Back Index Next

Kitu kingine muhimu kinachojitokeza katika Aya hii ni kwamba, Mwenyezi Mungu anamtaka mwanamke wa kiislamu apambike kwa sifa tofauti na wanawake wasio Waislamu katika mavazi na Uchaji Mungu. Hali hii ni kwa sababu wanawake wa ki-Yahudi, ki-Kristo na washirikina huwa hawajilazimishi kufuata hukmu hii ya sheria ambayo ndani yake mna hekima nyingi . Wao hutoka bila kujali kulinda heshima zao kama wanawake na mapambo yao huwa wazi mbele ya kila mtu.

Suala la kutojiheshimu kwa wanawake wa kiislamu, Mwenyezi Mungu hapendezwi nalo, ndiyo maana akawatakia utukufu na heshima kwa kuwachagulia vazi litakalowasitiri na kulinda hadhi yao. Kutokana na maelezo haya, linapatikana fundisho ambalo linamtaka kila mwanamke alizingatie kuhusu namna ya kuvaa.

Na iwapo mwanamke wa kiislamu ataacha kuvaa Hijabu na akaamua kuuacha wazi mwili wake, basi atakuwa kajifanananisha na wanawake wa kiyahudi kikristo na washirikina. Pia huonekana kama mtu anayekataa heshima na utukufu ambao Uislamu unamtaka awe nao. Si hivyo tu bali huwa anajisogeza taratibu hadi kwenye mwelekeo mbaya unaomchukiza Mwenyezi Mungu. Kuna hadithi isemayo kwamba; Mwenyezi Mungu alimpelekea Wahyi (ufunuo) Mtume fulani miongoni mwa Mitume wake akamwambia, “Waambie Waumini; wasivae mavazi ya maadui zangu, na wala wasile vyakula vinavyoliwa na maadui zangu, na wala wasipite katika njia wanazopita maadui zangu, (ikiwa watayafanya haya niliyoyakataza) basi nao watakuwa miongoni mwa maadui zangu kama walivyo hao ambao ni maadui zangu.”[9]

Aya hizi tatu zimekuja kuzungumzia maana ya Hijabu, na kuna Aya nyingine nyingi kuhusu suala hili ambazo hatujazitaja ili kufupisha maelezo.

BIBI FATIMA (A.S) KIIGIZO CHEMA KWA WANAWAKE.

Bibi Fatimah (a.s.) ni mwanamke anayezingatiwa kuwa ni mwanamke wa kutolea mfano katika dini ya kiislamu, na pia ni kiigizo chema kwa kila mwanamke anayetafuta mafanikio katika maisha yake. Bibi Fatimah binti Muhammad (s.a.w.w) ndiye mwanamke bora ulimwenguni aliyezaliwa na kupata malezi katika nyumba iliyokuwa ikishuka ndani yake Wahyi kutoka mbinguni.

Si hivyo tu bali Bibi Fatimah alihitimu mafunzo ya Uislamu katika madrasa ya Utume, na kutokana na mafunzo hayo aliweza kufikia daraja ya juu na tukufu. Katika kuthibitisha ubora wa Bibi Fatimah, Mtume (s.a.w.w) amepata kusema, “Hakika Mwenyezi Mungu huwa radhi kwa radhi ya Fatimah, na huchukia kutokana na kuchukia kwa Fatimah.”[10]

Kwa ajili ya daraja kubwa aliyonayo Bibi Fatimah katika Umma wa Nabii Muhammad (s.a.w.w) imekuwa ni wajibu kwa kila mwanamke duniani kuiga mwenendo wa Bibi huyu katika maisha yake, ajing’arishe kwa nuru yake nzuri na afuate nyayo zake ambazo zitamuelekeza kwenye mafanikio na utukufu.

Hakika Bibi Fatimah (a.s), ni mfano wa kila utukufu na kila jema. Mwanamke yeyote atafanikiwa iwapo ataamua kufuata mwenendo wa Bibi Fatmah (a.s.), na kinyume chake ni kuwa, kila mwanamke ataangamia iwapo ataamua kujichagulia mwenendo wake au kuiga usiyokuwa mwenendo wa Bibi Fatimah. Pia Fatimah (a.s.) alikuwa Mchaji Mungu na mwenye kutekeleza vilivyo maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Pia ile maana nzima ya Hijabu aliifahamu vema na kuitekeleza kama ilivyoamriwa na Mwenyezi Mungu.

