Yaliyomo endelea

Dibaji[1]

Imam Ruhullah al-Musawy al-Khomeini — Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Tumaini la Wanyonge Duniani — alizaliwa katika mwaka 1900 katika ukoo wa wasalihina* mjini Khomein, kusini-magharibi ya Tehran (Iran). Babu yake na baba yake wote wawili walikuwa maulamaa*. Baba yake, Ayatullah Mustafa, aliuawa na magaidi miezi mitano kabla ya kuzaliwa Ruhullah; hivyo, akalelewa na mama yake na shangazi yake. Alipokuwa na umri wa miaka 16, mama na shangazi yake walifariki dunia; na kaka yake, Sayyid Murtaza (mashuhuri kwa jina la Ayatullah* Pasandide) ndiye akawa na jukumu la kusimamia masomo yake. Ayatullah Pasandide alimfundisha Khomeini lugha ya Kiarabu, mantiki* na masomo mengine ya kimsingi.

Alipokuwa na umri wa miaka 18, Khomeini akiwa kijana, alipelekwa chuoni karibu na mji wa Arak. Mwalimu wake alikuwa Ayatullah Shaykh Abdul Karim Hairi ambaye alikuwa mwanafunzi wa maulamaa wakubwa wa Kishia wa vyuo ya Iraq, k.v. Ayatullah Mirza Hasan Shirazi. Kupata mafunzo kutoka kwa Shaykh Hairi kulimfanya Khomemi kuwa ni aalimu mkubwa na mwanaharakati.

Mwaka uliofuatia, Hairi alipokea mwaliko kutoka kwa wakazi na maulamaa wa Qum kumtaka ahamie huko. Mji wa Qum ulikuwa ni makao ya elimu na ziara*. Shaykh Hairi alipofika mjini Qum akaanza kuratibu upya mpango wa hawza* ya Qum. Hii ilikuwa ni hatua ya kwanza ya maendeleo kati ya hatua mbalimbali zilizo uinua mji wa Qum kufikia kuwa ni mji mkuu wa maarifa ya Kiislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hatua ya mwisho na muhimu ya maendeleo ilikuwa ni mapambano ya taifa zima dhidi ya utawala wa kifalme wa Pahlavi ambayo yalianzishwa na Imam Khomeini (Khumayni) katika mwaka 1962 mjini Qum.

Ishara zenye kuonyesha kwamba Imam Khomeini atakuwa na wadhifa muhimu katika siku za mbele zilikuwa zimeshaanza kuonekana katika miaka hiyo. Akawa mwanafunzi mashuhuri miongoni mwa wanafunzi wa Shaykh Hairi kwa kuwashinda katika fani mbalimbali hasa katika maadili*, falsafa* na irfani*. Alipokuwa na miaka 27, aliandika kwa Kiarabu kitabu kiitwacho Misbahul Hidaya katika maudhui* ya maadili, falsafa na irfani. Kitabu hiki kilisifiwa sana na walimu wake. Wengi wa masahibu muhimu wa Imam Khomeini ambao walijulikana sana katika kipindi cha harakati za Mapinduzi — k.v. Ayatullah Muntadhari[2]», wana-kumbuka kwamba wao walivutiwa sana na Imam Khomeini kutokana na ustadi wake katika elimu za maadili na falsafa na kwamba mihadhara* yake aliyokuwa akitoa kila juma mara mbili mjini Qum ilikuwa ikihudhuriwa na mamia ya watu.

Tukiangalia umaarufu wa sasa uliompatia Imam Khomeini kama ni kiongozi mwanamapinduzi aliyepata mafanikio ya kipekee katika uwanja wa kisiasa, tusistaajabu kuona kwamba awali alikuwa maarufu kama ni mwandishi na mwalimu anayehusika na mambo ya kiibada na kiirfani (kiwalii). Walakini, kushughulika kwa Imam Khomeini katika mambo ya kiroho na kiirfani hakukuwa na maana ya kujitenga na mambo ya kijamii au kutoingilia siasa, bali hayo mambo ya kiroho na kiirfani yalikuwa ndiyo msingi wa kujengea nguvu zenye kuleta taathira katika nyanja za kijamii na kisiasa.

Maisha ya Imam Khomeini yanabainisha kwamba Mapinduzi yanayotokana na Uislamu lazima yawe na msingi wa kimaadili na kiroho. Madarasa aliyokuwa akifundisha mjini Qum katika mwaka 1930 inathibitisha jambo hili. Maudhui ya kimaadili na kidini yalikuwa yakijadiliwa pamoja na matatizo ya kila siku, na wasikilizaji walikuwa wakiwaidhiwa* kuyatatua matatizo yao ya kijamii, kisiasa, kiuchumi n.k. kama ni wajibu wa kidini kwao.

