rudi nyuma Yaliyomo endelea

Upambanuzi huo umetubainishia hayo yote. Baada ya hayo, ni juu ya mafaqihi wote kwa pamoja au kila mmoja wao ajishughulishe kuziendeleza sheria za Mwenyezi Mungu, ailinde mipaka ya sheria, astawishe nidhamu na aunde serikali yenye sheria za Mungu. Anayestahili kuyaongoza mambo hayo lau atakuwa ni mmoja tu, basi yatakuwa ni wajibu juu yake, na iwapo wamepatikana wengi, basi utakuwa ni wajibu wa kutoshelezeana (wajibu kifai*), yaani mmoja akitimiza wajibu huo, kwa mwingine huwa si lazima.

Ama uwezekano wa kuunda serikali ukikosekana, ule utawala (uongozi) haubatiliki, kwa kuwa mafaqihi tayari Mwenyezi Mungu kawatawalisha, kwa hivyo ni wajibu wa faqihi kuyatumia madaraka yake aliyopewa kadiri ya uwezo wake. Ikiwezekana, akusanye zaka, khums, kharaj na jizya ili awape wanaostahiki kupewa. Kushindwa kwa muda kuunda serikali yenye nguvu na yenye maongozi ya Kiislamu kusitufanye kujificha bali tukabiliane na haja za Waislamu na tutengeneze sheria kwa kadiri ya uwezo wetu.

UTAWALA WA ASILI

Kuthibitisha kwamba utawala na serikali ni wa Imam AS haina maana kwamba Imam hana cheo cha kiroho. Imam AS ana vyeo vya kidini na kiroho ambavyo ni mbali na wadhifa wa utawala. Cheo cha kiroho cha Imam AS ni cheo cha ukhalifa wa ulimwengu mzima au utawala wa asili unaotokana na Mwenyezi Mungu, cheo ambacho kimetajwa na Maimamu Maasumu AS. Ni cheo cha ukhalifa na utawala wa ulimwengu mzima, na kufuatana na cheo hiki, viumbe vyote humnyenyekea mwenye mamlaka. Kufuatana na riwaya kadhaa, kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mtume Mtukufu SAW na Maimamu Maasumu AS walikuwa wamekwisha umbwa katika umbo la nuru na walikuwa na utukufu zaidi kushinda watu wote. Vilevile kuna hadithi moja katika hadithi za miraji}* inayomnukulu malaika Jibrail akisifia vyeo vyao katika Arshi* ya Allah. Mtume Mtukufu SAW amesema pia kwamba, "Sisi tuna vyeo mbele ya Mwenyezi Mungu ambavyo havifikiwi na malaika wala Mitume." Hii ni katika imani yetu kwamba Mtume Mtukufu SAW na Maimamu Maasumu AS walikuwa na vyeo hivyo hata kabla ya kuzuka suala la utawala wa sheria na serikali duniani. Bibi Fatima AS bintiye Mtume Mtukufu SAW alikuwa na cheo kama hicho ingawa yeye hakuwa mtawala (hakimu) wala kadhi wala khalifa. Vyeo hivi vya kiroho ni tofauti na wadhifa na kazi za kiserikali. Hivyo, tunaposema kwamba Bibi Fatima AS hakuwa kadhi wala mtawala, haina maana kwamba yeye alikuwa sawa na mimi na wewe, au kwamba yeye hakuwa na daraja tukufu zaidi kuliko sisi. Vivyo hivyo, Qur'ani inaposema kwamba "Nabii ana haki zaidi kwa waaminio kuliko nafsi zao" (33:6) huwa imempa Mtume Mtukufu SAW cheo kikubwa zaidi kuliko cheo cha utawala wa kiserikali na kisheria. Sasa hatutolizungumzia suala hili kwani linahusu fani nyingine.

SERIKALI N1 NJIA YA KUTIMIZA LENGO AALI

Kuyaendesha mambo ya dola hakumfanyi anayeyaendesha kuongezeka shani na utukufu, kwa sababu serikali ni njia ya kutimiza hukumu na kustawisha mfumo adilifu wa Kiislamu na pia kuiondoa serikali katika tuhuma ya kuzingatiwa kiongozi wake kuwa na lengo la kutaka cheo.

