Yaliyomo endelea

(VIZITO VIWILI)
HADITHI YA THAQALAIN

MWANDISHI: SEYYID MUHSIN ALKHARRAZI

MTARJUMI : SALIM NG’ANG’A MWEGA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

Na kwake twaomba msaada

Himidi zote ni za Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu. Kisha swala na salamu zimshukie Mtume wetu Muhammad pamoja na aali zake watoharifu. Na hasira ya Mwenyezi Mungu iwafikie maadui zao wote hadi siku ya kiyama.

Utangulizi

Kuambatana na Hekima ya Mwenyezi Mungu

Baada ya hayo, jua ya kwamba hekima ya Mwen-yezi Mungu inamlazimu yeye kuwaongoza watu katika kuyafikia yaliyo mema na yenye maslahi kwao, humu duniani na huko akhera, ili waweze kuupata ukamilifu unaoambatana na lengo la maumbile yao, ambao ni, kumjua Mwenyezi Mungu na kuupata ukurubifu wake.

Uongofu wake unapatikana kwa njia ya wahyi na kuviteremsha vitabu vitukufu na kwa kuwatuma manabii na marasuli na kuwateua mawasii. Huu uon-gofu umeendelea kupatikana tangu alipoumbwa Nabii Adam (a.s) na wala watu hawakuwahi kutouhitajia kamwe katika zama mojawapo, kwani akili zao hazikuyajua maslahi yao yote (yanayowafaa) ya humu duniani na huko akhera, bali daima walikuwa ni wenye kuuhitajia msaada wa Mwenyezi Mungu kwa kupitia wahyi na mitume watukufu. Nao wahyi hautengamani na Mtume bali vyote viwili ni kama mapacha, vina-shirikiana katika kuwafikishia watu uongofu wao.

Basi kila Mtume alikuwa na wahyi na kila wahyi ulikuwa na Mtume. Naam, kuteuliwe kwa mitume (manabii) na wajumbe (marasuli) kulipo khitimishwa, Kitabu kitukufu kilichokuwa kimeteremshwa na Mwenyezi Mungu kilibaki mikononi mwa wasii, kwa-ni watu walikuwa ni wenye kukihitajia daima Kitabu hiki pamoja na mfafanuzi wa yaliyomo ndani yake, ambaye ni mwalimu na mlezi na mtakasaji.

Hili ni jambo lenye uhakika linaloungwa mkono na kila mwenye akili safi, pamoja na riwaya (hadithi) zilizo mutawatir (nyingi).

Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa kuonyesha mshangao kutokana na kukanusha kwa makafiri amesema;

وكيف تكفرون وانتم تتلى عليكم آيات الله وفيكم رسوله ومن يعتصم بالله فقد هدى الى صراط مستقيم

“Na mnakanushaje, hali nyinyi mnasomewa aya za Mwenyezi Mungu na Mtume wake yuko pamoja nanyi? Na mwenye kushikamana Mwenyezi Mungu (sawa sawa) basi yeye amekwisha ongozwa katika njia iliyo-nyooka”.[1]

Yaani, mnakufuruje na kukanusha ilhali aya za Mwenyezi Mungu zasomwa mbele yenu na mjumbe (Rasuli) wake, naye yu pamojo nanyi anawapa mawa-idha na kuwakataza mabaya. Na Mwenye kushika-mana na Mwenyezi Mungu kwa hakika atakuwa amepata uongofu bila shaka. Kwa hivyo tunaona wazi kuwa aya tukufu inatuthibitishia kuwa kufuru na upotofu havipatikani vinapokuwepo vitu viwili, navyo ni:

kwanza: Aya zinazosomwa, nazo ni Qurani tukufu.

Pili: kuwepo kwa Mtume (s.a.w.a).

Mwenye kuvikhalifu hivi viwili basi amekwisha-potea na kutoka kwenye njia iliyonyooka, kinyume cha mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu kwa kuzipokea aya na kumfuata Mtume (s.a.w.a). Basi huyo amekwishaongoka na kuipata njia iliyonyooka.