Miaka ya awali ya harakati za Imam Khomeini mjini Qum ilianza wakati wa kuanzishwa kwa utawala wa kifalme wa Reza Khan Pahlavi. Reza Khan aliugeuza ufalme wa Kiirani kuwa ni wa kidikteta wa kisasa ambao shabaha yake kuu ilikuwa ni kuuangamiza Uislamu kutokuwa na nguvu za kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Imam Khomeini mwenyewe alikuwa akishuhudia mjini Qum jitihada zilizokuwa zikifanywa katika kutekeleza shabaha hiyo, isitoshe, habari kutoka miji mingine kama Mash'had, Isfahan na Tabriz zilikuwa zikimfikia. Yale aliyoyaona au kuyasikia katika miaka hiyo yalimwathiri sana, na maonevu yaliyokuwa yakifanywa na Mohammed Reza (Shah wa pili na wa mwisho katika ufalme wa Pahlavi) dhidi ya taasisi ya Kiislamu yalikuwa kwake kama mfululizo wa mwenendo mmoja wa maonevu ya baba yaliyorithiwa na mwanawe.

Kauli* ya kwanza iliyotangazwa ya Imam Khomeini yenye maneno ya kisiasa ilichapishwa katika mwaka 1941 katika kitabu kiitwacho Kashful Asrar. Kitabu chenyewe ni kikubwa kilichoandikwa kukikosoa kitabu kilichoandikwa dhidi ya dini. Kitabu hicho kina mafungu mengi ya maneno ya kisiasa na yenye kupinga vikali utawala wa Pahlavi.

Ayatullah Hairi aliaga dunia mwaka 1937, na chuo cha kidini kikawa kinasimamiwa kwa muda najopo* la wasaidizi wake watatu waitwao: Ayatullah Sadr, Ayatullah Hujjat na Ayatullah Khunsari. Kisha Ayatullah Burujardi akachaguliwa kuwa kiongozi kushika wadhifa wa Shaykh Hairi. Imam Khomeini alikuwa akimfanyia kampeni Ayatullah Burujardi kupewa wadhifa wa uongozi akimtarajia kwamba atatumia fursa na wadhifa wake mkubwa wa kidini katika kupambana dhidi ya utawala wa Pahlavi. Alishirikiana sana na Ayatullah Burujardi mpaka alipofariki katika mwaka 1962. Ingawa historia inamhesabu Ayatullah Burujardi kwamba alikuwa kiongozi mcha Mungu sana na mwendeshaji hodari lakini kutokana na sababu kadhaa hakuwa na harakati za kisiasa.

Baada ya kufariki Ayatullah Burujardi hakutokea hata mtu mmoja kushika cheo chake. Khomeini alisita kuruhusu jina lake lifanyiwe ' kampeni, lakini mwishowe akaitikia maombi ya masahibu zake kwamba fatwa na masiala yake ya kidini yakusanywe na kupigwa chapa. Hii ikawa na maana kwamba alikuwa tayari kushika hatamu za uongozi na mamlaka ya kidini. Ndipo hapo umashuhuri wa Imam Khomeini ukaenea mjini Qum na nchini kote Iran. Jambo lililokuwa muhimu zaidi ni kule kuwa tayari kuukabili utawala wa Shah katika wakati ambao watu wachache tu walithubutu kufanya hivyo. Kwa mfano, yeye alikuwa marja taklidi* wa pekee wa Qum kuweza kuwaunga mkono hadharani wanafunzi wa hawza ambao walikuwa wakifanya kampeni ya kuzuia maduka ya ulevi yasifunguliwe mjini Qum.

Baadaye akawa anashughulikia mambo yaliyo muhimu zaidi. Hatua ya kwanza aliichukua katika mwezi wa Oktoba 1962 wakati Shah alipotangaza sheria ya kuondoa masharti ya kuwa Mwislamu na mwanamume katika kugombea uchaguzi wa mabaraza ya mikoa. Imam Khomeini alijiunga pamoja na maulamaa wengine nchini kote kupinga vikali hatua hiyo; na hatimaye Shah akashindwa.

Hatua yenyewe haikuwa muhimu sana kwa sababu uchaguzi wa mabaraza ya mikoa ulikuwa haufanyiki kwa njia ya halali. Lakini kampeni iliyofanywa dhidi ya hatua hiyo ilikuwa ni chanzo cha harakati kubwa zaidi dhidi ya utawala, na vilevile fursa nzuri ya kuwaunganisha viongozi wa kidini katika kujiandaa kwa ajili ya shabaha muhimu zaidi kwa ajili ya siku ziyazo.

Hatua ya pili ilichukuliwa katika mwaka 1963 wakati Shah alipoanza kutangaza maazimio mapya kwa ajili ya kugeuza hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya Iran. Maazi mio hayo yalijulikana kama "Mapimduzi Meupe".

