rudi nyuma Yaliyomo endelea

Maisha ya Mtume Muhammad SAW yalikuwa duni kabisa. Hakutumia cheo chake cha Utume kwa ajili ya kujinufaisha na mambo ya dunia. Kitu kikubwa alichokiacha ni elimu ambayo chimbuko lake ni ufunuo unaotoka kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja. Kwa hivyo, kutaja elimu katika hadithi hizo ni kwa ajili ya kukabiliana na kupambana na mali na mambo ya upuuzi wa kiulimwengu.

Lau tutaamua kwamba, hadithi zote hizo za kwanza zina maana moja tu, ya urithi wa elimu, hata ingawa Mtume Mtukufu SAW alisema, "Ali ni mrithi wangu" tuchukulie hadithi zote hizo hazikusudii ukhalifa wake wala uongozi na utawala wa serikali, basi mambo yakiwa ni hivyo, tunahitajika kuzirudia hadithi nymgine zinazoonyesha ukweli wa ukhalifa wake na utawala wa mafaqihi kufuatana na kauli ya Mtume kwamba mafaqihi ni makhalifa wake.

USHAHIDI KUTOKA FIQIffl YA RADHAWI JUU YA UTAWALA WA FAQIHI

Kitabu kiitwacho Awaidu Naraqi (uk. 186) kinanukulu hadithi juu ya fiqihi ya Radhawi, ikisema:

"Daraja la faqihi kwa wakati huu ni kama daraja la Manabii kwa wana wa Israil."

. Naam, kwa kawaida, hatuyazingatii yote yaliyomo katika fiqihi ya Radhawi kuwa ya kweli. Lakini hebu tuichukue hadithi iwe ushahidi wa upekuzi wetu.

Makusudio ya "Manabii wa wana wa Israil" ni mafaqihi walioshirikiana na Nabii Musa AS, na pengine nao walikuwa kwa upande mwingine, wakiitwa Manabii. Walikuwa wakimfuata Mtume Musa AS wakiuiga mwenendo wake katika tabia zao na matendo yao. Kila alipokuwa akiwatuma kwenda sehemu fulani huwakabidhi utawala wa mambo yote ya sehemu wanakoelekea. Hata hivyo, sisi hatujui kwa mapana hali zao zote isipokuwa tu tunajua kwamba, Mtume Musa AS yeye mwenyewe alikuwa ni Nabii miongoni mwa Manabii wa Bani Israil. Na lolote alilokalifishwa kulitenda Mtume wa Islamu (Muhammad SAW) naye (Musa) vilevile alikalifishwa kulitenda hata ingawa pana tofauti ya utukufu baina yao.

Nasi tunafahamu kutokana na neno 'daraja' lililo katika hadithi ambalo lilikuja kwa maana ya ujumla kwamba, yote aliyoyaendesha Mtume Musa AS yakiwa ya kiserikali na mengineyo, yote hayo yamewathibitikia pia mafaqihi.

USHAHIDI ZAIDI JUU YA UTAWALA WA FAQIHI

Kitabu kiitwacho Jaamiul Akhbaar kuna hadithi kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW isemayo: "Nitaona fahari siku ya Kiyama kwa maulamaa wa umma wangu; na maulamaa wa umma wangu ni kama Manabii walionitangulia." (Awaidu Naraqi. uk. 187)

Katika kitabu Mustadrikul Wasaail mmenakiliwa hadithi kutoka kwa Gharaar juu ya madhumuni haya, "maulamaa ni mahakimu (watawala) wa watu."

Na katika kitabu Tuhfatul Uqul chini ya kichwa cha maneno, mapitio ya mambo ya sheria yamo mikononi mwa maulamaa" mna hadithi ndefu. Sehemu ya kwanza kati ya hadithi hiyo, aliyoyanakili Sayyidna Husayn AS kutoka kwa babake Sayyidna Ali AS juu ya aliyoyasema kuhusu kuamrisha mema na kukataza mabaya.

Sehemu ya pili yake, ni hotuba aliyoitoa Sayyidna Husayn AS kwa watu huko Mina akielezea shani ya utawala wa faqihi na wajibu wake katika kupambana na viongozi wafisadi na serikali zao pamoja na kuwaondolea mbali, na badili yake kuweko serikali zenye maongozi ya sheria za Kiislamu. Mumo humo alitaja sababu zilizomfanya atoe tangazo lajihadi (vita vitakatifu) dhidi ya utawala dhalimu wa Bani Umayyah. Hadithi hii inatupa faida mbili kubwa:

1- Utawala wa faqihi, na

2- Dharura au haja ya kujitokeza mafaqihi kuwafichua watawala wadhalimu, kuvitingisha viti vyao vya enzi, kuwaamsha watu na kuwalinda hadi waungane ili kuiangusha serikali fisadi na kuunda serikali yenye misingi na sheria za Kiislamu. Njia ya pekee ya kuhakikisha ushindi nijihadi, kuamrishana mema na kukatazana maovu.