Kufuatana na msingi huu wa haki Mtume (s.a.w.a) alitaka kuubainishia umma wa kiislamu njia ya sawa ili wasipotee baada ya kufa kwake, bali waifwate njia iliyonyooka. Na hii ndio sababu hasa ya kuwaongoza katika kukifuata Kitabu cha Mwenyezi Mungu na katika kuwafuata Ahlulbait (a.s), ili kwamba sababu za uongofu na saada yao ya dunia na akhera zidumu kuendelea. Mtume (s.a.w.a) aliwabainishia kwa njia tofauti tofauti na katika sehemu na nyakati zilizona-sibiana na maudhui.

Miongoni mwazo ni; hadithuth thaqalain (Hadithi ya vizito viwili) iliyo maarufu na yenye kuafikiana ma-dhehebu ya kishia na kisunni. Mtume (s.a.w.a) kwa maneno yoliyoko kwenye hadithi hii alitaka kuuongoza umma katika mustakbali wao hadi siku ya kiyama.

Hadithuth Thaqalain

Hakuna shaka kuwa hii hadithi inayopatikana kwenye vitaba vya madheheba yote inaelezea kwa uwazi kwamba Mtume (s.a.w.a) hakuupuuza umma wa kiislamu na kuuacha hivi hivi bila ya mwongozo, bali aliwaelezea cheo kitukufu cha Quran na kizazi chake kitoharifu, na kuuwajibishia umma kushika-mana navyo. Kisha akawadhaminia washikanao navyo kuwa hawatapote, na kisha akasisitizia kuwa kamwe havitatengana hadi vitakaporudi kwake huko hodhini mwa kauthar. Kwa maneno haya alibainisha wazi kabisa kutotengana na kutofarikiana kwa kizazi kutokana na Quran, na kutotengana kwa Qurani kuto-kana na kizazi chake. Kisha akauainsishia umma wa kiislamu maregeleo yao katika mambo ya kielemu na katika mambo ya kisiasa.

Haya, pamoja na kuwa hadithi haionyeshi kuwa mambo haya yanahusu zama fulani makhsusi, bali inanyesha kuwa ni wajibu unaoendelea juu ya wais-lamu wote katika kila pembezoni mwa ardhi na katika kila wakati na zama.

Kutokana na haya, na yatakayokuja tunatambua ya kwamba uchunguzi na kufikiria kwa makini kuihusu hadithi hii ni kitu chenye faida kubwa kwetu na kwa ndugu zetu waislamu ambako kutaondosha dhana mbaya zinazosababisha kukhitilafiana na kufarikiana.

Uchunguzi wa hadithi hii unagawanyika katika sehemu zifwatazo.

SEHEMU YA KWANZA

Sanadi (Silsila ya wapokezi wa hadithi)

Waislamu wanaafikiana kuhusu kuwepo kwa hadithi hii na maulamaa wa kiislamu wameinukuu kwenye vitabu vyao tofauti tofauti, vya hadithi, vya tafsiri (ya Qurani) na vya historia, kwa kuzitaja njia nyingi za wapokezi na sanadi zilizosahihi zenye kutegemewa.

Katika kitabu kiitwacho “Ghayatul Muram”, mwa-ndishi wake ametaja hadithi thalathini na tisa kutoka kwa njia za wapokezi wa kisunni na hadithi thamanini na mbili kutoka kwa njia za wapokezi wa kishia.[2]

Vile vile Allama Mir Haamid Husein(r.a) ameipo-kea hadithi hii kutoka kwa kikundi cha maulama wakubwa wa madhehebu yote, wanaokaribia baina ya tisini na mia, tangu karne ya pili hadi karne ya kumi na tatu.[3]

Naye seyyid Almuhaqqiq Abdul Aziz Attaba tabai (r.a) amemzidi kwa kuwataja maulama mia na ishirini na moja wa karne ya pili hadi karme ya kumi na nne.[4]

Kwa hivyo basi, idadi ya maulama wa kisunni walioinakili hadithi hii, imefikia mia tatu na kumi na moja.