Kura ya rai (referendum) ilifanywa kwa ulaghai mnamo Januari 26, 1963 ili kuunga mkono maazimio hayo. Hata hivyo, wananchi wengi wa Iran waling'amua barabara hatua hiyo kuwa ni hila ya Marekani ya kutaka kumpatia madaraka na utajiri zaidi Shah. Hii pia ilikuwa ni mbinu ya Marekani ya kuitawala zaidi Iran, kama inavyofahamika kwamba CIA (Shirika la Upelelezi la Marekani) ndilo lililoiangusha serikali ya Waziri Mkuu Muhammad Musaddiq katika mwezi wa Agosti 1953. Imam alilaani vikali hayo "mapinduzi" ya kilaghai na akafichua madhumuni hasa ya maazimio hayo. Hotuba alizozitoa katika Madrasa Fayziya[3] mjini Qum zilileta taathira nzuri nchini kote.

Ili kuukomesha upinzani huo, utawala wa Shah ulipeleka askari wa miamvuli kushambulia Madrasa Fayziya tarehe 22 Machi 1963. Wanafunzi wengi waliuawa na madrasa yenyewe ikaharibiwa. Lakini tukio hilo si tu halikumtisha Imam Khomeini bali likawa ni chanzo cha kipindi kipya cha kupambana kikakamavu dhidi ya makosa na ufisadi wa utawala, na vilevile likawa ni chanzo cha kupambana dhidi ya utawala wenyewe. Mashambulizi hayo yakawa ni mfano wazi wa kuonyesha uhasama wa utawala huo dhidi ya Uislamu na taasisi za Kiislamu, na kuonyesha mwendo wake wa kikatili, kishenzi na kidhalimu.

Imam Khomeini aliendelea kuushutumu utawala wa Shah kati ya miezi ya Machi na Mei mwaka 1963. Aliushambulia sana utawala wa Shah hasa kutokana na udhalimu wake, unyenyekevu wake mbele ya Marekani, na ushirikiano wake na Israel. Mkabala huo ulifikia kilele kipya kabisa mwezi wa Juni ulioandamana na mwezi wa Muharram. Mwezi wa Kiislamu wa Muharram huadhimishwa kila mwaka kukumbuka ushahidi wa Imam Husayn AS, mjukuu wake Mtume Muhammad SAW,* ambaye alipambana dhidi ya udhalimu na upotevu wa Yazid. Mwezi huu huadhimishwa ili kuhuisha mfano huo kwa kupambana dhidi ya madhalimu wa kila zama. Siku ya Ashura* (tarehe 10 Muharram), Imam Khomeini alitoa hotuba ya historia mjini Qum na akazidi kuushutumu utawala wa Shah na akamwonya Shah asitende jambo ambalo litawafanya watu wamlazimishe ahame nchini na wafurahiye kuondoka kwake*[4] Siku mbili baadaye alikamatwa na kupelekwa Tehran.

Kukamatwa kwa Imam Khomeini kulizidisha upinzani wa umma na mapambano yao makubwa yakautingisha utawala wa Shah. Katika miji ya Qum, Tehran, Shiraz. Mash'had, Kashan na miji mingineyo, waandamanaji wasiokuwa na silaha walikabiliana na askari wa Shah waliofunzwa na Marekani na kushika silaha zao. Askari hao walipewa amri ya kufyatua risasi na kuua papo hapo, na matokeo yake watu wasiopungua 15,000 waliuawa katika muda wa siku chache. Tukio hilo ambalo lilitokea tarehe 15 Khordad 1342 (kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani sawasawa na tarehe 5 Juni 1963), likafungua ukurasa mpya wa historia ya Iran. Tukio hilo lilimwainisha Imam Khomeini kama ni kiongozi wa taifa na mwenye kuwakilisha matakwa ya umma. Imam Khomeini alianzisha mapambano dhidi ya Shah na vibaraka vyake kufuatana na msingi wa itikadi ya Kiislamu, na akawaelekeza watu kuendeleza harakati zao chini ya uongozi wa maulamaa na mashekhe badala ya kusimamiwa na vyama visivyokuwa vya kidini ambavyo vilipoteza imani ya watu baada ya kupinduliwa Musaddiq. Kwa hivyo, mzinduko wa Khordad 15 ukawa ni msingi ulioleta Mapinduzi ya Kiislamu.

Ingawa upinzani ulikandamizwa lakini wananchi na maulamaa walikataa kuvumilia kufungwa kwa Imam Khomeini. Machafuko yalienea nchini kote, na maulamaa wengi wakakusanyika mjini Tehran kusisitiza kuachwa huru kwa Imam Khomeini. Hatimaye, Imam Khomeini aliachwa huru tarehe 6 Aprili 1964, na wakati huohuo magazeti yanayodhibitiwa na serikali yalitangaza kwamba ameachwa huru kwa sharti kwamba hatojiingiza katika mambo ya kisiasa. Imam alikanusha haraka habari hiyo, na akaendelea kuupinga vikali utawala.

