rudi nyuma Yaliyomo endelea

Samuel Smiles amesema:

"Kwa kadiri ambayo historia inavyoonyesha, jambo hili limethibitika kwamba wenye vipawa vikubwa wote walikuwa ni watu wenye furaha na wachangamfu, kwa kuwa wamefahamu maana halisi ya maisha na wakazidhihirisha roho zao katika kazi na athari zao. Wakati mtu anapozisoma athari zao (za utafiti), huona waziwazi humo alama za busara, roho safi, shauku na uchangamfu wao. Watu wote wenye roho bora kabisa na hekima kubwa huwa wana furaha na bashasha, na tabia zao ni viigizo ambavyo kila mtu akivutika navyo huvifuata na hupata mwanga wa furaha na uchangamfu halisi kutoka kwao."

Mtume Mtukufu SAW amesema:

"Vitakavyowaingiza kwa wingi umma wangu katika Pepo ni ucha Mungu na tabia njema."

(Wasa'ilu 'sh-Shi' ah,jz. 2, uk. 221)

39

Kwa hivyo, mtu ambaye ameifanya akili yake kuwa ni kiongozi wake wa maisha, na anataka kuishi kwa heshima na hadhi, inampasa aitafute rasilimali hii ya kiruhani yenye thamani. Vivyo hivyo, mtu inampasa awe na shabaha madhubuti na uwezo mkubwa ili aweze kuing'oa mizizi ya sifa na tabia mbaya. Kuzingatia madhara yanayotokana na tabia mbaya kunatosha kumfanya mtu apigane dhidi yake.

2 - DHANA NZURI

43

Matumaini na Utulivu wa Roho

Katika uwanja wa misukosuko ya maisha, binadamu hahitajii kitu chochote isipokuwa utulivu wa moyo. Katika medani ya mapambano ya kimaisha, mtu asipokuwa na silaha hiyo, atashindwa katika mapambano mwisho wake. Kwa kadiri maisha yanavyokuwa magumu zaidi ndivyo mahitaji yanavyozidi kwa kadiri hiyohiyo. Tuangalie vipi tutaweza kujitoa katika fadhaa na misukosuko hiyo na tukafuzu kuingia katika mazingira ya utulivu.

Kutafuta utajiri, madaraka, umaarufu, mambo na hali za kimaada na kidunia ili kujipatia raha na starehe ni kazi bure; kwa sababu chimbuko la raha linaanza katika umbile la mtu mwenyewe, kama vile ambavyo chanzo cha visirani kinaanza katika ulimwengu huohuo wa ndani. Kile kinachowezekana kutumiwa katika hazina za thamani za nguvu za ndani kwa madhumuni hiyo, hakipatikani katika mahitaji ya nje; kwa sababu machimbuko yote ya ustawi na raha ya nje na vilevile nyenzo na mategemeo yote yanayotumika katika njia hii, huwa ni ya muda na ya kupita mara moja tu, na ni muhali kwa binadamu kupata raha kamili. Utajiri wa tafakuri na sifa njema ni vitu vya pekee visivyoweza kuangamia ambavyo kwamba humtosheleza mtu kikamilifu asitegemee mambo yasiyokuwa na msingi.

Apictatus, mwanafalsafa mashuhuri wa Kiyunani, amesema:

44

"Ni lazima tuwafunze watu kwamba hawawezi kupata ufanisi na bahati nzuri katika mahali wanapopatafuta ovyoovyo. Ufanisi halisi hauko katika nguvu na uwezo, kwa sababu Mirad na Angluis walikuwa ni watu wenye bahati mbaya ingawa walikuwa na nguvu na uwezo mkubwa sana. Ufanisi haupatikani kwa kuwa na vyeo na madaraka ya kisiasa, kwani makaizari (wafalme) wa Kirumi walikuwa na vyote lakini hawakuwa na furaha wala raha.

"Kwa kweli, ufanisi hauwezi kupatikana kwa kuwa mashuhun na kuwa na neema na vipawa vyote hivyo, kwani Nero, Sandpapal na Aghamnin ambao walikuwa navyo vyote hivyo, lakini daima walikuwa na majonzi na wakilia, na kila msiba ulikuwa ukiwasibu wao. Kwa hivyo, ni lazima kila mtu atafute raha na ufanisi halisi katika nafsi na dhamiri yake mwenyewe."

