rudi maktaba >Akida >Yaliyomo >

UKRISTO NA UISLAMU

Kwa namna yao ya kufikiri, Mungu aliwafanya Wayahudi kuwa ni watu wake wateule. Kwa hadhi hii waliyopewa Wayahudi, ilimanisha kwamba ni wao tu (Wayahudi) waliotengwa na Mungu kwa ajili ya kuteremshia ufunuo na kupata Mitume wa Mungu kutoka miongoni mwao. Kwa hiyo Wakristo wanahisi kwamba wanaweza kumwamini tu Mtume ambaye ni Mwisraeli, na kwamba wengine wote ni walaghai.

Uislamu unawaletea Wakristo suala jingine kwa ajili ya mjadala. Mara tu baada ya kuanza kuenea kwa kasi kwa Uislam muda mfupi baada ya kuondoka duniani Mtukufu Mtume Muhammad (SAWW), Wakristo walianza kueneza ukweli kwamba mtu mmoja kutoka Uarabuni ni kweli kwamba alikuwa na ujasili wa kwenda na kuzunguka maeneo mbalimbali akidai (tangaza) kuwa yeye ni Mjumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Licha ya Uislam kusisitiza kwamba ingekuwa kinyume na busara na uadilifu wa Mwenyezi Mungu kuteremsha Mitume kutoka katika taifa moja tu, lakini bado wakristo hawakutaka kusikia. Mtume Muhammad hakuwa Myahudi, kwa hiyo mbele ya macho yao, alikuwa ni mtume wa uongo aliyekuja na ushuhuda wa uongo kutoka kwa Mungu wa Uongo.

Awali, mashambulizi ya Wakristo dhidi ya Uislam yalikuwa ni manung'uniko madogo madogo. Baada ya Khalifa wa Ukoo wa Fatimid aliyeitwa Hakim kuyavunja makaburi ya Wakristo Jerusalem katika mwaka 1010, manung'uniko yalibadilika na kuwa ngurumo za simba. Wazungu Ulaya walianza kuishi kwa hofu kubwa ya kuvamiwa na Waislamu, na hii ilikuwa ni sababu ndogo iliyoamsha chuki iliyokuwa imerundikana kwa muda mrefu. Papa Urban II alipoitisha vita vitakatifu "Crusades" mnamo mwaka 1095 ili kuikomboa Ardhi Takatifu kutoka kwa "makafiri", kampeni ya chuki dhidi ya Uislam ilianza kwa kasi ya roketi, ambapo ilifikia kilele chake katika karne ya kumi na mbili.

Katika mashambulizi yao ya maneno dhidi ya Uislam; mambo mengi maovu ya aibu na ya uongo yalipakwa rangi ya ukweli na wale waliodaiwa kuwa ni "wasomi na wanazuoni" wa wakati ule na yakasambazwa kwa wingi kwa karibu watu wote.

Mtume Muhammad (SAWW) alichukuliwa kuwa ni adui wa Kristo, mtume wa uongo, mwenye kujifaharisha na kujisifia sana, mtawala wa kimabavu, mwenye tamaa nyingi za kimwili, na mengine mengi.

Qur'an alidaiwa kuwa ni mkusanyiko wa hotuba, maneno ya kipuuzi na yasiyokuwa na maana na kwanza ni "kitabu kinachotia uvivu" kusoma kutokana na kilivyoandikwa mpangilio mbaya na mvurugiko usioweza kueleweka. Mbele ya macho ya Wakristo wa Medievo (yaani walioishi kati ya mwaka 1100 - 1500 B.K), Qur'an haingewezekana kwa namna yoyote ile kuwa ni Maneno ya Mwenyezi Mungu kwa sababu Muhammad alikuwa ni mtume wa uongo. Kwa hiyo walidai kuwa Mtume (SAWW) aligushi (aliandika mwenyewe). Kisha akadai kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu. Waliendelea kudai kwamba hakuna ufunuo wowote ulioteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu isipokuwa yalikuwa ni maneno ya kuweweseka ambayo Mtukufu Mtume Muhammad (SAWW) alikuwa anayasema alipokuwa anabanwa na kifafa, ambayo yeye (Mtume SAWW) alidai kuwa ni ufunuo.

Dini ya Uislam ilionekana kuwa si chochote isipokuwa ni upotofu na kwamba ni mafundisho yenye makosa, mafundisho yaliyochukuliwa kutoka katika Ukristo. Uislam ulichukuliwa kuwa ni dini ya upanga, na katika jitihada zao za kulichafua jina la Uislam, wakaupachika jina la "Mohammedanism" (yaani dini iliyoanzishwa na kuletwa na Muhammad (SAWW) badala ya Mwenyezi Mungu.)