Ifuatayo ndiyo hotuba kamili aliyoitoa Imam Husayn AS Bwana wa Mashahidi huko Mina:

"Enyi watu! Yazingatieni mawaidha ya Mwenyezi Mungu aliyowawaidhia watu wake wema kuwaonyesha uovu uliofanywa na watawa. Akasema Mungu, 'Mbona wanavyuoni (watawa wa Kiyahudi) na maaskofu hawawakatazi (wafuasi wao) kauli zao za. dhambi na ulaji wao wa haramu? Ni mabaya kabisa wanayoyafanya,' (5:63). Mungu akasema tena, 'Wamelaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israil, kwa ulimi wa (Mtume) Daudi na wa Isa bin Maryam. ' Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wakipindukia mipaka. Walikuwa hawakatazani mabaya wanayoyafanya, ni mabaya kabisa hayo waliyokuwa wakiyafanya,' (5:78, 79).

"Kwa hakika si jingine bali Mwenyezi Mungu aliwatia aibu kwa sababu walikuwa wakiziona dhuluma zote mbaya na ufisadi mbele ya macho yao na nyuma ya migongo yao wala wasizuie kwa tamaa ya waliyokuwa wakiyapata, na kwa kuogopa waliyokuwa wakijihadhari nayo. Mungu asema, 'Wala msiwaogope watu niogopeni Mimi. '(5:44). Pia amesema, 'Na waaminio wanaume na •waaminio wanawake ni marafiki wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza mabaya.' (9:71)

"Hapo Mwenyezi Mungu alianza kutaja wajibu wa kuamrisha mema na kukataza mabaya, kwa maana lau mambo hayo mawili yangesimamiwa vyema na kutekelezwa sawasawa fardhi zote ngumu na nyepesi zingesimama itakikanavyo. Hilo ni kwa maana kuamrisha rnema na kukataza mabaya ni kulingania kwenye amani pamoja na kuiacha dhuluma na kumhalifu dhalimu. Ni kukaa kivulini na ni kugawana ghanima (ngawira). Pia ni kuzichukua sadaka na kuziweka mahali pake zinapostahiki.

"Enyi maulamaa ambao mmekuwa mashuhuri kutokana na elimu yenu! Mmepata umaarufu katika jamii kutokana na uongozi na nasaha zenu mnazozitoa. Kwa ajili ya Mungu mnaogopewa katika nafsi za watu. Mkubwa huwaogopa. Na mnyonge anawaheshimu. Msiyekuwa na amri kwake anawafadhilisheni wakati hamna uwezo wowote mbele yake. Mnawaombea wenye haja wanaponyimwa, na mnapotembea njiani huwa na haiba na heshima ya kifalme na ya wakubwa.

"Je, hayo yote si mmeyapata kutokana na mnayotarajiwa kuyasimamia katika mambo ya Mungu japo haki nyingi za Mungu mnazififiza? Haki za umma mmezitupa. Haki za wanyonge mmezipoteza. Ama zile mnazodai kuwa haki zenu mnazitafuta kwa bidii. Hamkutoa mali (katika kuyahudumia maslahi ya umma), wala hamkujitolea nafsi zenu kwa ajili ya Yule aliyeziumba. Wala hapana ukoo uliojitolea mhanga kwa ajili ya Dhati ya Mungu.

"Mnataka kwa Mungu Pepo Yake na kuwa karibu na Mtume Wake pamoja na kuamini kusalimika na adhabu Zake.

"Enyi mnaotaka si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ninawaogopeeni yasije yakawapata maangamizo ya Mungu, maana mmefikia utukufu aliowafadhili Mwenyezi Mungu. Anayejulikana (au anayemjua) Mungu hamheshimu, na nyinyi kwa ajili ya Mungu katika waja Wake mnaheshimika. Mnaziona ahadi za Mungu zikibadilishwa wala msishikwe na fadhaa ambapo mnashikwa na fadhaa wakati baba zenu wanapovunjiwa heshima zao. Vilevile hamfadhaiki wakati utukufu wa Mtume unapofanyiwa mzaha! Vipofu na mabubu hamuwahurumii, wala nyumba zenu hamzitumikii, waliomo hamuwasaidii, na badala yake mnapendelea kujitia mafuta na kujipendekeza mbele ya madhalimu.

"Hayo yote ni miongoni mwa aliyowaamrisha Mwenyezi Mungu myakanye na myazuie na nyinyi mmeghafilika nayo.

Nyinyi mmepatwa na msiba mkubwa zaidi kwa kughilibiwa kwenu kutoka daraja la maulamaa lau mgekuwa wenye kusikia. Hayo ni kwa sababu, mapitio ya mambo na hukumu, yako juu ya mikono ya wamjuao Mungu wenye kusalimika juu ya halali Zake na haramu Zake.