Ibnu hajar katika kitabu cha Assawaiqul Muhriqa amesema kuwa “Na hadithi hii ina njia nyingi za wapokezi”.[5]

Hata hivyo hadithi hii imetajwa katika vitabu vyenye kutegemewa na vilivyo maarufu. Miongoni mwavyo ni Sahihu Muslim, Sunanut Tirmidhi, Sunanud Darami, Musnadu Ahmad, Ibnu Hanbal, Khasaisun Nasai, Mustadrakul Hakim, Usudul Ghaba, Alaqdul Farid, Tadhkiratul Khawaass, Dhakhairul uqba, Tafsiruth Tha’alabi na vinginevyo.

Hii, ni bila ya kuvitaja vitabu vyote vya kishia. Hata hivyo wameipokea hadithi hii, maswahaba wengi, wake kwa waume.

Ibnu Hajar amesema katika Assawaiqul Muhriqa kuwa “Hadithi ya tamassuk (yaani hadithuth thaqalain) ina njia nyingi za wapokezi, (zilizotufikia) kutoka kwa maswahaba zaidi ya ishirini”[6]

Kitabu cha Abaqatul Anwar kimeinukuu hii hadithi kutoka kwa vitabu vya kisunni kutoka kwa maswahaba thalathini na wanne, wake na waume.[7] Bali idadi ya maswahaba wa kike na kiume inafikia zaidi ya hamsini ikiwa tutaongezea pia njia zote za upokezi za kisunni na za kishia zilizo tajwa katika vitabu vya Ihqaqul Haqq na Ghayatul muram na vinginevyo.

Haya ndio majina yao, kama ifwatavyo:-

1) Amirul muumin Ali ibnu Abi Talib (a.s).

2) Al-imam Alhasan ibnu Ali (a.s).

3) Salman Alfarisi.

4) Abu Dhar Alghaffari.

5) Ibnu Abbas.

6) Abu Sa’id Alkhidri.

7) Jabir Ibnu Abdillah Al-Ansari.

8) Abul Haitham Ibnu Attaiham.

9) Abu Rafi’I – mtumwa wa Mtume Mtukufu (s.a.w.a.)

10) Hudhaifa Ibnu Alyaman.

11) Hudhaifa Ibnu Usaid Alghaffari.

12) Khuzaima Ibnu Thabit Dhush shahadatain.

13) Zaid Ibnu Thabit.

14) Abu Huraira.

15) Abdullah Ibnu Hantab.

16) Jubair Ibnu Mut-im.

17) Albarrau Ibnu Aazib.

18) Anas ibnu Malik.

19) Talha ibnu Abdillah Attamimi.

20) Abdul Rahman Ibnu Auf.

21) Sa’ad Ibnu Abi Waqqas.

22) Amru Ibnu Al-aas.

23) Sahal Ibnu Sa’ad Al-ansari.

24) Udai Ibnu Hatam.

25) Uqba Ibnu Amir.

26) Abu Ayyub Al-Ansari.

27) Abu Shuraih Alkhuza’i.

28) Abu Qudama Al-ansari.

29) Abu Laila Al-ansari.

30) Dhamira Al-aslami.

31) Aamir Ibnu Laila.

32) Seyyidatuna Fati Matuz Zahra (a.s).

33) Ummu Salama.

34) Ummu Hani.[8]

35) Zaid Ibnu Arqam.

36) Ibnu Abi Dun-ya.

37) Hamza Al-Aslami.

38) Abdu Ibnu Hamid.

39) Muhammad Ibnu Abdur Rahman Ibnu Fulad.[9]

40) Abu Tufail Aamir Ibnu Waathila.

41) Amru Ibnu Murra.

42) Buraira.

43) Habashi Ibnu Junada.

44) Khalifa Umar Ibnu Alkhattab.

45) Malik Ibnu Alhuwairith.

46) Habib Ibnu Badlil.

47) Qais Ibnu Thabit.

48) Zaid Ibnu Sharahil Al-Ansari.

49) Aisha Binti Sa’ad.

