rudi nyuma Yaliyomo endelea

Serikali adili ni miongoni mwa amana ambazo ni wajibu kuikabidhi mwenyewe na ni juu ya watu wake wawe na msimamo mzuri juu yake. Serikali ya namna hii inatenda kwa mujibu wa vipimo vya sheria tukufu na kanuni. Na hakimu (kadhi) anayeitumikia huamua kwa usawa na kwa uadilifu wala si kwa uonevu, dhuluma au upendeleo akitegemea maongozi ya dini yake safi. Nayo idara (halmashauri) ya kisheria inatakiwa kuhakikisha mafunzo ya sheria yanaimarishwa na wala hayakiukwi.

Nayo halmashauri ya utekelezaji amri inatakiwa ihakikishe kwamba watu wanatendewa mambo yaliyo na manufaa kwao na kuwaondolea taabu za umaskini, njaa na uhalifu. Pia ihakikishe amani, nidhamu na mipaka ya dini inalindwa. Yote hayo yatimizwe kwa usawa pasina kupetua nidhamu zake.

Amirul Mu'minin Ali AS baada ya kuwakata wezi wawili mikono yao kama sheria inavyoamrisha, alikuwa akiwaonea huruma, akiwabembeleza na kuwachukulia upole. Kadhalika alikuwa akiwauguza na kuikaza mikono yao kwa mafuta ya zeti mpaka wale wezi waliokatwa mikono walikuwa kwake ni wapenzi hata kuliko watu wengineo. Na alipofikiliwa na habari za uvamizi wa jeshi la Muawiyah kwa bohari (ghala) la umma na kwamba baadhi ya askari wake walimshambulia mwanamke mdhimmi na mwanamke mwengine akapokonywa vipuli vyake na furungu zake, alikaribia kupasuka kwa huzuni na masikitiko juu ya unyama wa watu hao, akiona uchungu mno na akisema "Lau angekufa mtu baada ya visa hivi kwa ajili ya masikitiko, basi mtu huyo halaumiki, bali mauti yake hayo kwangu ni wema na anastahiki." (Nahjul Balagha) Pamoja na mapenzi hayo yote ya Imam Ali AS na huruma zake, alikuwa akiubeba upanga, hali inapomlazimu kufanya hivyo, ili kuiweka shingoni mwa waharibifu ambao wanaoeneza uovu kote ulimwenguni. Huu ndio uadilifu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW ni hakimu (mtawala). Akiamuru mahali fulani patekwe au pakombolewe, au akitoa hukumu juu ya kijopo fulani kiovu kitiwe adabu, huwa ameamua kwa uadilifu kabisa, kwani lau yeye (Mtume) hangetoa amri kama hiyo mahali kama hapo, ndipo angekuwa siyo mwadilifu, kwani kiigizo cha uamuzi wake ni kwa maslahi ya maisha ya Waislamu wote.

Kwa hivyo, hakimu yeyote yule awe mtawala au kadhi ni lazima aamue kulingana na maslahi ya watu wote na wala asiyajali matamanio ya nafsi yake ili lawama yoyote juu ya utekelezi wa amri za Mungu isimshike.

Tunaijua wazi historia, jinsi Uislamu ulivyopambana na vikundi fulani fulani vya watu vilivyokuwa vikisababisha madhara kwa umma. Mtume Mtukufu SAW aliwakomesha Mayahudi wa Bani Quraidh kutokana na madhara yao waliyo yachochea kwa Waislamu na utawala wao.

Ujasiri wa hakimu na umaarufu wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hutokana na kutekeleza amri zake na kuisimamisha mipaka yake pasina kuyanyenyekea matamanio ya nafsi yake au kuvutwa na matamanio pamoja na kuwa na huruma, imani na upole juu ya watu. Sifa hizi mbili lau atakuwa nazo hakimu, kadhi au kiongozi yeyote yule, bila shaka atakuwa ni kinga au ngome ya watu kujikinga. Ama huu wasiwasi tulionao siku hizi na hofu za siku zote ni kwa ajili ya ukosekano wa utekelezi wa sheria kisawasawa, kwa maana utawala wa kisasa ni wa kulimbikizana madhara na kujigamba tu. Ama serikali kama ya Sayyidna Ali AS au serikali yoyote ile yenye Uislamu wa kikweli, katu raia wake hawawi na hofu wala wasiwasi wowote ule, bali kila mtu huishi kwa amani na utulivu maadamu hakufanya hiana, dhulma au kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu.