Ni lazima isemwe kwamba ufumbuzi wa siri na mafumbo mengi ya maumbile ya ajabu, na vilevile kuzidi na kukamilika kwa suhula za kimaisha katika zama hizi hakutoshi kumpatia mtu maisha yasiyokuwa na mashaka na matatizo. Licha ya hayo, teknolojia na suhula hizo zimemwongezea binadamu wasiwasi na mashaka mapyamapya. Kwa hivyo, ili kujiondoshea dhiki na mashaka ya daima ya maisha na mawingu mengi yanayothakilisha roho zetu, tunahitajia haraka fikra wazi na nyongofu; fikra ambayo ni nguvu amilifu kabisa katika dunia yetu iliyoweza kummilikisha binadamu ulimwengu wa kimaada na kuleta mabadiliko makubwa katika nyanja zote za maisha, inaweza pia kumpatia raha. Hapa ndipo panapobainika nafasi ya

45

kimsingi ya kutafakari na athari zake za kushangaza katika maisha ya binadamu.

Akili ing'aayo ni chemchemi neemevu inayomwendeleza mtu mbele zaidi kuliko mahitaji ya kidunia na inamjulisha ulimwengu mwingine pia. Fikra nzito na aali humzuia mwerevu asidanganyike na ulimwengu. Yule aliyekikuza na kukiimarisha kipaji chake cha fikra (akili) na akakifanya kuwa ni kitovu cha uvutano katika maisha yake, atakapofikwa na matukio machungu na mabaya, atachukua hatua inayofaa ya kifikra badala ya kuyakabili vibaya, na atabaki imara kamajabali.

Ili tujitoe katika mazingira ya fazaa najahazi la uhai wetu lisikumbwe na mawimbi makubwa na madogo, ni lazima tuzidhibiti fikra zetu mpaka tafakuri sahihi zishike uongozi wetu, na nguvu zetu zote za kiroho ziweze kujizatiti na kusimama dhidi ya vitu vinavyoleta madhara na vinavyosababisha wasiwasi.

Mwanachuoni mmoja wa Magharibi amesema:

"Huenda hatuna uwezo wa kuwachagua kati ya marafiki na wasio marafiki watu ambao wanaweza kufanana nasi kwa upande wa tabia, maadili au mambo mengineyo, lakini tuko huru katika kuchagua fikra, kwa sababu katika nchi ya akili sisi ndio watawala na watendaji wenye amri kamili. Hapo hapana taathiri, vishawishi au vitu vinginevyo kutoka nje ambavyo vingeweza kutuhukumu au kutulazimisha kuchagua fikra tusizozitaka. Kwa hivyo, ni lazima kwetu tuchague njia sahihi ya kufikiri na tuziweke kando fikra yoyote isiyofaa. Siku zote tunafuata njia ambayo fikra zetu

46

zinatuelekeza; na kwa maana nyingine fikra zetu ndizo zinazotuongoza popote tunapopataka. Hivyo, inatulazimu tusiruhusu kufikiria fikra yoyote iliyo mbaya, wala tusiiruhusu akili yetu ishughulishwe na mambo tunayoyachukia, kwa sababu fikra kama hizo ndizo zinazotutia katika balaa. Ni lazima daima tufikirie kujipatia ukamilifu, si upungufu! Ni lazima tufikirie kupata matumaini bora kabisa na kufikia malengo ya juu kabisa, kwa sababu siri ya kila ufanisi na mafanikio iko katika kufikiri kwa njia sahihi tu."

Natija na Matunda ya Dhana Nzuri

Kama vile ambavyo utulivu wa mwili husumbuliwa na aina mbalimbali za maradhi, vivyo hivyo, utulivu wa fikra na akili husumbuliwa na vitu mbalimbali, tabia na sifa mbaya. Kwa sababu fikra, licha ya kuwa na nguvu zote hizo, haiwezi kukua na kuimarika bila ya msaada wa maadili (akhlaki). Mtu huweza kuonja raha na furaha pale atakapofaidika na maadili wakati ambapo amali za kifikra zitakapokwenda sambamba na za kimaadili. Kwa hivyo, itambidi aazimie kwa nguvu kuing'oa katika nafsi yake mizizi ya tabia mbaya inayochafua na kuharibu maisha yake, na badala yake apande mbegu zitakazomzalia utulivu na raha.

Mojawapo kati ya mambo yanayosaidia kuleta utulivu wa fikra ni kuwa na dhana nzuri na kuwaamini watu. Kwa wale wanaoingiliana na watu, dhana nzuri ni aina moja ya dhamana na matumaini. Kinyume cha dhana mbaya ambayo huzuia vipawa vya kifikra na

47

hupunguza uwezo wa kujikamilisha, dhana nzuri ni kama umeme unaong'aa katika kiza cha uhai na katika mwangaza wake upeo wa fikra hupanuka. Mapenzi ya kufanya mema hustawi katika moyo wa binadamu, na kwa njia hiyo hupatikana maendeleo katika mtazamo wake wa dunia. Katika mtazamo wake mzuri, dunia huiona ina rangi yenye kumvutia zaidi, na vitu vyote na watu wote huwaona katika mwangaza na huwaamua kwa haki. Mtu akiwa na dhana nzuri, hupungukiwa na ghamu na taabu na huzidiwa na matumaini na matarajio, na kutokana na athari ya sifa hiyo huweza kuhifadhi vizuri uhusiano wake wa kidhahiri, kiroho na kimapenzi pamoja na watu mbalimbali katika jamii.

