rudi maktaba >Akida >Yaliyomo >

UCHUNGUZI JUU YA MISINGI, MAFUNDISHO NA IMANI ZA KIKRISTO

Wayahudi walifanikiwa kuyazimisha mafundisho ya Yesu; lakini si Wayahudi tu bali hata dini ya Ukristo tuliyo nayo leo ambayo mafundisho na imani zake zote muhimu zimeanzishwa na Paulo pia imeyafutilia mbali mafundisho na imani zote zilizofundishwa na Yesu. Licha ya hoja zozote zinazoweza kutolewa na mkristo, hatuwezi kupata ushahidi wowote ambapo Yesu amethibitisha au kazitaja imani hizi nne (uungu wa Yesu, Utatu Mtakatifu, kufa kwa Yesu kwa ajili ya dhambi za wanadamu, na uokovu kwa imani peke yake) katika Injili. Maadamu Yesu hakuwa na mpango wa kuanzisha dini mpya, basi bila ya chembe ya shaka ni wazi kwamba pia hakuunda au kuanzisha misingi au imani zozote za dini, kwani kama angekuwa na nia ya kuanzisha dini mpya basi angelazimika pia kuanzisha imani na misingi mipya ya dini. Lakini maadamu hakuanzisha wala hakuwa na nia ya kuanzisha dini yoyote mpya basi pia hakuna imani yoyote mpya ya dini aliyoianzisha.

Imani, misingi na mafundisho yote ya Ukristo ni kazi ya Paulo ambayo aliifanya kwa shabaha ya kuungwa mkono na kukubalika kwa wafuasi wapya miongoni mwa ambao hawakuwa Wayahudi wa zama zake. Kwa kuingiza na kuchanganya imani za kipagani katika mafundisho ya Yesu, Paulo alipata mafanikio makubwa mno katika kazi yake lakini kwa kufanya hivi aliharibu na kuivunjilia mbali imani ya kuamini Mwenyezi Mungu mmoja asiye kuwa na mshirika. Kwa kufanya hivi Paulo alifanikiwa kuyapotosha kabisa mafundisho yote ya Yesu na badala yake akaanzisha maradhi mabaya na yaliyoenea kwa haraka aliyotatoa katika upagani - ambapo imani hizi bado tunazo mpaka leo katika ukristo. Ni hapa kwenye kiini na kitovu cha mafundisho ya Yesu palipotoshwa na hii ndio sababu kuu ya tofauti za msingi kati ya Uislamu na Ukristo.

Inafurahisha kuona kwamba "imani na misingi ya Ukristo" ambayo Quran inaikubali inaweza pia kuthibitishwa kwa urahisi kabisa, kuwa ni sehemu ya mafundisho ya wanafunzi wa mwanzo kabisa wa Bwana Yesu, ambapo imani na misingi ambayo Quran inaikataa inaweza kuthibitishwa kuwa ni maongezo (nyongeza) yaliyoongezwa na viongozi wa juu wa kanisa au Paulo. Waliyaongeza haya kwa sababu walipendezwa na falsafa na mifumo ya dini za Wapagani wa Kigiriki na wa Kirumi".[15]