rudi nyuma Yaliyomo endelea

(Ma Wa Farzandane Ma)

Imam Ali AS amesema:

"Wenye akili huhitajia adabu kama vile shamba linavyohitajia mvua."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 224)

Dk. Gilbert Robbin amesema:

"Huenda wengine wakachukiwa tukisema kwamba adabu, kama kwenda na kusema,- huwa ni jambo la

230

kawaida kwa mtu. Kwa maana nyingine, adabu ni wajibu wa kwanza wa kijamii au msingi wa ustaarabu. Ni lazima ieleweke kwamba akili haisaidii katika kufunza adabu, kwani adabu huitumia akili na kwa vyovyote vile haichukui msaada wake. Adabu humtawala mtu kabla ya fikra kuzinduka na alama za akili kujitokeza. Moyo wangu huniuma ninapomsikia mama akisema: 'Akiwa mkubwa atafahamu', kwani adabu isiyofunzwa udogoni haiwezi kupatikana kwa (njia ya) akili na fahamu (peke yake). Tunaweza kusema kwamba adabu ni akili ya kimatendo inayotuepusha na upotofu na inayotufungulia njia fupi na sahihi ya amali zetu. Adabu hutukinga na kila aina ya uzembe na uzorotaji, na kama vile ambavyo hupingana na hisia kali na tamaa mbaya, vivyo hivyo, hutuepusha kutokana na uadui na uchukivu. Adabu humfanya mtu apende kuingiliana na watu na humzuia mtu na tabia ya kutowajali watu au kujiona kunatokana na mazoea mabaya. Kwa kawaida, mwenye adabu hajihisi upweke. Kwa kuwa adabu ni mwendo wa kijamii, hivyo, humfanya mtu aingiliane na watu. Kwa hivyo, adabu ni jambo la kimataifa, ni lugha ya kwanza ya kijamii iliyo nzima, na ni chanzo cha kuyazindua mawazo."

(Cheh Midanam)

Ingawa leo juhudi nyingi zinafanywa kuweka sheria kali za kuzuia khiana na kupunguza uhalifu huo; na ingawa vyombo vingi vya kisheria hupambana dhidi ya watu wanaofanya khiana, lakini hatua zote hizo hazikufaa kitu wala hazikutoa natija, bali uhalifu huo huendelea kuzidi siku baada ya siku.

15 - UBAKHILI

233

Kusaidiana na Kushirikiana

Kufuatana na muundo wa kimaumbile, binadamu na vipawa mahsusi. Kila mtu anahitajia misaada ya kidhati ya wenzake kwa ajili ya kustawisha, kukamilisha na kuzalisha matunda ya vipawa vyake. Moyo wa kushirikiana na kusaidiana daima hujitokeza kama ni msingi muhimu katika kuleta maendeleo na nafanikio.

Muundo wa uumbaji wa binadamu umeundwa kwa ajili ya maisha ya kijamii, hivyo, kimaumbile binadamu hupenda kushirikiana na wenzake katika kutatua natatizo yake ya kimaisha.

Kila tukio la dunia na kila matakwa ya nafsi

•yanamletea matatizo mtu. Kila kitambo katika uwanja wa maisha kinahatarishwa na matukio machungu na

•.inakabiliwa na mashaka ya kila aina. Kwa ufupi, binadamu hatajiona kabisa kwamba hana haja ya kutaka misaada ya wenzake katika kutatua matatizo ya kimaisha. Kufuatana na msingi huuhuu wa kawaida usiobadilika, majukumu ya watu haya hodhiki katika ntu mmoja, bali hugawanyika kati ya watu mbalimbali na matabaka tofauti. Msaada wa kila mtu, hata uwe ndogo vipi, unafaa katika kustawisha jamii na kuziba Jaadhi ya mapengo yake.

Ilivyokuwa sifa za jamii zinapatikana katika umbo la mtu pia, hivyo, kwa upande mmoja, tunaweza

•kufananisha jamii na mwili wa mtu. Kwa kuwa umbo la

234

mtu limefanyika kwa viungo na vitu vingine mbalimbali, na kati yao kuna uhusiano wa kimaumbile, na kuendelea kuishi kwa mtu kunategemea kwamba kila kiungo kifanye kazi zake zilizopangiwa bila ya kukosea au kukiuka mpaka wa wadhifa uliowekewa; vivyo hivyo, jamii imefanyika kwa watu mbalimbali ambao kila mmoja wao inampasa atambue wajibu wake muhimu na wa kimsingi na atekeleze kwa moyo safi kila dhima aliyopewa ili kwamba jamii iweze kuhifadhika, kustawi na kubaki. Inambidi kila mtu kufuatana na wadhifa na uwezo wake atumie vipawa vyake, ujuzi wake katika fani maalumu na hazina yake ya kimaada au kiroho kwa ajili ya maslahi na uendeshaji wa mambo ya kijamii. Jambo hili linamwajibikia mtu kutokana na kufaidika kwake na matunda ya kijamii ambaye yeye ni sehemu moja ya wazalishaji wake.