Hakuna kitu chochote kinachoweza kupunguza mzigo wa matatizo ya maisha ya mtu kwa kadiri ambavyo dhana nzuri inavyoweza. Mwenye kuwa na tabia hii njema si tu kwamba alama ya furaha na maridhawa huonekana katika sura yake, bali hata wakati anapokumbwa na mabaya na roho yake inaposumbuka huweza kwa urahisi kuikunjua sura yake na kukabiliana na matatizo hayo kwa fikra sahihi na kwa nguvu ya matumaini. Hivyo, roho ya mwenye dhana nzuri humulika miali ya matumaini na nishati.

Kuna haja ya lazima kupata imani ya watu mbalimbali katika maisha yao. Ili imani ipatikane kati yao, ni lazima nafsi ya dhana nzuri iwe ni sehemu ya maingiliano na utaratibu wa maisha yao. Na huu ni ukweli wenye athari ya moja kwa moja katika ufanisi wa mtu na jamii. Kuaminisha au kutoaminisha ni mojawapo kati ya  mambo yanayoimarisha au

48

yanayovunja jamii. Maingiliano na mawasiliano kati ya watu yanapokuwa imara na madhubuti zaidi, ndivyo maendeleo ya jamii yanavyostawi na kuendelea zaidi. Kuzidi roho ya kuaminiana na kushirikiana, na kuungana nyoyo za watu, ni matunda ya kwanza ya kijamii ya dhana nzuri. Maisha ya masikilizano yaliyosimama juu ya msingi wa mapenzi makubwa yanawezekana kupatikana kama watu wataaminiana na kudhaniana vizuri. Kinyume chake, ikiwa katika mazingira moja watu hawatakuwa na dhana nzuri na watatazamana kwa macho ya shaka na wasiwasi, msingi wa ushirikiano hautakuwepo hapo, hivyo, watakuwa wakitatizana katika mambo madogomadogo na wakisumbuana. Hapana shaka kwamba jamii kama hiyo itaonekana ikizorota na ikipungukiwa na athari na matunda yenye manufaa.

Mwanachuoni mmoja amesema:

"Sura dhahiri ya dhana nzuri ni imani, na hakuna kazi yoyote inayoweza kufanyika bila ya kuwepo imani na kuaminiana."

Kila mtu anavyozidi kuwaamini wenzake ndivyo imani yao juu yake inapozidi pia. Na hii ni radiamali ya kawaida inayotokea katika maisha. Lakini tusije tukasahau kwamba kuna tofauti kubwa baina ya kumdhania mtu vizuri na kuwa mwepesi katika kumwaminisha mtu. Kumdhania mtu vizuri hakumaanishi kwamba umwamini mara moja mtu usiyemjua, au uamini maneno ya wengine bila ya kuhakikisha au kuwachungua. Isitoshe, hatuwezi kuwaingiza katika suala la dhana nzuri wale watu

49

ambao wanajulikana waziwazi kwa uchafu na uhalifu wao. Kwa ufupi, dhana nzuri si msingi usiokuwa na sharti hata kwamba ungewezwa kutekelezwa kwa mtu yeyote katika hali au masharti yoyote. Ingawa dhana nzuri huwapa watu mtazamo mwema juu ya wengine na huwaonyesha matendo yao katika njia sahihi, lakini kwa wakati huohuo huwatahadharisha wawe waangalifu katika mwendo na matendo yao, na wazingatie matokeo ya kila jambo. [Kwa hivyo, inampasa kila mtu amwamini mwenziwe na awe na dhana nzuri juu yake, lakini kwa wakati huohuo awe macho juu ya tabia yake na aangalie vitendo vyake.]

Uislamu Huhimiza Msingi wa Dhana Nzuri

Uislamu kwa kutia nishati ya imani katika nyoyo za wafuasi wake, huhimiza na huimarisha msingi wa kudhaniana vizuri na kuaminiana kati ya watu; na kwa njia hiyo huuelekeza mwendo wa jamii katika mazingira yanayofaa na yaliyojaa itibari na utulivu. Mtume Mtukufu SAW alikuwa na sifa hiyo kwa kadiri fulani, hata kwamba wanafiki walitaka kumtuhumu kwamba Mtume alikuwa mwepesi wa kuamini na kusadiki. Sifa nzuri hii ilikuwa ikionyeshwa na wanafiki kuwa ni ya kuchukiza.

