Yaliyomo endelea

SHADA LA MAUA KUTOKA BUSTANI YA AHADITH ZA MTUME s.a.w.w. & AHLUL – BAYT a.s.

Zimekusanywa na kutarjumiwa na : AMIRALY M.H.DATOO

UTANGULIZI

Allah swt anatuambia katika Al-Qur’an tukufu: Sura al-Nahl, 16 Ayah 43 na Sura Al-Ambiya,21 Ayah 7

Ayah hii Tukufu inawasihi Waumini kujielekeza kwa Ahl-Dhikr yaani watu wenye busara na Wanazuoni wa Ummah ili kuweza kubainisha baina ya haki na batili, wakati ambapo Waumini wanapokumbana na shida au ugumu katika masuala mbalimbali, kwa sababu Allah swt baada ya kuwafundisha ilimu, aliwachagua hao kwa hayo. Hivyo, wao wamebobea katika ilimu na ambao ndio watu halisi wanaoielewa, kuifundisha na kuitekeleza kwa usahihi mafunzo ya Qur’an.

Ayah hii iliteremshwa kwa ajili ya kuwatambulisha Ahlul-Bayt a.s. nao ni Mtume Muhammad s.a.w.w., Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s., Fatimah a.s., Al-Imam Hassan ibn Abi Talib a.s. na Al-Imam Husayn ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. , ambao kwa ujumla wanaitwa Watukufu watano au ‘Al-i-‘Aba ambapo pamoja na hao wameongezeka Ma-Imamu a.s. wengine tisa kutokea kizazi cha al-Imam Husayn ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. Mtume s.a.w.w. mara nyingi katika nyakati mbalimbali aliwatambulisha hao kuwa ni Ma-Imam waongozi, nuru katika kiza, na ni wale ambao wamebobea katika ilimu na bila shaka Allah swt amewajaalia Ilimu ya Kitabu Kitukufu.

Ukweli huu, kama ilivyorejewa mahala pengi katika Ahadith mbalimbali kuanzia zama za Mtume s.a.w.w. kuanzia ufunuo hadi leo hii, na vile vile wanazuoni wengi na Wafasiri kutokea Ahl-Sunnah wamekiri waziwazi katika vitabu vyao kuwa Ayah hizi za Qur’an zilikuwa zimeteremshwa hususan kwa ajili ya kuelezea na kuwatambulisha Ahl-ul-Bayt a.s. Baadhi ya mifano ya vitabu vyenyewe ni kama ifuatavyo:

  1. Imam Tha’labi katika tafsiri ya kitabu chake juu ya Ayah hiyo ya 42 kutokea Sura An-Nahl, namba 16
  2. Tafsir ibn Kathir, j.2, uk.591
  3. Tafsir at-Tabari, j.14, uk.75
  4. Tafsir-i-Alusi, ijukanavyo kama: Rahul-Bayan , j. 14, uk. 134
  5. Tafsir-i-Qartabi, j.11, uk. 272
  6. Tafsir-i-Hakim, au Shawahid-ut-Tanzil, j. 1, uk. 334
  7. Tafsir-i-Shabistrary, au: Ihqaq-ul-Haq, j.3, uk.482
  8. Yanabi’-ul-Muwaddah, cha Ghanduzi Hanafi, uk. 119

Kwa kutegemea ukweli huu, sisi lazima tujielekeze kwa Wananyumba ya Ahlul-Bayt a.s., na kutekeleza maneno yatuongozayo ili kuelekeza maisha yetu mema. Kwa sura hii, Imam-ul-Hadi a.s. anasema katika Man la Yahdhuruh-ul-Faqih, Tahdhib na ‘Uyun-i-Akh-bar-ur-Ridha :

“Maneno yenu yenye busara yanatupa nuru, maamrisho yenu ni hidaya kwa watu na usia zenu ni Taqwa na usawa.”

MUWE TAHADHARI ENYI WASOMAJI

Kwa kupitia Watuku hawa ndipo sisi tunaweza kuokoka humu duniani na Aakhera na maisha yetu yakawa mema na salama.

Twapata katika Man la Yahdhuruh-ul-Faqih, Tahdhib na ‘Uyun-i-Akh-bar-ur-Ridha :

“Ni kwa sababu yenu Allah swt ametutoa nje ya upotofu (wa ukafiri), ametufanya huru kutoka huzuni na masikitiko, na kutuchukua pa usalama dhidi ya maangamizo ya dunia na mioto ya Jahannam pia.”

Katika katika Man la Yahdhuruh-ul-Faqih, Tahdhib na ‘Uyun-i-Akh-bar-ur-Ridha twasoma :

“Ni kwa sababu ya Ukuu na uongozi wenu kuwa Allah swt ametufundisha ilimu ya kanuni za Dini , na kuweka sawa na vyema yale yote yaliyovurugika na kufasidika katika dunia. (Naye ametuepusha na umasikini, udhalilifu na ujahili, na kututunukia ilimu, heshima na hadhi.)

Kwa hakika, iwapo sisi tutawaacha hawa watukufu waliobarikiwa na kutukuzwa na Allah swt, basi hakuna shaka kuwa tutatumbukia katika upotoshi na maangamizi katika kila hali. Ndipo Mtume s.a.w.w. amesema :

“Mfano wa Ahlul-Bayt a.s. yangu ni sawa na Safinah ya Mtume Nuhu a.s. Yeyote yule atakaye ipanda basi kwa hakika ameokoka na yeyote yule atakayekhilafu kuipanda, basi kwa hakika amezama na kutokomea mbali.”

Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. :

“Inawezekana nikaitwa hivi karibuni nami nikaitikia. Hivyo, mimi ninawaachieni miongoni vitu viwili vilivyo vizito (vyenye thamani na maana kubwa mno) : Kitabu cha Allah swt (yaani Qur’an) ni kamba iliyovutika kutoka mbinguni hadi ardhini , na Ahlul-Bayti a.s.yangu; kwa hakika Allah swt, Mrehemevu, Mwenye kuwa Makini, amenijulisha kuwa kamwe, kamwe vitu hivi viwili havitatengana hadi kukutana na mimi hapo Hawdh-Kauthar (Chemchemi ya milele). Hivyo, muwe waangalifu mutakavyojishikiza navyo wakati ambapo mimi sitakuwapo.”

Na vile vile katika Hadith nyingineyo imeongezeka:

“Kamwe, kamwe, hamtapotoka iwapo mutakuwa mumeshikamana navyo hivi vitu viwili.”