Imepokewa hadithi juu ya neno Lake Mwenyezi Mungu, "Zirudisheni amana kwa wenyewe"kwamba 'amana' ni Maimamu. Na neno Lake Mungu, "Na mnapotoa hukumu baina ya watu" wanaokusudiwa ni viongozi. Na kauli Yake Mungu isemayo, "NamtimiMwenyeziMungu" ni uzungumzi kwa Waislamu wote wakiamrishwa humo kuwafuata wenye mamlaka juu yao ambao ni viongozi — Maimamu.

Hapo mbeleni mnakumbuka tumeeleza makusudio ya kumtii Mwenyezi Mungu ni kufuata amri Zake kwa mambo yote ya ibada na yasiyokuwa ya ibada. Mtume SAW hakutoa amri yoyote iliyo yake mwenyewe juu ya sala isipokuwa ni yale yale maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Sisi tunaposali huwa tunatii amri ya Mwenyezi Mungu. Kumtii Mtume ni kufuata maamrisho yake yote yanayofungamana na serikali, nidhamu za maisha ya kijamii, kujijenga kinguvu na kifedha ili kuutetea Uislamu ambapo kumtii yeye ni kumtii Mwenyezi Mungu. Kwako wewe kumtii Mtume ni kuyafuata maamrisho yake anayokuamuru. Akikwambia ujiunge na jeshi la Usamah au kuilinda ngome ya vita vyajihadi au utoe mchango, kodi au ushuru, au amekuamuru utangamane na watu kwa wema, haikufalii hata kidogo kujitenga au kuhalifu amri hizo za Mtume Mtukufu SAW.

Mungu alituamuru tuyapokee aliyotuletea Mtume na tukomeke kwa aliyotukanya kama alivyotuamuru kuwaheshimu na kujifunza kwa wenye mamlaka (mawalii) juu yetu ambao ni Maimamu huku tukijua wazi kwamba, kumtii Mtume na wenye mamlaka juu yetu ni kumtii Mwenyezi Mungu, kwa maana utiifu wetu kwao ni kufuata amri yake Mungu ya kuwafuata.

Baadaye kuna aya isemayo: "Mnapogombana juu ya jambo lolote lile, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na kwa Mtume ikiwa mnamwamini Mungu na siku ya Mwisho, hayo ni bora kwenu na ni maelezo mazuri mno. " (4:59)

Utesi na ugomvi baina ya watu hutokea juu ya mambo ya umilikaji wa haki fulani ambayo kadhi au hakimu huhitajika kutoa uamuzi kwa mujibu wa ushahidi uliopo mbele yake na viapo. Wakati mwingine, huwa ugomvi ni jambo lililozuka kwa mtu mwingine kumwonea mwingine, kumdhulumu, kumchokoza, kumwibia au mambo mengine. Ugomvi katika hali kama hii, pande zote mbili zinazohusika zitahitajika kuanza kutoa madai yake ndipo sheria iangalie uamuzi wake. Uamuzi wake ni adhabu itolewe kwa mhalifu.

Qur'ani Takatifu, inatupa agizo la amri ya kumrejelea Mtume Mtukufu SAW katika kesi zote. Ziwe za daawa, yaani umilikaji (civil case) au zajinai, yaani uvunjaji sheria (criminal case) kwa kuwa yeye ndiye rais wa dola la Kiislamu aliyetakiwa kuhakikisha haki mafuatwa na batili kuangamizwa. Baada yake watayaendesha mambo Maimamu na halafu mafaqihi waadilifu.

MAANA YA TAGHUTI

Baada ya hayo, Mwenyezi Mungu asema:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُواْ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُواْ اِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُواْ أَن يَكْفُرُواْ...

"Je, huwaoni wale wanaodai eti wameyaamim yale uliyoteremshiwa na yaliyoteremshwa kabla yako? Wanataka [ugomvi wao na kesi 2.0.0] wahukumiane kwa shetani (taghuti) na hali waliamrishwa kumkana..." (4:60).

Makusudi ya taghuti (shetani) ni kila chama, idara ya utawala, halmashauri au serikali isiyotumia aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, mbali na uonevu, dhuluma, uchokozi na maovu mengineyo. Mwenyezi Mungu alituamrisha kuyakataa mambo ya namna hiyo na akatuhimiza tuiasi na kuigomea kabisa serikali yoyote dhalimu hata kama uasi wetu una uzito na mashaka kwetu.

