JIBU LA JIBU

BISMILLAHIR-RAHMANIR-RAHIM

MAJIBU YA MAKALA IITWAYO JIBU LA JIBU ILIYOANDIKWA NA AL-TARKIZOUN WA S.L.P.19650 DER ES SALAAM 

Hivi karibuni tumepokea makala inayoitwa "JIBU LA JIBU" iliyoandikwa na jamaa waliojitambulisha kwa Anuani ya "Al-TARKIZOUN"

Madhumuni ya jamaa hawa ndani ya makala yao, ni kukijibu kijitabu kiitwacho "JIBU" (kama walivyoandika wao) ambacho ndani yake imo barua ya Al-marhuum Shekh Abdallah Saleh Fars kwenda kwa Al-marhum Imam Muhammad Hussein Kaadhiful-Ghitaa wa Najaf Iraq.

Ndani ya barua hiyo Shekh Abdallah Saleh Fars alimuuliza Imam Muhammad Hussein Kaashiful-Ghitaa iwapo ni kweli Mashia Ithnasharia wanaamini kwamba, Masahaba waliobashiriwa Pepo wakiwemo Abubakar, Umar na Uthman (R.A) ni watu wa motoni?

Zaidi ya hapo, Shekh Saleh Fars alisema kuwa "Yeye ameelezwa na Mashia kwamba, wao wanawalaani Masahaba wengi" Ndipo alipouliza kwa kusema, "Hivyo ndivyo inavyostahiki kuwafanyia masahaba wetu?"

Isitoshe Shekh Abdallah Saleh Farsi katika suali lake alinukuu aya kadhaa za Qur'ani Tukufu zinazo ashiria ubora wa Masahaba ikiwemo kutangulia kwao katika Uislaam, Qur'ani 9: 100, kufungamana kwao na Mtume (s.a.w) chini ya miti (siku ya sul-hu ya Hudaibiyyah) Qur'ani 48: 18, na nyingine inayoelekeza wanachotakiwa wakifanye watakaokuja baada ya Mtume (s.a.w) na Masahaba (r.a) Qur'ani 59:10

Mwisho Shekh Abdallah S. Faris alimtaka Imam Kaashiful-ghitaa asimfanyie ubakhili katikakumjibu na akamuonya kwa aya inayowalaani wanaoficha yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu ambazo ni hoja zilizowazi……. Qur'ani 2: 159.

Amma Imam Muhammad Hussein Kaashiful-Ghitaa jawabu lake lilianza kwa kumuelewesha Shekh Abdallah Saleh Fars kwamba, " Mashia Ithnasharia wenye akili na wenye adabu, si watu wenye kulaani wala kutukana, kwa kuwa mafunzo ya Maimamu wetu wa nyumba ya Mtume (s.a.w) wamewakataza kufanya hivyo"

Imam Muhammad Hussein Kaashiful-Ghitaa aliendelea kusema, "Sisi hatuwalaani Makhalifa waongofu na Masahaba walioridhiwa ambao Mwenyezi Mungu amewaridhia nao wakawaradhi naye"

Zaidi ya hapo Imam Muhammad Hussein kaashiful-Ghitaa  alimtanabahisha Shekh Abdallah Saleh Farsi kuwa, " Kwa hakika si Masahaba wote waliosuhubiana na Mtume (s.a.w) miongoni mwa Muhajirina waliohama pamoja naye na Answari waliomnusuru, wameridhiwa na wamejumuishwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo, " Mwenyezi Mungu ameridhika nao, nao wameridhika naye" Qur'ani 9: 100. Wala si Masahaba wote wanaoingia katika "Ndugu zetu waliotutangulia" Qur'ani 59:10

Imam Muhammad Hussein Kaashiful-Ghitaa katika kueleza msimamo wake juu ya hili alisema, (Qur'ani inajifasiri yenyewe kwa yenyewe na hujifafanua yenyewe kwa yenyewe, hivyo inalazimika kuziunganisha baadhi ya aya nyinginezo ili ukweli uweze kudhihirika ukiwa mweupe wenye kung'ara."

