Yaliyomo endelea

UCHUNGUZI WA KIHISTORIA JUU YA UKUSANYAJI NA UANDISHI WA HADITH

Kimeandikwa na: RASUL JA'AFARIYAN

Kimetarjumiwa na : AMIRALY M. H. DATOO

UTANGULIZI

Umuhimu wa Hadith katika maadili ya mafunzo ya Kiislamu – ikiwemo Tafsir, Fiqh (Sharia), na maadili, n.k.- unakubalika katika madhehebu yote ya Kiislamu. Leo itakuwa ni vigumu kumpata mtu yeyote yule aatakayekuwa akidai kuwa Qur’an Tukufu inajitosheleza kwa Shariah ya mafunzo ya Kiislamu pamoja na maelezo bila ya msaada wa Sunnah na Hadith. Zaidi ya hayo, yapo matamko mengi ya Mtume sa.w.w., na baadhi ya taarifa katika Qur’an yenyewe, ambazo zinaelekeza katika umuhimu wa amri na matendo ya Mtume s.a.w.w. Kwa hivyo ni dhahiri umuhimu uliopo juu ya Hadith na Sunnah za Mtume s.a.w.w., hivyo hapana shaka wala haja ya ushahidi kwa swala hili.

Madhumuni ya makala yafuatayo ni kuchambua na kutazama vile mfumo wa Hadith ulivyokuja kuandikwa na kutazama muda uliotumika kukusanya matamko (kauli), matendo (fi’l) na kukubaliwa kwa ukimya (taqrir) wa Mtume s.a.w.w. hadi kufikia katika sura ya ukusanyaji na uandishi. Ni dhahiri, swala hili linaweza kuwa na umuhimu wa kuchambua ushahidi wa mfumo wa Hadith.

Ama kuhusu swala la Qur’an, sisi twajua kuwa hapakuwapo na pengo la muda baina ya kufunuliwa Ayah za Qur’an na kuandikwa kwao.Vivyo hivyo, hapana shaka juu ya usahihi wa Qur’an, kwani Mtume s.a.w.w. alikwishawachagua waandishi kuanzia mwanzoni mwa ufunuo na hapo walipatiwa kazi za kuzikusanya na kuzindika. Hata hivyo, utaratibu huu haukutumika katika swala la Hadith, ambavyo imekuja kupokelewa vinginevyo.

Umuhimu wa hadith na daraka lake katika maswala ya kijamii na kisiasa vimesababisha baadhi ya makundi kuonyesha hali ya kiasi fulani cha kutovumilia kelekea hayo. Kutovumilia huku ndiko kuliko sababisha Hadith kucheleweshwa kusimuliwa na kuandikwa na kuenezwa. Na kwa masikitiko makubwa, kucheleweshwa huku kumeleta hali ya mtatanisho kwa ajili ya uthamini wake kwa vizazi vya baadaye.

Hata hivyo, ni lazima kutambulisha kuwa hali ya Hadith katika Shiah ilikuwa ni tosauti na ile hali ya Hadith za Ahl al-Sunnah . Tofauti hii inatokana na imani ya Mashiah kuhusu Uimamu wa Shia wa Ahl al-Bayt a.s. ambapo kuwapo kwao ulikuwa ukiendelea hadi katikati ya karne ya 3 A.H. / 9 A.D. Kwa hivyo, Hadith zilizonakiliwa na Mashiah hazikukumbwa na matatizo ya kucheleweshwa kwa kuandikwa.

Hapa sisi tutatazama kwa kimukhtasari sana uthibitishaji kuhusu swala hili, lakini sehemu kubwa ya uchambuzi huu utakuwa ukihusiana na historia ya uandikaji wa Hadith miongoni mwa zile za Ahl as-Sunna.

Historia hii inaonyesha kuwa Hadith zilikuwa hazikuandikwa kwa kioindi fulani. Siyo hayo tu, hata kuzieneza kwao pia kulipigiwa marufuku kwa muda fulani, kwa kipindi cha miaka mia moja. Ahadith (wingi wa Hadith) zilienezwa kwa desturi ya matamshi tu. Ingawaje sehemu ya Hadith ilianza kuandikwa katika karne ya 2 A.H. / 9 A.D., sehemu yake kubwa iliandikwa tu baada ya muda wa kutosha kupita.