50) Afif Ibnu Aamir.[10]

51) Abdullah Ibnu Umar.[11]

52) Ubai Ibnu Ka’ab.[12]

53) Ammar.[13]

Muhammad Mubin Allak-hanwi[14] na waliyyullah Allakhanwi.[15]

Naye Alhaithami anaseme wazi ya kuwa wapokezi wa hadithi hii ni thiqa (waliyosifiwa kuwa wakweli katika upokezi wa hadithi) [16] pamaja na dalili nyingi nyinginezo zenye ushahidi juu ya usahihi wa hadithi hii na ya kuwa ni mutawatir (Yaani hadithi iliyo pokelewa na watu wengi sana, kiasi cha kutuondolea shaka kuwa huenda ikawa Mtume Mtukufu (s.a.w.a) hakuwahi kusema maneno haya.)

Vile vlie kikundi kikubwa kimesema wazi kuwa ni hadithi mutawatir, miongoni mwao akiwa ni Assanani katika Kitabu chake, Mulhaqatul abhathul musaddada, aliposema, “Na riwaya zake (hadiththuth thaqalain) pa-moja na ushahidi zinazoutoa ni mutawaatir kimaana”[17] (yaani kuwa riwaya zake zinatafautiana kamatamshi lakini zinapatana kimaana pamoja na kuwa ni nyingi sana).

Na kwa vyovyote vile, madhehebu ya kislamu yameafikiana kuhusu usahihi wa hadithi hii na wala hakuna chembe ya shaka kuwa imetoka kinywani mwa Mtume Mtukufu (s.a.w.a).

SEHEMU YA PILI

Kuwafikishia watu wote ujumbe

Hadithi hii tukufu ilitoka kinywani kitukufu cha Mtume (s.a.w.a) katika sehemu nyingi tofauti tofauti, kiasi cha kudhihirisha kuwa lengo lake likikuwa kuu-fikisha ujumbe huu kwa waislamu wote ili kutimiza hoja kwa umma wa kiislamu.

(a) Siku ya arafa: Miongoni mwa sehemu hizi ni siku ya arafa kama ilivyo katika Sunanut Tirmidhi, kwa Sanadi ya Jaabir ibnu Abdillah, ya kwamba alisema.

(رأيت رسول الله(ص) في حجته يوم عرفة وهو على ناقته القصواء يخطب فسمعته يقول: ((يا أيها الناس اني تركت فيكم ما ان اخذتم به لن تضلوا: كتاب الله، وعترتي اهل رواية)).

“Nimliwona Mtume Mtukufu (s.a.w.a) katika hijja yake siku ya arafa, huku akiwa juu ya ngamia wake (aitwaye) qaswa akihutubu, nikamsikia akisema. “Enyi watu, hakika mimi ninaacha kati yenu ambavyo mkishikamana navyo hamtapotea kamwe, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu (ambao ndio) wapokezi wa hadithi zangu)”[18]

(b) Huko mina: Miongoni mwazo ni Mina, kama ilivyo katika kitabu cha Ghaibatun Nu’umani, kwa sanadi ya Hariz ibnu Abdillah kutoka kwa Abu Abdillah Ja’afar ibnu Muhammad (a.s) kutoka kwa babu yake (a.s.) kutoka kwa Ali(a.s.), ya kwamba alisema,

((خطب رسول الله (ص) في مسجد خيف – قال ((اني فرطكم وانكم واردون علي الحوض حوضاً عرضه ما بين بصرى الى صنعاء فيه قدحان عدد نجوم السماء، الا واني مخلف فيكم الثقلين: الثقل الاكبر والثقل الاصغر الثقل الاكبر القرآن والثقل الاصغر عترتي أهل بيتي هما حبل ممدود بينكم وبين الله جل وعز ما ان تمسكتم به لن تضلوا سبب منه بيد الله وسبب بأيديكم)).

