rudi maktaba >Maadili >

Rudi nyuma Yaliyomo  

Ewe mwanamke mu’umin!

Ewe Mtetezi wa Mwenyezi Mungu, usiwe na kipenzi ila Mwenyezi Mungu, kwani yeye humpenda yule ajipendekezaye kwake. Na ufunge milango yako ya duniani ili Mwenyezi Mungu akufungulie milango ya mbinguni! Wacha maneno ya kipuuzi, wacha matamanio na ujue ya kwamba hakuna uokovu mwingine ila wa Mwenyezi Mungu tu na Mugu hana khiyana yeye ndiye mbora, mwenye kunusuru, kata uhusiano wako wa upuuzi na ufanye uhusiano na jihadi na kina dada wana-dini.

Heshimika na hijab yako na uifanye kuwa ndiyo silaha ya kuwapinga mataghuti wanao kutaka uwe kama mwanaserere (kijisanamu). Ukiwa na hijab yako, geuka uwe mwangaza wa uchagamfu, kwani hijab siyo jela na kaburi la kuzikia uwezo wako, bali ni njia ya kuwa huru na kutenda. Usitosheke na kuwa mtumwa mwenye thamani tu, bali uwe mwenye nafasi yenye thamani.

Zielewe mbinu za mataghuti za kusaga shaksiya ya mwanamke, kwani mbinu zake ni chafu na zenye mizunguko mingi, mara nyingi hutumiwa mbinu zitakazofurahisha kuliko zitakazochukiza. Taghuti ni bidhaa isiyochoka ya Iblis. Taghuti hutumia vitimbi, mizunguko na udanganyifu, yeye huyachochoea matamanino ili azivunje heshima, na anasa ili kuivua heshima na hutumia ngoma na muziki ili kuiba imani za ucha Mungu. Na ili uihifadhi heshima yako, basi ni lazima upambane na njia potofu ambayo ni nafsi inayoamrisha maovu na utahadhari na matamanio yako. Kisha jiulize: ni mwanamke gani anayeogopewa na taghuti? Je! Ni yule ambaye asubuhi akitafuta virembesho, marinda mazuri na hutoka akiwaonyesha watu wenye “Kiu” mapambo yake? Au ni yuke anayekwenda kwenye duka la vitabu akatafuta magazeti yenye fedheha na visa vya uongo vya mapenzi? Au je ni yule anapokuwa kwenye sherehe ataka awe mithili ya tausi akiringia nakshi za nguo zake na alivyotengeza nywele na mipaka ya muhimu kwake ni Jiografia ya mwili wake tu (alivyoumbika)? Au mwanamke anayeogopewa na Taghuti ni yule mpiganaji jihadi anayetafuta medani ya mapambano, kama kipepeo atafutaye ngome ili awe kama askari mwenye tahadhari.

Usiabudu virembesho na mapambo, kwani wewe ni mkuu kuliko chupa ya manukato au mti wa kupakia wanja, au kitambaa cha rinda, na fahamu ya kuwa uzuri wa roho ndio wanaowaunganisha watu na si uzuri wa mwili. Jipambe na tafakuri na hisia zako zitie huruma kwa familia maskini, kwani moyo ni kama mmea, mtu asipouangalia kwa huruma na upole utakufa.

Tahadhari sana na kushindwa, kwa sababu silaha kubwa ya mkoloni ni kushindwa kwa watu, yaani ndiko kushindwa kwa mwanamke; na ikiwa mwanamke ameshindwa, ni kizazi gani basi kitakacholelewa ila kitakuwa ni kizazi cha walioshindwa tu?

Kuwa ni mwenye kutengeza mustakbali, na uingie kwenye mapambano ya kishujaa, kwani jihadi ni wajibu wako wa kimsingi na zama hizi tunazoishi ni zama za hujuma za kikafiri dhidi ya uislamu, kwa hivyo kujilinda hakuhitaji ruhusa!

Shiriki kwenye mipango na wanaume, kwani si haramu kuzungumza na wanaume na kukaa nao maadam muko katika njia ya Mwenyezi Mungu na uchunge heshima ya kisharia.