"Enyi mliopokonywa daraja hilo! Hamkupokonywa cheo hicho ila kwa sababu ya kujitenga kwenu na haki na kuhalifu kwenu hadithi baada ya uwazi wake. Lau mgesubiri juu ya maudhi, na mkastahamilia madaraka yenu kwa ajili ya Mungu, mambo ya Mwenyezi Mungu yangekuwa yanarudi juu yenu, yanatoka kwenu na kwenu yanarudi, lakini mmeiachilia dhuluma mpaka ikawakalia, na mkayatoa mambo ya Mungu mkawapa madhalimu wakayaendesha kiudanganyifu watakavyo wakifuata matamanio ya nafsi zao.

"Kule kuyakimbia kwenu mauti, na kuringia maisha haya duni ya kidunia tena mafupi ndiko kulikowatwika taabu hizo zote. Wanyonge mmewatoa mkawapa madhalimu wawatumie watakavyo kwa kuwafanya watumwa watendeshwe nguvu na madhalili wataabishwao. Wao (hao madhalimu) wanaupindua pindua ufalme kwa maoni yao watakavyo. Wanafanya mambo ya fedheha kwa kuandama shari na kuonyesha ujasiri wao wa kutomwogopa Mungu. Mijini mwao (hao madhalimu) kila mmoja wao yu juu ya jukwaa anahutubu kwa kunguruma. Ardhi ni tupu na mikono yao wameipanua na watu wao wanaostahiki haki hawapewi. Wanawatawala watu kwa vitisho, yaani kwa mabavu na kuwadhalilisha wanyonge pasina kumjua Mwenyezi Mungu.

"Ewe ajabu! Kwa nini nisishangae hali ardhi ipo chini ya watesao wenzao, wakorofi na madhalimu! Hawana huruma kabisa wala hawawaonei watu imani! Mungu Ndiye Hakimu wa tuliyoyabishania, na ni Mwamuzi juu ya utesi wetu.

"Ewe Mola wetu, kwa hakika Wewe unajua kwamba, yaliyokuwa baina yetu hayakuwa ubishani wa kubishania usultani, wala kuyaandama mambo ya upuzi wa kidunia isipokuwa ubishani wetu ulikuwa wa kutaka kuyarudisha mafunzo Yako, kudhihirisha utengevu ulimwenguni Mwako, waja Wako wanaoonewa wasalimike na watu Wako waweze kutenda amali zao na kutumia hukumu Zako pamoja na kuzitekeleza fardhi Zako. Mungu anatutoshea mambo yetu, Kwake tumetegemea na Kwake ndiko tutakakorejea na marejeo yote ni Kwake." Hotuba ya Imam ikamalizika.

N1 WAJIBU KWA MAULAMAA KUPINGA DHULUMA

Imam asema, "Enyi watu! Yazingatieni mawaidha ya Mungu aliyowawaidhia watu Wake wema kuwaonyesha uovu uliofanywa na watawa (wa Kiyahudi)."

Hotuba hii, haikuwahusu tu waliouhudhuria mkutano wake peke yao au wakazi wa Mina au watu wa zama hizo peke yao, bali yawahusu watu wote wa kila mahali na wa zama zote kama ambavyo tunaona katika Qur'ani Tukufu Mungu anavyokariri neno Lake, "Enyi watu!"

Watu wa Mungu waliokusudiwa (katika hotuba hiyo ya Imam) ni wale wenye kuelekea na kuyabeba mambo yaliyo wajibu juu yao na wala sio Maimamu waliokusudiwa.

"Mbona •wanavyuoni (wa Kiyahudi) na maaskofu hawawakatazi kauli zao za dhambi na ulaji wao wa haramu? Ni mabaya kabisa wanayoyafanya, " (5:79). Bila shaka mashtaka hayo na lawama hizo si kwa wanavyuoni wa Kiyahudi na wa Kinasara peke yao, bali huwakusanya pia maulamaa wa Kiislamu iwapo watakaa kimya juu ya dhulma na uonevu wanavyoviona.

Ni wazi kabisa kwamba, lawama hizo si za wanavyuoni wa zama zilizopita, bali hata wa zama hizi. Imam alitoa ushahidi wa Our'ani kuwakumbusha maulamaa kuuzingatia na kuutekeleza wajibu wao wa kuamrisha mema, kukataza mabaya, kupinga dhuluma na kuizuia kabisa isisambae.

Ushahidi wa aya aliyoitoa Imam unaonyesha mambo mawili:

1- Maulamaa kujiweka nyuma na kunyamaza kwao kuna madhara zaidi kuliko kujirudisha nyuma kwa watu wengineo wasio maulamaa. Uhalifu au maasi yanayofanywa na mtu wa kawaida aghlabu hayaleti hasara kubwa wakati ambapo yakifanywa na aalimu (mwanachuoni) au akiinyamazia dhuluma huwa ni dhara kubwa la hatari kwa uislamu wote. Lau aalimu atatenda kwa mujibu wa wajibu wake kikamilifu, na akasema panapofaa aseme, manufaa yake yote hurudi kwa Uislamu.

