rudi nyuma Yaliyomo endelea

Je, tuuache utajiri huu mkubwa upotee au uendelee kubaki ardhini mpaka Imam Mahdi AS adhihirike? Je, utajiri huo wagawanyiwe masharifu? Masharifu wanataka kuutumia vipi utajiri huo wakati tunajua kwamba haki ya masharifu na mafakiri ni kiasi kile ambacho chatosha kuendesha maisha yao. Bajeti ya Kiislamu imegawanywa kwa namna ambayo kila pato limewekewa matumizi yake. Kuna mfuko mahsusi wa zaka, mwingine wa sadaka, khums na mifuko mingineyo. Pato la masharifu linatoka katika khums. Kuna hadithi inayosema kwamba sharifu akibakiwa na fedha baada ya kutoa gharama zake mwisho wa mwaka, basi arejeshe kwa mtawala wa Kiislamu zile fedha zilizozidi, na ikiwa atapungukiwa na fedha, basi lazima mtawala amsaidie.

Fedha na mali zinazopatikana kwa kupokea jizya kutoka kwa wadhimmi*, na kharaj inayopatikana kwa kukodisha mashamba makubwa ni kubwa mno. Ni wadhifa wa mtawala au walii kuwatoza jizya na kharaj wadhimmi na wapangaji wa mashamba kiasi wanachostahili na wanachokimudu. Kodi ya kharaj inayopatikana kwa kukodisha mashamba makubwa, ambayo ni mali ya Mwenyezi Mungu inamilikiwa na serikali ya Kiislamu. Kwa hivyo, kuna haja ya kuwepo utawala na mfumo mkamilifu wa Kiislamu ili kuzuia machafuko, kukusanya na kugawanya mapato kufuatana na maslahi ya Waislamu wote.

Kwa hivyo, utaona kwamba sheria za Kiislamu juu ya fedha na mali zinathibitisha dalili ya kuunda serikali ya Kiislamu ili sheria hizo zipitishwe.

2- SHERIA ZA ULINZI

Kule kuwepo sheria zajihadi (vita vitakatifu), na kupigana kuulinda uhuru wa Waislamu na dini yao, pia ni katika mambo yanayodhihirisha haja ya kuwepo serikali yenye maongozi ya kiislamu.

Uislamu umeweka sheria ya kuwa macho, kujiandaa na kujiweka tayari tayari kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu akisema:

وَأَعِدُّواْ لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ...

"Na waandalieni nguvu (silaha) mwezavyo ..." (8:60).

Lau kama Waislamu wangeshikamana na amri ya aya hii ya kujiweka tayari na kujiandaa kwa mapigano wakati wote, halingekuwa rahisi kwa Mayahudi kumudu kuiteka ardhi yetu na kuuharibu msikiti wa Baitul Muqaddas (Jemsalem) uitwao Masjidul Aqsa[18] na hatimaye kuuteketeza bila kukabiliwa na upinzani wowote. Lakini hayo yote yamewafika Waislamu kutokana na mbinu kabambe za kuwazuia na kuwaweka nyuma wasiandame utekelezi wa sheria za Mwenyezi Mungu na pia wasiwaze jinsi ya kujiundia serikali iliyo safi na yenye utengevu.

Kwa hivi sasa, lau viongozi wa Kiislamu wote wataziandama na kuzitimiza sheria za Kiislamu zilivyo, kisha wazitupilie mbali tofauti zao na uovu wao mpaka wote wawe kitu kimoja kwa kila jambo, kwa hakika kabisa gengi dogo la Mayahudi, vibaraka wa Marekani na Uingereza, hawataweza tena kuyafikia na kufanya yote wanayoyafanya hata wakisaidiana. Lakini wapi, na tangu lini viongozi wa nchi za Kiislamu wakazifuata sheria za Kiislamu! (Maana wote wamewafikiana kutowafikiana).

Aya isemayo, "Na waandalieni nguvu (sUaha) mwezavyo " inatusisitiza kuwa tayari kabisa kwa vyovyote vile ili maadui wasituchokeshe na kutudhulumu. Lakini tulipokosea njia na huku tunaonekana tu pamoja hali tuko mbalimbali kwa vitendo na mawazo, maadui zetu waliikiuka mipaka yetu, wakatuingilia, wakatufanyia ufidhuli na hatimaye kutufanyia dhulma na kutubagua.

3- SHERIA ZA ADHABU, FIDIA NA KISASI

Palipo na utekelezi wa sheria hizo tatu, usawa huenea kwa kumtoza faini (fidia) mwenye kuhalifu na kukabidhiwa mlalamishi, kuchukuliwa kisasi na kadhalika. Lakini mambo hayo hayatimiziki pasipokuwa hakimu au mtawala wa Kiislamu, na utawala wa serikali halali.