Bin Abbas siku moja alikwenda kwa Sayyidna Ali bin Abi Talib AS akamkuta ameshika kiatu mkononi akikishona. Sayyidna Ali AS akamuuliza (mgeni wake) Bin Abbas:

"Wafikiri kiatu hiki kina bei (thamani) gani?" Bin Abbas akajibu, "Kiatu kama hiki kwa sasa hakina thamani yoyote." Imam Ali AS akasema: "Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, kiatu hiki ni bora kwangu kuliko mambo yenu haya ya kutawala isipokuwa tu ikiwa nitaisimamisha haki na kuiondoa batili." (Nahul Balagha)

Imam huyo si ati ni mwoga wa kuongoza au mwenye tamaa ya uongozi, kwani ndiye yule yule aliyesema:

"Naapa kwa jina la aliyepasua punje na akawaumba watu, lau siyo kupatikana wenye kunisaidia, na (lau pia si) ahadi aliyoichukua Mwenyezi Mungu kwa wanavyuoni kuwa wasimpe nafasi (wasimwachilie) dhalimu mwenye shibe aendelee kudhulumu, na lau pia si njaa ya mdhulumiwa, ningeiachilia huru hatamu ya utawala wa ukhalifa, na mgeiona dunia yenu kwangu ni duni hata zaidi ya chafya ya mbuzi." (Nahjul Balagha)

Utawala si lengo maarubu*, bali ni njia tu ya kufikia lengo. Ama lau mtu aufanye utawala (au uongozi) kuwa lengo lake, bila shaka hataokoka makosa. Na wote wawazao hivyo watakuwa katika jumla ya wenye makosa.

Kwa hivyo, ni juu ya mafaqihi waadilifu wajibidiishe hadi wahakikishe maongozi ya Kiislamu yanafuatwa ili sheria za Mungu zitekelezwe ingawa kutimia jambo hili kunataka zahama. Kwani kuleta utawala wa faqihi ni wadhifa ulio wajibu kutekeleza.

Maneno haya aliyoyasema Amirul Mu'minin (Kiongozi wa Walioamini) Ali bin Abi Talib AS katika hotuba aliyoitoa baada ya watu kumbai (kumpigia kura ya imani) katika msikiti wa Mtume huko Madina, ni dalili ya kutosha kuwa, serikali ni njia tu wala silo lengo. Alisema: "Ewe Mwenyezi Mungu, bila shaka unajua yaliyotokea kati yetu hayakuwa ya lengo la kupigania usultani, wala kujinyakulia chochote kati ya mambo ya upuzi ya humu duniam, bali yalikuwa na lengo la kurudisha mafunzo ya dini Yako, na tuuoneshe ushwari na utengevu wa mambo nchini Mwako ili mja Wako mwonewa asalimike, na mipaka Yako iliyokiukwa isimamishwe inavyo takikana."

SIFA ZA MTAWALA

Katika hotuba hii ya Imam, alitufahamisha sifa za mtawala anayestahiki au anayetakiwa kutimiza lengo lenyewe aliponena: "Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni wa kwanza wa aliyerudi Kwako akasikia mwito wa Mtume Wako akauitikia. Hakunitangulia kusali ila Mtume Wako Muhammad SAW. Kumbuka kwamba, hafai kabisa kuyaongoza mambo ya umma, hasa kuwaongoza Waislamu, sheria na ulinzi kwa watu, mtu ambaye ni mlafi asije akazivamia mali zao. Wala jahili (mjinga) asije akawapoteza kwa ujinga wake. Wala mtu katili asije akawakatakata (kuwanyonga) kwa ukatili wake. Wala mtu mwoga asije akawaingiza watu wa nje kutawala akawaacha watu wake yeye mwenyewe. Wala mlaji rushwa na hongo wakati wa kuhukumu asije akazipoteza haki za wenyewe. Kadhalika hafai kuyaongoza mambo ya umma mtu ambaye hafuati sunna za Mtume Mtukufu SAW asije akauangamiza umma."

