USAMEHEVU KATIKA ISLAM

  

 

                   Kimekusanywa na kutarjumiwa na:

                          AMIRALY  M.  H.  DATOO

                                   BUKOBA - TANZANIA


                             MANENO MAWILI ….

 

Namshukuru Allah swt pamoja na Mtume Muhammad s.a.w.w. na Aimma Tahirin a.s. kwa kunijaalia  katika kukitarjumu kijitabu hiki.

 

Kijitabu hiki ambacho kiko mikononi mwako nimekitayarisha katika muda wa takriban siku 11 na ni kitabu cha tatu katika mfululizo kama huo. Cha kwanza kilikuwa juu ya uharamisho wa kamari  na cha pili ni  uharamisho wa ulevi katika Islam. Na Insha…. Vitafuatia vinginevyo moja baada ya kingine kama uharamisho wa uongo n.k. na vile vile ninakitayarisha kijitabu juu ya uharamisha wa ulawiti katika Islam.

 

Ni matumaini yangu kuwa maudhui kama haya yatatusaidia sisi sote tuweze kuyarekebisha maisha yetu na tujirudi katika Dini na kujaribu kufuata njia iliyonyooka na wala si ya wale walioghadhibikiwa na Allah swt.

 

Ndugu msomaji, iwapo utapenda kusoma vitabu na makala  mbalimbali za Kiislam katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza basi unaweza kufaidika kwa hazina iliyopo hapo katika mtandao wa komyuta yaani internet kwa anwani ifuatayo:  http://www.islam.org/kiswahili

 

Mshukrani wenu, iwapo kuwa maoni yoyote musisite kuniandikia:

 

Amiraly M.H.Datoo    23rd  April 2001 ( 28th Muharram 1422 )

P.O.Box 838,

BUKOBA

Tanzania  (E.Africa)

 

e-mail: datooam@hotmail.com

 

 


Hoja mojawapo iliyo ya muhimu na yenye maana sana katika Islam ni kwamba katika mafundisho yake, imezipatia muhimu mno nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Kinyume na madhehebu zingine, Uislamu umechukua maanani masuala yote ya maisha ya uhai wa mwanandamu; zaidi ya hayo, imetimiza mahitajio yote anayoyahitaji mwanadamu katika maisha yake bila ya kuacha chochote hata kwa kiasi cha punje ndogo.

 

Kwa upande mmoja Uislamu unawasisitiza Waislamu kutafuta nyenzo za kujipatia mahitajio yao ya kila siku katika maisha yao kwa njia zifuatazo:

1.       Ibada ni za aina saba, na mojawapo ni kule kujitafutia mahitaji ya kila siku kwa njia zilizo halalishwa katika Dini. [1]

2.       Yeyote yule aliye na maji pamoja na ardhi katika uwezo wake, na wala halimi katika ardhi hiyo, na iwapo atakumbwa na hali ya kukosa chakula cha kujilisha yeye pamoja na familia yake, basi atambue wazi kuwa huyo amekosa baraka za Allah swt. [2]  

3.       Moja ya matendo yaliyo bora kabisa ni kilimo kwani mkulima anajishughulisha katika kilimo na upandaji wa mazao ambayo yanawafaidisha wote bila ya kuchagua iwapo huyu ni mwema au mwovu. [3]  

4.       Yeyote yule asiyejitafutia mahitaji yake ya maisha basi kamwe hatakuwa na maisha ya mbeleni kwani atateketea.

5.       Na yeyote yule anayejitahidi kwa bidii kubwa kwa kujipatia mahitaji kwa ajili ya familia yake basi huyo ni sawa na yule ambaye anapigana vita vya Jihad. [4] 

 

Kwa upande wa pili, Islam inaamini kuwa iwapo mtu atakuwanavyo mali na milki, kilimo na viwanda, utajiri na starehe lakini bila ya Taqwa ya Allah swt  kama vile imani juu ya Allah swt na Mitume a.s, Imani juu ya siku ya Qiyama, thawabu, na adhabu na bila ya kuwa na tabia njema na kuuthamini ubinadamu kama vile msamaha, ushirikiano katika mambo mema, moyo wa utoaji, kuonea huruma n.k. basi kamwe haviwezi kumpatia maendeleo.

 

Allah swt anatuambia katika Qur’an Tukufu Sura 103 : Ayah 1-3

  ‘Naapa kwa alasiri.’

‘ Hakika mwanadamu yumo hasarani !’

‘ Ila wale ambao wameamini wakatenda mema na wakausiana kwa haki na subira.’