“Mtume Mtukufu(s.a.w.a) alihotubia katika masjid-ul khiif – (nayo ni khutba mashuhuri katika hijja yake ya mwisho) na kusema “Hakika mimi ninawatangu-lieni, nanyi mtanikuta kwenye hodhi. Hodhi ambayo upana wake ni (mfano wa umbali ulioko) baina ya Basra na Sana. (Kwenye hodhi hii) kuna vyombo vya kunywea (maji ya kauthar) kwa idadi ya nyota za binguni. Basi jueni kwamba, Mimi ninaacha kati yenu viwili vizito; kizito kikubwa na kizito kidogo; kizito kidogo ni kizazi changu (ambao ni) ahlu baiti wangu. Hivi viwili ni kamba iliyonyooshwa baina yenu na baina ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka na Mwenye Nguvu, ambavyo mkishikamana navyo hamwezi kupotea kamwe. Upande mmoja uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na upande mwingine uko mikononi mwenu”.

(c) Huko Ghadir Khum: Miongoni mwa sehemu hizi ni Ghadir khum. Kama ilivyo katika Musta-drakul Haakim na katika vitabu vinginevyo, kutoka kwa Zaid ibnu Arqam, alisema “Mtume Mtukufu alipo kuwa akirejea kutoka hijja yake ya mwisho na kufikia (sehemu iitwayo) Ghadir aliamrisha kuwa miti mikubwa ikatwe, (waislamu wakafanya kama alivyo-sema) na kuitumia katika kuitengeza mimbar, kisha akasema;

((كأني قد دعيت فأجبت اني تارك فيكم الثقلين احدهما اكبر من الآخر كتاب الله وعترتي فانظروا كيف تخلفوني فيهما فانهما لن يتفرقا حتى يردا علي الحوض)).

“Naona kuwa nimeitwa (na Mola) nami nikajibu. Mimi ninaacha kati yenu viwili vizito, kimoja ni kikubwa zaidi kuliko kingine (nacho ni) Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu. Basi angalieni vile mtakavyo vitendea baada yangu kwani havitatengana kamwe mpaka vitakaponijia katika hodhi (ya kauthar)”. Kisha akaseme,

((ان الله عزوجل مولاي وانا مولى كل مؤمن))

“Hakika Mwenyezi Mungu Mwenye Nguvu na aliyetukuka ni Bwana wangu nami ni bwana wa kila Muumini” kisha akachukua mkono wa Ali (a.s) na kusema,

((من كنت مولاه فهذا وليه)).

“Ambaye mimi na bwana wake basi huyu ni bwana wake”.[19]

Muslim katika Sahihu Muslim[20] Attabrani katika Almu’ujamul Kabir[21] na wengineo[22] wameinukuu hii hadithi.

(d) Huko Madina: Miongoni mwa sehemu hizo ni Mji Mtukufu wa Madina, pale alipokuwa akirejea kutoka safarini, kama alivyopokea ibnu Almaghazili Ash-shafii katika Kitabu chake cha manaqib kutoka kwa Alhaakim, kutoka kwa Ibnu Abbas, ya kwamba alisemu, “Mtume alirudi kutoka (mojawapo ya) safari zake huku rangi (ya uso wake) ikiwa imebadilika. Alitoa hotuba yenye ufasaha wa hali ya juu huku akilia, kisha akasema,

((ايها الناس قد خلفت فيكم الثقلين كتاب الله وعترتي))

“Enyi watu hakika nimacha vizizo viwili kati yenu, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu”.

(d) Katika hotuka yake ya mwisho: Na miongoni mwazo ni hotuba yake ya mwisho (wa uhai wake) kama ilivyo katika Yanabiul Mawaddah kutoka kwa Alhamwini, ya kwamba Ali (a.s) alisema”,

((وفي آخر خطبة النبي(ص) يوم قبضه الله عزوجل: اني تركت فيكم امرين لن تضلوا بعدي ان تمسكتم بهما: كتاب الله عزوجل وعترتي اهل بيتي فان اللطيف الخبير قد عهد الي انهما لن يفترقا حتى يردا علي الحوض كهاتين ـ وجمع مُسّبحتيه ـ ولا اقول كهاتين ـ وجمع مسبّحته والوسطى ـ فتمسكوا بهما ولا تقدموهم فتضلوا)).