Hapa sisi tutatazama kwanza Maimamu a.s. wa Kishia wakisisitiza uandikaji wa Hadith. Na baadaye tutachukua historia ya uandikaji wa Hadith miongoni mwa Ahlal-Sunnah. Uchunguzi wa aina hii utatusaidia kama mwongozo kwa ajili ya kuthamini misingi halali ya Hadith ya Madhehebu zote za Islam na kutudhihirishia ipi iliyo na ufululizo wa uandikaji wa Hadith (bila ya kuvunjika kwa mfululizo huo) Umuhimu mkubwa wa uchunguzi huu ni utamini kwa undani wa sanad na mutun (kiini) cha Hadith, jambo ambalo linalohitaji utafiti maalum ingawaje baadhi ya kazi kama hizi zimeshaandikwa juu ya somo hili, lakini bado kunahitajika juhudi zaidi katika uchunguzi kama huu.

Kwa kifupi, kitabu hiki ni mkusanyiko wa makala yaliyokuwa yakichapishwa katika jarida la Al-Tawhid J. V, II uk. 39-55; j. V, III & IV uk. 71-84 na VI, I uk. 19-35 – Sazmaan Tablighaat Teheran Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Niliona kuwa itakuwa ni kazi yenye manufaa iwapo nitayakusanya hayo na kuyatarjumu katika lugha ya Kswahili katika sura ya kitabu.

1. MAIMAMU WA SHIA KATIKA UANDIKAJI NA UENEZAJI WA HADITH

Katika sehemu hii, twategemea kuzungumzia kwa mukhtasari msimamo wa Shia kuhusu uandikaji wa Hadith kutokea mwanzoni. Itaonekana kuwa ni kinyume na msimamo wa wengine kuhusu swala hili. Msimamo wa Kishia ulisisitiza mno juu ya uandikaji wa Hadith zikisaidia uhifadhi wake wakati ambapo Maulamaa mashuhuri wa Kisunni, hata kufikia mwanzoni mwa karne ya 3A.H./9 A.D. walikuwa wakipinga uandikaji wa Hadith. Ni baada ya uandikaji wa Hadith ulipokuwa dhahiri hao wanaopinga walipoanza kwenda kinyume na Hadith walizokuwa wamezitoa wakipinga uandishi na uenezaji wake na hapo wakaanza kuziandika.

Alba ibn al-Ahmad ananakili kuwa mara moja Ali ibn Abi Talib a.s. wakati akitoa Hotuba juu ya mimbar, alibainisha: "Je, ni nani atakayeinunua elimu kwa Dirhamu moja?" Al-Harith ibn al-A' war alinunua karatasi yenye thamani ya Dirhamu moja na kumwijia Imam Ali ibn Abi Talib a.s. na kuandika kiasi cha kutosha cha elimu juu yake. Riwaya hii inatuonyesha vile Imam a.s. alivyokuwa akisisitiza juu ya uandikaji.

Imam Hassan ibn Ali ibn Abi Talib a.s. ameripotiwa akiwashauri watoto wake kama ifuatavyo:-

"Nyinyi sasa ni watoto wa Ummah ambao katika maisha ya mbeleni mtakuwa wakubwa wao. Jielimisheni Elimu; na yeyote yule miongoni mwenu atakayeweza kuhifadhi (kukariri) elimu (yaani Hadith), basi aiandike na kuiweka nyumbani mwake."

Imeripotiwa kuwa Hujr ibn Adi, mmoja wa Sahaba wa Mtume s.a.w.w. na Imam Ali ibn Abi Talib a.s., aliziandika Hadith za Imam Ali ibn Abi Talib a.s. katika kitabu na kuzirejea pale alipohitaji msaada wa mwongozo katika masuala mbalimbali Mifano hii inadhihirisha umuhimu aliokuwa ameuambatanisha Imam Ali ibn Abi Talib a.s., watoto wake na Sahaba wake katika uandikaji wa Hadith. Mifano miwili ifuatayo itaonyesha dhahiri vile Imam Ali ibn Abi Talib a.s. alivyokuwa akisisitiza umuhimu wa Hadith na kuzihifadhi.