DHARURA YA KUFANYIKA MAPINDUZI

Baada ya kufariki kwa Mtume Mtukufu SAW, maadui wa dini, yaani Bani Umayyah[19] walijitahidi sana kuhakikisha kwamba serikali ya Kiislamu chini ya utawala wa Ali bin Abi Talib AS haitothibiti; juu ya kuwa serikali hiyo iliridhiwa na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Chuki zao hizi zilivuruga utulivu wote uliokuwepo mpaka wakafaulu kuupeleka kombo Uislamu kabisa kama walivyoazimia, kwani lengo lao ni kinyume na Uislamu wenyewe.

Baada yao, walikuja Bani Abbasi[20] Nao wakafanya vilevile mpaka ukhalifa ukageuka usultani na ufalme wa kirithiana. Mwisho, sheria na hukumu zikafanana kabisa na zile za Shahanshah wa Uajemi, au Mafirauni wa Misri, hali iliyoendelea hadi leo hii. Muundo na siasa ya Bani Umayyah na Bani Abbasi zilikwenda dhidi ya sheria za Kiislamu.

Sheria za Kiislamu na hata akili zetu sisi wenyewe zinatuwekea wazi hatari ya kuachilia mambo kama hayo kuendelea ambapo pana ushahidi mwingi wa Qur'ani Takatifu na hadilhi unaoelezea misingi yote na mifumo isiyofungamana au iliyo kinyume na Uislamu kuwa ni shirki*. Na mtawala wa mambo kama hayo ni taghuti* au shetani Nasi tunatakiwa kuondoa shirki katika jamii ya Kiislamu na kuiweka mbali kabisa na umma wetu, na wakati huohuo tunatakiwa kuasisi mfumo wa usawa unaolingana na malezi bora yatakayoupondaponda utaghuti (ushetani) na kuuangusha chini utawala usiofuata sheria za Kiislamu, kwani ndio unaoeneza ufisadi na uharibifu wote. Kwa hivyo, inapasa kwa mwenye kueneza ufisadi kuondolewa kabisa na kukomeshwa kwa kutiwa adabu kali.

Firauni aliiharibu jamii katika utawala wake na asiitengeze, ndiyo maana Mwenyezi Mungu akasema:

إِنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ  

"Alikuwa miongoni mwa wafisadi (waharibifii)," (28:4).

Pana njia mbili tu wala hakuna ya tatu zinazomwongoza mja: Aidha akakamie juu ya kutenda maovu; au akaidi na kuuasi utawala wa kitaghuti (kishetani) na aupige vita kadiri ya uwezo wake japo kwa kuutingisha tu, kuuondoa au kuupunguza nguvu. Muumin halisi, huichagua hii njia ya pili. Na huu ndio mwendo wetu na tunalenga kuziangusha mifumo yote potoshi, na kuwakomesha majambazi wahaini wanaowadhulumu raia. Na si sisi tu wenye wajibu huu, bali ni wa kila Mwislamu popote alipo ajishughulishe na kuyaleta mapinduzi ya Kiislamu.

HAJA YA KUWEPO UMOJA KATI YA WAISLAMU

Kwa upande mwengine, tunayo taabu ya kujiunganisha, kwani wakoloni na madikteta waliigawanya nchi yetu na wakawatenga Waislamu katika makundi mengi.

Dola la Ottoman (Uthman) lilipofanikiwa kujiunga na kujiunda pamoja, wakoloni walikwenda mbio, mwisho wakalitawanya. Bila shaka mnakumbuka Warusi na Wazungu waliwapiga Waottoman (Waturuki) na kugawana ardhi walizoziteka. Hatukatai ni kweli kwamba baadhi ya watawala hao walikuwa na nguvu, akili na ustadi. Na wengi wao wakawa mafisadi wakubwa hata wakawatawala watu kifalme hasa, lakini pamoja na hayo, wakoloni waliwaogopa wale watu wema wasije wakasaidiana na watu wengine kuchukua usukani wa kuongoza dola lenye uchumi na lenye nguvu za kuutimua ukoloni. Kwa sababu hiyo baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia haikuchukua muda mpaka nchi wakaigawanya katika madola madogo madogo vingi na wakampachika kibaraka katika kila dola. Hata hivyo, haikuchukua muda, baadhi ya madola yalijitoa katika ubeberu huo.

Na sisi hatuna njia ya kuunganisha umma wa Kiislamu kuwa kitu kimoja, na kuikomboa ardhi yetu kutoka mikononi mwao, na kuziangusha serikali za vibaraka wa wakoloni ila kwa kuiweka serikali yetu ya Kiislamu. Na hatutaweza kuitimiza ahadi hii ya kuunda serikali ya Kiislamu yenye kuwahudumia wananchi mpaka kwanza tuvunje vipengele vyote vya hiana, tuyateketeze masanamu na watu mashetani wanaosambaza dhulma na uharibifu humu duniani.