Kushamiri ustawi, kupatikana raha na utulivu, na kufanikiwa katika kuvipita vikwazo vinavyomzuia mtu katika njia yake, huwezekana wakati mtu anapokuwa na hisia ya kusaidiana na wenzake. Unapokuwepo ushirikiano kati ya watu ndipo maisha hufana na hushamiri, kazi hutoa matunda mazuri, na magurudumu ya jamii huzunguka kwa ulinganifu maalumu katika njia ya ustawi na maendeleo.

Ubakhili Waondoa Mapenzi

Katika kiini cha roho ya mwanadamu hububujika hisia ya kimapenzi ambayo matokeo na matunda yake yana thamani kubwa mno. Hisia hiyo ni chanzo cha

235

ushirikiano na usaidiano kati ya watu. Hisia zinazotoka kwenye moyo mweupe kwa sura ya misaada zina manufaa bora kabisa ya kiroho na silika njema za kiungwana. Hisia hizo humfanya mtu aathirike anapoona masumbuko na masaibu ya mwenzake na humfanya awe tayari kujitolea kwa hali na mali kumwondolea au kupunguzia hayo bila ya kutumainia malipo ya kibinafsi hata kidogo.

Dk. Carl ameandika:

"Jambo lolote haliendelei ila kwa kujitolea, na utukufu wa roho haupatikani ila kwa mtu kujitolea au kufidia roho, umashuhuri na maisha yake kwa ajili ya mapenzi yake juu ya wenzake, nchi yake au lengo lake kuu. Mfano wa kujitolea ni kama ule wa askari anayeingia kwa hiari yake katika medani ya vita vya kutisha vya leo. Mfano mwingine wa kujitolea ni kama ule wa daktari fulani aliyekuwa mgonjwa na dhaifu lakini akaiacha maabara yake iliyokuwa katika Taasisi ya Rockefeller ya New York na akaenda peke yake katika bara la Afrika kutibu homa ya manjano naye mwenyewe akafa kwa ugonjwa huohuo. Kujitolea ni mwendo wa wale waliotambua uzuri wa haki, wakamwamini Mola wao kwa uwezo wao wote, na wakajitoa mhanga ili kwamba uadilifu na upendo utawale ulimwenguni. Kile kinachomfikisha mtu kwenye kilele cha ukamilifu ni hisia (za kimapenzi) wala si akili (peke yake), kwani nafsi hutukuka zaidi kwa njia ya hamu na ghamu kuliko kwa msaada wa akili. Katika njia hiyo akili huwekwa nyuma kutokana na uzito wake, na hisia ya mapenzi huota mzizi katika kiini cha nafsi. Kila

236

mtu anaweza kupita katika njia hiyo kwa kuyavuka mawingu mazito na kuona mwanga kileleni."

(Rah Wa Rasm Zindagi)

Wakati mwingine sifa mbaya huganda katika dhamiri ya mwanadamu kwa kadiri kwamba huunguza mizizi ya upole na huruma na huandalia moyo upoteze kila aina ya sifa njema. Ubakhili ni sifa mbaya inayomfanya mtu aende kinyume na dhamiri na tabia zake nzuri na adharau msingi wa ubinadamu. Isitoshe, ubakhili hubana fikra za mtu, humtweza na humshushia hadhi, na huwafanya watu wamchukie. Kwa kutegemea namna ugumu ulivyomwathiri, mawazo ya bakhili daima hufikiria mambo ya kimaada (kidunia), utajiri na mali, na kwa sababu hiyo, hafaidiki na utamu wa kuwa na fikra huru, kutambua ukweli wa maisha na thamani ya kiroho na kimaadili.

Nafsi ya utajiri wenyewe si lengo, bali ni chombo tu cha kukidhi mahitaji, hivyo, baada ya kukidhiwa mahitaji muhimu na ya kimsingi, huwa hauna faida kwa ajili ya raha na ustawi, wala hauwezi kuondoa masumbuko na wahaka wa tajiri.

Kitisho cha umaskini na ukata ni maradhi yanayomtia kiherehere na kihoro mchoyo na kumkosesha raha na utulivu, hivyo, kuhodhi na kurundika kwake hakumletei faida yoyote isipokuwa mashaka na wasiwasi.

