Back Index  

HABARI MOTOMOTO.

1. AL- AZHAR YASEMA: WANAWAKE WA KIISLAMU WALIOKO UFARANSA WANAWEZA KUVUA HIJAB KAMA WAKILAZIMISHWA

Cairo, Desemba 30, 2003 (IslamOnline, net): Imamu Mkuu wa Al-Azhar Sheikh Mohammad Sayed Tantawi siku ya jumanne, Desemba 30, 2003 alisema kwamba: Wanawake wa kiislamu wanaoishi Ufaransa wanaweza kuvua Hijab zao kama wakilazimishwa kwa shida, alikuwa akirejea kusudio la sheria ya kupiga marufuku Hijab katika shule za serikali.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy (aliyekuwa anaizuru Misir), Tantawi alisisitiza kwamba Hijab “ni sharti la   Mungu kwa mwanamke wa kiislamu… Hakuna Mwislamu yeyote, awe yeye ni mtawala au mtawaliwa, awezaye kulipinga hilo.”

Lakini alihoji kwamba Ufaransa wana haki ya kupiga marufuku Hijab katika shule za serikali, akaongeza kwamba chombo chochote cha kiislamu au nchi ya kiislamu haina haki ya kulipinga hilo, kwa sababu Ufaransa sio nchi ya kiislamu.

“Hijab ni wajibu kama mwanamke anayeishi katika nchi ya kiislamu. Kama anaishi katika nchi isiyo ya ki-Islamu, kama Ufaransa, ambayo watawala wake wanataka kufuata sheria inayopinga Hijab, ni haki yao,” alisema Imamu mkuu huyu wa Al-Azhar, mwachuoni aliyeteuliwa na serikali.

Alisema kwamba iwapo mwanamke wa kiislamu atafuata sheria za nchi isiyo ya kiislamu (kwa kuvua Hijab yake), basi Uislamu humchukulia kama aliyelazimishwa kwa shida. Sheikh Tantawi alitetea maoni yake hayo kwa kusoma Aya Tukufu, ambayo inasema: “Mmeharamishwa (kula) nyama mfu na damu na nyama ya nguruwe, na kilichosomewa jina lisilo la Mwenyezi Mungu…Lakini mwenye kusongeka kwa njaa, pasipo kuelekea kwenye dhambi, wala kupituka mipaka - basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe mwenye kurehemu.” “Nasisitiza na kukazia: Ni haki yao na siwezi kuipinga… sisi, kama nchi ya kiislamu, hatuwezi kumruhusu mtu yeyote kuingilia katika mambo yetu ya ndani,” alisema akisherehesha juu ya upigaji marufuku wa Ufaransa ulio na majadala. “Mimi mwenyewe, katika wadhifa wangu kama Imamu Mkuu wa Al-Azhar, siwaruhusu watu wasio Waislamu kuingilia katika mambo yetu ya ndani, na kwa mantiki hiyo hiyo, siwezi nikaruhusu nafsi yangu kuingilia katika mambo ya ndani ya nchi isiyo ya kiislamu,” aliongeza Sheikh Tantawi.

Rais wa Ufaransa Jacques Chirac siku ya jumatano, 17 Desemba, 2003 aliunga mkono kusudio juu ya utungaji mpya wa sheria ya kupiga marufuku uvaaji wa Hijab katika shule za serikali. Waziri wa sheria wa zamani wa Ufaransa, Bernard Stasi, ambaye aliongoza kamati ya serikali juu ya mazingira ya kilimwengu na dini, alipendekeza mapema katika mwezi huo kuwekwa sheria ya kupiga marufuku Hijab, misalaba mikubwa na vikofia vya ki-Yahudi.

Hatua hiyo iliyopendekezwa, imepangwa kuwakilishwa mbele ya Bunge la Ufaransa mwezi Februari 2004, na inatarajiwa kuanza kutumika katika mwezi wa Septemba 2004. [Kwa mujibu wa fatwa za wanachuoni wengi pamoja na Mkuu wa Mamlaka kubwa ya ulimwengu wa Waislamu-Mashi’a, Ayatollah Mkuu Sayyid Seestani (H.A); hairuhusiwi kwa msichana wa kiislamu kuvua Hijab yake Shuleni, na kama akilazimishwa kuvua, basi asihudhurie Shuleni hapo.][77]

2. KUJIFUNIKA KICHWA NA UHURU WA DINI

Nchi kadhaa za Ulaya zinachochea sheria za kupiga marufuku au kuzuia uvaaji wa mitandio ya kichwa kwa wanawake wa kiislamu. Sheria hizo huzua maswali kwenye misingi ya kuvumiliana na usawa katika jamii ambayo hupigania mfumo wa kutambua mawazo, misimamo mbali mbali na uhuru wa dini. Hivi sasa Ufaransa inafikiria kupiga marufuku uvaaji wa Hijab (shela) mashuleni, wakati ambapo katika nchi ya Ujerumani, majimbo mawili yamependekeza itungwe sheria ambayo itapiga marufuku moja kwa moja uvaaji wa ushungi (Hijab) katika taasisi za elimu.