Ili kuonyesha kwamba Qur'ani inajifasiri na kujifafanua yenyewe kwa yenyewe, Imam alinukuu aya ya 144 sura ya Al-imaran inayoeleza kuhusu badhi ya Masahaba  " Kurudi nyuma kwa visigino vyao" Si hivyo tu bali Imam Muhammad Hussein Kaashiful-ghitaa kabla ya kunukuu aya hiyo aliuliza kwa kusema "Kama Masahaba wote wangekuwa ni wenye kuridhiwa kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye, basi maneno haya ya Mwenyezi Mungu yatakuwa na maana gani? Yaani aya ya 144 sura 3.

Kwa kumuongezea faida muulizaji na kumuwekea mambo wazi Imam alisema " Kama ilivyo Qur'an Tukufu inajifasiri yenyewe kwa yenyewe, hivyo hivyo sunna za Mtume na Hadithi zinaifasiri Qur'an Tukufu na kuifafanua".

Baada ya maneno haya, alinukuu Hadithi za Mtume (s.a.w) zinazoifafanua aya ya 144 katika sura ya 3, na hapa tunanukuu Hadithi moja tu kama mfano.

Amesema Mtume (s.a.w) "Mimi nitakutangulieni kufika kwenye hodhi (Birika la maji) na wanaume miongoni mwenu watanikimbilia lakini watazuwiwa (wasinifikie), nitasema Ewe Mwenyezi Mungu! (hao ni) Masahaba wangu! Patasemwa, hakika wewe hujui waliyoyazusha baada yako, basi itatolewa amri waingizwe motoni. Nami nitasema maangamio, maangamio ni kwa wale walioyageuza na kuyabadilisha mafunzo ya Uislaam baada yangu"

Rejea

(1) Fat-hulbari Shar-h ya Bukhari kitabur-riqaq Babul-Haudh.

(2)Sahihi Muslim, Kitabul-Fadhail Babu Haudhi Nabiyina Waasifatihi.

Humo utakuta Hadithi nyingi zenye maana kama hiyo iliyotangulia hapo juu.

Alipokwishakunukuu Hadithi za Mtume (s.a.w) kama ile tuliyoitaja hapo kabla, Imam aliyarejea baadhi ya matukio yaliyomo ndani ya historia ya kiislaam na miongoni mwake ni ile ya watu wa Madina wakiwemo baadhi ya Masahaba kumuua Sayyidina Uthman Ibn Affan (r.a) kifo kibaya, wakati katika Hadithi mashuhuri Mtume (s.a.w) amesema, " Si halali kumuua Mwislaam ila kwa moja kati ya mambo matatu:

1.Kuritadi kwenye imani

2. Zinaa katika ndoa

3. Kisasi kwa kuua nafsi iliyoharamishwa kuuawa"

Imam Muhammad Hussein Kaashiful-ghitaa alimaliza kifungu hiki kwa kusema, "Mimi sijui ni lipi mojawapo kati ya hayo matatu walilohalalishia tendo la kumuua Khalifa, na labda watu wa Madina ndio wajuzi wa hayo!!

Mwisho, Imam Muhammad Hussein Kaashiful-Ghitaa alionesha masikitiko yake kutokana na kuulizwa mambo yanayoeneza chuki miongoni mwa Waislaam, lakini alilazimika kujibu kwa sababu Shekh Abdallah Saleh Fars alisisitiza apewe jawabu la suala lake kwa kumbana Imam na kumtishia kwa aya ya Qur'an Tukufu isemayo, "Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha nazo ni hoja zetu zilizowazi na uongozi baada ya sisi kuzibainisha kwa watu kitabuni, hao anawalaani Mwenyezi Mungu na wanawalaani (kila) wenye kulaani".

Baada ya mukhtasari huu ambao tumeuleta ili kutoa mwanga kuhusu kijitabu hicho, sasa hebu na tuirudie makala ya ndugu zetu wa Al-Tarkizoun.

Kwanza: Tunapenda kuwafahamisheni kwamba, kijitabu hicho hakiitwi “Jibu” bali kinaitwa “Swali la Shekh Abdallah Saleh Fars wa Zanzibar na jibu la Imam Muhammad Husain Kashiful-Ghitaa wa Najaf.”  Isitoshe Shekh Ramadhani Idris Kwezi siyo mtunzi, bali yeye amefanya Tarjuma (amefasiri) tu kama inavyoonyesha ndani ya kijitabu chenyewe.