Umar bin Handhala alisema: "Nilimuuliza Abi Abdillah (Imam Sadiq AS) juu ya watu wawili miongoni mwa masahaba (wafuasi) wetu waliogombana juu ya deni au urithi, kisha wakayapeleka malalamiko yao kwa mfalme au hakimu (asiyefuata sheria za Mwenyezi Mungu). Je ni halali kufanya hivyo? Akajibu: 'Kushtakiana au kupelekana korti ya aina hii kwa jambo la kweli au la uwongo (ubatilifu) ni kushtakiana kwa taghuti (shetani). Na mmoja wao atakachohukumiwa apewe japo ni haki yake inayotambuliwa, atakichukua hali ni haramu kwake, kwa maana amekipokea kutokana na hukumu

iliyotolewa na taghuti (shetani) ambaye Mwenyezi Mungu alitoa amri kumkataa na kumkana. Mungu asema, "Wanataka [ugomvi wao na kesizao] wahukumiane kwa taghuti (shetani) na hali waliamrishwa kumkana.' " Nikamwuliza, 'Watafanyaje basi?' Akajibu, 'Watamwangalia miongoni mwenu aliyezipokea hadithi zetu, akatizama (vyema) halali zetu na haramu zetu. Mtu wa aina hiyo wamridhie awe hakimu wao, na kwa hakika mimi mtu kama huyo nimemfanya awe hakimu wenu.' "

Maelezo ya Imam juu ya aya hiyo yanathibitisha hukumu zote. Tumeeleza mbele pia kwamba ili kusuluhisha ugomvi juu ya madai mbalimbali yawe ya umilikaji wa haki au jinai, lazima warejelee katika mahakama na kwa wanaohusika na utekelezaji wa sheria, yaani watawala. Sababu ya wateti kwenda mahakamani ni kupata haki inayostahiki katika kuamua ugomvi, na sababu ya kwenda kwa wanaohusika na kutekeleza sheria ni kuwalazimisha kufuata uamuzi unaotolewa kwa pande zote mbili. Kwa hivyo, katika hadithi hii Imam anaulizwa ikiwa inaruhusiwa kupeleka mashtaka kwa madhalimu na watawala wasiofuata sheria za Mwenyezi Mungu.

UHARAMU WA KULALAMIKIANA KWA MAHAKIMU WAONEVU

Jawabu hilo la Imam limemkataza mwulizaji juu ya kupelekana kuhukumiana kwa mahakimu waonevu katika masiala ya umilikaji haki, yaani kesi za madaawa (civil case) au juu ya masiala ya uhalifu, yaani kesi za uvunjaji sheria (criminal case) hata ikiwa hasa imethibitishwa iko upande gani. Vilevile Imam alifahamisha kwamba, yeyote mwenye kuwalalamikia huwa amewataka mataghuti (mashetani) wamhukumu ambao Mwenyezi Mungu aliamuru wakataliwe. Sheria yakanya kukipokea kilichotolewa na mahakama hayo. La sivyo, ni kupokea haramu hata kama ni haki yako inayotambulikana. Kwa hivyo, Waislamu wanatahadharishwa, wanapodaiana madeni, kutopelekana mbele ya mahakimu wa aina hiyo wasije wakapoteza haki zao za halali kwa kugeuka kuwa haramu. Mafaqihi wekevu nao wameutilia sana mkazo uamuzi huu, kwa hivyo hata ugomvi wa kitu au matumizi ya kitu kama joho, haifai kuwaendea watu kama hao kukutolea hukumu.

Maeleweko ya hadithi hii ya Handhala, ni uamuzi wa kisiasa au hekima wa kuwafanya Waislamu kutowarejelea masultani wajeuri wa namna hiyo na mahakama yao, kusudi watu wakiwahama, shughuli zao zisimame na kuwafungulia milango Maimamu au mafaqihi wawasawazishe watu. Lengo hasa la hadithi hii, ni kutowapa nafasi mahakimu waonevu kuendelea kuwahukumu watu huku wazipoteze haki zao, kwani Mwenyezi Mungu amewazuia watu kuwarejelea, na akaamuru kuwauzulu na kuzikana hukumu zao kwa kosa lao tu la kudhulumu na kuacha kwao kufuata njia iliyo sawa. Hii ni hukumu ya kisiasa ya Kiislamu ambayo ikifuatwa, serikali za kidhalimu zitaanguka.

MAULAMAA WA KIISLAMU NDIO MAREJEO YA WAISLAMU KWA MAMBO YOTE

Kwa mujibu wa mapokezi kutoka kwa Imam, anayerejelewa katika maswala ni yule ambaye kazipokea hadithi zao, akajua halali zao na haramu zao, na pia akachungua kwa uangalifu sana hukumu zote kulingana na mizani alizonazo juu ya jitihadi. Imam vilevile katika jibu lake hakuacha sharti la uangalifu kwa mpokezi wa hadithi na hukumu. Kwa hivyo, mnakili wa hadithi asiye na maarifa au uangalifu harejelewi.

