Hadithi kutoka Qur’an
: Hadithi no.2

 

                                                   WATU WA RAS

 

Makala haya yametarjumiwa na:

Amiraly M.H.Datoo   Bukoba - Tanzania  

E-mail : datooam@hotmail.com  

 

Allah swt anatuambia katika Qur’an Tukufu Sura al-Qaaf, 50, Ayah: 12 - 14

Walikadhibisha kabla yao watu wa Nuhu na wakazi wa Rass na Thamudi.

Na Adi na Fir’auni na watu wa Luti.

 

Na wakazi wa kichakani, ( watu wa Nabii Shuaibu ) na watu wa Tubba ( Yemen ).Wote walikadhibisha Mitume; kwa hivyo onyo langu likathubutika ( juu yao ).

 

Watu wa Ras walikuwa ni wale watu ambao walikuwa wakiishi ukingoni mwa mto uliokuwa ukiitwa Ras. Wao waliishi katika zama za baada ya Mtume Suleyman a.s. mwana wa Mtume Da’ud a.s.

 

Mto Ras ulikuwa ni mto mkubwa na watu  waliitumia ardhi iliyoizunguka katika kilimo. Wao walikuwa wakiishi maisha ya raha na mustarehe na walitosheka na mahitajio ya maisha, vyakula kwa wingi, maji matamu kwa ajili ya kunywa, miti ilijaa kwa matunda, hali ya hewa ilikuwa nzuri, ardhi nzuri na yenye mandhari nzuri ya kuvutia.  Ukingoni mwa mto huo kulikuwa na mti mmoja mkubwa na mrefu kabisa kiasi kwamba unaweza kudhani kuwa ulikuwa ukigusa mawingu, uliota kwa sababu ya hali nzuri ya hewa, ukiitwa msonobari.  Hatimaye Shaitani alifanikiwa kuwapotosha watu hao kuuabudu mti huo kwani ulikuwa wa aina yake pekee wakati huo. Masikini watu waliingia katika mtego huo wa Shaytani na wakaanza kuabudu mti huo kama ndio mungu wao. Watu walianza kuchukua matawi yake na kwenda kupanda sehemu zao kila mahala na kuanza kuabudu baada ya kukua katika miti kamili. Imani za watu ziliendelea kuwa madhubuti katika mti huu kiasi kwamba ukafika wakati ambapo hawakuwa na imani hata kidogo juu ya Allah swt. Wao walikuwa wakifanya sujuda mbele ya mti huo na walikuwa wakitoa dhabihu hapo. Ujahili na upagani wao huo kiasi kwamba wakafika wakati ambapo wao walijifanyia maji ya mto huo kuwa haramu kwa ajili yao na wengine wote na badala yake wakawa wanatumia maji kutokea sehemu zinginezo kama mito na chemichemi. Wao walikuwa wakidhani kuwa maisha ya mungu wao huyo, yalikuwa yameunganika na mto Ras na hivyo hakuna mtu yeyote aruhusiwaye kuyatumia maji hayo. Na kama ilitokea kuwa kuna mtu au mnyama yeyote aliyekunywa maji ya mto huo, basi wao walimwua kwa kitali kabisa.

 

Watu hawa walikuwa wakisherehekea siku moja katika mwaka kama ndiyo siku yao tukufu. Wao walikuwa wakikusanyika karibu na chini ya mti huo huku wakitoa sadaqa zao za wanyama na baadaye kuichoma moto nyama yao.  Wakati moshi ulipokuwa ukipaa juu hadi kufikia mawinguni, wao walikuwa wakijiangusha chini kusujudu hapo mtini na walikuwa wakisoma ibada zao kwa sauti. Kwa kuyaona hayo, Shaytani alifurahishwa mno kwani alishuhudia ufanisi wake katika kuwapotosha hawa majaheli kwa kuwazuzua kuuabudu msonobari. Yeye alikuwa daima akiwazuzua kwa kila njia ili mradi watu hao wasirejee katika kumwabudu Allah swt .

 

Ikapita miaka huku watu wa Ras wakiendelea na kuabudu msonobari huo.  Hatimaye Allah swt alimtuma Mtume wake kuja kuwaongoza katika njia ya Allah swt na hivyo kuwaokoa. Mtume huyu alitokana na kizazi cha Mtume Ya’qub a.s. na kama Mitume a.s. yote iliyokuwa imetumwa sehemu zote, naye pia alianza kazi zake za tabligh  na kuwaita watu katika njia ya Allah swt. Ili wafanye ibada ya Allah swt tu na wala si mwingine hata mti huo wa msonobari. Lakini watu hao walitupilia mbali maneno ya Mtume huyo na waliendelea kuuabudu msonobari huo. Ikatokea kuwa siku yao ya maadhimisho ikawadia na Mtume huyo akashuhudia vile watu wao walivyokuwa wamejiandaa kwa matayarisho kamambe kwa ajili ya sikukuu yao hiyo ambayo ilisherehekewa na watu wote.

 

Wakati Mtume huyo alipoyaona mambo hayo ya ujahili, alimwomba Allah swt aukaushe kamili mti huo ili watu hao waweze kuzinduka kutoka ndoto yao hiyo kuwa mti huo haustahili kuabudiwa.

 

Kwa hakika dua ya Mtume huyo ikakubaliwa na msonobari huo ukakauka kabisa kwa ghafla, na majani yake yote yakanyauka na kuanza kudondoka ardhini. Lakini watu badala ya kujipatia funzo kutokana na tukio hilo, wao waliukaribia zaidi mti huo na kudhani kuwa Mtume huyo kwa uchawi wake ameudhuru mti wao.  Wengi wao walisema kuwa Mtume huyo alikuwa ameudharau na kuukashifu mti huo hivyo kuingiwa na hasira, mti huo umebadilisha hali yake. Hivyo Mtume huyo lazima auawe kikatili kabisa ili mti huo ukifurahi uweze kurudia hali yake ya kawaida. Na hivyo mungu wao huyo (msonobari) utawawia radhi tena.

 

Kulibuniwa njama za kutaka kumwua Mtume huyo. Wao walichimba shimo kubwa mno na kumtupa Mtume huyo humo huku wakiufunika mdomo wa shimo hilo kwa jiwe kubwa. Kwa muda fulani kulikuwa kukisikika sauti za mlio wa Mtume huyo kutokea shimoni, na hatimaye sauuti hiyo haikusika kamwe kwani Mtume huyo alikuwa amejitolea mhanga kwa ajili ya kutaka kuwanusuru watu wasipotee wasiangamie katika adhabu za Allah swt.  Kwa matokeo ni kwamba Allah swt alikasirishwa mno na kulianza kutokezea dalili za adhabu za Allah swt.  Kulitokea kimbunga chekundu cha upepo ambacho kiliwateketeza watu wote. Kulitokezea na wingu jeusi kabisa ambalo lilifunika eneo zima kuwa kiza tupu. Hivyo watu wa Ras wamekuwa ni funzo la kujifunza kwa vizazi vilivyofuatia.


 

The .HTML version of this book is taken from
www.al-islam.org and ebooked by www.ShiaLibrary.com and www.islamkutuphanesi.com . May Allah be pleased with all.