrah al-Hamdani anasema: Abu Murrah al-Kindi alikileta kitabu kutoka Syria (al-Shaam) na alimpatia Ibn Mas'ud alikipitia kitabu hicho, akaleta maji na kuyaosha yale maandishi yaliyokuwa yameandikwa katika kitabu hicho. Na hapo alisema, 'Watu walioishi kabla yenu waliangamia kwa sababu ya kuvifuata vitabu kama hivi na kukiacha cha Allah (yaani Quran)" Al-Husayn anasema, "Kwa hakika asingeteketeza maandishi hayo kama yangalikuwa ni Quran na Sunnah (yaani Hadith za Mtume s.a.w.w. Bali kilikuwa ni kitabu cha Ahl al-Kitaab."

    Imam Ali ibn Abi Talib a.s. ameripotiwa akisema: "Yeyote yule miongoni mwenu aliyenacho kitabu (mbali na Quran na Sunnah) akiteketeze.Watu waliowatangulia nyinyi waliangamizwa kwa sababu ya kufuata masimulizi ya Wanazuoni wao huku wakikiacha Kitabu cha Allah (yaani Quran)."

    Al-Imam al-Sadiq a.s. ameripotiwa akisema: "Baadhi ya Wanazuoni wapo wanafuatilia riwaya za Mayahudi na Wakristo, huku wakitegemea kuongeza elimu yao. Watu kama hao, nafasi yao ipo chini mno ndani mwa Jahannam. Imeripotiwa kwa mamlaka ya amr ibn Yahya ibn Ju'dah kuwa kilipokuwa kimeletwa kitabu mbele ya Mtume s.a.w.w. alisema: "Inatosheleza kwa upumbavu na upotofu wa Ummah kwa kuyaacha yale yaliyokuwa yameletwa na Mtume wake na kuanza kuangalia yaliyokuwa yameletwa na Mitume mingine." Riwaya hii pia inatuonyesha aina ya kila kitabu kilichokuwa kimeletwa mbele ya Mtume s.a.w.w. na pia kutupia nuru juu ya maana ya:

    'Kitabu sambamba na Kitabu cha Allah (yaani Quran).'

    Vile vile Ibn Abbass anasema: "Je utawaulizaje swali Ahl al-Kitaab kuhusu matatizo wakati ambapo Al-Qur’an ipo miongoni mwetu ?"

    Riwaya na masimulizi na mapokezi yote haya yanaonyesha kuwa Mtume s.a.w.w. aliharamisha kutayarishwa kwa kitabu sambamba na Quran huku akitahadharisha hatari ya uingiliaji wa Israiliyyat na kamwe, vyovyote vile, hakumaanisha Sunnah yake, ambayo ipo imeshikamana (wajib al-'ita'ah), kama vile wanavyokubalia Waislamu wote.

    Mabishano yetu yanazidi kupata nguvu kwa uhakika kuwa Wanazuoni wa Hadith wa Islam walikuja baadaye wakaziandika na kuzikusanya Hadith. Ama kwa mfano wa wale kama 'Urwah walichoma moto Hadith walizokuwa wameziandika kwa kudai kuwa "sisi hatutaki kuwanacho kitabu sambamba na Kitabu cha allah (al-Quran),' basi ni lazima tuseme kuwa wao walitenda kwa sababu ya kutoelewa vyema mafhumu ya kauli ya Mtume s.a.w.w.

    Kama itakavyokuwa imeonekana hapo awali kuwa sisi hatuwezi kusema kuwa Mtume s.a.w.w. ndiye aliyehusika na uharamishwaji huo wa kuziandika Hadith; na msimamo kama huo unaweza kuchomoza maswali ambayo hayana majibu. Ilieleweka hapo awali kuwa baadhi ya Makhalifa walihusika moja kwa moja katika swala hili la kutoziandika Hadith na wao ndio walioharamisha uandishi wa Hadith. Hapa, baada ya kutaja sababu zilizotolewa nao kwa kuchukuwa hatua kama hiyo, sisi tutajaribu kutafuta maelezo yake. Baada ya kuthamini sababu chache zilizotolewa nao katika swala hili, sisi tutajaribu kuelezea kile tunachokiona kuwa ndiyo sababu maalum kuhusiana na uharamishwaji huo, pamoja na uthibitisho wa kutosheleza katika kuugana na maelezo yetu.

    rudi nyuma Yaliyomo endelea