2- Kutoa mwangaza kamili wa kuonyesha ubaya wa kuchukiza wa kunena maneno ya dhambi na kula haramu. Mambo hayo mawili (kusema maneno ya dhambi na kula haramu) ni hatari zaidi kuliko mabaya yote, na yanapaswa kupingwa kwa nguvu kabisa. Baadhi ya maneno na matamko machafu yanayotolewa na viongozi madhalimu huuletea Uislamu madhara makubwa tena ya hatari, kwani hueneza siasa zao mbovu na matendo yao machafu yasiyo ya kisheria.

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya hii anamtia lawamani mtu yeyote yule anayenyamaza kimya huku anasikia maneno ya dhambi yakinenwa wala asiyapinge au kutafakari namna ya kuyaondoa. Vilevile Mwenyezi Mungu analingania kumtia uwongoni (kumkadhibisha) mtu yeyote anayedai ukhalifa wa Mungu pasina haki au anayedai kuyaendesha mambo ya dini na matumizi yake hali matendo yake ni mbali kabisa na sheria za dini. Laana ya Mwenyezi Mungu inamfikia yule mtu anayedai ni mwadilifu hali yeye hana uadilifu wowote.

Imepokewa hadithi inayosema: "Pindi zikionekana bidaa* (uzushi katika dini) waziwazi katika umma wangu, basi ni lazima kwa aalimu (mwanachuoni) aidhihirishe elimu yake, la sivyo, laana ya Mungu iwe juu yake."

Aalimu kujitenga na wenye kuzua mambo, akaweka wazi sheria za Mungu na mafunzo Yake yenye kuwazoza wazushi wa bidaa, dhuluma na maasi mengine, kutawafanya watu kuufichua ufisadi katika jamii unaotokana na viongozi madhalimu, wahaini, mafasiki na makafiri. Kisha wataweza kuwanyoosha na kuikata mirija yao pamoja na kuwagomea na kuyakataa maamrisho yao yanayofungamana na uhaini, dhuluma na ufisadi.

Aalimu katika kuuongoza msimamo wake mshupavu, atakuwa akifuatisha mwito wa kuyakataza mabaya ambayo watu wote kwa umoja wao na wingi wao wataweza kujiongoza dhidi ya utawala haramu hata japokuwa utawala huo hautajirudi na kufanya aliyoyaamrisha Mungu isipokuwa tu kuwafyatulia watu risasi.

Kikundi cha aina hii kikifikia hadi hii, kizingatiwe kuwa kiovu kinachopaswa kupingwa na kupigwa vita na watu wote, hadi kitakaposalimu amri kwa Mwenyezi Mungu.

Hivi leo, nyinyi hamna nguvu za kupambana na uongo wa viongozi au kuuondoa ufisadi wote waliokwisha kuutawanya. Lakini, kwa nini kukaa kimya? Hao jamaa wanawadhalilisheni. Kwa uchache, wapigieni makelele, muwapinge, muwaasi na muwaite waongo. Ili kukabiliana na vyombo vyao vya habari wanavyovimiliki na matangazo yao wanayoyatangaza humo ya uwongo eti kuonyesha mambo ya usawa waliyoyafanya, ni lazima mshikilie silaha yenu hiyohiyo kwa mikono yote miwili, yaani silaha ya kusema kwa sauti ya nguvu tena kwa pamoja kwamba, "Yote wanayoyadai kuwa ya usawa si katika usawa wa Kiislamu hata kidogo."

Usawa wa Kiislamu Mungu aliompa kila mmoja, kilajamii na kila familia tayari uliandikwa na kuthibitiwa kwa uangalifu mkubwa tokea siku ya kwanza. Ni wajibu wenu muwe na sauti yenye kusikika ili karne zijazo zisije zikahalalisha, kusamehe au kuona ni haki matendo ya kidhulma yakiwa ni pamoja na kusema maneno ya dhambi, kula haramu na kula mali za watu pasina haki kutokana na kunyamaa kwenu.