Mbele ya mataghuti: toa hoja ya nguvu, kataa, piga kelele. Kumbuka kuwa mataghuti wengi wameanguka kutokana na upinzani wa kina Zainab na mikono yao ya chuma.

Toka kwenye upenu wa khofu uliotiwa na vibaraka wa wakoloni, au kulala na kuzunguka jikoni tu kama wanavyokutaka uwe.

Ewe mwanamke mu’min!

Wakati tunaposoma Qur’an tukufu kuhusu mwanamke tunapata ukweli ufuatao:

Mwanamke na mwanamume kwa pamoja wana jukumu la kuchunga nafsi na watu. Mwenyezi Mungu amesema:

“Waambie waislamu wanaume wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao, bila shaka Mwenyezi Mungu anazo habari za (yote) wayafanyayo. Na waambie waislamu wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao.”

(24: 30-31)

Kwa hakika mwanamke na mwanamume ni vipenzi wao kwa wao, mwanamume yampasa amthamini mwanamke na kumtakia mema, na mwanamke pia afanye hivyo hivyo.

“Na waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki (vipenzi) wao kwa wao. Huamrisha mema na hukataza mabaya, na husimamisha Swala na kutoa Zaka na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake; hao ndio Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.” (9:71)

Mwanamke na mwanamume wana haki ya kupata sawa kulingana na wajibu wao watakaoutekeleza, na Mwenyezi Mungu anahifadhi haki ya mwanamke kama anavyohifadhi ya mwanamume, kama alivyosema katika Qur’an:

“Na watakaofanya vitendo vizuri wakiwa ni wanaume au wanawake hali wao ni wenye kuamini, basi hao wataingia peponi wala hawatadhulumiwa hata kokwa (konde) ya tende.” (4:124)

Amesema tena Mwenyezi Mungu:

“Mola wao akawakubalia (kwa kusema): “Hakika mimi sitapoteza amali ya mfanya juhudi miongoni mwenu awe mwanamume au mwanamke” (3:195)

“Wafanya wema wanaume au wanawake hali ya kuwa ni waislamu, mtawahuisha maisha mema, na tutawapa ujira wao (akhera) mkubwa kabisa kwa sababu ya yale mema alilyokuwa waliyatenda.”

(16:97)

“Siku utakapowaona waislamu wanaume na waislamu wanawake, nuru zao zitakwenda mbele yao na kuliani kwao (wanaambiwa): “Furaha yenu leo (mnapewa) mabustani yapitayo mito mbele yake kukaa humo daima, huku ndiko kufaulu kukubwa”

(57:12)

Hapana tofauti kati ya mwanamume na mwanamke katika uharamu wa kuingilia haki zao. Mwenyezi Mungu amesema:

“Na wale wanaowaudhi waislamu wanaume na waisalmu wanawake pasipo kosa lolote, bila shaka wamebeba adhabu ya Jahannam na watapata adhabu ya kuungua.” (85:10)

“Hakika wale waliowaadhibu (kuwaudhi) waislamu wanaume na waislamu wanawake, kisha wasitubie, basi watapata adhabu ya Jahannam na watapata adhabu ya kuugua.” (85:10)

Na kuna Aya nyingi ambazo kwanza Mwenyezi Mungu anazungumza na Mtume wake juu ya mwanamke mwislamu, akimtaka Mtume akubali kuahidi kwao kubeba majukumu, amesema (s.w.t.):

“Ewe Nabii! Watakapokuja wanawake walioamini wanaokuahidi ya kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba wala hawatazini, wala hawataua watoto wao, wala hawataleta uzushi wanaozusha tu wenyewe baina ya mikono yao na miguu yao wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana ahadi nao na uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghfira, mwingi wa rehma.”