Kwa hivyo, tujifunze kutokana na usemi wa bintiye Mtume Mtukufu SAW Fatimah Zahra aliponena: "Kututii sisi ni utengevu kwa watu, na uongozi wetu ni masalimiko (amani) kutokana na utengano. . ."

N1 LAZIMA KUWAOKOA WANAODHULUMIWA NA WANAONYANYASWA

Wakoloni wakisaidiwa na vibaraka wao, walifanikiwa kutekeleza lengo lao dhidi ya uchumi wetu. Matokeo yake ni kuwagawa watu makundi mawili — wanaodhulumu na wanao dhulumiwa. Mamilioni ya wananchi waliodhulumiwa na kunyanyaswa waliachwa wakitaabika na kufa kwa njaa huku pia wakikabiliwa na taabu za huduma za afya na elimu. Wakati huohuo hapakukosekana watu wachache wenye mapato ya hali ya juu wakiueneza ufisadi.

Wenye taabu na dhiki ya njaa walipokuwa katika mapambano ya kujikomboa kutoka katika minyororo ya taabu waliyonayo, genge la watu wachache nao walikuwa mbioni kuyaondolea mbali mapambano hayo. Kwa hivyo ni wajibu wetu sisi kuwaokoa watu wa namna hii, kwani tunahimizwa na tunaambiwa, kuwasaidia wanaodhulumiwa na kuwapinga wanaodhulumu kama Amirul Mu'minin Ali AS alivyowausia wanawe, Imam Hasan na Imam Husayn aliposema, "Muwe mahasimu (maadui) kwa dhalimu, na kwa mdhulumiwa muwe wasaidizi."

Maulamaa na viongozi wa Kiislamu wanatakiwa kuyasimamisha, yaani kuyaweka mapambano dhidi ya watu wenye nia mbaya, wakorofi na mabepari ili katika jamii kusiwe na mwombaji mwenye kunyimwa haki yake akabaki kumnung'unikia mlafi aliyekolea katika anasa.

Amirul Mu'minin Ali AS asema, "Naapa kwa jina la yule ambaye alizipasua tembe (punje) na akawaumba watu, lau si kuwepo wenye kunisaidia, na lau si ahadi aliyoichukua Mwenyezi Mungu kwa wanavyuoni kwamba asimakinishwe (asi-achiliwe) dhalimu mwenye shibe kuendelea na dhulma yake, na (lau pia si) njaa ya mdhulumiwa, ningeachilia huru hatamu (nisingeshughulikia kamwe mambo ya utawala) na ningeiona dunia yenu kwangu mimi ni kitu kisicho cha thamani hata kuliko chafya ya mbuzi." (Nahjul Balagha)

Haya basi, itakuwaje halali kwetu tuwanyamazie watu wachache walio mahaini na vibaraka wa wakoloni wakitwaa mamlaka kwa kutumia nguvu za silaha na huku mamilioni ya watu wananyimwa haki ya kufurahia neema za uhai! Bila shaka ni wajibu juu ya wanavyuoni na Waislamu wote kwa pamoja, dhuluma hii waiwekee mpaka na wahangaike kwa minajili ya kuwasaidia mamilioni ya wenye dhiki ili kuziangushilia mbali serikali za madhalimu, na badala yake kuasisiwe utawala halisi wenye maongozi ya Kiislamu.

HADITHI ZIONESHAZO HAJA YA KUUNDA SERIKALI

Tayari nyuma tumethibitisha dharura ya serikali ya Kiislamu kiakili na kisheria. Hadithi hii ya Imam Ridha AS itatuwekea wazi zaidi jambo hili:

Kumepokewa hadithi kutoka kwa Abdul Wahid bin Muhammad inayosema, "Mwulizaji aliuliza, 'Je nieleze, inafaa kwa Mwenyezi Mungu kukalifisha (waja wake)? Ikiwa ni la, mbona basi aliwaweka wenye mamlaka (mawalii au waangalizi) na akaamrisha lazima kutiiwa?' Jibu ni, 'Hilo ni kwa sababu nyingi. Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba, viumbe (watu) walipowekewa mipaka maalum na kuambiwa wasiikiuke mipaka hiyo ili wasije wakajitatiza, hawakuwa ni wenye kutimiza hivyo, basi palihitajika awepo kati yao kiongozi mlinzi wa sheria, mwenye mamlaka juu yao ambaye atawazuia kukiuka waliyozuiwa, kwani bila kufanya hivyo, mtu hangekuwa tayari kuacha uraibu* wake, starehe zake na manufaa yake kwa kumnusuru mwengine.