“Na katika hotuba ya Mtume Mtukufu (s.a.w.a) ya mwisho katika siku ile aliyoaga dunia na kurudi kwa Mola wake(alisema); “Hakika mimi ninayaacha mambo mawili (kati yenu) mkishikamana nayo hamtapotea kamwe baada yangu; Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na aliyetukuka, na kizazi changu (ambao ni) Ahlubaiti wangu; kwani Mjuzi wa yaliyo-fichika na yaliyodhahiri amenijulisha ya kwamba mambo (haya mawili) hayatotengana kamwe mpaka yatakaponijia katika hodhi (ya kauthar) kama hivi viwili – (akavishikanisha vidole vyake viwili vya shahada) na wala sisemi kama hivi viwili – (akaki shikanisha kidole chake cha shahada na kidole cha kati) – basi shikamaneni nayo (mawili) na wala msi-watangulie (Ahlu baiti) msije mkapotea”.[23]

Vile vile imepokewa mfano wake katika Gha-ibatun Nu’umani[24] na katika Arjahul Matalibi.[25]

Katika uganjwa wake (s.a.w.a): Na miongoni mwazo ni katika ungojwa wake ambao alifariki nao, kama ilivyo katika Yana biul Mawaddah Mwandishi wake amesema kuwa “Ibnu Uqba ameinukuu kutoka kwa njia ya upokezi ya urwa ibnu Kharijah kutoka kwa Fatima Azzahrah (a.s) ya kwamba alisema:

((سمعت ابي (ص) في مرضه الذي قبض فيه يقول وقد امتلأت الحجرة من اصحابه: ايها الناس يوشك ان اقبض قبضاً سريعاً وقد قدمت اليكم القول معذرة اليكم، الا واني مخلف فيكم كتاب ربي عزوجل وعترتي اهل بيتي ثم اخذ بيد عليّ فقال هذا علي مع القرآن والقرآن مع علي لا يفترقان حتى يردا علي الحوض فاسألكم ما تخلّفون فيهما)).

“Nilimsikia baba yangu (mpendwa) (s.a.w.a) katika ugonjwa wake aliofariki nao akisema, huku chumba chake kimejaa maswahaba wake, “Enyi watu, kifo changu kimekaribia sana, nami nime watangulizieni kauli, ili msiwe na udhuru (wa kutoa baada yake). Basi jueni kuwa nakiacha kati yenu Kitabu cha Mwen-yezi Mungu Mwenye Nguvu na Aliyetukuka, pamoja na kizazi changu (ambao ni) Ahlubaiti wangu”. Kisha akaushika mkono wa Ali (a.s) na kusema, “Huyu Ali yuko pamoja na Qurani na Qurani iko pamoja na Ali, hawatoachana (tengana) mpaka watakaponijia huko hodhini (mwa kauthar), nami niwaulizeni mlicho watendea baada yangu”.[26]

Na kuna mfano wa hadithi hii katika Addaru Qutni.[27]

Ibnu Hajar, baada ya kuwa tumenakili kutoka kwake ya kwamba hadithi hii imepokewa kwa njia nyingi za wapokezi amesema kuwa “(Tuna-pata kwamba) katika, baadhi ya njia hizo za upokezi, Mtume Mtukufu (s.a.w.a) aliyasema (maneno haya) akiwa Arafa na katika njia nyengine (tunapata kuwa) alisema akiwa Ghadir Khum, na katika njia nyengine alisema akiwa Madina katika ugonjwa wake, na huku chumba kimejaa maswahaba wake, na katika njia nyingine alisema aliposimama kuhotubia baada ya kutoka (mji wa) Taif, wala hakuna kupingana kwa maneno, kwani hakuna ubaya wowote katika kukariri katika sehemu hizo na nyinginezo ili kuonyesha umuhimu wa Kitabu Kutukufu na kizazi chake kitoharifu” [28].