Umar ibn Ali anaripoti kuwa mtu mmoja alimwuliza Imam Ali ibn Abi Talib a.s. ni vipi kuwa yeye (i.e. Ali) aliweza kunakili na kusimulia Hadith nyingi za Mtume s.a.w.w. kuliko Sahaba wengineo. Imam Ali ibn Abi Talib a.s. alijibu: "Hii ni kwa sababu daima nilipokuwa nikimwuliza swali Mtume s.a.w.w., alikuwa akinijibu maswali yangu. Na pale nilipokuwa nikiwa kimya, basi Mtume s.a.w.w. alianzisha mazungumzo mwenyewe."

Ali ibn Hawshab anaripoti kutoka Makhul, mwanachuo kutokea Syria, kuwa Mtume s.a.w.w. aliisoma Ayah (69:12)

Na hapo alimwambia Imam Ali ibn Abi Talib a.s. "Mimi nimemwomba Allah swt kuwa masikio hayo yawe ni yako." Baadaye Imam Ali ibn Abi Talib a.s. alisema: "Mimi kamwe sikusahau Hadith yoyote au chochote kile kilichosikilizwa na sikio langu kikisemwa na Mtume s.a.w.w.

Umar ibn al-Harith anasema:

"Wakati mmoja Ali a.s. aliuelekeza uso wake kuelekea mbinguni na kuurudisha chini akisema:"Mwenyezi Mungu na Mtume wake s.a.w.w. wamesema kweli." "Je, kilikuwa nini?" Kikundi cha watu kiliuliza. Imam Imam Ali ibn Abi Talib a.s. alisema: "Mimi ni mpiganaji wa vita na vita vinarithishia mtu ulaghai. Vivyo hivyo, ninaweza kukubali iwapo nitaporomoka kutokea mbinguni kwa ajili ya kunaswa na ndege kuliko kumsingizia uwongo Mtume wa Allah swt. Kwa hivyo fuateni chochote kile mukisikiacho kikitoka kwangu........"

Kauli juu ya uandishi wa Hadith pia zimenakiliwa kutoka Maimamu wengine.

Al-Imam al-Sadiq a.s. alisema:

"Andikeni na kuieneza elimu yenu miongoni mwa ndugu zenu, na iwapo mtafariki basi watoto wenu watarithi vitabu vyenu. Itafika siku ambapo patatokea machafuko na hapatakuwapo na mtu wa kumfanya rafiki na wala hapatakuwa na chochote cha kuweza kutegemewa isipokuwa ni vitabu tu....

Al-Imam al-Sadiq a.s. pia amenakiliwa kwa kusema: "Hifadheni vitabu vyenu kwani mutakuja kuvihitaji hivyo siku moja." Vile vile ameripotiwa akisema kuwa nguvu za moyo na kuhifadhi akilini inategemea mno juu ya maandishi.

Abu Basir anaripoti kuwa aliambiwa na Imam al-Sadiq a.s.: "Baadhi ya watu waliotoka Basrah walikuwa wakija na kuniuliza kuhusu Hadith na waliziandika. Je, kwa nini nawe hauziandiki?" Na aliongezea kusema, "Elewa wazi wazi kuwa wewe kamwe hautaweza kuhifadhi Hadith bila ya kuiandika."

Idadi kubwa ya mapokezi yanaonyesha kuwa Maimamu a.s. walikuwa navyo vitabu na maandishi ambavyo walirithi kutoka vizazi vilivyowatangulia.

Katika riwaya nyingine Imam Ali ibn Abi Talib a.s. ameripotiwa akiwa amesema: "Ikamateni elimu (kwa kuiandika)," ambavyo aliirejea mara mbili Imeripotiwa kutoka Ja'bir kuwa Abu Hanifa alikuwa akimwita al-Imam al-Sadiq a.s. "Kutubi" (yaani mwenye vitabu) kwa sababu ya kutumia mno vitabu, na Imam a.s. alifurahishwa kwa jina kama hilo.

Vile vile imeripotiwa kuwa al-Imam Muhammad ibn Ali al-Baqir a.s. ameziandika Hadith za Mtume s.a.w.w. ambazo zilikuwa zikinakiliwa na Jaabir ibn Abdullah Ansaari.

(Ingawaje taarifa hii inaonyesha kuwa siyo ya ukweli kwani Jaabir alikuwa ameshakwisha kufariki wakati Imam a.s. alikuwa na umri wa miaka mitano tu, labda inawezekana kuwa Hadith ziliandikwa na mjumbe).