Ni uchache mno wa fikra ulioje kwa baadhi ya watu kudhani eti makusudio ya kula haramu si mengine isipokuwa tu kufifiza vipimo vya miizani na kuwapunja watu katika vyeo wala ulaji huu wa haramu haumo katika mambo mengine hasa yenye kutisha uthabiti wa nchi, kama vile wizi wa mali za wananchi, na kuidokoa hazina ya taifa! Jamaa hao tayari wameyaiba mafuta yetu na kuyauza katika masoko ya magendo wakidai kuzalisha mali. Kwa njia hii hii ya unyang'anyi huufikia utajiri wa haraka haraka usio wa kisheria. Juu ya wizi huu, mataifa kadha wa kadha ya kigeni husaidiana kuyachimba na kuyauza, na hutoa ujira mkubwa kwa vibaraka wao, yaani viongozi wenye kuwasaliti wenzao ili waruhusiwe kurudi tena bila kupingwa na yeyote. Katika kuhongana huku, kile kinachotolewa kutoka katika hazina ya taifa hakuna ajuaye isipokuwa Mwenyezi Mungu. Kinachotolewa na kinachotumiwa, ni lini na ni wapi kilipotumika? Hakuna ajuaye majibu yake. Huu ndio ulaji haramu. Na kulingana na kauli ya kielimu, ulaji huu wa haramu ni mbaya kabisa na wa hatari ya kufadhaisha kuliko mabaya yote.

Jamani fikirieni kuustawisha jamii yetu, na stahmilini mnapofanya kazi za taifa lenu ili tatizo kubwa la ulaji haramu libainike kwa watu wote.

Kunapotokea tetemeko la ardhi mahali fulani ulimwenguni, viongozi hao haramu huwa ndio wakati wao wa kujipatia mali kemkem kutoka kwa waliokumbwa na mkasa. Maafikiano na mikataba ya misaada inayotiwa sahihi baina ya viongozi hao wahaini na mataifa au mashirika ya kutoa msaada ya nje, wao huingiza mamilioni ya fedha hizo katika akiba zao, na zingine huzificha katika mataifa fulani ya kigeni. Ama wananchi, wao hubaki mikono mitupu bila kufaidi chochote katika mapato ya nchi yao.

Hayo yote ni matokeo ya matatizo ya ulaji haramu yanayojiri tukisikia na kuona. Ama yale tusiyoyajua ndiyo mengi ajabu.

Mambo hayo hasa, hutokea katika maafikiano ya kibiashara na hati za mikataba ya uchimbuaji mafuta na kuyatoa, hati za mikataba ya kustawisha kilimo na mambo mengineyo yanayohusiana na utafiti wa mambo ya kale na mazingara pamoja na mali asili, mikataba ya ujenzi, mawasiliano na ununuzi wa silaha kutoka kwa wakoloni wa Kimagharibi au mabeberu wa Kikoministi.

Tunapaswa kuukomesha kabisa mtindo wa ulaji haramu na kuhujumu uchumi wa taifa. Wajibu huu ni wa watu wote, lakini umuhimu wake kwa maulamaa una mkazo zaidi kuliko watu wengine. Katika jihadi hii tukufu, ni wajibu juu yetu tuwe mbele ya watu wote katika kuudhihirisha wajibu wetuna msimamo wetu.

Japokuwa kwa sasa hatuna nguvu za kutuwezesha kuyanyoosha mambo, kuwakanya wahami, walaji haramu na wadokozi wa mali ya umma, na vilevile japokuwa tunashindwa kuwatia adabu, ni wajibu wetu tufanye bidii kupitia njia zote ili tufanikiwe baadaye pamoja na kuzingatia tusije tukapetua wakati wa kuidhihirisha haki na kuufichua udanganyifu unaolikumba taifa. Hapo tutakapofanikiwa kuzipata nguvu hizo (inshallah) hatutatosheka tu na kuuinua uchumi na kutengeneza hukumu baina ya watu kwa usawa, bali pia tutawaonjesha wahaini hao waovu adhabu kali kwa kuyalipia waliyokuwa wakiyafanya.

Masjidul Aqsa (msikiti wa Jerusalem) tayari waliuteketeza huku sisi tukipiga makelele, "Acha maovu yaendelee" na wakati huohuo Shah alifungua hesabu katika mabenki ili kuuchangia ujenzi mpya wa msikiti huo. Kwa njia hii ya uchangishaji pesa za ujenzi wa msikiti, hazina yake na akiba yake ya kibinafsi inazidi kufura ambapo hatimaye huwa na lengo la kuyaficha maovu yanayofanywa na Israel (Wasayuni).

Hii ndiyo misiba ya umma. Na imefikia hali hii. Je, haifai maulamaa kutoa maoni yao juu ya mambo hayo? Haifai wapige makelele ya kupinga na kuyanyosha yaliyokwenda mrama au kombo? "Mbona wanavyuoni na watawa hawawazuii (wafuasi wao) kauli zao za dhambi na ulaji wao wa haramu?"

Kisha Imam anaongeza, "Hakika si jingine bali Mwenyezi Mungu aliwatia aibu kwa maana wao walikuwa wakiiona dhuluma mbele yao na nyuma ya migongo yao ikiwa ni pamoja na mabaya na ufisadi wala wasizuie kwa ajili ya tamaa ya waliyokuwa wakiyapata kutokana na wao, na kwa ajili ya kujikinga na wanayoyaogopa."