Ni wajibu kwa kila Mwislamu amdhanie vizuri Mwislamu mwenzake, na aitazame amali ya mwenzake kwa njia sahihi na ya kisheria. Haruhusiwi mtu yeyote kuchukulia kitendo fulani cha Mwislamu kuwa ni kibaya

50

na cha kifisadi kama hana ushahidi madhubuti na wa dhahiri.

Imam Ali AS amesema:

"Chukulia jambo la ndugu yako [wa imani] kwa maana nzuri kabisa mpaka ulione kinyume chake wala usilidhanie vibaya neno analolitoa ndugu yako wakati kuna uwezekano wa kuwa sahihi na kheri."

(Jami'u 's-Sa'adaat, jz. 2, uk. 28)

Matunda mojawapo ya dhana nzuri ni kupatikana urafiki wa watu na kuwepo mapenzi na usafi wa moyo.

Amirul Muuminin Ali AS ametaja matokeo na matunda ya dhana nzuri katika maneno yake mbalimbali. Kwa mfano, amesema:

"Mwenye kuwadhania vizuri watu hujifaidia mapenzi yao."

(Ghuraru 'l-ffikam, uk. 687)

Dk. Marden amesema:

"Unapokutana na mtu yeyote jaribu utazame uzuri wa sifa, tabia na moyo wake tu, na sifa na tabia nzuri hizo zifanye kubwa zaidi katika moyo wako. Ikiwa utaweza kuweka jambo hili moyoni mwako, basi maisha yako yatakuwa yenye furaha zaidi, na kila mtu atakuonyesha uso wa maridhawa na moyo safi na atajaribu kufanya urafiki nawe."

(PimziFikr)

Kumdhania mtu vizuri na kumwamini huenda kukabadilisha hata tabia na fikra ya mtu mwovu, na kukawa ni sababu mojawapo inayoweza kurekebisha

51

tabia zake.

Imam Ali AS amesema:

"Dhana nzuri humwokoa mwenye kufuata madhambi."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 378)

Dk. Dale Carnegie amesema:

"Hivi karibuni nilionana na meneja mmoja wa shirika la mikahawa. Shirika hilo ni la umoja wa mikahawa 26 linaloitwa 'Biashara ya Heshima' kutokana na uendeshaji wake mahsusi. Katika mikahawa hiyo iliyoanzishwa tangu mwaka 1885, washitiri hawapewi bili kabisa. Kila kitu unachotaka unaagizia, kisha wewe mwenyewe unafanya hesabu ya chakula ulichokula, na wakati wa kutoka unalipa pesa kwa keshia na unakwenda zako bila ya kuchunguzwa, kutolewa risiti au kuulizwa kitu. Kutokana na mshangao wangu nikamwuliza meneja: 'Hapana shaka una wachunguzi wa siri, kwani utawezaje kuwaamini washitiri wote?' Meneja akasema: 'Hapana! Sisi hatumweki mchunguzi yeyote, lakini kwa kadiri hii tunajua kwamba uendeshaji wetu ni sahihi kwa jumla, kama si hivyo isingewezekana kuendelea zaidi ya nusu karne.' Katika mikahawa hiyo, kila mshitiri huhisi kwamba yeye ni mtu mwenye heshima na ni mzuri. Kwa sababu hii, maskini, tajiri, mwizi na mwombaji hutaka wawe ni watu wenye kustahiki kuaminiwa.

"Bwana Louis ambaye ni mtaalamu mzoefu katika fani hii amesema: 'Ikiwa utakuwa na kazi na mtu laghai na utataka umwongoze na urekebishe tabia yake, basi

52

mfanye akuhisi kuwa unamwamini au mshughulikie kama ni mtu mheshimiwa na mtukufu. Utaona kwamba mtu huyo atavutika sana kwa kuaminiwa kwake kwa kadiri kwamba atajaribu astahiki sifa hiyo.' "

Bw. Gilbert Roben amesema:

"Mwamini mtoto kwa kuendeana naye kwa namna ambayo kana kwamba hakutenda kosa lolote. Kwa maana nyingine, jaribu kumpa wadhifa muhimu mtundu, au mchafu asiyefuata maagizo ya afya ya umma, au hata mhuni anayevuruga nidhamu ya watu. Hakikisha kwamba mwendo wake umekuwa bora baada ya kupewa wadhifa huo mpya na kwamba anastahiki kwelikweli kuaminiwa kwake. Inawezekana kuondoa vikwazo kwa kuwaamini na kuwatendea watu vizuri. Kwa hivyo, tunaweza kusema kwamba vitendo vingi visivyopendeza ni radiamali kujibu hali au maisha waliyokabili watu hao. Sir Yale Burt amependekeza njia bora za mwendo wa tabia. Yeye anaamini kwamba ni lazima mtoto mwizi apewe pesa kama amana; na mtu anayependa kufanya uhuni apewe kazi itakayochangamsha mwili wake na itakayolingana na raghba yake."