Mtaalamu wa Kiingereza aitwaye Auibury, ameandika:

"Watu hawatamani kitu chochote isipokuwa utajiri,

237

kana kwamba hakuna kitu kingine cha kutamaniwa ghairi ya utajiri. Wako watu wengi wasioona utamu wa elimu na maarifa, hali hupiga mbio usiku na mchana kama Mayahudi wakitafuta mali na wakihiari kukosa usingizi na raha zao. Wale wanaotaka kuishi kwa kukusanya mali huwa wako mbali na uhakika na hawajui kwamba ukwasi ni wenzo wa raha tu na wala si raha yenyewe. Mali ni daraja linalotuvusha kwenye shimo kubwa la umaada na maangamizo. Ole wao wanaopoteza umri wao kulirefusha daraja wakisahau lengo lake. Tusipoteze maisha yetu katika kutafuta utajiri, bali tutake mali kwa ajili yetu badala ya kujitoa wenyewe kwa ajili ya mali. Maskini watu wanaopiga mbio katika jangwa wakitafuta mali kama walioshikwa na kiu kali. Kwa hakika hawana bahati ya utajiri wao, kwani hawachumi kitu ila mashaka. Hupoteza umri wao wote kutafuta mali, na huhitajia umri mwingine ili wastarehe na waliyoyachuma. Haihata! Hayarejei maneno yaliyotamkwa wala umri uliomalizika!"

(DarJostojue Kfioshbakhti)

Inaonekana kana kwamba kuna uhusiano na mfungamano madhubuti baina ya ukwasi na uchoyo! Tunawaona wakwasi wengi ndio wachoyo wenyewe. Uchunguzi mdogo juu ya mambo ya kijamii unatubainishia ukweli huu kwamba wenye kuwasaidia maskini na kushughulikia hali za akina hohehahe aghlabu huwa ni watu wa tabaka la kati.

Matajiri wagumu wanaochukiwa na maskini na mafakiri ndio wanaosababisha baadhi ya ufisadi wa

238

kijamii, kwa sababu mafundo ya nyoyoni na mashaka wanayohimili maskini ni miongoni mwa mambo yanayoeneza upotovu wa kila aina. Hakuna mtu anayekataa kwamba uchungu na udhia huo husaidia katika kuzidisha uhalifu na upotofu wa namna kwa namna. Wako matajiri wengi ambao kutokana na kutia kwao fora katika kupenda mali na utajiri hutoka katika mhimili wa utu na murua, na kutokana na kuwanyima watu haki zao huzidisha uonevu na udhalimu—utasema kana kwamba nyoyo zao hazina hisia za huruma na upendo!

Ukarimu ni kitendo kinachomtukuza na kumwendeleza mwanadamu na ambao unajulisha kuwemo upendo ulioshika mzizi katika moyo wa mtu. Ukarimu ni alama ya uthabiti wa fikra na utukufu wa roho, na ni kitambulisho cha mwanadamu halisi na huru. Kati ya sifa zote njema, ukarimu una sura inayopendeza zaidi. Ingawa karne nyingi zimepita, lakini sura ya Hatim Tai huendelea kung'ara katika historia iliyotanda kiza, na watu wanausifu ubinadamu na ukarimu wake.

Ukarimu unastahiki kusifiwa wakati mpaji anapotoa kwa lengo la kumkurubia Mwenyezi Mungu na kupunguza shida na matatizo ya wahitaji, bila ya kutaka kujionyesha hata kidogo.

Wasemavyo Viongozi wa Kidini

Uislamu umezingatia kwa kadiri ya kutosha masuala ya kijamii, na umeusia mno suala la ukarimu ili

239

kuimarisha misingi ya ufungamano na upendo kati ya matabaka ya maskini na tajiri, na kwa wakati huohuo umepinga vikali ubakhili na ugumu.

Kwa kukuza hisia nzuri za kibinadamu na kuimarisha moyo wa ushirikiano na usaidiano katika jamii, Uislamu umetilia mkazo suala la mahaba kati ya watu. Uislamu haumruhusu kabisa Mwislamu tajiri kusahau wajibu wake kwa maskini na kuuelekeza mwendo wake upande wa uchoyo, kwa kuwa ubakhili husababisha matajiri waache kutimiza wajibu wao wa kidini na kisheria ambao Uislamu umeweka sehemu fulani katika mali zao kwa ajili ya kusaidiwa tabaka la maskini.

Qur'ani Tukufu inasema:

"Wala wasifikiri wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Allah katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao, bali ni vibaya kwao. Karibuni watafungwa (pingu) za yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Kiyama, na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allah; na Allah ana habari za mnayoyafanya."