Mwenyezi Mungu anawakumbusha na kuwatia aibu wasioamrisha mema wala kukataza mabaya kwa ajili ya kuogopa au tamaa. Asema, "Wala msiwaogope watu (bali) niogopeni Mimi. " Kwa nini kuogopa? Basi na kuwe kuwekwa kizuizini, kufungwa au kuuawa. Lakini watu wema, wao huziuza nafsi zao kwa ajili ya kutaka radhi ya Mungu. "Waumini wanaume na waumini wanawake, ni marafiki wao kwa wao. Huamrishana mema na kukatazana maovu, husimamisha sala na hutoa zaka na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake," (9:71).

Kisha Imam asema, "Mwenyezi Mungu alitanguliza kuamrisha mema na kukataza mabaya kuwa fardhi kutoka Kwake kwa vile alijua kwamba, lau kunatekelezwa itakikanavyo, na kusimamiwa vyema, faradhi zote nyepesi na ngumu zitanyooka. Hayo ni kwa sababu, kuamrisha mema na kukataza mabaya ni kulingania kwenye Uislamu pamoja na kurudisha nyuma udhalimu na kujitenga na dhalimu, na ni kukaa chini ya kivuli kugawana ghanima, na ni kuichukua sadaka na kuiweka mahali pake na kumpa anayeistahiki."

Kutokana na mambo makubwa kama hayo, ndiyo Uislamu ukaweka sheria ya kuamrisha mema na kukataza mabaya, na wala siyo kwa ajili ya mambo madogo madogo tunayoyaona na kuyasikia kila siku. Yote hayo ni wajibu kuyapinga na kuyakanya.

Kutatokea madhara gani lau maulamaa wote watajitenga na kuwa kitu kimoja katika kupambana na dhulma? Watadhuriwa na nini iwapo watajikusanya wote kisha watume simu za maandishi (telegram) kote ulimwenguni - hasa kuliko na Waislamu - wakipinga uonevu unaofanywa na watawala madhalimu?

Hivyo basi, tuwawekee wakoloni vikwazo na tuwashurutishe kwa kuwatisha, kwani wao kama ninavyowajua ni waoga goigoi, na wakijua sisi ni makabwela tu — yaani tu madhaifu, basi watasusurika (watatangatanga) watuchachamie (watung'ang'anie) na warukeruke kwa furaha.

Siku zile maulamaa wote walipokuwa ni kitu kimoja, nyuma yao wakiungwa mkono na wananchi kote ulimwenguni, tawala dhalimu ziliweza kuchungua tena misimamo yao. Walipoona maulamaa na wafuasi wao wamejikunyata tena, walirudia tena fitina zao za kupanda mbegu za uharibifu na uhalifu. Matokeo yake, ni watawala kutoogopa kufanya walitakalo hata likiwa ni kinyume na matakwa ya wananchi, hatimaye wakawa watahiarika kwa ambalo si ruhusa kwa yeyote kufanya hiari.

Kuamrishana mema na kukatazana mabaya ni kulingania kwenye Uislamu, kukomesha dhuluma na kujitenga na dhalimu. Yule jamaa maskini anayefanya kosa dogo haleti dhara kwa Uislamu bali kwa nafsi yake. Lakini wale ambao wanaleta dhara kwa Uislamu ndio ambao yafaa kukabiliana nao. Basi kwa hivyo, inapaswa uwezo mkubwa wa kuamrisha mema na kukataza mabaya utumiwe dhidi ya wanaozichezea roho za watu na mali zao.

Baadhi ya magazeti, mara nyingi yamesimulia kimaskhara juu ya wizi na upokonyaji wa misaada ya kujitolea inayoletwa kuwasaidia waliokumbwa na maafa ya mafuriko, maporomoko ya majabali, ukame na tetemeko la ardhi. Mmoja wa wanavyuoni wa mji wa Malayer alikuwa akisema mara kwa mara kwamba, "Katika tukio fulani la mkasa lililosababisha watu wengi kufariki dunia, tulitumia lori moja lililojaa misaada ya nguo za sanda, ila jambo la kusikitisha ni kwamba, wanaohusika na kutupokea walitukataza kuufikisha msaada huo, mpaka kwanza tuwahonge, kwani walitaka kuzitwaa." Jambo kama hilo na mengineyo ni miongoni mwa maovu yanayopaswa kukatazwa na kulaaniwa.

Nawaulizeni sasa: Je, hatuizingatii hotuba ya Imam aliposema, "Enyi watu?" Je, sisi si watu? Hotuba haikutukusanya sote? Je, hotuba za Imam ziliwahusu tu masahaba zake na walioshirikiana naye peke yao?

Hapo awali nimetangulia kusema kwamba, mafunzo ya Qur'ani Takatifu, hayahusu tu kame maalum bali ni mafunzo ya wote, awe kiongozi, waziri, hakimu au faqihi. Wanadamu wote wa zama yoyote na mahali popote hadi siku ya Kiyama, ni wajibu wayatekeleze na wayafuate.