Dhana nzuri hutuliza moyo wa mtu, kama alivyosema Imam Ali AS:

"Dhana nzuri ni raha ya moyo na usalama wa dini." (Ghuraru 'l-Hikam.uk. 376)

Dhana nzuri humpunguzia mtu taabu na matukio mabaya.

Imam Ali AS amesema:

53

"Dhana nzuri hupunguza majonzi."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 377)

Dk. Marden amesema:

"Hakuna kitu kilicho sawa na dhana nzuri kinachoweza kufanya maisha yawe mazuri zaidi, kupunguza taabu na kuleta mafanikio kwa mtu. Ogopa fikra zinazotia huzuni kama vile unavyoogopa maradhi na athari za hatari. Fungua milango ya fikra zako kwa ajili ya fikra nzurinzuri. Kwa njia hii utashangaa utakapoona jinsi ulivyokata kwa urahisi minyororo ya fikra nyeusi."

(PimziFikr)

Ni lazima Waislamu waendeane kitabia kwa namna ambayo haitaota mizizi ya dhana mbaya katika jamii. Kwa sababu hii, Imam Ali AS ameusia kwamba kila mtu amdhanie vizuri mwenzake, na ikiwa watu wengine watakuwa na dhana nzuri juu yako, basi angalia mwendo wako usije ukaharibu hisia yao ya dhana nzuri waliyonayo juu yako, na ukasababisha wakudhanie vibaya. Imam amesema haya:

"Mwenye kuwa na matumaini juu yako huwa amekuamini na kukudhania vizuri, hivyo usiharibu dhana yake (ukamvunja moyo)."

(Ghurani 'l-Hikam, uk. 680^

Imam Ali AS amefanya mawazo na dhana za watu kuwa ni kiegezo cha kupima akili yao, pale aliposema:

"Dhana ya mtu ni mizani ya akili yake, na kitendo

54

chake ni ushahidi wa kweli kabisa wa dhati yake."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 74)

Kutojali mawazo mabaya na kutoshughulika na dhana mbaya ni alama ya nguvu za kiroho na utulivu wa moyo.

Imam Ali AS amesema:

"Mwenye kutojali dhana mbaya juu ya ndugu yake, huwa ana akili timamu na moyo mtulivu."

(Ghurani 'l-Hikam, uk. 676)

Samuel Smiles amesema:

"Imethibitishwa kwamba kila mtu mwenye kuwa na maumbile madhubuti na roho kubwa, basi huwa ni mtu mchangamfu na mwenye furaha na matumaini; na huangalia kila kitu na kila mtu kwa jicho la kuaminisha na dhana nzuri. Wenye busara na tafakuri huona jua na mwangaza nyuma ya mawingu mazito na meusi; huona matumaini na ufanisi nyuma ya kila mashaka na msiba;

hupata nguvu mpya kutoka kila uchungu na taabu, na hupata matumaini na maarifa mapya baada ya kila ghamu na majonzi. Maumbile hayo huleta bahati nzuri na mafanikio kwa wenye kuwa nayo, na hapana shaka hujivunia nayo, kwa sababu katika macho yao huonekana nuru ya furaha, na pembezoni mwa midomo yao huonekana tabasamu ya kifalsafa. Nyoyo za watu hao hung'ara kama jua, na kila wanachokitazama hukiona kinang'ara na kinametameta rangi kwa rangi."

Imam Sadiq AS anahesabu dhana nzuri kuwa ni miongoni mwa haki za Mwislamu mmoja kwa mwenziwe, pale aliposema:

"Miongoni mwa haki za muumini kwa muumini

55

mwenzake ni... kutomkadhibisha (kumsadiki)."

(Usulu 'l-Kafi, ]z. 1, uk. 394)

Nguvu muhimu kabisa inayosababisha mtu awe na dhana nzuri ni imani. Ikiwa watu watakuwa na imani kamili, hapana shaka wataaminiana. Utovu wa imani ni maradhi mabaya yanayoondoa dhana nzuri katika watu na badala yake yanaweka dhana mbaya mahali pake. Mwislamu wa kweli na mwenye dhana nzuri huwa anamtegemea na anamtumainia Mola wake tu, hivyo, wakati anapohisi kuwa hana nguvu na uwezo, hutegemea uwezo wa juu na ulio bora zaidi kuliko wake. Wakati wa mashaka na matatizo hutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu ambaye ni chimbuko kubwa kabisa la nguvu na uwezo. Na jambo hili ndilo linalomwathiri sana katika kurekebisha na kusafisha roho na maadili yake.