Makala hii inazungumzia suala la Hijab, adabu ya kufunika kichwa kwa wanawake wa ki-Islamu, na vile vile na desituri za Wayahudi na Wakristo za uvaaji wa shela na ushungi.

Hijab na shela?

Baadhi ya watu katika nchi za magharibi (yaani, Ulaya na Amerika) hufikiria adabu ya kufunika kichwa inayofuatwa na wanawake wa kiislamu kama alama kubwa ya ukandamizaji wa wanawake na utumwa. Je, ni kweli kwamba hakuna desturi zinazo fanana katika mila za Mayahudi-Wakristo? Hebu ngoja tuiweke rikodi hii sawasawa. Kwa mujibu wa Rabbi Dr. Menachem M. Brayer (Profesa wa Biblical Literature, Yeshiva University) katika kitabu chake, ‘The Jewish woman in Rabbinic Literature,’ ilikuwa ni desturi ya wanawake wa ki-Yahudi kutoka nje wakiwa na shungi (nguo ilyofunika kichwa), ambayo wakati mwingine, hufunika hata uso wote na kuachilia jicho moja tu nje.[78] Anawanukuu baadhi ya Marabbi wa zamani wakisema, “Haifanani kwa mabinti wa Israeli kutembea bila kufunika vichwa” na “Laana iwe juu ya mwanaume ambaye anaruhusu nywele za mkewe zionekane…mwanamke ambaye anaonesha nywele zake kwa ajili ya kujirembesha huleta ufukara.”sheria za ki-Yahudi hukataza usomaji wa dua za kuomba baraka au maombi (yoyote) mbele ya mwanamke aliyeolewa akiwa kichwa wazi, kwa vile kutokufunikwa kwa nywele za mwanamke huchukuliwa kama ‘uchi’.[79]

Dr. Brayer vile vile anataja kwamba ,”wakati wa kipindi cha utawala wa Marabi (wanachuoni wa dini ya ki-Yahudi) kushindwa kwa mwanamke wa ki-Yahudi kufunika kichwa kulichukuliwa kama tusi kwa heshima yake. Akiwa hakufunika kichwa chake anaweza kupigwa faini ya zuzim mia nne kwa kosa hili.” Dr. Brayer vile vile anaelezea kwamba shela ya mwanamke wa ki-Yahudi haikuchukuliwa wakati wote kama alama ya adabu.

Wakati mwingine, shela huashiria hali ya ubora na anasa kuliko adabu. Shela huupa utu heshima na ubora wa wanawake watukufu. Vile vile huwakilisha kutokuwezekana njia yeyote ya kumuendea mwanamke kama miliki ya mume iliyotakaswa.[80] Shela huonesha kujiheshimu kwa mwanamke na hadhi ya kijamii katika jamii. Wanawake wa daraja za chini mara kwa mara huvaa shela ili kutoa picha ya daraja la juu. Ukweli kwamba shela ilikuwa ni alama ya utukufu, ilikuwa ndio sababu ya makahaba kutokuruhusiwa kufunika nywele zao katika jamii ya ki-Yahudi ya zamani. Hata hivyo, makahaba mara kwa mara walivaa mitandio maalum ili waonekane wa heshima.[81]

Wanawake wa ki-Yahudi huko Ulaya waliendelea kuvaa shela mpaka karne ya kumi na tisa wakati maisha yao yalipokuwa yameingiliana zaidi na utamaduni wa kisekula ulioyazunguka. Shinikizo la nje la maisha ya Kizungu katika karne ya kumi na tisa liliwalazimisha wengi wao kutoka nje vichwa wazi. Baadhi ya wanawake wa ki-Yahudi waliona inafaa zaidi kubadilisha shela

yao ya asili kwa kuvaa wigi (nywele za bandia) kama muundo mwingine wa kufunika nywele. Leo, wanawake wachamungu zaidi wa ki-Yahudi hawafuniki nywele zao isipokuwa katika Hekalu.[82] Baadhi yao, kama vile madhehebu za Hasidic bado wanaendelea kutumia wigi.[83]