2. MASHIA NA UANDISHI WA HADITH:

Kwa kuwa riwaya (desturi) ya uandishi wa Hadith ilikuwapo miongoni mwa Shia tangia mwanzoni, wao walikuwa wanaongoza katika uandishi wa Hadith na Fiqh.

Dr. Shawqi Dayf anaandika:

"Mwelekeo na umuhimu wa Mashia katika uandishi wa Fiqh umekuja daima ni madhubuti mno. Sababu nyuma yake ilikuwa ni imani yao katika Maimamu wao ambao walikuwa ni kiongozi wao (haad) na wakiwa wameo ngozwa na Allah swt (mahdi) na fatawa zao zimekuwa zimeshikamana. Kwa hivyo, wao walipatiwa uzito na umuhimu katika misemo ya Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Na kwa sababu hiyo, mkusanyiko wa kwanza ulifanywa na Mashia, ulifanywa na Sulaym ibn Qays al-Hilali, katika zama za al-Hajjaj."

Al-Allamah al-Sayyid Sharaf al-Din anaandika:

“Imam Imam Ali ibn Abi Talib a.s. na wafuasi wake walitilia mkazo na kufuatilia swala la uandishi kuanzia mwanzo kabisa. Jambo la kwanza kabisa lililotiliwa mkazo na kufuatiwa na Imam Ali ibn Abi Talib a.s. ilikuwa ni kuiandika Quran nzima, ambayo aliifanya baada ya kifo cha Mtume s.a.w.w. kwa kuiandika kimpangilio wa ufunulio wa Aya za Qurani.Katika Qurani hiyo pia alikuwa ameonyesha ni aya zipi zilizokuwa 'amm au khass, mutlaq au muqayyad, muhkam au mutashabih. Baada ya kukamilisha hayo, aliendelea na kazi ya ukusanyaji wa kitabu kwa ajili ya Fatimah, ambacho kilikuwa kikijulikana kwa vizazi vyao kama Sahifat Fatimah. Baada ya hayo, aliandika kitabu juu ya diyat (fidia) ambacho kilijulikana kama Sahifah. Ibn Sa'id amenakili hivyo katika musnad kutoka kwa Imam Ali ibn Abi Talib a.s. mwishoni mwa kazi yake mashuhuri al-Jami.' Mtunzi mwingine wa Kishia ni Abu Rafi, ambaye alikusanya maandiko yakiitwa kitab al-Sunan wa al-ahkam wa al-qadhaya. ”

Marehemu Sayyid Hassan al-Sadr anaandika kuwa Abu Rafi, aliyekuwa mawla wa Mtume s.a.w.w. ndiye aliyekuwa wa kwanza miongoni mwa Mashia kwa kukikusanya kitabu. al-Najashi katika Fihrist ameelezea kuwa Abu Rafi alikuwa ni mtunzi katika kizazi cha kwanza cha Mashia. Mfuasi wa Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Abu Rafi alishiriki katika vita vya Imam Ali ibn Abi Talib a.s. na alikuwa ni mwangalizi wa hazina ya Serikali huko Kufah. Kitabu chake kilichokuwa kikiitwa Kitab al-Sunan wa al-ahkam wa al-qadhaya, ambacho kilikuwa kimeanza kwa sura izungumziayo Salat, kufuatiwa na sura juu ya Saumu, Hajj, Zakat, kutolewa kutoka kwa Imam Ali ibn Abi Talib a.s. katika Kufah, Kitabu hiki kilinakiliwa na Zayb ibn Muhammad ibn Ja'afer ibn al-Mubarak katika nyakati za al-Najashi.

Ali ibn Abi Rafi, mwana wa Abu Rafi, aliye tabi't na Mshia khalisi ameweza vile vile kukusanya kitabu kilichokuwa na sura mbali mbali juu ya mambo ya Sheria kama vile wudhuu, Salaat, n.k.

Kama ilivyoelezwa hapo awali, abu Hanifa alimwita al-Imam al-Sadiq a.s. kutubi (akisema 'innahu kutubi') sifa ambayo ilimtambulisha na wengineo. Wakati Imam a.s. aliposikia kuhusu hayo, alicheka na kusema, "...... lakini kila alichokisema kuwa kwangu suhufi ni kweli; mimi nimesoma suhuf (vitabu) vya mababu zangu." Riwaya hii inaonyesha kwa wazi wazi kuwa Imam a.s. alikuwanavyo vitabu fulani ambavyo alipewa na mababu zake, na hiki kilikuwa ni kipindi ambacho Ahl al-Sunnah walikuwa hawakutilia mkazo katika uandishi wa Hadith.

