MLANGO 1

SAUMU

Saumu (kufunga) ni kitu gani na vipi inatubidi kufunga?

Maana ya saumu inavyoelezwa katika kitabu cha lugha (Kamusi) ni kujizuia kufanya jambo fulani. Na maana yake kwa kisharia ni hii:- Mtu kujizuia kutwa na mambo yafuatayo yanayovunja saumu; kuanzia alfajiri ya pili iitwayo Subh-Saadiq hadi magharibi ya kisharia .[1]

Ukikaribia kuja mwezi mtukufu wa Ramadhani, utawaona watu wengi wameshughulika kuandalia huo mwezi mtukufu kwa furaha, vile vile (utawagundua) utawaona baadhi ya watu wanatafuta masingizio ya kutokufunga. Laiti wangefikiria faida ya kufunga na makusudio yake, ijapokuwa udhuru wenyewe wenye maana, na akajaribu kufunga. Ikiwa anafahamu fadhila na faida ya roho ambayo bupatikana kwa kufunga tu bila shaka hatawacha saumu hata siku moja.

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wenye baraka nyingi, na bwana wa miezi yote, na huitwa mwezi wa Mwenyezi Mungu. Katika mwezi huu Mwenyezi Mungu anawafungulia viumbe wake milango ya rehema, na rehema hizo kuwafikia na huwazingia viumbe wake. Basi ndugu zangu tufanye bidii kama tuwezavyo tuziteke hizo baraka na rehema za mwezi huu. Neema bora na kubwa ya mwezi huu ni hiyo kufunga saumu.

Hakika mwezi wa Ramadhani huwazindua na kuwaamsha katika usingizi waovu na wahalifu na kuwanabihisha kuyafahamu na kuyafuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu (mwenye hekima) ili kuepukana na yaliyo katazwa na dini ya Kiislam, wapate kujitenga nafsi zao kwa kutenda maovu, na kukimbilia kwa Mola wao, kwa kusali, kusoma dua kulisha na kufanya utiifu mwingi.

Walevi wengi huwacha kulewa mwezi wa Ramadhani na wafasiki na waovu wengi hawatubii ila katika mwezi wa Ramadhani na Wasiye amini wengi hawaoni huruma nyoyoni, lakini ukiingia mwezi huu mtukufu huruma inawajia na hulainisha nyoyo, na wenye mali (tajiri) wengi wasiowaonea huruma masikini ila ukiingia mwezi mtukufu ndipo huonyesha huruma.

Unapoingia mwezi wa Ramadhani tu basi huingia baraka, heri, na utiifu. Usiku na mchana wake hunawirika na kung'aa kwa ibada na utiifu wa watu. Misikiti na mahala pa ibada hujaa wachamungu wanaosujudu na kurukuu na huku wakiomba waghufuriwe. Wengine hushughulika kuisoma Qur'ani usiku na mchana, na kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mwenye huruma kwa nyoyo ya unyonge iliyo sali, huku macho yakilia na wakimwomba kwa sauti ya huzuni.

Huu ndio mwezi mtukufu wenye uzuri na jamala na kuwa bora kuliko miezi yote. Katika mwezi huu wanatubia wenye kutaka kutubia, na wanaomba kughufuriwa wenye kutaka kughufuriwa, na huo ndio msimu wa wenyekufanya ibada. Basi ewe mwenye kufanya ibada hima kimbilia kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu.

Usije mwezi mtukufu huu ukapita, ila nawe uwe na tamaa ya kuwa umekwisha ghufuriwa.

Ewe tajiri, masikini, mwenye miliki, mkulima, na waungwana wakubwa na wadogo, msiwadhulumu walio chini yenu na msishindane na wakubwa wenu.

Ewe, mwislamu mahala popote ulipo, kimbilia kufanya mema ya kumridhisha Mola na Mtume, na pia waridhishe Maimamu "Masoomeen" (A.S.) kwani mwezi huu ni mwezi ule ambao Mwenyezi Mungu huyafuta madhambi na huongeza juu ya hayo thawabu kwa viumbe, na huinua daraja zao; basi tukimbilie kumridhisha Mola, tukimbilie kufanya ibada, na tukimbilie kutubia kwa Mwenyezi Mungu.

Tukitaka kueleza kwa urefu manufaa yote ya saumu kwa kiwiliwili, kwa tabia na mwenendo, kwa roho, na kwa dini, itakuwa taabu sana. Hapa tutatoshelea kueleza kwa ufupi kwa kutoa mifano tu.

Faida kwa kiwiliwili

Ni maalumu kwamba kiwiliwili cba binadamu ni kama mashini ambayo huhitajia mapumziko kidogo. Na mapumziko hayo hayawezi kupatikana hadi mtu ajizuie kula na kunywa kwa muda ambao ala ya kuyeyusha chakula (tumbo) itulie. Vile vile upatie moyo na vifaa vyote vya ndani mapumziko na kusafisha yenyewe. Basi kwa kufunga saumu hupungua, na pengine hutoka kabisa maradhi.

