rudi nyuma Yaliyomo  

Enyi ndugu zangu, waelezeni watu mipango na siasa ya serikali ya Kiislamu. Iwekeni wazi kwa walimwengu wote huenda watawala na marais (viongozi) wakatosheka na usahihi wake wakafuata, na sisi hatuwapokonyi viti vyao, bali walio waaminifu tutawaacha waendelee kutumika.

Idadi ya Waislamu hivi sasa ni zaidi ya 700 milioni. Wote wanatufuata sisi, lakini kwa kuwa sisi hatuna hima wala shauku hatuwezi kuwaongoza. Ndugu zangu, tunapaswa kuunda serikali yenye kuaminika, watakayoiamini watu nayo iwasalimishie mambo yao yote. Sisi tunamtaka kiongozi atakayejitolea kwa uaminifu na usafi wa moyo ili watu wote waishi chini ya serikali yake salama. Naye Mwenyezi Mungu anajua kwamba ustahiki na uwezo wenu wa kuyaendesha mambo ya watu haulinganishwi na watu wengine, isipokuwa tu sisi hatuna udikteta wa kuwaua watu pasina haki, kuoneana na kuwakemea watu, maana mambo hayo si katika maongozi yetu.

Afisa mmoja[50] wa Iran aliniambia huko kizuizini nikiwa na Sayyid Qummi alipokuwa akiendelea kutaabika (Mungu am-salimishe) kwamba, "Siasa ni mbaya. Ni uwongo na unafiki. Tuachieni sisi!" Hii ni kweli. Ikiwa ni kweli kwamba siasa haina maana nyingine isipokuwa hii (yaani uwongo na una-fiki), basi maana ya siasa kama wanavyoifahamu wao ni sawa. Ama siasa katika Uislamu, na siasa kwa Mtume Muhammad SAW na kwa Maimamu ambao ni wanasiasa wakubwa kuliko watu wote haina maana hiyo aliyoyasema afisa huyo. Jamaa huyo, alitaka tu kutuhadaa na kutufunika akili zetu.

Siku ya pili yake, magazeti yalitoa habari yakisema, "Kulingana na maafikiano yaliyofikiwa kwa masikilizano, kuanzia leo hii mashekhe hawatajiingiza katika siasa." Nilipoachiliwa tu kutoka kizuizini, nilipanda mimbari na kukanusha habari zilizotokea magazetini na nikasema, "Mtu huyo ni mwongo. Ikiwa Khomeini au yeyote miongoni mwetu atathubutu kusema hivyo, tutamtoa katika ushekhe!"

Tangu awali hao walikuwa wakikutieni fikra kwamba siasa ni kusema uwongo na kufanya ulaghai ili kwamba nyinyi msipendelee kuingilia katika mambo ya utawala bali muwe mnavuta uradi tu. Wao wanatutaka tushughulike na ibada tu ili wao waweze kufanya kila kazi waitakayo na kila ufasiki waupendao. Alhamdulillah, wao wenyewe hawafahamu shabaha hasa ya wanayoyafanya kwani wao ni vibaraka tu. Wataalamu na weledi wa mabeberu wa Kiingereza ndio walioiratibu mipango hiyo zaidi ya miaka mia tatu iliyopita wakati walipopenya katika nchi za mashariki na kuanza upekuzi wao. Baada ya Waingereza wakaja mabeberu wa Kimarekani na kwa shauri moja wakaendelea kufanya njama zao.

Nilipokuwa mjini Hamadan (Iran), alinijia mtu mmoja. Ni mtu mcheshi kidogo, akiwa ameshikilia ramani mkononi mwake ambayo ina alama nyekundu za kuonyesha sehemu zilizo na kanzi za madini zilizohifadhiwa ardhini humu nchini mwetu. Angalia, haya yaliwafikia kitambo vidudu watu — watu wa kigeni hasa Wazungu — wakajua dhahabu iliko, kunakopatikana shaba, na mafuta yaliko. Baada ya wao kutuvinjari na kutufanyia ujasusi, waligundua kwamba, kizuizi cha pekee ambacho chaweza kuwakomoa kabla ya kutekeleza lengo lao, ni dini ya Kiislamu na mashekhe wakakamavu.

Watu hao, walizijua nguvu kamili zilizo katika Uislamu na walizifanyia hesabu, maana historia iliwafunza kwamba, Uislamu ndio uliofungua milango ya Yuropa na kuitawala kwa muda mrefu. Kwa hivyo walijua Uislamu halisi hauwapi nafasi ya kufanya watakavyo.

Kwa upande mwingine walihisi kwamba, mashekhe wa kweli hawangeweza kuwapeleka watakapo au kuwapanda migongoni. Hapo, walikwenda mbio toka siku ya kwanza, kukiondoa kizuizi hiki njiani mwao na kupunguza nguvu za hima ya uislamu na imani ya rohoni kwa njia mbalimbali. Hivyo, ndiyo sababu unawaona watu wengi wakiuangalia Uislamu na kuuchukulia kuwa chombo tu cha masiala ya dini pekee, na wengine utawaona hata hawana dhana nzuri juu ya mashekhe. Vibaraka wa wakoloni walifanya juhudi za kuwakashifu mafaqihi na maulamaa na kuwatangaza kwa ubaya mpaka mmoja wao pasina hofu tena kwa ujasiri bila haya alisema, "Maulamaa mia sita wa huko Najaf (Iraq) na wa Iran walikuwa wakipokea mishahara yao kutoka kwa Waingereza. Shaykh Ansari[51] alipokea kwao mshahara kwa muda wa miaka miwili." Kibaraka huyo katika kuyaeneza hayo, alitegemea waziri wake wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza huko India. Tuhuma hii ya kikoloni ni ya kuropokwa tu wala haina msingi wowote.

