rudi nyuma Yaliyomo endelea

Kuanzia leo hii tena hivi sasa, tufanye juhudi za kuweka jiwe la msingi wa dola lenye sheria za Kiislamu. Tumwombe Mungu, tuwalinganie watu, tuzitawanye fikira za Kiislamu, tuyatoe mafunzo ya dini yetu pangoni yalimokuwa yamefichwa na walaghai. Tuwatafute watakaotusaidia kwa kututia hima ili mawimbi ya maelekezo kwenye usawa yawepo, na maongozi yaliyopangika kwa ajili ya serikali yetu yapatikane. Kwa kufanya hivyo, taathiri nzuri itawaathiri Waislamu wote wenye kushikamana na dini yao namna mlivyoathirika nyinyi kwa kujitokeza kutaka kuunda serikali yenye maongozi ya Kiislamu.

Kufanya tablighi na kuwafunza watu ni vitendo viwili vya msingi na muhimu katika shabaha yetu. Hivyo, ni juu ya mafaqihi kuyabainisha masiala, hukumu za kisheria, nidhamu za Kiislamu na kuzipanda nyoyoni mwa watu ili kuleta udongo mpya ambao nidhamu (mfumo) na sheria za Kiislamu zitaweza kustawi juu yake. Kama mnavyokumbuka hadithi ya Mtume Mtukufu SAW aliponena kwamba makhalifa (mafaqihi) wake "Wawafunze watu" hadithi zake.

Wajibu wetu leo hii ni mkubwa zaidi tena zaidi kuliko siku zilizopita nyakati za kupambana na ukoloni mamboleo, wakoloni wenyewe, vibaraka wao wahaini, Wasayuni na wanafiki walioutia Uislamu doa baya.

Jamani, sisi hivi leo tunawaona Mayahudi (Wasayuni) jinsi wanavyoichezea Qur'ani. Maneno yake wanayageuza na kuyaweka mahali pasipo pake katika chapa wanavyovichapisha na kuvigawanyia watu walio katika ardhi yetu waliyoiteka na kwingineko[44]. Ni juu yetu kuifichua hiana hii, na tupige mayowe na kelele kwa sauti kubwa yenye kishindo mpaka watu wote wafahamu kwamba, Mayahudi na mabwana zao wa Ulaya wanaufanyia Uislamu hila na wanatayarisha mbinu za kuwafanya Mayahudi wautawale ulimwengu wote. Ninachelea sana wasije wakalifikia lengo lao hilo. Kwa ajili ya udhaifu wetu na unyonge wetu (wa kijitakia) huenda siku moja akatokea Myahudi kuihukumu (kuitawala) nchi yetu — Mungu asijaalie.

Kwa upande mwingine, wataalamu wa mambo ya Mashariki wameungana na mashirika ya kikoloni ya Magharibi kuupindua uhakika wa dini ya uislamu na hivyo kuibomoa.

Wahubiri wa kikoloni kwa upande wao, nao wanakwenda juu chini kuwapotosha vijana wetu kokote waliko kwa ghururi mbalimbali ili wawe mbali nasi. Sisemi wao wanajitahidi kuwafanya Wakristo au Mayahudi, kwani yawatosha kwao kuwafanya vijana wetu mafisadi na wenye kutupa dini pamoja na kutojali. Jambo hili lawatosha wakoloni.

Mjini Tehran (Iran) pekee, vituo vya Wakristo, Wasayuni na Mabahai vinazidi kuongezeka na kusambaa kwingineko ikiwa ni hatua mojawapo ya kuwapotosha watu na kuwaweka mbali na dini ya kiislamu na misingi yake.

Je, kuvivunjavunja vituo hivi si katika wajibu wetu? Je, itatutosha tu kuumiliki mji wa Najaf (Iraq) ambao tena haumo mikononi mwetu? Je, tutakaa kitako tu na kushinda mjini Qum na kusoma majilisi ya maombolezi kwa kuuawa Imam Husayn AS pekee, au itatupasa pia tufanye kazi kwa bidii na uthabiti ili kuwalinda watu wetu?

Enye vijana nmaosomea ushekhe! Amkeni! Muwe watu walio hai, na fanyeni kwa ajili ya kuyahuisha maamrisho ya Mungu wenu. Pia jitahidini kuihifadhi nidhamu zake. Enyi vijana wa kame hii, mawazo yenu yawekeni pamoja na mambo yenu. Kisha mfanye kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na Yeye pamoja na Mtume Wake na watu wema (wasalihina) watayashuhudia matendo yenu.

Jikamilisheni! Mambo ya kuwagonganisha yawacheni, jiepusheni kurarama hadharani na msimamieni wajibu wenu vilivyo. Uokoeni na unusuruni Uislamu, kwani Uislamu unawalilieni nyie, na waokoeni Waislamu kutokana na hatari zinazowakodolea macho.

