rudi nyuma Yaliyomo endelea

MADHUMUNI YA UTUME

Kwa mnasaba wa hukumu ya akili mbali na sheria, lengo la kutumwa Mitume si kubainisha na kuweka wazi hukumu na sheria ambazo huzipokea kupitia ufunuo (Wahyi). Mitume hawakuteuliwa kuzifikisha hukumu hizi kwa watu tu wakitumia uaminifu kamili, wala nao hawakuwataka mafaqihi watosheke na kuwabainishia watu mambo waliyowafunza pasina jambo jingine. Pia kifungu "Mafaqihi ni waaminifu (wawakilishi) wa Mitume" hakina maana ya uaminifu wao kwa yale wanayoyanakili kutokamana na Mitume tu.

Umuhimu mkubwa waliotakiwa kuutimiza hao Mitume, ni kuhakikisha utengevu wa nidhamu adilifu katika jamii na kutekeleza sheria. Hayo yanathibitishwa na maneno ya Mwenyezi Mungu aliponena:

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ

Hakika tuliwapeleka Mitume Wetu (kuwaongozd watu) kwa dalili waziwazi, na tukakiteremsha pamoja nao kitabu na mizani ili watu wasimame kwa uadilifu. "(57:25)

Lengo kubwa la kupelekwa Mitume ni kusimamisha, yaani kuweka uadilifu na usawa kwa watu, pia kuwapangia maisha yao kulingana na mujibu wa mizani za kisheria. Lakini hayo hayatimii ila kupitia kwa serikali itakayozipitisha sheria. Namna mambo yatakavyokwenda yakiongozwa na Nabii au Mtume, ndivyo yatakavyokuwa kwa Maimamu na mafaqihi wenye imani na waadilifu watakaoongoza baada ya hao Mitume. Kwa hali yoyote ile, nidhamu, uadilifu na kutumia haki ni jambo linalotakikana na watu, na hasa viongozi kuwa nalo.

Mwenyezi Mungu anasema juu ya khums: "Na jueni ya kwamba, chochote mnachokichuma [na kufaidika] basi sehemu yake ya tano itolewe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa (ajili ya) Mtume na kwa jamaa. . . " (8:41). Na pia aliposema juu ya zaka:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم.

"Chukua sadaka katika mali zao"(9:103), na aliposema juu ya ushuru mwingine hakuwa na maana ya Mtume kufikisha ujumbe huu tu, bali ameamriwa aoneshe kwa vitendo na apitishe sheria za utekelezi. Aliamriwa aikusanye michango hii ili aitumie katika maslahi ya Waislamu. Kadhalika alitakiwa aeneze uadilifu baina yao, ailinde mipaka ya Mwenyezi Mungu na ngome ya Waislamu. Pia aliamriwa kuilinda nchi isitwaliwe na maadui, na hazina ya umma aitunze barabara ili isifanyiwe hiana na yeyote.

Kuna aya katika Qur'ani inayosema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَطِيعُواْ اللّهَ وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُوْلِي الأَمْرِ مِنكُمْ

Enyi mlioamini, mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka miongoni mwenu " (4:59).

Aya hiyo haituhimizi tuwasadiki tu kwa wanayotueleza, bali makusudio hasa ni kutenda na kufuata ambayo ndani yake mna radhi ya Mwenyezi Mungu ikiwa tutafanya hivyo, kwani Mwenyezi Mungu ameelezea mahali pengine akasema:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

" Na alichowapeni Mtume basipokeeni, na anachowakatazeni basi jiepusheni nacho ..." (59:7). Kufanya kazi zote zilizo au zisizo za kiibada ambazo zahusiana na sheria za Kiislamu ni sawa na kumtii Mwenyezi Mungu. Kumtii Mtume Mtukufu SAW si tu kuzikubali amri zake bali ni kuzitekeleza.