Waislamu pia hawa kunusurika na ghadhabu hii ya Wakristo wa Medievo (Wakristo walioishi miaka ya 1100 - 1500 B.K) ambao waliwaita (Waislam) makafiri, wapagani, mabedui wa jangwani na wafuasi wa Muhammad (Muhammedans).

Kwa sababu ya kutotaka kwao kuukubali Uislamu, Wakristo wakawa maadui dhahiri wa Uislamu na Waislamu. Katika mashambulizi yao ya maneno, viongozi wa kanisa walitumia mbinu mbalimbali katika hila zao za kuudhuru Uislam; kama vile kuelemea upande mmoja katika hoja zao, upotoshaji, kutafsiri vibaya kwa makusudi, kubuni mambo ya uongo ili kuwashambulia n.k. Wakati haujabadili hali ya mambo, kwa bahati mbaya; zama za vita vitakatifu dhidi ya Uislamu "Crusades" zimepita siku nyingi lakini wakristo bado hawawezi kuukubali Uislamu. Wakristo wa zama hizi, wanatumia mbinu mpya ili kukabiliana na kile wanachokiona kuwa ni "hatari" ya uislamu.

Jitihada za Wamishenari

Matumizi ya nguvu dhidi ya Waislamu ambayo kilele chake ilikuwa ni vita vitakatifu dhidi ya Uislamu (crusades) yaliungana na jitihada za wamishenari kwa upande wa wakristo katika jitihada zao za "Kuwarejesha makafiri kwa Bwana". Jitihada hizi za wamishenari, hata hivyo zilipata mafanikio kidogo sana licha ya muda wote na fedha zilizotumika kwa mamia na mamia ya miaka ambapo jitihada hii imekuwa ikiendelea.

Jitihada za mwanzo katika kujaribu kuwabadili Waislamu kuwa Wakristo zilikuwa malumbano / mabishano kama yale yaliyotumika kwao, Waislamu walikataa kuyasikiliza malumbano hayo. Uzoefu umewaonyesha Wakristo kwamba matusi hayasaidii kitu, kwa hiyo jitihada za wamishenari wa Kikristo wa zama hizi zimechukua mwelekeo mpya kabisa. Wamejiwekea sera mpya ya "kuwahubiria Waislamu kwa upendo."

Nchini Marekani kuna taasisi moja inayoitwa "Center of Ministry to Muslims" (CMM), kituo cha Mahubiri kwa ajili ya Waislamu, taasisi hii imeandaa mpango maalumu (kifedha na kielimu), unaokusudia kufikisha ujumbe wa Ukristo wa kwa Waislamu. Malumbano (mabishano) hayatumiwi lakini bado njia zinazotumiwa sio za uadilifu kama vile upotoshaji, kutafsiri vibaya kwa makusudi hata kuzua mambo na habari za uongo. Ukweli juu ya Ukristo umefunikwa kwa utando wenye sukari, na taasisi hii (CMM) unawalenga Waislamu ambao wako peke yao katika nchi hii, bila msaada wa maadili ya familia na marafiki wa kiislamu.

Moja ya jitihada za CMM zinazofurahisha ni gazeti lao la "Noor ul Haq" au "Nuru ya ukweli". Gazeti hili linachapishwa kwa Kiingereza na Kiarabu muundo (format) wake una sura ya kuwa gazeti la kiislamu, lakini ilivyo ni gazeti la kikristo linalokusudiwa kuwafikia Waislamu. Linatumia misamiati ya Kiislamu na aya za Quraani, lakini uangalifu ni muhimu sana hapa kwa vile aya hizi za Quran zinapotoshwa na kutafsiriwa tofauti na zilivyotafsiriwa na Mtume (SAWW), ili kuwamezesha Waislamu mafundisho ya kikristo. Kwa Muislamu mwenye elimu ndogo ya dini, ni rahisi kupotoshwa na mafundisho haya.

CMM ni tasisi ndogo sana ikilinganishwa na "Zwemer Institute For Muslim Studies" (Tasisi ya Zwemer kwa ajili ya mafunzo ya Uislamu). Taasisi hii yenye kituo chake California, ambayo imechukua jina lake kutoka kwa mmishenari raia wa Netherlands ambaye alitumia takriban miaka hamsini katika kipindi cha mwanzo cha karne hii kuwahubiria Waislamu katika Mashariki ya Kati, huwafundisha Wakristo mbinu za kuwahubiria Waislamu. Wanafunzi katika taasisi hii wanajifunza Kiarabu, Historia ya Uislamu, Utamaduni wa kiislamu na imani ya Uislam na utekelezaji wake. Watu hawa wamejizatiti kwelikweli, na sio wajinga wa Uislamu kwa namna yoyote ile. Wamefundisha na wamekubali kuuchukia Uislamu lakini sio kwamba hawajui Uislamu.