MAULAMAA WALIWEKWA KUTOA HUKUMU

Imam AS asema, "Kwa hakika mimi nimemfanya awe hakimu wenu," hivyo, ni juu ya watu kumridhia awe hakimu wao katika utesi wao wote pasina kumwendea mwingine.

Na hukumu ya kisheria atakayoitoa, itawahusu Waislamu wote na wala si Umar bin Handhala peke yake aliyejibiwa na Imam, namna Imam Ali AS alivyokuwa akiwateua maulamaa na mafaqihi kabla ya kufariki kwake.

Hadithi hii inayohusu uteuzi wa wanavyuoni na mafaqihi mahakimu ambao watayaendesha mambo yote ya umma, haitiliwi shaka yoyote juu ya mategemeo yake na dalili zake. Na bila shaka Imam aliwateua mafaqihi wa kuyaendesha mambo yote yakiwemo kuhukumu na kutawala.

Baada ya ufafanuzi huo, hebu basi tugeukie upande wa hadithi ya Abi Khadija ili kuyakuza mazungumzo yetu. Abi Khadija alisema kwamba Imam Sadiq AS alimtuma kwa mmoja wa masahaba wao kumwambia: "Waambie kwamba, jihadharini unapozuka ugomvi baina yenu au uzungushi wa kitu chochote cha kutoa au kupokea (jihadharini) kupelekana katika mahakama ya mmojawapo wa hao mafasiki, bali mwekeni baina yenu mtu ambaye anajua halali kwetu na haramu kwetu, kwani mimi nimemfanya awe hakimu (kadhi) juu yenu. Vilevile jihadharini kuupeleka utesi wenu rnbele ya mtawala mjeuri (mwenye dhulma)." (Wasaail, jz. 18, uk. 100, hadithiya6)

Mafasiki waliotajwa, ni mahakimu walioteuliwa na viongozi wa nyakati hizo. Katika hadithi iliyotangulia, Imam alikataza kuwarejelea watawala madhalimu na mahakimu waonevu, na akawaweka wa kurejelewa. Katika hadithi ya Handhala, alimbaini hakimu mtekelezi na mpitishi wa uamuzi. Mwisho wa hadithi, yaonesha, masultani walikuwa wakirejelewa katika ugomvi mwingine ambao haukurejelewa mahakimu.

JE, MAULAMAA WALIJIUZULU VYEO VYA UHAKIMU?

Hivi sasa, lazima tufahamu kwamba kufuatana na hadithi hii Imam aliwateua mafaqihi kuwa mahakimu (makadhi) katika uhai wake mwenyewe. Na kwa mujibu wa hadithi ya Umar bin Handhala, Imam aliwapa vyeo vyote viwili — uhakimu na uongozi. Je, baada ya kufariki kwa Imam waliuzuliwa vyeo vyao?

Sote tunajua wazi, amri za Maimamu ni tofauti na amri za watu wengine. Imani ya madhehebu yetu ni kwamba amri zote zilizotolewa na Maimamu ni lazima zitimizwe na ni wajibu zifuatwe hata baada ya kufa kwao. Basi itakuwaje kwa mahakimu walioainishwa hasa kwa dalili wazi kama hizo?

Mataifa mbalimbali yanayotawaliwa na wafalme au jamhuri, pindi afapo rais au mfalme au kutokea mapinduzi, jambo kama hilo halipangui nidhamu za idara na wizara au vyeo vya majeshi hata ingawa serikali inayofuata itakuwa na maongozi tofauti na ya kwanza. Japo huwepo mabadiliko madogo madogo, lakini hayafanywi palepale.

Hivi sasa tunaona kwamba, lau faqihi atamteua mtu kumwakilisha sehemu fulani maalum, au atampandisha cheo mtu, hilo laweza kugeuzwa palepale pakitokea kifo cha faqihi huyo. Lakini, lau atamwainisha mtu awe mlinzijuu ya mtoto au atawalie mambo ya wakf, hayo hayana taathiri yoyote pakitokea kifo cha faqihi huyo, bali mambo yataendelea kama kawaida. Basi ni kwa namna gani utakuwa uteuzi wa mafaqihi ili watoe hukumu baina ya watu na mahakimu?

