rudi nyuma Yaliyomo endelea

Kanuni zenye kupinga mfumo wa utawala wa kimapinduzi wa kikatiba (Mashruta)[9] ambazo huunga mkono utawala wa kifalme na utawala wa kurithiana kama utawala halali wa nchi, ziliagizwa kutoka Uingereza na Ubeligiji. Vilevile kanuni hizo ziliigwa kutoka katika katiba za madola ya Ulaya zilikuwa ni ngeni na zinapingana na kugongana kabisa na misingi ya Kiislamu.

Jee katika Uislamu kuna utawala wa kifalme? Au utawala wa kurithiana?Au serikali ya urithi wa kifalme? Itawezekanaje kuwa hivyo hali tunajua nidhamu za utawala wa kifalme hupinga hukumu za Kiislamu na nidhamu zake za kisiasa? Kutokana na sababu kama hii, Uislamu ulibatilisha serikali zote za namna hii za kurithiana na za kifalme.

Tangu Uislamu kulimbuka kwake, ulizichukulia tawala zote za kifalme za Iran, Misri, Yemen na Roma kuwa hazikuwa za kisheria na kihalali. Hata Mtume Mtukufu SAW alimwandikia barua Mfalme Hercules wa Rome na Mfalme wa Iran, akiwataka waache kuwafanya watu watumwa wao — watu ambao walikuwa wakiwaabudu. Pia akawataka wawaache wajiamulie wenyewe nia zao zinavyoazimia ili (wapate nafasi ya) kumwabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake.

Tawala za kifalme ni tawala batili na korofi ambazo Imam Husayn bin Ali AS akikataa kuzinyenyekea na akainuka kupigana nazo ili kuzitokomeza kabisa.

Imam Husayn AS alikataa kuutii na kuutambua ufalme wa Yazid[10] na akawataka Waislamu wote wampinge Yazid.

Kwa hivyo, katika dini ya Islamu hamna nafasi ya tawala za kifatme za kurithiana. Ama ikiwa huu ndio upungufu katika Uislamu sawa na fikra zao, basi ni sawa wakisema "Uislamu una upungufu."

Pia mbali na upungufu huo katika Islamu, kuna upungufu mwingine — ambao sijui jamaa hao waliusahau ama vipi — na waseme kwamba Uislamu ulighafilika kumfikiria atakavyo fanywa achukuaye mlungula au apokeaye riba. Pia ulisahau kuweka maanani uovu wa vilabu vya pombe, na madanguro mfanyikamo machafu yote ya aibu.

Ni ajabu tena aibu, eti ili kuziba ufa huu wa upungufu, na kulijaza pengo hili, tawala za vibaraka wa kikoloni, zililazimika kuweka sheria na kanuni za kutuliza mambo, na sheria ambazo zingefaa sana, ni zile za kutoka Uingereza, Ufaransa, Ubeligiji na Marekani. Sisi kama Waislamu tunaojivunia dini yetu isiyo na fikra kama hizi, tunajua kuwa yote hayo ni haramu katika sheria zetu.

Njama ya serikali ya kikoloni ya Uingereza iliyofanywa mwanzoni mwa Mashruta [utawala wa katiba mwanzoni mwa karne hii katika Iran] ilikuwa na malengo mawili:

(a) Kufukuza na kuzishinda nguvu za ufalme wa Kizari wa Urusi nchini Iran; na

(b) Kuuondoa Uislamu na kuupindapinda kusudi usiwepo tena uwanjani ili papatikane mwanya wa kuigiza na kuingiza kanuni na mila za Wamagharibi ili zifanywe halali badala ya sheria za Kiislamu.

Desturi na mila hizi za kigeni zilizoigwa kutoka Magharibi zimeiletea jamii ya Kiislamu matatizo chungu nzima; na wanaotetea haki za binadamu, wamenung'unika sana juu ya jambo hili. Na yeyote aliyeumizwa au kupatwa na tatizo la kuitetea haki yake au kuhukumiwa chini ya desturi hizo katika Iran au kwengineko, bila shaka humchukua muda mrefu kuipata haki yake.

Mmoja wa mawakili hodari aliniambia tulipokuwa tukijadiliana, "Mimi ninaweza kuishikilia kesi moja tu ya wanaoteta mahakamani muda wa uhai wangu, pia nadhani hata mwanangu ataweza kuiendesha baada yangu."

Ni kweli, hili ni jambo ambalo lipo hivi sasa. Hata hivyo, hili huwahusu mahohehahe tu. Ama wenye vitimbi na hila, waliozoea rushwa na hongo, na hasa watawala haramu, wao kesi zao hukatwa haraka haraka kwa njia zisizo za kisheria. Hayo ni kwa sababu wao wana njia nyingi za ghururi na hadaa. Na sisi kwa wakati huu, tumeshuhudia na kuona kanuni za uamuzi wa kisasa hazimtakii mtu ila mazito tu.