Hivyo utekelezaji wake katika maamrisho ya Mwenyezi Mungu ulikuwa wa hali ya juu, kwani hakupata kutoka nje ila huwa amevaa vazi la kumsitiri mwili wake wote tangu kichwani hadi

miguuni. Isitoshe alikuwa akiichukia mno tabia ya wanawake kutoka majumbani mwao bila kujisitiri kisheria. Bibi Fatimah alichukizwa na tabia hiyo kwa sababu Mwenyezi Mungu pia anaichukia tabia ya kutokujisitiri na hasa kwa kuwa kukosa sitara ya kishera kwa wanawake ni ufunguo wa kuyaendea maovu na ni miongoni mwa vitangulizi vinavyosababisha watu kuteleza, bali wanaanguka kabisa. Sasa hivi tunawaletea baadhi ya mafundisho kuhusu Hijabu na

tutaona pia utukufu wa Bibi Fatimah katika mafunzo hayo.

NI KITU GANI KILICHO BORA KWA MWANAMKE?

Inasimuliwa katika historia kwamba, Mtume (s.a.w.w) siku moja aliwauliza Masahaba suali lifuatalo: “Je! ni kitu gani kilicho bora kwa mwanamke?”  Masahaba walinyamaza kwa kuwa jibu la mkato na sahihi hawakulifahamu, ikawa kama kwamba akili zao zinahangaika baina ya kuwa kilicho bora kwa mwanamke ni mali, uzuri wake, kuolewa au kitu gani? Kipindi chote hiki Bibi Fatimah alikwisha lisikia swali hilo, na baada ya kimya cha kukosekana jibu, Bibi Fatimah alimtuma mtu aende kwa Mtume (s.a.w.w) akatoe jibu sahihi la swali hili nalo ilikuwa; “Kilicho bora kwa mwanamke ni yeye mwanamke asimuone mwanaume na mwanaume naye asimuone mwanamke.”[11]

Baada ya jibu la bibi Fatimah Masahaba walikuwa wakisubiri jibu la Mtume atasema nini kuhusu jawabu alilotoa Binti yake. Mtume (s.a.w.w) akasema “Amesema kweli Fatimah. ”Na akaongeza kusema, “Fatimah ni sehemu iliyotokana na mwili wangu.” Maana ya maneno ya Mtume yalimaanisha kwamba hilo ndilo jawabu sahihi na hiyo ndiyo imani. Kutokana na jawabu hili, Bwana Mtume (s.a.w.w.) akawa ameitangazia dunia nzima kwamba; Utu, heshima, utukufu, na wema wa mwanamke unapatikana ndani ya Hijabu, na kinyume chake ni uovu na shari, isitoshe hasara humfika mwanamke anapoitupa Hijabu.

MAZUNGUMZO YA KUSTAAJABISHA

Historia inaendelea kutufahamisha kwamba Bibi Fatimah (a.s.) alikuwa amekaa na baba yake ambaye ndiye Mtume (s.a.w.w), mara alibisha hodi Sahaba Abdallah ibn Ummi Maktum ambaye

alikuwa kipofu. Kabla Sahaba huyu hajaingia Bibi Fatimah (a.s.) alisimama akaondoka mahali hapo. Baada ya kwisha mazungumzo baina ya Mtume na Sahaba huyu, Sahaba Abdallah ibn Ummi Maktum aliondoka. Bibi Fatima alirudi na akaendelea kuzungumza na Mtume (s.a.w.w.) Bwana Mtume (s.a.w.) akamuuliza Binti yake sababu ya kuondoka wakati alipoingia Sahaba Abdallah ibn Ummi Maktum hali kuwa anafahamu kabisa kwamba yule ni kipofu haoni.[12]

Bibi Fatimah alijibu kama ifuatavyo.”Ikiwa yeye hanioni basi mimi namuona na yeye ananusa harufu ya wanawake. “Mtume (s.a.w.w) alifurahishwa mno na jawabu la Binti yake ambalo linaonyesha kipimo cha Uchamungu na utukufu unaotoka kwa Binti yake Mwenye hekima. Isitoshe kwa jawabu hilo, Bwana Mtume hakumlaumu binti yake kutokana na mkazo huu mkali unaohusu Hijabu, bali furaha ya Mtume iliendelea kwa upeo mkubwa na akaunga mkono kwa dhati kabisa kisha akasema; “Nashuhudia kwamba wewe ni sehemu iliyotokana nami”.[13]

TUKIO MUHIMU NDANI YA MSIKITI WA MTUME (S.A.W.W.)