Kumtii Mtume ni sawa na kumtii Mwenyezi Mungu Mwenyewe, kwa maana Mtume hatamki kwa matamanio ya nafsi yake bali kwa ufunuo anaofunuliwa. Mtume alipoamuru kujiunga na msafara wa jeshi la Usamah haikuwa sawa kulihalifu, yaani kujitenga nalo au kulirejesha, kwani katika kufanya hivyo ni sawa na kumwasi Mtume Mtukufu SAW ambaye ni rais na kiongozi wa umma wa Kiislamu. Mwenyezi Mungu alimpa Mtume utawala wa kuyasimamia mambo yote ya Waislamu mkiwemo kuwaongoza na kuwaelekeza, pia kuwateulia mahakimu na viongozi, na kuwauzulu wengine akilazimika kufanya hivyo.

MAFAQIHI N1 WAAMINIFU WA MITUME KATIKA KUYAONGOZA MAJESHI, KUIHUDUMIA JAMII, KUUTETEA UMMA NA KUTOA HUKUMU BAINA YA WATU

Hadithi iliyoelezwa hapo mwanzo ambayo imebainisha uaminifu wa mafaqihi kwa Mitume, mna sharti kwa mafaqihi kutojiingiza katika mambo ya kidunia. Sababu iwapo faqihi mawazo yake yatakaposhughulika na upuzi wa kidunia, hataweza kuwa mwadilifu na hatahesabika katika wale walio waaminifu na wawakilishi wa Mitume, na wala hawezi kuzitimiza sheria za Kiislamu. Ama mafaqihi waadilifu ndio peke yao wanaostahili kutoa maamuzi ya Kiislamu, kuimakinisha mipango yake, kuisimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu na kuilinda ngome ya Waislamu.

Mwenyezi Mungu alimfanya Mtume Muhammad SAW kuwa ni kiongozi (rais) na mtawala wa Waislamu, akamwamuru azipitishe sheria za Kiislamu na kuweka nidhamu ya Kiislamu na akaamuru kutiiwa kwake kuwa ni lazima. Vivyo hivyo, kumekuwa lazima kwa mafaqihi waadilifu kuchukua madaraka ya utawala na uongozi ili kutekeleza sheria za Mwenyezi Mungu na kuunda nidhamu ya umma wa Kiislamu.

SERIKALI INAYOSHIKAMANA NA KANUNI (SHERIA)

Kwa vile serikali ya Kiislamu ni yenye maongozi ya kisheria, basi mafaqihi ndio watakao simamia mambo ya serikali hiyo na wala si watu wengine. Watafanya vilevile alivyokuwa akifanya Mtume pasina kuongeza kitu au kupunguza, yaani watasimamia mambo yote ya idara, utaratibu na kutekeleza mipango ya nchi. Wataisimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu aliyoiweka ili isikiukwe kwa namna alivyofanya Mtume, wahukumu kwa kutumia katiba na sheria za Mwenyezi Mungu, wakusanye kinachozidi katika mali za raia wakiweke katika Baytul Maal (Hazina ya Taifa au Umma) na wawe waaminifu juu yake ili kiasi hicho wasikikodolee macho baadaye.

Ikiwa faqihi anataka kumpa adhabu mzinifu ni lazima atowe hukumu kufuatana na sheria iliyowekwa na utaratibu wake wa kumpa adhabu, yaani mzinifu lazima aletwe mbele ya watu na apigwe viboko mia moja. Hana haki ya kumpiga kiboko kimoja zaidi, au kumpiga kofi, au kumtukana au hata kumfunga siku moja. Na ikiwa faqihi atatoza ushuru na kodi basi lazima ifanywe kufuatana na masharti yaliyowekwa katika kanuni za Kiislamu bila kuchukua hata senti moja zaidi ili kwamba Hazina ya Umma (Baytul Maal) ihifadhiwe kutokana na ufisadi.

Iwapo faqihi atazihalifu sheria za dini — na Mungu atusamehe kwa kusema hivyo - huyo moja kwa moja auzuliwe palepale, yaani aondolewe uongozini kwa kukosekana asili ya uaminifu katika uongozi wake. Kwa hivyo basi itaeleweka wazi kuwa, hakimu mkuu ni sheria, na watu wote wako chini ya kivuli chake.