 

Imam Hussein a.s. amenakiliwa akisema:

“Kama kwa kweli kuna milki ya mali ya mtu humu duniani, basi hiyo ni  kuwa na tabia njema. Iwapo watu wote watakufa, basi kifo jema kabisa mbele ya Allah swt ni kule kujitolea mhanga katika njia ya Allah swt.”

 

Hivyo, kwa mujibu wa Islam, maendeleo katika mambo ya dunia bila ya kuwa na sifa za taqwa basi haina dhamana ya kuitwa maendeleo ya mtu binafsi au jumuiya. Ili kukamilisha maendeleo hayo kunabidi kuambatane sambamba na taqwa pamoja sifa za ubinadamu.

 

Leo hii sisi tumegundua kwa mujibu wa uzoefu tulivyoona kuwa maendeleo yaliyopatikana bila kuwa na taqwa na adabu njema, si kwamba zimezifanya zisiwe na mafanaikio halisi, lakini pia kunauwezekano wa kuwa janga kuu kwa mwanadamu. Hivyo, sisi tunaona kuwa mbali na maendeleo yao ya kisayansi na kiviwanda, Wakoloni wa Mashariki na Magharibi wanatenda maovu kupindukia kiasi dhidi  ya mataifa dhaifu kwa sababu wao hawana sifa za kiroho, adabu za kibinadamu na imani juu ya  Allah swt.  Sisi vile vile tumeshuhudia dhuluma zao katika kuteka nyara njia zote za kupata mali za nchi zinazokandamizwa na hao wadhalimu bila huruma.  Sisi vile vile tumejionea mauaji na umwagikaji wa damu wa raia wasio na hatia kwa ajili ya uchu wao wa kutaka kuuza silaha zinazoleta maangamizo, bila kujali pale zinapokwenda kutumiwa hizo silaha.

 

Hata katika jamii yao pia, humo zipi tofauti za tabaka zilizodhalilishwa. Kwa kutokana na kumomonyoka kwa utamaduni wao, na jamii zao zipo katika mwelekeo wa kutokomea, kwani wao wametumbukia katika maovu na maangamizo yaliyokithiri.

 

Haya yote ni matokeo ya sayansi isiyokuwa na imani na adabu za mambo yanayomsibu mwanadamu.

Hadi hapo mtu hatakaporejea katika adabu njema, utukufu wa kiroho na mafundisho ya Mitume a.s., basi maovu yataendelea kukithiri na maafa ndiyo yatakayokuwa hatima yao.

 

Kwa sababu hizi, ndiyo maana Islam inawataka wanaadamu wawe wenye tabia bora kabisa, wajipatie utakaso wa  maisha yao na kiroho na ukamilifu wa kiroho katika maisha yao na wawe wenye moyo na uwezo wa kuvitolea mhanga vitu vya humu duniani visivyo na uhakika kwa ajili ya kujipatia utukufu na ukuu katika ubinadamu.

 

Katika aya nyingi za Quran tukufu, kwa kutumia njia mbalimbali za kuelezea, Qur’an tukufu imesisitiza mno juu ya tabia njema na kuwasifu Mitume a.s. kwa kuwa na tabia na sifa hizo kama vile subira, unyenyekevu, moyo wa usamehevu, kutimiza ahadi na ucha-Mungu.

 

Kwa ajili ya kuwaletea wasomaji wetu habari zaidi  juu ya adabu za Kiislamu, sisi tutalizungumzia swala moja lililo la maana mno katika Islam, nalo ni Usamehevu katika Islam na Insha-Allah, tutaendelea kutoa vijitabu juu ya maudhui mbalimbali ili kuwanufaisha wasomaji ili kuyatengeneza maisha yetu kwa mujibu wa amri na utiifu wa Allah swt.

 

Usamehevu kunamaanisha kutoangalia kosa na dhambi la mtu ambaye amekufanyia kwa makusudi au kwa kutokukusudia kwa mfano kukukashifu kwa maneno yake, kukupiga au kukudhulumu mali yako.  Kwa kutozingatia masuala kama haya na wala kutomwadhibu huyo aliyoyatenda hayo ndiko kunakomaanisha usamehevu.

 

Usamehevu upo wa aina mbili:

1.       Sisi tunamsamehe mtu pale tunajikuta kuwa hatuna uwezo wa kulipiza kisasi. Kwa hakika aina hii ya usamehevu unatokana na subira na kuvumilia na kamwe si kusamehe. Kwa maneno mengine, ni aina mojawapo ya kutoweza kujisaidia na udhaifu.