Hivyo, je ni heshima gani itakayopita kuliko Qur’an , Mtume s.a.w.w. na Ahlul-Bayt a.s. vikawa ni mifano yetu, waalimu na viongozi wetu ?

Na kwa sababu hizi ndipo sisi kwa moyo halisi na unyenyekevu tunasema:

Sisi tumefadhilika kwa sababu sisi ni wafuasi wa Madhehebu ambayo muasisi wake Mtume Muhammad s.a.w.w. na Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. (mja ambaye amekombolewa kutokana na minyororo ya udhalili na kuchaguliwa kuwa mkombozi wa binadamu wote kutoka utumwa mbali na ule wa Allah swt ) kwa kufuata mwongozo kutoka Allah swt.

Sisi tumetukuzwa kwa kuwa na kitabu kitakatifu cha Nahjul-Balagha, ambacho ni kitukufu baada ya Qur’an Tukufu, chenye maandiko matukufu kwa ajili ya maisha yetu wanaadamu, ni kitabu kikubwa kwa ajili ya ukombozi wa mwandamu na maelekezo yake ya kiroho na kisiasa yanayo thamani kubwa kwa ukombozi na kimeandikwa na Ma’sum Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.

Vile vile tumebarikiwa kwa Imam Al-Mahdi a.s. atokanaye na Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. yu bado hai na kwamba anahabari na kujua habari zetu zote.

Sisi tumebarikiwa kuwa na Doa ambazo ndizo zilizofunzwa na Ma-Imam a.s. kama Dua za Sha’baniyyah, Dua ya ‘Arafah ya al-Imam Husayn ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s., Sahifa-i-Sajjadiyah ya al-Imam Zayn-al-‘Aabediin a.s. , na Sahifa-i-Fatimah.

Vile vile sisi tumebarikiwa kuwa na Mwanazuoni mkubwa katika zama zetu ambaye hawezi kueleweka kwa watu wengine isipokuwa Allah swt, Mtume s.a.w.w. na Ma-Imamu a.s. kwa sababu ya kipaji chake kikubwa cha ilimu na hekima.

Vile vile sisi tumebarikiwa kwa kuitwa Madhehebu ya Ja’afariyyah na kwamba Fiqh ambayo ni bahari isiyo na mwisho ( ya ilimu ), ambayo ni mchango mmojawapo wa al-Imam as- Sadique a.s. Vile vile sisi tunafakhari kubwa sana kwa kuwa na Ma-Imamu a.s. wote, na tunawafuata kikamilifu.

Sisi tumebarikiwa kwamba Maimam a.s. wetu walikuwa wameteswa, kuwekwa mahabusu na vile vile kutolewa makwao kwa sababu wao walikuwa daima wamejitolea muhanga kuutetea ubinadamu na kuinua hali ya Dini ya Islam na kuyatekeleza maamrisho ya Qur’an yakiwemo maamrisho ya kutengeneza Serikali adilifu na hatimaye hao Ma-Imamu a.s. waliuawa katika harakati zao za kutokomeza serikali dhalimu na Taghuti katika kila zama.

Sasa, ewe mpenzi kaka na dada !

Wewe ni shahidi wa macho, katika dunia hii ndogo, ndogo zaidi kuliko kijiji katika ulimwengu, unajionea kuwa hali ya binadamu inaendelea ipo inateketea katika jangwa la dhuluma na pasi na haki, wakati mwanadamu huyo yupo anatumbukia chini zaidi katika matingatinga ya kutokuhurumiwa na kukosekana kwa uadilifu.

Wale wote wanaojidai kuhusu uhuru na raha ya mwanadamu wanashuhudia kwa makini kumomonyoka kwa maadili katika mazingira waliyoyaumba wao wenyewe. Wao hawana tena uwezo wa kudhibiti hali hiyo isipokuwa kuangamia kwa binadamu na ubinadamu. Lakini, je ni kweli kuwa huo ndio mwisho wa mstari huo ?

Jibu kwa kushangaa litakuwa ndiyo, hadi hapo mwanadamu atakaporejea katika uumbwaji kwake wa kimungu, akimulika makosa na kasoro zake zilizopita kama ndiyo tochi kwa maisha yake ya mbeleni na akiitumia Islam kama ndiyo dawa ya matatizo yake yote.

Katika zama hizi, Islam ambayo ndiyo tukufu, na bora kabisa katika kutuongoza, bora katika katika historia, imetoa mikono yake kwa ajili ya kumnusuru mwananadamu ili asije akazama na kughalibiwa na maovu na kwa baraka za Allah swt, imesimama imara kumtibu mwanadamu dhidi ya magonjwa maovu kabisa ya maovu.

Islam ipo kwa ajili ya kutuliza kiiu cha mwanadamu anayezurura katika majangwa ya chumvi kali zisizo na taqwa kwa kumnywisha maji matamu na baridi ya itikadi zilizonurishwa kwa ilimu na maarifa na utukufu wa Ahlul-Bayt a.s. , ambayo ndiyo sura halisi ya tafsiri kamili ya ufunuo ambayo kamwe haikuwa na kosa au kasoro ya aina yoyote ile. Inatoa mwanga kwa hali zote na kimwili na kiroho ya maisha ya mwanandamu. Hivyo, imefungua milango kikamilifu kwa mwanadamu kukamilika kikamilifu.

Lakini Ewe rafiki mpendwa

NI jambo la muhimu na kwanza kabisa kwa kutaka kujua habari za shule yoyote ile pamoja na mafunzo yake, inatubidi sisi kutazama kwa undani maandiko na kuelewa mazungumzo na maneno ya viongozi wake. Na kwa njia hii ndipo sisi tutakapoweza kujua kuhusu itikadi na imani na malengo ya shule hiyo kuhusu dunia na matatizo yake na hivyo kuweza kufikia maamuzi na makisio ya upeo wake.

Al-Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. amesema katika Bihar al- Anwar j.2, uk.40; Ma’aniy-ul-Akhbaar, cha Saduq, uk.180; na Was’il al-Shiah’, j. 27, uk. 92

“Rehema za Allah swt zimfikie mja ambaye huisha maamrisho yetu” Nami nilimwuliza ni vipi mtu anaweza kuziweka hai maamrisho yenu ? Imam a.s. alijibu “Yeye anaweza kujifunza ilimu na maarifa yetu na kuwafundisha wengineo. Kwa hakika, iwapo watu watazijua faida na mema za miihadhara na misemo yetu, basi kwa hakika watazifuata kuzitekeleza.”