Watu wote toka kuzaliwa kwao ni waungwana walio huru kuzitumia haki zao za halali, wala haiwi kwa yeyote kuwa na haki ya kuwa juu ya mwingine, wala haimfalii mtu baada ya upitishi wa sheria kumshurutisha mwengine kukaa mahali maalum au kwenda mahali maalum pasina haki. Maongozi ya Kiislamu huwatunza watu wake kwa usalama na amani wala hayawapokonyi utulivu wao.

K.ama mnavyozishuhudia, Mwislamu na hata asiye Mwislamu huishi kwa hofu katika serikali nyingi za siku hizi, akichelea wakati wowote atavamiwa nyumbani mwake na kupokonywa roho yake, mali yake na chochote anachokimiliki. Mambo kama hayo ya kutooneana imani yalifanyika sana zama za utawala wa Muawiyah[33]. Yeye mwenyewe aliwaua mamia ya watu kwa kuwatuhumu au kuwadhania kula njama za kumpindua. Wengine aliwaweka kizuizini kwa muda mrefu sana, wengine akawahamisha nchini mwao na kuwapeleka kwingine, na wengine akiwatoa majumbani mwao kupelekwa kusikojulikana pasina haki isipokuwa alichokiona kuwa ni kosa kwake, nacho ni wao kusema, "Mola wetu ni Allah." Serikali ya Muawiyah haikwenda rnwendo wa Kiislamu, wala haikufanana kabisa kwajambo lolote la karibu au la mbali na maongozi na sheria za Kiislamu.

Mwenyezi Mungu akiijalia serikali ya Kiislamu kusimama sawasawa — jambo ambalo kwake si kubwa - watu wote wataishi kwa amani, na kila mtu ataisalimisha mali yake, watu wake na chochote kile anachokimiliki. Kwa maana halitakuwa jambo rahisi kwa viongozi kuwaendea watu (raia) kichnichini wala kuyakiuka maamrisho mema ya Kiislamu, na hayo ndiyo maana ya 'ulinzi wa amana.'

Hapo mbeleni, tumegusia kwamba, amana au uaminifu si upokezi wa hadithi au uandishi au utoaji wa fatwa tu bali ni utendaji, utengezaji na utekelezi hasa wa sheria, ijapokuwa uaminifu katika kunakili hadithi na utoaji fatwa una shani kubwa. Mtume Mtukufu SAW na Sayyidna Ali bin Abi Talib AS na Maimamu wengineo waaminifu walikuwa wakisema na kuonyesha kwa vitendo wanayoyasema. Vilevile Mitume wamechukua ahadi kwa mafaqihi wawe wakisema na kutenda, wasimamishe sala, waitoe zaka, waamrishe mema, wayakanye maovu na wawaongoze watu kwa mwendo wa uadilifu. Uislamu unaizingatia sheria kuwa ala na njia za kuhakikisha kupatikana kwa uadilifu katika jamii, na njia ya kumfunza mtu huluka njema, imani na matendo.

Jambo kubwa walilolitilia maanani sana Mitume ni kuunda na kuhakikisha sheria zinafuatwa na kuzitumia kwa watu juu ya jambo waliloteta, pia kwazo waliongoza na kuyaweka wazi yaliyo na ufanisi ndani yake humu duniani na huko akhera.

Kuna hadithi iliyopokewa kwa Imam Ridha AS akisema: "Lau Mwenyezi Mungu hangewawekea watu mwongozi na mlinzi wa sheria, mila (ya Kiislamu) ingeharibika . . ."(Ilalu Sharaai, jz. 1, uk. 172).

Kwa ujumla, hadithi hii na nyingine tuliyoitaja mbele zina fahamisha kwamba kuna dhamira ya kuwepo kiongozi, aliye kaimu, mlinzi na mwaminifu kwa ajili ya watu. Hii ina maana kwamba ni lazima mafaqihi waadilifu na wawakilishi wa Mitume wawe viongozi wa watu ili Uislamu usiharibike na sheria zake zikakomea.