Kwa mfano, kesi iliyokuwa ikimchukua kadhi au hakimu wa sheria muda wa siku mbili au tatu hivi, hivi sasa huendelea mpaka miaka ishirini. Katika muda huu, mtoto kijana atalimbuka akue huku kesi yaendelea tu asubuhi na jioni wakizungushana pasina matumaini ya kumalizika. Kila wanapotaka kuiachilia mbali, wale wateti hujikuta wamerudi mumo humo kesini.

Jamaa hao, wakati mwingine huandika katika vitabu vyao na magazeti yao eti, "Sheria za Kiislamu ni ngumu sana na za hovyo, sheria" Kuna mmoja wao aliyethubutu kwa ufidhuli wake na usafihi alionao kuandika akasema, "Ugumu wa sheria hizi (za Kiislamu) ulitokana na ugumu au ushenzi wa mabedui (Waarabu wa kuhamahama wasio na makao). Ugumu wao ndio uliosababisha- ugumu wa sheria zao hizi za Kiislamu."

Mimi hushangaa na sijui jamaa hao vipi hufikiri! Wao huwahukumu watu wengi sana kunyongwa wakidai kufuata sheria kwa makosa madogo ya kufanya magendo ya gramu 10 tu za dawa za kulevya (kama bangi na heroini). Nimepata habari kwamba watu kumi walihukumiwa kunyongwa hivi karibuni kwa makosa hayo.[11] Kisha mmoja baadaye akahukumiwa kwa ajili ya kufanya magendo ya gramu 10 tu za heroini. Walipopitisha hukumu hizo za kinyama kwa kisingizio cha kuzuia ufisadi, hawakuona ushenzi wala ukatili.

Nisemapo hivyo, sina maana ya kukubaliana na uvutaji kasumba, la hasha, ila napinga tu adhabu hii ya kunyongwa kwa watu hao. Kuuzuia uharibifu huu, ni jambo jema, lakini sharti busara itumiwe na adhabu inayostahili kosa lenyewe.

Kumcharaza aliyekunywa tembo (ulevi) viboko 80 kama Uislamu unavyopendekeza eti ni ushenzi! Ama kuwanyonga watu kwa ajili ya kosa dogo la kufanya magendo ya gramu 10 tu za kasumba si ushenzi pamoja na kuwa ufisadi mwingi ulioikumba jamii unasabaishwa na ulevi! Ajali za barabarani, unyang'anyi, kujinyonga, kushikana kabari na hata uvutaji wa kasumba (bangi) ni matokeo ya ulevi na mafunzo ya vilabu vya pombe.

Ingawa hivyo, jamaa hao hawakuwatahadharisha wanywaji tembo kwa kuwapa adhabu inayowastahil, kwa sababu Ulaya iliruhusu ulevi Kwa ajili hiyo, wao (vibaraka) hutoa kibali kamili, yaani leseni yenye uhuru kamili kwa muuzaji na mnunuzi wa ulevi.

Mbona watu hao wameutia Uislamu jangani jamani! Uislamu unapomhukumu mnywaji ulevi achapwe viboko 80 tu, mzinifu achapwe 100 na mume au mke aliyeoa au kuolewa apigwe mawe hadi afe anapofanya uzinzi, hawa hapa hupiga makelele, "Sheria hizi ni za kishenzi, katili na zilisababishwa na ujinga na ukaidi wa mabedui" na hali Uislamu uliweka adhabu zote kwa watu wote wenye makosa ya jinai ili kuzuia uchafu na mambo yote ya aibu yasisambae kwa watu wote.

Haya basi, hivi sasa uharibifu umeenea na kutapakaa kiasi cha kuwapotoa vijana wetu na kuwafanya watangetange bila lengo, kwani ufisadi waliupokea kwa njia ambazo waliouleta walikuwa wamewakusudia.

Uislamu ukitaka kuiingilia hali hii mara moja kwa kuwachapa walevi mijeledi hadharani mbele ya waaminio ili washuhudie adhabu, hao jamaa huutuhumu Uislamu kuwa "hovyo, wa kishenzi na mzito."

Hata hivyo, hatutaki kujikumbusha mauaji ya kikatili na ya kinyama yaliyofanywa na jamaa hao wanaodai uwanasheria kwa muda wa zaidi ya miaka 15 huko Vietnam, mbali na gharama kubwa kupita kiasi iliyotwaliwa kutoka katika mifuko ya umma. Wakati huohuo, Uislamu unapotaka kujitetea na kutangaza vita vya kuikata mirija ya ufisadi, wao huchachamaa na kupiga makelele, "Vita hivi ni vya nini?"

Hayo yote ni mipango na mashauri yaliyotayarishwa na kuazimiwa mamia ya miaka iliyopita, na wao wanazitekeleza polepole ili wasigunduliwe.