VYEO VYA MAULAMAA VIMEHIFADHIKA DAIMA

Sisi tunayo imani kwamba, cheo Maimamu walichowapa mafaqihi kimehifadhiwa, kwa maana Maimamu ambao hatuwezi kuwa na dhana ya ughafilivu kutokana na wao, mbali na kuitakidi uzunguko wao kwa mambo ya Waislamu, walijua wazi kwamba, cheo hiki hakiwabanduki maulamaa japo baada ya kufa kwao. Pia kwa vile Imam alijua kwamba uteuzi huo ni katika jukumu lake, lau angejua wateuliwa wake wataendesha shughuli zama za uhai wake, bila shaka angewatana bahisha watu kwamba uteuzi huu ni wa muda tu wa uhai wangu, ama baadaye nikisha kufa, watauzuliwa.

Hivyo basi, hadithi hii yatumakinishia kuhifadhika kwa vyeo vyao, wala hapana uwezekano wa kuamini kwamba, Imam aliyemfuata Ja'far Sadiq AS aliwaondoa mafaqihi madarakani, kwani machukuliko au imani hiyo ni dhaifu na wala haikupokewa. Pia huyohuyo Imam mwenyewe, alizuia kuwarejelea masultani madhalimu, na anaowakusudia kuwarejelea ni kurejelea mataghuti (mashetani), akishikamana na aya inayokanya kumwandama taghuti. Iwapo Imam aliyepo angewauzulu wanavyuoni na asiwateue wengine, basi je Waislamu watamwendea nani kunapozuka tofauti baina yao wao kwa wao na katika utesi wao? Je, tena wawarudie walewale mafasiki? Au mataghuti? Au basi wataishi katika hali ya ukosekano wa maongozi ili mali zao zipotee bure na ulaji wa mali za batili utawale na mipaka ya Mungu ikiukwe pasina upinzani?

Sisi hatuna imani kabisa ya kumdhania Imam Musa bin Ja'far AS kuwa aliyapinga aliyoyafanya Imam Sadiq AS juu ya jambo hili au lile. Hangeweza kuzuia mafaqihi waadilifu warejelewe au kuruhusu mataghuti warejelewe, pia hangeruhusu upotevu wa haki za watu, mali na nafsi. Imam hawezi kuipinga au kuiondoa misingi aliyoiimarisha na kuwaelekeza kwayo yule aliyemtangulia isipokuwa tu uwezekano wa kufanya mageuzo kidogo katika watu au mahakimu na makadhi zama za uhai wake ili kuleta maslahi fulani kwa umma. Na kwa kufanya hivyo, hazingatiwi wala hachukuliwi kuwa anapinga waliyoyajenga waliomtangulia.

Dalili zote hizo za kwanza ziko wazi kabisa tena dhahiri. Hivi sasa tutaendelea kuyajenga mazungumzo yetu kwa hadithi hizi.

HADITHI ILIYOPOKEWA NA QADDAH

Qaddah (Abdallah bin Maamun) alipokea hadithi kutoka kwa Imam Ja'far Sadiq AS akisema kwamba Mtume SAW alisema:

قال رسول الله «ص»: من سلک طريقاً يطلب فيه علماً سلک الله به طريقاً إلی الجنة، وإن الملائکة لتضع أجنحتها لطالب العلم رضاء به، وإنه ليستغفر لطالب العلم من في السماء ومن في الأرض حتی الحوت في البحر، وفضل العالم علی العابد کفضل القمر علی سائر النجوم ليلة البدر، وان العلماء ورثة الانبياء.

"Mwenye kuishika njia kutafuta elimu, Mwenyezi Mungu (siku ya Kiyama) atamshikisha njia ya kwenda peponi, nao malaika humkunjulia mabawa zao mtu anayetafuta elimu ili kuonyesha radhi yao kwake. Kadhalika waliomo mbinguni na ardhini, hata samaki walio baharini, nao humwombea msamaha mtu anayetafuta elimu. Na ubora wa aalimu (mwanachuoni) juu ya mfanya ibada (asiyejua) ni kama ubora wa mwezi juu ya nyota. Na maulamaa (wanavyuoni) ni warithi wa Manabii. Manabii hawakurithisha dirham wala dinari, bali walirithisha elimu. Basi anayeichukua huwa amechukua fungu kubwa sana." (al-Kafi, jz. 1, uk. 24)

Hadithi hii ni sahihi, na imepokewa na watu wanaoaminika upokezi wao, kama Ibrahim bin Hashim. Hadithi hii imepokewa kwa njia zenye mategemeo sahihi ingawa kuna kutofautiana baina ya wapokezi wake juu ya kufuatisha neno kwa neno.