Tukiangalia historia ya dini ya Uislamu tutaona kwamba maneno hayo ya Imam Ridha AS yamethibitika, kwani Uislamu umeharibika na sheria zake zimekoma kwa sababu kutokuwepo tawala za mafaqihi waadilifu katika nchi za Kiislamu.

Je sasa Uislamu haujaharibika? Kweli Uislamu bado haujafutika? Sheria zake si zimeachwa? Tena katika nchi za Kiislamu? Je maamrisho ya Kiislamu yanachungwa na kuzingatiwa? Je mambo hayajachafuka? Niambieni, je Uislamu unaotakiwa ndio huu wino ulioandikwa makaratasini? Je mnadhani kwamba Uislamu ni kuibusu Qur'ani, kuandika vitabu vya hadithi k.v. al-Kafi kisha kuvisoma na kuviweka rafuni bila ya kutekeleza hukumu zake? Je ni kweli Uislamu utahifa dhika itakikanavyo iwapo tutaipokea Qur'ani Tukufu kisha tusome sura ya Yasin kila usiku wa Ijumaa pasina kuyafuat yaliyomo?

Haya basi, mambo tayari yamefikia kiwango hiki cha kutisha, kwa sababu toka mwanzo hatukufikiria namna ya kuistawisha jamii na kuinufaisha kupitia kwa maongozi ya Kiislamu. Hivi sasa, Waislamu tayari wametawalishwa sheria shenzi, mbovu zenye lengo la kuukandamiza Uislamu, kwani Mwenyezi Mungu hakuziteremshia sheria hizo uwezo.

Baadhi ya wanavyuoni ambao walianza kuondokewa na Uislamu ubongoni mwao, wakaanza kuusahau kiasi cha kuwafanya watoe maelezo ya kifungu "Mafaqihi ni waaminifu wa Mitume" kwamba eti maana yake ni 'uaminifu wa kuyalinda masiala na kuwaambia watu tu." Je, huu ndio uaminifu? Je, mwaminifu aliyeaminiwa wajibu wake si kuzilinda sheria za Kiislamu ziwe nzima na kamili na aziepushe na kuachwa kutumiwa? Je, si wajibu juu ya mjumbe au afisa wa mji kutowaacha maadui wachochezi waendeshe harakati zao bila kuguswa na yeyote? Je, si juu yake kuzuia machafuko na apigane na upuuzi, uzushi na upotoshi huku akiwatia adabu wanaozichezea mali za wenzao na roho zao? Naam, huu ndio 'uaminifu' wa amana ambao ulitekelezwa na Mitume na wao wakawaachia mafaqihi.

JUKUMU LA KUTOA HUKUMU LIMEKABIDHIWA NANI?

Hadithi imepokewa kutoka kwa Imam Sadiq AS akisema: "Amirul Mu'minin (Sayyidna Ali AS) alimwambia Shuraih,[34] 'Ewe Shuraih, umekaa mahali ambapo hapakai (hakupakaa) isipokuwa Mtume au wasii wa Mtume au mtu mwovu.' (Wasailush Shia, mlango wa 3, Nam. 1;Man Laa yahdhuruhul Faqiih, jz. 3, uk. 4)

Shuraih huyu, alikitumia cheo cha uhakimu na alikuwa akimsifu sana Bwana Muawiyah bin Abu Sufyaan akimtolea madaha na sifa ambazo kamwe hanazo wala hazistahili. Msimamo wake hasa huyu Bwana Shuraih, ulikuwa ni kuyabomoa mambo yote yaliyoimarishwa na Serikali ya Sayyidna Ali AS. Ali AS aliujua msimamo wake, lakini hakuweza kumuuzulu, yaani kumsimamisha kazi kwa sababu alikuwa ameteuliwa na waliomtangulia. Imam hakumwondoa kazini bali aliendelea kumchunguza na kutumaini kuwa atakuwa mwema siku za mbeleni huku akimkemea (kidogo kidogo) juu ya kujiingiza katika mambo yaliyo kinyume na mafunzo ya Kiislamu.