2.       Sisi tunamsamehe mtu ingawaje tunao uwezo wa kulipiza kisasi. Aina hii ya usamehevu ndio unaofundishwa na Islam pamoja viongozi wetu.

 

Katika Ahadith nyingi mno za Maimamu wetu a.s., neno uwezo umetumika mara nyingi mno popote pale palipotumika swala la usamehevu lilipozungumzwa. Hapa chini tunapenda kuwaleteeni baadhi ya madondoo:

1.       Amesema Al-Imam Ali as. : “Mtu anayestahiki kusemehe wengine ni yule ambaye ni mwenye uwezo mkuu  zaidi katika kuwaadhibu wengine.”[5]

2.       Katika wusia wake wakati akiongea na Harith Hamdani, Al- Imam Ali a.s. alisema: “Tuliza ghadhabu zako na kumsamehe mtu aliyekukosea wakati wewe ukiwa na uwezo au cheo chako.” [6]

3.       “Wakati wewe utakapomzidi nguvu adui yako, basi zingatia kumsamehe ikiwa ndiyo shukurani ya kupata uwezo huo.” [7]

4.       Amesema al-Imam as- Sadique a.s. “Kuwasamehe wengine wakati mtu yupo katika madaraka ni sambamba na tabia na desturi za Mitume a.s pamoja waja wema.” [8] 

 

Wewe utakuwa umejionea katika kauli zote hizo kuwa neno uwezo na madaraka yametumika: hivyo katika Uislamu kusamehe hasa kunamaanishwa pale ambapo mtu anao uwezo wa kulipiza kisasi; ama sivyo msamaha unaotokana na mtu kutokuwa na uwezo, kama ilivyokwisha elezwa hapo awali, ni ishara ya kutokuwa na uwezo na ndiyo udhaifu wa mtu.  Kwa maneno mengine,  ni aina mojawapo ya uvumilivu .

 

Baadhi ya Ayah za Qur’an tukufu zizungumziazo maudhui haya:

 

1.       Sura  Al- A’araf  (7) Ayah ya 199

Uchukulie kusamehe na kuamrisha mema na kujiepusha na majaheli[9]

 

Vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’an : Sura A’araf ( 7 ) Ayah ya 200

‘Na iwapo wasiwasi wa Shaitani utakusumbua basi jikinge kwa Allah, Yeye ndiye Asikiaye na Ajuaye yote.’

 

2.       Sura  Aali ‘Imran  (  3 )  Ayah  134

Wale wanaotumia wakiwa katika hali nzuri na dhiki na ambao huzuia ghadhabu zao na kusamehe (makosa ya) watu ; kwani Allah huwapenda wafanyao mema.  [10]

 

Katika kufanyia utafiti zaidi wa Ayah hizo za Qur’an Takatifu, sisi tunatambua kuwa Allah swt anamwamuru Mtume s.a.w.w. wake usamehevu na kutoangalia makosa yaliyofanyika  Allah swt anamsisitiza kuwa na tabia njema wakati akiwaongoza na kuwahubiri watu., na kumweka mbali asije akajihusisha na majaheli. Ili kumfanya Mtume s.a.w.w. afanikiwe kikamilifu, Allah swt anamwonya asiyaitikie mavutio ya Shaitani ambayo ndiyo vizuizi vikubwa kabisa mbele ya mwanadamu katika kutenda matendo mema. Kwa ajili ya kumnusuru Mjumbe Wake, Allah swt anamtaka awe akimwomba msaada wake.

 

Inatuwia dhahiri kuwa kumsamehe dhalimu na kujiepusha na hasira za kulipiza kisasi ni vigumu mno na si rahisi kama tunavyofikiria.  Kwa hakika mwanandamu anahitaji upeo mkubwa wa nuru ya kiroho ambayo itaweza kumfanya azike tamaa zake na hisia zote za kulipiza kisasi  (ama sivyo atakaa akiteseka yeye mwenyewe) na badala yake akatoa msamaha wakati ambapo anao uwezo kamili wa kulipiza kisasi.  Na kwa sababu hizi hizi ndipo Allah swt anapotutambulishia kujizuia na hasira kuwa ndiyo sifa mojawapo ya Mumiin halisi.  Sifa hii huwatukuza wale ambao huzikandamiza hasira, chuki na kisasi na kwa moyo mpana huwa wepesi mno katika kuwasamehe wengine.