Yote hayo, kama mnavyoona, yako chini ya ujuzi na'uadilifu ambayo ni masharti ya kwanza kabisa na muhimu ambapo pia Imam ameyagusia kwa neno lake, "Wala mjinga asije akawapoteza watu kwa ujinga wake." Sifa mbili hizi, yaani uadilifu na ujuzi, ni lazima kuwa nazo walii (mtawala). Maana hasa ya uadilifu ni kuleta usawa na haki katika uhusiano wa serikali, wananchi, maamuzi n.k. kama Sayyidna Ali AS alivyokuwa akifanya kufuatana na miongozo aliyowapa Malik Ashtar, maliwali na mahakimu wake. Mafaqihi watakapotawala lazima pia wayafuate maongozi yao.

UTAWALA WA FAQIHI WATHIBITISHWA KATIKA HADITHI

Makhalifa wa Mtume ni Mafaqihi Waadilifu

Sayyidna Ali bin Abi Talib AS asema:

قال أمير المؤمنين علي (ع): قال رسول الله (ص) : اللهم ارحم خلفائي، - بعد ثلاث مرات - قيل: يا رسول الله، و من خلفائک؟ قال : الذين يأتون من بعدي، يرون حديثي، وسنتي، فيعلمونها الناس من بعدي.

"Mtume Mtukufu SAW alisema mara tatu, 'Ewe Mwenyezi Mungu, warehemu makhalifawangu.' Akaulizwa, 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni nani hao makhalifa wako?' Akajibu, 'Wale ambao watakuja baada yangu, watazipokea hadithi zangu na sunna zangu, kisha wawafunze watu baada yangu.' " (Wasailush-Shia)

Shaykh Saduq,[24] Mungu amrehemu, ametaja hadithi kama hii katika vitabu vyake viitwavyo, 'Uyuun Akhbaarur Ridha, Jaami'ul Akhbaar na al-Majaalis. Amepokea hadithi hii kwa njia na watu mbalimbali; hivyo, jumla ya mwisho ilitofautiana hivi: ". . . kisha wawafunze," ". . . kisha wafunze watu" na ". . . kisha wawafunze watu baada yangu."

Mazungumzo yetu juu ya hadithi hii yataduru juu ya mambo mawili:

1- Hebu tuchukulie hadithi hii ni moja kisha ikaongezewa jumla nyingine 'Kisha wawafunze . . . ." au pengine jumla (kifungu) hiyo ilikuwemo kisha ikaondolewa — na dhana hii inaweza ikafungamana na ukweli — kwa sababu haiyumkiniki kwetu kuwatuhumu wapokezi (wa hadithi hii) kwa sababu walikuwa watatu na kamwe hawana ufungamano wowote baina yao. Mmoja wao alikuwa akiishi Balkh, mwingine Nishapur na wa tatu mji mwingine. Ni vigumu sana kwao kutokana na umbali huu uliopo baina yao mbali na kutojuana kuwafikiana kukiongeza kifungu hicho. Hivyo basi, tunaweza kukata shauri kuwa, kifungu "Kisha wawafunze .. .." kulingana na hadithi iliyonakiliwa kwa njia ya Shaykh Saduq iliondolewa na wafutaji, au pengine Saduq alikisahau (katika mapokezi yake ambayo hayana kifungu hicho).

2- Hebu tuchukulie kuwa kuna hadithi mbili. Mojawapo haina kifungu "Kisha wawafunze . . . ." na nyingine inacho. Na tuchukulie jumla hiyo ipo. Basi hadithi haikuwaweka ndani (haikuwakusanya) wale wanaojishughulisha tu na kunakili hadithi bila kuichunguza wala kuitizama kwa uangalifu, wala kufanya jitihadi wala kufanya uchambuzi na kuweza kufikia hukumu ya kufaa. Kwetu sisi, haiyumkiniki kuwataja watu kama hao kuwa wenye kustahili ukhalifa madamu kazi yao ni kunakili hadithi tu na kuziandika. Wao husikiliza hadithi kisha wakazinakili na kuwafikishia watu, kwani kupokea hadithi na kuzinakili tu hakumfanyi mtu astahili kuwa faqihi, kwani "Si kila mwenye kusoma fiqihi aweza kuwa faqihi." Hata hivyo, hatuna maana ya kutokuwepo faqihi miongoni mwa wapokezi wa hadithi. Wako mafaqihi wengi sana waliokuwa wapokezi wa hadithi kama vile Kulayni[25], Shaykh Saduq na babake na wengineo (Mungu awarehemu).