KUTOA HUKUMU N1 MIONGONI MWA WAJIBU WA FAQIHI MWADILIFU

Hata ingawa pana maelezo tofauti baina ya marehemu Naraqi[35] na marehemu Naini[36] juu ya wadhifa (wajibu) wa faqihi, hapana tofauti baina yao kuhusu cheo cha kuhukumu (utawala) kuwa ni mahasusi kwa faqihi mwadilifu, kufuatia uchunguzi wa hadithi iliyotangulia iliyo na 'Mtume, wasii* na mwovu.' Inajulikana wazi mafaqihi si katika Mitume, na hapana shaka wao hawamo katika jumla ya waovu. Kwa hivyo wanasadikika jina la 'mawasii'. Kwa kuwa aghlabu mara nyingi neno wasii hutumika kwa Imam wa kwanza Amirul Mu'minin Ali AS, baadhi yetu wanaiona hadithi hii haifungamani na mazungumzo yetu haya.

Lakini, hapo mbeleni, tumewahi kukumbusha kwamba, haifai mtu kudhania kwamba cheo cha utawala (uongozi) humnyanyua mtu daraja na kuwa Imam au Mtume, kwa sababu kuwaongoza watu na kuwaamua baina yao, hakukuwa ila ni kusimamisha jambo la wajibu tu, kuhakikisha haki inatumika, kuongoza jamii na kueneza uadilifu baina ya watu.

Mitume na Maimamu walikuwa na utukufu ambao hapana aujuao isipokuwa Mwenyezi Mungu tu peke yake, na kule kuteuliwa kwao (hao Maimamu) kuwa makhalifa, hakuwaongezi daraja wala hakuwapunguzi, kwani kuteuliwa huku hakuna shani kwa mtu bali shani yake ya asili ambayo ndiyo humwezesha kuteuliwa.

Kwa hivyo, kwa vyovyote tunafahamu kutokana na hadithi hii kwamba, mafaqihi ndio mawasii wa Mitume baada ya Maimamu na wana wajibu uleule mmoja.

Kuna hadithi nyingine itakayotilia nguvu mazungumzo yetu. Pengine sanadi (mategemeo) yake na dalili zake zina nguvu kuliko ile hadithi ya kwanza ingawa Kulaini aliipokea hadithi hii kwa njia iliyo dhaifu, ila Saduq aliyeipokea kwa njia ya Sulaiman bin Khalid ndiyo sahihi ya kuzingatiwa.

Imepokewa kwa Abi Abdillah AS[37] akisema: "Ogopeni kazi ya kuhukumu, kwani kuhukumu ni kazi ya Imam ambaye ana ujuzi wa kuhukumu kiadilifu kati ya Waislamu, kama vile Nabii au wasii wa Mtume." (Wasaail, mlango wa 3, Nam. 3)

Eleweni kwamba sharti la kwanza kwa mtu anayetaka kuhukumu (au kutawala) lazima awe Imam. Neno ' Imam ' lilivyotumika katika hadithi hii lina maana ya kiongozi au rais wala halina maana ya kitaalamu yenye kukusudiwa Imam (katika Maimamu Thenashara) aliyechaguliwa na Mtume Mtukufu SAW. Kwa maana hii tunaweza kusema kuwa Mtume pia ni Imam, yaana kiongozi. Sharti la pili ni lazima awe mjuzi (alim) wa sheria. Ikiwa hakimu ni Imam (kiongozi) lakini hana ujuzi katika sheria na kanuni za Kiislamu, hana haki ya kuhukumu. Sharti la tatu ni lazima awe mwadilifu. Hivyo basi mtu anayetaka kuhukumu (au kutawala) lazima awe na masharti matatu, yaani lazima awe kiongozi, mjuzi na mwadilifu. Na masharti haya hanayo yeyote isipokuwa nabii (mtume) au wasii wa nabii.