Kwa upande mwingine, maadui zetu hao wanajitahidi kwa bidii zao zote kuishusha hadhi ya dini ya Islamu na kusema eti maulamaa na mafaqihi, shughuli zao za lazima ni kuyabaini masiala ya ibada tu, kutoa mawaidha na miongozo mbalimbali. Nao baadhi ya walio duni waliyasadiki baadhi ya makala hayo wakapotea pasina kutambua. Mimi nawaambieni kwamba, uwongo huu tunaotuhumiwa, na bidii zote wanazozitoa zina lengo la kuyatwaa mapato yetu na kunyonya utajiri wa nchi yetu.

Taasisi zote za kibeberu, zimewatia watu wasiwasi kwa kuwahadaa eti dini ni tofauti na siasa. Kwamba, haifai mashekhe kujiingiza katika mambo ya jamii, na kwamba si haki kwa mafaqihi kuyashughulikia mambo ya umma. Hayo si neno, lakini jambo la kusikitisha ni kuona baadhi yetu wameusadiki uwongo huu. Kusadiki huku kumeleta matumaini makubwa mno nyoyoni mwa wakoloni.

Hebu viangalieni vyuo vya kidini, mtaona athari na madai hayo yako wazi kabisa. Kuna wabatilifu fulani wasio na akili, na kuna wavivu fulani ambao wao huomba dua tu na kuyazungumza masiala ya ibada peke yake kana kwamba hawana jukumu jingine linalowangojea.

Tunaweza kuona athari hizo kutokana na sauti na maneno ya kusikitisha yanayotoka vinywani mwa wengine wakisema eti, "Kusemasema mambo ya kisiasa kunapinga hadhi ya shekhe. Mujitahidi hafai kusemasema, bali ni murua kwake kunyamaa kimya atosheke kusema 'Laa ilaha illallah!' (Hapana Mungu isipokuwa Allah tu) na akilazimika kusema basi na aseme kidogo tu." Hayo ni makosa na ni kinyume cha sunna tukufu ya Mtume. Mwenyezi Mungu akizungumzia kuhusu bayani* katika sura ya ar-Rahman asema, "Aka-mfundisha bayani (kunena), " (55:4). Kwa mujibu wa aya hii Mwenyezi Mungu aliwapa waja wake neema hii ya usemaji na anawakumbusha fadhila Yake na neema Zake kwao zilizo katika sura hii. Usemaji au bayani ni hisani ya kuwaelimisha watu imani zao tukufu, hukumu za dini yao na maongozi yao mbalimbali. Mtume Muhammad SAW na Amirul Mu'minin Ali AS walikuwa wasemaji wakubwa. Hivyo, tushikamane na maneno ya Mtume kwamba tuwafunze watu hadithi zake, na tuyafuate mawaidha ya Imam Ali AS kwa kusimama mbele ya madhalimu.

TUWASAHIHISHE WATAWA WA KUJIGAMBA

Mawazo ya kipumbavu ambayo yanaenezwa na maadui miongoni mwetu na ambayo tumeeleza baadhi yake hivi karibuni, yanaaminiwa pia na baadhi yetu. Katika kuyaamini, kunaupa ukoloni na ubeberu upenyo wa kujipatia makao ya kudumu. Kikundi hicho cha (mashekhe) wapumbavu kinajidai kuwa ni cha watakatifu na watawa hali si watakatifu wala watawa kamwe ila tu hujipachika utakatifu na utawa. Watu kama hao tunapaswa kuwarekebisha (kuwatengeneza) na kuwaonyesha msimamo wetu kwao, maana wao wanatuzuia kujitengeneza, kujisahihisha na kujiendeleza.

Siku moja walijumuika nyumbani kwangu, Marehemu Bwana Burujardi, Marehemu Bwana Hujjati, Marehemu Bwana Sadr na Marehemu Bwana Khunsari (ambao wote ni marjaa wakubwa wa Kishia) ili kujadiliana juu ya jambo muhimu la kisiasa. Katika ujumbe wangu, niliwaomba waeleze msimamo wao dhidi ya wapinzani hao wanaojigamba kuwa ni watakatifu, na wawachukulie kuwa maadui wetu wa ndani kwa ndani, maana wao hawana hima na wala hawayatilii maanani tunayoyaendeleza, na wanatuzuia kuipinga serikali na bunge.

Watu hao, wanaupiga Uislamu kofi kubwa na wanazusha hatari kubwa sana kwa Uislamu na wanautangaza Uislamu kwa sura mbaya kabisa. Wengi wao wanaishi Najaf, Qum na Mash'had miji ambayo ni makao makuu ya kidini. Watu hao, mbali na kuwapotoa watu na kuwaathirisha athari chafu, pia wanawapinga wanaojitokeza kuwakanya au kuwaamsha watoke katika yale waliyojifunikiza. Vilevile wanawafanya watu kuwa wavivu na madhalili na wanawazuia wasipinge ubeberu wa Kiingereza na Kimarekani na uchokozi wa Israel dhidi ya Waislamu.

Lazima kwanza tuwape mzinduko na nasaha jamaa hawa. Tuwaambie, "Je, hamwoni hatari inayotukabili? Je, hamwoni kwamba Waisraeli wanawaonea na kuwaua Waislamu na kuwaangamiza burebure? Mmarekani na Mwingereza wanamsaidia, wakati nyinyi (mashekhe waongo) mmekaa kimya mnaangalia tu! Lazima mwamkeni! Mfikirie njia za kuwaondolea watu mashaka yao! Mazungumzo matupu hayana faida! Kufanya ibada peke yake na kutoa fatwa hakuondoi shida za watu."