Pili: Al-Tarkizoun mmeonyesha wasiwasi juu ya kuwepo kwa mawasiliano baina ya Shekh Abdallah Saleh Fars na Imam Muhammad Husain Kashiful-Ghitaa.

Ili kuonyesha kwamba, mawasiliano haya yalifanyika, tunaambatanisha kivuli cha swali na jibu baina ya wanachuoni hawa wawili kama tulivyokipata kutoka ndani ya kitabu kiitwacho “Jannatul-Maawa” ambacho ndani yake umo mkusanyiko wa barua ambazo Imam Muhammad Husain Kashiful-Ghitaa aliandikiana na wanachuoni mbali mbali akiwemo Shekh Abdallah Saleh Fars.

Tatu: Al-Tarkizoun katika makala yanu mmesema kuwa, “kama ni kweli mawasiliano haya yalitendeka ya Shekh Fars na Imam Kaashiful-Ghitaa, basi ni lazima kabisa kuwa baada ya kupata maelezo au jibu alilojibiwa na Imam Kashiful-Ghitaa basi ni lazima kuna jibu pia alilojibu Shekh huyu maarufu.”

Sisi tunasema, “Ni kweli Shekh Abdallah Saleh Fars ni Shekh maarufu lakini kujibu au kutojibu hilo halituhusu, bali atakaye na afuatilie, pia yawezekana Shekh Abdallah Saleh Fars alikinaika na jibu alilopewa na mwanachuoni mwenziwe, hivyo akaamua kunyamaza.

Nne: Kutokana na kutopatikana jibu la Shekh Abdallah Saleh Fars, Al-Tarkizoun mnasema, “Sisi tunachukua fursa hii kujibu” Na mmenukuu baadhi ya maelezo ya jawabu la imam Muhammad Husain Kashiful-Ghitaa khususan aya 144 sura ya tatu ndiyo mliyoishughulikia, na tunainukuu:-

“Na hakuwa Muhammad ila Mtume tu, wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa), akifa au akiuwawa ndiyo mtarudi nyuma kwa visigino vyenu (muwe makafiri kama zamani)?

Mlipokwisha nukuu aya hii, Al-Tarkizoun mmeelekeza shutma zenu kwa Imam Kaashiful-Ghitaa au Shekh Kwezi kuwa wawili hawa wamegeuza, wamepindua, wameongeza na kuyapuuza maneno matukufu (ya Mwenyezi Mungu) na kwamba aya hii siyo mahali pake (kuweza kujibu masuali ya Shekh Fars) kwa sababu tatu za wazi kabisa kama ifuatavyo:-

Sababu yenu ya kwanza: “Wamepita kabla yake Mitume wengi kabisa” Mnasema, “ Tunaamini kuwa katika Qur’an kila kitu kimewekwa kwa mpangilio na sababu maalum, hapa kufuatana na hoja yenyewe ya Shekh Fars ni jibu la Imam Ghitaa, utaona wazi kuwa Aya hii haikubaliani”. Mwisho wa kunukuu.

Sisi tunasema kuwa, “Hatuelewi makusudio yenu ndani ya kifungu hiki cha kwanza, lakini mnaposema kuwa aya hii haikubaliani si kweli, bali mumeshindwa kulifahamu suali na jawabu lake, kwani suali la msingi la Shekh Abdallah Saleh Fars ni kutaka kujua iwapo ni kweli Mashia Ithnasharia wanaamini kwamba Masahaba kumi waliobashiriwa Pepo wakiwemo Abubakar, Omar na Uthman (r.a) ni watu wa motoni? Na vilevile (kama) Mashia hao wanawalaani Masahaba wengi badala ya kuwaombea rehma”

Jibu la Imam kwa ufupi alisema kwamba, “Sisi (Mashia Ithnasharia) hatuwalaani Makhalifa waongofu na Masahaba walioridhiwa,” kwa ziyada rejea mukhtasari wa jibu hilo ndani ya makala hii au kijitabu chenyewe ambacho utakipata kupitia anuani tutakayoitaja baadye.