Kama nilivyoeleza mbele, katika elimu ya fiqihi imetajwa kwamba mambo ya kisheria lazima yaendeshwe na faqihi mwadilifu. Sasa tuangalie ikiwa faqihi anayo masharti yenye kumwezesha kuhukumu. Kwanza kabisa faqihi anayekusudiwa ni yule aliye mwadilifu wala si kila faqihi. Kwa maana kamili ya neno 'faqihi', faqihi lazima ajue sheria na kanuni za kuhukumu pamoja na kuwa anajua itikadi zote, hukumu, nidhamu na mienendo yote ya Kiislamu. Faqihi anapokuwa mwadilifu huwa na masharti mawili. Sharti lingine analokuwa nalo ni Imam, yaani kiongozi. Tulisema pia kwamba faqihi mwadilifu huwa na cheo cha uongozi katika kuhukumu, cheo ambacho kama alivyosema Imam AS huwa nacho mtume au wasii wa mtume. Ilivyokuwa mafaqihi si manabii (mitume) basi wao ni mawasii wa manabii, yaani washika makamo wao. Kwa hivyo, itafahamika kwamba faqihi ni wasii (khalifa) wa Mtume Mtukufu SAW, Imam wa Waislamu na kiongozi wa dola la Kiislamu katika zama za ughaibu. Faqihi tu ndiye mwenye haki ya kuhukumu na kutawala.

N1 NANI ANAYEREJELEWA KATIKA MAMBO YA KIMAISHA?

Katika kitabu kiitwacho Ikmaalud Din wa Itmaamun Ni'amah kuna hadithi kutoka kwa Is'haq bi Yaqub akisema:

"Nilimwambia Muhammad bin Uthman al-Umari [38] anifikishie barua yangu iliyokuwa na maswali yaliyonitatiza kwa Imam Mahdi AS. Katika jibu lililokuwa na sahihi ya Maulana Imam Mahdi AS imeandikwa 'Ama matukio yanayotokea, yarejeleeni kwa wapokezi wa hadithi zetu, kwani wao ni huja wangu kwenu, na mimi ni huja[39] wa Mwenyezi Mungu.'"

Kwa vyovyote, kilichokusudiwa katika swali la "matukio yanayotokea", siyo masiala na hukumu za kifiqihi. Muulizaji alikuwa akiwajua wa kuwarejelea katika masiala kama hayo. Watu wote walikuwa wakiwarejelea wanavyuoni katika masiala mbalimbali ya kuwatatiza, hata katika zama za Maimamu wenyewe, watu waliokuwa wakiishi mbali na Maimamu, walikuwa wakitatuliwa mushkili wao na wanavyuoni.

Muulizaji lengo la swali lake ni juu ya matatizo ya kijamii yanayotokea sasa na juu ya maendeleo ya watu. Alipoona mambo hayo hurejelewa Imam, naye (Imam) hayuko kaghibu, alitaka ufafanuzi juu ya wa kumrejelea katika mambo kama hayo hasa mambo mapya mapya yanayozuka wakati kwa wakati, kwani hakuwa anajua la kufanya. Swali lake lilikuwa la jumla halikuhusu upande maalum na kuuacha mwingine, yaani halikuwa mahasusi. Nalo jibu likaja kwa njia ya ujumla nalo ni "Warejeleeni wapokezi wa hadithi zetu, kwani wao ni huja wangu kwenu na mimi ni huja wa Mwenyezi Mungu."

Maana ya 'huja' ni nini? Mmefahamu nini juu ya neno 'Huja wa Mwenyezi Mungu'? Je, maana ya neno huja ni Imam huyo akiipokea hadithi kutoka kwa Mtume akatufahamisha tutaipokea kama tunavyopokea kutoka kwa Zarara? Je, yeye ni huja wa Mwenyezi Mungu katika masuala ya kifiqihi tu? Je, Mtume SAW aliponena: "Nimewawekea Ali awe huja juu yenu" ana maana ya kuwa, "Nitaondoka na kuwaachia Imam Ali awabainishie na kuyaweka wazi masiala ya kifiqihi tu" au vipi?