Elimu ya afya siku hizi imethibitisha kwamba mtu kuweka siha yake vizuri, inampasa kwa uchache afunge saumu, siku moja katika kila wiki, au wiki moja kila mwezi na bora mwezi mmoja kila mwaka.

Vile vile imethibitisha elimu za sasa kwamba bidii za akili na nguvu ya mwili huzidi kwa kuuweka mwili katika

hali ya njaa. Bila shaka faida na maendeleo yanaweza kupatikana kwa kufunga saumu, kuliko mtu anapokuwa amejaa tumbo na uvivu pia umemshika. Madaktari na matabibu katika maradhi nyingi huwaongoza wagonjwa wao kufunga. Zipo baadhi ya maradhi kama mtu akifunga saumu tu badili ya kutumia dawa atapona kabisa. Baada ya kujua na kufahamu hayo yote, basi tutapata hakika kuwa Mwenyezi Mungu kwa njia na taratibu bora kabisa ametuamrisha kuwacha kula; na kitendo hicho kakifanya kuwa ni Ibada. Hii ni uthibitisho dhahiri wa huruma juu ya viumbe wake, isitoshe haya kakifanya hicho kitendo (kufunga) si faida ya duniani tu, bali kwa akhera pia. Juu ya hayo yote ikiwa tutahalifu, tutakuwa watu wajinga mno, tusio na mfano kwa kuzisahau hisani zake.

Si vibaya hapa tukisema kwamba baada ya kujua faida ya saumu kwa kiwiliwili, basi mtu haifai kwake ukifika usiku ale chakula kwa wingi kulipia njaa ya mchana, au kula vitu ambavyo vizito kwa tumbo na vyaweza kumletea taabu na maradhi. Kwa hiyo ni bora sana kutumia chakula chepesi anapofuturu ili apate faida kwa kiwiliwili na roho                            

Faida Kwa Roho

Tunaelewa vizuri kwamba makusudi ya kuumbwa kwetu ni kutupatia kufikia ukamilifu wa roho. Na kwa ajili ya kutimiza makusudi hiyo roho kuelekea upande wa juu utakatifu; vile vile inapasa roho iangalie huku utaratibu na usalama wa kiwiliwili. Anapokuwa mtu yu macho, tena madhali tumbo lake limejaa, basi roho haijaliwi kupata wasaa kuelekea upande wa Mola kwa vile umeshughulika na mambo ya mwili; inaziwika kuipata shabaha ya kuumbiwa kwake. Kwa hivyo mtu akifunga mchana kiwiliwili kinakuwa chepesi, na tukifanya mazowea usiku pia tule chakula chepesi na kiasi cha dharura tu, hapo roho itapata wasaa na faragha kwa upesi. Ijapokuwa kwa muda huo mdogo wa mwezi mmoja mfululizo bila ya taabu itaweza kushikamana uhusiano wake wa juu kwa furaha na kupata daraja tukufu za akhera.

Faida kwa mwenendo na utamaduni

Wapo viumbe wengi humu duniani ambao hawakupata chakula cha shibe yao; hao ni watu wale ambao Mwenyezi Mungu amewapa fungu katika mali ya matajiri, na Mola amesema hivi: "Mali ni mali yangu na maskini ni watu wangu wa nyumbani, na matajiri ni wajumbe (wakili) wangu". Matajiri na wenye mali hawawezi kuhisi na kujua taabu ya njaa inavyowapata maskini; ndipo Mwenyezi Mungu akafaradhisha saumu juu ya matajiri na maskini, ili matajiri waone taabu ya njaa, na wapate kujua inawapata taabu gani katika nyoyo za maskini na wahitaji. Imam Jaffar As-Sadiq (Imaam wa sita) amesema: "Saumu imefanywa faradhi kwa ajili ya kuwafundisha usawa katika kujionea njaa na kiu kati ya watu wote, wala hakuna tafauti kati yao, na vile vile matajiri wahisi maumivu ya njaa (hata wapate kuwasaidia na kuwahurumia kikweli maskini)".

       Mwezi wa Ramadhani huwazoeza watu utaratibu na kawaida katika maisha. Tunawaona wanafuturu kwa wakati mmoja kama wanavyojizuia kwa yavunjayo saumu kwa wakati mmoja pia.

Hakika mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kufungamana, wa ukarimu na upaji, ikiwa kuna uadui kati ya Mwislamu na mwenziwe, kama ugomvi au kuachana usuhuba, basi katika mwezi huu mtukufu hufanya bidii ya kupatana, na kuanza kupendana na kufanyiana hisani. Kwa kufahamu kwamba katika mwezi kama huu mtukufu na adhimu mtu hujipatia thawabu zaidi kwa kuwa ni mmoja katika aamali nzuri zenye kutukuka na kumfaa hapa duniani na kesho akhera. Thibitisho juu ya jambo hili tunaona katika haditbi za Mtume (S.A.W.) aliyohutubia kabla ya kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani, anasema hivi: "Enyi watu, mwenye kumfuturisha aliyefunga katika mwezi huu hupata thawabu kwa Mwenyezi Mungu ya kumweka huru mtumwa na kughufiriwa madhambi yake yote yaliyopita". Akasimama sahaba mmoja akasema: "Yaa rasula-llah, Siwote kati yetu twaweza kufanya hivyo (kufuturisha) Mtume (S.A.W.) akajibu: "Jilindeni na moto (wa Jahannam) kwa nusu ya tende, jilindeni na moto kwa kumnywesha maji" Yaani, ikiwa huna uwezo wa kulisha basi hata nusu tende, au kunywesha maji kutafidia.                