Bila Shaka, Ibnu Hajar ametoa faida njema na kutenda wema kwa maneno aliyoyasema, kwani kuka-riri hakukuwa ila tu kwa ajili ya umuhimu uliomo katika mambo haya ili asibaki yeyote na udhuru katika hayo kama alivyoseme Mtume (s.a.w.a) katika kauli yake:

((وقد قدمت اليكم القول معذرة اليكم))

“Nami nimewatangulizieni kauli hii ili msiwe na udhuru (wa kutoa baada yake)”.

Arafa, Mina, Ghadir Khum, hotuba ya mwisho, na katika hali ya ugonjwa aliofariki nao, ni mfano wa sehemu na nyakati ambazo kiongozi hawezi kuzungu-mzia ila tu yale yenye uhusiano kamili na uhai na mustakbali wa uislamu na waislamu.

Kwa hivyo kukariri kulikotajwa, na hususan katika sehemu na nyakati zilizotajwa, pamoja na joto kali na msongamano wa watu na hasa katika siku ya mwisho wa uhai wake na katika ugonjwa aliofariki nao; kisha kuwajulisha waislamu kuhusu kifo chake, kulikuwa na lengo la kuwaelekeza waislamu kwenye jambo hili muhimu. Basi ni juu yetu na ndugu zetu waislamu (Mwenyezi Mungu awazidishie utukufu na sharafa) kufikiria kikamilifu kuhusiana na yaliyoelezwa katika hadithi hii tukufu, kisha kutenda kufwatana na maagizo yali yomo ndani yake..

Na yatupasa kujua pia, je sisi ni katika washikama-nao na Qurani na kizazi cha Mtume Mtukufu (s.a.w.a) au la?

Naapa kwa uhai wangu kuwa hii hadithi tukufu inayokubaliwa na waislamu wote, inatosha kuwa-bainishia waislamu njia sahihi na kuwasahilishia njia za kupata umoja na maafikiano baina yao.

Ewe ndugu muislamu, fikiria, taamuli na kuitakasa nafsi yako, kwani njia iko wazi, wala usiyakhalifu aliyousia Mtume Mtukufu (s.a.w.a) katika hali tofauti tofauti na katika hali zenye uzito na umuhimu mkubwa.

Basi wajibu wetu mbele ya maneno ya Mtume (s.a.w.a) ni kuyafikiria kisha kutenda kufwatana nayo, na kisha kuyaeneza katika pembezoni mwa ardhi ili kuiga mwenendo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.a) kama alivyofanya Abu dhar (r.a) alipoishika sehemu ya mlango wa kaaba na kusema mbele ya watu (walio-kuwepo) “Mimi nilimsika Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema”:

((إني تارك فيكم الثقلين: كتاب الله وعترتي فانهما لن يفترقا حتى يردا عليّ الحوض فانظروا كيف تخلفوني فيهما)).

“Hakika mimi ninaacha kati yenu vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu, kwani havitatengana kamwe mpaka vitakaponijia katika hodhi (ya kauthar). Basi angalieni mtakavyovitendea baada yangu”.[29]

Kusimamisha hoja kwa kutumia hadithi hii

Amirul Muuminin Ali (a.s) alitoa hoja kwa kutumia hadithuth thaqalain katika kikao cha shura ili kuthibitisha haki aliyokuwa nayo ya kuwa khalifa zaidi ya yeyote mwingine.

Ibnu Almaghazili amenakili kwa isnadi yake (njia ya upokezi) kutoka kwa Aamir ibnu waathila aliyese-ma “Nilikuwa chumbani pamoja na Ali siku ya shura nikamsikia akiwaambia (waliokuwemo);

((لأحتجنَّ عليكم مما لا يستطيع عربيكم ولا عجميكم بغير ذلك)) ثم قال: ((انشدكم بالله ايها النفر جميعاً أفيكم احد وحّد الله قبلي؟)) قالوا اللّهم لا ـ الى ان قال ـ ((فانشدكم بالله اتعلمون ان رسول الله (ص) قال: اني تارك فيكم الثقلين: كتاب الله وعترتي لن تضلوا ما استمسكتم بهما ولن يفترقا حتى يردا علي الحوض؟)) قالوا: اللهم نعم))

  Yaliyomo endelea