Huja wa Mwenyezi Mungu maana yake ni, Imam wa kurejelewa na watu juu ya masiala yote, na ameachiwa uwezo wote wa matumizi na nidhamu zilizo na manufaaa kwa watu na zenye kuwaletea faida. Vilevile mafaqihi nao ni marejeo na viongozi wa umma.

Huja wa Mwenyezi Mungu ni ambaye kateuliwa na Mwenyezi Mungu ili kuyasimamia mambo ya Waislamu ili matendo yake na maneno yake yawe huja juu wa Waislamu ili walazimike kuyatekeleza pasina kuyaendea kinyume. Waisimamishe mipaka ya Mwenyezi Mungu, wachangishe (wakusanye) kodi au malipo ya khums, zaka, ushuru, ghanima pamoja na kuitumia katika njia zake. Hayo yana maana, lau baada ya kupatikana hoja hii mtakengeuka tena na kuwa wadhalimu waonevu, basi huko siku ya Kiyama mtaulizwa na hatimaye kuadhibiwa kwayo.

Mwenyezi Mungu aliyetukuka ataleta hoja ya Amirul Mu'minin kwa wale waliojitenga naye na kuhalifu amri zake kamaatakavyotoa hoja kumtia daawani Muawiyah, mahakimu wa Bani Umayyah na Bani Abbasi na wasaidizi wao kwa kuzipokonya haki za watu na kujipachika vyeo wasivyostahili.

Mwenyezi Mungu atawahoji na kuwaadhibu mahakimu waonevu na kila serikali iliyoyaacha mafunzo ya Kiislamu juu ya ufujaji wa mali za Waislamu, na atawapa adhabu juu ya uharibifu wa fedha katika kuendeshea sherehe za kutawazwa na katika sherehe za kusherehekea karne ya 25 ya utawala wa kifalme katika Iran (na kwingineko) .[40]

 Je, mdaiwa atasema nini wakati wa kuhesabiwa? Pengine atasema: "Ili kuuimarisha utawala, na kufuatana na mambo ya kiserikali ya wakati huo, ilitubidi kufanya hivyo." Ala! "Pia usulutani wetu ulituvutia kujenga majumba (ikulu) makubwa

makubwa. Pia huo huo ufalme wetu ndio uliotufanya kutumia mamilioni ya pesa yasiyo na hesabu katika sherehe za kutawazwa na mambo mengineyo ili kutaka umashuhuri na kueneza umaarufu wetu kote ulimwengini." Ataambiwa:

"Mbona hukumwiga Mtume Mtukufu SAW na Imam Ali AS? Je, uliwafanyia raia mambo makubwa zaidi ya Mtume Mtukufu SAW au Imam Ali AS? Je, wao hawakuwa watawala? Je, ulitaka kuuinua Uislamu zaidi ya alivyouinua Mtume au Imam Ali? Dola(utawala)wanani mkubwa,wako ama yao?Je, dola lako si lilikuwa tu mkoa au jimbo katika majimbo ya serikali ya Imam Ali AS ambayo yalienea Misri, Iraq, Hijaz (Saudi Arabia) na Yemen? Mbali na hayo, je huna habari wala hujui kwamba mabaraza yake aliyoendesha aliyaendeshea misikitini? Uamuzi akiutolea nje mbele ya hadhara ya watu? Pamoja na hayo, alikuwa akiyaandaa majeshi na kuyakabidhi bendera ili yaanze safari za vitani akiwa huko huko msikitini? Je, hukuwaona wanajeshi hao wanapokwenda vitani huenda na nia moja safi yenye makini huku sala zao zilikuwa haziwapiti kabisa ambapo nyinyi mliokuwa majumbani makubwa mkistarehe hamkuwa mkisali? Je hukujua namna walivyokuwa wakiongozana na kushirikiana bega kwa bega, na Mwenyezi Mungu akawapa ushindi?