Haya basi, hao mashekhe wa kujigamba wanauua Uislamu kwa jina la (kusingizia) Uislarnu na kwa jina la (kumsingizia) Mtume Muhammad SAW, madai yao na wao wenyewe hawako mbali na ukoloni na tayari kila kukicha wanazidi kutawanyika kote ulimwenguni. Wametapakaa sehemu zote za mashambani na vijijini, na wakawarejelea watoto, vijana, na mabarobaro wetu kisha kuwapoteza kabisa.

Amkeni mkawaokoe waliomo upotevuni, wasaidieni, wafanyieni hima ya kuwaokoa, waokoeni na mwaauni. Jilazumisheni kuieneza elimu yenu, kwani yaliyotajwa katika Qur'ani na katika hadithi kuwasifu na kuwatukuza mafaqihi hakika si jingine bali kwa ajili ya anayoyafanya faqihi yakiwemo kuwafunza wengine na kuwaokoa waliopotea. Fanyeni bidii zenu zote, zitoeni kule ziliko ili maeleweko ya Uislamu na nidhamu zake ziwafikie watu wote.

Kadhalika tufanye bidii tukifunue kifuniko kilichofunikizwa Uislamu na maadui wa Uislamu. Pia tuyaondoe yote yaliyosingiziwa. Tusipofanya hivyo, yaani tusipoyafanya hayo yote, kamwe hatutaendelea wala kufaulu.

Mbali na hayo, tunapaswa tuwe tukipeana nasaha sisi kwa sisi, na wengine pia tuwape nasaha nao wawausie wengine ili tuyaondoe malimbikizo yote yaliyoshindiliwa Uislamuni, na shaka nyingi zilizojazwa na maadui nyoyoni mwa watu hata mwa wenye maendeleo yao tangu kame nyingi zilizopita.

Vijana wa karne hii tunawausia wazieleze karne zijazo utukufu wa dini ya kiislamu, sheria zake kuhusu jamii na mambo yote yaliyopangwa na Uislamu. Kadhalika wawazungumzie watu sheria za Islamu juu ya haja ya kuunda serikali ili watu wote waujue Uislamu ni nini na ulituletea kanuni gani na sheria zipi.

Vyuo vikuu vya Kiislamu vilivyoko Qum, Mash'had na kwingineko, vinapaswa kuwaonyesha watu njia ya kuwapeleka kutambua Uislamu wa hakika, wazisambaze fikira zake ili kila mmoja aelewe.

Jamani, watu hawaujui Uislamu. Wala hawaelewi lolote wala chochote juu yake. Kwa hivyo, mnapaswa kujijulisha kwao na itikadi zenu na yale yanayopaswa kutekelezwa na serikali yenu yenye maongozi ya Kiislamu. Ulimwengu wote ujulisheni mambo hayo yote hata wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wanayaelewa mambo kuliko watu wote. Pamoja na hayo, muwe na imani ya ushindi kwamba matokeo ya kuunda serikali ya Kiislamu yatakuwa mema na yatashangiliwa na kupokewa kwa heshima kuu. Kadhalika muwe mkiwathibitishia kwamba, wakiyakubali maneno yenu watapokewa na Uislamu kwa heshima wanayoistahili.

Wanavyuo vikuu ndio maadui wakuu wa kutawaliwa kiharamu, kulimbikizwa, hiana, udokoaji wa mazuri ya wengine yakiwemo mapato ya nchi, na ulaji wa haramu. Na wataona katika Uislamu ambao mnawapelekea, na katika mafunzo yake, sheria zake, maamuzi, iktisadi (uchumi) na hali ya utangamano wa kijamii, watayaona yale ambayo yanawafaa kujiunga nayo.

Haohao wanachuo wanainyoshea mikono yao Najaf (Iraq) — makao ya elimu ya Kiislamu — kuomba msaada wa kufahamu uhakika wa dini yao! Je, ni halali kwetu tuwe kimya bila kutaharuki hadi wanavyuo vikuu hao waje kutunyang'anya wajibu wetu wa kuamrisha mema na kukataza mabaya huku sisi tukiwa katika lepe (usingizi) hatuna habari? Je ukimya wetu huu si katika jumla ya mabaya yanayopaswa kukanywa? Je hatuoni aibu watu kama sisi kuyaacha mambo hovyo mpaka vijana kutoka Ulaya waunde vyama vyao vya Kiislamu huko ugenini ili kudai msaada wa kimaendeleo, uongozi na maelekezo kisha waje kutuelekeza sisi?

Tunapaswa kuwakumbusha watu namna serikali ya Kiislamu ilivyokuwa siku za mwanzo wake. Tunapaswa tuwaambie kwamba, uamuzi wa kesi ulikuwa ukitolewa misikitini wakati Uislamu ulipokuwa kila mahali mkiwemo Iran, Misri, Hijazi (Saudi Arabia), Yemen na kwingineko. Ama mambo yalipobadilika na kuwa mikononi mwa watu wengine — wanaodai kuwa Waislamu hali ni waongo — ukhalifa na serikali za kisheria viligeuka na kuwa chini ya wafalme wapumbavu wasio na maana.