(Aal ^fmraan, 3:180)

Ni lazima Waislamu washike misingi ya mapenzi na huruma, waendeshe maisha yao kwa kusaidiana, na wajaze nyoyo zao wema na upole. Ubakhili haupatani na roho ya Kiislamu kwa kuwa huondoa huruma.

Mtume Mtukufu amesema:

"Hakuna jambo linalochukiwa mno katika Uislamu kama uchoyo."

(Nahju 'l-Fasafiah, uk. 549)

240

Ugumu ni sifa ambayo humwondolea mtu raha na makini na huadhibisha roho yake.

Mtume wa Uislamu amesema:

"Mwenye kuwa na raha kidogo kabisa kati ya watu wote ni bakhili."

(Nahju 'l-Fasahah, uk. 81)

Mwanasaikolojia mmoja ameandika:

"Kwa kawaida, mtu mwenye kukosa huruma (upendo) hujilaumu mwenyewe na huwa haridhiki na amali zake. Kwa sababu hii, wengi kati yetu huyaonea wivu maisha ya wengine na hujifanyia uchoyo wenyewe kwa wenyewe. Tabia hii haihusikani na utajiri wala cheo cha mtu. Kila mtu, awe na hali yoyote ile, anapoona maisha (mema) ya wenzake hutafuta kisingizio cha kuzidisha tamaa yake. Kwa mfano, ikiwa mtu ana nyumba, cheo, maisha mazuri, na mke na mtoto azizi, bado hatosheki na alivyonavyo, bali huwa na tamaa juu ya alivyonavyo rafiki yake ambavyo havishindi alivyonavyo yeye mwenyewe. Husononeka kwa nini mwenzake huvaa vizuri kuliko yeye, au ni kijana zaidi kuliko yeye. Kama si hayo, bado husononeka na husema: 'Amebarikiwa kwa kuwa hana matatizo yoyote kama niliyonayo mimi. Amebarikiwa kwa kuwa hana mwana, miliki wala cheo, wala hana habari ya matatizo yoyote.' Kwa njia hii, mara nyingi mtu mwenye kukosa upendo hutafuta sababu ya kujidunisha na kujilaumu mwenyewe ili kwayo ajisumbue kwa kuwaonea wivu wengine."

(Ravankavi)

241

Mwenyezi Mungu humrehemu na humbariki yule mtu asiyefanya uroho wa mali, na akawasaidia wahitaji kwa ziada ya mahitaji yake.

Mtume Mtukufu amesema:

"Mwenyezi Mungu amrehemu mtu anayebana mengi (ziada) ya maneno yake, na anayetoa ziada ya mali yake."

(Nahju 'l-Fasahah, uk. 81)

Vilevile amesema:

"Jihadhari na uchoyo, kwani uchoyo umewaangamiza waliokutangulia, umewafanya wamwage damu zao, na wahalalishe yaliyo haramishwa."

(Nahju 'l-Fasahah, uk. 8)

Imam Ali AS amesema:

"Nashangaa juu ya bakhili mwovu: huuharakisha umaskini anaoukimbia na huupoteza utajiri anaoutafuta. Huishi katika dunia maisha ya maskini na atahukumiwa katika Akhera kwa hesabu ya matajiri."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 497)

Dk. Auibury ameandika:

"Kuna baadhi ya watu ambao dhahiri yao ni matajiri lakini nyoyo zao ni maskini. Hawamiliki mali zao wenyewe na hushindwa kuzitumia kwa sababu ya kuzidi uchoyo wao. Mali zao ni kama mikufu ya dhahabu inayofungwa kwenye shingo zao ambayo haiwapi kitu ila maumivu na adhabu. Hapa ndipo mali huwa kero na

242

utajiri huwa ukuba."

(DarAghiishe Khoshbakhti)

Ubakhili ni tabia mbaya sana kwa kadiri kwamba husababisha mtu kuchukiwa na watoto wake wenyewe.

Amirul Muuminin Ali AS amesema:

"Ukarimu wa mtu huwafanya maadui zake wampende, na ubakhili wake humfanya achukiwe na watoto wake."

(Ghurani 'l-Hikam, uk. 368)

Vilevile amesema:

"Uroho na uchoyo umesimama juu ya msingi wa shaka na kutoaminiwa."

(Ghurani 'l-Hikam, uk. 488)

Dk. Farmer amesema:

"Sifa mbili za ukarimu na kujitegemea ambazo zinatokana na kuamini wengine na kujiamini wenyewe zinapoungana pamoja husababisha kukamilika kwa maadili ya kijamii na kupatikana raha kamili ya maisha ya kijamii. Zisipoungana sifa mbili hizo, maadili ya kijamii hayawezi kukamilika wala watu hawataweza kufaidika na maisha ya kijamii kwa ukamilifu."

