Ulul Amr Ni Nani

Kimeandikwa na : Sayyid Saeed Akhtar Rizvi

Kimetafsiriwa na : Maalim Dhikiri Omari Kiondo

UTANGULIZI

Waislamu wamegawanyika makundi wawili kuhusu maana ya maneno "Ulul-Amr" yaliyotumika katika Aya ya 59 ya Surat An-Nisa.

Wako wasemao kuwa maana ya maneno haya ni "Watawala kutoka miongoni mwenu" - yaani watawala wa Kiislamu; na hii ndio tafsiri ifuatwayo na Waislamu walio wengi (Masunni).

Wako wengine wasemao kuwa, maana ya maneno hayo ni "Makhalifa (au Maimamu) Maasumiin (Watakatifu) Walioteuliwa na Allah kushika mahali pa Mtukufu Mtume [s] baada ya yeye Mtume [s] kuondoka. Hii ndio tafsiri ifuatwayo na Mashia-lthna-ashariyah.

Kutoafikiana huku ni tatizo lihitajilo kutatuliwa kwa njia fulani. Kwa vile msingi mkuu wa Uislamu ni kutumia akili, inatuIazimu kuutumia, msingi huu huu katika suala hili.

Maneno yafuatayo ni maelezo ya Ndugu yetu Sayyid Saeed Akhtar Rizvi aliye Mhubiri Mkuu wa Misheni yetu, akijaribu kulitatua tatizo hili kwa njia hii ya kutumia akili na kwa kuzichunguza aya nyingine za Qur'ani. Tunategemea kuwa, lnsha-Allah wewe msomaji wetu nawe utafaidika kutokana na kijitabu hiki.

Mwisho tunamwomba Allah Atujaalie Tawfiq katika kuyasoma maneno Yake na kupatamaana yake halisi itakayotuongozea kwenye Mwongozo wake halisi - Amin.