Tunapaswa kuyasema hayo yote na kisha tubaini urembo wa serikali ya Kiislamu tunayodhamiria kuiunda. Palepale tuzifafanue sifa za mtawala, wajibu wake, yanayomhusu na hulka zake. Lazima tuwaeleze siasa yetu.

Kiongozi na mtawala wa umma baada ya Mtume Mtukufu SAW alikuwa Sayyidna Ali bin Abi Talib AS, ambaye alimkemea nduguye Aqil[45] na akamlindisha chuma ili asiyafanyie tamaa mali ya umma wa Kiislamu. Na akamlaumu bintiye alipoazima mkufu kutoka kwa hazina ya umma. Akasema, "Lau si kwamba yeye ameuazima na kudhaminiwa, angekuwa mwanamke wa kwanza kabisa katika ukoo wa Hashim kukatwa mkono wake (kwa wizi)." Kisha aliuchukua na kuurudisha kwenye hazina.

Hakimu kama huyo ndiye tumtakaye. Na kwa ajili ya mambo kama hayo, na wafanye bidii wenye kufanya. Na kwa ajili ya jambo kama hilo, na washindane wenye kushindana.

Sisi hatumtaki kiongozi au mtawala atakayetuamrisha kufanya jambo fulani isipokuwa tu awe ametutangulia kufanya. Wala hatumtaki anayetukataza mambo fulani isipokuwa awe amejizuia nayo yeye kwanza.

Tunamtaka kiongozi atakayeleta usawa baina yetu sote mbele ya uadilifu wakati wa kutuamua. Tunamtaka yule atakayeleta usawa baina ya watu pasina kuchagua au kupendelea. Tunamtaka yule atakayetoa hukumu ya uadilifu na haki hata kama ikiwa si kwa maslahi yake au jamaa zake. Tunamtaka kiongozi asiyewatawala watu kimabavu na atakayewahesabu jamaa zake sawa na raia wengine. Tunamtaka hakimu atakayemkata mkono mwanawe yeye mwenyewe atakapoiba. Hakimu atakayemchukulia hatua ya kumtia kitanzi nduguye au dadake pindi afanyapo biashara ya magendo ya kasumba au dawa za kulevya kama anavyowachukulia hatua watu wengineo wanaopatikana wakifanya biashara ya magendo ya kuuza dawa hizo hizo.

JAMII YENYE KUHUDUMIA UISLAMU NA MAFUNDISHO YAKE

Hukumu nyingi na mikusanyiko ya ibada inaweza kutoa huduma kadha wa kadha za kijamii na kisiasa. Kwa kawaida, ibada za Kiislamu zinashirikiana na mipango ya siasa ya jamii. Kwa mfano, sala ya jamaa, mkusanyiko wa watu wakati wa msimu wa Hija na sala ya Ijumaa, mbali na athari zake za kiroho na mapenzi baina ya watu, pia zinaleta matokeo mema na athari za kisiasa kwa watu.

Uislamu ulianzisha mikutano ya namna hii, na ukawahimiza na kuwasisitisa watu wawe wakihudhuria, ili maarifa ya kidini yaenee, pia yaenee mapenzi ya kindugu, urafiki wa kujuana baina ya watu ustawi, na fikra za Kiislamu zimee, zikue, zikomae na hatimaye kuiva tayari kutoa matunda ili kutoa manufaa, ili waweze kuyatatua matatizo yao ya Kiislamu, ya kisiasa na ya kijamii.

Katika mataifa yasiyo ya Kiislamu, mamilioni ya pesa za mapato ya nchi hutolewa kwa ajili ya kufanyika mikutano ya lengo kama hili. Mikutano kama hiyo ikifanywa, aghlabu huwa haina msingi wa mapenzi, udugu na uaminifu, kinyume na tunavyofanya sisi katika mikutano yetu ya Kiislamu.

Uislamu tayari uliwawekea watu hisia ya kindani sana inayomfanya mwenye kusafiri kwenda Hija ajihisi kuwa na maisha matamu ya hali ya juu, na kumfanya ahudhurie sala za jamaa, Ijumaa na Idi kwa furaha na shangwe. Kwa hivyo, ni juu yetu tuichukulie mikutano ya namna hii kuwa fursa ya pekee ya kwenda kuiasisi misingi na imani ili tukiwa huko tueleze itikadi zetu, sheria, hukumu na nidhamu mbele ya wote waliohudhuria ambao kwa kawaida huwa ni watu wengi sana.