Imam Ridha AS[21] aendelea kusema kwamba, "Hakuna kundi la watu walioweza kudumu na kuendelea vyema pasina kuwa na kiongozi mwangalizi wao, kwani ni lazima wawe na mambo yao ya kidunia na ya kidini. Hivyo basi, haingewezekana kwa Mwenyezi Mungu kuwaacha viumbe wake kwa jambo analojua ni lazima juu yao, na wala hawanyoki pasina jambo hilo ili kwalo wapigane na adui wao, wawe chini ya kivuli chake, wasali sala ya jamaa na Ijumaa nyuma yake, wajijumuishe pamoja kwalo na dhalimu azuilike kudhulumu kwalo."

Imam aendelea kusema, "Lau Mwenyezi Mungu hangewa wekea kiongozi mwema, mwaminifu na mwenye kuwahifadhi sawasawa, mila zao (hao watu) zingemea mizizi, dini inge ondoka, sunna na sheria zingepanguka, wazushi wange ongezeka, makafiri na walahidi'*' wangeonekana kupungua, kwani wangejishabihisha na Waislamu na hali zao zngetofautiana sana. Hayo ni kwa sababu watu ni wapungufu na wenye haja wasio kamili mbali na kutofautiana kwa mazingira yao. Kwa hivyo, lau hakungekuwa na kiongozi (walii) mwenye kuhifadhi sheria za Mtume Mtukufu SAW watu wote wange fisidika." (Halush-Sharayi'. jz. 1, uk. 183, hadilhi ya tisa).

Dalili zote alizozitoa Imam Ridha AS juu ya dharura ya kuwepo mtawala mwadilifu (waliyul-amr) zipo kila wakati hadi leo hii. Na kwa hivyo, mwongozo halisi wa Kiislamu watakikana kila wakati.

Kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, kuzama katika anasa za kila namna, kuutawanya uharibufu kote ulimwenguni na kudokoa haki za wanyonge, ni mambo yanayoendelea kila wakati na wala hayatokei wakati fulani yasitokee wakati mwingine ndipo sheria za Mungu zikahitajika kushika zamu (kuendelea) ili mtu aishi kwa raha na asiikiuke mpaka aliyowekewa. Hatuwezi kusema kwamba mambo hayo yalikuwepo katika zama ya Sayyidna Ali AS na baadaye watu wakawa malaika. Hii ni hekima ya Mwumba kwamba watu waishi daima kwa uadilifu chini ya sheria za Mungu. Sheria za Mwenyezi Mungu haziwezi kubadilishwa. Kwa hivyo, leo na sikuzote kuna haja ya kuweko walii, yaani mlinzi na mtawala mwenye mamlaka ya kusimamia sheria na kanuni za Mwenyezi Mungu.

Nitakariri tena na tena kwamba, ili kufagilia mbali dhulma, ukiukaji wa sheria, ufisadi na uonevu kwa wanyonge, na badili yake uaminifu uenee, watu waongozwe kwenye njia nyoofu, walaghai na wapinzani watokomezwe na sheria zifuatwe vilivyo, ni lazima tuanzishe serikali halisi na halali ambayo itaondoa mabunge yaliyo haramu na itawazuia wageni wasiingilie nchi za Kiislamu. Kazi hii haiwezekani bila ya kuwepo serikali inayoongozwa na mtawala aliye mwaminifu na salihi*.

Hapo mbeleni hatukufanya lolote. Na wala hatukujishughulisha kuuangusha utawala wa wahaini wahuni, bali tuliweka nyuma tu, jambo lililosababisha unyonge, udhaifu na utengano kati ya Waislamu. Sheria za Kiislamu si tu zilibaki bila kutekelezwa, bali zilibadilishwa badilishwa pia, na badala yake mabeberu waliwatumia wanasiasa walio vibaraka wao ili kuleta sheria za kikoloni na mila ya kigeni katika taifa la Waislamu na kuwafanya watu wawe na kasumba ya magharibi. Hawangeweza kuyafanya mambo machafu hayo lau tungekuwa na kiongozi wa serikali yenye maongozi halisi ya Kiislamu. Najambo hili ni wazi kabisa.

Mfumo wa Serikali ya Kiislamu

TOFAUTI NA MIFUMO MINGINE YA KISIASA

Serikali ya Kiislamu tunayoisisitiza haifanani na serikali tuzijuazo sisi zinazoongozwa na kiongozi aliye dikteta anayechezea mali ya umma na maisha ya raia wake. Mtume Mtukufu SAW, Sayyidna Ali AS na makhalifa wengineo hawakuwa na utawala wa kiimlaa*.

