Back Index Next

Kipo kisa kingine kinasimuliwa kuhusu hali kama hizi na kinasema kuwa: “Kuna mtu mmoja ambaye kazi yake ilikuwa kuteka maji na kupeleka ndani ya nyumba ya Sonara fulani kwa muda wa miaka thelathini. Bila shaka kuna wakati yule mume hakuwako nyumbani, kwahiyo, mke wa sonara alikuwa akija kumfungulia mlango yule mchota maji ili apate kumimina maji mahala panapostahili. Kipindi chote hiki yule mchota maji hakuwahi kufanya hiyana yoyote dhidi ya mke wa sonara japo kumuangalia kwa jicho la hiyana.

Siku moja wakati yule mama anamfumngulia mlango yule mchota maji, mara ghafla aliunyoosha mkono wake na kumvuta yule mama na akambusu!! Kwa bahati nzuri mwanamke huyu aliuvuta mkono wake kwa nguvu kisha akapiga makelele na hapo hapo akamfukuza yule mchota maji kutoka mule ndani. Baadaye huyu mama alianza kufikiria huku akishangazwa na hali ile iliyojitokeza. Imekuwaje mchota maji yule kufanya hiyana ile baada ya kuwa muaminifu kwa muda wa miaka thelathini?!!

Mumewe aliporudi nyumbani mkewe akamuuliza: ‘Je leo kuna jambo gani limetokea huko dukani kwako?’ Yule mume akajibu kwa kusema: ‘Leo kuna mwanamke alikuja dukani kwangu kununua bangili, basi nilipomfunua mikono yake ili apate kuvaa bangili zile, nilimshika mkono wake kisha nikambusu.’!! Basi pale pale mkewe alipiga makelele akasema: ‘Allahu Akbaru!’[59] Baada ya hapo alimsimulia mumewe mambo yaliyotendwa na yule mchota maji.”[60]

Naam chochote atakachokifanya mtu kuwafanyia wenziwe na wake wa wenzake, basi na yeye yatamfika hivyo kwa mkewe, mama yake, dada yake na binti yake. Ndani ya hadithul Qudsi inasemwa kuwa: “Vile uwatendeavyo wenzako, basi na wewe utatendewa hivyo hivyo.” Maana yake ni kwamba: Iwapo utawatendea wema wenzako basi na wewe utatendewa wema, na iwapo wewe utawatendea ubaya wenzako fahamu wazi kuwa na wewe utatendewa ubaya.

Ewe msomaji mpendwa: Narudia tena kuzungumzia suala la kumuangalia mwanamke asiyekuhusu na ninasema; Hapana shaka kwamba Uislamu ni dini yenye mafunzo yanayokuhamasisha kutenda mema, na wakati huo huo inayo mafunzo ya kukuonya usiyaendee maovu. Ndiyo maana utaiona Qur’an Tukufu pindi Mwenyezi Mungu anapoitaja pepo na neema zake, hapo hapo hufuatisha kuelezea habari za moto na adhabu zake. Yote haya lengo lake ni kumfanya mtu awe katika mazingira ya kutumainia neema na thawabu, na pia awe na khofu ya moto na adhabu kwa upande wa pili. Hivi punde tu umesoma baadhi ya hadithi tukufu zilizosimulia kuhusu adhabu za kumuangalia mwanamke asiyekuhusu na pia matokeo mabaya yanayoletwa na tabia hiyo mbaya.

Hivi sasa umefika wakati wa kuzungumzia hadithi zinazoelezea malipo mema aliyoyaandaa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya wale watakaojiepusha na mambo ya haramu. Kadhalika hadithi hizo zitaelezea athari njema zinazopatikana kutokana na tabia njema za kujiepusha na mambo aliyoyakataza Mwenyezi Mungu.

Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: “Kuyatazama mapambo ya wanawake wasiokuhusu ni mshale miongoni mwa mishale ya ibilisi iliyo na sumu, atakayeliacha jambo hilo kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu (s.w.t) basi Mwenyezi Mungu atamuonjesha ladha ya ibada itakayomfurahisha.[61]

“Katika hadithi nyingine Mtume (s.a.w.w) anasema; “Kumtazama mwanamke asiyekuhusu ni mshale miongoni mwa mishale ya ibilisi iliyo na sumu, atakaye acha jambo hilo kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu (s.w.t) basi Mwenyezi Mungu atampa mtu huyo imani ambayo furaha ya imani hiyo ataihisi moyoni mwake.”[62]

Bwana Mtume anaendelea kutufunza anasema kwamba: “Yainamisheni macho yenu, kwa kufanya hivyo mtaona maajabu (makubwa).[63]

Hapana shaka kwamba Mwenyezi Mungu humfunika mtu huyo kwa wingi wa baraka kutokana na kitendo chake cha kuinamisha macho na kutowaangalia wanawake wasiomhusu. Imam Ja’far Sadiq (a.s) anasema: “Mwenye kumuangalia mwanamkeasiyemhusu kisha akanyanyua macho yake juu au akayafumba (ili tu asimuone mwanamke huyo), Mwenyezi Mungu humuozesha mtu huyo mwanamke wa peponi kabla hajarudisha macho yake chini.”[64] Anasema tena Imam Ja’far (a.s): “Hawezi mtu yeyote kujihifadhi isipokuwa kwa kuyainamisha macho yake, kwani macho hayatainamishwa kutokana na mambo aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, isipokuwa ndani ya moyo wa mtu huyo huwa kumetangulia kuuona utukufu wa Mwenyezi Mungu.”[65] Sasa hivi kumebakia kitu cha mwisho ambacho ni: Je! Ni namna gani basi mtu anaweza kuepukana na jambo hili la haramu, wakati sote tunafahamu kwamba, gonjwa hili la kansa ya wanawake kuvaa nusu Hijabu na kutokujisitiri kwa mujibu wa sheria limeenea?

Na kwa bahati mbaya sana hata katika nchi zetu za Ki-Islamu gonjwa hili limo. Hivi kweli kwa hali tuliyonayo mtu anaweza tena kuinamisha macho yake na ni vipi ataiona njia? Jawabu la suali hili ni kama ifuatavyo: Sina shaka umesoma baadhi ya Aya na hadithi tulizozitaja. Kinachotakiwa ni

kuinamisha macho siyo kuyafumba, na hii ndiyo maana iliyokusudiwa, yaani uangalie chini.

Anachopswa mtu kukifanya wakati anapomuona mwanamke asiyemhusu, haraka sana ateremshe macho yake chini au aangalie upande mwingine. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hawezi kupoteza malipo yake.

Usimpe mkono mwanamke asiyekuhusu: Ndugu Mwislamu, Mwenyezi Mungu ameharamisha kumpa mkono mwanamke asiyekuhusu. Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema: “Yeyote atakayepeana mkono na mwanamke asiyemhusu mtu huyo hujiingiza katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na anayedumisha uhusiano (wa kimapenzi) na mwanamke asiyekuwa mkewe, atafungwa kwa mnyororo wa moto pamoja na shetani kisha wasukumizwe motoni.[66]

Usimtanie mwanamke asiyekuwa mkeo: Miongoni mwa mambo ambayo Mwenyezi Mungu amekukataza na kukuharamishia ewe ndugu Mwislamu, ni kufanya utani na mwanamke asiyekuhusu kisheria, kwani jambo hili mara nyingi hukaribisha uovu na pia husaidia kwa kiasi kikubwa kuamsha hisia za maumbile zilizokuwa zimejificha katika pande mbili hizi. Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: “Yeyote anayemtania mwanamke asiye na milki naye (asiyekuwa mkewe) Mwenyezi Mungu atamfunga mtu huyo miaka alfu moja (huko akhera) kwa kila neno moja alilomsemesha mwanamke huyo.”

Usichelewe kuoa: Ndugu yangu Mwislamu, kuoa ni jambo la lazima kwa Mwislamu anapofikia umri wa kubalehe. Ni lazima Mwislamu aoe ili ailinde dini yake, na ndiyo jambo la kwanza apasalo kufahamu.