Siku moja Bibi Fatimah (a.s.) alitaka kutoa mhadhara ndani ya msikiti wa Mtume (s.a.w.w). Kabla ya kuanza kuhadhiri alitengenezewa sitara humo Msikitini, akakaa yeye na Waumini wengine wakike upande mmoja na Waumini wanaume wa Kiansari na Muhajirina nao wakakaa upande wa pili. Sitara hii aliyotengenezewa Bibi Fatimah (a.s) ilikuwa ina maana nyingi ndani yake.

Kwanza ilikuwa ni kutekeleza sheria inayohusu Hijabu katika sura ya kuweka kizuizi, ambapo pande mbili hizo zilitenganishwa. Pili, hali hiyo ilikuwa ni kuonesha kutokuukubali kwa vitendo mchanganyiko wa wanaume na wanawake, jambo ambalo maadui wa Uislamu wanatumia kila mbinu kulihalalisha kwa kulitolea hoja batili. Sasa nakutazama ewe dada yangu wa kiislamu, nikitarajia umeiona mifano hii mitatu inayohusu maisha ya Bibi Fatimah (a.s.) ambaye ni mwanamke bora kuliko wanawake wote duniani, na ni mwanamke anayestahiki kuigwa katika Uislamu. Inafaa uige na ujifunze kwake ili upate kupambika kwa umbile la kike (yaani kuwa na haya) na utukufu, kadhalika ifanye nafsi yako iwe ya mwanamke Mchamungu mwenye kushika mafunzo ya kiislamu na hukmu za Qur’an. Ewe dada wa kiislamu hebu shikamana na mafunzo ya kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu amekupa ili ufanikiwe duniani na akhera. Mafunzo haya

yatakupandisha kwenye daraja tukufu la wenye imani na mafanikio. Fahamu kwamba hutafanikiwa isipokuwa uwe umeshikamana na kuyatumia mafunzo hayo kwa kuyatekeleza maishani mwako.

KUJIHESHIMU NDIYO PAMBO LA MWANAMKE.

Bwana Mtume (s.a.w.w) amesema, “Kujiheshimu ndiyo pambo la Mwanamke.”[14] Hapana shaka kwamba pambo limegawanyika sehemu mbili: Pambo lisilo halisi na pambo halisi. Ama pambo lisilo halisi ni lile ambalo linaloonekana wazi, na ni lenye kubakia kwa muda maalum, kisha hutoweka bila hata ya kumuongezea kitu muhusika katika utu wake. Ama lile pambo halisi, ni lile ambalo hubakia muda wote na pia humfanya mwanamke aupate ule utu wake kamili na kumfikisha kwenye daraja ya ukamilifu. Ukweli usiokuwa na shaka ni kuwa, pambo halisi ndilo lenye umuhimu mno kuliko lile jingine, bali ndilo lengo analopaswa kulishughulikia kila mtu.

Endapo mtu atakosa kuwa na fungu fulani katika pambo hili halisi, basi pia huwa hana faida yoyote ndani ya lile pambo la dhahiri. Hapana shaka kwamba kujiheshimu ndilo pambo pekee

linalomfaa mwanamke kama alivyosema Bwana Mtume (s.a.w.w). Pambo hilo humjengea mwanamke utu, heshima na utukufu hapa duniani na kesho akhera. Ama madawa ya kujirembesha, manukato na mengineyo miongoni mwa mapambo, yote hayo ni mapambo ya nje tu na hayana maana yoyote khususan mwanamke mwenyewe atakapokuwa si Mchajimungu; Mwenyezi Mungu apishe mbali.

Hijabu ndiyo alama pekee inayoweza kutambulisha Uchaji Mungu wa mwanamke na pia heshima yake na utu wake. Wakati huo huo tabia ya kutokuwa na Hijabu huchafua heshima ya mwanamke na kuacha maswali chungu nzima kuhusu Uchaji Mungu wake na kujiheshimu kwake kwa jumla.

Yote haya yanakuja kwa sababu yeye mwenyewe kauweka mwili wake kuwa maonesho mbele ya maelfu ya watu siku zote. Kutokana na hali kama hiyo, hata huwezi kutambua ni mikono mingapi iliyowahi kuushika mwili wake kwa kuuacha wazi na kutokujisitiri kwa mujibu wa sheria!!