(Raze Khoshbakhti)

Imam Musa Kadhim AS ameelezea juu ya thamani ya ukarimu:

"Karimu mwenye murua yuko katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu hamwachi

243

mpaka amtie Peponi. Mwenyezi Mungu Mtukufu hamtumi Mtume wala Wasii yeyote ila kwamba huwa ni karimu; wala hakutokea mwema yeyote ila kwamba alikuwa karimu. Babangu hajafariki mpaka aliponiusia ukarimu."

(Funi'al-Kafi,y..^v^.3S)

Wakati jeshi la Kiislamu lilipokabiliana na washirikina katika vita, Imam Ali AS alikuwa akibariziana na mushriki (mshirikina) mmoja. Mushriki akamwomba Ali ampe upanga wake. Ali akampa upanga wake bila ya kusita. Mushriki alishangaa mno na akasema: "Ewe mwana wa Abu Talib! Ni ajabu mno kwangu kuona unampa adui wako silaha yako katika wakati huu wa hatari nawe ukabaki bila ya silaha." Imam Ali AS akajibu: "Nimekupa kulitikia ombi lako, kwa sababu mimi naona ni kinyume na uungwana na ukarimu kukataa ombi la mtu katika hali yoyote ile." Mushriki alivutiwa na moyo mtukufu wa Ali, roho yake ikabadilika, akasilimu palepale na akajiunga katika jeshi la Waislamu!

Hakuna kitu anachohitajia zaidi bakhili kama uongozi wa kifikra. Ikiwa atakosa uongozi huo, basi atabaki daima katika matope ya umaada na masumbuko.

16 - TAMAA

247

Uchunguzi wa Mahitaji ya Maisha

Tangu siku ya mwanzo wakati binadamu alipoweka "mguu wake katika dunia hii na kuanza maisha mapya, ilikabiliwa na anuwai ya mahitaji ambayo yalimzunguka barabara maisha yake. Sehemu moja ya mahitaji hayo ni vitu muhimu kabisa vya kimaisha ambavyo kuendelea na kuhifadhika kwa mfumo wa uhai wa binadamu kunategemea hivyo. Kwa mfano, chakula, nguo na nyumba ni vitu vya mahitaji ya asili ambavyo huwezi kuvikosa. Sehemu nyingine ya mahitaji ni yale yasiyokuwa ya lazima ambayo yanabadilika daima. mahitaji kama haya hayana kikomo katika kutakiwa kwake, kwani ni mengi na wala hayumkiniki kuyapata yote ila katika ndoto na mawazo tu.

Kila mtu hutafuta mali kufuatana na lengo lake la isili na hisia yake ya kuhitaji. Hupambana na matatizo na vikwazo anavyovikuta kwa kutumia uwezo wake vote. Kwa kuwa kudumu na kustawi kwa maisha kunategemea mali kwa ukamilifu, hivyo, hapana haka kwamba ni lazima hali ya mtu iwe ibadilikabadilika pia. Mtu huhisi unyonge na udhaifu wakati maisha yake yanapokuwa magumu sana na uhitaji wake unapomletea mashaka katika maisha yake. .hutafuta kila njia kuondoa umaskini wake ambao unayadhikisha na kuyasumbua maisha yake. Kwa upande mwingine, utajiri mwingi mara nyingi huambatana na kiburi, majivuno na tabia chafuchafu

248

kana kwamba kuna uhusiano maalumu kati yao. Mtu anapokuwa na mali nyingi kupita kiasi na suhula na vyombo vya kutosha,ubinafsi na ufakhari humlevya kwa kadiri kwamba tamaa zake hazimaliziki.

Maisha ya mwanadamu yana sura mbalimbali na kila mtu huyaangalia kwa mtazamo wake, kwa sababu kiwango cha uwezo wa kufikiri na kutumia akili kinatofautiana kati ya watu. Fikra za watu wengi hazijapevuka kwa ukamilifu kuweza kutambua maisha halisi na kupambanua baina ya eneo la usalama na uwokovu na eneo la hatari. Kutambua uhakika huu na kupanda vidato vya juu vya chumu na ufanisi kunalazimika kutafiti siri za ulimwengu na hatimaye mtu kujijua mwenyewe. Jambo hili haliwezekani ila kwa kutumia akili na mantiki.

Ni lazima mtu ajue amekuja duniani kwa madhumuni gani ili kwamba aanze jitahada za kutafuta ufanisi kwa kutumia maarifa hayo. Ni lazima achague njia bora inayolingana na mahitaji yake ya kinafsi na silika yake, na aepukane na dosari zinazoharibu ukamilifu wa roho na utukufu wa shakhsia.