Namna walaumiwavyo wanavyuoni wa Kiyahudi na watawa kwa kunyamazia kwao lisilostahiki kunyamaziwa, ndivyo wanavyolaumika maulamaa wakinyamazia mabaya wasijitokeze kuyakanya au kutumia nguvu zao zote kuyaondoa.

Imam aliendelea kuwazungumzia watu na kuwatupia lawama. Akasema, "Vipofu na mabubu wameachwa hamuwahurumii." Je, jamani, mnafikiri hizo kelele zinazotawanywa na vyombo vya habari kutudanganya eti tumefanyiwa hili na lile mnafikiri yote ni ya kweli? Hebu nendeni vijijini na sehemu za mashambani. Kwa kila vijiji mia moja au mia mbili mtampata mwuguzi (daktari) mmoja tu au zahanati moja.

Hawakuwajali wala hawakuwafikiria walio na njaa, watembeao uchi, wala hawakuwaacha wenyewe wajifikirie, wala hawakuipa nafasi dini ya Islamu iwatatulie matatizo yao.

Kama mjuavyo, Uislamu toka siku yake ya kwanza, ulimfikiria mnyonge na namna ya kumwondolea ufakiri wake. Mungu asema, "Hakika sadaka ni kwa mafakiri. . . " na Uislamu ulipanga namna ya kuutekeleza wajibu huu kwa wanaohusika, lakini jamaa zetu hao hawakuiacha wazi njia ya Uislamu kwa Waislamu.

Jamani umma unaishi katika hali mbaya ya taabu huku watawala wa Iran wakijirundikia mali. Wanakiongeza kiwango cha utoaji kodi na ushuru kisha kulitumia pato hilo kununulia ndege za kivita za phantom ili marafiki zao Waisraili wazifanyie majaribio ya kujiandaa kutuangamiza sisi tuliotoa kodi ya kuzinunua. Kwa kuwa Waisraili wako katika hali ya kupigana na Waislamu, basi na yeyote anayewasaidia huwa anapigana vita na Waislamu.

Waisrali wamepata mapenyezo nchini mwetu na kufikia kiwango kisichowezekana. Askari wa Israili wameitwaa ardhi yetu na kuifanya makao yao ya kudumu, pia wakaifanya kuwa soko la bidhaa zao jambo litakalosababisha kuanguka polepole masoko ya Waislamu.

Haya basi mmejionea wenyewe. Hadithi yote hii ya Imam inazunguka juu ya watu wote wanaomjua Mungu, wala sio Maimamu peke yao au wanafalsafa wa Kiislamu, kwa sababu maulamaa wa Kiislamu wanamjua Mungu nao ni wanavyuoni walinzi wa mipaka na sheria za Mungu na ni waaminifu katika halali Zake na haramu Zake.

Imam aliposema, "Hakika mapitio ya mambo na sheria yamo mikononi mwa wanaomjua Mungu, waaminifu kwa halali Zake na haramu Zake," hakuwakusudia maulamaa wa zama hizo peke yao isipokuwa aliwajumlisha wote.

Iwapo maulamaa wote watakuwa waaminifu kwa halali za Mungu na haramu Zake, mbali na ujuzi wao, pia wawe waadilifu na wenye tabia nzuri, itakuwa katika uwezo wao kuyaongoza mambo, kuilinda mipaka ya Mungu na kuistawisha nidhamu ya dini. Hapo basi hakutakuwa na taabu wala dhiki wala njaa wala umasikini wala ukwamishi wa sheria zisitumike.

Hadithi hiyo ndiyo ushahidi wa upekuzi wetu ambao tungeufanya nguzo imara katika uzungumzi wetu lau sio udhaifu wa mategemeo yake.

Kwa hapo, tutaumaliza uchunguzi wetu juu ya Utawala wa Faqihi (Serikali ya Kiislamu) wala hatuoni haja ya kuingia katika matawi ya uchunguzi juu ya namna ya utoaji kodi na ushuru, hududi (mipaka ya Mungu) italindwa vipi, na kadhalika mambo kadha wa kadha ambayo hatuna nafasi ya kuyaingilia kwa sasa.

Tayari tumefanya uchunguzi na kuchambua juu ya asili (shina) la mazungumzo yetu ambayo ni Utawala wa Faqihi au Serikali ya Kiislamu na tukathibitishiwa kwamba, lililomthibitikia Mtume Muhammad SAW na Maimamu Watakatifu AS pia limemthibitikia faqihi (mjuzi wa sheria za Kiislamu).

Bila shaka maongozi yetu haya si mapya tuliyoyazua sisi, bali ni maswala yaliyofikiriwa na kuchunguzwa toka mwanzo siku nyingi zilizopita sasa.