Serikali ya Kiislamu si serikali ya kidikteta au kisultani, bali ni serikali ya kikatiba. Lakini pia si ya kikatiba tuijuayo sisi ambayo kupasishwa kanuni zake kunategemea rai za watu walio wengi. Ni serikali ya kikatiba kwa kuwa wanaoongoza na wanaoendesha serikali huwa wanatunga kufuatana na masharti yaliyomo katika Qur'ani na sunna za Mtume. Kwa hivyo, huwa ni serikali yenye maamuzi ya kanuni za Mungu Mwenyewe. Msingi wa tofauti ni hiyo, ya kuwa, serikali za kikatiba za kisultani au kijamhuri sheria zake ni za kutungwa na watu, na ile ya Kiislamu, sheria zake hutoka kwa Mungu. Katika serikali hizo wanabunge waliochaguliwa na watu au mfalme hutunga sheria walakini katika dini ya Islamu Mwenyezi Mungu tu Ndiye Mwenye haki ya kutunga sheria, na ghaira ya sheria Zake sheria zingine haziruhusiwi kupitishwa. Kwa sababu hii, kazi ya bunge (majlis)[22] katika serikali ya Kiislamu ni kupanga mipango (taratibu) yenye kuwahudumia wananchi kwa ajili ya wizara tofauti na kupasisha miswada inayofuatana na sheria za Kiislamu.

Imani ya Waislamu ni kuwa, yote yaliyomo katika Qur'ani na katika hadithi ni lazima yafuatwe.

Serikali ya Kiislamu hufuata sheria kikamilifu kwani mwamuzi au hakimu ni Mungu Peke Yake ambaye Ndiye Mtunga sheria Zake..Kila mtu, Mtume Mtukufu SAW, makhalifa wake na watu wengineo hufuata hukumu (sheria) ya Kiislamu ambayo hushuka katika wahyi (ufunuo) ukabainishwa na Mtume halafu kuhifadhiwa katika Qur'ani Takatifu.

Mtume Mtukufu SAW alichaguliwa kuwa "Khalifa (Mjumbe) wa Mwenyezi Mungu"(2:30) ili kuwasawazisha watu kwa kuamua wanayohitalifiana kwa uadilifu, na alisema na Mwenyezi Mungu kwa njia ya wazi akaelezwa watakao kuwa makhalifa wake baada yake, na yeye alipomtangaza Ali bin Abi Twalib kuwa khalifa wake ilikuwa ni kuutekeleza wajibu wake na wala si kwa kuwa ni mkwewe au kuwa ni tajiri sana au kwa lengo jingine.

Naam, serikali katika Uislamu ina maana ya kufuata sheria, nao mawalii (walinzi) wa sheria walio amuriwa na mwenyewe Mwenyezi Mungu ni lazima watiiwe pasina kutoa rai au maoni haya na yale au kufuata matamanio ya nafsi. Mwenyezi Mungu asema, "Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka miongoni mwenu " (4:59).

Utawala wa Kiislamu hauwi wa kifalme kwa sababu unapinga kukiuka mipaka na kutweza watu kwa roho zao na mali zao pasina haki. Ndiyo maana humpati kiongozi halisi wa Kiislamu akistarehe katika majumba makubwa makubwa ya maghorofa au yenye ukumbi mkubwa wa baraza la kifalme na mengineyo yenye maana ya anasa kubwa ambayo huteketeza karibu nusu ya pato la nchi.

Maisha ya Mtume Mtukufu SAW mnaelewa wazi yalivyo kuwa, pamoja na kuwa alikuwa kiongozi wa hali ya juu anayetoa hukumu yeye mwenyewe. Makhalifa wake walio mfuata nyuma nao walikuwa vilevile mpaka Bani Umayya walipounyakuwa utawala.

Historia ya uongozi wa Amirul Mu'minin Ali bin Abi Talib AS inajulikana wazi. Hakuwa mtu wa mambo mengi, yaani alikuwa mtovu wa anasa licha ya Iran, Misri, Hijaz (Saudi Arabia), Yemen, na majimbo mengine mengi yalikuwa chini ya himaya yake. Sidhani kama kuna mwanafunzi maskini anayeweza kustahamilia maisha duni kama aliyokuwa nayo Sayyidna Ali AS. Imepokewa kwamba, Sayyidna Ali AS alipokuwa nazo nguo mbili alitoa ile nzuri akampa mtumishi wake Qambar, naye akavaa ile yenye viraka. Jambo hili alilifanya wakati yeye alikuwa akitawala milki* kubwa yenye watu wengi. Mwenendo kama huu lau ungeendelea hadi leo hii, basi bila shaka masultani, watawala wadhalimu na ukoo wao wasingethubutu kutwalia na kuiba hazina za taifa, wakfu na mali ya wananchi na kutumia katika ufisadi wao wa kujenga majumba ya fakhari, uasherati na anasa[23].