Tunapaswa kuufaidi wakati wa msimu wa Hija, na tutoe wakati huo matunda yaliyo bora katika kuwalingania watu waungane na kuwataka wautawalishe Uislamu kati ya watu wote. Wakati huohuo, tanapaswa kuyachungua matatizo yetu, na tuyang'oe mashina yote yaliyoukaba Uislamu, na kufunua kifuniko kilichowekewa juu yake. Kadhalika tunapaswa kufanya bidii ili kuikomboa ardhi yetu iliyotekwa na kukaliwa huko Palestina na kwingineko.

Hapo mwanzoni mwa Uislamu, Waislamu walikuwa wakijichumia matunda mema katika mikutano yao ya sala za jamaa, Ijumaa, Idi na katika ibada zao huko Hija.

Zamani, hotuba zilizokuwa zikitolewa misikitini siku za Ijumaa, katika sala za Iddi na katika hafla zinginezo, hazikuzungumzia tu habari za siku ya Kiyama, maonyo juu ya adhabu za motoni na sura fulani fulani kusomwa au dua ndogo ndogo au kubwa kubwa kama tuonavyo siku hizi. Isipokuwa hotuba hizo zilikuwa zikileta taathira kubwa za kuwaandaa watu (Waislamu) kwenda mapiganoni kwa ushujaa na kwa ujasiri. Nao wapiganaji walikuwa wakiondoka misikitini au majumbani mwao kwenda kwenye mapigano bila ya kushikwa na hofu wala kuogopa ufukara, maradhi, kufa au kupoteza kitu chochote, maana wao walikuwa hawamwogopi yeyote wala chochote isipokuwa Mwenyezi Mungu tu. Watu kama hao ndio wanaoandikiwa ushindi.

Hebu angalieni hotuba za Amirul Mu'minin ili mjue kwamba, hotuba hizo zilikuwa za kuwaongoza Waislamu kwenye uwanja wa vita, na zilikuwa za kuwahimiza watu kujitoa mhanga kwa ajili ya dini yao, na zilikuwa vilevile na lengo la kuyaondoa matatizo ya kimaisha. Lau hotuba za Ijumaa, lengo lake, nafsi yake na mazingatio yake yangeendelea na kudumu hadi leo hii, mambo haya tunayoyaona hayangefikia kiwango hiki.

Tunapaswa kuzirudisha jamii zote kama zilivyokuwa. Tuzidumishe kwa maelekezo na kwa uongozi wa kuzifikisha kwenye ufanisi na ushindi. Tukifanya hivyo, harakati za kiitikadi na kisiasa za Kiislamu zitaweza kutimia na kuupanua uwanja uwe mkubwa na hatimaye kuenea kila mahali.

ASHURA MPYA

Dini ya Kiislamu ina makumbusho kwa ajili ya watu kuyakumb'uka, kuyahuisha na kuyaadhimisha. Moja katika makumbusho hayo ni maombolezi ya siku ya Ashura[46]. Umati wa watu hukusanyika katika mahafili kusikiliza hotuba na mashairi yanayotolewa na wahubiri stadi, na hupiga vifua vyao ili kuomboleza na kuadhimisha Ashura — siku ambayo Imam Husayn AS alijitoa mhanga kuiokoa dini ya Kiislamu.

Nyinyi leo pia mfanye vivyo hivyo. Wakusanye watu, pandeni mimbari na wahubirieni kwamba Uislamu una mfumo ambao unahitaji kuundiwa serikali yake ili uhuike na ustawi.

Lau mtauzungumza Uislamu kwa roho safi, mwafahamishe watu mizizi yake, sheria zake na nidhamu zake, bila shaka watu wote wataipokea dini hii na wataifuata. Kwani hata Mwenyezi Mungu anajua kwamba, waipendao dini hii ya Kiislamu ni wengi sana, lakini hukumu zake nyingi hawazijui wala hawazielewi. Jambo hili hata mimi mwenyewe nimelijaribu na kulihakikisha.

Wakati ninapowahutubia watu, mimi mwenyewe hushuhudia mabadiliko na taathira nyusoni mwa watu na rohoni mwao. Kwa sababu, watu wote wamechoka kutokana na maisha wanayoishi — maisha ya kuwatia hofu kila kukicha kutokana na madhalimu. Kwa hivyo, wao wanamhitaji mtu ambaye atazungumza kwa niaba yao kwa ushujaa na ujasiri.

Enyi vijana wa Kiislamu, muwe washupavu na wakakamavu wakati mnapowaeleza watu haja na hoja zenu ili mwashinde adui zenu pamoja na silaha zake, askari wake na walinzi wake. Waelezeeni watu ukweli na mwazindue. Watieni moyo wa jihadi nyoyoni mwa wachuuzi wa sokoni, walio barabarani, wafanyakazi, wakulima na wanafunzi, hasa wa vyuo vikuu. Watu wote watakuwa wanaharakati kupigana jihadi kwani wote hao wautaka uhuru wa kujitawala, heshima na ustawi.