3 - DHANA MBAYA

59

Hali Angavu na Kiza katika Maisha

Maisha ya binadamu yamechanganyika taabu na raha. Kila moja katika hali mbili hizo huathiri maisha na umri mfupi wa binadamu. Kila mtu kwa upande wake hukabiliwa na matukio, matatizo na masaibu mbalimbali, na kutokana na ukweli huo usioepukana katika maisha ya mtu, daima huwa katika mabadiliko baina ya shida na raha.

Sisi hatuwezi kuibadilisha sheria hii ya daima ya dunia na kuifanya namna tunayoipenda. Lakini baada ya kuelewa uhakika na maana ya maisha, tunaweza kuuelekeza mtazamo wetu kwenye upande mzuri wa vitu na matukio ya ulimwengu, na tukayaondoa mambo yasiyopendeza katika uso mpana wa dunia iliyojaa mazuri kwa kuzingatia maana mahsusi na uzuri unaovutia wa kila kilichoumbwa (hata kama kinaonekana ni kibaya kwetu). Kwa upande mwingine, katika kukabiliana na hali hiyo, tunaweza kuvisahau vipengee vinavyong'ara na kupendeza vya vitu na tukavizingatia vipengee vyake vinavyochusha na vyenye weusi. Kwa ufupi, kila mtu ana uwezo wa kuielekeza fikra yake upande wowote anaoutaka na kuipaka rangi anayoipenda.

Inabidi tujiandae kukabiliana na matatizo yanayotatiza mwendo wa maisha kwa kujidhibiti nafsi zetu. Tusipofanya hivyo, tutapata hasara kubwa isiyoweza kufidiwa, na huenda tukazama katika matukio

60

hayo.

Baadhi ya watu wanadhania kwamba lau matukio ya dunia yangetokea katika sura nyingine, wangekuwa na furaha na ufanisi. Ukweli ni kwamba matatizo ya watu hao hayahusiani na matukio hayo, bali ni namna gani wanavyokabiliana nayo. Inawezekana kuzibadilisha athari za matukio hayo katika nyoyo za watu kwa kupatikana faida na mafanikio badala yake. Mwandishi mmoja mashuhuri ameandika:

"Fikra zetu haziko radhi daima. Haturidhiki katika kila hali. Chimbuko la manung'uniko hayo ni dhamiri zetu. Nafsi ya mwanadamu imeumbwa kwa namna ambayo daima mwili na roho yako huteseka kutokana na kukosa utulivu. Kila siku tunataraji matumaini mapya bila ya kujua tunataka nini na tunatamani kitu gani. Tunadhani kwamba wengine wana raha, hivyo, tunawaonea wivu na tunajiunguza roho zetu. Tunajifanya kama mtoto mdogo anayetafuta kisingizio cha kulia na kukasirika. Mtoto huyo hukera roho zetu kwa kulia kwake, na hatuwezi kupumua na kupata raha mpaka tumfanye aelewe ukweli na aache tabia mbaya hiyo. Ni lazima tumfumbue macho ya mtoto huyo aone mazuri, kwa sababu kwa kujitakia mengi amejifanya anaona mabaya tu. Ni lazima tumfahamishe kwamba kila mwenye kufumbua macho yake katika bustani la maisha atachuma maua, na kila atakayefumba macho yake atachuma miba. Ikiwa tutaacha tutuo na dhana mbaya na tutafumbua macho kutafiti, tutaona kwamba katika kila zama, na hata katika zama hii ambapo dunia imezama katika matope ya kutisha na maisha yetu

61

yamechafuliwa na tufani, zuri na baya na safi na chafu yanaenda vyema. Naam, maua mazuri na yenye kuvutia yamejaa katika bustani la maisha ambayo yanayavutia macho yenye kuona."

Mawazo na fikra zina athari kubwa katika furaha ya mtu, na kitu cha pekee kinachoathiri ufanisi wa mtu ni kiwango cha akili na fikra zake. Tukio au ajali isiyotazamiwa ikimfikia mtu mwenye dhana mbaya huiona ni kubwa, isiyoweza kuvumiliwa na hanbifu. Lakini mwendo wa mtu mwenye kuyatazama mambo kwa dhana nzuri na huona mazuri badala ya mabaya, hutegemea msingi wa "kujitolea" anapokabiliana na misukosuko na masaibu, na hashindwi kuvumilia hata akikabiliwa na misiba mikubwa. Mwenye dhana nzuri hapotoki kwenye njia ya wastani na utulivu. Wale waliozoea kujifikiria kwamba chanzo cha bahati mbaya na balaa ni wao wenyewe, huishi maisha ya kiza na yaliyojaa taabu. Kutokana na tabia zao za kuathirika sana mbele ya misukosuko, hupoteza burebure nguvu na vipawa vyao, hujinyima na hujikosesha neema na baraka zilizoenea duniani.