Huu si ufanisi wala uhodari mtu kutumia njia za kupata mali ili kuwashinda wenzake na kutafuta utukufu, kwani mali si kiini wala msingi wa maisha, na wala haifai kukiukwa mipaka ya ucha Mungu, wema na uadilifu kwa ajili hiyo na kusababisha kusahauliwa ubinadamu.

Dk. Carl ameandika:

"Maslahi ya kibinafsi yanayotawala fikra zetu yamesababishwa na kutokeza uhuria katika mazingira

249

ya kifikra. Utajiri unaonekana ni kipawa kikubwa kabisa cha mafanikio katika maisha ambayo fedha ni kigezo chake. Kutafuta faida katika mabenki, viwanda na biashara, sasa kumepanuka katika shughuli nyinginezo zote za mtu, na juhudi za maendeleo ya mtu huthaminiwa ikiwa amefanikiwa katika kujipatia mali. Jamii inayoupa umuhimu mambo ya kiuchumi kuliko kitu kingine haiwezi kupendelea murua, kwa sababu murua huhitaji utiifu wa sheria za maisha. Mtu anapojishughulisha katika mambo ya kiuchumi peke yake hataweza kabisa kuzifuata sheria za asili. Hakuna haja ya kutia chumvi tukisema kwamba murua wetu hutufikisha kwenye uhakika, na shughuli zetu za kimwili na kinafsi huziendesha kuambatana na utaratibu wa muundo wake. Mtu mwenye murua amefanana na mashine inayofanya kazi sawasawa. Misukosuko na migogoro inayodhoofisha jamii ya leo inatokana na kutokuwepo murua na maadili mema."

(Rah Wa Rasm Zindagi)

Kuwa na rasilimali ya kiroho (kimaanawi) ni shabaha halisi ya maisha na ni mali iliyo na thamani kubwa kabisa. Mtu ambaye hazina yake ya roho imefurika kwa mali ya kiroho, huwa ni nadra kwake kuwa na hisia ya kutamani mali ya kidunia (kimaada), kwani utajiri wa kiroho hukinaisha roho yake na humtosheleza katika vipindi vyote vya maisha yake. Mtu kama huyo hayuko tayari wakati wowote kubadilisha hadhi na hazina yake kwa mali na ufakhari wa kidunia.

250

Mwenye Tamaa Hatosheki

Tamaa au uroho ni hali ya kinafsi inayomfanya mtu daima atafute mali na manufaa ya kidunia kwa kadiri kwamba mambo ya kimali huwa ni chimbuko la fikra na juhudi zake.

Mwelekeo huu uliotia fora kwa ubaya ambao unatokana na nguvu za hatari za matamanio unahesabiwa kuwa ni miongoni mwa mambo yanayomletea mtu balaa na ukuba. Tamaa humzungusha akili ya mtu kufikiria ndoto za ufanisi. Roho ya mwenye tamaa hukufia mali kwa kadiri kwamba husahau kila kitu na huwa tayari kufidia hata murua na msingi wa kiutu! Kila anavyozidisha juhudi zake za kutafuta utajiri, ndivyo anavyozidi kuhisi uhitaji wake.

Dk. Shaupenhaur amesema:

"Ni vigumu sana kuainisha kiwango cha tamaa zinazohusiana na pesa na mali, kwa sababu ukinaifu wa watu haufanani, matamanio yao hayako thabiti siku zote, na uroho wa binadamu unabadilikabadilika. Baadhi ya watu wanaridhika na mali kidogo ambayo inakifu gharamazao za maisha, lakini wako watu wengine ambao wana pesa na mali nyingi mno na mapato yao yanazidi matumizi yao lakini daima hulalamika kwa kuwa hawakupata matakwa yao kikamilifu. Kwa hivyo, tamaa na matakwa ya kila mtu yana kiasi chake maalumu, na anapokuwa na hakika kwamba atayapata matakwa na matarajio yake kwa

251

kiasi hicho, hufurahi na huridhika, lakini anapo ona vikwazo katika kufikia muradi wake huvunjika moyo na hukata tamaa. Ukwasi wa matajiri hauwalaghai maskini, ilhali matajiri juu ya kuwa na baraka ya mali na pesa hawaridhiki wakati wowote, bali daima wanajitahidi kukusanya mali zaidi na zaidi. Mali na pesa zina athari mfano wa maji ya chumvi  kila mtu akizidi kuyanywa maji hayo huzidi kuona kiu."

Hakika mwenye tamaa hatosheki na neema zote za ulimwenguni bali huzidi kuwa na tamaa, kama vile ambavyo moto hauzimiki kwa kuongezewa kuni bali huzidikuwaka!!