Mwanzo walijenga chuo mahali fulani ambapo sitaki kupataja, na sisi Waislamu hatukujitingisha bali tulighafilika, na walio mfano wetu katika kukandamizwa pia nao walikaa kimya. Waliendelea vivyo hivyo hatua kwa hatua mpaka hivi leo wana vituo vilivyo na wawakilishi wao kila mahali, mjini na vijijini.

Bidii zao, zilianziwa kwa watoto wetu ku'watanasarisha*' au kuwabaidisha (kuwaepusha) na dini yao, na sisi wakatufunga fikra ili tubakie siku zote katika kutengana, unyonge na taabu ili wao wanufaike kutokana na uchumi wetu, madini yetu, ardhi yetu na hata nguvu zetu ziwe ni za kuwatumikia tu - mabwana wakubwa hao - kwani tukiinyenyekea hatua yao hii, bila shaka tutabaki kuwa wenye taabu na mafakiri ambapo hatutaweza kujibidiisha kujua maamrisho ya dini yetu ya Islamu. Na pia hatutamudu kuwazanamna ya kutatua umaskni wetu, bali wao —mabwana wakoloni — waishi tu wao, katika maghorofa na majumba makubwa makubwa wakiponda raha.

Ole wetu! Athari hizi za ubwanyenye pia hupatikana katika vyuo vyetu vya Kiislamu ambapo lau mmoja ataja tu juu ya kuunda serikali halisi ya Kiislamu, sharti atumie takiya* (asidhihirishe imani. yake), la sivyo, nyang'au* wako tayari kumnyakua. Hata kitabu hiki kilipochapishwa mwanzo, kiliwaathiri sana majasusi wa Ubalozi wa Iran katika Iraq, kwani kilifichua wazi waliyoyafanya katika harakati zao zisizo na faida[12].

Naam, kuna baadhi yao wanaochukulia kuvaa nguo za kivita eti huondoa muma na heshima ya mtu! Wasikumbuke kuwa Maimamu wa dini walikuwa wanajeshi, walikuwa majemedari waliojitolea kujihatarishia maisha yao ili kuinyosha dini, waliua watu na watu wao wakauawa.

Amirul Mu'minin[13] (Kiongozi wa Walioamini) Ali bin Abi Talib AS alikuwa hayambanduki mavazi ya kivita na panga. Imam Hasan [14] AS naye vivyo hivyo. Imam Husayn[15] AS, Bwana wa Mashahidi, hali kadhalika. Na lau nafasi ingepatikana, pia Imam Muhammad Baqir AS na waliokuja baada yake wangefanya vivyo hivyo.

Itakuwaje tudai tuna serikali ya Kiislamu hali tunaona ugumu na twahofia kwamba kwa kuingia mapiganoni murua na heshima zetu zitaondoka? Je tutaujenga Uislamu tukisalia tu kuvaa vilemba na majoho makubwa makubwa kwa kuwa hayavunji heshima?

Bila shaka hizi ni fikra tulizoziiga kwa wapotoshi wetu ambao tayari wamefanikiwa katika lengo lao. Na sisi ni juu yetu kufanya bidii na juhudi kadiri ya uwezo wetu kuuthibitishia ulimwengu kuwa Uislamu umetufunza mambo yote yatuwezeshayo kujiundia utawala.

Hii ndiyo hali yetu. Nao wageni wameuimarisha uongo wao nyoyoni mwa watu kwa msaada wa vibaraka wao. Wameziondoa kabisa sheria za Kiislamu za maamuzi na za kisiasa, na badala yake wamepachika kanuni za nchi za Ulaya ili kusudi kuudharaulisha Uislamu tu na kuufutilia mbali.

Hii ni misingi mibaya ya kikoloni. Kwa upande mwingine, kuna udhaifu wa kindani ulio kwa baadhi yetu sisi wenyewe. Baadhi yetu wamejidhalilisha na kujidharaulisha mbele ya wakoloni kwa upande wa maendeleo. Mataifa fulani yanapopiga hatua ya maendeleo kiufundi au kielimu, baadhi yetu hujifanya duni na kuituhumu dini yetu ya Islamu kuwa ndiyo iliyowakosesha kufikia ujuzi huo, na kwamba, hapana uwezekano wa mtu kuufikia utaalamu kama huo ila sharti kwanza aachane na dini na mismgi, yaani mafunzo yake. Na pia azikufuru kabisa sheria zake na itikadi zake ndipo afanikiwe kitaalamu.

Baadhi yetu wenye mawazo hayo, ndio wale waliosikitika walipowaona Wazungu wamekwenda mwezini kwa kudhania dini na kanuni zake ndiyo iliyowapinga kutangulia kwenda. Kwenda mwezini kuna uhusiano gani na kanuni za Kiislamu?