Hii ni jitihada kubwa kabisa. Wahubiri (daiya) wanafunzi na wamishenari wanaoandikishwa katika taasisi hii huchukua aina zote za mafunzo juu ya Uislamu. Kuna zaidi ya haya. Pia kuna semina fupi zinazotolewa kwa vikundi vya kanisa vinavyopendelea (kufanya hivyo), na taasisi ina kituo cha uchapaji ambacho huchapisha majarida, vitine (pamfleti), vitabu na hata filamu na kanda za video.

Ni taasisi nzuri sana kwa Wakristo, lakini ni hatari sana kwa Waislamu. Wamishenari wa Kikristo wanaotoka katika taasisi hii hawajaribu hata kidogo kuonyesha kuwa Uislamu "ni rundo la kasoro na dosari". Wanajaribu kuonyesha kuwa Uislamu una "vipande vya ukweli ambavyo havikuunganishwa", na kutoka hapa, wanajaribu kumshawishi Mwislamu kwamba vipande hivi vya ukweli vimeunganishwa na kuwa kitu kizima katika Ukristo. Mashambulizi ya maneno sasa hivi yameachwa na baadala yake wanajaribu kujenga mashaka katika nyoyo za Waislamu juu ya imani yao. Wakristo wana matumaini kwamba mashaka haya baadaye yatasababisha kutoridhika, ambako kutapelekea kuhama kutoka kwenye Uislamu kwenda kwenye Ukristo.

Wamishenari wa Kikristo wanaangalia kwa furaha kabisa migogogro iliyomo ndani ya ulimwengu wa Kiislamu leo hii. Taasisi ya Zwemer inawaambia watu wake kuwa:

"Kuhamahama na ukimbizi (unaosababishwa na migogoro) pamoja na kuvurugika kwa maisha ya kawaida kumesaidia kuvuruga utamaduni wa zamani na umeleta uwazi mpya miongoni mwa Waislamu katika kusikia habari njema za Yesu kristo. Imani ya zamani kwamba Uislamu una nguvu isiyoweza kushindwa sasa hivi haina nguvu tena".[30]

Tarakimu zinazotolewa na Taasisi ya Zwemer kuwa ni ya Wakristo wapya bila chembe ya shaka yoyote zimekuzwa. Hii ni kwa sababu ikitajwa idadi ya ndogo ya Wakristo wapya itakuwa vigumu kupata wanafunzi na fedha za kutosha kwa hiyo wanalazimika kutoa tarakimu kubwa ili ionekane kuwa "mti" wa Ukristo unazaa matunda.

Kwa kadri Uislamu unavyoendelea kukua, mashirika kama CMM na Taasisi ya Zwemer ndivyo yanavyopata nguvu na kujizatiti zaidi. Huu sio wakati kwa Mwislamu kukaa na kulipuuza hili. Siku moja litakuja mpaka mlangoni pake, lazima ajiandae, lazima awe na imani thabiti, na ni lazima mjue jamaa yake (ukristo) ili asitetereke katika imani yake.

Kampeni Dhidi ya Chuki

Ingawa mashirika kama "CMM na The Zwemer Institute" yanatangaza "kuwafikia na kuwahubiria Waislamu kwa upendo", nyuma ya migongo yao kuna mbinu nyingine (ambayo haitangazwi) ambayo hutumiwa mara nyingi katika kuudhibiti Uislamu. Ni mbinu iliyoanza zama za vita vitakatifu dhidi ya Uislamu (Crusades) na mbinu hiyo kamwe haijafa kifo halisi. Mbinu hii inayotumika katika hila zao za kuudhuru Uislamu imepewa jina la "Vita vitakatifu vya kiakili dhidi ya Uislamu''. Mashambulizi haya ya mdomo dhidi ya Uislamu ni maendelezo ya kazi iliyoanza miaka zaidi ya 900 iliyopita ambapo Papa Urban II alihamasisha vita vitakatifu dhidi ya "makafiri" wa Mashariki ya kati alipokuwa akihutubia umati wa watu katika mji wa Clemont.

Ushahidi kwamba kampeni hii ya chuki dhidi ya Uislamu bado inafukuta unaweza kuonekana katika maduka ya vitabu - hususan maduka ya Wakristo - na katika maktaba za umma (public libraries).