 Jambo la pili: Pindi atakapooa atapata radhi za Mwenye Mungu Mtukufu.

 Na jambo la tatu: Atakuwa amehifadhi nafsi yake kutokana na mambo ya haramu.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu amemuumba mtu na akamuwekea matamanio ya kijinsiya, na akayafanya kuwa ndiyo matamanio yenye nguvu kuliko mengine yote. Kwa matamanio hayo Mwenyezi Mungu akafanya kuwa ndiyo njia ya kukidumisha kizazi cha wanaadamu, na akafanya kuoa ndiyo njia ya pekee kuyatosheleza matamanio haya. Kwa hiyo kuoa ndiyo njia nzuri na tukufu na ndiyo ufumbuzi wa pekee uliopo kisheria kuhusu tatizo hili la kijinsiya.

Ukweli ulivyo ni kwamba, kuchelewa kuoa kunamfanya mtu akumbwe na mambo mawili.

Kwanza: Katika kushindana na matamanio yake kutamfanya aiumize nafsi yake na kupata taabu

kubwa ya kuvumilia katika muda huo. Pili: Huenda hatimaye akaingia katika haramu ikiwa ni pamoja na njia isiyo ya kawaida katika kuyatosheleza matamanio yake, au akajikuta anafanya mambo machafu zaidi ambayo ni kinyume na maumbile. Au huenda akafanya uzinifu na matokeo yake ni kuvunja heshima yake au heshima za watu wengine. Na kutokana na hali halisi ilivyo, kila jambo moja katika hayo lina hatari kubwa kwa mtu yeye mwenyewe na heshima yake na utu wake. Kwani kuzuia matamanio na kuyadhibiti kunasababisha kuiadhibu roho na matokeo yake huleta athari mbaya mwilini na hasa katika akili.

Hali hii husababisha kuingia katika dhambi na hatimaye mtu ndipo hujikuta akifanya ambalo hakulitarajia, hapo utu wake huporomoka na mwisho hupata akahukumiwa kwa kosa la jinai na kuingia gerezani na kuishi humo sawa na wezi na wanyang’anyi.

BASI NINI UFUMBUZI WA TATIZO HILI?

Ufumbuzi wa tatizo hili ni kuoa, kitu ambacho Uislamu unakitanguliza mbele na hata akili inakubaliana kabisa na ukweli huu, kwa kuwa kuoa ndiyo dawa pekee ya kutibu maumbile haya. Kuoa kunatimiza furaha ya kiroho kwa mtu na kuiliwaza nafsi na kuyapamba mazingira na tabia ya mtu. Kwa jumla ladha ya maisha na starehe vimo ndani ya ndoa, na kwa upande mwingine kuoa kunazuia mtu kuyaingia maovu na madhambi. Zaidi ya hapo ni kwamba, Mwenyezi Mungu hakumuumba mtu ili aishi maisha ya ujane na upweke, bali amemuumba aishi na mkewe aliye Muumini bega kwa bega ili wajenge familia na jamii bora hasa katika malezi ya watoto. Kwa hakika ujane ni miongoni mwa mambo yanayomchukiza Mwenyezi Mungu, pia Uislamu unapinga kwa nguvu zake zote jambo hili na hata Mawalii wa Mwenyezi Mungu wanachukizwa na ujane. Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: “Waovu miongoni mwenu ni wajane, (wasiyooa au kuolewa) nao ni ndugu wa shetani.”[67] Na akasema tena: “Watu wengi wa motoni ni wale wajane ( wasiyooa au kuolewa).”[68]