Katika hali ambayo maadui wanafanya njama ya kuuangamiza Uislamu na kuyapotosha mafundisho yake, haifai mkakaa kimya kama Wakristo. Wao suala la Utatu na Roho Mtakatifu, liliwasahaulisha kabisa kila kitu na wakabaki mikono mitupu bila chochote. Nyinyi amkeni mwangalie ukweli wote namna ulivyo, na yazingatieni mambo yote ya maisha ya leo na ya kesho.

Je ndugu zangu, mnadhani mkikaa tu malaika watawakunjulieni mabawa yao chini ya miguu yenu kama ishara ya kuwatukuzeni? Je, malaika humshughulikia mtu anayejishughulisha au kina nyinyi? Malaika humkunjulia mabawa yao Mtume Mohammad SAW kwa kazi kubwa aliyoifanya. Humkunjulia Sayyidna Ali AS kwa kutangulia kwake kusilimu na kwa kueneza kwake Uislamu duniani kote.

Watu hao (Mtume na Sayyidna Ali) na anayefuata mwenendo wao ndio wanaonyenyekewa na malaika na watu wote, hata maadui zao, maana mwenendo wao ulikuwa ni wa haki tu. Katika mema na maneno yao, na katika kunyamaa kwao, na katika hotuba na sala zao, na pia katika vita vyao walikuwa wana mwenendo mzuri. Ama nyinyi ni heshima ipi mnayostahiki? Hapana kitu!

Sisi tutasema kwa maneno kama hayo na watu hao wanaojidai wacha Mungu. Ikiwa nasaha zetu zitawafaa, sawa. Na hilo ndilo tulitakalo. La kama hazikufaa, basi tunajua la kufanya, na msimamo wetu mbele yao utakuwa mwingine.

TUVITAKASE VYUO VYETU VYA KIDINI

Vyuo vya kidini ni mahali pa kuendesha elimu ya dini. Ni vyuo ambavyo kazi mbalimbali za ufunzi na uongozi wa kidini unataalamishwa humo, na ni makao ya mafaqihi waadilifu. Ni taasisa ya wanafunzi na walimu wakuu toka pembe mbalimbali za ulimwengu. Ni chimbuko la washika amana (wawakilishi) wa Mungu na makhalifa wa Mitume. Yeyote ambaye ni mwakilishi wa Mungu katika waja Wake na nchini mwake kamwe hawi na tamaa ya chochote kati ya mambo ya kimaisha, wala hawatii madhalimu kwa jambo lolote, wala hazioni amali zake kuwa tukufu na wala hashirikiani nao.

Lakini yule faqihi ambaye hushirikiana na mtawala dhalimu, akahudhuria baraza lake na akamtii, kwa hakika si mwakilishi wa Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu ni shahidi jinsi maulamaa hao walio vibaraka walivyoiletea misiba dini ya Islamu. Kwa mfano, jamaa mmoja alikuwa mmoja wa mafaqihi waliokuwa wakimtumikia Muawiyah. Alileta msiba mkubwa kwa dini ya kiislamu kwa kutunga hadithi na sheria za uwongo. Kushirikiana maulamaa na watawala waonevu ni tofauti na kushirikiana watu wa kawaida pamoja na watawala madhalimu. Wakati mtu wa kawaida anaposhirikiana na serikali ya kidhalimu yeye mwenyewe hufasidika walakini faqihi au kadhi anaposhirikiana na serikali ya kidhalimu kwa kuitukuza huwa analetea madhara makubwa mno kwa Uislamu.

Hapo, ndipo hasa Maimamu wetu watakatifu walipolitilia mkazo sana jambo hili, na wakalaumu kuwafuata au kuwaandama watu kama hao kwa namna yoyote ile, pia kusaidiana na kufanya kazi pamoja na mahakimu wajeuri kwa lolote hatajambo likiwa dogo namna gani. Hayo yote ni kwa ajili ya kutahadhari balaa isije ikasambaa na kuufikia Uislamu na Waislamu hadi kufikia hali hii tunayoiona hivi leo.

Maimamu waliwawajibisha mafaqihi wajibu muhimu kabisa na wakawalazimisha kuitekeleza amana hiyo na kuitunza. Kwa hivyo basi, haifai kukakamia kwa takiya kwa kila jambo dogo au kubwa, yaani kudhihirisha kinyume cha imani yako wakati wa hatari ili kujisalimisha. Takiya iliwekwa na sheria ili kujihifadhi nafsi au kuihifadhi nafsi ya mwingine kutokana na madhara katika matawi au vitendo vya sheria. Lau Uislamu wote utakuwa hatarini, hapo hapana ruhusa ya kutumia takiya au kunyamaza. Mwaonaje ikiwa madhalimu hao watamshurutisha faqihi kubuni au kuzua katika dini! Je, mnahalalisha wakati huo faqihi huyo awe kimya eti kwa kufuata hadithi isemayo, "Takiya ni (hifadhi ya) dini yangu na dini ya wazee wangu." Hapo hapafanyiwi takiya wala haikufundishwa namna hiyo.

Lau shughuli za takiya zitamwingiza mmoja wetu katika serikali za watawala waovu, hapo ni lazima kukataa japo kutamfanya kuuawa, isipokuwa tu lau atajiingiza kutaka kuyatawalisha mafunzo ya dini ya kiislamu na pia kuwaingiza Waislamu kama Ali bin Yaqtin na Nasuruddin Tusi (Mungu awarehemu) walivyojiingiza katika mambo ya wafalme madhalimu na hatimaye kuyapindua.