Mafunzo ya dini ya Islamu yagawanyeni kwa wote, kwani ni ya wote, na mtaona yatawaongoza kwenye njia waitakayo inayong'ara, yatawasahihishia fikra na itikadi zao, na yatawafanya wajitolee na kujitoa mhanga ili kuuangusha utawala wenye siasa za kijeuri na ukoloni mamboleo, na badala yake kuanzisha serikali ya Kiislamu yenye msingi imara.

Mafaqihi ni walinzi wa uislamu na wanapaswa kuwaambia watu ukweli mtupu juu ya imani za kweli, nidhamu za Kiislamu na njia za kuyastawisha mapambano matakatifu. Wawaongoze watu, nao bila shaka (inshallah) watawafuata haraka wakihisi ustahili wao wa kuongoza, usafi wa roho zao na upinzani wao wa ubwanyenye.

Mafaqihi kama hao, kukosekana kwao ni msiba mkuu kwa watu na kwa taifa. Ni msiba ambao huwaachia watu katika maisha yao nafasi kubwa tupu yenye kutisha, na huacha pengo ambalo haliwezi kuzibwa na chochote. Nafasi hii iliyo wazi, isiyo na mtu wa kuijaza, na pengo hilo, haliwezi kutokea lau nitakosekana mimi au yeyote yule aliye mfano wangu ambaye hujikalia tu kwake nyumbani asiyajali maslahi ya Waislamu. Bali pengo hilo na nafasi hiyo iliyo wazi, huwapata Waislamu kwa kupotelewa na Mtume Mtukufu SAW. Ni hasara ilioje kwa Waislamu kupotelewa na mwenyewe Mtume ingawa alikufa baada ya kuutimiza muda wake! Kadhalika pengo kama hilo hutokea kwa Waislamu kwa kupotelewa na mtu kama Imam Husayn AS na Maimamu waliokuja baada yake. Lakini ikiwa Waislamu watapotelewa na mwanachuoni asiyejali maslahi yao hakuna hasara itakayopatikana wala hakutakuwa pengo lolote katika Uislamu.

Vilevile hasara hii ya kuwepo nafasi isiyo na mtu, yaani iliyo tupu na yenye pengo, huwapata Waislamu kwa kumpoteza mtu kama Shaykh Khwaja Nasiruddin Tusi[47] na mashaykh wengineo walioujenga Uislamu kama tunavyojionea katika historia. Ama mimi na wewe, tumeufanyia nini Uislamu ili tustahiki kusadikika juu yetu maneno yale yaliyomo katika hadithi inayosema: "Pengo huingia katika Uislamu ambalo haliwezwi kuzibwa na chochote." Hapana nafasi yoyote itakayoachwa wazi wala pengo lolote litakalotokea kwa kufa watu elfu moja walio mfano wetu, kwa maana, kule kuwa kwetu hai ni pengo na ni kuiweka nafasi kuwa tupu ambayo ni lazima izibwe na watu wasio kama sisi. Na pengine kufa kwetu (wanavyuoni tusiofaa) ni kizibika pengo hilo na knjazika nafasi hiyo isiyo na mtu; kwa kuwa sisi si mafaqihi tunaotumia elimu yetu kama inavyotakikana wala si watu • wenye imani ambao hudhihirisha imani yao kwa dhati bila kuogopa.

MAPAMBANO YA MUDA MREFU

Tusiwe na tamaa kuwa, mafunzo yetu na bidii zetu zitafanikiwa baada ya muda mfupi, kwa maana, kuikaza na kuiimarisha nguzo za serikali ya Kiislamu kunahitaji muda mrefu na bidii kabambe. Mara nyingi, tunawaona watu wekevu wenye busara zao wanaweka jiwe la msingi wa ujenzi fulani ili waje kulijenga watu wengine japo baada ya miaka 200.

Mkulirna mmoja alipoupandikiza mti fulani uzaao matunda aliulizwa sababu ya kufanya hivyo ingawa hatawahi kuyala matunda ya mti huo, alijibu "Walipanda wengine sisi tukala, na sisi tunapanda watakula wengine."

Ikiwa bidii najuhudi zetu tunazozitoa na harakati tunazozifanya hazitatoa matunda katika zama zetu, jambo hilo tu haliwezi kuulegeza msimamo wetu tuliouazimia, maana uletaji wa huduma kwa mtu haufai kutimizwa kwa kufuata misingi ya maslahi ya mtu mmoja, bali kwa Waislamu wote. Kwa mfano, Sayyidna Husayn AS, Bwana wa Mashahidi, lau angekuwa akijifikiria tu au kufikiria katika mawazo ya maslahi ya kibinafsi, angejitolea kusalimu amri kwa wapinzani wake na mambo yangekwisha.

