MLANGO 3

DARAJA (CHEO) ZA SAUMU

Saumu (kufunga) ina daraja tatu:

     Daraja ya kwanza: Ni kwa watu wote, na hiyo ni kujizuia na vitu vinavyovunja saumu, navyo ni kumi, kama tutavyoeleza baadaye. Na daraja hizi za saumu faida yake hasa ni kuondoa Wajibu wako tu, na kujiepusha na adabu iliyowekwa na Mwenyezi Mungu kwa wale wasiofunga. Lakini tusitoshelezwe na hayo tu, bali tujitahidi tuzipate daraja za mbele kama tuwezavyo ili tupate faida ya roho na baadhi ya thawabu waliowekewa wafunga saumu. Mtume (S.A.W.) amesema, "Katika vitu rahisi zaidi, alizofaradhisha Mwenyezi Mungu juu ya mwenye kufunga katika kufunga kwake, ni kuwacha kula na kunywa".

     Wakati wa saumu hii, kama tulivyoeleza, huanzia Subh Sadiq mpaka  magharibi.  Baadaye, mfunga  ameruhusiwa kuvunja saumu yake.

Daraja ya pili: Kufunga kwa mahsusi (ya peke yake) na hiyo ni kwanza kujizuia yavunjayo saumu zile kumi, na juu ya hayo kujizuia viungo vyake na mambo yaliyoharamishwa. Zimepokewa hadithi nyingi sana za Mtume (S.A.W.) na za Maimamu (A.S.) zinazotilia mkazo za kuhimiza jitihada kwa kila mwenye imani kuwa anafunga saumu kama hivyo na awe anajiepusha viungo vyake vyote kwa kila dhambi na ubaya aliokataza Mwenyezi Mungu viumbe wake.

     Anahadithia sahaba Bw. Muhammad bin Ajlaan, kwamba amemsikia Imaam Jaffer As-Saadiq (A.S.) anasema, "Kujizuia kula na kunywa tu hakuitwi kufunga siyamu, lakini ukifunga, ujifunge masikio, macho, ulimi, tumbo, utupu wako, pia na uzuie mikono na miguu yako, pia kwa kila kinachokatazwa, na ujaribu kukaa kimya kama uwezavyo ila kwa jambo la kheri na uwe mpole na mtumishi wako.

    Aina hii ya saumu haimaliziki unapokucha jua; kwa sababu mwislamu haruhusiwi kutenda dhambi wakati wowote. Kwa hivyo wakati wa saumu ya daraja hii huanzia siku mtu anapobalehe, na huishia wakati wa kufa kwake, kwani kanuni za sharia ni ya kufuatwa maisha mazima ya binadamu.

    Lakini saumu namna hiyo huharibika ikiwa mtu atatenda dhambi yoyote. Mtume wetu (S.A.W.) alimwona mwanamke mmoja aliyefunga saumu anamtukana mtumishi wake. Hapo Mtume akaagiza chakula na akamtaka yule bibi ale. Yule mwanamke akasema: "Yaa Rasuulal-llah, nimefunga mimi". Mtume akamjibu: "Hukufunga, kwa sababu umemtukana mtumishi wako".

    Amehadithia sahaba mmoja wa Imaam Al-Baqir (A.S.) kwamba Imaam alisema, "Uongo humfuturisha aliyefunga, na tazamo la pili [2] na udhalimu kidogo au mwingi, yote hayo bila shaka humharibia saumu mfunga".

    Na zaidi ya hayo, Dini ya Kiislaam inampendelea kila Mwislamu, kwa kila ubaya na taabu atakayofanyiwa, aikabili na kustahimili kwa wema, hasa anapokuwa amefunga, kwa heshima ya saumu, na kujipatia hiyo daraja tukufu ya saumu.

   Imepokewa kwa Imaam As-Sadiq (A.S.) Kwamba Mtume (S.A.W.) amesema, "Hakuna Kiumbe.aliyefunga akiamka asubuhi na kuamkia huku anatukana na kusema nimefunga basi yule anaetukanwa akavumilia matusi hapo Mwenyezi Mungu huwaambia Malaika, 'Mtumwa wangu kajilinda na saumu mbele ya  Mtumwa mwenziwe, basi Nyie Malaika mlindeni na moto wangu wa Jahannam na mtieni Peponi" (Maana ya kujilinda na saumu ni kuwa isingekuwa yule mtu aliyetukanwa amefunga. angeliweza kulipa matusi, lakini kaikabili kwa utulivu kwa taadhima ya ile saumu): Kwa kuwa thawabu zote za kufunga saumu, na daraja na cheo cha ,akhera, viliyyo wekewa kwa ajili ya wanaofunga ya daraja hii,. ndivyo mfunga saumu hujitenga na kila alichoharamisha Mwenyezi Mungu.

      Basi binadamu juu ya kujizuia nafsi yake na madhambi, afanye juhudi awezavyo kupata wema wote ambao imsaidie mtu kuwa karibu na Mola. Lazima afanye bidii kutenda amali ya heri kwa nia safi.

Daraja ya tatu: Kufunga mahsusi zaidi, naye kuepukana na kujitenga na yenye kuvunja saumu, na kila kilicho haramishwa na juu ya hayo kutenga moyo na tabia mbaya na dhamiri ya uovu, na mawazo ya mambo ya Dunia.

Mwenye kufunga saumu ya daraja hii bila shaka moyo wake husafika na kila kitu; hashughulikee jambo lolote isipokuwa ya Mwenyezi Mungu; na anaondoa moyoni mahaba ya kila kitu kwa ajili ya mahaba ya Mola.

      Daraja hii imeelezwa katika aya hii ya Qurani: Qul-illah Tthumma dhar-hum.   (Sema 'Allah', baadaye waachiye wote).

      Kufunga hivi haiwezi mtu isipokuwa yule aliye mwepusha Mwenyezi Mungu, kama Mitume na Maimaam (A.S.).

Saumu hii haina kuishia na kumalizika. Roho tukufu ya Wali wa Mwenyezi Mungu hukaribia zaidi kwa Mola baada ya kifo, na usafi wake hukamilika zaidi. Kwa hivyo saumu namna hii haina kufuturu.