Kikawaida, kama mjuavyo, mafaqihi wetu tokea siku ya kuanza Uislamu, hawakujitia katika mambo kama hayo. Na daima mafaqihi wa wafalme hawakuwa katika jamii yetu wala katika kikundi chetu wala hawana maoni au rai kama au sawa na yetu. Nao mafaqihi wetu toka zama hizo zote, kokote waliko wanapinga dhuluma zote za hovyo zinazoendelezwa.

Kwa hivyo, bila shaka Uislamu unatoa kibali cha kujiingiza katika vyama vya madhalimu ikiwa lengo ni kuuwekea udhalimu kikomo au kuzusha mapinduzi katika vyama hivyo. Si hivyo tu, bali kujiingiza kwa namna hii ni wajibu hasa wala hatuna ushindani kwa hilo. Upinzani wetu ni juu ya mtu ambaye hujiingiza kwa kutaka kulijaza tumbo lake, akafuata maisha ya anasa na akaiuza akhera yake kwa dunia ya wengine mbali na shetani kumpambia akaziona nzuri amali zake mbaya kwa kufanya kazi akishirikiana na wahaini kwa kuwatilia nguvu, kuwasaidia na kuwashika mikia yao. Naye Mwenyezi Mungu juu ya anayoyafanya au kusema ni Shahidi. Naam, tuwafanye nini watu kama hao?

WATIMUENI MASHEKHE WA WAFALME

Watu hao kamwe si mafaqihi. Kuna kikundi miongoni mwao ambao wanashirikiana na SAVAK na wanajipendekeza kwa kuvaa vilemba vikubwa vikubwa ili wapate wasaa wa kuwatukuza wafalme, kuwaombea baraka, ufanisi na rehema • za Mungu. Watu kama hao, hadithi zinatwambia, "Waogopeeni dini yenu," kwani wanahatarisha dini.

Watu hao ni lazima wafedheheshwe, maana wao ni maadui wa Uislamu. Ni wajibu juu yajamii njema ya Kiislamu kuwatupilia mbali, kwani kufanya hivyo na kuwadharau kutanusuru Uislamu na maslahi ya Waislamu.

Vijana wetu na watoto wetu wanapaswa kuvua vilemba vyao toka vichwani mwao. Je, vijana wetu wako wapi nchini Iran? Je, wamekufa au wanaghafilika tu? Sisemi (mashekhe waongo) wauawe, la hasha, bali yatosha tu vilemba vyao vivuliwe hadharani. Na ni juu ya watu wote wawazuie kabisa watu hao kuonekana katika jamii au hadharani wakiwa wamevalia mavazi ya dini, maana kufanya hivyo ni kutia uchafu na najisi mavazi ambayo ni tohara tena matukufu.

Hapo mbeleni tayari nimewaambia kwamba, maulamaa wa Kiislamu walio wakweli wametakasika kabisa na wataendelea kuwa hivyo. Wao hawajigambi.

Hao mnaowaona na mnaowasikia siku zingine ni watu waliojipachika wao wenyewe ushekhe na ufaqihi, lakini (kihakika) hawana chochote, bali wao nijamii ya walaghai tu. Na sasa watu wamewajua na hesabu yao ipo kwa Mola katika daftari. Na Mungu hakosi wala hasahau.

Sisi tumekalifishwa kuwaelimisha watoto wetu na kuwaepusha maangamizo ya mambo ya upuzi ya kiulimwengu. Nanyi jiandaeni kuzilinda amana alizowapa Mwenyezi Mungu kuzitunza.

Muwe waaminifu kwa dini yenu wala msiupendekeze ulimwengu na kujituliza humo, na wala hamtaweza aliyoyaweza Imam wenu Ali AS ambaye dunia kwake hata haikuwa sawa na chafya ya mbuzi kwa uduni. Yaepukeni mambo yote mliyojaribiwa nayo humu ulimwenguni. Zitakaseni nyoyo zenu. Mcheni Mola wenu na mtegemeeni Yeye tu.

Lau mtajifunza elimu ya kidunia ili kujipanulia maisha ya kiulimwengu — na Mungu awaepushe — basi ninawahakikishieni katu hamtapokea chochote kutoka kwa Mwenyezi Mungu wala hamtapata kwake heshima yenye kusifika. Na inshallah Mwenyezi Mungu atawaongozeni kwenye fadhila za juhudi, ujuzi, na kuzielewa hukumu za dini yenu.

Jiandaeni kuitumikia dini yenu. Jitayarisheni kumpokea Imam wa Zama zenu ili muweze kuutanda uadilifu humu ulimwengum. Jitengenezeni na jisahihisheni kwa tabia nzuri alizotufunza Mwenyezi Mungu, tabia ambazo zitaleta manufaa kwa jamii. Acheni kuutanguliza ulimwengu na toshekeni kwa maisha ya kiasi ili watu nao wawafuate katika kuzihifadhi nafsi na matamanio na tena ili muwe mfano mwema kwao. Muwe askari wa Mwenyezi Mungu ili mahali popote Uislamu uwe mikononi mwenu.

Sisemi yaacheni masomo yenu — Mungu aniondolee usemi huo — bali someni hasa kwa bidii muielewe dini yenu na sheria zake barabara, muwe mafaqihi, mwaonye watu wenu na mvisimamie vyuo vyote hivi vya kidini, wala msiviache kuendelea kupayuka; isipokuwa tu mnapokuwa huko masomoni, fanyeni tablighi, waongozeni watu na mwaamshe watoke usingizini mwao.