Ushahidi mwingine kuthibitisha utiifu wa Shah kwa Marekani ulionekana katika mwezi wa Oktoba 1964, wakati sheria ilipopasishwa katika bunge yenye kuwapa haki watumishi wa Kimarekani wasishtakiwe kwa kosa lolote watakalo lifanya katika ardhi ya Iran. Imam aliposikia kwamba Majlis* imepasisha sheria hiyo, hakupata usingizi usiku huo. Siku ya pili yake, yaani tarehe 27 Oktoba, aliishambulia hadharani sheria hiyo kwamba inahatarisha utawala wa Iran .na uhuru wake. Mpaka wakati huo ikadhihirika kwa Shah na mabwana zake wa kigeni kwamba Imam Khomeini hawezi kunyama zishwa kimya, na ikaamuliwa abaidishwe* eti kwa kutaraji kupunguza nguvu na taathira zake. Hivyo, tarehe 4 Novemba 1964, Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni nchini Uturuki akifuatwa na SAVAK*.

Baada ya kuishi kwa muda mfupi mjini Ankara, ilimbidi Imam Khomeini akae Busra mji ulio magharibi mwa Uturuki. Utawala wa Shah ulikuwa ukishikiliwa sana kumruhusu Imam Khomeini aondoshwe Uturuki na apelekwe Najaf, mahali panapofaa zaidi kukaa uhamishoni na mojawapo katika miji ya Kishia yenye haram"' nchini Iraq. Idhini ilitolewa katika mwezi wa Oktoba 1965, na Imam Khomeini akahamia mjini Najaf ambapo ukawa ni makazi yake kwa muda wa miaka kumi na mitatu.

Utawala wa Shah ulikubali kuchukua hatua hiyo; kwanza, kwa kutaka kuepukana na hasira za watu; pili, kwa kudhani kwamba lau Imam Khomeini angeishi Najaf asingejulikana kwa sababu ya kuwepo maulamaa wengi wakubwa hapo. Dhana hiyo ikathibitika kuwa si sawa, na Imam Khomeini akapata heshima kubwa na akawa na haiba* kubwa mjini Najaf. Isitoshe, alizidi kupata wafuasi na kujulikana zaidi katika Iran. Mara kwa mara alikuwa akitoa matangazo kuhusu mambo yanayopita Iran, matangazo ambayo yalikuwa yakisambazwa kwa siri nchini kote. Vivyo hivyo alikuwa akitoa risala kwa Waislamu wote duniani ambazo zilikuwa zikigawanywa kila mwaka katika Makka katika msimu wa Hija. Mjini Najaf kwenyewe, alikuwa akiwapokea Waislamu wahashamu* na watu waliokuwa wakizuru haram na maziara ya Iraq ambao walikuwa wakitoka miji mbalimbali ya Iran na kwingineko.

Jina na shakhsiya* ya Imam Khomeini pamoja na harakati aliyoipa sura havikusahauliwa katika Iran. Mfano wake uliwavutia maulamaa wengi na vikundi vingi, mfano ambao uliendelea kuimarisha misingi aliyoiweka katika miaka ya 1963 na 1964 na ukasababisha harakati za Kiislamu zisizo kuwa na mfano zipanuke na zikue.

Kwa hivyo, ikawa nijambo la kawaida kwa Imam Khomeini kujitokeza haraka kuwa kama kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ingawa kimwili hakuwa katika Iran lakini alikuwa katika nyoyo za watu wake na alikuwa akisema kwa mujibu wa sauti yao, jambo ambalo lilikosekana miongoni mwa wanasiasa ambao hawakuhamishwa wala hawakufungwa.

Tarehe 23 Novemba 1977, mwana mkubwa wa Imam Khomeini, Ayatullah Haji Mustafa, aliuawa ghafla na SAVAK katika Najaf. Imam Khomeini alivumilia msiba huo lakini wananchi wa Iran walishikwa hasira. Ufisadi ulioenea katika jamii, utovu wa usawa katika uchumi na ukandamizaji wa kisiasa ulizidi kuwafanya watu wote wa Iran waichukie serikali. Na utawala wa Shah ulipokusudia kuchukua hatua nyingine dhidi ya Imam Khomeini, hasira za umma zikazidi na kugeuka kuwa mapambano, na mapambano yakamea Mapinduzi.