Amma sababu za Imam kuileta aya hii ndani ya mtiririko wa jawabu lake, ni kwa lengo la kuzifafanua aya alizozileta Shekh Fars katika suali lake, aya ambazo zinaonyesha kuwa Masahaba wote wameridhiwa na Mwenyezi Mungu. Hivyo basi aya hii ilikuja kufafanua kwamba, “Si Masahaba wote wameridhiwa” kwa kuwa baadhi yao watarudi nyuma kwa visigino vyao.

Maelezo zaidi kuhusu aya hii ya kurudi nyuma yatafuata baadaye inshaalaah.

Sababu yenu ya Pili” “Akifa au Aakiuawa” Al-Tarkizoun mnasema, “Hapa haingii akilini, sababu Muhammad (s.a.w) hakuuawa maishani mwake” Mwisho wa kunukuu.

Sisi tunasema,

(A) “Kisichoingia akilini ni haya maelezo yenu, kwani maneno “Akifa au akiuawa” siyo ufafanuzi uliofanywa na Imam Kashiful-Ghitaa wala Shekh Kwezi, bali hivyo ndivyo aya ilivyoshuka, na ikibidi mjadala kuhusu maneno hayo, basi kama munaweza adilianeni na Mwenyezi Mungu yeye ndiye aliyesema “Akifa au akiuawa” kisha Muhammad (s.a.w) akafa na hakuuawa maishani mwake”

(B) Yaonesha wazi hamuelewi matumizi ya neno “au” lililotumika ndani ya aya hiyo, ndiyo maana mmekanganyikiwa na hatimaye mkahukumu kuwa “Haingii akilini”!.

Kwa faida yenu na wasomaji, hapa chini tunabainisha kwa mukhtasari maana na matumizi ya “Au” ili kuitakasa Qur’an.

Neno Au lina maana nyingi, lakini sisi tunataja mbili tu ili tuweze kuipata maana ya Au iliyotumika katika aya hiyo ya 144 sura ya 3.

(1) Au humaanisha “Ibaha”

(2) Au humaanisha “Takhyir”

Mfano wa “Au” ya Ibaha ni kama huu:- “Kaa na Sefu au Rashid”

Na mfano wa “Au” ya Takhyir ni huu:- “Muoe mwanaidi au dada yake”

Tofauti iliyopo baina ya Au ya Ibaha na ile ya Takhyir ni kwamba, katika Au ya Ibaha upo uwezekano wa kukichanganya kilichopo kabla ya Au na kile kilicho baada yake, kwa maana unaweza ukakaa na Sefu na Rashidi kwa pamoja bila kuwa na kizuwizi. Amma Au ya “Takhyir” haikubali kukichanganya kile kilichopo kabla ya Au na kile kinachokuja baada ya Au.

Je hamuoni kwamba haijuzu kumuoa mwanaidi ikiwa dada yake tayari yumo nyumbani mwako akiwa ni mkeo?

Taz: Qut-run-nada uk 305 chapa ya kumi na moja ya mwaka 1963 kilichochapishwa Misri.

Kutokana na mifano hiyo miwili tunakuta kwamba “Au” iliyotumika ndani ya aya 144 sura ya 3 ni Au ya Takhyir, kwani akifa basi hakuna kuuawa na iwapo atauawa basi hakuna kufa.

Ni vema pia ifahamike kwamba, Mwenyezi Mungu aliposema akifa au akiuawa haimaanishi alikuwa anababaika hajui ni kipi kitatokea, bali alikuwa akielezea uwezokano wa kutokea kwa mauti ya Mtume (s.a.w) kupitia moja kati ya njia hizi mbili, na hilo halina maana eti Mwenyezi Mungu hafahamu ni lipi litakalotokea.

Sababu yenu ya tatu: “Muwe makafiri kama zamani”? Al-Tarkizoun mnasema hii ni nyongeza aliyoipachika Imam Ghitaa au Shekh Kwezi, na nia hapa  ni kutaka kukuongoza kungine nje ya ukweli.” Mwisho wa kunukuu.