Hivi leo dini ya Islamu ni kana kwamba ni ngeni, hakuna aijuaye sawasawa. Kwa hivyo ikaribisheni nyoyoni mwa watu, muipambanue barabara ili watu wote waifahamu na waweze kuziepuka shaka na kauli za uwongo zinazosemwa kuhusu dini hii. Waambieni watu maana ya serikali yenye maongozi ya Kiislamu ilivyo. Waambieni maana ya Utume na Uimamu. Sababu ya kuja Uislamu na unachotaka. Mkifanya hivyo, kidogo kidogo Uislamu utaanza kutua nyoyoni mwao na inshallah siku moja tutaunda serikali ya Kiislamu.

JINSI YA KUZIANGAMIZA SERIKALI DHALIMU

Ili tuhakikishe kuondolewa kabisa kwa madhalimu hao, ni lazima:

1- Tukate uhusiano wetu na taasisi zote za serikali ya kidhalimu;

2- Tuache kushirikiana na madhalimu;

3- Tuzihepe kazi za aina zote zinazowapa madhalimu manufaa; na

4- Tuasisi taasisi za kisheria, kifedha, kiiktisadi (kiu-chumi, kiutamaduni na kisiasa ambazo zitachukua mahali pa zile za kwanza.

Wakati huohuo, tunapaswa kuzipindua serikali za kitaghuti, yaani nguvu za kisiasa za kidhalimu ambazo zinatawala katika nchi zote za Kiislamu. Mashirika, taasisi, wizara na idara za serikali ya kidhalimu na inayopinga umma lazima zisimamishwe na badala yake ziundwe taasisi, wizara na idara zenye kuwahudumia wananchi na zenye kuendeshwa kwa mujibu wa sheria za Kiislamu. Taasisi hizi zitaendelea na kazi zake mpaka itakapoundwa serikali ya Kiisiarnu.

Katika Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu ametukataza kumtii taghuti na ametukataza pia kufuata siasa za kidhalimu, na amewasisitiza watu wasimame kupambana dhidi ya watawala madhalimu. Pia alimwamuru Nabii Musa AS kumpinga na kumkomoa Firauni. Kuna hadithi nyingi sana zilizopokewa zikiwasisitiza watu wapambane dhidi ya udhalimu na dhidi ya yeyote yule anayepinga dini.

Maimamu wetu na wafuasi wao kwa miaka mingi waliziendesha mbio tawala jeuri kila mahali na wala hawakuzipa nafasi. Kwa ajili hiyo, taabu na udhia mwingi uliwapata kama tunavyohadithiwa juu ya maisha yao kutoka katika somo la historia. Kwa muda mrefu Maimamu walikuwa wakihangaishwa na watawala madhalimu hata ikawabidi watumie takiya ili kuilinda dini siyo nafsi zao. Pamoja na hayo yote hawakuacha kutoa maneno ya kuwahimiza wafuasi wao wajitokeze kuwakomoa wanafiki na kuwakataza watu kuwa kimya.

Nao watawala na viongozi madhalimu walikuwa wakiwa ogopa sana Maimamu, maana walijua wakipata fursa watajitolea haraka kuushika usukani wa uongozi na kuyafanya maisha ya anasa wanayoishi madhalimu kuwa hayatakikani (ni haramu). Hata nyinyi wenyewe mnajionea jinsi Harun Rashid alivyomtia kizuizini na kumfungia Imam Musa bin Ja'far AS kwa miaka mingi. Huyu Maamun naye alimlazimisha Imam Ridha AS kwenda kukaa Marw ambapo alimweka chini ya ulinzi mkali na baadaye kumwua kwa kumpa sumu. Taabu hizi hazikuwapata kwa kuwa wao ni wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW bali kutokana na fikra, rai na misimamo yao.

Harun na Maamum walikuwa wakijiita Mashia lakini watauachaje ufalme na hali wanajua wazaa wa Sayyidna Ali AS wanaudai ukhalifa popote wawapo, na wanajitahidi sana kuhakikisha wameunda serikali yenye maongozi ya Kiislamu wakiamini kufanya hivyo ni mojawapo ya sehemu iliyo wajibu katika maisha yao. Safari moja walitoa shauri kwa Imam Musa Kadhim AS kwamba watamrejeshea shamba la Fadak[52] lililonyang'anywa na wakamtaka achore mipaka ya shamba hilo, lakini Imam akachora mipaka ya mamlaka nzima ya Kiislamu na akasema kwamba, "Utawala wote wa mamlaka ya Kiislamu ni wetu, nanyi mnatawala kwa mabavu!"

Watawala madhalimu walikuwa wakijua wazi kwamba, lau Imam Musa bin Ja'far AS atawaponyoka, bila shaka maisha yao yatawageukia ambapo Imam atafanikiwa kuwapata wasaidizi na wala hatalegea. Wala msiwe na shaka yoyote kwamba lau Imam angepata wasaa wa kuongoza angeisimamisha haki na kuuondolea mbali ubatili na kuijaza ardhi uadilifu na usawa.

Hebu mtizameni Maamun namna alivyokuwa akimzunguka Imam Ridha AS akimtawalisha na akimsemesha kwa upole kwa kumwita "Ewe binamu yangu. Ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu'" Pamoja na hayo alikuwa akimpeleleza na kuchungua harakati zake maana alikuwa ni tisho kwa usultani wake kutokana na maarifa na taathira zake nyoyoni mwa watu na utukufu wake kwa Mtume Muhammad SAW.

Kikawaida masultani huupenda sana ufalme wao na huusifu kwa kila namna. Lau Imam angejumuika nao katika chombo chao — naudhubillah — angefanywa mkwasi wa anasa, nao wangembusu mikono yake na miguu yake.