(60:12)

Ingia kwenye sehemu yako aliyoitaka kwako Mwenyezi Mungu ya ukhalifa wa dunia na kujenga maisha na usingoje wanaume wakwambie la kufanya katika kutetea na ujipatie nguvu za wanaume kwa uthabiti wao. Na uizuwie dhulma ya wanaume kwa matakwa yao; na ujue ya kwamba mwanamke anaweza kufanya mambo mengi na kutoa mchango wake katika mambo mema. Na mwanamke ni mtukufu pale anapojuwa kuwa yeye ni mtukufu.

Pambana na ada na desturi potofu za kijamii ambazo Mwenyezi Mungu hakuteremsha uhalali wake hasa zifanywazo katika nyanja za kijamii k.v. kwenye harusi ambapo mwanamke hukubali bei rahisi au kujiuza kwa vitu vya anasa tu. Fikiri sana juu ya mali ya mumeo, ibadilishe hali yake, mwenendo wake, badili washirika wake wasiofaa, na katika mali yake badilisha mfumo wake.

Kazi yako si kulea watoto tu, kama wasemavyo, bali kazi hiyo ni jukumu lako na mumeo, wajibu wako ni kama ule wa mwanamume katika nyanja zote. Usikubali kuchukua nafasi ya pili kuwekwa pembeni; ondoa fikra za kufuata. Jivishe vazi la uongozi usijiweke nyuma katika njia ya uongofu.

Muige mwanamke mtukufu katika Historia, muige bibi Maryam bint Imran, mamake Masih (Isa (a.s.)) mtetezi, mpambanaji aliyawakemea Waisrael. Au muige bibi Asya bint Muzahim, mke wa dikteta Fir’aun, mwanamke aliye muamini Musa (a.s.) na kufa shahid katika njia ya haki akikataa maisha ya anasa duni. Au uwe mfano wa bibi Khadija ambaye alimcha Mungu alimpa Mungu na cha kaizari pia alimpa Mungu! Aliyejitolea kwa hali na mali kwa ajili ya wakandamizwaji. Au pia uwe mithili ya bibi Fatima aliyehama (Hijra) akapambana kwa jihad, akakemea, akatoa hoja za nguvu na kuwanyima usingizi matapeli. Au pia jifanye kama bibi Zainab, sauti ya kimapinduzi iliyokata kusalimu amri kwenye huzuni, kukata tamaa na kutishwa.

Usikubali kuvunjwa moyo na nduguzo, jamaa zako au marafiki juu ya kufuata njia ya jihadi na kupambana na taghuti, kwani kumridhisha Mwenyezi Mungu ndilo jambo la kwanza kabla ya viumbe, na watu wako hawana mamlaka ya kupigana na hukmu ya Allah.

Jiweke kwenye kushiriki na wanaume na wanawake, na uwe na nafasi muhimu kwani lau kama Mwenyezi Mungu hakutaka mwanamke awe na nafasi muhimu asingemuumba mwanamume kwa njia ya mwanamke.

Uwe mume, pale panapokosekana mwanamume, kwani uume si mwili bali ni wa mwamko na msimamo. Wanawake wangapi wana nguvu kushinda wanaume elfu, na kuna wanaume wangapi walio madhaifu kuliko wanawake.

Kuwa mwana mapinduzi. Kuwa mpiganaji. Kuwa kila kitu lakini usiwe pambo la jikoni au godoro la kitandani au sahani iliyoangikwa ukutani, au sauti katika nyimbo, au picha ya kupamba ukurasa wa jarida.

Jisome sana, fikiri sana, kwani “Kufikiri saa moja ni bora kuliko ibada sabiini.”

Ukuze mwamko wa leo wa kisiasa kwa kusoma vitabu vya siasa, na kufuatilia matukio ya kila siku, kwani yule anayezijua zama zake na hali zilivyo, hawezi kuvamiwa na majanga na kushtuliwa na matukio.

Jizoeze mbinu za mapambano, kwani mwanamke mwislamu mwenye nguvu ni bora kuliko mwanamke mwislamu dhaifu, na hivyo hivyo mwanamume mwislamu mwenye nguvu ni bora kuliko asiye na nguvu.

Rudi nyuma Yaliyomo