Miongoni mwa mapokezi ambayo inatuonyesha kuwa ma-Imam a.s. walikuwa navyo vitabu kama hivyo, ni mojawapo iliyoripotiwa na Muhammad ibn 'Udhafir al-Sayrafi anasema:

"Mimi nilikuwa pamoja na al-Hakam ibn Utaybah na tulimtembelea al-Imam al-Baquir a.s. Al-Hakam alimwuliza swali Imam a.s. Abu Ja'afer a.s. alikuwa akimstahi sana. Wao walitofautiana juu ya swala fulani na hapo Abu Ja'afer alisema: "Mwanangu (mtoto wake), inuka na ukilete kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Huyo mtoto alimletea kitabu kikubwa, ambacho Imam a.s. alikifungua, na kulipitishia macho hadi kulipata swala walilokuwa wakilizungumzia. Na hapo Abu Ja'afer a.s. alisema: "Haya ni maandishi ya Imam Ali ibn Abi Talib a.s. na yaliyosemwa na Mtume s.a.w.w..........."

Katika riwaya nyingineyo ameripotiwa Imam al-Baquir a.s. akisema: "Katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. nimepaona ambapo Mtume s.a.w.w. akisema: 'Wakati zakat itakapokuwa hailipwi, basi baraka itapotea kutoka ardhi."

Vile vile ipo imeripotiwa kuwa Imam al-Sadiq a.s. amesema:

Baba yangu alisema: "Mimi nimesoma katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa Mtume s.a.w.w. ameandika mkataba baina ya Muhajirun na Ansar na watu wengineo wa Yathrib ambao waliungana naye, ikisemwa humo hivi: "Jirani ni sawa na mtu mwenyewe; asitendewe visivyo haki au kutendewa madhambi. Utukufu wa jirani wa mtu ni sawa na ule utukufu wa mama yake."

Katika riwaya nyingine al-Imam al-Sadiq a.s. amesema:

Imeelezwa katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. "Mfano wa dunia ni sawa na mfano wa nyoka: ngozi yake nyororo mno, lakini ndani yake ni sumu kali mno. Mtu aliye mwenye busara hujiweka naye mbali, lakini jahili anafanya kila aina ya jitihada ya kutaka kuikaribia."

Kwa mujibu wa riwaya nyingineyo, habari ifuatayo imetoka katika kitab adab Amir al-Muminiin:

Mtu yeyote asijaribu kurejea katika mithali katika masuala ya Din, kwani amri ya Allah swt haiwezi kutambuliwa kwa mithali. Watatokezea watu ambao watakuwa wakirejea katika mithali, na hao watakuwa na uadui pamoja na Din.

Zurarah anaripoti:

Nilimwuliza al-Imam al-Baquir a.s. kuhusu hisa ya babu katika urithi. Imam a.s. alijibu: "Sijawahi kumwona mtu yeyote yule akilisemea swali hili bila ya kuongezea mawazo yake ya kibinafsi, isipokuwa Amir al-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s.." Mimi nilimwuliza: "Na jee alisema nini?" Imam a.s. alinijibu: "Njoo kesho, mimi nitakusomea kutoka kitabuni." Mimi nilisema, "Mimi niwe fidia juu yako, naomba uiseme katika mtungo wa Hadith kwani Hadith zako ni afadhali kwangu kuliko kukisoma kitabu." Imam a.s. alisema: "Tafadhali usikilize kile nilichokuambia. Njoo kesho na mimi nitakusomea kutoka kitabu hicho." Siku ya pili mimi nilimwendea Imam a.s. wakati wa adhuhuri. Jaafer ibn Muhammad mwanae Imam a.s. alinikaribia na Imam a.s. alimwambia kunisomea kitabu hicho........

Katika riwaya nyingine, Imam al-Sadiq a.s. anasema: "Ipo imeelezwa katika Kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa mtu anywaye pombe na mwenye kumsaidia aliyelewa (muskir) basi wote wanastahili kuadhibiwa, ambavyo ni sawa katika sura zote mbili."