Tunapoeleza tofauti iliyopo baina ya Shaykh Saduq na Shaykh Mufid, hatumaanishi kuwa, Shaykh Saduq hakuwa faqihi ukimlinganisha na huyo Mufid, la hasha. Itakuwaje kuwa hivyo hali Shaykh Saduq alibainisha msingi (usul) na matendo (fumu) yote ya kimadhehebu katika kikao kimoja?

Tofauti tunayokusudia ni kwamba, ShaykhMufid[26] alikuwa mujtahidi mwenye kutoa fikra zake katika hadithi na Shaykh Saduq alikuwa faqihi asiyetoa fikra zake ila wakati mwingene.

Hadithi yenyewe ilikusudiwa wanaojitahidi kusambaza elimu za Kiislamu na hukumu zake, kisha wanawafunza watu kama alivyokuwa Mtume na Maimamu wakiwafunza watu na kuwapa shahada maelfu ya wanavyuoni waliohitimu.

Na tunaposema "Islamu ni dini ya ulimwengu wote" hili li wazi kabisa, kwa hivyo, ni lazima juu ya maulamaa wa Kiislamu waeneze mafunzo yote ya Kiislamu kote ulimwenguni.

Hebu tuchukulie jumla "Wawafunze watu" si katika madhumuni ya hadithi, basi na tutizame. Mtume Mtukufu SAW alikusudia nini kwa kusema, "Ewe Mwenyezi Mungu, warehemu makhalifa wangu ambao watakuja baada yangu, watazipokea hadithi zangu na sunna zangu..."

Lengo la hadithi hii haliwakusudii wasiojua fiqihi, kwa sababu sunna za Mtume ni sunna za Mwenyezi Mungu, na anayetaka kuyasambaza mafunzo hayo (sunna hizo) ni sharti kwanza azijue hukumu zote za Mwenyezi Mungu aweze kupambanua hadithi sahihi na zisizo sahihi, zinazowahusu watu maalum na zinazowahusu watu wote na zinazokubaliana kisheria na kiakili. Vilevile awe anaweza kuzipambanua hadithi zilizopokewa kutoka wakati wa hofu ambao ulibidi kutodhihirisha hukumu zingine kwa mnasaba wa hali ilivyo kuwa. Mpokezi hadithi yeyote asiyefikia daraja ya ijtihad* na akawa mujitahidi bali anatosheka tu na kunakili hadithi, hawezi kuufikia ukweli wa hadithi na sunna za Mtume Mtukufu SAW na kulingana na mafunzo ya Mtume, mtu kama huyo na mafunzo yake hayachukuliwi.

Kusudio la Imam Ali AS la kutaja chanzo cha hadithi yenyewe kwa kusema, "Mtume Mtukufu SAW alisema ...." au "Imepokewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema . . . ." halikuwa ni kumtaja msemaji, bali lilikuwa ni kutaka hadithi za Mtume zisambazwe na sheria za Kiislamu zitumike.

Ama hadithi isemayo:

قال رسول الله «ص»: من حفظ من أمتي أربعين حديثاً حَشرهُ الله فقيهاً.

"Mwenye kuhifadhi hadithi arobaini kati ya wafuasi wangu, Mwenyezi Mungu atamfufua siku ya kiyama akiwa faqihi" na zinginezo nyingi zinazomsifu au kumwonesha bora anayejitahidi kuzitawanya na kuzieneza hadithi, hazimkusudii mpokezi hadithi (muhaddith) asiyejua anayoyanakili. Na pengine huenda ananakili hadithi na kumfikishia anayejua zaidi elimu ya sheria za Kiislamu (yaani faqihi). Lengo hasa la hadithi ni anayewafikishia watu mafunzo ya Kiislamu kama yalivyo. Na hili halitendeki ila kwa mujitahidi na faqihi. Hao wajitahidi na mafaqihi wa namna hii, ndio makhalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ambao huyaeneza mafunzo ya Islamu na hadithi zote kihakika na kuzipitishia sheria zake, na ambao huwafikishia watu mambo kwa namna yalivyo. Kwa ajili hiyo, lazima wanastahiki dua ya Mtume Mtukufu SAW ya kuwaombea rehema kwa Mwenyezi Mungu.