Hivi leo, mafaqihi ndio huja kwa watu wote namna alivyokuwa Mtume Muhammad SAW ni huja juu yao, na lolote lililokuwa mikononi mwake alilikabidhi Maimamu na mafaqihi watakaokuja baada yao ambao ni marejeo ya watu kwa mambo yote na matatizo ya kila aina. Wao wametegemezewa uongozi wa serikali, kuwaendesha watu, kukusanya kodi na kuitumia au kuwapa wanaostahiki, na yeyote anayekwenda kinyume nao bila shaka Mwenyezi Mungu atamdai na kumchukulia hatua kali juu ya uhalifu wake huo.

Hadithi hizi tulizozinakili, ni wazi kabisa na dalili hata ingawa hazikufikia rai yetu ya mwisho juu ya mazungumzo yetu kwa kuwa tumezileta kwa uchache.

AYA KUTOKA QUR'ANI TUKUFU

Kuna hadithi zingine nyingi mno zinazotilia mkazo mazungumzo yetu haya. Hadithi hizo zinatiliwa nguvu na aya hizi za Qur'ani Takatifu tutakazoziweka uwanjani kabla ya kuziingilia hadithi hizo zenyewe. Mwenyezi Mungu asema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَطِيعُواْ اللّهَ وَأَطِيعُواْ الرَّسُولَ وَأُوْلِي الأَمْرِ مِنكُمْ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللّهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ ذَلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلاً  (59) إِنَّ اللّهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤدُّواْ الأَمَانَاتِ إِلَى أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُواْ بِالْعَدْلِ إِنَّ اللّهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ إِنَّ اللّهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا  (58)

"Hakika Mwenyezi Mungu anawaamuruni kuzirudisha amana kwa wenyewe, na kwamba mnapotoa hukumu baina ya watu hukumuni kwa uadilifu, kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapeni mawaidha mazuri mno na kwa hakika Mwenyezi Mungu husikia nahuona(yote). Enyimlioamini, mtiiniMwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka miongoni mwenu, na mnapoteta juu ya jambo lolote lile, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na kwa Mtume ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu (kweli) na siku ya Mwisho. Kufanya hivyo ni bora kwenu na ni maelezo bora. " (4:58, 59)

Baadhi ya watu huchukulia maana ya amana, kwa mali anayowekeshwa mtu, na sheria za Mwenyezi Mungu alizompa mtu atende kwa mujibu wa maamrisho Yake. Ya kwanza ni amana za watu na hii ni amana ya Mwenyezi Mungu.

Kundi jingine hufasiri maana ya amana kuwa ni uimamu (uongozi) wakiutoa ushahidi wa Maimamu waliponena, "Sisi Maimamu ndio amana", na kwamba Mwenyezi Mungu aliamrisha amana — yaani uimamu, uongozi na utawala — arudishiwe wenyewe. Yaani Imam Ali AS, naye awape walioainishwa wapewe baada yake.

Kifungu cha jumla ya aya ya kwanza, "Mnapotoa hukumu baina ya watu amueni kwa uadilifu" kinawahusu wale walioshika mambo ya uongozi mikononi mwao na wala hakiwahusu mahakimu peke yao hata ingawa uamuzi hutokana na wao, kwa sababu, mahakimu ni sehemu tu ya serikali iliyo na jukumu la mambo yote na wala wao sio serikali yote.

Ni maarufu hata kwa serikali za kisasa kwamba, ili ziwe na maongozi, yaani uwezo imara na zimudu kuiunda serikali kamili, kwanza ni lazima zihakikishe zina:

1- Halmashauri ya Wanasheria (Judicature),

2- Halmashauri ya Watunga Sheria (Legislature), na

3- Halmashauri ya Utendaji, yaani halmashauri ya utekelezaji amri au sheria (Executive).

Neno Lake Mungu aliposema, "Namnapotoa hukumu..." ni maongezi ya jumla kwa serikali yenye mambo hayo matatu.

rudi nyuma Yaliyomo endelea