Ndugu zangu, nyote mnatambua wazi jinsi ufisadi ulivyoenea, na kuharibika kwa jamii nyingi, bila shaka husababishwa na ufisadi wa familia inayotawala.

Ni amani gani au sheria ipi itakayoandamwa hali viongozi kila kukicha hujenga majengo ya ajabu ya dansi, sinema na vilabu mbalimbali vya kuendeleza mambo ya aibu, ufisadi na madanguro hali majumba ya Mungu anamotajiwa (misikiti) yanavunjwa? Lau si gharama kubwa kubwa za ujenzi wa majumba ya kifalme (ikulu), na lau si wizi wa fedha za serikali unaofanywa hasa na hao vibaraka wa kujibandika uongozi kimabavu, dola au taifa lingeshindwaje kujitegemea mpaka kulazimika kuomba msaada toka Marekani jambo linalofuata unyonge na kudharauliwa!? Je, visima vya mafuta vyetu vimekauka? Au madini yetu yaliyo chini ya ardhi yetu yamekwisha?

Kila kitu tunacho, wala kamwe hatuna haja na msaada wa Marekani wala wa kwingineko lau si matumizi mabaya ya kifalme.

Kwa upande mwingine, kuna vitu kadhaa visivyo muhimu vinavyotuangamizia uchumi wa nchi. Israfu, yaani matumizi mabaya hutatiza mambo ya jamii. Zama za maamuzi ya Kiislamu, uamuzi kamili ulikuwa ukitolewa na kadhi akiwa na karatasi chache na wasaidizi watendaji wawili au watatu, pasina kuhitajia makaratasi mengi na kalamu nyingi namna zilivyo siku hizi ambapo kesi moja humaliza chungu nzima ya madaftari ambayo hayaleti faida yoyote isipokuwa ziada ya matatizo na kupoteza wakati mwingi na fedha za umma, na hatimaye kuipoteza haki ya mtu na uamuzi wa kweli kutopatikana.

MASHARTI YA HAKIMU (MTAWALA)

Mbali na masharti ya kawaida, kama akili, utu uzima, na kadhalika, ni sharti hakimu, yaani faqihi, walii au kiongozi wa umma awe:

1- Mwenye ujuzi kamili wa sheria na kanuni za Kiislamu.

2- Mwadilifu, asiyependelea.

1- Maadamu serikali ya Kiislamu ni ya kisheria, ni lazima kiongozi wa Waislamu azijue sheria kama ilivyopokewa katika hadithi. Na si yeye tu, bali kila mwenye madaraka fulani au mfanya kazi ni lazima ajue mpaka na kadiri ya haja yake. Maimamu (viongozi) wetu waliuthibitisha ufao wao kutokana na utangulizi wao wa elimu. Nao wanavyuoni wa Kishia waliweza kuwapita watu wengine kwa kuwaandama kidhati Maimamu hao.

Kuzijua sheria na kuwa mwadilifu, ni miongoni mwa nguzo muhimu za uongozi. Iwapo mtu ajua barabara mazingara ya watu, na vilevile fani mbalimbali, akawa hajui sheria, basi elimu yake hiyo haimwezeshi kuwa kiongozi (Imam) na badili yake atatangulizwa mjua sheria mwadilifu.

Toka zamani hadi leo hii, ujuzi wa sheria pamoja na kuwa mwadilifu mwenye imani na tabia njema vilizingatiwa sana katika kumfanya mtu awe anastahili kuwa kiongozi. Asiyejua sheria hafai kuongoza, kwani hatakuwa na utisho, yaani heshima kwa serikali yake na atashindwa kuzitekeleza. Kwa sababu hii, hadithi moja inasema:

الفقهاء حکام علی الملوک

"Mafaqihi ni mahakimu wa kuwahukumu wafalme." Ikiwa wafalme wanafuata dini ya uislamu basi inawabidi wawatii mafaqihi (mabingwa wa sheria za Kiislamu), watake mashauri yao juu ya kuzitekeleza sheria na kanuni za Kiislamu. Hii ina maana kwamba watawala wa kweli hasa ni hao hao mafaqihi. Kwa hivyo, mafaqihi lazima wawe na utawala rasmi, na wengineo wawafuate wao.

Naam, kama Ulivyokuwa toka zama za Mtume Mtukufu SAW na zama za Khalifa wake Sayyidna Ali AS kiongozi wa umma ni lazima azizunguke, yaani azithibiti sheria zote za dini ya Islamu. Ama watumishi wa serikali, mabalozi, wafanya kazi na maliwali mbalimbali, wao huwatosheleza tu kujua yaliyo muhimu yanayofungamana na madaraka yao.