Matumaini mema

Twategemea kuwa msomaji kwa kuyasoma na kuyazingatia maneno yenye thamani isiyosemekana, kuwa kwa kupitia maneno na maongozao ya Ahlul-Bayt a.s. vizazi vyetu hususan vijana wataongoka na kamwe hawatapotoka wala kuvutiwa na mavutio yanayotuongoza kuelekea maangamizo ya milele na kwamba utamaduni wetu hautamomonyoka siku baada ya siku na badala yake tutatengeneza utamaduni wetu uwe utamaduni wa Kiislamu kwa baraka na miongozo za Ahlul-Bayt a.s. na kwamba tutakuwa washupavu na maaskari kulinda imani na Din ya Islamu dhidi ya maadui wake walio ndani na nje. Tutakuwa Waislamu bora na mfano kwa watu wote.

Amani na Salaam ziwafikie wale wote waliongoka.

HADITH YA UFUNGUZI

1. Amesema al-Imam as- Zayn al-‘Aabidiin a.s. katika Bihar al- Anwar, j.90, uk

187 na Sahifah as-Sajjadiyyah, uk. 572

“Sifa zote ni za Allah swt, na kusiwa Kwake ni haki Yake: sifa zisizo na kifani ndizo zinazomstahiki Yeye. Na mimi najiepusha kwa msaada wake dhidi ya shari za nafsi yangu: Kwa hakika mwanadamu yupo katika kutenda madhambi isipokuwa wale waliobarikiwa na Mola wao. Naomba msaada wake Allah swt dhidi ya maovu ya Shaitani ambaye daima ananiongezea dhambi moja juu ya lingine. Naomba msaada wake Allah swt dhidi ya watawala waovu, watawala katili, na maadui wa nguvu.”

“Ewe Mola ! Naomba unifanye mimi kuwa mmoja wa Majeshi yako, kwa sababu kwa hakika Majeshi Yako tu ndiyo yenye kushinda; na unifanye miongoni mwa wanachama Wako, kwani kwa hakika, chama Chako tu ndicho kitakachofanikiwa; na unikubalie kama mmoja wa wapenzi Wako, kwani kwa hakika, wapenzi wa Allah swt hawana hofu na kamwe hawatahuzunika.”

“Ewe Mola ! Naomba uniimarishie Dini kwa ajili yangu, kwani hiyo ndiyo hifadhi ya matendo yangu yote; na unitengenezee Aakhera yangu, kwa sababu hakuna shaka kuwa hiyo ndiyo mwisho wangu wa kudumu na kuepukana na watu wenye dharau na dhihaka, na uyafanye maisha yangu yawe ya kuniongezea mema, na mauti yangu yawe ndiyo kujitoa huru kutokana na kila aina ya kasoro za magonjwa.”

“Ewe Mola ! Mbariki Mtume Muhammad s.a.w.w., Mtume wa mwisho katika jamii ya Mitume yote, na Ahli Bayti a.s. tukufu, na vile vile Masahaba wake wema, na naomba unijaalie mahitaji matatu kwa leo: Usinibakizie dhambi lolote lile isipokuwa umenisamehe na wala huzuni yoyote ile isipokuwa umeniondolea, wala kusikwapo na adui isipokuwa wewe umemwondosha kwa jina lako tukufu la Allah ambayo ni jina bora kabisa i.e.Bismillah, Mola wa Mbingu na Ardhi …..”

KUMJUA ALLAH SWT, UKUU NA BARAKA ZAKE

2. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika Al-Khisal, 322

“Enyi Watu ! Kwa hakika hakutakuwapo na Mtume baada yangu, na wala hakutakuwapo na Ummah baada yenu (Waislamu). Hivyo, Muwe waangalifu katika kumwabudu Allah swt, musali sala tano za siku, mufunge saumu katika mwezi uliowekwa (Ramadhaan al-Mubarak), mufanye Hijja ya Nyumba ya Allah swt (Al-Ka’aba huko Makkah al-Mukaramah), mutoe Zaka kutoka mali zenu kwa ajili ya kuitakasisha nafis zenu kwa hayo, na mutii amri za Wale wenye mamlaka, ili muweze kuingia Pepo ya Mola wenu.”

3. Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Nahjul-Balagha,Semi na.129

“Kwa kuwa na tasawwuri ya Ukuu wa Mola wako basi itakufanya wewe utambue udogo wa viumbe katika mitazamo yako.”

4. Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Bihar al- Anwar, j. 77, uk.

289

“Tawba ni kwa ajili ya yule ambaye ametakasisha kwa ajili ya Allah swt matendo, ilimu, mapenzi, bughudha, kuchukua, kutoa, misemo, ukimya, matendo na asemavyo.”

5. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. katika Bihar al- Anwar, j. 70, uk. 25

“Moyo ni mahala pa takatifu ya Allah swt, hivyo, basi hakikisha hapawi kitu kingine chochote isipokuwa Allah swt tu.” (Moyo mtukufu ni wa Allah swt tu. Hivyo mapenzi ya dunia isivyo sahihi, lazima iwekwe mbali.)

6. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. katika Bihar al- Anwar,j. 93, uk. 162

“Wafuasi wetu ni wale ambao wanapokuwa peke yao, wanamkubuka Allah swt kwa kupita kiasi.” (Kwa hivyo, wao hujiepusha kutenda madhambi wanapokuwa peke yao wakati ambapo kuna hakuna kizuizi cha kuwazuia wao wasitende madhambi na badala yake humkumbuka Allah swt kwa kupita kiasi.).

7. Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika Al-Kafi, j.2, uk. 426

“Kwa kiapo cha Allah swt ! Yeye, aliyetukuka, huwategemea kwa mawili:wao waungame na kushukuru Kwake kwa neema ili Yeye awaongezee wao; na waungame kwa madhambi yao ili kwamba Yeye awasamehe madhambi yao.”

8. Amesema al-Imam Husayn ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika Safinat-ul-Bihar, j.2, uk. 180

“Kwa hakika, Allah swt, aliye Mkuu, hakuwaumba wanadamu isipokuwa kwa kumjua Yeye na baada ya kumjua Yeye kumwabudu kwa kumjua Yeye; na wakati wanapomwabudu basi kusikuwepo na haja tena ya kumwabudu yeyote mwingine isipokuwa Yeye peke yake.”