Hivyo bila shaka imeeleweka, "Ewe Mwenyezi Mungu, warehemu makhalifa wangu" haina uhusiano wowote na wapokezi wa hadithi na wanaozinakili ambao hawajui fiqihi, kwani kuandika tu hadithi pekee hakumstahilishi mtu kuwa khalifa wa Mtume, bali waliokusudiwa ni mafaqihi ambao huyasambaza mafunzo yote ya Kiislamu kwa ustadi na uadilifu na ambayo kwayo kuzitekeleza sheria zake.

Faqihi tu ndiye mwenye kuweza kuwapambanulia watu hukumu na sheria kiadilifu. Wapo baadhi ya wapokezi wa hadithi na mashekhe wa kujigamba waliozua uwongo. Kwa mfano, Samura bin Jandab[27] alizua hadithi zinazompinga Sayyidna Ali AS. Ikiwa mpokezi wa hadithi si faqihi, atawezaje kufahamu elimu ya fiqihi na kuhukumu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu? Makadhi waongo na wasio waadilifu hawakuacha kubuni maelfu ya hadithi kuwasifu wafalme waonevu ili mradi waupambe ufalme wao na kuzitukuza kazi zao. Mambo kama hayo hadi leo kama mnavyojua, yangali yakiendelea. Sielewi kwa nini baadhi ya watu wanashikilia sana hadithi mbili hizi[28] ambazo hupingana na Qur'ani Tukufu yenye maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa Musa AS kwamba asimame mbele ya Firauni. Hadithi mbili hizi zitalinganishwa vipi na hadithi nyingi zinazoamrisha kuwapinga madhalimu? [29]

Naam, waghafilifu miongoni mwa watu, ndio ambao huyatupa hayo yote kando wakashikamana na hadithi mbili hizi dhaifu kuwatukuza wafalme na kuhimiza wasaidiwe. Watu kama hao, lau wangekuwa wenye dini hasa, kando ya hadithi zao hizo dhaifu wangeongezea zingine zinazopinga dhulma na uonevu pamoja na? kukanya kuwasaidia madhalimu. Hao hawana uadilifu kwa kuwasaidia maadui wa Mwenyezi Mungu na kuepukana kwao na mafunzo ya Qur'ani na hadithi sahihi za Mtume. Undani wao, uliwafanya kuyatenda hayo. Undani na kutaka ukubwa humvutia mtu kusaidiana na madhalimu.

Hivyo basi, kuzitawanya elimu na sheria za Kiislamu ni jambo muhimu sana ambalo hulitekeleza mafaqihi waadilifu ambao ni rahisi kwao kupambanua baina ya haki na batili, na wanajua namna takiya inavyostahili kutumiwa kwa maslahi ya kulinda njia nyoofu zisichafuliwe kama Maimamu Watakatifu walivyokuwa wakifanya.

Kama tunavyojua, wakati mwingine Maimamu wetu walibanwa na watawala wadhalimu kwa hali ambayo iliwabidi wafanye takiya kwa sababu ya hofu waliyokuwa nayo kwamba madhalimu hao wangeikatilia mbali mizizi ya dini lau wangelitoa hukumu ya hakika.

Hapana shaka kwamba hadithi tuliyoitaja juu inathibitisha utawala wa faqihi ambao ni huohuo ukhalifa (ushika makamu) katika mambo yote yanayohusiana na Utume.

Ukhalifa uliopokewa katika hadithi, "Ewe Mwenyezi Mungu, warehemu makhalifa wangu," hauna tofauti ya wadhifa wa ukhalifa ambao umo katika hadithi nyingine isemayo, "Ali ni khalifa wangu."

Jumla "Ambao watakuja baada yangu, watazipokea hadithi zangu" hufafanua ni nani khalifa na wala siyo ukhalifa ni nini, kwa maana tangu mwanzo wa Uislamu ulikuwa unafahamika wazi. Pia kwa mwulizaji alipomwuliza Mtume Mtukufu SAW hakumwuliza maana ya khalifa au ukhalifa, bali aliuliza "Ni nani hao makhalifa wako?"