Wiki moja baada ya Rais Jimmy Carter wa Marekani kuzuru Tehran na kumsifu Shah kama ni mwanasiasa mwenye busara anayependwa na taifa lake[5] — yaani tarehe 8 Januari 1978 — magazeti yaliyokuwa yakidhibitiwa na serikali yalichapisha makala yaliyotolewa na Wizara ya Mahakama ambayo yalimshutumu Imam Khomeini kama ni kibaraka wa nchi za kigeni. Wananchi walighadhibika haraka. Siku ya pili yake, mjini Qum, kulifanyika maandamano ambayo yalikabiliwa vikali na kusababisha vifo vingi. Hayo yalifuatiwa na mfululizo wa maandamano mengine yaliyoenea nchi nzima ambayo hayakulibakisha hata eneo moja bila ya kupatwa na hasama ya kimapinduzi. Tangu mwezi wa Aprili mpaka Septemba 1978, Imam Khomeini alikuwa akitoa matangazo, risala na miongozo akiwaunga mkono watu kwa sababu ya ukakamavu na ushujaa wao, na akawahimiza waendelee na mapambano yao hadi lipatikane lengo lao la mwisho — nalo ni kuupindua utawala wa kifalme na kuanzisha Jamhuri ya Kiislamu.

Imam Khomeini alijulikana tangu awali kama ni kiini cha mapambano ya kimapinduzi. Jina lake lilikuwa daima likitungiwa mashairi na kuimbwa katika maandamano. Picha zake zikawa kama ni bendera ya Mapinduzi. Na moja katika madai ya waandamanaji lilikuwa ni kutaka Imam arejee uharnishoni na asimamie kuundwa kwa utawala wa Kiislamu. Utawala wa Shah ulifanya kosa jingine kwa kuitaka serikali ya Baath ya Iraq katika mwezi wa Septemba 1978 kumfukuza Imam Khomeini kutoka Iraq ikidhania na kutaraji kwamba Imam atakosa kituo cha kuendeshea harakati zake, na Mapinduzi yatakosa kiongozi wake. Imam Khomeini hakuwa na uhusiano mzuri pamoja na serikali zote zilizotawala Iraq tangu kufika kwake huko katika mwaka 1965, hivyo, akawaarifu watawala wa Iraq kwamba angependelea kuhama Iraq na kwenda katika nchi ambayo haitofuata amri ya Shah. Ilisemekana kwamba Imam angehamia Syria au Algeria, lakini baadaye Imam akasema kwamba hakuna nchi ya Kiislamu ambayo ilimdhaminia kwamba ingempa uhuru kamili wa kuendelea na harakati zake. Kwa hivyo, Imam alikwenda Ufaransa katika mwezi wa Oktoba 1978 na akaishi katika Neauphlele Chateau, kitongoji cha Paris.

Kuhamia kwake Ufaransa kulileta faida. Mawasiliano kati ya Ufaransa na Iran yakawa rahisi zaidi kuliko yalivyokuwa katika Iraq. Matangazo na miongozo aliyokuwa akitoa ilikuwa ikisomwa moja kwa moja kwenye simu ya mdomo inayopigwa Tehran, na jiji la Tehran likawa ni makao ya kueneza matangazo na miongozo hiyo katika mikoa yote. Mkururo wa Mairani kutoka Ulaya na Marekani na hata Iran kwenyewe walikuwa wakija kumzuru Imam na kushauriana naye. Waandishi wa habari kutoka dunia nzima walikuwa wakimzuru katika nyumba yake ya kawaida, na maneno yake yakaanza kuenea ulimwengu mzima.

Mwezi wa Muharram wa mwaka 1399 Hijiria uliangukia katika mwezi wa Desemba wa mwaka 1978 wa Kikristo. Katika mwezi huo kulifanyika maandamano mengi mjini Tehran na katika miji mingine ya Iran yakitaka kuondoshwa kwa ufalme na kuanzishwa kwa Jamhuri ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini. Ingawa Shah alitumia kila aina ya unyama na ukatili, k.v. kuwaua maelfu ya waandamanaji wasiokuwa na silaha, kuwaadhibu na kuwatesa wafungwa wa kisiasa na hata kuwaua na kuwajeruhi waandamanaji waliolazwa hospitalini, lakini hata hivyo utawala wa kifisadi na kikatili wa Shah ulikuwa unakaribia mwisho wake, juu ya kuwa Marekani na nchi zingine za kigeni zilikuwa zikimsaidia na kumwunga mkono Shah. Mabwana zake waliamua kwamba itakuwa jambo la busara kwake kuondoka Iran; na maandalizi yalipofanywa kumweka Shah pur Bakhtiar[6] kuendesha nchi, ndipo Shah akaondoka Iran kwa mara yake ya mwisho, tarehe 16 Januari 1979. Shangwe na furaha zilizofuatia baada ya kuondoka kwake zilitimiza utabiri wa Imam Khomeini alioutoa miaka 16 iliyopita.