Tamaa ikitawala katika taifa moja, huyabadilisha maisha ya kijamii kuwa ni uwanja wa mapigano na mashindano badala ya kuwepo amani na uadilifu, na huzuka ugomvi mkubwa kati ya watu. Ni dhahiri kwamba katika mazingira kama hayo huwa hakuwezekani kukua maadili mema na mwendo mnyoofu.

Ni lazima izingatiwe hapa kwamba suala la maendeleo na ukamilifu katika mambo mbalimbali ya maisha lina tofauti kubwa na msingi wa kuabudu pesa. Kwa hivyo, ni lazima uchorwe mstari baina ya mambo mawili haya na kila moja liwekewe hesabu mbali. Binadamu hana tatizo lolote linalomzuia kuleta mabadiliko na maendeleo katika jamii, bali ni lazima asonge mbele kwa haraka katika maendeleo hayo kwa kutumia vipawa vyake vya kiasili na kidhati.

Kwa kawaida, mbinu wanayoitumia wenye tamaa huleta balaa na matatizo katika jamii. Hutaka kukidhi

252

haja zao bila ya kufuata msingi wa uadilifu na hivyo kuleta masaibu kwa watu wote. Kwa sababu hii, huhodhi vyombo vyote vya uzalishaji wa mali kusudi wajichumie manufaa zaidi, na kwa njia hii, huzidi matatizo ya kiuchumi na umaskini.

Watu wengi wanadhani kwamba utajiri ni sababu ya kufanyika kazi nyingi, hivyo, huupa umuhimu mkubwa. Lakini ukweli ni huu kwamba kazi nyingi na kubwakubwa zimefanywa na maskini. Watu wengi waliokuwa maarufu, waandishi na wavumbuzi walitoka katika tabaka la maskini au la kati.

Utajiri mwingi unaleta madhara kwa watu wengi, na unawachafua kutokana na mwendo mbaya unaoambatana na mali na pesa. Kwa mfano, ikiwa kijana mmoja atarithi mali nyingi, basi juhudi zake zitapungua na hatakuwa na hima ya kujitahidi. Huenda utajiri huohuo ukamfanya afanye maasi na atumie wakati wake katika kustarehe badala ya kutumia katika kutafuta elimu.

Siku moja, tajiri mmoja mashuhuri alikwenda kuonana na mwanafalsafa wa Kiyunani aitwaye Apictos. Apictos hakumkaribisha vizuri tajiri kwa kuwa hakumwamini. Hivyo, akamwambia:

"Kwa kweli wewe hutaki kujifunza kaida na kanuni za kielimu kutoka kwangu, bali umekusudia kuubomoa mwendo wangu wa maisha."

Tajiri akasema: "Kama mimi nitataka kufuata mwendo kama wako, nitakuwa maskini kama wewe. Sitakuwa na vyombo vya dhahabu na fedha, farasi, mtumishi, ardhi wala miliki."

253

Apictos akajibu: "Mimi sitaki kuwa navyo vitu hivyo, na ingawa kwa dhahiri ni maskini, lakini wewe ni maskini zaidi kuliko mimi. Tofauti baina yangu na wewe ni hii. Mimi sijali wala simhitajii msaidizi wala mfadhili, lakini wewe unawahitajia. Kwa hivyo, mimi ni tajiri na mwenye nguvu zaidi kuliko wewe. Mimi sijali iwapo Kaizari ananitazama kwa macho mazuri au mabaya. Kwa hivyo, sina haja ya kujisifu wala kujipendekeza kwake. Mimi badala ya kumiliki vyombo vya dhahabu na fedha, namiliki uhuru wa nafsi yangu na si mhitaji. Wewe una vyombo vya dhahabu na fedha pamoja na fikra na itikadi zilizoganda na zilizo kavu. Fikra zangu ni pana kama nchi na najishughulisha nazo katika umri wangu kwa furaha kamili. Lakini wewe una nini isipokuwa majivuno na wasiwasi usiokwisha? Mali zako zote ni kidogo mbele yangu, lakini ninayomiliki mimi ni mengi na makubwa. Wewe huyapati matakwa wala matumaini yako, lakini mimi nimeyapata matakwa yangu yote na yamekidhiwa mahitaji yangu!"

Kila mtu ategemee elimu na akili, si dhahabu wala fedha, kwani wapumbavu tu ndio wenye kutegemea dhahabu na fedha.

Hapana shaka kwamba dhiki na faraja na ghamu na hamu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Kila mtu duniani, awe maskini au tajiri, anaathirika navyo kufuatana na hali yake, lakini utajiri unaopita kiwango cha mahitaji hausaidii katika kumletea raha mtu.