Vipi kuhusu mila ya Ukristo? Inajulikana sana kwamba watawa wa Kanisa Katoliki wamekuwa wakifunika vichwa vyao kwa mamia ya miaka sasa, lakini hiyo sio mwisho. Mt. Paulo katika agano jipya ameandika maelezo ya kuvutia sana kuhusu shela: Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanaume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanaume, na kichwa cha Kristo ni Mungu. Kila mwanamume asalipo, au anapohutubu, naye amefunika kichwa yuaaibisha kichwa chake. Bali kila mwanamke asalipo, au anapohutubu, bila kufunika kichwa, yuaaibisha kichwa chake; kwa maana ni sawa sawa na yule asiye nyolewa. Maana mwanamke asipofunikwa na akatwe nywele. Au ikiwa ni aibu mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa, na afunikwe. Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunika kichwa, kwa sababu yeye ni mfano wa utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume. Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume. Kwa hiyo imempasa mwanamke awe dalili ya kumilikiwa kichwani, kwa ajili ya malaika. 1Wakorintho 11:3-10 Mantiki ya Paulo ya kuwavisha wanawake shela ni kwamba, shela huwakilisha alama ya utawala wa mwanaume, ambaye ni mfano na utukufu wa Mungu juu ya mwanamke, ambaye ameumbwa kutokana na mwanaume na kwa ajili ya mwanaume.

Mt. Tertullian katika tasnifu yake mashuhuri, ‘On the veiling virgins’ (‘Juu ya kuwavisha wanawali shela), anaandika hivi: “Wanawake vijana, mnavaa shela zenu nje mitaani, hivyo ni lazima mzivae mkiwa kanisani, mnazivaa mkiwa pamoja na wageni, basi zivaeni mkiwa pamoja na kaka zenu... “Miongoni mwa sheria za kanisa Katoliki za sasa, kuna sheria inayowataka wanawake kufunika vichwa vyao wakiwa kanisani.[84]

Baadhi ya madhehebu ya Kikristo kama vile Amish na mennonites kwa mfano, wanawavalisha wanawake wao shela hadi sasa. Sababu ya kuvaa shela, kama inayotolewa na viongozi wa Kanisa ni kwamba, “Kufunika kichwa ni alama ya mwanamke kuwajibika kwa mwanaume na Mungu,” ambayo ni mantiki ile ile iliyotolewa na Mt. Paulo katika Agano Jipya.[85] Kutokana na ushahidi wote huo hapo juu, ni wazi kwamba Uislamu haukubuni ushungi. Hata hivyo, Uislamu umeuthibitisha.

Qur’an inawahimiza wanaume waumini na wanawake waumini kuangusha macho yao chini na kulinda tupu zao, na kisha huhimiza wanawake waumini kuteremsha shungi zao ili kufunika shingo na kifua:

“Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao, bila shaka Mwenyezi Mungu anazo habari za yale wanayoyafanya. Na waambie

waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, na wasioneshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao, au wanawake wenzao, au wale waliomilikiwa na mikono yao, au wafuasi wanaume wasio na matamanio (kwa wanawake) au watoto ambao hawajajua siri za wanawake. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubieni nyote kwa Mwenyezi Mungu enyi wenye kuamini ili mpate kufaulu.” Qur’an...24:30-31

Qur’an iko wazi kabisa kwamba shela ni muhimu kwa ajili ya adabu, lakini kwa nini adabu ni muhimu? Qur’an bado iko wazi:

“Ewe Nabii! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wake wa waumini: Wateremshe juu yao shungi zao. Kufanya hivyo inaelekea zaidi wajulikane na wasiudhiwe, na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” Qur’an...33:59

Hii ndiyo nukta yote, adabu imeamriwa ili kuwakinga wanawake kutokana na usumbufu au kwa lugha nyepesi, adabu ni kinga. Hivyo, dhumuni pekee la Hijab katika Uslamu ni kinga. Hijab, tofauti na shela ya mila ya Kikristo,sio alama ya mamlaka ya mwanaume juu ya mwanamke, wala sio alama ya mwanamke kuwajibika kwa mwanaume. Hijab, tofauti na shela iliyoko katika mila ya ki-Yahudi, sio alama ya anasa na ubora wa baadhi ya wanawake watukufu walioolewa. Katika Uislamu Hijab ni alama ya adabu ambayo hulinda salama uadilifu binafsi wa mwanamke.