Muhammad ibn Muslim, Sahaba wa Imam al-Baquir a.s. asema: "Abu Jaafer alinisomea kitabu kitab al-faraidh, ambacho yalikuwemo yaliyosemwa na mtume s.a.w.w. na kuandikwa na Imam Ali ibn Abi Talib a.s.."

Habari zote zilizotajwa hapo juu, ambazo ni chache sana kutokea riwaya nyingi mno kama hizo, zinatudalilisha kuwa desturi ya Mashia ya kuandika Hadith imetangulia mawaidha ya ma-Imam a.s. kwa sahaba wao kuhusu uandishi wa Hadith. Ilikuwa ni desturi ambayo ilianzia katika zama za Mtume Mtukufu s.a.w.w. na ilikuwa imeanzishwa na Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Zipo Hadith, nyingi katika desturi ya Mashia ambazo zimetimiza kanuni za tawatur, na vile vile yapo marejeo katika Sunni ambazo zinathibitisha na kushuhudia Hadith kama hizo.

Mambo yote hayo yanakuelekeza katika uimara na uhakikisho wa usahihi wa Hadith zilizonakiliwa na Mashia. Hii ni kwa sababu pamoja na kuendelea na maongozo ya Maimamu a.s. hadi kufikia katikati ya karne 3 A.H./9 A.D., Hadith za Mashia zilitoa watunzi wengi mno na ambao maandishi yao kuanzia kipindi cha al-Imam al-Sadiq a.s. yamekuwa kwa hakika ni katika idadi kubwa sana. Iwapo mtu ataweza kutupia macho Rijal al-Najashi, basi huyo ataweza kuona kuwa wafuasi wa Imam a.s. wametupatia kazi kubwa ambazo zimetumika kama misingi ya Fiqh katika Ushia.

Ukweli ni kwamba, Mashia idadi yao ndogo kwa upande mmoja na maisha ya hatari waliyokuwa wakiishi kwa upande wa pili ambayo iliwazuia watu waovu na wenye kuvizia majukumu kuingia katika Ushia pamoja na umuhimu uliosisitizwa na Maimamu a.s. na wafuasi wao katika uandishi, ndivyo vilivyoleta matokeo ya utajiri na usahihi wa Fiqh ya Kishia. Haya ndiyo faida ambazo hazikupatikana kwa Ahl al-Sunnah kwani, kwanza, wingi wa idadi yao, pili, kwa kuwa madhehebu ya Sunni ndiyo iliyokuwa Dini ya utawala wa Dola, na tatu, kwa sababu ya ukosefu wa Hadith zilizoandikwa kwa Waislam kwa ujumla kuyafuatilia yale yanayotokana na ukweli wa misingi ya kihistoria.

3. HISTORIA YA UANDISHI WA HADITH KATIKA SUNNI:

Kazi zote zilizopo hadi leo zinazohusu Hadith zilikuwa zimekusanywa katika kipindi cha karne 2 A.H./8 A.D. au katika karne ya 3 A.H./9 A.D. Historia inatuonyesha kuwa katika kukaribia karne ya 2 A.H. kulitokezea idadi ndogo ya Muhaddithun ambao walianza kuziandika Hadith, ingawaje hazikuwa na mpangilio. Baadaye mkusanyiko huu mdogo ulikuwa kiini cha kazi zote kubwa. Hata hivyo wingi wa Hadith zilizopo sasa kwa kukusanywa, zilienezwa kwa desturi ya kutamkwa (kusemwa), na wakati zilipokuja kuandikwa vitabuni, zilikuwa hazikuwahi kuandikwa popote kabla yake.

Ucheleweshwaji katika kuandikwa kwa Hadith ni swala mojawapo muhimu katika historia ya Hadith. Umuhimu wake ni wa ukweli kwamba kucheleweshwa huu kuliathiri hasa kuhusu utunzi na idadi ya Hadith pamoja na uwepesi wao wa kuzushwa (zikaongezwa na kupunguzwa na hatimaye zikawa ni zile zilizo na uongo) na matatizo mengi mengineyo yanayohusiana.

Jambo la umuhimu huu katika swala hili linawahusu wale ambao ndio waliokuwa wamesababisha ucheleweshwaji huo wa kuandikwa kwa Hadith. Mwelekeo wao ulikuja kama ni mfano kwa ajili ya wengine katika kutoziandika Hadith. Katika sehemu yetu hii, tutaweza kuchambua makusudio yao na athari za mwenendo wao wa aina hiyo juu ya Hadith.