Imepokewa katika hadithi kwamba, Imam Ridha AS alipoingia kwa Harun aliambiwa kuingia ikulu yake akiwa amempanda mnyama, mpaka alipofika karibu na jukwaa lake la kihalifa, Harun alimsimamia, akamsalimia, akamtukuza sana na kumpa heshima zote anazozistahili. Lakini ajabu ni wakati wa kuwagawia watu mali. Bani (wana wa) Hashim aliwapa kiasi kidogo sana, jambo ambalo lilimwathiri sana na kumshangaza Maamun, mpaka akapigwa na mshangao ambapo wakati huohuo tayari alikuwa ameziona heshima za babake kwa mgeni wake. Hapo alimwuliza babake sababu iliyomfanya kukipunguza kiasi cha Bani Hashim. Akajibu, "Ewe mwanangu, hakika wewe hujui. Yafaa Bani Hashim wasipewe zaidi ya kiasi hiki maana jambo hili la utawala ni lao, nao wanalistahiki zaidi kutushinda sisi. Na lau tutawamakinisha watatumikia tuukose utawala. Hivyo lazima waendelee kuwa mafakiri, wafungwe, wafukuzwe, wauawe na wapewe sumu."

Si Maimamu tu waliojitokeza kuupinga utawala wa watawala waonevu, bali Waislamu wote walilinganiwa kufanya hivyo. Katika vitabu vya Wasaail. Mustadrakul Wasaail na vitabu vinginevyo mna hadithi zaidi ya 50 zinazo amuru kuziepuka dhuluma na viongozi wajeuri. Maimamu wametoa amri ya kuwarushia michanga machoni na midomoni mwa wale wanaowasifu madhalimu. Na tuwafanye vivyo hivyo wanao wasaidia madhalimu japo kwa wino au kalamu. Wote hao tunaamrishwa kuuvunja uhusiano wetu nao kwa mambo yote.

Katika kukabiliana na hayo, kulipokewa hadithi zenye kuwasifu mafaqihi waadilifu. Hayo yote si kwa jingine bali kwa lengo la kutaka kuundwe serikali yenye maongozi ya Kiislamu ambayo itaongozwa na mafaqihi waadilifu, na kuwaondoa watu katika utumwa wa kibeberu, wa kikoloni na vibaraka wao ili watu wote waishi kwa amani, mapenzi na umoja. Wakati wowote ule, waislaamhawataweza kuyafikia wanayoyataka ila baada ya wao kujikomboa kwa imani kamili na huluka njema chini ya kivuli cha serikali adilifu inayo-fuata sawasawa sheria za dini ya Islamu na kuyaacha yasiyo-kuwemo katika Uislamu.

Wajibu tuliokuwa nao sasa ni kuunda serikali yenye muundo na mfumo wa Kiislamu. Tunataraji kwamba mwongozo huu juu ya muundo wa utawala wenye misingi ya kisiasa na kijamii ya Kiislamu utaelezwa kwa watu wote, ili kupatikane fikra mpya na harakati kakamavu za watu ambazo zitasababisha kuundwa kwa serikali ya Kiislamu.

Ewe Mola wetu, tukinge kutokana na nguvu za madhalimu waonevu. Uwang'oe kabisa watawala wajeuri, uupeleke uadilifu, huruma, upole na uangalifu nyoyoni mwa viongozi wa Waislamu ili wafanye yaliyo na maslahi kwa raia wao na waziache athari zote walizonazo hivi sasa. Tunakuomba uwafikie (uwakubalie) vijana wetu, wanavyuo vikuu na wataalamu mbalimbali wayatengeneze mambo kusudi matakwa ya dini ya Islamu tukufu yafaulu. Uwajaalie Waislamu wote wawe safu moja ili wajiokoe na wauokoe umma wao na ulimwengu wote kutokamana na makucha ya wakoloni na wahalifu wengineo. Uwawafikie kuihami nchi yao wakiwa safu moja kama kwamba wao ni jengo lililoimarika.

Vilevile Mola wetu tunakuomba uwawafikie heri mafaqihi, maulamaa na watafutao elimu ya dini kwa kutaka kujua, uongofu na kufanya amali njema. Kadhalika wape ushindi wanaokwenda mbio kuiasisi serikali ongofu ya Kiislamu, kwani Wewe ni mwenye uwezo, na hapana nguvu wala uwezo ila kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye juu.

TAMATI

Msamiati

aali: bora kabisa; tukufu; -enye fahari; adhimu

aalimu:(maulamaa) mtu mwenye ujuzi mwingi wa mambo ya dini yaKiislamu; mwanachuoni |

ainisha:dhihirisha; teua

alhamdulillah: sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu tu (hutumika kuonyesha shukrani au furaha ya mtu anapopata zawadi, cheo, neema, n.k.)

amali: matendo; kazi; mazoea

Arshi: kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu -|

Ashura: tarehe 10 Muharram 61 Hijria — siku ambayo aliuawa shahidi Imam Husayn AS na masahaba zake katika Karbala (lraq)

Ayatullah: lakabu anayepewa aalimu wa Kishia, agh. aliyefikia daraja la .1 ijtihad yenye maana ya 'ishara au nishani ya

bai: unga mkono mtu kwa kitendo anachotaka kufanya; kumwunga mkono mtu kuonyesha utiifu wako juu ya madaraka yake

baidi: weka mbali na makazi; peleka uhamishoni; peleka ukimbizini; kuwa mbal

barobaro:(ma-) kijana wa kiume aliyekwisha baleghe ;

bayani:ufundi wa kusema j

benibeni:sio sawa; kombo

bidaa: jambo au kitendo kilichozushwa na ambacho hakikuwepo katika 1 mazingira fulani

daawa: kesi; utesi; ugomvi

dhhnmi: (wa-) mfuasi wa dini ya Kiyahudi, Kikristo, n.k. ambaye anaishi katika himaya ya dola la Kiislamu na amefunga mkataba na Waislamu