Mara baada ya Shah kuondoka tu, Imam Khomeini akajitayarisha kurejea nyumbani. Aliporejea Iran tarehe mosi Februari 1979, alipokelewa na umati mkubwa sana wa watu ambao haukuonekana katika historia. Kuwepo kwake tena katika Iran kulikuwa na maana ya kukoma kwa serikali ya Bakhtiar. Utawala wa kifisadi, kibaraka na kifalme wa Shah ulianguka kwa fedheha tarehe 10 na 11 Februari 1979 na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikazaliwa.

Tangu kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini ameendelea kushika wadhifa wake kwa busara na hekima na kuliongoza taifa kufikia shabaha yake. Kwa mujibu wa vifungu 107 - 112 vya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran[7], madaraka makubwa ya nchi yamo katika wadhifa wa Utawala wa Faqihi[8] (Kifarsi, Wilayate Faqih). Cheo hiki kinashikiliwa na kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye hivi sasa ni Imam Khomeini.

Imam Khomeini anaendelea kuimarisha Mapinduzi ya Kiislamu akiwa na mamlaka ya juu kabisa inayompa katiba. Hotuba zake nyingi alizowatolea watu wa aina mbalimbali na katika sherche tofauti zinathibitisha kuwa yeye ndiye mwalimu wa kweli na kiongozi shupavu wa Mapinduzi ya

Kiislamu. Katika muda wote huu, Imam Khomeini amedhihirisha sifa zake za pekee, k.v. ucha Mungu, ujuzi, uwalii, ushupavu, ukakamavu, uadilifu, na ni mwanasiasa na kiongozi mwenye hekima. Yeye ni mpole na mwenye huruma kwa maskini na wanyonge, lakini ni mkali kwa madhalimu na mabeberu. Shahid Ayatullah Mutahhari amemfananisha Imam Khomeini pamoja na Sayyidna Ali bin Abi Talib AS kwa ushujaa wa Kiislamu, busara na ucha Mungu. Wote wale waliopata fursa ya kuonana na Imam Khomeini wanakubaliana na maoni hayo.

Kitabu hiki ambacho kinajulikana kwa jina la Utawala wa Faqihi (Wilayate Faqih) au Serikali ya Kiislamu (Hukumate Islami) ni kitabu maarufu kabisa cha Imam Khomeini. Asili yake ni mihadhara aliyowatolea wanafunzi wa chuoni kati ya tarehe 21 Januari na 8 Februari 1970. Mihadhara hii ilirekodiwa na mwanafunzi mmoja kisha ikapigwa chapa katika sura ya kitabu.

Tanbihi: Maneno yaliyotiwa alama ya nyota (*) yamepewa maana yake katika ukurasa wa msamiati. Ni afadhali kwa msomaji kabla kusoma kitabu hiki kwanza ayafahamu maana ya maneno yaliyomo katika msamiati

Utangulizi

DINI NA SIASA

Suala la utawala wa faqihi* ni suala lililo wazi kwa kila mwenye fikra safi ambalo halihitajii dalili wala ushahidi. Lakini hali ya jamii ya Kiislamu kwa namna ilivyo hivi sasa imelifanya suala hili libabaishe bongo za watu hata hivi sasa likahitajia dalili na ushahidi. Jambo lililosababisha suala la utawala wa faqihi lisizungumzwe, ni kule kuwepo hali mbaya ya umma wa Kiislamu kwa ujumla, na vyuo vya kidini hususan.

Tangu Uislamu ilipodhihiri, ulikabiliwa na tatizo la upinzani wa Mayahudi waliojitahidi kwa bidii zao zote kuuzuilia yasiyo kweli na kutumia kila jambo ovu juu yake, hali ambayo ingali inaendelea hadi hivi leo.

Katika karne tatu zilizopita, kumezuka tena kundi lingine kubwa ambalo lasemekana kuwa baya zaidi na lenye hatari kwa ustaarabu wa mwanadamu hata kuliko iblisi na askari wake.

Mradi wa kundi hili ambalo tayari limeusambaza ukoloni wake kote ulimwenguni, hasa katika sehemu zenye Waislamu wakakamavu, ni kuufutilia mbali Uislamu usiwepo tena mbali na kutokusudia kuwasaidia watakaouacha Uislamu wao, bali lengo ni kuwatawala kimabavu na kuzipumbaza akili za watawaliwa.

Njama za kutanguliza kuupotoa Uislamu, ni mbinu zilizo gunduliwa baada ya wao kuona siku zote na hasa baada ya vita vya msalaba (crusades) kwamba, kizuizi kikubwa katika kutekeleza lengo lao ambacho hufifiza hali yao ya kisiasa, ni Uislamu kutokana na uimarifu wa hukumu zake na misingi yake na hasa kutokana na imani thabiti ya wafuasi wake. Uislamu tu, uliwafanya jamaa hao wahangaike.