Wale wanaojiita "Wataalamu bingwa wa historia, utamaduni, dini" (Orientalists) katika karne ya kumi na tisa na ishirini, wameandika mambo mengi ya kuchukiza juu ya Ulimwengu wa Kiislamu: Mifano mizuri ni kama vile "Story of Civilization" (Simulizi juu ya ustaarabu) kilichoandikwa na Durant. "The Decline and Fall of the Roman Empire" (Kudidimia na Kuanguka kwa Dola ya Urumi) kilichoandikwa na Gibbons. "Inside Asia" (Ndani ya Asia) kilichoandikwa na Gunther. "The Outline of History" (Dondoo za Historia) kilichoandikwa H. G. Welles -- ambavyo vyote vinahesabiwa kuwa ni vitabu "vyenye ubora wa kiwango cha juu kabisa" katika ulimwengu wa historia. Uelemeaji upande mmoja katika uchambuzi wa hoja na uadui umetapakaa katika maeneo yote na katika kila kona. Mtu anaweza kushangaa na kujiuliza vipi watu hawa wajizatiti kulisoma eneo fulani la ulimwengu, eneo ambalo wana chuki kubwa sana dhidi yake. Hata kitabu cha hivi karibuni cha Albert Hourani ambacho kimesifiwa sana kiitwacho "A History of the Arab Peoples" (Historia ya Waarabu) kimejaa uelemeaji upande mmoja katika uchambuzi wa hoja na uadui dhidi ya Uislamu.

Cha ajabu ni kwamba hawa wanaodaiwa kuwa wanapiga vita chuki dhidi ya Uislamu ni Wakristo wenye imani kali. Angalia kwa mfano kitabu "Islam Revealed" (Uislamu wawekwa wazi) kilichoandikwa na Mkristo wa Kiarabu mwaka 1988. Nyuma ya kitabu hiki mwandishi anaahidi kuwapa wasomaji wake "Mtazamo" utakaowafungua macho juu ya imani hatari kama ukoma walivyonayo kila mtu mmoja katika watano hapa duniani (yaani imani ya Uislamu). Mwandishi wa kimarekani Robert Morey, "anayedaiwa kuwa ni mwanazuoni (msomi) wa kimataifa" katika fani ya ulinganishaji wa dini mbalimbali - zaidi ya hili ni Mkristo mwenye msimamo mkali kidini - hivi karibuni ameandika kitabu kiitwacho "Islam Unveiled: The True Desert Storm" (Uislamu waachwa wazi: Kimbunga (Dhoruba) halisi cha Jangwani) alichokiandika mwaka 1991. Ndani yake anadai "Kuthibitisha" kwamba vitendo vyote vya ibada na imani za Uislamu zimetokana na Ukafiri (upagani) uliokuwepo kabla ya Uislamu. Dr. Morey pia huandaa kipindi cha redio (Radio show) ambacho ni maalum kwa ajili ya kuushambulia Uislamu. Hivi karibuni, katika kipindi hiki alisema: "- - - kama Muhammad angekuwa hai leo hii, bila shaka angechunguzwa kama mharibifu wa akili za watu, muuaji wa halaiki (ya watu,) na mdhalilishaji (mnyanyasaji) wa watoto".

Taarifa kama hizi ni mfano tu wa marundo na marundo ya taarifa zinazokusudiwa kujenga chuki zinazotolewa kila siku dhidi ya Uislamu na ambazo zinastahili kudharauliwa. Taarifa hizi zinakusudiwa kuimarisha na kueneza zaidi propaganda mbalimbali za chuki dhidi ya Uislam zinazoaminiwa na Wakristo walio wengi, na pia kuzidisha kutoaminiana na uadui, inawezekana vipi watu wakahubiriana kirafiki na kwa upendo na ilhali akili za watu zinashindiliwa takataka kama hizi?

Kwa kadri Uislamu unavyoendelea kukua na kuenea, ndivyo mashambulizi haya yatakavyozidi kuongezeka. Wakristo wanahofu, na hii ndiyo mbinu waliyoamua kuitumia katika kukabiliana na hofu hiyo. Ni mbinu ambayo imekuwa ikitumika kwa mamia ya miaka, na ni mbinu ambayo wametokea kuipenda sana. Badala ya kufungua milango ya mazungumzo juu ya tofauti za imani zao, wanafanya haraka kutumia jazba, hasira, na kujenga uadui.