Ni jambo la kustaajabisha kuwa hakukuwepo hata mtu mmoja katika zama za Sayyidna Ali AS aliyekifasiri cheo cha ukhalifa kuwa ni cheo cha kumrithi Mtume tu, bali Waislamu wote walikifasiri cheo hicho kuwa utawala na uendeshaji wa serikali na utekelezi wa maamrisho ya Mwenyezi Mungu, na walikuwa wakitoa dalili nyingi mno. Lakini kwa nini baadhi yetu hawakutia maanani maana ya kifungu "Ewe Mwenyezi Mungu, warehemu makhalifa wangu?" Mbona baadhi hudhania eti ukhalifa baada ya Mtume ni wa mtu maalumu? Kwa kuwa Maimamu AS walikuwa ndio makhalifa wa Mtume Mtukufu SAW basi haiwi kwa maulamaa wengene wasio wao kuwahukumu watu na kuwatawala bali umma wa Kiislamu hubaki kiholela bila ya mwamuzi wa sheria? Na sheria za Kiislamu zisimamishwe zisifuatwe na milango yao waiache wazi kwa maadui wao? Bila shaka dhana ya namna hii na msimamo huu ni mbali sana na Uislamu, kwani ni uvurugifu wa fikra ambayo Uislamu umejitenga nayo.

قال أبوالحسن موسی بن جعفر «ع»: إذا مات المؤمن بکت عليه الملائکة، وبقاع الأرض التي کان يعبد الله عليها، وأبواب السماء التي کان يصعد فيها بأعماله، وثلم في الاسلام ثلمة لا يسدها شيء، لأن المؤمنين الفقهاء حصون الإسلام کحصن سور المدينة لا...

Ali bin Abi Hamza alimsikia Imam Musa Kadhim AS[30]akisema: "Muumin (aaminiye) anapokufa, malaika humlilia. Vilevile humlilia sehemu za ardhi alizokuwa akiabudia Mwenyezi Mungu. Na milango ya mbingu ambako amali zake zilikuwa zikipitia kupanda juu. Na huacha katika Uislamu pengo ambalo halizibiki kwa chochote, kwa sababu waaminio walio mafaqihi ni walinzi wa Uislamu kama kitalu (au seng'enge) inavyoulinda mji (au boma)."

UCHUNGUZI JUU YA HADITHI HII

Katika kitabu hicho hicho al-Kafl, mlango huohuo, kuna mapokezi mengine yasemayo: "Anapokufa Muumin aliye faqihi . . ." ambapo upokezi wa hadithi ya kwanza hauna neno "faqihi", lakini itaeleweka kutokana na kuiongezea hadithi iliyotangulia jumla "Kwa sababu waaminio walio mafaqihi" kwamba, neno "faqihi" liliondolewa mwanzoni mwa hadithi hiyo kwa kuwa hulingana na maneno "Huacha katika Uislamu pengo" na neno "walinzi" na mfano wa hayo yanayolingana na hali ya wanavyuo wajuzi na waumini.

UELEWEKO WA HADITHI

Maneno "Waaminio walio mafaqihi ni walinzi wa Uislamu . . ." yana maana ya kuwalazimisha mafaqihi wazilinde itikadi na imani za Kiislamu, sheria zake, hukumu zake na mipango yake. Maneno hayo kamwe hayakumtoka Imam AS kwa kutaka kusifu, kutukuza au kama tunaitana kwa majina ya heshima, kama 'Mtukufu' au 'Mheshimiwa' au 'Hujjatul islam' na kadhalika.

Iwapo faqihi atawaacha watu, mambo yao asiyajali, bali aketi tu nyumbani mwake ajifiche huko, asizitetee kanuni za Kiislamu wala kuzieneza, wala asifanye lolote la kuuletea umma wa Kiislamu maslahi na kamwe asiwe na hima juu ya Uislamu na Waislamu, je, mtu kama huyo jamani, anafaa kuzingatiwa au kuchukuliwa kuwa ni mlinzi wa Uislamu! Au anafaa kuitwa kitalu cha nyumba au boma la uislamu?