Kwa ajili hiyo, hawakuwa na hila ila kutafuta maarifa ya kuuangamiza kwanza kwa kutumia njia mbalimbali za upotoshi mkiwemo mashekhe wa kujigamba waliomo katika vyuo vya kidini, vibaraka waliomo katika vyuo vikuu na mashirika ya kiserikali ya habari, utangazaji na uchapishaji, na wataalamu wa mambo ya Asia (orientalists) waliomo katika wizara mbalimbali za serikali za kikoloni wote hao walishirikiana pamoja kuwahadaa watu na hasa walio staarabika kwa kuwarai* na kuwabaidisha na Uislamu hadi walipowatumbukiza mahali wasipotarajia kuongokewa tena baada ya hapo.

Uislamu ni dini ya watu wote wapendao haki na usawa, ni dini ya watu wote wapendao uhuru wa kujitawala, na ni dini ya wale wasiopenda majeuri kuwakandamiza watu wema.

Pamoja na kuwa ni hivyo, maadui zake waliutangaza Uislamu kinyume cha hayo. Waliuwekea yasiyo ya haki. wakausingizia mambo yaliyohofisha bongo za watu, hasa awamu (wajinga). Mbegu hizi za chuki miongoni mwa watu zilipandwa hata katika vyuo vya kidini. Lengo kubwa likiwa kuufutilia mbali, kuyafanya mapinduzi ya kweli yasipatikane, na Waislamu wenyewe wasipate tena mwamko wa kuyafikiria maslahi ya uhuru wa nafsi zao, na mafundisho ya dini yao ambayo huwahimiza kuunda serikali itakayowadhaminia utengevu wa maisha yao kwa utaratibu wake bora wa Kiislamu.

Mfano wa hayo, ni yale masingizio yao juu ya Uislamu katika kuwapotoa watu waliponena, "Uislamu hauna uhusiano wowote ule na mipango ya maisha ya kijamii, wala haukupangika kiasi cha kuweza kuunda serikali yoyote ile, isipokuwa unafundisha mambo ya hedhi, kondo (nifasi) na tabia njema (akhlaq) tu."

Sikitiko letu kubwa kwa mawazo hayo machafu ni kwamba, hayakupandwa tu nyoyoni mwa maamuma* peke yao, bali pia nyoyoni mwa wanavyuoni wakubwa walio na madigrii na wanafunzi wa Kiislamu pia wamekumbwa na ulaghai huu. Vijana hao wa Kiislamu wamekosea katika kuuelewa na kuufahamu Uislamu, mpaka hivi leo dini yao imekuwa ni kitu kigeni sana kwao, sawa na mgeni atokaye ugenini wasiyemjua. Mwislamu anayedai Uislamu hivi leo, ni vigumu sana kwake kuweza kuthubutu kuwapambanulia watu na kuwafahamisha Uislamu. Na akijaribu kuwa fahamisha Uislamu kwa hakika ulivyo, wale vibaraka wa mabeberu waliomo katika vyuo vya kidini watapiga makelele!

Ili tuweze kupambanua sawasawa baina ya Uislamu ulivyo kihakika na baina ya wauelewavyo watu, ningependa kuzielekeza fikira zenu, kwanza, kwenye tofauti iliyopo baina ya Qur'ani Tukufu na hadithi dhidi ya vitabu vingine vyenye kuelezea matendo kuambatana na ibada.

Qur'ani Takatifu na vitabu vya hadithi ambavyo ndivyo hasa misingi ya sheria za dini na za kiulimwengu, vina tofauti kubwa sana na vitabu vya mujitahidi* na walivyovitunga marjaa wa zama hii, kwani Qur'ani na hadithi vimekusanya mambo yote'yanayohusu uhai na maisha.

Yafaa ieleweke kwamba, aya za Qur'ani Tukufu zinazo husiana na mambo ya kijamii ni nyingi zaidi tena sana zikilinganishwa na aya zinazohusiana na ibada, kinyume na wanavyodai wapotoshi hao eti Islamu ni dini isiyo kamili, isiyo na sera* na mipango yoyote juu ya utawala wa jamii ila ibada tu.

Mbali na hayo, hata vitabu vya hadithi, huwezi kupata zaidi ya milango mitatu minne hivi inayohusiana na ibada ya mwanadamu na wajibu wake kwa Mola wake, na milango michache sana inayozingatia maadili, ila utakuta milango yote na hadithi zote zina fungamano lenye kutilia nguvu sana umuhimu wa kuzingatia jamii, iktisadi (uchumi), haki za mwanadamu, mipango ya maisha na siasa za utawala.