Hebu niwaeleze jamaa zetu hawa na wajue kuwa, mipango au nguvu za vituo vya kijeshi za Kimashariki au za Kimagharibi sizo zilizowafikisha mwezini kamwe wala kwenye maendeleo haya kemkem ya kiangani na mengineyo.

Na waende kwenye sayari na kwingineko wakutakako, lakini daima siku zote wataendelea kubakia nyuma kwa upande wa kudumisha na kuutawanya utengevu kwa watu kote ulimwenguni. Vilevile kuhusu kufunza tabia njema wataendelea kuwa nyuma.

Tukumbuke kwamba, kuleta maendeleo ya kiroho, ni sawa na ni bora zaidi kuliko maendeleo ya mali. Kamwe hawataweza kuyatatua matatizo ya kijamii, kwani kuyatatua na kuuondosha uovu mwingine huhitaji kwanza imani na tabia njema ya kiroho. Ama mali, kudhalilishana na kuvumbua mienendo na safari za angani hakufui dafu. Mali, uwezo wa nguvu za kiatomiki na mengineyo, huwa na sharti ya imani na itikadi. Pia maadili kamili ya Kiislamu ya kumhudumia mtu kwa uadilifu kwa kumwondolea unyonge, taabu na uonevu wa aina zote.

Misingi hii yote, ni sisi tu peke yetu Waislamu tunaomiliki. Na kwa ajili hiyo, haitufalii kule tu kumwona mtu aenda mwezini au afanya hili au lile, tukaitupe dini yetu na sheria zetu zenye ufungamano wa utengevu wa mwanadamu humu duniani na huko akhera.

Baadhi ya fikra za wakoloni walizozitawanya kati yetu, ni maneno yao eti, "Hakuna mfumo wala muundo wa kiserikali katika sheria za Kiislamu. Na kama kuna sheria za kutawala, basi bila shaka sheria hizo hazina faida yoyote, kwani Uislamu unapanga sheria tu,basi."

Uwazi wa maneno hayo na mengine mfano wa hayo, ni sehemu isiyotofauti au isiyoepukana na mipango ya kikoloni ambayo hukusudiwa kuwaepusha Waislamu kufikiria mambo ya kisiasa, kiserikali na ya idara mbalimbali ambayo ndiyo msingi wa imani yetu toka mwanzo.

Sisi tunaitakidi na tuna imani ya utawala halisi na wa halali wa Kiislamu. Tunayo itikadi ya umuhimuwa Mtume Mtukufu SAW kumchagua mshika makamu (khalifa) wake baada ya kuondoka kwake. Na hivyo ndivyo alivyofanya.

Hebu kwanza tuulize. Kuna maana gani Mtume Mtukufu SAW kumchagua mshika makamu wake baada yake? Je, kuna maana ya kubainisha tu hukumu peke yake? Jibu ni "La." Kubainisha tu hukumu na kuziweka wazi hakuhitaji mshika makamu. Kwani ilikuwa rahisi sana kwake Mtume kuwafunza watu na kuyatawanya mafunzo yake kati ya watu na mwisho ayathibiti katika kitabu akiwaachia watu ili wakirejee baadayake.

Baada ya upambanuzi huu, imekuwa wazi kuwa, haja ya khalifa baada ya Mtume Mtukufu SAW ni kupitisha na kuzitekeleza zile hukumu, kwani sheria haziheshimiwi wala hazitiiwi asipokuwepo mwenye kuzipitisha. Pia katika desturi za hapa ulimwenguni, utungaji na uwekaji wa sheria hauna faida yoyote ya kumsalimisha mtu pasipokuwepo utawala wenye mamlaka ya kuzitumia na kuzitekeleza ipasavyo. La sivyo, utakuwa ni utawala dhaifu na mpungufu.

Uislamu unatufunza hivyo; na hivyo basi, mtawala (walii)'" au mwenye amri na mamlaka hutakiwa azitekeleze sheria namna alivyokuwa akifanya Mtume Mtukufu SAW, na lau hangefanya hivyo, tungekuwa na haki ya kudai kuwa, "Hakutekeleza wajibu wake."

Kwa hivyo, uteuzi wa Mtume Mtukufu SAW wa khalifa* baada yake ni kwa ajili ya kuzilinda sheria na kuzitekeleza kwa kuamua usawa na uadilifu baina ya watu, kwani hata yeye mwenyewe katika zama zake hakuwa akitosheka tu na kuweka wazi hukumu na kuufikisha ujumbe, bali alikuwa akizitekeleza sheria hizo. Kwa mfano, alikuwa akitekeleza adhabu kwa wenye hatia, akimkata mkono mwizi kama sheria ilivyo, akimjeledi (akimpiga viboko) mwenye hatia ya kujelediwa, kadhalika akiitekeleza sheria ya kumpiga mawe mwenye jinai ya kumjumiwa. Na kwa jumla alikuwa akiamua kwa uadilifu pasina kumwonea huyu na kumpendelea yule. Vivyo hivyo ndivyo inavyotazamiwa kwa mshika makamu wake. Khalifa si mletaji au mtungaji wa sheria, bali kazi yake ni kuzilinda na kuzitumia kwa kuzitekeleza zile sheria za Mwenyezi Mungu zilizoletwa na Mtume Mtukufu SAW.