HADITHI ILIYOPOKEWA NA ABUL BAKHTARI

Abul Bakhtari amepokea hadithi kutoka kwa Imam Sadiq AS akisema: "Hakika maulamaa ni warithi wa Manabii, kwani Manabii hawakurithisha dirham wala dinari, na si jingine bali walirithisha hadithi zao. Basi anayepokea chochote katika hadithi hizo huwa amenufaika fungu kubwa, kwa hivyo angalieni wenyewe, elimu yenu mtaichukua kwa nani?" al-Kafi, jz. l,uk.32)

Makusudio yetu hasa ya kuinakili hadithi hii ambayo marehemu Naraqi aliishika kwa mikono yake yote miwili, ni kufafanua maana ya jumla, "maulamaa ni warithi wa Manabii" na tutaichunguza kama ifuatavyo:

1- Makusudio hasa ya neno maulamaa katika hadithi hii ni nini? Wengine waliyachukulia kuwa ni Maimamu. Lakini lililo sahihi zaidi ni kuwa, makusudio ni wanavyuoni (maula-maa) wa Kiislamu, kwa dalili ya kuwa, Maimamu kulingana na utukufu wao hawangeweza kusemwa kwa namna kama hii. Wala hadithi hii haiwezekani kuwa kitambulisho chao kwa vyovyote vile.

Hadithi hii ya Abul Bakhtari, baada ya kutajwa kifungu "maulamaa ni warithi wa Manabii" aliongeza kifungu kingine, "angalieni wenyewe, elimu yenu mtaichukua kwa nani?" Maneno kama hayo hayaaminiki kuwalenga Maimamu, bali kila atakayeyachunguza yaliyopokewa kuhusu shani zao na daraja zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, ataamua moja kwa moja kwamba, waliolengwa katika hadithi zote hizo mbili sio Maimamu, bali ni maulamaa (wanavyuoni). Utukufu kama huu maulamaa kuwa nao si jambo geni la kushangaza, hasa tukikumbuka mapokezi mengi yaliyopokewa kuthibitisha shani, heshima na utukufu wao mkiwemo hadithi inayosema, "Maulamaa wa umma wangu ni kama Manabii wa kabla yangu" na hadithi nyingine vilevile ya Mtume isemayo, "Maulamaa wa umma wangu ni kama Manabii wa Bani Israil." Hivyo, muradi na makusudio ya maulamaa, ni wanavyuoni wa umma wa Kiislamu.

2- Pengine atatokea mtu ayapinge hayo aseme, "Kifungu ' maulamaa ni warithi wa Manabii,' hakitupi faida ya kuthibitisha uongozi au utawala wa faqihi, kwani urithi huu unaokusudiwa, unazingatiwa waliyopewa Manabii yakiwemo ufunuo, na hukumu za sheria ambapo zingatio hili halina maana ya uongozi wa mambo ya watu, kwani utawala wao huthibitika lau pangekuwa na zingatio jingine lisilo hilo la kwanza. Kama hadithi ingeeleza waziwazi kwamba daraja la maulamaa ni sawa na daraja la Nabii Musa AS au Nabii Isa AS, hapo tungefahamu kuwa maulamaa pia wana itibari ya kutawala, kwa kuwa mmoja katika wadhifa wa Manabii hao ulikuwa ni kutawala. Hivyo basi, hadithi hii haithibitishi daraja la utawala wa maulamaa."

Jibu la upinzani huu, nasema, kwamba kipimio cha kuyaelewa na kuyafahamu mapokezi ya hadithi kwa kuchukua udhahiri wa matamshi yake, ni sheria na upeo wa fahamu za kawaida. Na wala sio utatuzi wa kielimu au upekuzi wa kindani. Sisi hufahamu kutokana na sheria. Faqihi akikadiriwa awe akitumia utatuzi wa kielimu na uchunguzi wa ndani wa maana, bila shaka mambo mengi sana yatampita.

Tukiirudia sheria ili tufahamu maana ya ibara "maulamaa ni warithi wa Manabii," na kuiuliza (hiyo sheria), je ibara hii ina maana, cheo cha faqihi ni kama cha Mtume Musa na Isa AS? Jibu lingekuwa, "Ndiyo," kwani hadithi hii inawafanya maulamaa kuwa sawa na Manabii. Na kwa kuwa Musa na Isa ni katika Manabii, basi maulamaa ni kama Musa na Isa. Pia lau tungeiuliza sheria, "Je, faqihi ni mrithi wa Mtume Mtukufu SAW?" Jibu lingekuwa, "Ndiyo" kwa maana yaleyale ya kwanza.