Matumaini makubwa ya viongozi wa Bani Umayyah yalikuwa ni hayo. Lakini Sayyidna Husayn AS mawazo yake na fikra zake ziliutanguliza Uislamu na Waislamu wa zama zijazo. Kujitokeza kwa Sayyidna Husayn AS, kuuawakwake na kupigana kwake jihadi ilikuwa kwa ajili ya kuieneza dini ya kiislamu, na kudhihirisha sheria zake za kisiasa na nidhamu za kijamii kati ya watu.

Watu wakubwa wakubwa nao huzipangia ratiba zama zitakazokuja baada yao wala hawasikitiki iwapo ratiba zao hazikupendwa wakati wao wapo maadamu wana yakini ya ratiba zao kutoa matunda na matokeo mema siku za mbele, wala hawakati tamaa kwa kudhalilishwa, kutekwa au kufungwa gerezani. Ili lengo lao litimie hata wakiwa huko gerezani, huko huwa ndio wakati wao mzuri wa kuyapanga yatakayozifaa zama zijazo na wala hawawi na hima ya wao wenyewe wafikie lengo walitakalo. Sukamo, rais wa zamani wa Indonesia alikuwa na fikra kama hiyo na alipokuwa gerezani aliratibu mipango mingi ambayo aliitekeleza alipopata mamlaka. Vivyo hivyo, vyama na makundi ya kisiasa hufikia lengo la mipango iliyoipanga baada ya miaka mia mbili au mia tatu hivi.

Imam Sadiq AS hakutosheka na kuweka ratiba tu za uanzishi wa serikali ya Kiislamu, bali aliainisha ni hakimu na kiongozi gani anayefaa kuongoza. Kwa yakini, hakuwa na lengo la kumteua zama alipokuwa yeye, kwani yeye mwenyewe alitoshea mambo yote, bali alitazamia baada ya zama zake. Fikra zake zote, zaidi zilikuwa kwa umma wake kuliko udhati wake. Alikuwa akipendelea sana kuudhamini na kuunawirisha utu wa kila mtu, na ulimwengu wa walimwengu wote chini ya kivuli cha dini adili ya Kiislamu.

Dini, asili yake, hasa madhehebu ya Shia, na dini zote nyinginezo, zilianza kwa taabu na matatizo ya mafunzo na mipango. Ama kwa kuwa viongozi wake, Manabii, walikuwa na uthabiti, uvumilivu na azma imara, kidogo kidogo, polepole na hatua kwa hatua walizidi kufanikiwa.

Nabii Musa AS alikuwa mchungaji kondoo na msimamizi kwa miaka mingi. Siku aliyoambiwa amkabili Firauni hakuwa na wa kumsaidia. Ama kutokana na ujasiri na kipawa cha nguvu alichokuwa nacho, akiwa na fimbo yake, aliweza kuuponda ufalme wa Firauni.

Msidhanie kwamba, fimbo ya Mussa lau ingekuwa mkononi mwangu au mkononi mwa yeyote yule miongoni mwenu ingeweza kutufanyia ilivyomfanyia Mussa. La hasha! Kwa maana sisi hatuna ule utisho wake, hima yake na bidii zake za kazi zake. Mambo ambayo hanayo mtu yeyote yule (miongoni mwetu).

Naye Mtume wetu Mohammad SAW alipoanza kutangaza Utume wake, hakuwa na kitu cha kumtia nguvu wala mtu wa kumtia hima isipokuwa tu mtoto mdogo ambaye hata miaka kumi alikuwa hajaflkisha bado. Naye ni Sayyidna Ali bin Abi Talib AS. Vilevile hakuwa na mtu mwingine isipokuwa mwanamke mwenye umri wa miaka arobaini, naye ni mkewe Bibi Khadija. Wao ndio wa kwanza waliomwamini, wakamnusuru na kumsaidia katika mambo yake wakati watu wengine walikuwa wakimuudhi, kumpinga na kumwita mwongo. Lakini Mtume na wasaidizi wake waliokuwa wachache, hawakukata tamaa, bali waliimarika kwa uthabiti, kwa subira na kwa azma madhubuti hadi Mwenyezi Mungu alipolidhihirisha neno Lake na wabatilifu kuwatia adabu na hasara katika mambo yao. Hapo, Uislamu ukatia vigingi vyake imara sehemu za Mashariki na Magharibi ya dunia mpaka watu wenyewe wakaanza kuamini kidogo kidogo mpaka kufikia leo hii ambapo idadi ya Waislamu kote ulimwenguni si chini ya milioni mia saba (700,000,000)[48]

 Madhehebu ya Shia, nayo ilianza sifuri (haina kitu). Mtume Mtukufu SAW alipouweka msingi wa ukhalifa, alikabiliwa na mzaha na kuchekwa. Huo ni wakati alipowakusanya watu wake na kuwauliza, "Ni nani atakayekuwa khalifa wangu, wasii wangu na waziri wangu juu ya jambo hili?" Hapo hakuna aliyesimama kumjibu isipokuwa tu mtoto mdogo ambaye hata hajabaleghe. Naye ni Imam Ali AS. Wakati huo, mmoja wa waliokuwepo alimwambia Abi Talib, babake Sayyidna Ali AS kwa njia ya uchochezi, "Mtoto wa nduguyo anakutaka umsikize mwanao na umtii."[49]