Hapa basi, bila shaka umuhimu na haja ya kuunda serikali ni wazi kabisa na ndiyo lengo halisi la imani yetu juu ya utawala [Kiarabu, Wilayah].

Enyi vijana, wadhifa wenu dhidi ya maadui wanaopotoa Uislamu ni kuudhihirisha kwa namna unavyofaa kudhihirishwa. Waambieni watu utawala wa Kiislamu ulivyo. Waambieni, "Sisi tunao mfumo wa kujitawala tukitumia sheria zetu za Kiislamu. Sisi tunayo itikadi juu ya yale ambayo Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume Wake, k.v. kuzileta na kuzitekeleza sheria za Kiislarnu, kumwainisha makamu wake na walii wa Waislamu (yaani msimamizi na mlinzi wa mambo ya Waislamu)."

Kutetea uundaji wa serikali yenye maongozi ya Kiislamu, ndiyo imani halisi. Kwa hivyo, andikeni na mtawanye mafundisho ya Kiislamu juu ya kanuni pasina kuficha kitu, ili watu waelewe faida zake katika jamii. Wakati huohuo mnapofanya hivyo, muwe na imani yenye yakini ya ushindi. Kamilisheni siasa yenu na mwendo wenu katika kutangaza na kuzidisha harakati zenu. Yapasa mjue kwamba mna wadhifa najukumu la kuunda serikali ya Kiislamu.

Wakoloni walijiandaa zaidi ya miaka 300 iliyopita. Wakaanza toka mwanzo wa sifuri na bila shaka walipata waliyoyapata. Kwa hivyo na sisi tuanze mwanzo hasa kwenye sifuri. Msiogope makelele ya watu wachache wenye kasumba ya Kimagharibi na vibaraka wa wakoloni.

Waambieni watu, hasa vijana, ukweli wote wa Kiislamu ili wasione au kuwadhani mashekhe wa hapa Najaf (Iraq) au wa huko Qum (Iran) kuwa wanaitenganisha dini na siasa, na kwamba wao hawafunzi zaidi ya hedhi na nifasi kama walivyosingiziwa, na kwamba hawajui chochote kuhusu siasa.

Wakoloni walieneza katika mafunzo yao ya shuleni na kwingineko ulazimishaji wa kuiweka dini mbali kabisa na siasa, yaani wakavitenganisha. Isitoshe, waliwahadaa watu mpaka wakaamini kutostahili kwa mashekhe kuwa wanasiasa. Na si wao tu, bali pia vibaraka wao na wafuasi wao wasio na dini huyakariri mara kwa mara maneno hayo.

Je, katika zama za MtumeMtukufu SAW dini ilikuwa mbali na siasa? Je, katika zama za makhalifa na zama za Imam Ali bm Abu Talib AS siasa ilitengwa na dini? Au kulikuwa na kikundi cha wanadini tu na kingine cha wanasiasa? La hasha! Hizi ni fikra mpya tu za wakoloni na vibaraka wao. Wamezitawanya kusudi wawagawanye watu wawe mbali na wanavyuoni (mashekhe).

Kwa nini basi? Kwa sababu maulamaa (wanavyuoni wa kidini) wanafanya juhudi kuhakikisha uhuru wa Waislamu umepatikana, kwani wakifaulu kuwatenganisha watu wakawa mbali na maulamaa, tayari watakuwa wamepenya, na hivyo basi kutunyonya, kuyachota mafuta yetu na kutuhukumu.

Jamani nawaambieni, ikiwa mawazo yetu ni kusali tu, na kumwomba Mola wetu na kumtaja pasina mengine, basi wakoloni na maadui zetu hawatatuingilia wala hawatasitushwa. Wewe sali utakavyo, na uadhini kutwa kucha, uwaache wakoloni wachukue mali zako alizokupa Mungu, usiseme kitu ila "Laa hawla walaa quwwata illaa billahi (yaani hapana mwenye uwezo wala nguvu ila yeye tu Allah), na tutakapokufa malipo yetu ni juu ya Mwenyezi Mungu." Hivyo ndivyo watakavyo wakoloni. Ikiwa fikra zetu ni hizo, basi hakuna yatakayotupata kutoka kwao wala tusiwe na wasiwasi wowote.