Sisi hatuyachukui maana ya Utume au Unabii kuwa na maana tu ya kuletewa wahyi au kujua sunna na hukumu za kisheria. Japo lau machukulio haya yamepokewa katika lafdhi ya umoja, lakini hayachukuliwi katika neno 'Manabii' lenye lafdhi ya wingi. Upokezi wa neno 'Manabii' kwa lafdhi ya wingi, hakika si jingine bali hukusudiwa manabii wote, si kuwa tu wao ni Manabii wanaopelekewa wahyi (ufunuo), bali kwa kuwa wao pia ni mawalii (wenye mamlaka). Kwa maana, kuwaepusha Manabii, yaani kutowasifu, kwa sifa zote na shani zote wanazozistahiki isipokuwa tu elimu na ufunuo, halafu kuwatuza maulamaa matulio yao (yaani katika vyeo vya kuwalinganisha na Mitume) katika hukumu za hadithi na hukumu za kisheria peke yake, ni kuelewa kimakosa kabisa ambako ni kinyume hasa na sheria za wenye busara.

3- Hata lau tutawatuza, yaani tutawaweka maulamaa katika vyeo vya Manabii kwa kuwaita Manabii, basi itafaa kumpa mfananishwa mambo yote ya mfananishiwa. Kwa mfano, ukisema fulani ana daraja ya mwadilifu, kisha ukasema, ni lazima kumheshimu mtu mwadilifu, basi kwa hapo sisi tutafahamu kwamba, huyu ambaye ana daraja ya mwadilifu, ni lazima aheshimiwe. Kwa hapo tena ndipo tutaweza kuyastafidi maneno ya Mwenyezi Mungu aliponena "Mtume ana haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao," (33:6) kuwa yanathibitisha cheo cha utawala kimewastahiki maulamaa kama ilivyo katika kitabu Majmaul Bahrayn katika hadithi ya Imam Baqir AS baada ya aya hii aliposema, "Aya hii ilishuka katika kuthibitisha utawala." (uk. 457)

Mtume Mtukufu SAW ni mtawala wa waumini wote na ni amiri wao. Maulamaa nao baada ya Mtume pana uthibitisho wa kuongozana wao kwa wao japo hawakutajwa katika aya hii.

Hivyo hivyo, tunaweza kupata dalili zaidi kwa kutumia aya kama, "Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume," (4:59) ili kuthibitisha kwamba hakuna tofauti baina ya Mtume na Nabii katika majina, ingawa katika baadhi ya hadithi kunatolewa tofauti zao katika namna ya upokezi wa wahyi. Lakini kiakili na kisheria lakabu za Mtume na Nabii zinaeleweka kuwa na maana moja. 'Nabii' ni yule mtu ambaye ananabii (anabashiri) kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na 'Mtume' (au Rasuli) ni yule mtu ambaye huwafikishia watu yale anayoamrishwa na Mwenyezi Mungu.

4- Huenda kukawa na atakayesema kwamba, urithi wa Mtume ni hadithi tu alizoziacha, na atakayepata chochote katika hadithi hizo atakuwa amemrithi Mtume Mtukufu SAW. Lakini hamna uthibitisho wa faqihi kumrithi utawala na uongozi.

Jibu: Upinzani huu si wa kweli, maana umesimama juu ya misingi ya kukataza urithi wa utawala.

Sisi kama mjuavyo, tunachimbua usemi wetu kutoka kwa sheria. Lau tutawauliza watu, hasa walio na busara juu ya uwezekano wa kukirithi kiti fulani cha enzi cha kifalme, jawabu yao haitakuwa "haiwezekani" bali watamtaja mrithi. Nao utawala huu tunaouzungumzia, unaweza kutoka kwa mtu ukamwendea mwingine kulingana na maoni ya kisheria ya wenye busara.

Tukifananisha neno la Mungu, "Mtume ana haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao " kisha tuangalie "Maulamaa ni warithi wa Manabii" tutajua kwamba, utawala ni katika mambo ambayo yanazingatiwa na ambayo inamkinika kutoka hapa na kwenda pale, na wala hilo si muhali kabisa. Hata lau tutafaridhia jumla, "Maulamaa ni warithi wa Mitume" kwamba ni kwa Maimamu peke yao, bila shaka ni katika mambo yote, pamoja na elimu na sheria.