Katika pahali paitwapo Ghadir Khum, katika Hija yake ya mwisho, Mtume Mtukufu SAW alimteua Imam Ali AS kuwa khalifa baada yake. Wakati huo ndipo hitilafu kubwa ikazuka nyoyoni mwa watu. Lau Mtume angekuwa amemchagua Sayyidna Ali AS kuwa mbainishi wa sheria tu, hangepingwa na yeyote. Alipingwa na kupigwa vita kwa sababu aliteuliwa kuwa mtawala na kiongozi wa kisheria kwa watu wote na kwa mambo yote.

Vilevile nyinyi lau mtakaa majumbani mwenu msijishughulishe na lolote, hakuna litakalowapata wala kuwagutusha. Ama siku mtakayotaka kuudhihirisha ujamaa wa kiudugu katika jamu, na kuyapiga dambini siasa ya nchi, hapo mtatangazwa watu wasiotakikana, na vita vya kupambana na nynyi vitatangazwa.

Ni kutokana na misimamo ya Maimamu na wafuasi wao juu ya sheria na idara katika Uislamu, ndiyo yakawapata yaliyowapata ambayo mnayaelewa sana yakiwa ni pamoja na kuudhiwa, kusutwa, balaa na kudhalilishwa. Hata hivyo, hawakukata tamaa na wangali wana matumaini. Kwa juhudi yao idadi ya Mashia kote ulimwenguni ikazidi kuongezeka. Hivi leo hawapungui milioni mia mbili (200,000,000).

MAREKEBISHO KWA VYUO VYA KUSOMEA USHEKHE

Kuuongoza umma kwa kuufikisha kwenye ufanisi, na kuujua Uislamu namna ulivyo, kwanza ni lazima pawepo hali ya kujisahihisha kwa maulamaa wenyewe na wasimamizi wa sheria, yaani, kwanza bidii zao zikamilike katika elimu, kujitegemea, kujiamini na kuepukana na uvivu, uzembe, udhaifu na ugoigoi. Wakati huohuo wafanye bidii ya kuzifuta athari na kasumba zote mbovu zilizoenezwa miongoni mwa watu na wawaelimishe baadhi yetu ambao fikra zao ni sawa na mawe kwa ushupavu wa kukaidi na inadi. Pia kuwafukuzilia mbali mashekhe waongo wasio na maana ambao wanaitumikia serikali ya kidhalimu na ambao wanaiuza dini yao ya Kiislamu kwa dunia ya wengine. Hao, tuwavue vilemba na majoho yao, tuwaweke mbali nasi, tuwaaibishe na tuzifichue hadharani kazi zao.

KUZITOKOMEZA ATHARI, MAADIU NA FIKRA ZA KIKOLONI

Karne nyingi zimepita, vibaraka wa wakoloni, vituo vya mafunzo na wanasiasa wamekuwa wakiendelea kupuliza sumu mbaya katika fikra za watu na katika huluka zao mpaka hivi leo tayari wamezifisidi kabisa; nao watu waliofisidiwa kutokana na sumu hizo wanautilia mashaka utetezi wetu na hawauoni kuwa ni wa kweli.

Vyuo vya kidini vinahitajika kutengenezwa vizuri ili tuvute hatua yenye nguvu za kuyakongoa mashina ya fikra zilizo benibeni zilizowaingia watu kutoka nje, na kupambana kwa makini na maovu yote, ufisadi na uharibifu ulio katika jamii zetu.

Watu wengi walioathiriwa na sumu hizo tunawaona kwa macho yetu, maana tunaishi pamoja nao. Pia katika wao mna baadhi yao wanaonong'onezana wakisema, "Kazi hizi si zetu wala hazituhusu. Sisi tutamwomba Mungu tu na kuwaeleza watu masiala (ya dini tu)." Matamshi hayo na mengine kama hayo ni matokeo ya vitisho vilivyosambazwa nyoyoni mwa watu na mabeberu miaka mingi iliyopita, na mambo kama hayo ndiyo yanayowafanya mashekhe wa (miji mitakatifu ya) Najaf, Qum na Mash'had kuwa watu walio na nyoyo tupu na bure zisizo na kitu wala uongofu kwa kudai eti, "Mambo haya si yetu wala hayatuhusu."