fadhaa: wasiwasi; hangaiko la moyo

falsafa:elimu ya asili, maana na sababu za mambo au vitu; busara; hekima

faqihi: mtu mwenye utaalamu wa fiqihi ambayo ni elimu ya maamrisho, hukumu na sheria za Kiislamu inayotafitiwa kwa kutumia dalili za Qur'ani, sunna, ijmaa (mwafaka wa wanazuoni) na akili; mujitahidi

fatwa: uamuzi wa mwanachuoni wa Kiislamu katika masiala ya dini

fiqihi: elimu ya sheria za Kiislamu

ghairi: bila ya; mbali ya ghanima: ngawira

ghibu: ondoka machoni; toweka ghururi: hila; hadaa; majivuno

hadithi: mapokezi ya semi au vitendo vya Mtume Muhammad SAW, au mmoja wa Maimamu Thenashara AS

hafla: mkusanyiko wa watu, agh. walioalikwa kwa ajili ya shughuli fulani

haiba: hali katika mtu inayowafanya wengine wavutike naye; uvutio wa heshima

haram: eneo tukufu linalozunguka Kaaba, kaburi la Mtume Mtukufu au kaburi la Imam Maasumu

hawza: mahali panapotolewa mafunzo ya ushekhe; chuo; madrasa hedhi: damu inayomtoka mwanamke katika uke wake kila mwezi hisabati: elimu ya hesabu

hohehahe: mtu ambaye hali yake ya maisha si nzuri; mtu asiye na mbele wala nyuma; maskini sana

hududi: sheria za adhabu za Mwenyezi Mungu ambazo kadhi, hakimu au mtawala wa Kiislamu hutekeleza kwa kumtia adabu mkosa; miiko ya Mwenyezi Mungu; mipaka

huja: (hujjah) thibitisho;ushahidi;dalili

hulka: tabia ya mtu; mwenendo wa mtu; maumbile

hukumu: uamuzi unaotolewa na hakimu katika daawa; amri; utawala; mamlaka

ijtihad: elimu ya kustanbiti (kutafiti) maamrisho na hukumu za sheria za Kiislamu kwa kutegemea misingi minne — Our'ani, sunna, ijmaa na akili. Daraja 1a ijtihad: ni daraja analolifikia aalimu kumwezesha kustanbiti

ijmaa: mwafaka wa wanavyuoni wa Kiislamu katika jambo fulani. Msingi mmoja katika misingi minne ya ijtihad — Our'ani sunna na akili imlaa: udikteta

inadi: hali ya kurudiarudia kumwambia mtu jambo asilolipenda ili akasirike

irfani: mafundisho au imani inayohusiana na maarifa ya hakika ya Mwenyezi Mungu yapatikanayo kwa njia ya mtu kujisahau nafsi yake na kumwabudu Mwenyezi Mungu tu; usufii; uwalii

itibari: heshima; utukufu; muamana; sifa zisizokuwa za dhati yenyewe;heshima na sifa zilizotunikiwa

jihadi: vita vitakatifu;jitahada kubwa;mapambano matakatifu

jizya: kodi au malipo maalum yanayolipwa na wadhimmi — yaani wafuasi wa dini yenye Kitabu Kitakatifu, k.v. Wakristo, Wayahudi, n.k. -wanaoishi katika himaya ya dola la Kiislamu kulipia usalama wao na haki wanazopewa. Wadhimmi hulipa jizya badala ya khums na zaka zinazolipwa na Waislamu jopo: kikundi cha watu wanaoshughulikia jambo au kazi maalum

kalifu: lazimu;wajibisha

kauli: maelezo; maoni

kengeua: fanya mtu kufuata njia au tabia mbaya; potoa

kharaj: kodi inayotolewa kwa ajili ya kutumia mashamba ya dola la Kiislamu

khums: asilimia ishirini (20%) ya faida inayopatikana katika mapato baada ya kutoa gharama zilizo muhimu, au 20% ya mali mahsusi zinazopatikana ardhini, baharini, na katika mazao na mifugo

lakabu: jina ambalo mtu hujipa au hupewa mbali na jina lake hasa

lingana: tangaza; omba haja au matakwa; kuwa sawa na

liwali: (ma-) mtawala aliyechaguliwa na serikali na anayeshughulikia mambo ya hukumu katika sehemu futani; gavana

maadili: elimu inayohusiana na tabia njema au mwenendo sahihi wa mtu;akhlak

maamuma: mtu asiye na ujuzi fulani na inambidi amfuate mwenye ujuzi

Maasmnu: otovu wa dhambi au makosa. Mairnamu Maasumu: Maimamu Thenashara wasio na dhambi

madaha: mbwembwe; matendo mazuri ya kuonyesha adabu

mahafali: mkusanyiko mkubwa wa watu kwa ajili ya shughuli fulani mahiri: mwenye ujuzi na hodari kufanya mambo; mwenye busara

majlis: bunge

majilisi: mkusanyiko wa watu, hasa kwa Mashia, kwa ajili ya kuomboleza agh. msiba wa Karbala. Soma nvijilisi: soma habari agh. kuhusu tukio la Karbala

makinika: kuwa katika hali ya utulivu; tua

mantiki: elimu inayohusiana na utumiaji wa akili

marja taklidi:mujitahidi mkubwa agh. mwenye wafuasi wanaofuata amri au fatwa zake

maudhui: wazo au somo kuu linalozungumziwa

milki: jumla ya mali aliyonayo mtu, watu au chombo fulani minajili: kwa sababu ya; kwa madhumuni ya

rniraji: usiku ambao Mtume Mtukufu SAW alipazwa kwa Mwenyezi Mungu

mhadhara: (mi-) maelezo yanayotolewa mbele ya watu au wanafunzi >hasa katika vyuo vya juu kwa ajili ya kufundisha