Kumrithi Mtume Mtukufu SAW kulingana na jumla hiyo, ni juu ya mambo yote yakiwemo kuwaongoza watu na mambo yao. Na hili ni kwa Maimamu baada yake, kisha mafaqihi baada yao, isipokuwa tu mambo yaliyo mahsusi kwa Mtume peke yake ambayo hatuna haja kuyazungumzia hapa.

Nguzo inayoitilia nguvu shaka ya kwanza yenye jumla, "Maulamaa ni warithi wa Manabii" ni ule urithi wa hadithi tu kama hadithi ya Qaddah inavyoonyesha, "Hakika Manabii hawakurithisha. . . isipokuwa elimu" na hadithi ya Abul Bakhtari inavyojieleza wazi, ".. . hawakurithisha dirham wala dinari, na hakika si jingine bali walirithisha hadithi zao" ni uwazi wa kuonyesha kwamba, urithi wao ni katika hadithi pasina urithi mwingine na hasa kwa kutumia neno "Na hakika si jingine bali" katika hadithi hii ya mwisho.

Shaka hii ni dhaifu tena sana, kwa maana, lau alichokirithisha Mtume Mtukufu SAW kingekuwa ni hadithi tu bila jambo jingine, basi hilo lingehitalifiana na msimamo wa madhehebu yetu, maana Mtume aliyekuwa akiyaendesha mambo yote ya watu, alimteua Imam Ali AS awe mtawala baada yake, na uongozi huu ukaendelea kutoka kwa huyu hadi kwa yule. Zaidi ya hayo, jumla "Hakika si jingine bali" haikuthibitika kuwa kila inapotumika daima huwa kikomo cha maongezeo. Tenajumla hiyohiyo haimo katika hadithi ya Qaddah isipokuwa tu katika hadithi ya Abul Bakhtari ambayo kwa upande wa sanadi (mategemeo) yake ni dhaifu.

Hebu tuitazame hadithi yenyewe. Je, ina maana ya urithi wa hadithi peke yake ama vipi?

"Mwenye kushika njia kutafuta elimu, Mwenyezi Mungu humshikisha njia ya kwenda peponi ..." Jumla hii inawasifu maulamaa. Na taarifa kamili juu ya aalimu (mwanachuoni), sifa zake na wadhifa wake, kirejeleeni kitabu kiitwacho al-Kafi ili mtambue kwamba sifa hii haitumiki kwa mtu yeyote asiyekuwa na elimu ya kutosha, bali kuna masharti kadha wa kadha na vipengee vigumu.

"Na kwa hakika malaika humwekea anayetafuta elimu mabawa yao kuonyesha radhi yao kwake." Hii ni kuonyesha heshima yao ya kumtukuza na kumwadhimisha.

"Na waliomo ardhini na mbinguni hata samaki wa baharini, humwombea msamaha ..." Jumla hii ingehitaji ufafanuzi zaidi tukiwa nje ya mazungumzo yetu haya.

"Na ubora wa aalimu (mwanachuoni) juu ya mwenye kufanya ibada (pasina kujua) ni kama ubora wa mbalamwezi juu ya nyota." Maana ya kifungu hiki yajieleza yenyewe.

"Na kwa hakika maulamaa ni warithi wa Manabii." Jumla hii ni katika kuonesha utukufu wa maulamaa na ubora wao mbali na tuliyoyaona mwanzo wa hadithi hii. Urithi wa maulamaa kwa manabii ni katika fadhila ikiwa watatua mahali pao katika kuwaongoza watu, kuyaendesha mambo yao yote ya kiserikali na kutiiwa.

Ama kifungu cha mwisho cha hadithi kinachosema, "Hakika Manabii hawakurithisha dinari waladirhamu" hakina maana ya kutorithi kwao zaidi ya elimu, sheria na hukumu, bali kifungu hiki kina maana kwamba, mbali na kuyaongoza mambo ya watu na utawala, hawatakuwa na tamaa itakayowachukua kujishughulisha na ulimwengu na kuukusanya ubatili wa ulimwengu pamoja na kuweka mbele anasa na mapambo ya kimaisha. Maisha duni waliyoishi Mitume — pamoja na kuwa uwezo wote walikuwa nao — yalikuwa tofauti sana na maisha ya kifalme na wakuu wa serikali za kisasa wanaoufanya uongozi wao na madaraka yao kuwa njia ya kuwafungulia milango ya kufanya mambo machafu tena ya aibu yasiyo ya kisheria yakiwemo anasa, utajiri wa kibinafsi na ukosefu wa ridhaa.

rudi nyuma Yaliyomo endelea