2- Ni lazima juu ya mtawala, yaani kiongozi, awe mfano mwema wa imani, tabia mjema, uadilifu na uepukaji wa madhambi, kwani hataweza kuitekeleza mipaka na kutoa haki itakikanavyo mkiwemo ulinzi wa fedha za umma na matumizi yake na kuepuka kuwa dhalimu asipotimiza masharti hayo ili afuatwe na watu. Mungu asema:

لاَ يَنَالُ عَهْدِي الظَّالِمِينَ  

 "Ahadi yangu haitawaftkia madhalimu "(2:124).

Kiongozi asipokuwa mwadilifu, hatasalimika na kufanya hiana na kudhulumu amana za watu. Kisha, familia yake ataifanya kuwa mbele na kumkabidhi madaraka yote makubwa serikalini.

Maoni ya Shia juu ya rntu anayestahiki kuwatawala watu, yalijulikana toka siku aliyokufa Mtume Mtukufu SAW hadi leo. Shia humtanguliza aliye bora kwa ujuzi wa sheria za Kiislamu, mwadilifu katika kuzitekeleza na asiyeogopa lawama yoyote juu ya kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

HAKIMU BAADA YA UGHAIBU WA IMAM

Tunapokuwa na imani ya haja ya kuendeleza sheria za Kiislamu, na kwamba sheria hizo zinapinga ukosekano wa serikali na nidhamu katika nchi, uundaji wa serikali halali utatulazimu. Akili nazo tayari zimetoa uamuzi kama huohuo na hasa iwapo pana uwezekano wa sisi kushambuliwa au kuvamiwa na adui. Serikali yetu itaweza kupambana vikali vita vitakatifu vya kuwatetea Waislamu iwapo watachokozwa.

Hapo mbeleni, tumeamriwa kujiweka tayari tayari kwa nguvu za kumtishia adui wa Mwenyezi Mungu na adui wetu, na sheria inatuhimiza kumrudisha nyuma anayetuvamia na kumtendea alivyotutendea. vilevile Uislamu unatulingania kumsaidia anayeonewa hadi apewe haki yake, wakati huo huo kumtia adabu mwonevu (dhalimu). Yote hayo yanahitaji kuwepo serikali ya Kiislamu yenye nguvu. Matumizi ya serikali ya kutimiza wajibu huu, yatatolewa katika hazina iliyokusanywa kutokana na khums, zaka, kharaj na mapato mengineyo.

Hivi leo tangu kughibu kwa Imam Muhammad Mahdi AS hakuna hadithi yenye kumbainisha Imam au kiongozi maalum wa kuyaendeleza mambo na maslahi ya dola la Kiislamu, basi itakuwaje? Je hukumu za Kiislamu ziachwe? Au tuuache Uislamu tuandame mengine? Au tuseme Uislamu ulikuja kuwaamua watu kwa muda wa karne mbili hivi ndipo basi au ni vipi?

Sote tunatambua wazi kwamba, ukosekano wa serikali husababisha mvurugano wa Waislamu kupotelewa na haki yao, kudhalilishwa na kuchukuliwa ardhi yao. Je, mambo kama haya Uislamu utayaruhusu? Je, kuwa na serikali si lazima? Iwapo hapana aliyeainishwa kuongoza mambo ya Waislamu, bila shaka masharti ya kumwezesha mtu kutawala yatachunguzwa ambayo ni elimu, yaani ujuzi wa sheria na uadilifu, masharti ambayo mafaqihi wetu wa zama hii wanayo. Lau mafaqihi wote wangeshirikiana na ndugu zao Waislamu na kujiamulia mambo yao kwa pamoja, ingekuwa rahisi sana kwao kuunda serikali adilifu duniani.

UTAWALA WA FAQIHI

Lau kiongozi mwanachuoni, mjuzi wa sheria za Kiislamu na mwadilifu ataunda serikali, basi atatawala na kuyaongoza mambo ya janiii kufuatilia alivyokuwa Mtume Mtukufu SAW akitawala na kuongoza, na watu watalazimika kumsikiliza na kumtii. Kiongozi (au mtawala) huyo atayamiliki mambo yote ya idara, ulinzi na siasa kufuatilia mwenendo wa Mtume Mtu-kufu SAW na Sayyidna Ali bin Abi Talib AS, na atahitajika kuwa mwadilifu, mtatuzi wa daawa* baina ya watu, mjenzi wa maendeleo ya nchi, mbali na ujuzi na ulinzi wa sheria.