Kamanda mmoja wa jeshi la Wazungu chini ya utawala wa Mwingereza katika Iraq alipomsikia mwadhini akiadhtni alitaka aelezwe madhara na hatari ya maneno ya mwadhini huyo kwa utawala waWazungu. Akaambiwa, hakuna madhara yoyote. Akasema, "Na aseme yote atakayo maadam hatupingi."

Basi na wewe usipozigusa siasa za kikoloni, ukawa washughulikia tu maamrisho ya hedhi, nifasi, kutawadha, kusali, kufunga, n.k., hakuna mgogoro wowote baina yako na wao. Wewe sali utakavyo, lakini huku nyuma mafuta yako yanachukuliwa, wana haja gani na sala zako? Wao wanataka madini yako. Isitoshe, huja kukuuzia mali walizozichukua kwako katika soko lako mwenyewe. Sababu kama hizi ndizo zinazotufanya tuone serikali za vibaraka wao zinaendelea miaka kadha wa kadha bila kuleta maendeleo ya kimsingi katika nchi, bali hudanganywa wakadanganyika kwa viwanda vidogo vidogo tu. Lengo lao wanataka tusizindukane kufikia daraja la mwanadamu kamili aliyeukusanya uanadamu na utu.

Naam, kwasababu wao huogopa binadamu. Pindi wafikapo mahali palipo na wanadamu majuha, huwatisha kwanza. Kwa nini? Kwa sababu mwanadamu aliyeamka, na mstaarabu atatupilia mbali rai na mawazo yao na hatimaye atatingisha kabisa misingi ya uonevu, hiana na kutumiliwa. Sababu kama hii huwafanya wanapomkuta mtu aliyeamka mahali popote pale, hufanya njama za kumwua au kumpachika mahala au kumkimbiza kwa kisingizio eti shekhe fulani ajiingiza katika siasa.

Je, Mtume Muhammad SAW hakuwa mwanasiasa? Je, kuwa mwanasiasa ni aibu? Ala, mbona hivi! Lakini si ajabu, kwani hayo ni maneno tu ya wakoloni na vibaraka wao ya kuwaweka watu hasa maulamaa mbali na siasa na mambo ya kijamii, na kuwazuia kuung'oa utawala uliojaa maonevu, jeuri na upendeleo ili waweze kujitengenezea maslahi yao na waendelee na siasa yao ya kupinga Uislamu na kujitawala kwa wananchi. Wanafanya watakavyo ili mradi asiwepo anayewapinga.

Hajaya KuundaSerikali ya Kiislamu

LAZIMA KUWEPO TAASISI YA UTEKELEZAJI

Kama tulivyobainisha hapo nyuma kidogo, sheria tuzilizonakiliwa hazitoshi kuzistawisha jamii na kuzitengeza, bali ni lazima zipitishwe na zitekelezwe.

Mwenyezi Mungu, mbali na kuzileta sheria, alikuwa pia alimleta Mtume atakayezitekeleza. Mtume Mtukufu SAW aliyekuwa kiongozi na mtawala wa mambo yote, hakuwa akitosheka na kuwafahamisha watu ujumbe wake na sheria mbalimbali, bali alikuwa akitimiza matekelezo yake kwa kuwakata mikono wezi, kuwapiga viboko wenye makosa ya jinai, na akiwarujumu* wazinifu. Kufanya kwake hayo yote kulikuwa ni kusimamisha nidhamu ya Kiislamu na kuasisi serikali ya Kiislamu. Baada yake, mshika makamu wake aliendelea na wadhifa huo huo. Kwani Mtume hakumteua khalifa baada yake ili abainishe itikadi na sheria za Kiislamu, bali jukumu lake lilikuwa kuzitekeleza pia.

Hii ndiyo imani ya Waislamu, na ndiyo haja na dharura kubwa ya kuwepo mwangalizi na mpitishi wa sheria za Mwenyezi Mungu katika watu ifi kuyadhamini maisha yao yatengemae humu duniani na huko akhera.

Kwa hakika utengevu wa jamii na mipango inayoweza kuwaletea watu matunda ya sheria adilifu humu ulimwenguni ni sharti kuwepo mpitishi na mtekelezi wa sheria. Ama sheria tu pasina hivyo hazileti natija yoyote. Ndiyo maana utaona katika nchi zote duniani, licha ya kuwepo kwa mabaraza ya utungaji wa sheria, pia kuna mabaraza ya utendaji na utekelezaji wa sheria ambayo hushughulika na kupitisha kanuni za mahakama n.k. kama inavyotakikana. Ilivyokuwa katika dini ya Kiislamu kuna sheria na kanuni , basi pia amewekwa mtu mwenye uwezo na mamlaka ya kupitisha na kutekeleza sheria. Walii au mtawala ndiye mwenye mamlaka ya kupitisha sheria za Kiislamu[16]

MWENENDO WA MTUME MTUKUFU SAW

Tutauzingatia umuhimu wa serikali ya Kiislamu lau tutastafidi mwenendo wa Mtume Mtukufu SAW katika mambohaya mawili.