9. Amesema al-Imam Zayn-al-‘Aabediin a.s. katika Safinat-ul-Bihar, uk. 517

“Hakuna maangamizo (Jahannam au Motoni ) kwa ajili ya Mumiin aliye na sifa tatu : Kuungama na kukubali kuwa hakuna mungu mwingine isipokuwa Allah swt tu peke yake, pekee ambaye hana mshiriki; Mtume Muhammad s.a.w.w. ni mtetezi; ukubwa usio na kipimo cha Rehema za Allah swt.”

SALA NA ATHARI ZAKE

10. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w., katika Man la Yahdhurul Faqihi, J.1, Uk. 206

“Mtu yeyote aichukuliaye sala pasi na uzito wake, basi si hatokani nami. Hapana, Kwa kiapo cha Allah swt, mtu kama huyo hatafikia chemchemi ya Haudh Kawtha. “

11. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , katika Bihar al-Anwaar, Juzuu 82, Ukurasa 236:

“Iwapo kutakuwapo na mto unaopita nyumbani mwa mtu ambamo mtu huyo anaoga mara tano kwa siku, je kutabakiapo aina yoyote ya uchafu mwilini mwake ? Kwa hivyo sala ndivyo ilivyo mfano wa mto huo. Mtu ambaye anasali sala zake basi hujiondolea madhambi yake yote isipokuwa kutabakia madhambi yale ambayo yanamtoa katika Imani yake.

12. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w., katika Bihar-ul-Anwaar, J.99, uk. 14

“Sala iliyofaradhishwa kwa Allah swt ni sawa na kutimiza Hajj elfu moja na ‘Umrah elfu moja ambazo ni sahihi na zilizokubalika.”

13. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w.,katika Bihar-al-Anwaar, J.83, Uk. 14

“Kamwe musizipoteze sala zenu, kwa hakika, mtu yeyote anayezipoteza nyakati za sala zake atainuliwa pamoja na Qarun na Hamaan na itamwia haki Allah swt awatumbukize katika moto wa Jahannam pamoja na Munafiqiin (wanafiki).

14. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , katika Bihar-ul Anwaar,Juzuu 69, Uk. 408

“Musali sala zenu kama kwamba hiyo ndiyo sala yenu ya mwisho”

15. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s.,katika Tasnif-I-

Gurar ul-Hikam, uk.175:

“Iwapo mwenye kusali angalikuwa akifahamu kiasi alichozungukwa na rehema za Allah swt, basi kamwe asingaliinua kichwa chake kutoka hali ya kusujudu”

16. Amesema Al-Imam Al-Muhammad al-Baqir a.s., katika Bihar al-Anwaar,

J.7, Uk. 267:

“Siku ya Qiyama, jambo la kwanza litakalo hisabiwa ni kuhusu sala; kwa hivyo, iwapo itakuwa imkubaliwa, basi matendo mengine pia yatakuwa yamekubaliwa (amasivyo matendo yake mengine mema hayatamnusuru)”.

17. Amesema Al-Imam Al-Sadiq a.s. , Bihar Al-Anwaar, J.82, Uk. 236:

Katika siku za mwishoni mwa maisha yake, Imam As-Sadiq a.s. aliwaita jamaa na wafuasi wake na kuwaambia “Kwa hakika, Uokovu wetu hautamfikia yule aichukuliaye sala kiepesi (bila ya kuichukulia kuwa ndiyo fardhi na lazima)”

18. Amesema Al-Imam Al-Muhammad al-Baqir a.s. , Al-Khisaal cha Sadduq, uk. 432:

“Yapo mambo kumi ambayo mtu atakapokutana na Allah swt siku ya Qiyama ataingia Peponi:

Kuamini na kukiri kuwa hakuna mungu mwingine isipokuwa Allah swt,

Na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah swt

Kukiri na kuamini kuwa kile kilichoteremshwa juu ya Mtume Muhammad s.a.w.w.w.kutokea Allah swt ni Qur’an tukufu,

Kutimiza sala

Kutoa Zaka

Kufunga saumu mwezi wa Ramadhani,

Kuhiji Makkah,

Kuwatendea mema wale wampendao Allah swt,

Kujiepusha na maadui wa Allah swt,

Na kujiepusha mbali na ulevi wa kila aina.

19. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s. katka Nahjul Balagha, Msemo 136::

“Kwa kila mwenye kusali, sala ndiyo sababu kubwa ya kumfanya amkaribie Allah swt,; na kwa yule aliye dhaifu, Hajj – kuhijji Makkah – ni sawa kabisa na Jihadi – kupigana katika njia ya Allah swt. Kwa kila jambo kuna zaka yake, na hivyo zaka ya mwili ni saumu. Jihadi ya mwanamke ni kuwa mwenzi mwema wa mume wake.”

20. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , ‘Irshad-ul-Qulub, uk. 53

“Hakuna usiku unaopita isipokuwa Malaika wa Mauti huwaita ‘enyi watu wa maqaburi!’ na huwauliza kile kinachowasikitisha kwa siku hiyo kwa yale waliyoyaona na maisha yajayo. Kwa hayo wafu husema ‘kwa hakika, sisi twasikitika na kuwaonea wivu muminiin wale ambao wapo misikitini mwao ambapo wao wapo wansali wakati sisi hatusali; wao wanatoa zaka wakati sisi hatutoi; wao wanafunga mwezi wa Ramadhan wakati ambapo sisi hatufungi; wao wanatoa misaada kwa kile walichonacho ziada ya familia yao, wakati sisi hatufanyi hivyo; ….”

21. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Mustadrak-ul-Wasa’il, J.3, Uk.102

“Kwa kila wakati uliyofanywa muayyan kwa ajili ya sala , mimi huwa ninamsikia mpiga mbiu ambaye huita na kusema ‘Enyi wana wa Adam ! Dumisheni sala ili muweze kuuzima moto ambao nyinyi wenyewe muliuwasa kwa ajili yenu (kwa kutenda madhambi).”

22. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. Bihar-ul-Anwaar, J.82, Uk.202

“Lazima muwe waangalifu wa Sala, kwani siku ya Qiyama Allah swt atakapomsimamisha mja wake (kwa hisabu) basi jambo la kwanza la kuulizwa litakuwa ni kuhusu Sala. Iwapo mtu atakuwa amekujanayo kamilifu, basi atakuwa miongoni mwa watu waliookoka, ama sivyo, atatupwa Motoni (Jahannam).”