Hivi unadhani watu wa kale na hata wa leo hii, nyoyo zao zitasalimika vipi katika mazingira hayo ya wanawake kuicha wazi miili yao? Kamwe hawatasalimika kabisa, kwani wanawake wanapoiacha wazi miili yao ni jambo linalopelekea tuhuma mbaya kwa wanawake. Imam Ali (a.s.) anasema ; “Yeyote mwenye kuiweka nafsi yake mahala penye tuhuma mbaya, basi asimlaumu mtu atakaye mdhania vibaya.”[15] Hapana shaka kwamba, mwanamke asiyekuwa na Hijabu huwa anaidhuru nafsi yake mwenyewe kwa sababu; Kwanza, huwa anapata hasara mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Pili, heshima yake ndani ya jamii huwa inaporomoka. Hasara anayoipata mwanamke huyo mbele ya Mwenyezi Mungu inakuja kwa sababu mwanamke huyo huwa amekwenda kinyume na kanuni za mbinguni na kukosa utiifu kwa Mwenyezi Mungu.

Baadaye tutaeleza adhabu za huko akhera atakazozipata mwanamke asiyejali kujisitiri kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Ama hasara atakayoipata mwanamke kutokana na heshima yake kuporomoka ndani ya jamii, hali hiyo inasababishwa na yeye mwenyewe kutokana na tabia yake ya kuyaacha wazi maungo yake yaonekane kwa kila mtu, hali ambayo humuingiza ndani ya kila aina ya uovu na ufisadi na hatimaye akadhalilika vibaya. Na tukirejea kwa mwanamke mwenye kujisitiri kwa mujibu wa sheria ya kiislamu, huyu hupata faida za aina mbili kwa pamoja:

Faida aipatayo mbele ya Mwenyezi Mungu ni kwamba, yeye huwa ni mwanamke mtukufu mbele ya Mwenyezi Mungu na Malaika wake pamoja na Mawalii wa Mwenyezi Mungu. Utukufu huu anaupata kwa kuwa amemtii Mola wake, ametekeleza maamrisho yake na ameyasitri maungo ambayo Mwenyezi Mungu ameamrishsa yasitiriwe. Na kwa ajili hii basi, mwanamke kama huyu kamwe hatonyanyua unyayo wake bali rehma za Mwenyezi Mungu huwa ziko pamoja naye, pia radhi za Mwenyezi Mungu huambatana naye, na wakati huo huo Malaika wa Mwenyezi Mungu wanamuombea msamaha. Mwenyezi Mungu anasema; “Kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na ni chenye kubakia.”[16] Ama faida atakayoipata ndani ya jamii, ni pale mwanamke huyo anapokuwa ni mwenye kuheshimiwa na kutukuzwa, yote haya anayapata kwa kuwa yeye amejipamba kwa pambo la kujiheshimu na kuuhifadhi utu wake, kisha akausitiri uzuri huo aliopewa na Mwenyezi Mungu.

MAJADILIANO NA MSICHANA WA KIKRISTO.

Msichana mmoja wa Kikristo alikwenda kwa mwanachuoni wa kiislamu na kumwambia. “Mimi nimefahamu mambo mengi kuhusu Uislamu na kwa hakika dini hii imenishangaza sana kwa kanuni zake na miongozo yake, na nimeupenda Uislamu kwa mapenzi ya kweli. Lakini kanuni moja tu kwangu mimi imekuwa ni kikwazo kuingia katika Uislamu. Nimewauliza watu wengi kuhusu kanuni hiyo, mpaka sasa sijapata jawabu la kunitosheleza. Iwapo wewe Sheikh utaweza kunibainishia hekima iliyomo ndani ya kanuni hii, basi nakuthibitishia kuwa nitaingia katika Uislamu.”