Mwanachuoni mmoja amesema:

"Dunia huamiliana sawasawa na binadamu. Ukicheka, itacheka nawe. Ukinuna, itakununia. Ikiwa utakuwa mwanafikra, basi utakuwa pamoja na wanavyuoni na wanafikra. Na ukiwa mpole na mnyofu, utawaona wako watu pamoja nawe ambao hukupenda na hukufungulia hazina za mahaba ya nyoyo zao!"

Ingawa maumivu na masaibu yanaonekana kuwa ni machungu na mabaya, lakini hutoa matunda mahsusi na

62

manufaa kwa ajili ya fikra na mawazo. Vipawa vya kiroho vya mtu hudhihirika waziwazi katika kiza cha taabu. Katika misukosuko hiyohiyo na kujitolea daima huko ndipo akili na roho hupanda na kufikia kwenye kilele cha ukamilifu wa utu.

Madhara ya Dhana Mbaya

Dhana mbaya ni mojawapo kati ya maradhi ya hatari ya roho na ni chanzo cha hasara nyingi, kuvunjika moyo na kukata tamaa. Dhana ni msiba unaochoma ambao huitesa roho ya mtu na athari yake haiondoki katika shakhsia ya mtu. Taabu na dhiki ni kiini cha hatari, na huenda dhana mbaya imeanzia hapo na kusababisha tufani na mapinduzi makubwa katika hisia za mtu. Mbegu ya dhana mbaya ambayo kwa njia hiyo hupandwa katika shamba la moyo, huzaa matunda machungu na mabaya katika fikra na mawazo ya mtu.

Yule ambaye kioo cha roho yake kimefunikwa kwa mavumbi ya dhana mbaya, licha ya kutoonekana uzuri wa maumbo, hata furaha (saada) pia hubadilisha sura yake na kuonekana kama dosari na doa. Mwenye kuwa na dhana mbaya hutazama mwendo wa mtu mwingine kwa chuki na shaka. Watu kama hao ambao nyoyo zao zinashuku huwa hawana vipawa vilivyo safi, na kwa sababu hiyo daima hujitia mashakani kutokana na dhana zao mbaya; na hata wakati mwingine hujitia wasiwasi na kihoro juu ya ajali ambayo huenda hakuipata kamwe!

Kama ilivyo kwamba taathira za mtu mwenye

63

matumaini na nishati huwaathiri walio karibu naye na wote hupata moyo kutokana na moyo wake mkubwa na matumaini, vivyo hivyo, mtu mwenye dhana mbaya huwakera na huwatia wasiwasi walio karibu naye na huwapokonya mwanga wa matumaini ambao humulika njia zinazopindapinda za maisha!

Athari mbaya za dhana mbaya hazikomi katika roho tu, bali pia huuathiri mwili vibaya na hufanya vigumu matibabu ya maradhi yake.

Daktari mmoja mashuhuri amesema:

"Ni taabu zaidi kumtibu mtu mwenye kumpinga (kumdhania vibaya) kila mtu na kila kitu kuliko kujitahidi kumwokoa mtu aliyeamua kujiua kwa kujitosa baharini. Kumpa dawa mtu ambaye anaishi maisha ya huzuni na wasiwasi ni sawa na kutia maji katika mafuta ya zeituni yanayochemka. Kwa Sababu, ili dawa iwe na athari na faida, inapasa mgonjwa awe na moyo wa matumainina utulivu wa fikra!"

Hali ya kujiweka kando na kutoingiliana na watu, mara nyingine huonekana waziwazi katika mwendo wa mtu mwenye dhana mbaya. Kutokana na mwendo huo usiofaa, mtu huyo huviangamiza vipawa vyake vyenye kumstawisha na kumwendeleza, na matokeo yake ni kujiangamiza katika maisha ya huzuni na yasiyofaa. Mojawapo kati ya sababu inayomfanya mtu ajiue ni kutawaliwa na dhana mbaya katika fikra na roho yake. Uamuzi wa kutenda dhambi hiyo isiyosamehewa aghlabu yake hutokana na sababu hiyo.

Ukiangalia hali ya jamii moja, utaona kwamba maneno mengi wanayosema watu wenyewe kwa

64

wenyewe huwa hayakuchunguzwa wala kuzingatiwa bali yanatokana na dhana mbaya na kushuku. Ingawa uwezo wao wa kuamua kwa haki ni dhaifu, lakini juu ya hayo wanatoa uamuzi wao wa mwisho bila ya kuhakikisha sawasawa na kuwa na yakini, na matokeo yake aghlabu hukosea katika uamuzi wao wasiochungua kabla yake. Na mara nyingine chuki zao binafsi zinadhihirika waziwazi katika maneno yao. Ila hii kubwa ndiyo inayosababisha kuvunjika umoja wa kidhati na kutokuwepo hali ya kuaminiana ambayo kwayo huharibu sifa zao njema za kitabia na kiroho.