Imesimuliwa kutoka kwa al-Ukaaf al-Hilali anasema: “Nilikwenda kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) akaniambia ‘ewe U’kaafu unaye mke?’ Nikamwambia, Hapana sina mke. Mtume

akaniambia: ‘Je unaye mjakazi?’ Nikasema: Hapana sina. Bwana Mtume akasema: ‘Je wewe ni mzima na mwenye uwezo (yaani unao uwezo wa mali na unalimudu tendo la ndoa)? ‘Nikamjibu: Ndiyo tena namshukuru Mwenyezi Mungu. Bwana, Mtume akasema: ‘Ikiwa unayamudu hayo na hujaowa, basi kwa kweli wewe ni miongoni mwa ndugu wa mashetani, au basi utakuwa miongoni mwa mapadri wa ki-Kristo na kama si hivyo, fanya kama wanavyofanya Waislamu kwani miongoni mwa mila zetu ni kuowa.’ Mtume aliendelea kunionya na kusisitiza suala la kuowa mpaka akafikia hatua ya kuniambia: ‘Ole wako ewe U’kaafu, owa hakika wewe ni miongoni mwa waovu ( ikiwa hukuowa).’ Nikamwambia Bwana Mtume: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu niozeshe kabla sijaondoka hapa.” Bwana Mtume akamuozesha Bwana huyo kabla hajaondoka.[69]

Na katika kulitilia mkazo suala la kuoa na kuhimiza watu waowe, Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: “Hakuna jengo bora lililojengwa katika Uislamu na likawa linapendeza mbele ya Mwenyezi Mungu na likapata utukufu kuliko kuoana.” Na akasema tena: “Kijana yeyote anayeowa katika umri wake wamwanzo katika ujana, shetani huchukia na kusema; Lo nimepata hasara theluthi mbili za dini yake kijana huyu amezikinga kutokana na uovu wangu.” Kisha Mtume akamuusia kijana wa aina hii akasema: Na amuogope Mola wake kijana huyu katika theluthi iliyobaki.”[70]

Makusudio ya maelezo haya ni kuonesha kwamba kuoa kunahifadhi theluthi mbili ya dini, kwa hiyo mtu anatakiwa awe mchamungu katika theluthi iliyobakia. Na kama hali ni hii, umuhimu wa kuoa katika maisha ya mtu ni jambo ambalo linayo nafasi ya pekee na tukufu, na pia mwanaadamu anatakiwa alipatie nafasi kubwa ya kulitekeleza katika mipango yake.

Tukamilishe mazungumzo juu ya kuowa kwa hadithi ya Mtume (s.a.w.w) inayosema kuwa: “Rakaa mbili anazoswali mtu aliyeowa, ni bora zaidi kuliko rakaa sabini anazoswali mtu asiyeowa.”[71]

MAKAZI YA MWANAMKE ASIYEJISITIRI.

Ni yapi makazi ya mwanamke asiyevaa Hijabu wala hajisitiri Kiislamu huko akhera?  Sote tunafahamu kwamba, Mwenyezi Mungu ameweka adhabu kali kwa wale wanaokiuka maamrisho yake na wanaamua kuyaingia mambo ya haramu. Je ni adhabu gani atakayoadhibiwa mwanamke asiyejisitiri kwa vazi la Kiislamu na akaona ni bora kuutembeza mwili wake wazi kinyume na sheria inavyomtaka avae? Jawabu lake ni kama ifuatavyo: Kwa mwanamke asiyejsitiri hujisababishia laana na kujiweka mbali na rehma na radhi za Muumba wake. Pia hujiingiza mwenyewe katika unyonge na adhabu za Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume (s.a.w.w) anasema: “Katika zama za mwisho watakuja watu katika umati wangu ambao wanawake zao nusu wamevaa na nusu wako uchi. vichwani watasuka mafundo ya nywele na kuyaacha wazi bila kuyafunika. Basi sikilizeni (niwaambieni) kuweni wenye kuwalaani wanawake hao kwa kuwa wamekwisha kulaaniwa, wala hawataipata harufu ya pepo na iko mbali nao kwa masafa ya mwendo wa miaka mitano.”[72] Naye Imam Ali (a.s.) amesema: “Katika zama za mwisho kitapokuwa kiamakimekaribia, watatokea wanawake watakaokuwa wakitembea uchi bila kujisitiri kisheria.