Yule Mwanachuoni akasema, “Ni ipi kanuni hiyo?”Msichana akajibu. “Kanuni ya kuvaa Hijabu, ni kwa nini Uislamu haumuachi mwanamke akatoka nje apendavyo kama ilivyo kwa wanaume.?”Mwanachuoni yule wa kiislamu akasema, “Je umepata kumuona sonara ameweka dhahabu na johari nyinginezo katika sanduku la kioo, kisha akalifunga sanduku hilo kwa kufuli? Msichana akajibu, “Ndiyo.”Sheikh huyu akamwambia tena yule msichana, “Je, ni kwanini sonara

hakuziacha johari hizo zikawa zinashikwa na kila mtu ajaye kutaka kununua? Kwa nini amezihifadhi ndani ya sanduku la kioo lililofungwa?”Msichana akasema; “Amefanya hivyo ili azilinde johari zake kutokana na wezi na mikono yenye khiyana.”Yule Mwanachuoni akamwambia msichana; “Hii ndiyo hekima ya Hijabu, fahamu kwamba mwanamke ni johari ya thamani ambayo ni lazima kuilinda kutokana na waovu na wahaini.

Pia ni wajibu kumhifadhi mwanamke kutokana na macho ya watu waovu ndani ya kitu ambacho kitamsitiri barabara kama inavyolindwa lulu katika kola lake, ili asije akaangukia mikononi mwa watu hao na kumgeuza kuwa ngawira yao.”Hakuna njia bora isipokuwa Hijabu, hicho ndiyo kizuwizi na ni mlinzi wa mwanamke. Kwa hakika mwanamke mwenye Hijabu huwa salama kutokana na shari. kwa kuwa mwili wake umesitirika, na mapambo yake nayo hayaonekani mbele ya kila mtu.

Hali ya kuvaa Hijabu inawafanya watu wasimtamani mwanamke huyo kwa kuwa hakuna wakionacho cha kuwafanya wamtamani. Kutokana na hali hiyo huwa wanamuepuka, wala hakiwageuzi kitu chochote cha kuwafanya wamuangalie mwanamke huyo, bali humuogopa na kumuheshimu. Mwisho wa yote watu humuogopa na kumpa heshima yake kama anavyostahiki.

Yote hayo yatapatikana kwa ajili ya kuvaa Hijabu, na hali hii inamaanisha kwamba, Hijabu ndiyo mlinzi wako na ni hifadhi ya heshima, na utukufu wako. Ewe msichana huu ndio upande mmoja wa falsafa ya Hijabu.” Baada ya maelezo hayo ya Sheikh, msichana yule wa Kikristo alionesha furaha na akaridhishwa na maelezo ya Sheikh kisha akasema, “Sasa nimetosheka na falsafa iliyomo ndani ya kanuni hii ya kiislamu, na pia nimefahamu hekima iliyomo na ninapendezwa kuingia katika Uislamu.”Baada ya hapo msichana akatoa Shahada mbili na akawa Muislamu.

Majadiliano haya mazuri ya kidini yanatubainishia kwamba Uislamu unakusudia kuihifadhi hehsima na utukufu wa mwanamke, pia Uislamu unataka kuilinda jamii. Na kwa sababu hizo basi, Uislamu umewajibisha Hijabu kama sharti la msingi kuweza kutimiza malengo hayo.

TOFAUTI YA MWANAMKE MWENYE HIJABU NA ASIYE NA HIJABU.

Mmoja wa marafiki zangu alinisimulia tukio la kufurahisha lililomtokea Muumini mmoja wa kiislamu. Tukio hili lilikuwa kama ifuatavyo. Siku moja Muumini huyo alikuwa akitembea pamoja na mkewe aliyekuwa kavaa Hijabu. Matembezi hayo yalimfikisha katika moja ya bustani zinazotembelewa na watu wa aina tofauti.

Ghafla Muumini huyo alijiwa na mtu fulani ambaye naye alikuwa na mkewe. Mke wa mtu huyu hakuwa amevaa vazi la Hijabu na hivyo basi kwa dharau na kejeli alimwambia yule Muumini. “Kwa nini umemvalisha mkeo Hijabu, kwa nini hukumuacha akatoka bila Hijabu kama jinsi alivyo mke wangu? Hijabu ina faida gani?”Jawabu alilotoa Muumini yule lilikuwa la kushangaza na la kishujaa. Alimwambia. “Je unafahamu tofauti ya mwanamke mwenye Hijabu na asiyekuwa na Hijabu? Bwana yule mwenye kejeli akasema “Nini tofauti yake?”Yule Muumini akajibu kwa njia ya kuuliza, je, kuna tofauti gani baina ya taxi na gari ambalo mtu hulitumia yeye binafsi? Yaani kwa matumizi yake pekee yake.”Bwana yule akajibu akasema, “Taxi hutumiwa na kila mtu, wakati ambapo gari maalum linamuhusu mwenyewe peke yake. Hii ndiyo tofauti iliyopo.”Basi yule Muumini akasema, “Hali hiyo ndio iliyopo baina ya mwanamke aliyevaa Hijabu na yule asiye na Hijabu.