Baadhi ya uhasama na uadui ambao madhara yake juu ya mtu na jamii hayawezi kutengenezeka unatokana na kudhania juu ya jambo moja kinyume na ukweli wake.

Dhana mbaya hupenya katika matabaka mbalimbali ya jamii, na hata huzishughulisha fikra za wanavyuoni na wanafalsafa. Katika awamu tofauti kati ya kila kaumu na taifa, wametokeza wanavyuoni ambao kutokana na kuwa na dhana mbaya, wamefanya makosa makubwa katika tafakuri ya jamii. Badala ya kutumia elimu na maarifa yao na kuhudumia jamii ya watu, wameimarisha itikadi zao juu ya msingi wa kuupinga na kuukosoa mfumo wa uumbaji. Kutokana na fikra zao potofu na zenye madhara, wanavyuoni hao wametia sumu roho ya jamii na wakaichezea shere misingi yao ya kiitikadi na kimaadili.

Kuona vibaya kwa baadhi yao kulifikia hadi hii kwamba waliogopa kuongezeka kwa idadi ya watu na kuzidi umaskini, na kwa sababu hiyo wakaruhusu

65

kutumia kitu chochote kitakachozuia kuzidi kwa watu hata ikiwa ni kwa kuwaua watu na kumwaga damu ili mradi watu wapungue duniani. Hapana shaka kwamba kama watu wa dunia wangefuata fikra zao za sumu, basi leo hakungebaki athari yoyote ya elimu na ustaarabu.

Abul 'Alaa' alikuwa ni mwanafalsafa mashuhuri aliyekuwa na dhana mbaya. Msingi wa fikra zake ulikuwa dhana mbaya na aliamini kwamba maisha yote yamejaa taabu na adhabu. Yeye aliharamisha kuoana na kuzaliana ili jamii ya wanadamu imalizike. Inasemekana kwamba alipokuwa akikata roho, aliusia jumla hii iandikwe kwenye jiwe la kaburi lake:

"Kaburi hili ni athari ya jinai aliyonifanyia baba yangu, lakini mimi sikumfanyia jinai mtu yeyote!"

Uislamu Wapinga Dhana Mbaya

Our'ani Tukufu inasema waziwazi kwamba dhana mbaya ni dhambi, na inawatahadharisha Waislamu wajiepushe na kudhaniana dhana mbaya:

"Enyi mlioamini! Jiepusheni sana na kuwadhania watu dhana mbaya, kwani kuwadhani watu dhana mbaya ni dhambi."

(al-Hujaraat, 49:12)

Mafundisho ya kidini yanamkataza mtu mmoja kumshuku na kumdhania vibaya mtu mwingine bila ya kuwa na ushahidi kamili.

Mtume Mtukufu amesema:

"Mwenyezi Mungu amewaharamishia Waislamu

66

vitu vitatu: damu zao, mali zao, na kudhaniana vibaya.'

Kama ilivyo kwamba si halali kutoa hukumu ya kuhawili mali ya mtu mmoja kwa mwingine bila ya kuwa na ushahidi wa kutosha, vivyo hivyo, kuhusu dhana mbaya hakuruhusiwi kumshuku mtu yeyote kwa urahisi na kumtuhumu pasina kuthibitika jambo.

Imam Ali AS amesema:

"Si uadilifu kutoa hukumu kwa kutegemea dhana." (Nafiju 'l-Balaghah, uk. 1174,)

Kwa kutumia ibara tofauti, Amirul Muuminin Ali AS ametaja kwa ufasaha madhara ya dhana mbaya, sababu za kinafsi na ufisadi wa roho:

"Jihadhari na kudhania vibaya, kwani dhana mbaya huharibu ibada na huifanya dhambi kubwa zaidi."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 154}

Vilevile amesema kwamba kuwadhania vibaya watu wanyoofu ni aina moja ya udhalimu:

"Kumshuku mtu mwema ni dhambi mbaya kabisa na ni udhalimu unaochukiza sana."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 434)

Kuwadhania vibaya marafiki husababisha uhusiano uharibike na mapenzi yaondoke.

Imam Ali AS amesema:

"Mwenye kutawaliwa na dhana mbaya hakubakii amani baina yake na rafiki yake."

(Ghuraru 'l-Hikam, uk. 698,)

67

Licha ya dhana mbaya kuwa na athari katika roho na maisha ya mtu mwenyewe, hata pia ina athari mbaya juu ya roho na maadili ya watu wengine.

rudi nyuma Yaliyomo endelea