Marehemu Mirza Hasan Shirazi[41] alipotoa hukumu (fatwa) ya kuharamisha tumbaku, alikuwa ameitoa katika msimamo wa utawala wa faqihi kwa watu wote na mafaqihi wengineo. Nao mafaqihi wa Iran isipokuwa wachache wao, walishikamana na hukumu hii. Hukumu yake hii, haikuwa ni hukumu ya ugomvi baina ya watesi wawili, bali ilikuwa ni hukumu ya kiserikali yenye kuleta maslaha kwa Waislamu kwa mnasaba wa wakati na mashindilio ya maovu kati ya watu.

Marehemu Mirza Muhammad Taqi Shirazi[42] wakati naye alipotoa fatwa ya Jihadi (vita vitakatifu vya kujihami), kisha maulamaa wote kuungana naye katika uamuzi wake, alikuwa amefuata msimamo wa serikali yake na utawala wake wa kisheria.

Inasemekana kwamba marehemu Kashiful Ghitaa[43] ameeleza pia yale niliyoyaelezea mimi. Marehemu Naraqi ambaye ni katika maulamaa wa zamani, ana maoni kwamba, mambo yote aliyoyaongoza Mtume SAW yanawalazimu mafaqihi isipokuwa tu yale yaliyokuwa mahsusi kwake peke yake.

Naye marehemu Shaykh Naini asema, "Faida yote ya mazungumzo haya yapatikana katika hadithi ya Umar bin Handhala."

Kwa hali yoyote ile, mazungumzo yetu haya si katika mambo mapya, na tumefuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu yaliyomo katika Kitabu Chake kupitia kwa Mtume Wake wakati wa kuyajadili, na tumebaini tunayoyahitaji katika maisha yetu. Lakini mazungumzo yenyewe ni yaleyale waliyoyafahamu walio wengi.

Sehemu nyingine juu ya mazungumzo haya, tumewaachia viongozi wa kesho ambao watapaswa kujitahidi kwa bidii zao zote, wawe imara na wawe na uthabiti pamoja na moyo wa kuendelea usio mwepesi wa kukata tamaa. Na inshallah Mungu akipenda watafanikiwa kulifikia lengo la kuunda serikali ya Kiislamu na kuyapanga mambo yote kwa njia nzuri. Kadhalika inshallah mambo yote yatatengemaa yakiwa mikononi mwa watu wajuzi wenye busara na wenye imani ambao wataweza kuikata mikono ya wahaini wanaoinyoshea (kudokoa) hazina ya taifa. Na Mungu Ndiye Msaidizi wetu.

Mipango kwa ajiliya Kuunda Serikali ya Kiislamu

Ni juu yetu kufanya juhudi hadi kuhakikisha tumeiunda serikali yenye maongozi ya Kiislamu na tuanze hatua zetu kwa bidii na juhudi kabambe ili tusonge mbele kwa haraka.

Ulimwenguni kote zama kwa zama, kwanza fikira huwaathiri watu wote, kisha kukawepo kuazimia na kukata shauri, kisha kazi kuanza na kufanya majaribio ya kuanza kuzitawanya fikira hizo polepole kwa watu halafu ndiyo wenye fikira hizo hupenya serikalini na kufanya mageuzo (mapinduzi) ili mambo yawe sawa kwa namna waitakayo. Fikra zenyewe zinazokusudiwa zaweza kupenya au kuhujumiwa kutoka nje ili kuing'oa misingi hiyo na kuiweka serikali itakayoendelea badala ya fikra hizo.

Fikra zenyewe huanza ndogo kisha zikakua, kisha watu wakajiunga nazo, halafu zikapata nguvu na hatimaye kushika usukani wa kuyaongoza mambo.

Kama mwonavyo, nguvu hazikuwa zimeshikana pamoja toka mwanzo. Katika hayo yote tuliyoyashuhudia, yawapasa wananchi wazifanye nguvu zao kuwa nguzo madhubuti itakayowashikilia huku wawe wanakakamia kuwa macho na kujihadhari kitaifa ili wapate wasaa wa kuzifichua njama za ufisadi pamoja na kutoa nje uharibifu walionao viongozi wa kisasa. Polepole inshallah watafaulu kuungana wote katika kuunda dola na baadaye kulifikia lengo.

Enyi wananchi! Hivi leo hamna jeshi wala dola lenu, lakini mnao na mnaumiliki uwezo wa kumwomba Mungu. Adui wenu hawajawapokonya uwezo huu wa kulingania, kuelekezana na kufanya tablighi. Jilazimisheni wakati mnapoyabaini maswala ya ibada, wakati huohuo waelezeeni watu masiala ya kisiasa katika Uislamu, yaani msimamo wa Islamu, sheria zake za umilikaji, za adhabu (penal laws), za itikadi na za kijamii, na yafanyeni mambo haya kuwa kiungo muhimu katika viungo vya kazi zenu.

rudi nyuma Yaliyomo endelea