Mwanamke asiye na Hijabu ni sawa na taxi ambayo kila mtu anaweza kuikodisha na kuitumia. Mwili wa mwanamke huyo huwa wazi na kuonesha mapambo yake na uzuri wake, na kuwafanya watu wavutike kutokana naye, jambo ambalo linaweza kusababisha kutendewa maovu, kama ambavyo mara kwa mara hali hii inavyowapata wanawake wa aina hii. Ama mwanamke aliyevaa Hijabu yeye ni bibi aliyemtukufu, ni maalum kwa ajili ya mumewe, mapambo yake na uzuri wake havionekani kwa kila mtu. Pia watu wenye nyoyo chafu na dhaifu hawamuangalii, na uso wake na mapambo yake havikutani na macho yenye khiana, kwa kuwa amehifadhiwa ndani ya Hijabu.

Kwa hiyo utukufu wa mwanamke huyu na mwili wake vimo ndani ya hifadhi bora, pia bibi huyu hupendwa na kupendeza mbele ya mumewe na kumfanya mume kuwa na imani na mkewe, kwa sababu ya hifadhi hiyo inayomkinga kuwa na mahusiano na watu wengine kwa njia mbaya.”Baada ya maelezo yaliyotolewa na yule Muumini wa kiislamu, bwana yule mwenye kejeli aliona haya na akaanza kumwambia yule Muumini, “Najuta kwa kukuudhi, kwani maneno yako ni ukweli mtupu, na mifano uliyonipa ni sawa kabisa naomba samahani kwa haya niliyokutamkia na pia natubia kwa Mwenyezi Mungu kwa kitendo nilichokitenda na sasa…... Kabla bwana huyu hajamaliza kujieleza mkewe alimkatiza na kusema. “Naam; naapa maneno haya aliyosema bwana huyu ni sawa na mfano aliotoa ni mzuri sana, kwani kabla ya leo nilikuwa sijasikia mawaidha kama haya. Mfano huu umeniingia moyoni nami pia natubia kwa Mwenyezi Mungu.”

Baadaye yule mume akarudia kukamilisha usemi wake akasema, “Na mimi sasa naiamini Hijabu na kuanzia leo mke wangu ataingia katika uwanja mtukufu kwa kuvaa Hijabu. Kamwe sikubali mke wangu atoke bila Hijabu, kwani ndiyo vazi la amani na imani. Nafsi yangu haipendi kabisa kumuona mke wangu akidhihiri mbele za watu kama kwamba yeye ni kwa ajili ya kila mtu.”

NI LIPI LENGO LA WANAOPINGA HIJABU?

Baada ya kuusoma Uislamu kwa undani, maadui wa Uislamu wameandaa mikakati ya kuuangamiza Uislamu na Waislamu kidogo kidogo, bila Waislamu kuigundua hali hii isipokuwa wachache. Na miongoni mwa mikakati yao ya kishetani katika kutilia mkazo kuiondoa Hijabu, wametumia na bado wanatumia kila njia za kuvutia na madai batili kutimiza lengo lao hilo. Kuna

mambo mengi machafu wanayoyaeneza katika jamii ya Waislamu, chini ya kiza kinene chenye ibara zinazovutia na kampeni ambazo matokeo yake ni mabaya. Kwa kutumia mbinu za kimaendeleo na utaalamu, wamefaulu kuwapotosha Waislamu, na wakasambaza uovu mwingi. Kwa madai hayo hayo ya maendeleo na kupigania uhuru na haki za binadamu., uchafu wao umeenea ndani ya jamii zetu za kiislamu. Kwa hakika wamefaulu kuzinyang’anya jamii zetu maumbile ya kuwa na haya na heshima. Ibara hizi zimewahadaa Waislamu wengi, wake kwa waume. Masikini Waislamu hawa wamekuwa wafuasi wa itikadi hizi zenye sumu kali inayovuja kuelekea kwenye maovu na maangamio. Wanawake wa kiislamu na mabinti wa kiislamu wanafanya upinzani hadharani dhidi ya vazi hili la kiislamu.

Back Index Next