Socrates amesema:

"Baadhi ya watu hawana johari wala pesa, hawana nguo za fakhari wala kasri madhubuti, lakini juu ya hayo

254

wanaishi kwa raha zaidi ya mara elfu kuliko matajiri."

Mwenye tamaa ni mtumwa wa mali; amejifunga mnyororo usioonekana kwenye shingo yake na amesalimu amri mbele ya fikra zake zisizokamilika. Hudhani kwamba ukwasi wake ambao ungewatosha hata kizazi chake cha baadaye, ni hazina ya dharura kwa ajili ya siku ya shida! Lakini anapotanabahi kosa lake huwa Izraili amekwishasimama mbele yake tayari kutoa roho yake; na katika wakati huo wa sakarati huzitazama kwa masikitiko na kwa kukata tamaa mali alizozikusanya kwa taabu na mashaka. Mwisho wake, huziacha mali hizo na huzikwa pamoja na uchungu na majuto kutokana na matarajio na ndoto alizoota.

Uislamu Wafundisha Iktisadi

Dini ya Kiislamu inawaita watu na kuwahimiza kuzidisha juhudi zao ili kuleta maendeleo na ustawi katika vipengee vyote vya maisha, lakini kwa wakati huohuo inawakataza kwa ukali kuwa na uchu wa mali uliotia fora ambao huleta mashaka, huzuia ufanisi wa kudumu na hupotosha shabaha halisi.

Imam Muhammad Baqir AS ameshabihisha maisha ya mroho na taswira hii:

"Mfano wa mwenye tamaa ya dunia ni kama kiwavi cha nondo, kila akizidi kujizungushia nyuzi (za hariri) ndivyo hujifungia mpaka hufa kwa kujisonga roho."

(Usulu 'l-Kafi, Babuya Hubaya Dunia)

Mtume Mtukufu amesema:

255

"Jihadharini na uchu wa mali, kwani uliwaangamiza waliokutangulieni. Uchu uliwashawishi mabakhili na wakafanya ubakhili; uliwaamrisha kukata ujamaa na wakakata; na uliwaamrisha ufisadi na wakafanya ufisadi."

(Nahju 'l-Fasahah, uk. 199)

Amirul Muuminin Ali AS amesema:

"Epukaneni na mwenye tamaa, kwani kuingiliana naye huleta udhalili na mashaka."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 135)

Dk. Marden amesema:

"Utajiri si kuwa na kila kitu katika maisha wala ufanisi halisi si kukusanya mali. Lakini vijana wengi wanafanya kosa hili wakidhani kwamba mali ni kitu muhimu kabisa kuliko kitu chochote kingine. Kwa sababu hii, hupoteza umri wao wenye thamani kubwa wakitafuta utajiri na kujinyima vitu vingine. Hii ni fikra isiyo sahihi na ndiyo chanzo cha kuzidi matatizo kati ya watu. Tunahangaika kumiliki majumba ya fakhari, magari, nguo na vitu vya anasa tukidhani kwamba ni vyombo vya kutupatia starehe na ufanisi ilhali ni chanzo cha kuudhika na kutofanikiwa kwetu.

"Ni makosa mtu kuishi kwa lengo la kukusanya mali, na kuifanya (mali) kuwa ni mungu wake wa pekee kama vile Wana wa Israil walivyomwabudu ndama wa dhahabu. Ikiwa tutaendelea kuwa na fikra potofu na kudhani kwamba mali hii iliyokuwa mungu wetu wa zamani ni chombo cha pekee cha kutufanikisha, basi

256

tuwe na yakini kabisa kwamba tutapotea na kuwa mbali kabisa na njia ya ufanisi na mafanikio."

(Pimzi Fikr)

Imam Ali AS amesema:

"Mwenye tamaa ni mfungwa wa udhalili na kifungo chake hakifunguki."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 50)

Mafundisho matukufu ya dini ya Kiislamu ambayo yanaafikiana na maumbile ya mwanadamu, yameonyesha msingi wa uwiano baina ya mambo ya kimaada na kiroho na yamewachagulia wafuasi wake njia inayodhamini ufanisi wao wa kimaada na kiroho. Kwa kuwa wafuasi wa dini wameutambua uhakika mtukufu, hivyo, huwa na nyoyo zisizotetereka wala kuyumbayumba. Wakati wowote wanaposhindwa kuendelea katika uwanja wa mapambano ya kimaisha kutokana na kuwepo hali mbaya, huvumilia umaskini kwa njia bora kabisa kwa kutumia hazina bora ya kiroho. Mashaka na matatizo hayawavunji nyoyo zao, bali nguvu hiyohiyo ya imani ndiyo inayowapa utulivu na uvumilivu maalumu.

rudi nyuma Yaliyomo endelea