Rais wa Jamhuri anapomchagua au anapomtuma ofisa fulani kwenda wilayani au kwenda katika mji mdogo ili ayawakilishe maslahi ya serikali ya ulinzi wa- eneo hilo, je, wajibu huu wa afisa huyo utampa nafasi ya kujifungia nyumbani mwake na kumwacha adui atawale na kuliangamiza eneo hilo kwa uharibufu wake wa kiadui? Au wajibu wake kamaafisa utamfanya atumie mbinu zote na juhudi zake zote azitoe ili kuimarisha usalama kwa kutoa ulinzi unaofaa eneo hilo!

Iwapo mtasema, "Sisi tunazilinda baadhi za hukumu" nitakuwa mwepesi sana wa kuwatupia swali hili, "Je, mnazitekeleza kanuni za adhabu za Kiislamu kwa wenye hatia?"

"La." Ndilo jibu lenu.

Basi nyinyi kwa hapa, yaani kwa kitendo chenu hiki, tayari mmezua upekecho na udhia wa kubomoa jengo la Ki islamu ambapo ilikuwa ni wajibu wenu kulitengeneza na kulitia kiraka au kuzuia kabisa toka mwanzo hatari hii inayolikabili jengo isitokee.

Swali la pili, "Je, ngome na uchumi wa nchi mmeutetea usinyakuliwe? Na je, mmejitoa mhanga kuhakikisha usalama wa nchi na ardhi yetu?"

"La, bali tunamwomba Mwenyezi Mungu atusaidie." Ndilo jibu.

Hapo tena mmeutoboa upande wa pili kuongezea wa kwanza.

Swali la tatu, "Je, mmezikusanya haki za mafakiri mlizoambiwa na Mwenyezi Mungu kuzitoa katika mali za matajiri ili kuwapa wenyewe?"

"La, hilo si katika wajibu wetu. Mungu atakapopenda litafanywa na mtu mwengine, Inshallah." Ndilo jibu hilo!!

Haya basi, je, mnaona, kwa sasa jengo limebakiza nini? Pana hofu ya jengo lote kuporomoka na kubaki gofu. Mfano wa Shah Sultan Hussein wa Isfahani, Iran[31] .

Nyinyi ni walinzi wa aina gani wa Uislamu? Hakuna jambo lolote la Kiislamu mnalotakiwa kulilinda ila mnalitolea udhuru kadha wa kadha ili rnsilitimize. Je ulinzi wenu kwa Uislamu ndio huo? Wajibu wenu hamuujui?

Maneno yake Imam kwamba "Mafaqihi ni walinzi wa Uislamu" yanakusudiwa kwamba wao wanakalifishwa kuutetea na kuulinda kwa uwezo wao wote, na kuulinda Uislamu ni katika mambo muhunu kabisa tena ya wajibu. Pia ni wajibu juu ya wanavyuoni, na vyuo vya kidini kuufikiria sana ili uhifadhike ipasavyo. Hukumu zake, itikadi na nidhamu zilindwe kama alivyofanya Mtume Mtukufu SAW na Maimamu waongofu.

Sisi hutosheka tu na kiasi kidogo cha hukumu huku tukiacha mengi ya masiala. Masiala mengi ya Kiislamu hivi sasa kwetu ni kama mageni kabisa hatuyajui. Bali Uislamu wote kwetu ni mgeni na wala haukubakiza ila jina lake tu. Adhabu zilizopendekezwa na Uislamu zimeachwa. Adhabu zilizopokewa katika Qur'ani Takatifu hivi sasa husomwa tu kama aya zinginezo bila kufuatwa mpaka sasa Qur'ani haikubakiza ila muundo wake tu. Tunapoisoma Qur'ani hatuisomi kwa lengo lake lililoteremshiwa, bali kwa lengo la kutoa sauti nzuri kama kinanda na kuzingatia herufi na makhariji yake ya asili tu. Ama kuyashughulikia mambo yajamii yaliyoharibika au kukomesha ufisadi unaotapakaa kote ulimwenguni kila kukicha, hayo kwetu ni mambo yasiyotukera kwa hivyo hayatuhusu. Yatutosha tu, kwa mfano kusoma aya hii:

الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ

"Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, kila mmoja mpigeni mijeledi mia moja. " (24:2). Lakini kuzitekeleza adhabu hizo na zinginezo, hayo si yetu — la!