Wanawake wa aina hii watakuwa wametoka katika dini na wataingia katika fitna, watapenda starehe na mambo ya fahari na watahalalisha mambo ya haramu. Wanawake hawa malipo yao ni

kuingia motoni, basi angalieni sana kipindi hicho ni kibaya kuliko vyote.”

Kuna hadithi nyingine kutoka kwa Bwana Mtume (s.a.w.w.) inayoelezea adhabu za wanawake wasiojisitiri kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Hadithi hii tunainakili kwa kifupi. Imam Ali (a.s.) anasema: “Mimi na Fatma (a.s.) tuliingia nyumbani kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu tukamkuta analia sana. Nikamwambia ni kitu gani kinakuliza? Mtume akasema: ‘Ewe Ali, usiku niliopelekwa mbinguni niliwaona wanawake katika umati wangu wakiadhibiwa vikali. Nilihuzunishwa na hali yao hiyo na nikalia kutokana na adhabu kali wanayoadhibiwa.’ Kisha Bwana Mtume (s.a.w.w) akaanza kueleza aliyoyaona katika usiku huo wa Miraji akasema: ‘Nilimuona mwanamke amefungwa kwa nywele zake kwenye moto na ubongo wake unatokota. Na nikamuona mwanamke mwingine amening’inizwa kwa ulimi wake huku moto ukimiminwa kooni mwake. Pia nikamuona mwanamke anakula nyama ya mwili wake hali yakuwa chini yake panawaka moto mkali, na mwingine amefungwa mikono yake na miguu kwa pamoja, kisha amezungukwa na mojoka mengi na nge wanamuuma. Pia nilimuona mwanamke kiziwi tena kipofu halafu hawezi kusema akiwa ndani ya moto ubongo wake unavuja kupitia puani, mwili umeenea vidonda mithili ya mgonjwa wa ukoma. Na kuna mwanamke mwingine anakatwa nyama za mwili wake kwa mikasi.

Bibi Fatma (a.s.) akasema kumwambia baba yake: ‘Baba hebu nifahamishe ni matendo gani waliyoyatenda wanawake hao hapa duniyani?’ Mtume (s.a.w.w.) akajibu: ‘Ewe Binti yangu, ama yule aliyekuwa amefungwa kwa nywele zake, yeye alikuwa hafuniki kichwa chake mbele ya wanaume wasiomhusu. Na yule aliyening’inizwa kwa ulimi wake alikuwa akimkera na kumuudhi mumewe. Ama aliyekuwa akila nyama ya mwili wake, huyo alikuwa akiupamba mwili wake kwa ajili ya watu wamuone. Na yule mwanamke aliyefungwa mikono na miguu kwa pamoja na akawa anaumwa na majoka na nge, huyu alikuwa mchafu hana udhu nguo zake chafu na alikuwa hakogi janaba wala hedhi na alikuwa akipuuza kuswali. Ama yule kipofu, kiziwi na hawezi kusema alikuwa akizaa watoto wa zinaa ( nje ya ndoa) na kisha humpachikia mumewe na kudai kwamba ni watoto wa mumewe.

Na huyu wa mwisho ambaye alikuwa akikatwa nyama za mwili wake kwa mikasi, alikuwa Malaya, akiitoa nafsi yake kwa kila mwanaume.”[73] Kwa hiyo imetudhihirikia wazi katika hadithi hiiaina mbali mbali za mateso na adhabu alizoziandaa Mwenyezi Mungu kwa wanawake wasiozingatia kanuni ya Hijabu kwa maana zake zote.

Miongoni mwa adhabu hizo ni kufungwa kwa nywele zake nwanamke na kutokota ubongo baada ya kupata adhabu ya moto unaowaka pande zake zote. Kwa hivyo basi, ina maana kila mwanamke atakayeshindwa kusitiri mwili wake na akauacha wazi kwa kila mtu, hapana budi ataadhibiwa kwa adhabu kali inayoumiza, kama zilizotajwa ndani ya hadithi.