Enyi vijana wa Kiislamu ambao ndio askari wa kuutetea Uislamu! Jilazimisheni kufuata yale mambo niliyoyaelezea kwa muhtasari. Na kwa muda wa uhai wenu, waelezeni watu mipango kamili, mafunzo ya Kiislamu na kanuni zake kwa kutumia uwezo wenu wote mkitumia njia zinazofaa kumfahamisha mtu zikiwa aidha maandishi, mazungumzo au matendo. Wazungumzieni watu kwa kuwafunza, balaa zote, taabu na maadui 'waliouzunguka Uislamu toka ulipoanza kudhihiri hadi leo hii. Msiwafiche watu mambo mnayoyajua. Wala haiwafalii kuwaacha watu kuendelea na dhana zao za kuufananisha na kuuona Uislamu kuwa sawa na Ukristo wa leo usio na msimamo, pia kuona kwao msikiti ni sawa, hauna tofauti na kanisa, kadhalika kuukejeli Uislamu eti hauna mipango zaidi ya uhusiano wa mtu na Mola wake.

Wakati giza lilipotanda barabara katika mataifa ya Magharibi, na wakati Wahindi Wekundu walipokuwa wakiishi Marekani, na tawala za kifalme za Warumi na Wafursi zilipo kuwa zikiwatawala wenzao kimabavu huku zikieneza ubaguzi na kutumia nguvu kwa njia zote ili kuyatoshelezea maslahi yao na kupuuza maoni ya wananchi walio wengi na kutofuata sheria, wakati huo Mwenyezi Mungu alimleta Mtume Muhammad SAW na sheria zenye ufafanuzi wa kila jambo ili mwanadamu asalimike na akae chini ya kivuli cha usalama.

Mtume Mtukufu SAW alipofika tu, kila kitu alikipangia kanuni zake na sheria zake. Kanuni hizi, zinamwongoza mtu kwa maamuzi yaliyo sawa toka kutungwa mimba na kuzaliwa kwake hadi kuteremka kwake shimoni (kaburini). Kanuni hizi zina upambanuzi kamili juu ya huduma za kijamii na namna ya kuiendesha serikali, upambanuzi ambao hauko kwenye shughuli za ibada tu kama wanavyodai walegevu wa akili. Uislamu unalinda haki kwa ulinzi wote wa juu na ulio kamili.

Vitabu vikubwa vimeandikwa tangu zamani vyenye kueleza haki mbalimbali zinazopatikana katika dini ya Kiislamu kutoka katika matendo yake, mipaka yake, visasi vyake, maamuzi yake na mipango yake ya kuweka uhusiano baina ya mataifa au utawala na watu ikiwa ni pamoja na kanuni za vita na haki za binadahiu.

Hivyo ndivyo namna Uislamu ulivyo wa kwanza kuongoza kuchambua kila jambo linaloambatana na maisha na ukatoa jukumu na hukumu yake. Lakini wageni waliwalaghai watu kwa kuwatia wasiwasi wakiwemo pia watu walio na utamaduni wao na wastaarabu kwa kuwaambia, "Uislamu hauna chochote. Mafunzo ya Kiislamu yameishia katika hedhi na nifasi tu, na mashekhe hawafunzwi zaidi ya hayo." Hayo ni kweli. Baadhi ya mashekhe hawajibidiishi zaidi ya hapo, kwa hivyo ni wazembe. Na mashekhe wa aina hii, ndio wanaowapa moyo maadui kupata lengo lao la kuukashifu Uislamu. Pia tendo lao hili, huwanufaisha sana wakoloni ambao toka miaka kadha iliyopita wamejitahidi kadiri wawezavyo kupandikiza mbegu za usahaulifu katika vyuo vya kidini ili wapate walitakalo kwetu sisi, katika uchumi wetu na hata katika mazuri ya nchi yetu.

Wakati mwingine — kama nilivyotangulia kusema - huwatia wasiwasi watu kwa kuwaambia eti, "Uislamu ni mpungufu, si kamili, wala sheria zake za maamuzi hazipo katika namna itakikanayo." Na ili kutekeleza agizo la kuwahadaa na kuwapotoa watu, vibaraka wa Wazungu (Waingereza) walikwenda mbio kuiga na kuagizia mila na kanuni za kigeni kutokana na mafunzo ya hao mabwana zao (Wazungu). Mambo kama hayo yamewapata wanamapinduzi na kutokea nchini Iran. Wanamapinduzi hao wa Iran, walipotaka nchi yao iwe na utawala wa kikatiba wenye msingi ya usawa, vibaraka hao walitegemea kanuni na katiba za Kibeligiji walizoziazima (walizoziiga) kutoka ubalozi wa Ubeligyi. Wakati huo idadi kubwa ya hao vibaraka ambao sipendi kuwataja majina, walifanya juu chini kufutilia mbali juhudi za wanamapinduzi huku wakijitahidi kuundaunda upungufu wa kanuni za Kifaransa na za IJlaya ambazo waliziiga wakazitumia huku wakiongezea kanuni za Kiislamu ili kujipendekeza na kuwa-hadaa watu wasigundue njama zao kusudi kutowapinga.

  Yaliyomo endelea