Hii dhana ya kuwa utawala wa Mtume Mtukufu SAW ulikuwa na mamlaka zaidi kuliko utawala wa Imam Ali AS, au utawala wa Imam Ali AS ulikuwa na mamlaka zaidi kuliko utawala wa faqihi haina msingi wowote. Hapana shaka kwamba Mtume Mtukufu SAW ana sifa na fadhila zaidi kuliko wanadamu wote, na baada yake Sayyidna Ali AS. Lakini ziada ya fadhila za kiroho hazizidishi mamlaka na madaraka ya utawala. Hayo hayo mamlaka na madaraka aliyotoa Mwenyezi Mungu kuwapa Mtume Mtukufu SAW na Maimamu Watukufu AS katika kutayarisha majeshi, kuchagua maliwali, kupokea kodi na ushuru na kutumia kwa ajili ya maslahi na maendeleo ya Waislamu, madaraka hayo pia amepewa mwanachuoni faqihi mwadilifu, isipokuwa hakutajwa kwa jina.

UTAWALA WENYE ITIBARI

Haifai kutoyaelewa vyema tuliyo tangulia kuyaeleza. Mtu asije akadhani kwamba kule kustahili kwa faqihi mwadilifu kuongoza mambo ya kiserikali ya Kiislamu humpandisha cheo na kufikia daraja ya Utume au Uimamu, kwa sababu maneno yetu haya hayahusiani na daraja, cheo au utukufu, bali tunazungumzia wadhifa na madaraka. Kutawala maana yake ni kuwaongoza watu, kupanga namna ya kuistawisha nchi na kutekeleza hukumu za sheria. Na mambo hayo ni muhimu sana tena mazito mno ambayo hawezi mtu kuyasimamia isipokuwa yule anayestahili. Hii haina maana kwamba kustahiki kwake ni kumweka juu zaidi ya watu wengine.

Utawala wa faqihi ni moja katika mambo yenye itibari* ya kiakili lililowekewa sheria kama mambo mengine yalivyo wekewa, kwa mfano kuwalea watoto. Jukumu la usimamizi wa taifa lote halina tofauti na jukumu la usimamizi wa watoto. Tukichukulia kwamba Mtume Mtukufu SAW au Maimamu jukumu lao ni kutunza watoto, basi jukumu lao hili halitakuwa tofauti na mtu mwingine akichaguliwa kuwatunza watoto haohao. Hali ni hii kwa utunzaji wa umma.

Je, faqihi mwadilifu anayeweza kutia adhabu barabara ataitoa kwa namna ambayo sivyo ilivyokuwa siku za Mtume au zama za makhalifa wake watakatifu ili tofauti ipatikane baina yao? Sheria ya Kiislamu iliyowekwa kumtia adhabu mzinifu ni kuchapwa viboko 100; hii haina maana kusema kwamba ilivyokuwa vyeo vya Mtume Mtukufu SAW, Imam Ali AS na faqihi vinatofautiana, basi hukumu pia itofautiane, yaani Mtume Mtukufu SAW ampige mzinifu viboko 150, Imam Ali AS 100 na faqihi 50. Sheria ni sheria ya Mwenyezi Mungu, hivyo kila anayehusika lazima apitishe sheria ya Mungu kama ilivyo bila ya kujali vyeo vya Mtume Mtukufu SAW, Amirul Mu'minin Ali AS au kadhi na mwakilishi wake katika Basra au Kufa (Iraq) au faqihi wa zama hizi.

Mtume Mtukufu SAW alikuwa akikusanya michango ya kodi, khums, zaka, kharaj na jizya. Je, kuna tofauti ya ukusanyaji wa Mtume, Maimamu na wa faqihi? Yaani tuseme Mtume alikuwa mahali fulani akikusanya asilimia kumi (10%) ya mapato na mahali kwingineko akikusanya asilimia ishirini? Je, Sayyidna Ali AS aliposhika ukhalifa alibadilisha sheria? La, hasha! Je, katika jambo hili tawala za Mtume Mtukufu SAW, Sayyidna Ali AS na faqihi zatofautiana? Mwenyezi Mungu alimfanya Mtume Muhammad SAW kuwa walii (kiongozi na mtawala) wa Waislamu wote. Katika madaraka yake alikuwa pia ana mamlaka juu ya Sayyidna Ali AS. Vilevile mshika makamu (Imamu) wa Mtume alikuwa na utawala baada ya kufariki kwake. Yaani Imamu au khalifa alikuwa na haki zote za kutawala, aliweza kutekeleza sheria, kumteua na kumstaafu kadhi.

Utawala uleule na uendelezi wa sheria uleule wa Mtume Mtukufu SAW na Imamu unatakiwa kwa faqihi atakayetawalia mambo ya serikali ya Kiislamu. Lakini kwa utawala kamili wa faqihi hauna maana kwamba faqihi mmoja ana mamlaka juu ya mafaqihi wote wa zama zake hata akaweza kumteua au kumstaafu faqihi mwingine. Hii haina maana kwamba mmoja ana daraja zaidi kuliko mwenziwe au mmoja ni mtawala na mwingine ni mtawaliwa.

rudi nyuma Yaliyomo endelea