Majibu yetu:

Mnashangaza sana mnaposema kuwa maneno, “Muwe makafiri kama zamani” ni nyongeza iliyoongezwa na Imam Kashiful-Ghitaa au Shekh Kwezi, ukweli ulivyo ni kwamba hivi ndivyo walivyofasiri wafasiri wengi wa Qur’an walipokuwa wanafafanua maana ya Aya inaposema “Mtarudi nyuma kwa visigino vyenu”

Taz:

(1) Tafsirul-kabir ya Fakhru-Razi, katika maelezo ya aya 144 sura ya 3 amesema “Mtarudi nyuma kwa visigino vyenu, maana yake mtakuwa makafiri baada ya kuamini.”

(2) Ad-Durrul-Manthoor ya Imam Suyuti, ameandika kuhusu aya hii, “Mtaritadi muwe makafiri baada ya kuamini” juz 2 uk. 335 chapa ya Beirut ya mwaka 1414 A.H. 1993 A.D.

(3) Ay-sarut-Tafsir ya Abubakri Al-jazairi juz 1 uk. 321 ameandika “ Mtatoka muwe makafiri baada ya kuamini”.

(4) Tafsiri ya Shekh Abdallah Saleh Fars chapa ya 1974 na 1984 ameandika “Muwe makafiri kama zamani”

Pia wafasiri wengi wengine wameandika hivyo hivyo.

Ikiwa ninyi Al-Tarkizoun mnadai kuwa “Shekh Kwezi na Imam Kashiful-Ghitaa nia yao hapa ilikuwa ni kutaka kutuongoza kwingine nje ya ukweli”, sasa mnatuambia nini juu ya wanachuoni hawa wakongwe (akiwemo Shekh Abdallah Saleh Fars) ambao nao wamefanya hivyohivyo. Je hawa nao nia yao hapa ilikuwa ni kutaka kutuongoza kungine nje ya ukweli?

Au kosa la Shekh Kwezi na Imam Kaashiful-Ghitaa ni kwa sababu wao ni Mashia?

Ndani ya makala yenu Al-Tarkizoun mmeendelea kuwatuhumu Shekh Kwezi na Imam Kashiful-Ghitaa kwamba wanajaribu kupotosha.

Mnasema “Na pia utaona kuwa, “Mtarudi kuwa makafiri” ndiyo ongezeko lake Imam au mtunzi, lakini kaweka mabano kwenye “kwa visigino vyenu” kitu ambacho kimo kwenye aya hii, ilipaswa mabano yawe kwenye “Mtarudi kuwa makafiri” maana ni ongezeko aliloliongeza Imam au Mtunzi, yote ni kujaribu kupotosha. Tunashindwa kufahamu sababu za mtu kufanya hivyo, jibu tunalolipata ni kwamba huo ni udhaifu wa imani, udhaifu wa kufikiri au ni udhaifu wa kushindwa kuzuwia tamaa binafsi” Mwisho wa kunukuu.

Sisi tunasema, “Kuhusu mabano kwenye “Kwa visigino vyenu” badala ya mtarudi kuwa makafiri” hilo ni kosa la uandishi au uchapaji na linaweza kumtokea yeyote yule awe Shia au Sunni.

Hivyo basi ikiwa ninyi mmewatuhumu Shekh Kwezi na Imam Kashiful-Ghitaa kwa kuwaambia kuwa wamefanya hivyo kwa ajili ya kutaka kupotosha, na kwamba huo ni udhaifu wa imani, udhaifu wa kufikiri au ni udhaifu wa kushindwa kuzuwia tamaa binafsi” Je mtasema nini kuhusu Shekh Abdallah Saleh Fars ambaye naye kafanya hivyo hivyo? Je alitaka kupotosha, ni mdhaifu wa imani au mdhaifu wa kufikiri na alishindwa kuzuwia tamaa binafsi? Twambieni……….!!

Kwa uthibitisho wa hili taz:

Tafsiri ya Shekh Abdallah Saleh Fars chapa 1974 na 1984.

Hatimaye Al-Tarkizoun ndani ya makala yenu mumeeleza kuwa “Ili kutoa jibu sahihi inabidi uchunguzi wa kina na si kujibu kitu mradi akili imekutuma kufanya hivyo tu” Na uchunguzi wa kina mlioufanya ni kurejea “Saf-wat tafasiri” ambapo mmegundua sababu ya kushuka kwa aya 144 sura ya 3 na mkasema:- “Aya hii iliteremshwa baada ya mtafaruku uliotokea kati ya Masahaba kwa kujeruhiwa Mtume (s.a.w) katika vita vya Uhud. Ikatokea mnong’ono kuwa Mtume ameuawa. Baadhi yao wakasema, kuwa Mtume amekufa, wakaacha kupigana huku wakisema kuwa Mtume amekufa hakuna haja ya kupigana” Mwisho wa kunukuu.