23. Abu Basir amesema kuwa yeye alimtembelea Umm-i-Hamidah (mama yake Imam Musa ibn Ja’afar a.s.) kwa ajili ya kumpa pole kwa kifo cha Ja’afar ibn Muhammad a.s. Yeye alilia na hivyo yeye pia alilia kwa sababu ya kilio cha mama huyo. Baadaye, mama yake al-Imam a.s. alisema

“Ewe Aba Muhammad ! Iwapo ungalikuwa umemwona Ja’afar ibn Muhammad alipokuwa kitandani wakati wa kufariki, basi ungalikuwa umejionea mambo ya ajabu kabisa : Yeye alifumua macho yake na kutaka majamaa wote wakusanywe.’ Na hapo yeye aliendelea kusema kuwa majamaa wote walikusanyika bila ya kubaki mtu. Hapo al-Imam a.s. alisema kwa kuwaangalia wote: “Kwa hakika, Uokovu wetu hautamfikia yule aichukuliaye Sala kiepesi (bila ya kuichukulia kuwa ndiyo fardhi na lazima)” Wasa’il-ush-Shiah, J.4, Uk. 26

24. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Bihar-ul-Anwaar, J.84, Uk.258

“Ibada ya yule mtu ambaye mapato yake yanatokana na njia zilizo haramu ni sawa na kujenga nyumba juu ya mchanga."

SALA ZA USIKU WA MANANE

25. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Bihar-ul-Anwaar, j.77, uk. 20

“Heshima ya Mumiin ipo katika kukesha kwake usiku na utukufu wake upo katika kujitawala mwenyewe miongoni mwa watu.”

26. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s. , Ghurar-ul-Hikam, uk. 289

“Yeyote yule alale zaidi wakati wa usiku, lazima atapoteza kitu mujimu kabisa katika matendo yake (i.e. sala ya usiku) ambayo hataweza kuipata wakati wa mchana.”

27. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Bihar al- Anwar , J. 13, Uk. 329

Allah swt katika ufunuo wake kwa Mtume Musa a.s., mwana wa ‘Imran a.s. alisema: “Ewe Mwana wa ‘Imran ! Wale tu ambao wanadai kunipenda mimi, wasema uongo, kwani usiku unapoingia wao hulala huku wakiniacha mimi.”

28. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Bihar al- Anwar ,J.83, Uk. 127:

“Kamwe usiikose Sala ya usiku wa manane ! Kwa sababu, ukweli ni kwamba, mpotezaji ni yule anayeikosa (faida zake) Sala za usiku wa manane.”

29. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Khisal cha Sadduq, Uk. 72

Mtume s.a.w.w. alimwambia Jibrail amwambie chochote, naye alimwambia: “ Ishi utakavyo huku ukitambua kuwa utakuja kufa; penda chochote kile utakacho lakini utatengana nacho; tenda utakavyo lakini utakutana nacho ( na kulipwa malipo yake). Heshima ya Mumin ni Sala yake ya Layl (usiku wa manane), na utukufu wake upo katika kujiepusha (na kuangamiza) sifa za watu.”

30. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Bihar al- Anwar , j.75, Uk. 107

“Vipo vitu vitatu ambavyo ndivyo sifa za Muumin na ndivyo vito vya thamani kwake humu duniani na Aakhera. Navyo ni: Sala katika sehemu ya mwisho wa usiku (Salat ul-Layl), kutotamani au kuwa na wivu kwa kile kidogo kilicho mikononi mwa watu, na mapenzi (na uongozi ) wa Imam kutokana na kizazi cha Mtume Muhammad s.a.w.w.”

31. Amesema al-Imam Muhammad ibn Ali al-Jawad ul-‘A’immah a.s. , Bihar al-Anwaar, J. 78, Uk. 79

“Yeyote yule aliye na imani kamili juu ya Allah swt, anaona furaha; na yeyote amwaminiaye, basi anatosheleza matendo yake.”

KUMWAMINI ALLAH NA KUIPATA FURAHA YAKE

32. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Bihar al-Anwaar, J. 71, Uk. 208

“Baba yangu aliniambia kuhusu baba yake kuwa mtu mmoja kutoka mji wa Kufa alimwandikia baba yake viz. Al-Husayn ibn Ali a.s., akimwuliza a.s. kumjulisha yeye kuhusu mema ya dunia hii na mema ya Akhera. Kwa hayo Imam a.s. alimwandikia (katika majibu): “Kwa jina la Allah,aliye Rahmaan na Rahiim’. Baadaye akiendelea ‘Kwa hakika yeyote yule atakaye furaha ya Allah swt hata wakati wa kutokuwafurahisha watu, Yeye humtosheleza katika masuala ya watu. Lakini, yule ambaye hutaka furaha za watu wakati anamuudhi Allah swt, basi Allah swt humwachia watu ( na yeye atakuwa mbali na baraka za Allah swt), Wassalaam’.”

33. Amesema Al-Imam Zayn Al-Abedin a.s. , Al-Kafi, J.2, Uk.81

“Yeyote yule atendaye matendo yake kwa mujibu wa vile alivyoamrisha Allah swt, ni miongoni mwa watu bora.”

34. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Al-Kafi, J.2, Uk. 124

“Yeyote yule aliye na mapenzi ya Allah swt,anachukia kwa ajili yake Allah swt, na anatoa msaada kwa ajili ya Allah swt, basi huyo ni miongoni mwa wale ambao Imani yao imekamilika.”

35. Amesema Al-Imam Al-Hasaan Al-Askari, Imam wa Kumi na Moja, a.s. , Bihar al-Anwaar,

J.17, Uk. 218

“Hakuna sifa zaidi ya hizi mbili: Kuwa na Imani kwa Allah swt na kuwa mwenye manufaa kwa Waislamu.”

TAQWA NA UMUHIMU WAKE KWA WAISLAMU

36. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Bihar al- Anwar J. 71, Uk. 373

“Miongoni mwa kitu kilicho muhimu kabisa kwa kuwafikisha watu hadi kufikia Peponi ni taqwa na tabia njema.”

37. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Bihar al- Anwar ,J.77, Uk. 130

“Wakati wa kutoa uamuzi wa kitu, fikiria matokeo yake. Iwapo ni nzuri kwako wewe kuendelea na maendeleo, fuata hivyo, lakini iwapo inakupotosha, uiachilie mbali …..”.

38. Aliulizwa Al-Imam As - Sadique a.s. kuhusu maana ya taqwa, na alijibu , Safinat ul-Bihar,

J.2, Uk.678:

“Allah swt hakukosi mahala pale alipokuamrisha wewe uwepo, na hakuoni pale ambapo amekuharamishia wewe kuwepo.”

39. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Mustadrak Al-Wasa’il-ush-Shi’h, J.8, Uk.466 no. 10027:

“ Onyesha heshima zako kwa ajili ya Allah swt kama vile utakavyoonyesha heshima zako mbele ya mtu mwema miongoni mwa ukoo wako.”

40. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s. , Ghura-ul-Hikam, Uk. 321:

“Kwa mtu kuinamisha macho yake kutamwia kama kizuizi dhidi ya matamanio (shahwa) yake.”

41. Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s. amewaambia wana wake Al Imam Al-Hassan na Al-Husayn a.s. wakati ‘Abdur Rahman ibn Muljim (Allah amlaani) alipokuwa amempiga dharuba ya upanga kichwani mwake, katka Nahjul Balagha, Barua no. 47:

“Ninawasihini nyote mumwogope Allah swt na nyinyi wala musiwe na uchu wa starehe za dunia hii hata kama itawakimbilia nyinyi. Wala musikisikitikie kitu chochote cha dunia hii ambacho mumekikosa. Semeni ukweli na mutende (kwa kutumai) malipo. Muwe adui wa mdhalimu na msaidizi wa mdhulumiwa.”

42. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s. , Nahjul Balagha, Barua no. 31

“Ninawauusieni kumwogopa Allah swt, Ewe mwana wangu, kubakia katika Amri Zake, kuujaza moyo wako kwa ukumbusho Wake na kubakia katika kumtegemea Yeye tu. Hakuna Hakuna ushikamano unaotegemewa kuwa madhubuti baina yako na Allah isipokuwa wewe iwapo utaishikilia menyewe.

43. Abi Osama amesema kuwa alimsikia al-Imam as- Sadique a.s. akisema, Al-Kafi, J.2, Uk. 77

“Mujiepushe na adhabu za Allah, taqwa, ijtihadi,kusema ukweli, uaminifu katika amana,tabia njema na ujirani mwema. Muwaite wengine kwenu (kwa tabia zenu njema), wala si kwa maneno tu. Muwe watu wenye kupendeza na kamwe musiwe watu wa kutuaibisha. Ninawausieni murefushe rukuu’ na sujuda zenu. Kwani kila mmoja wenu anaporefusha rukuu’ na sujuda basi Sheitani hulia nyuma yenu kwa kusea ‘ Ole wako ! yeye ametii; amesujudu na mimi nilikataa.”

44. Imam Ali ibn il-Husayn a.s. amesema, Bihar al- Anwar ,J.69, Uk. 277:

“Kwa hakika marafiki wa Allah hawatakuwa na khofu yoyote juu yao wala hawatakuwa watu wenye kuhuzunika) iwapo watadumisha yaliyofaradhishwa na Allah swt, wakafuata Sunnah za Mtume s.a.w.w., wakajiepusha na yale yaliyoharamishwa na Allah swt, wakawa wacha Mungu wema katika kile walichonacho katika utajiri na wadhifa wa humu duniani, wakajitahidi kujitafutia kile kilicho halali, wakaamua kutojifakharisha wala kutojilimbikia katika mali na utajiri isipokuwa katika kutoa misaada na kutoa malipo ya kulipa yaliyofaradhishwa kwake. Basi kwa hakika hao ndio waliobarikiwa katika mapato yao na watalipwa mema kwa yale waliyoyatanguliza huko Aakhera.”

45. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Mustadrak al-Wasa’il J. 12, Uk. 89

“Kwa hakika Wana wa Adam wapo sawa na meno ya kitana kuanzia zama za Mtume Adam a.s. hadi leo, na wala hakuna utukufu wa Mwarabu juu ya asiye Mwarabu, wala Mwekundu juu ya Mweusi isipokuwa kwa Taqwa.”

46. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Al-Kafi, J. 2, Uk. 76

“Kwa hakika, tendo dogo kabisa lifanywalo pamoja na Taqwa ni bora kabisa kuliko tendo kubwa (au matendo mengi) lifanywalo bila Taqwa.”

K U O M B A D U A

47. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Al-Kafi J.2, Uk.493

“Dua yoyote inayoombwa kwa Allah swt, inakuwa imezuiwa na mbingu hadi hapo iwe imeshirikishwa na Salawat i.e. kumsaliwa Mtume Muhammad s.a.w.w.pamoja na Ahlil Bayt a.s.”

48. Amesema al-Imam as- Sadique a.s., Al-Kafi J.2, Uk.491

“Muminiin ambao Dua zao hazikukubaliwa humu duniani watatmani kuwa dua zao hata moja

zisingelikubaliwa pale watakapoonyeshwa hapo Aakhera, mema kupita kiasi ya thawabu (akipewa yeye kwa kutokujibiwa Dua zake na kwa mateso na shida alizozipata akiwa humu duniani).”

49. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s., Bihar al- Anwar , J.93, Uk. 295

“Tendo lipendwalo sana mbele ya Allah swt humu duniani ni Dua na ibada iliyo bora kabisa mbele Yake ni unyenyekevu na ucha-Mungu.”

50. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s., Al-Khisal cha Sadduq, Uk. 302

“Milango ya Peponi ipo wazi kwa nyakati tano: wakati mvua inyeshapo; wakati wa Vita vitukufu; wakati wito wa Sala utolewapo (wanapotoa Adhaan) ; wakati wa kusoma Qur’an Tukufu wakati ambapo jua linazama na linachomoza alfajiri.”

51. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s., Bihar al- Anwar ,J.93, Uk. 343

“Mujiweke tayari kuomba Dua katika nyakati tano: Wakati usomwapwo Qur’an; Wakati utolewapwo Aadhaan; Wakati unaponyesha mvua; Wakati wa kwenda kupigana katika vita vitakatifu kwa ajili ya kuwa shahidi; Wakati madhulumu anapoomba dua, kwa sababu yeye hana kizuizi cha aina yoyote chini ya mbingu.”

52. Amesema Al-Imam al-Husayn a.s. ,katika Dua-i-‘Arafah

“Ewe Mola Wangu ! Wewe U karibu kabisa wa kuombwa; Na mwepesi wa kujibu; na Wewe Mkarimu wa kutoa; na unamtosheleza umpaye; unamsikia vyema akuulizae; Ewe Uliye Rahmaan wa dunia na Aakhera na Mremehevu kote !”

53. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s. , Nahjul Balagha, Msemo 135

“Anayejaaliwa vitu vinne hanyimwi vinne: Anayejaaliwa kuomba Dua hanyimwi kukubalika kwake; anayejaaliwa kufanya Tawba hanyimwi kukubalika kwake; anayejaaliwa kuomba msamaha hanyimwi kusamehewa kwake; anayejaaliwa kutoa shukuurani zake hanyimwi kuongezewa kwake.”

54. Amesema al-Imam as- Sadique a.s., Bihar al- Anwar , J. 78, Uk. 216

“Siku ya Qiyama, Allah swt atazihesabu Dua zote alizokuwa akiziomba Mja wake na kuuzibadilisha katika matendo mema na kwa hayo atawapandisha daraja katika Jannat (Peponi).”

55. Amesema al-Imam as- Sadique a.s., At- Tahdhib, J. 4, Uk. 112

“Ponyesheni magonjwa yenu kwa kutoa sadaqah na mujiepushe na balaa za kila aina kwa Dua

56. Amesema al-Imam as- Sadique a.s., Wasail-ush-Shi’ah J. 7, Uk. 60

“Mwombe Allah swt maombi yako na daima uwe ukisisitiza katika kumwomba kwani Allah swt mwenyewe anapenda mno kubakia kwa kumsisitiza miongoni mwa waja wake Muminiin.”

57. Amesema al-Imam as- Sadique a.s., Al-Kafi, J. 2, Uk. 467

“Ninakuusieni muombe Dua’, kwa sababu hamtaweza kumkaribia Allah swt kwa vinginevyo kama hivyo.”

58. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s., Ghurar-ul-Hikam, Uk. 185

“Inawezekana kuwa wewe umemwomba Allah swt Dua ya kitu fulani ambacho yeye hakukujaalia kwa sababu yeye anataka kukupa kitu kilicho bora zaidi ya kile ulichokuwa umekiomba, hapo mbeleni(unatakiwa kufanya subira - mtarjum).”

AHLUL BAYT a.s.

59. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Bihar al- Anwar ,J.27, Uk. 113

“Mfano wa Ahlul-Bayt yangu kwa Ummah wangu ni sawa na Safina ya Mtume Nuh a.s. Wote wale watakaoipanda ndani yake basi wameokolewa na wote wale waupingao, basi wamezama na kupotea ….”

60. Amesema Al-Imam Muhammad al-Baqir a.s., Imam wa tano, Bihar al- Anwar , J. 2, Uk. 144 :

“Ahadith zetu (za Alhul Bayt) zinahuisha nyoyo.”

61. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Bihar al- Anwar , j.38, Uk. 199

“Muhuishe mikutano na mikusanyiko yenu kwa makumbusho ya Ali ibn Abi Talib a.s.”

62. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Ikmal-ud-Din, j. 1, uk.253

na yenye maana yakaribiayo katikaYanabi-ul-Muwaddah, uk. 117

Ipo riwaya kupitia Jabir-il-Ju’fi iliyopokelewa kutoka Jabir-ibn-Abdillah isemayo: Mimi nilisema: Ewe Mtume wa Allah swt, sisi tunamwelewa Allah swt na Mtume wake s.a.w.w. Sasa jee hawa Ulul-Amr ni wakina nani ambao utiifu wao umefardhishwa sawa na wako ?

Hapo Mtume s.a.w.w. alisema: “Ewe Ja’abir ! Wao ni, baada yangu, Makhalifa wangu na Ai’mmah wa Waisilamu; wa kwanza miongoni mwao ni Ali ibn Abi Talib a.s.; atafuatia (Imam) Hassan, na (Imam) Husayn; atafuatia Ali ibn il Husayn; atafuatia Muhammad ibn Ali; ajulikanaye katika Tawrati kama Baqir, ambaye utakutana naye, Ewe Ja’abir ! Pale utakapomtembelea, umpe salaam zangu. Baada yake Musa ibn Ja’afar; atafuatia Ali ibn Musa, atafuatia Muhammad ibn Ali; atafuatia Ali ibn Muhammad, atafuatia Hassan ibn Ali; na baada yake (atakuja) Al-Qaim, ambaye jina lake ni sawa na jina langu. Yeye ndiye atakaye kuwa Mamlaka Ya Allah swt juu ya ardhi hii na Aliyebakia miongoni mwa Waja wake. Yeye ndiye mwana wa (Al-Imam) Hassan ibn Ali ( al-‘Askari). Huyu ndiye shakhsiyyah ambaye Allah swt atafungua Dhikiri zake Mashariki na Magharibi na huyu ndiye Shakhsiyyah ambaye atakuwa ghaibu kwa wafuasi na wapenzi wake ambavyo hakuna nyoyo zozote zile zinazoweza kukubali isipokuwa nyoyo za wale tu ambao Allah swt ameshakwishakuzijaribu kwa ajili ya Imani.”

Ja’abir alisema: “Mimi nilimwuliza ‘Ewe Mtume wa Allah swt ! Je wafuasi wake watafaidika naye wakati akiwa ghaibu ? Mtume s.a.w.w. alijibu: ‘Naam. Kwa kiapo cha Yule aliyenichagua kuwa Mtume, wao watafaidika kwa nuru yake na watafaidika kwa ibada akiwa ghaibu kama vile kufaidika kwa watu kutokana na (nuru ya ) jua hata pale linapofunikwa kwa mawingu…….’ “

63. Amesema Malik ibn Anas kuhusu mema ya Imam As-Sadique a.s. , Bihar al- Anwar J. 47. Uk. 28

“Hakuna macho yaliyowahi kuona, hakuna masikio yaliyokwisha kusikia, na wala hakuna moyo uliyokwisha shtushwa kwamba kunaweza kuwapo na mtu yeyote aliye bora zaidi kuliko (Imam) Ja’afar as- Sadique (a.s.) katika Taqwa, elimu, ibada na Ucha-Mungu.”

64. Amesema Al-Imam al-Husayn a.s., Al-Irshaad, uk. 204

“Kwa roho yangu, hakuna Imam isipokuwa ni Hakimu kwa Kitabu, anaimarisha uadilifu, anaamini katika Dini ya Ukweli, na anajizuia nafsi yake pamoja na njia ya Allah swt.”

MAPENZI YA AHLUL-BAYT a.s.

65. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Al-Jami’-ul-Saghir, J. 1 uk. 14

“Wafunzeni watoto wenu vitu vitatu: Mapenzi ya Mtume wenu, Mapenzi ya Ahlul-Bayt, usomaji wa Qur’an.”

66. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Bihar al- Anwar , J. 74, uk. 354

“Mtu yeyote ambaye hawezi kutufanyia wema wowote sisi Ahlul-Bayt basi wawafanyie mema wafuasi wetu walio wema; na yeyote yule asiyeweza kutuzuru, basi wanaweza kuwazuru wafuasi wetu walio wema ambavyo thawabu za kutuzuru sisi zitaandikiwa yeye.”

67. Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s., Al-Kafi, J.1, uk. 187

“Kwa kile kilicho bora kabisa kwa mja kumkaribia Allah swt ni utiifu kwake Allah swt, utiifu kwa Mtume s.a.w.w. na utiifu kwa ulil Amr.”

Aliendelea kusema: “Mapenzi yetu (ya Ahlul-Bayt) ni Imani na chuki dhidi yetu ni kufr.”

68. Amesema al-Imam as- Sadique a.s., Bihar al- Anwar , j.27, uk.91

“Kwa hakika zipo daraja za ibada, lakini mapenzi yetu , Ahlul-Bayt, ni ibada iliyo bora kabisa.

SIFA NA TABIA ZINAZOKUBALIKA

69. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. Al-Kafi, j.2, uk.235

“Je niwatambulisheni Mumiin ni nani? Mumin ni yule ambaye waumini wengine wanamwamini kwa nyoyo zao na mali pia. Je niwatambulisheni Mwislamu ni nani ? Mwislamu ni yule ambaye Waislamu wengine wanakuwa wamehifadhika kwa ulimi na mikono yake….. Ni haramu kwa Mumiin kumfanyia ubaya mumin mwenzake, au kumwacha katika hali ya shida, au kumsengenya au kumkataa kwa ghafla.”

70. Amesema al-Imam as- Sadique a.s., Usul-i-Kafi,j.2, uk. 374

“Haimpasi Muislamu kuhudhuria au kushiriki katika mikutano au mikusanyiko ambapo Sharia za Allah swt zinavunjwa na kwamba yeye (huyo Muislamu) hana uwezo wa kuyazuia hayo.”

71. Amesema al-Imam as- Sadique a.s., Khisal cha Sadduq, j.1, uk. 88

“Yeyote yule kwa tabia yake husema ukweli, basi matendo yake yametakasika; Na allah swt humwongezea riziki yule aliye na nia njema; na yeyote yule awatendeaye mema familia yake, Allah swt humwongezea umri mrefu.”

72. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s., Safinat ul-Bihaar, j.1, uk.599

“Mtume s.a.w.w. alijiwa na mtu mmoja aliyeomba kufundishwa tendo kwayo ataweza kupendwa na Allah swt pamoja na watu, utajiri wake utaongezeka, mwili wake utakuwa na siha nzuri, umri wake utaongezeka na atainuliwa Siku ya Qiyama pamoja na Mtume s.a.w.w.

Mtume s.a.w.w. alimjibu: ‘Hizi ndizo njia sita zinazohitaji sifa sita:

Iwapo wataka Allah swt akupende, lazima umwogope na ujiepushe na madhambi,

Iwapo wataka watu wakupende, lazima uwe mkarimu kwao na ukatae walichonacho mikononi mwao,

Iwapo wataka Allah swt akuongezee utajiri wako, hunabudi kutoa malipo yaliyofaradhishwa kwako i.e. Zaka, Khums, na zinginezo.

Iwapo wataka Allah swt aupatie mwili wako afya njema, basi uwe ukitoa sadaqa kila mara iwezekanavyo,

Iwapo wataka Allah swt aurefushe umri wako, basi uwe ukiwajali majamaa zako,

Iwapo wataka Allah swt akuinue pamoja nami Siku ya Qiyama, basi ni lazima urefushe sujuda zako mbele ya Allah swt, aliye Pekee na Mmiliki.”

73. Amesema Al-Imam Ar-Ridhaa a.s. Imam wa Nane, ‘Uyun-ul-Akhbaar ur-Ridhaa, j.1,uk.256

“Mumin hawezi kuwa mumin kamili hadi hapo atakapokuwa na mambo matatu: Sunna za Allah swt, Sunna za Mtume s.a.w.w. na Sunna za Imam a.s. wake. Ama Sunna za Allah swt ni kuzificha siri zake; kama vile Allah swt anavyosema katika Sura Al-Jinn, 72, Ayah 26 & 27.

Na ama Sunna za Mtume s.a.w.w. ni kule kupatana na kuelewana na watu, wakati ambapo Allah swt alimtuma Mtume wake kuwapenda watu na Amesema: ‘Uzoee usamehevu na uwafundishe mema na ujiondoe kutoka majaheli

Ama kuhusu Sunna za Imam a.s. (kuwa imara na) mwenye subira katika siku nzuri na siku mbaya na nzito, ambavyo Allah swt anatuambia katika Sura Al-Baqarah,2, Ayah 177. “

74. Amesema Al-Imam Muhammad ibn Ali a.s., al-Jawad, Imam wa Tisa, Muntah al-‘Amal, uk.229

“Mumin anahitaji mambo matatu: mafanikio yatokayo kwa Allah swt, mwenye kujipa mawaidha, kukubaliwa na yule ampaye nasiha.”

75. Imam ‘Ali ibn il-Husayn a.s., Imam wa Nne, aliulizwa “Ewe mwana wa Mtume ! Huanzaje siku yako ?” Na Imam a.s. alijibu, Bihar al- Anwar j.76, uk. 15:

“Mimi huanza siku yangu huku nikitakiwa kutimiza mambo manane (8): Allah swt ananitaka nitimize yaliyafaradhiwa juu yangu; Na Mtume s.a.w.w. ananitaka nitimize yale yaliyo Sunna yake; Familia yangu inanitaka mimi niwatimizie mahitaji yao kama chakula n.k.; Nafsi yangu inanitaka niitimizie matamanio yangu; Shaytani aninitaka mimi nitende madhambi; Malaika wawili wanaonihifadhi wananitaka mimi nitende matendo kwa moyo halisi, Malaika wa Mauti anataka roho yangu na Kaburi inautaka mwili wangu. Basi mimi ndivyo nilivyo baina ya mzunguko wa matakwa hayo.”

76. Amesema al-Imam as- Sadique a.s. , Bihar al- Anwar , j. 67 uk.305

“Kwa hakika kila kitu kinashawishiwa na Mumin kwa sababu Dini ya Allah swt inamfanya yeye awe ni mtu mwenye nguvu, na wala yeye kamwe hashawishiwi na kitu chochote kile, na kwa hakika hii ndiyo dalili ya kila Mumin.

  Yaliyomo endelea