Madhumuni na shabaha ya mambo hayo ni kuwafanya Waislamu wawe pamoja, na wapendane na kwa umoja wao waepuke na maovu na uchoyo, na kujipendelea raha ya binafsi, na hilo ni lengo kubwa la Uislam.

Faida kwa Imani

Mwenyezi Mungu kwa kuamrisha kufunga mwezi huu, ametayarisha mafundisho ya kuzoeza ugumu na taabu. Tunaelewa sote kwamba watu wanaokwenda kuchukua mafundisho ya aina yeyote, wakati wanapochukua hayo mafundisho hawawi na raha, bali wanapambana na taabu na mashaka mengi na inawabidi kustahimili. Kwa mfano, mwanajeshi anapokwenda kuchukua mafundisho usiku na mchana, saa ishirini na nne humpita kwa ilhali hafahamu; kula kunywa na mambo yote inakuwa chini ya mipango na kanuni, wakati wa kulala na kuamka umewekwa, majaribio na kazi ngumu lazima kufanya. Huchukuliwa masafa makubwa kupita majabalini na misitu na mahala pa hatari, chakula na tandiko begani. mara mbio mara pole pole mara anahema, masikini huyo mwana jeshi lazima avumilie; pengine kwa uchovu anapenda kukaa, miguu imekuwa mizito, kwa hali hiyo yote yule mkuu (Commanding Officer) wa amri kumwona yule mwana jeshi katika hali hii pia haoni huruma bali humwamrisha 'Quick March'. Kwa nini hivyo? Huyo mkuu anafanya hivi kwa kuwa ni adui wake? Sivyo, bali anamtakia katika mafundisho hayo ya taabu azowee kuvumilia ili wakati wa kazi ya ujeshi na kuwa askari wa vitani hata akipata taabu yeyote itakuwa ameshazoea nayo na itakuwa kwake kutekeleza rahisi na kwa furaha ataifanya.

Vile vile Mwenyezi Mungu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani wakati mtu amefunga, vitu vilivyo halali tu

mefanyiwa haramu. Kitu kama kula na kunywa ambavyo ni dharura ya maisha tumekatazwa. Ladha na mambo ya kufurahisha ambayo wakati mwingine ni ruhusa kuyafanya na labda baadhi ya wakati kutenda kwake ina thawabu, lakini siku hizi (Ramadhani) imekatazwa na imelazimiskwa Kwa nini? Yote haya tunafundishwa na kuzoweza kutii na kufuata maamrisho ya Mola, kujizuia na mambo mazuri na ya halali katika mwezi huu tunafundishwa utiifu, na majaribio hayo iendelee muda wa mwezi mmoja. Vile vile tujue kwamba Mwenyezi Mungu kadiri vitu alioturuhusu kufanya ni hisani yake Mola juu yetu, kama si hivyo angeweza vitu hivyo kuviharamisha maisha; lakini fadhili na upaji wake vitu vingi ametuhalalishia na kidogo sana ametuharamishia.

Kwa vyo vyote utaratibu na utii huu katika mwezi wa Ramadhani, inatufundisha na kutupa faida ya kuvumilia kwa kujitenga na vitu vilivyo haramishwa na visivyo faa kufanya. Ikiwa kwa mwezi mmoja tunaweza kujitenga na vitu vya dharura na halali, basi baadaye kujitenga na vitu vya haramu na visivyodharura bali vyenye kudhuru roho na kiwiliwili tutakuwa na taabu gani?

Basi usemi wa Mwenyezi Mungu katika Qur'ani kwamba, ""Imefanyiwa faradhi mfunge, ili mche Mwenyezi Mungu (mwogope Mola)". Tuseme binadamu kwa baraka na utukufu wa Ramadhani, sehemu moja katika sehemu kumi na mbili 1/12 ya mwaka anapitisha katika uchaji na utii wa Mwenyezi Mungu, ni kama mtu ambaye sehemu ya kumi na mbili ya maisha yake ameishi utiini. Kwa hivyo ikiwa tumechukua faida sahihi ya kweli yamajaribio ya mwezi wa Ramadhani, basi siku zilizobaki tunaweza kustahiki kupata maridhio ya Mola, na sehemu ya kumi na mbili ya maisha ikazidi ikazidi hadi ikafika nusu au maisha mazima; lakini shuruti lilioko ni hili kuwa ule uvumi na ustawi na maombolezo uliokuwa nao katika kumtii Mola, athari na matokeo yake baadaye uendelee, usiwe mchomko wa soda unapofungua chupa kuchemka baadaye ikanyama'a.