Sisi huuliza, je, hivyo ndivyo alivyokuwa Mtume Mtukufu SAW? Je, alikuwa akitosheka tu kwa kuisoma Qur'ani pasina kuyatekeleza maamrisho yake wala kuzipitisha hukumu zake? Je, makhalifa wake waliokuja baada yake walitosheka tu na kuzifikisha hukumu za sheria za Kiislamu kwa watu kisha baadaye wanaziachilia? Je, Mtume na makhalifa wake hawakuwa wakimchapa viboko mwenye hatia ya kuchapwa viboko au kumrujumu mwenye hatia inayostahiki adhabu hiyo? Rudini mkasome tena sheria za adhabu, visasi na fidia katika vitabu vya fiqihi ili mjue kwamba yote hayo yanatokana na shina hasa la Kiislamu. Dini ya Islamu ilikuja kuitengeza jamii kupitia kwa serikali adilifu ya watu.

Nakariri tena na tena kwamba, sisi tumekalifishwa kuuhifadhi Uislamu, na ni katika mambo yaliyo muhimu tena wajibu zaidi kuliko sala na saumu. Wajibu huu ndio kwao damu tukufu ya Imam Husayn AS ilimwagwa.

Ni juu yetu hayo yote tuyafahamu na vilevile tuwafahamishe wengine. Mtakuwa makhalifa (warithi) wa Mtume Mtukufu SAW iwapo mtawafahamisha watu wajue ukweli wa Uislamu. Wala msiseme: "Tutaacha kufanya hivyo hadi atakapodhihiri Imam Mahdi AS!" Je, pia mnaiacha sala kwa kumgojea Imam Mahdi AS? Kuhifadhi dini ya Islamu ni wajibu zaidi kuliko kusali. Msiseme kama alivyosema hakimu wa mji wa Khumayn, eti: "Inafaa kuyaeneza maasi ya kila aina ili kuharakishwe kudhihiri kwa Imam Mahdi AS." Yaani eti lau mambo machafu na ya aibu hayataenezwa, Imam Mahdi AS hatadhihiri[32]. Jamani msitosheke na kukaa katika vikao mbali mbali kujadiliana na kufanya utafiti wa mambo mahsusi tu, bali zameni katika kuzidurusu hukumu zote za uislamu. Uenezeni ukweli wa Kiislamu. Andikeni kisha myata-wanye, na Mungu akipenda Inshallah yatawaathiri watu, kwani hata mimi mwenyewe nimeijaribu njia hii nikaona mafanikio yake.

MAFAQIHI N1 WAWAKILISHI WA MITUME

عن أبی عبدالله الصادق «ع» قال: قال رسول الله «ص»: الفقهاء أمناء الرُّسل مالم يدخلوا في الدنيا. قال: يا رسول الله: وما دخولهم في الدنيا؟ قال: اتباع السلطان، فاذا فعلوا ذلک فاحذروهم علی دينکم.

Sukuuni amepokea hadithi kutoka kwa Imam Sadiq AS akisema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW amesema, 'Mafaqihi ni waaminifu (wawakilishi) wa Mitume, maadamu hawajajiingiza katika dunia.' Akaulizwa, 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, vipi kuingia kwao katika dunia?' Akajibu, 'Kuwafuata masultani. Wakifanya hivyo, basi jihadharini nao juu ya dini yenu.'" (al-Kafi)

Hatuna wakati wa kuzipekua hadithi zote kwa ukamilifu kwa sasa kwa kuchelea upekuzi mrefu, bali tuangalie tu jumla "Mafaqihi ni waaminifu wa Mitume" ambayo inahusiana na utawala wa faqihi.

Kwanza kabisa, hapana budi tujue wajibu, wadhifa na jumla ya shughuli za Mitume na Manabii ili tuweze kufikia utambuzi wa kujua taklifu ambazo mafaqihi wawakilishi wa Mitume walikalifishwa kwazo.

rudi nyuma Yaliyomo endelea