Kwanza, yeye mwenyewe aliunda serikali. Historia yatuju

lisha kwamba, yeye aliziimarisha huduma za jamii, na akawatuma maliwali sehemu mbalimbali. Isitoshe, alikuwa akikaa kwenye baraza na kuwaamua walioteta au waliohitalifiana. Aliwatuma wajumbe sehemu mbalimbali ili nao wafanye vivyo hivyo. Aliwatuma mabalozi nje ya mipaka ya dola lake kwa wakuu wa makabila na kwa wafalme. Alikuwa akiwekeana mikataba na akiitimiza. Na alikuwa akiongoza mapigano dhidi ya wachokozi wake. Na kwa jumla, alikuwa mtekelezi aliye mstari wa mbele kabisa wa hukumu za Kiislamu.

Pili, alimweka khalifa (hakimu) atakayetawala mambo baada yake ili apitishe hukumu baada yake. Uteuzi huu, bila shaka ni dalili ya kutosha ya umuhimu wa kuiendeleza serikali ya Kiislamu, na alifanya hivyo kwa amri ya MwenyeziMungu.

UMUHIMU WA KUENDELEA KUZIPITISHA HUKUMU

Ni wazi tena dhahiri kwamba, utekelezi wa sheria haukuwa mahsusi tu zama za Mtume Mtukufu SAW, bali ni lazima kuuendeleza hadi siku ya Kiyama, kwani Uislamu haukomeki na zama au mahali bali ni wa milele. Kwa hivyo, haifai kiziachilia sheria za Kiislamu namipaka yake au kutotunza mafunzo yake au kuzisahau hukumu za visasi au kuisimamisha michango inayotokana na kodi ya mapato au kuacha kuutetea umma wa Kiislamu na ardhi yao.

Imani ya kuwa Uislamu hukumu zake zina kikomo au zinahusu mahali fulani tu, ni kinyume na misingi halisi ya Kiislamu.

Imefahamika wazi umuhimu wa kuendelea na utekelezi wa sheria baada ya Mtume Mtukufu SAW. Kwa ajili hiyo ni lazima pawepo serikali yenye usawa kwa maisha ya jamii inayoweza kudumisha tabia njema, la sivyo, ghasia na misukosuko vitatawala.

Sheria na akili zinathibitisha kuwa,yaliyohitajika zama za Mtume Mtukufu SAW na zama za Imam Ali bin Abi Talib AS pia yanahitajika zama zetu hizi. Tangu kipindi kifupi cha kutoonekana Imam Mahdi AS zaidi ya miaka elfu moja imepita na huenda maelfu ya miaka mingine ikapita. Je, ni halali katika muda huo kuzisimamisha hukumu za Kiislamu zisifuatwe tena, watu wafanye watakavyo eti kwa kuwa mudiri wa hukumu za Kiislamu ameghibu (haonekani)? Je, tukifanya hivyo si tutakuwa tunasababisha rabsha na zahama? Je, yuko anayethubutu kudai kuwa miaka yote 23 aliyoshughulika kutekeleza sheria ilipotea bure? Je, Mwenyezi Mungu ameweka muda tu wa miaka 200 zitekelezwe sheria Zake, na baada ya Ughaibu Mdogo[17] hukumu zote za Kiislamu zimesahaulika?

Bila shaka rai yoyote ya aina hii ni mbaya zaidi hata kuliko kuamini kuwa Uislamu ulifutwa. Wala hapana yeyote amwaminiye Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho awezaye kusema kwamba, si lazima kuitetea au kuipigania ngome ya nchi, au kusema kwamba, inafaa kukataa kutoa zaka* au khums*, au akasema kuwa, hukumu za adhabu za Kiislamu, visasi, na fidia ziondolewe. Lau yupo asemaye hivyo au kuwaza kutostahili kuundwa serikali yenye maongozi ya Kiislamu, bila shaka lengo lake ni kutoukubali Uislamu kabisa.

ZAMA ZA AMIRUL MU'MININ ALI BIN ABI TALIB AS

Baada ya kufariki kwa Mtume Mtukufu SAW, hakukuwepo Mwislamu yeyote asiyetosheka, yaani aliye na shaka juu ya umuhimu wa kuwepo serikali yenye maongozi ya Kiislamu baada ya Mtume, bali wote waliwafikiana. ila tu tofauti zao ni juu ya anayefaa kuiongoza. Kwa hivyo, baada ya Mtume Mtukufu SAW, katika zama za makhalifa na zama za Sayyidna Ali AS kulikuwa na serikali za Kiislamu zenye wizara na idara mbalimbali zilizokuwa zikifanya kazi za kiserikali.