Sisi tunasema:- Tunashangazwa na uchunguzi wa kina mnaodai mmeufanya, kwani maelezo mliyoyapata ndani ya Safwat-Tafasiri ni sehemu tu ya mazingira yaliyotokea hapo Uhud, lakini wafasiri wa kutegemewa waliofasiri Qur’an pia wanahistoria wamelieleza tukio hilo zaidi kama ifuatavyo:-

Masahaba siyo tu waliacha kupigana, bali wengi walikimbia wakarudi Madina na wengine wakapanda mlimani, hawakubaki pamoja na Mtume (s.s.w) isipokuwa watu 12 (kumi na wawili) tu.

Taz:

(1) Fi Dhilal-Qur-an tafsiri ya Sayyid Qutb chini ya aya 144 sura 3

(2) Al-Muntadhim, Tarikh Al-Muluk Wal-umam cha Abul-Faraj Abdur-Rahman Ibn Ali Muhammad Al-Jauzi juz 3 angalia mlango wa vita vya Uhud. Na wengine wengi.

Kwa ajili hii Imam Muhammad Husain Kashiful-Ghitaa ameitaja aya hiyo ya 144 sura ya 3 katika majibu yake kwa Shekh Abdallah Saleh Fars ili kumuonyesha kuwa siyo Masahaba wote walioridhiwa na wala sio wote wanaoingia katika ndugu zetu waliotutangulia, kwani Qur’an inajifasiri yenyewe kwa yenyewe kutoa msimamo wa Qadhia husika kama ilivyo hapo juu.

Amma maelezo yenu yasemayo kuwa, “Sayyidna Umar aliposimama na kusema kuwa, nitamkata kichwa mtu yeyote atakayesema kuwa Mtume amekufa….. wasiwasi wake Sayyidina Umar alikuwa kuwa watu wenye imani ndogo wanaweza kuanza kugeuka baada ya Mtume kufa”  Mwisho wa kunukuu.

Sisi tunauliza:-

(A) Je hao aliowatilia wasiwasi Sayyidina Umar hawakuwa Masahaba?

(B) Na kama ni Masahaba, basi wangeanza kugeuka kutoka wapi na kuelekea wapi?

(c) Je hamuoni kwamba kwa kifungu hicho cha wasiwasi wa Sayyidina Omar tayari mumekwisha kubali ile tafsiri ya “Mtarudi nyuma muwe makafiri kama zamani?”

(D) Je nanyi mnataka kutuongoza kungine nje ya ukweli?

Twambieni…………….!!

Katika makala yenu Al-Tarkizoun mmechanganya mambo mengi, ikiwemo suala la Sayyidina Abubakar (r.a.) kusalisha wakati Mtume (s.a.w.) anaumwa na pia suala la kusilimu Sayyidina Umar (r.a.) kwamba kulisababisha mambo mengi ya Waislaamu yawe rahisi.

Kwa kuwa yote haya hayakuzungumzwa ndani ya kijitabu mlichokuwa mnakijibu, sisi hatuoni sababu ya kuyaunganisha humu, bali ikibidi kuyashughulikia tutayashughulikia inashaallah.

Mwisho wa makala yenu mmetaka kuthibitishiwa juu ya uhalali wa Imam Ali Ibn Abi Talib (a.s) kuwa ndiyo Khalifa wa Kwanza.

Hili nalo tunasema, “Kwetu sisi Shia Ithnasharia ni jambo la wajibu kulifanya na Inshaallah tutalifanya kwa nia njema”.

Was-salaam

KAMATI YA UANDISHI 

MASJID AMIRUL-MOMININ ALI (A.S)

MAGOMENI MAPIPA

KISIJU STREET

DAR ES SALAAM.

Ili kupata nakala ya kijitabu chenyewe wasiliana na wachapishaji kwa anwani ifuatayo:-

Bilal Muslim Mission of Tanzani

p.o.Box 20033

Dar-es-Salaam