Kila kinachoweza kukusanywa kwa shida katika Historia ni kwamba baadhi ya Makhalifa walizuia uandikaji wa Hadith kwa sababu fulani fulani. Baada yao kikundi cha Sahaba na Tabiun waliwafuata katika swala hili. Kwa mujibu wa msemo "Watu hufuata dini ya wafalme wao," wao walijiepusha na uandikaji wa Hadith kwa kukubali na kuridhia kwa kuharamishwa hivyo.

Wao walizihifadhi Hadith za Mtume s.a.w.w. kwa kuzikariri tu (kwa kuzihifadhi akilini mwao tu). Kama vile tutakavyoona hapo mbeleni, wao nyakati zinginezo walijaribu kurejea katika kuziandika, ili kuyateketeza maandishi yao katika kipindi cha mwisho wa maisha yao, kama kwamba maandishi hayo yaliwasaidia wao tu katika kuhifadhi kwao. Kumbukumbu hizo za Hadith zilizokuwa zimeandikwa hazikutumiwa kwa kutaka kuzihifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo. Ni jambo la kuvutia sana kuona kuwa kupigwa marufuku wa uandikaji wa Hadith katika Sunni ulitolewa na watawala wao; na vile vile ile amri ya kuziandika Hadith pia zilitolewa na watawala wao.

Al-Zuhri anasema:

"Sisi tulikuwa tukichukia mno uandishi wa elimu, hadi hapo wakuu wetu walipotulazimisha kuyaandika hayo. Hapo baadaye tulikuja kugundua kuwa hapakuwapo na yeyote miongoni mwa Waislam waliopinga."

Al-Zuhri anaendelea kusema:

"Wafalme waliniambia kuandika elimu ('ilm, i.e. Hadith) kwa ajili yao. Baada ya kuwaandikia kwa muda fulani, mimi nilishikwa na aibu mbele ya Allah swt; (mimi nilijiuliza): Je, kwa nini nimejitayarisha kwa ajili ya kuwaandikia wafalme na wala si kwa ajili ya watu wengineo!?"

Ni dhahiri, kama vile itakavyokuja kuonekana kwamba Hadith hazikuwa ni kweli kwa ajili ya Sahaba na Tabiun wote. Wengi wao na akiwemo Ali ibn Abi Talib a.s. waliziandika Hadith na vile vile waliwaambia wengine kufanya hivyo. Wengine walianza kuziandika Hadith wakati sheria zilizowekwa na Makhalifa juu ya kutoziandika Hadith zilipobadilishwa na amri ya Kikhalifa kutoka kuziandika Hadith.

'Umar ibn Abd al-Aziz (101 A.H./719 A.D.) ndiye aliyekuwa Khalifa wa kwanza kuamrisha wanazuoni wa miji mbalimbali kuziandika Hadith na kumpelekea huyo Khalifa maandishi yote. Imeripotiwa kuwa Khalifa alimwandikia Muraah ibn Kathir akimwomba amwandikie Hadith za Mtume s.a.w.w. Vile vile yeye alimwandikia Abu Bakr ibn Muhammad Hazm: "Andika Hadith yoyote ile ya mtume s.a.w.w. uliyonayo na kunitumia na chochote kile kilichonakiliwa kutoka kwa Umar, kwa sababu ninayo hofu kuwa utafika wakati ambapo Hadith zitakuwa zimetoweka." Yeye pia aliwaandikia watu wa Madinah akiwataka wamwandikie chochote kile kilichobakia cha Hadith za Mtume s.a.w.w.

Ripoti hizi zinaonyesha wazi wazi kuwa uandikaji wa Hadith haukuwa jambo lenye umuhimu hadi wakati huo, hata hivyo, haimaanishi kuwa hapakuwepo na Hadith zilizokuwa zimeandikwa hadi wakati huo.

Pamoja na kifo cha Umar ibn Abd al-Aziz kazi hii haikufuatiliwa na Makhalifa waliofuata, na kwa mara nyingine tena uandikaji wa Hadith uliangukia katika kusahauliwa. Kukariri (kuhifadhi katika akili) ndiyo iliyokuwa njia iliyobakia.