Mawazo hayo ni ya makosa. Je, kuna watawala miongoni mwa hao wanaotawala wanaomiliki busara zaidi kuliko tunazozimiliki sisi? Ni nani miongoni mwao anayestahili kuwaongoza watu? Je, si baadhi yao hawajui hata kusoma? Mfalme wa Hijazi alielimishwa wapi? Je, Reza Khan, babake Shah wa Iran hakuwa katika watu wajinga wasiojua kusoma? Na papo hapo historia inatusimulia visa vya watawala kadha wa kadha waliokuwa maamuma wakitawala bila kustahiki na kustahili. Naam, huyu Harun Rashid alifuzu katika maendeleo ya kitu gani? Kadhalika waliomtangulia na waliokuja baada yake!

Ama sisi, ni juu yetu (tunapaswa) kutumia utaalamu wa watu fulani fulani wenye elimu muhimu wa fani mbalimbali za kitaalamu, mambo yote yanayohusiana na kazi za utawala ili kuiendesha serikali. Ama yanayohusiana na utawala wenyewe wa nchi, mambo ya upanuzi wa usawa kati ya raia, kuleta utulivu na amani katika nchi kati yajamii, kuhukumu na kuamua kwa uadilifu, hayo ndiyo mambo hasa aliyoyasomea faqihi. Naye maisha yake yote huyaendesha katika kuyatekeleza mambo hayo. Kwake ni lazima awe na mambo yote yanayouhifadhi uhuru wa watu, kujitawala kwao na maendeleo yao, na aidhamini siasa nyofu. Faqihi kamwe hashawishiki na wageni Wala haelekei katika siasa ya mrengo wa kulia au kushoto, bali daima hupigania haki ya wananchi, uhuru na kulinda mipaka ya nchi ya Kiislamu.

Jamani tokeni kwenye utelezi wenu. Nanyi vijana zikamilisheni mbinu zenu za kufanya tablighi ili mwanze njia ya kuyakabili mambo haya mazito. Pangeni mpango wa kuunda serikali ya Kiislamu na mwanze hatua ya kuifuata mpango huo mkiwa pamoja bega kwa bega pamoja na wote wanaoutaka uhuru wa kujitawala. Na bila shaka mtafika tu kwenye lengo, inshallah.

Kisha jitegemeeni, na habari zenu za mapambano yenu ambayo ubeberu unayaogopa yatatangaa. Mimi binafsi nina yakini mtaweza kuyaendesha mambo ya utawala na kuwaongoza wananchi kuipindua serikali ya dhulma na uonevu.

Mipango ya kuiendesha serikali na utaratibu mwingine -tayari unapatikana katika dini yetu tukufu ya Islamu. Hii ikiwa ni pamoja na nidhamu za idara, kodi, ushuru, ulinzi wa haki za raia, sheria za adhabu na mengineyo. Nyinyi hamtakuwa na taabu wala haja ya kutunga sheria mpya bali kazi yenu itakuwa kutekeleza yaliyokwisha pangwa tu.

Kupatikana tayari kwa sheria hizi, kutawaondolea taabu ya kupoteza muda mrefu katika kutunga sheria, pia kutasaidia kutoingiza katika katiba yenu kanuni za nchi za Magharibi au Mashariki. Na tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupangia kila kitu. Kilichobaki ni kuipanga mipango ya wizara, kazi ambayo itafanywa na baraza la mawaziri, makatibu wakuu, washauri na wataalamu katika fani mbalimbali. Hayo yote yatatimia chini ya wasimamizi kwa muda mfupi sana, inshallah. Jambo muhimu na la kutia moyo ni kuona wananchi wote wako pamoja na nyinyi kufuata nyayo zenu. Nao wasaidizi wenu tayari wamejifunga vibwebwe kuwasaidieni.

Sisi tuna upungufu wa hima na silaha, lakini inshallah tutazipata. Jamani tufanye juhudi kwa pamoja ili fimbo ya Nabii Musa AS na upanga wa Sayyidna Ali AS na nguvu zao ziwe pamoja nasi, kwani lau tutaazimia kwa nia moja, halisi na safi kuiweka serikali yenye maongozi ya Kiislamu, bila shaka tutaipata fimbo ya Nabii Musa AS na pia upanga wa Sayyidna Ali AS.

Naam, ni kweli wako baadhi ya mashekhe katika vyuo vyetu vya kidini ambao ni wazembe walio katika usingizi wasioweza kuchukua jukumu la kuunda serikali. Hawawezi kuandika hata waraka mmoja juu ya jambo hilo wala kuvifungua vinywa vyao. Mbali na hayo, hawaelewi lolote katika mambo ya maisha, na kutokana na matokeo mabaya ya waliyoyatawanya wakoloni miongoni mwetu, watu hao wanathubutu kuwaambia wanaowakabili eti, "Mambo haya (ya kisiasa na kiserikali) si yako wewe wala hayakuhusu, wewe nenda madarasani kwako uyaendeshe masomo yako tu." Watu jinsi hii ndio wanaotutatiza kutokana na makosa waliyonayo yanayowafanya wasifikiri mambo ya Waislamu.

rudi nyuma Yaliyomo endelea