mhashamu: (wa-) mtu maarufu au mkuu anayeheshimiwa

mlahidi: (wa-) mtu anayekana kuweko kwa Mwenyezi Mungu

msalihina: (wa-) mtu anayefuata amri zote za kidini, makatazo yake na amri zake

msomi: mtu mwenye elimu kubwa

mtawala: mtu mwenye mamlaka juu ya nchi, watu, n.k. na mwenye uwezo wa kuhukumu, kutawalia, n.k; hakimu; kadhi; walii

mwanajopo: memba wa jopo fulani

mujitahidi: (wa-) aalimu aliyetafiti (aliyejitahidi) na akafikia daraja la ijtihad — daraja lenye kumwezesha kutoa fatwa katika masiala ya kidini kwa kutumia dalili za Our'ani, sunna, ijmaa na akili; faqihi

nidhamu: mfumo; mpango au utaratibu mzuri wa kutenda jambo, wa kufanya kazi au wa kuendesha jambo

nifasi: damu inayomtoka mwanamke katika uke wake baada ya kuzaa

nyang'au: (ma-) mtu mwenye tabia ya kinyama;mtu asiyekuwa na tabiaya kiutu

rai: sema na mtu kwa maneno mazuri kwa madhumuni ya kumtaka akubali kutimiza linalotarajiwa; Uchaguzi wa rai: uchaguzi unaofanywa kuwataka watu watoe maoni yao juu ya jambo fulani;referendum

riwaya: habari, hadithi au maneno yaliyopokelewa kutoka kwa mtu fulani

rujumu: piga kwa mawe

salihi: mtu mwema

SAVAK: kifupisho cha Shirika la Upelelezi na Usalama wa Nchi ya Iran ambalo lilikuwepo katika zama za Shah likiwapeleleza na kuwatesa wananchi; mwajiriwa wa shirika hilo

sera: mpango wa utekelezaji agh. wa serikali au taasisi wenye shabaha maalumu

Shah: mfalme wa Uajemi (Iran)

shahidi: mtu aliyeuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu

shakhsiya: dhati ya rntu; mtu mashuhuri;hulka na tabia mahsusi ya mtu

shirk: hali ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kiumbe au kitu cho chote katika ibada, uumbaji na tadbiri Yake ya ulimwengu

silika: maumbile

sunna: maneno, mwenendo na vitendo vya Mtume Muhammad SAW ambavyo ni mfano kwa mwanadamu kuvifuata katika maisha yake

tablighi: utangazaji au uenezaji wa fikra, mafundisho, n.k. ya Uislamu

tadbiri: uendeshaji mzuri wa jambo

taghuti: (ma-) kitu au kiumbe ambacho ni sababu ya uasi au uvunjaji wa sheria za Mwenyezi Mungu, k.v. miungu, masanamu, mashetani, viongozi madhalimu, utawala wa haramu, n.k; mtu yeyote anayefuatwa bila ya idhini ya Mwenyezi Mungu; mtu anayependelea mambo yenye kukiuka mipaka (sheria) ya Mwenyezi Mungu.

takiya: hali ya kutodhihirisha imani au itikadi ya mtu katika hali ya hatari

taklifu: wajibu

tanasari: toka katika dini ya Kiislamu na kuingia katika dini ya Kikristo

tengemaa: kuwa kama ilivyotakiwa; kuwa sawa

ughaibu: hali ya kutoweka au kutoonekana hasa kwa Imam Muhammad Mahdi AS ambaye alikuwa ghaibu tangu mwaka 329 H/939 K hadi hivi sasa

ukwasi: uwezo mkubwa wa kuwa na mali; utajiri

unajimu: elimu ya nyota

uraibu: mazoea ya kitu unachopenda kukitumia, k.v. sigara, kahawa, n.k.

utawala: namna ya kuendesha shughuli za kutawala; hali ya kuwa na mamlaka, madaraka au wadhifa fulani

wafiki: kubaliana na; kuwa sawa'iawa na

waidhi: toa hotuba au maelezo ya dini ili kueleza au kuonya watu; hubiri

wajibu kifai: wajibu au faradhi ambayo ikitekelezwa na mtu mmoja huwaondokea wajibu huo waliobakia

walii: mlinzi au mtu mwenye mamlaka juu ya mambo. Sifa za walii wa waumini ni kama zile za faqihi. Kwa maana nyingine walii wa Waislamu ni Mwenyezi Mungu, Mtume Mtukufu SAW, Maimamu Maasumu AS, wajitahidi na mafaqihi. Maananyingine ni mtawa,sufii, mtawala, n.k.

wasii: mrithi; mwakilishi

zaka: malipo yanayotolewa katika fedha, dhahabu, zabibu, ngano, tende, shayiri, ngamia, ng'ombe na kondoo

ziara: tendo la kwenda mahali fulani panapo heshimiwa kidini ambapo agh. huwa amezikwa mtu mtakatifu

Vifupisho

 SAW: kifupisho cha salla llahu alayhi wa-ali, m.y. baraka za Mwenyezi Mungu ziwe kwake na kwa ali (wazaa) wake

AS: kifupisho cha alayhis/ alayhas/ alayhimas salaam, m.y. amani iwe juu yake/yao

k.v.: kama vile

m.y.: maana yake

agh.: aghlabu

n.k.: na kadhalika

H: Hijria — kalenda ya Kiislamu

K: Kikristo — kalenda ya Kikristo

Marejeo:

Kamusi ya Kiswahili Sanifu,Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Dar-es-Salaam, 1981; na kamusi nyinginezo

rudi nyuma Yaliyomo