Hadith za kusemwa mdomoni tu (bila ya maandiko) ndiyo iliyokuwa njia ya uenezaji wakati ambao Sunni walirithi kutoka vizazi vyao vilivyowatangulia, ilisababisha upinzani mkubwa mno katika kuziandika Hadith. Sisi twaweza kuelewa vyema hali hii wakati tutakapokuja kujua kuwa baadhi ya Muhaddithun walichukizwa mno na uandishi wa Hadith hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 2 A.H./8 A.D. Kauli za wanahistoria kuhusiana na ukusanyaji wa Hadith hapo mwanzoni zinaelezea hayo hayo.

Abd al- Razzaq anaelezea kuwa mtu wa kwanza kuzikusanya Hadith alikuwa Abd al-Malik ibn Jurayj, aliyejulikana kama Ibn Jurayj (150 A.H./767 A.D.) Vile vile Abd al-Rahman Al-Awzai (88-157 A.H./707-773 A.D.) alikuwa ni miongoni mwa wale walioanza kuzikusanya Hadith.

Al-Dhahabi anaandika kuwa, katika kipindi hiki ndipo Wanazuoni wa Kiislamu walianza kuandika Hadith, Fiqh na tafsiri katika mwaka 143 A.H./760 A.D. Wafuatao ndio waliokuwa wakiongoza katika kazi hizo nao ni Ibn Jurayj katika mji wa Makkah, Malik (179 A.H./795 A.D.) huko Madinah, al-Anzai katika Syria, Said ibn Abi Urwah (156 A.H./783 A.D.) huko Basrah, Muammar huko Yemen, Sufyan al-Thawri (156 A.H./783 A.D.) huko Kufah. Kabla ya kipindi hicho, hata hivyo, Muhaddithun waliongoza wakiripoti Hadith kutokea kukariri au kutokea kwa waliotegemewa lakini zilikuwa ni mikusanyo isiyokuwa na mipangilio.

Mahali pengine yeye ni mbainifu zaidi wakati asemapo: "Ibn Jurayj na Ibn Abi Urwah walikuwa ni miongoni mwa watu wa kwanza katika ukusanyaji wa Hadith na Muammar ibn Rashid alikuwa ni wa kwanza miongoni mwao huko Yemen." Ipo habari iliyoripotiwa na Abd al-Aziz ibn Muhammad al-Darwardi kuwa mtu wa kwanza kukusanya elimu alikuwa Ibn Shihab al-Zuhri. Ibn Shihab al-Zuhr (124 A.H./742 A.D.) mwenyewe anaripotiwa akiwa amesema: "Umar ibn Abd al-Aziz alituamrisha kuzikusanya Hadith za Mtume s.a.w.w. Kufuatiwa hayo sisi tuliandika katika sura ya kitabu, na kupeleka nakala ya kitabu hicho katika sehemu zote za utawala wake."

Ni dhahiri, ingawaje Hadith zilikuwa zikikusanywa kwa kiasi fulani katika siku hizo, kazi ya ukusanyaji ilianza kuzorota kwa sababu ya upingamizi uliofuatia kifo cha Umar ibn Abd al-Aziz, na vile anavyosema al-Dhahabi, kazi hiyo ya ukusanyaji wa Hadith uliahirishwa au kuachwa kwa kipindi cha nusu karne.

Ibn Hajar anasema:

“Kazi ya ukusanyaji na upangaji (tabwib) wa Hadith ulianza katika miaka ya mwishoni mwa kipindi cha tabi'un, yaani ni kwamba, wakati ambapo Wanazuoni wa Kiislam walipokuwa wameenea katika miji. Wa kwanza katika ukusanyaji wa Hadith walikuwa ni Rabi ibn Subayh na Sa'id ibn Abi Urwah......hadi wakuu miongoni mwa Wanazuoni wa tabaka la tatu walipokusanya ahkam.

Al-Dhahabi pia anaelezea kitu kama hicho. Kutokana na taarifa hizo inaweza kudadisiwa kuwa ukusanyaji wa Hadith uliotokezea katika sehemu mbili: Sehemu ya kwanza ni mkusanyiko usio kamilifu mwanzoni mwa karne ya 2 A.H./8 A.D. na sehemu ya pili ni ukusanyaji uangalifu katika sehemu yake ya pili. Hajji Khalifah anakubaliana na haya pale asemapo:

  Yaliyomo endelea