Lakini ikiwa mwanamke mwenye sifa hizi zilizotajwa katika hadithi atatubia kwa Mwenyezi Mungu na kuacha kabisa makosa hayo aliyokuwa akiyatenda, kisha akavaa kama sheria ya Kiislamu inavyomtaka avae kwa ukamilifu, bila shaka Mwenyezi Mungu atakubali toba yake na atamsamehe. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema: “Ni yeye Mwenyezi Mungu ambaye anakubalitoba za waja wake (wanapotubia) na anasamehe makosa na anafahamu mnayoyatenda”[74] Na anasema tena Mwenyezi Mungu (s.w.t.): “Nami kwa hakika ni mwingi wa kusamehe kwa yule anayetubia na akaamini na kutenda mema kisha akaongoka”[75]  Hijabu Isiyokamilika: Kuna baadhi ya dada zetu ambao utawaona wamevaa Hijabu, lakini Hijabu yao hiyo siyo kamilifu kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Kina dada hao utawaona wamejistiri sehemu fulani tu ya kichwa, na au sehemu fulani ya mwili na halafu sehemu nyingine za mwili ziko wazi mbele ya kila mtu.

Wakati mwingine wanaweza kujisitiri vizuri kichwa chote, lakini utaona mikono au miundi iko wazi au ikawa haikusitiriwa ipasavyo. Kwa hakika Hijabu kama hii moja kwa moja ni Hijabu isiyokamilika ni Hijabu pungufu isiyoweza kutimiza lengo la Hijabu linalokusudiwa. Wakati huo huo, uvaaji kama huo si uvaaji ulioko juu ya msingi wa kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

Hali kama hii ya uvaaji usiokamili iliwahi kutokea katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w), ambapo walikuwako wanawake ambao hujistiri sehemu ya kichwa na kuacha sehemu nyingine bila kuisitiri ikiwa ni pamoja na masikio. Tendo kama hili Mtume (s.a.w.w) alilikemea na akawaamuru wanawake wajisitiri kikamilifu kwa mujibu wa sheria. Kumbuka ndugu msomaji ile hadithi ya Mtume aliposema: “Nusu wamevaa na nusu wako uchi.” Hadithi hii inamaanisha kwamba, wanawake watakuwa wanajisitri sehemu ya maungo yao na sehemu nyingine hawajisitiri. Kama hali ndiyo hii tuliyonayo, lengo la Mtume (s.a.w.w) ni kuwafahamisha wanawake wanaovaa hivyo kwamba wasidhani kuwa wamevaa Hijabu, bali inawapasa watambue kwamba uvaaji huo siyo kamili na haukubaliki kisheria.

NENO LA MWISHO

Wasomaji wapendwa imetudhihirikia katika yale tuliyoyataja ndani ya kitabu hiki kwamba, Hijabu ni vazi la Kiislamu na siyo fashion,[76] na ni kanuni iliyojaa hekima nyingi. Hijabu inalinda

heshima ya mwanamke na inaitakasa familia na jamii nzima.

Zaidi ya hapo ni amri ya kidini na hukumu ya sheria za Kiislamu, Mwenyezi Mungu ameithibitisha na kuitaja ndani ya Qur’an Tukufu. Naye Bwana Mtume (s.a.w.w) na watu wa nyumba yake wamesisitiza na kuitilia mkazo sheria hii. Kinyume cha maagizo haya na faida zilizomo ndani ya Hijabu, tayari tumekwishakuona wazi kwamba jamii huwa inaharibika na mwanamke kuangamia na ndipo familia inapotengana.

Zaidi ya hapo kutokuchunga mipaka ya mavazi, hasa Hijabu kwa wanawake ni uasi wa amri ya Mwenyezi Mungu, na maamuzi yake pia ni kinyume na maslahi ya wengi. Kwa hiyo ni wajibu wetu sote kufanya kila linalowezekana ili kuona sheria hii inafanya kazi na kuieneza baina ya wanawake waliomo katika jamii zetu, majumbani, mashuleni, maofisini na kila mahali. Kwa kufanya hivyo, tutapata radhi za Mwenyezi Mungu, pia huu utakuwa ni wema kwa ajili ya nafsi zetu hapa duniani na kesho akhera.

Back Index Next