Mbinu na Hila Nyingine Wanazozitumia Kuudhuru Uislamu

Mbali na vitabu, vitine (mapamfleti), vipindi vya redio, n.k. ambazo zimekusudiwa moja kwa moja kuudhuru Uislamu, pia kuna hila nyingine za chini chini zinazofanywa na Wakristo kupitia kwenye kazi za fasihi na zisizo za fasihi (fiction and non-fiction), pamoja na televisheni na mikanda ya video ambapo huuonyesha Uislam na Waislamu kuwa ni kundi chokozi la ugaidi na wagaidi.

Vitabu ni pamoja na "The Source" (chanzo) kilichoandikwa na James Mitchner na kingine cha hivi karibuni "The sum of All fears" (Jumla ya hofu zote) kilichoandikwa na Tom Clancy. Pia kuna vitabu vingine vinavyopotosha kama vile: "Jihad", "The Holy Sword" (Upanga mtakatifu) na "Sacred Rage" (Hasira Takatifu).

Kitabu kingine kinachoonyesha uadui mkubwa ni "Holy of Holies" (mtakatifu wa watakatifu); ambacho kinaelezea jinsi Wafaransa kwa msaada wa Warusi na Waisraeli, wanavyoharibu Msikiti Mkuu (Msikiti mtakatifu) wakati wa hijja. Na bila kusahau kitabu cha kikafiri cha Salman Rushdie, "The Satanic Verses". Mwandishi wa kitabu hiki, Salman Rushdie, amekuwa akieleza mara kwa mara kwamba nia yake haikuwa kuutukana Uislamu isipokuwa majina ya watu na majina ya sehemu (mahali) aliyoyatumia katika kitabu chake yamegongana mno na majina ya watu watukufu na sehemu tukufu za kiislamu kiasi kwamba inakuwa vigumu kuamini maneno yake.

Kashfa zinazofanywa dhidi ya Uislamu kupitia kwenye televisheni zinasikitisha. Katika kipindi cha kiangazi cha mwaka 1991, kulikuwa mfululizo wa midahalo (debates) iliyofanywa baina ya Waislamu wawili na Wakristo wawili kuhusiana na tofauti za dini zao. Midahalo sita ilionyeshwa kwenye televisheni kwa wiki (majuma) kadhaa juu ya injili. Na waislamu walifanya kazi nzuri sana ya kuwakilisha imani yao, hata mbele ya maadui dhahiri kutoka pande zote, ikiwa ni pamoja na msimamizi wa mdahalo, wazungumzaji wawili wa upande wa imani ya Kikristo, na hata hadhira ya wakristo.

Hata hivyo, waandaaji wa kipindi hiki cha televisheni walifanikiwa kupata walichokitaka, kwanza walibadilisha kanda za matangazo ili kuwaonyesha Waislamu katika mwanga mbaya. Pia walitoa kijitabu kuhusiana na mdahalo kwa ajili ya wasomaji wa majumbani ambacho walikipa jina "The facts on Islam" (Ukweli juu ua Uislamu). Jina lenye kufaa zaidi kwa kijitabu hiki lingekuwa "Mambo ya uongo na Fitna dhidi ya Uislamu" (Fallacies of Islam), kwa vile ndani ya yake kuna ukweli kidogo sana, ndani yake kimejaa upotoshaji na uongo dhahiri dhidi ya Uislamu.

Kwa upande wa filamu kuna "Black Sunday" (Jumapili Nyeusi) ambapo "Magaidi" wa kipalestina wanapanga njama za kuwaangamiza wale wote wanaohudhuria "Superbowl" (mashindano ya mwaka ya mpira wa miguu). Nyingine ni "Not Without My Daughter" (Si Bila Binti wangu ), filamu ambayo ianonyesha picha ya kutisha juu ya mahusiano ndani ya familia za Kiislamu.

Mambo na imani mbalimbali za uongo zinazodaiwa kuwa ni za Kiislamu zinapewa nguvu na kendelezwa kwa kutumia mbinu kama hizi. Uislamu una wakati mgumu kwani hautaonekana isipokuwa kwa dhana mbaya na ya uadui.

Sisi kama Waislamu, lazima tuwe thabiti pindi tunaposhambuliwa katika imani yetu - - ikiwa ni kwa "njia ya upendo" au uadui dhahiri. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia katika Quran tukufu.

"Mtapata misukosuko katika mali zenu na nafsi zenu, na mtasikia udhia mwingi kwa wale wwaliopewa kitabu kabla yenu, na kwa wale walioshirikisha. Na kama mkisubiri na kujilinda na aliyoyakataza Mwenyezi Mungu (mtakuwa mmefanya jambo) zuri; kwani mambo haya ni mambo makubwa ya mtu kuazimia kuyafanya". (Quran 3:186)