Qur’an inasisitiza kwa nguvu sana kuhifadhi heshima ya mwanamke, na kuwahukumu wanaume kuadhibiwa vikali kama kwa uwongo wanashutumu wanawake kwa uchafu:

“Na wale wanaowasingizia wanawake waaminifu kisha hawaleti mashahidi wanne, basi wapigeni mijeledi themanini na msiwakubalie ushahidi wao kabisa, na hao ndio mafasiki.” Qur’an 24:4 24:4

Baadhi ya watu, hususan katika nchi za magharibi, wamezowea kudhihaki hoja yote ya adabu kwa ajili ya kinga. Hoja yao ni kwamba, kinga bora ni uenezaji wa elimu, tabia za kistaarabu na kujizuia. Tungesema: Vema, lakini haitoshi. Kama ustaarabu ni kinga ya kutosha, basi kwa nini wanawake katika Amerika ya Kaskazini hawathubutu kutembea peke yao katika mitaa yenye giza - au hata kukatisha sehemu iliyotupu ya kuegeshea magari? Kama elimu ni ufumbuzi, basi kwa nini vyuo vikuu vyetu vina ‘huduma ya kusindikizwa nyumbani’ kwa wanafuzi wa kike katika kampasi (eneo la chuo)? Kama kujizuia ni ufumbuzi, basi kwa nini taarifa za unyanyasaji wa kijinsia katika sehemu za kazi huripotiwa kwenye vyombo vya habari kila siku? Mfano wa wale walioshutumiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia, katika miaka michache iliyopita, ni pamoja na: Mabaharia maofisa, Mameneja, Maprofesa wa vyuo vikuu, Maseneta, Mahakimu wa Mahakama

Kuu, na Rais wa Amerika! (Clinton).

Ifuatayo ni takwimu iliyochapishwa katika kipeperushi kilichotolewa na mkuu wa kitengo cha wanawake katika Queen’s University ya Canada: Nchini Canada mwanamke anashambuliwa kijinsia kila baada ya dakika 6, mwanamke mmoja katika wanawake watatu nchini Canada atakuwa ameshambuliwa kijinsia wakati fulani katika maisha yake. Mwanamke mmoja katika wanawake wanne wako katika hatari ya kubakwa au kujaribiwa kubakwa katika maisha yake. Mwanamke mmoja mmoja katika wanawake wanane watakuwa wameshambuliwa kijinsia wakati wakuhudhuria vyuo au vyuo vikuu, na utafiti umegundua kwamba wanaume 60% wenye umri wa kwenda chuo kikuu wamesema wangeweza kufanya shambulio la kijinsia kama watakuwa na uhakika kwamba hawatashikwa.

Kukabiliana na ushambuliaji wa wanawake, mabadiliko makali ya msingi katika muundo na utamaduni wa maisha ya jamii ni ya muhimu kabisa. Utamaduni wa adabu ni wenye kuhitajika sana, adabu katika mavazi, katika kuongea, na katika tabia za wote wanaume na wanawake, vinginevyo takwimu za kutisha huelekea kuongezeka , na kwa bahati mbaya mwanamke peke yake ndiye mwenye kulipa gharama hiyo. Kwa hakika, tunateseka, lakini kama alivyosema K. Gibran:”...kwa mtu ambaye anapigwa ngumi sio sawa sawa na yule ambaye anazihesabu.”[86]

Jamii kama ya Kifaransa ambayo inawafukuza wasichana kutoka mashuleni kwa sababu ya mavazi yao ya adabu, mwishowe inajidhuru yenyewe. Ni moja ya kejeli kubwa ya dunia yetu ya leo kwamba ushungi ule ule uanaoheshimiwa kama alama ya ‘utukufu’ wakati ukivaliwa na watawa wa Kanisa Katoliki, unakejiliwa na kushutumiwa kama alama ya ‘ukandamizaji wa wanawake’ wakati ukivaliwa na wanawake wa kiislamu kwa madhumuni ya adabu na kinga.

Wasalla Llahu ala Sayyidina wa Nabiyyina Muhammadin wa Alihit-taahiriina. Wal hamdulilahi Rabbil-alamin.

Mwandishi: Muhammad Ibrahim Kaadhim Al-Qaz-wini.

Mtarjumi: Msabah Sha’ban Mapinda.

27 Muharram 1412 -9 August, 1991

Back Index