UKWELI WA SHERIA ZA KIISLAMU

Sheria za Kiislamu zajieleza wazi bayana kuweza kwake kuiunda serikali iliyo na idara zenye uchumi na matumizi mema mbali na maendeleo kemkem.

Kwanza, sheria zenyewe za Kiislamu zimeyaweka wazi mambo yote yanayohusu jamii. Hii ikiwa ni pamoja na mipango ya kurekebisha haja za mtu binafsi, uhusiano na ujirani mwema, uhusiano wa watoto na ukoo wao, utunzaji au ulinzi kwa wananchi, na pia mambo yote yanayohusu unyumba. Kisha zimeeleza vipi namna ya kujihami, uhusiano na mataifa ya kigeni, sheria za mahakama, biashara, sanaa, ukulima, ndoa, ulezi wa watoto, heshima ya watoto kwa wazee wao na namna ya kuishi mke na mumewe. Kwa mfano, katika Uislamu kuna sheria zinazotakiwa kutekelezwa kabla ya kufunga ndoa na kutunga mimba, ndoa ifungwe vipi, chakula cha bwana na bibi arusi wakati wa kufunga ndoa au wakati wa kutunga mimba kiwe kipi, wadhifa wa wazee katika kipindi cha kumnyonyesha mtoto maziwa na jinsi ya kumlea mtoto, silika baina ya mume, mke na watoto ziweje. Katika mambo haya yote, Islamu imeweka sheria na maamrisho ili kumfanya mwanadamu kamili na mwungwana.

Uislamu umeyapambanua haya na mengineyo kwa manufaa ya jamii ili kuleta uhusiano kamili ulio bora wa kisiasa na wa kiuchumi kati ya walimwengu. Sheria zote hizi zimo katika Qur'ani Tukufu na Sunna* za Mtume Mtukufu SAW.

Katika kitabu cha hadithi cha al-Kafl kuna hadithi moja iliyopokewa kutoka kwa Imam AS akisema, "Maelezo ya mambo yote yanayohitajiwa na watu yamo katika Kitabu na Sunna." Kitabu ni Qur'ani Tukufu ambacho kimefafanua mambo yote na vitu vyote. Kufuatana na hadithi hiyo, Imam AS ameapa kwamba yote yale wanayohitajia watu yamo katika Kitabu (Qur'am) na Sunna za Mtume Mtukufu SAW. Jambo hili halitiliwi shaka.

Pili, tunapouchunguza kwa makini uwazi wa sheria hizi za Kiislamu, twaona kwamba hapana namna ya kuzitekeleza ila kwa sharti pawepo serikali yenye uwezo na muundo mkubwa. Nitawapa mifano michache nikiwaomba ndugu zangu wanaojua nao waongezee iliyobaki.

1- SHERIA ZA MALI

Njia zote zilizowekwa na Uislamu kuingizia mapato ya kifedha, hazikupangwa ili kuwaondolea dhiki mafakiri au kuwaongezea mapato wenye kujiweza, bali ziliwekwa ili kuliimarisha dola kubwa la Kiislamu. Kwa mfano, khums ikitolewa itaingiza kiasi kikubwa mno kwenye hazina (bajeti) ya taifa. Na khums yenyewe kulingana na madhehebu yetu, hutolewa kutokana na kazi ziletazo faida mkiwemo biashara, madini, nafaka na hata muuza mboga naye akipata faida zaidi ya matumizi yake ya mwaka atatoa khums.

Nahodha wa meli na mchimbua migodi na madini pia hutoa khums. Wote hao humkabidhi mtawala wa Kiislamu ili aziingize katika hazina ya taifa (Baytul-Maal).

Kwa hakika uwazi ni kwamba, pato hilo lote ni la kuendeleza mambo ya serikali ya Kiislamu ili kuondoa vipengele vyote yinavyohitajia fedha likiongezewa pato linalotokana na zaka, jizya* na kharaj*, na wala si kwa lengo la kupewa masharifu maskini au mashekhe tu.

Tangu lini masharifu (masayyidi) wakahitajia fedha kama hizo? Khums inayotoka katika soko moja tu la Baghdad (Iraq), inatosheleza haja zao wote na haja za maskini wote na vyuo vya kidini, mbali na soko la Tehran (Iran), Istanbul (Turkey), Cairo (Misri) na kwingineko. Lau mapato hayo ya khums, zaka na malipo mengine yangetolewa yangekuwa bajeti kubwa inayoweza kuiendesha serikali kwa kujengesha vituo vya matibabu, majengo, ulinzi na maendeleo mengine.

Ama mipango iliyowekwa na Uislamu juu ya pato hilo, inazilinda mali hizi zote na kuzisalimisha na maonevu ya upendeleo na dhuluma, kwani kiongozi, mawaziri na wanachama au maafisa wa serikali hawana uwezo wowote juu yamali hizo zaidi ya watu wengine.

rudi nyuma Yaliyomo endelea