 

3.       Allah swt anatuambia katika Sura Aali ‘Imran ( 3 ) Ayah ya 159 kuwa: [11]

‘Hivyo kutokana na Rehema itokayo kwa Allah  kuwa wewe umekuwa mlaini kwao na kama ungalikuwa mkali na mwenye moyo mgumu bila shaka wangalikukimbia. Basi uwasamehe wewe na uwaombe msamaha na ushauriane (kwa kuwaridhisha tu ) nao katika mambo. Na unapoazimia mtegemee Allah, Hakika Allah huwapenda wamtegemeao. ’

 

Aya hii tukufu imewateremkia kuhusu wale ambao walikwenda kinyume na amri ya Mtume Muhammad sa.w.w. katika Vita vya Uhud ambapo kulisababisha Waislamu kushindwa.  Watu hao walikuwa ni hamsini na wawili (52) kwa idadi ambao waliwekwa na Mtume s.a.w.w. kulinda pakuingilia huko bondeni na aliwaambia : “ Iwapo sisi tutashinda au kushindwa, nyinyi kamwe musisogee wala kuondoka  hata hatua moja kutoka sehemu hii iliyo nyeti.”

 

Mbinu hii ya Mtume Muhammad s.a.w.w. ikiwa pamoja na baraka za Allah swt na moyo wa kujitolea mhanga wa vijana wa Kiislamu wenye imani halisi, iliwafanikisha kuwashinda maadui ambao walikimbia. Wailsamu baada ya maadui kukimbia, walianza kukusanya mali iliyopatikana vitani hapo katika uwanja wa mapigano.

 

Mara hawa watu hamsini na wawili walipopata habari kuwa Waislamu wameshinda na wanakusanya mali iliyopatikana vitani, wote, isipokuwa kumi na wawili tu, waliacha ngome zao wazi na kukimbilia mali huku wakiwa wamevunja amri ya Mtume Muhammad s.a.w.w. iliyokuwa imewakataza wasiondoke hapo walipo katika sura yoyote ile ama iwe ya ushindi au kushindwa.  Kwa kuona haya, Khalid ibn Walid, ambaye alikuwa ni kamanda wa jeshi la makafiri, alikwenda hapo bondeni akiwa na jeshi la wapanda farasi mia mbili (200 ) wakiwa wamejiandaa kwa silaha. Makafiri hao waliwashambulia kwa ghafla Waislamu kumi na wawili na kuwaua wote na wakatokezea kwa nyuma kushambulia jeshi la Waislamu. Katika mapigano haya, Mashujaa sabini ( 70 ) wa jeshi la Waislamu waliuawa, akiwemo Hamzah ush-Shuhadaa ( kiongozi wa mashahidi).  Na Mas’ab ibn Umair vile vile wapiganaji wengi walijeruhiwa akiwemo Mtume Muhammad s.a.w.w. pamoja na Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.  Kwa hakika kuvunja amri ya Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa hao wachache kulileta maafa makubwa kwa upande wa Waislamu.  Watu walitegemea kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. atatoa amri kali kabisa dhidi ya hawa wachache; lakini sivyo na badala yake kuliteremka Ayah tukufu ikisema:

        Sura Aali ‘Imran ( 3 ) Ayah ya 159 kuwa:

‘… Basi uwasamehe wewe na uwaombe msamaha na ushauriane (kwa kuwaridhisha tu ) nao katika mambo….’

 

Kwa kuiteremsha Ayah hii, Allah swt alimwamuru Mtume Muhammad s.a.w.w. atoe msamaha kwa waliokuwa wamekosa.

 

Kauli zilizotolewa na viongozi wa Kidini

Pamoja na kuwaita watu katika kusamehe na kuachilia mbali makosa yao, viongozi wetu wa Kidini wamekuwa katika mstari wa mbele na mifano bora humu dunia ya wale wanaosamehe, na kwa kuwaacha wao basi hakuna wanaofuzu katika sifa hii ya usamehevu.  Sasa sisi tutawaleteeni yaliyozungumzwa nao na hapo mbeleni tutawaleteeni hoja za kihistoria:

 

1.  Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema:

 “Bora ya tendo lililo mbele ya Allah swt ni kusamehe mtu ambaye amekukosea, kuwapenda ndugu na jamaa ambao wameukata uhusiano pamoja nawe, na kuwa mkarimu kwa yule ambaye aliwahi kukunyima. “ Na hapo Mtume Muhammad s.a.w.w. aliisoma Ayah hii ya Qur’an:

    Sura  Al- A’araf  (7) Ayah ya 199

Uchukulie kusamehe na kuamrisha mema na kujiepusha na majaheli  [12]

 

2.  Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika mkataba aliokuwa amemwandikia Malik-i-Ashtar, aliandika:

Zijazeni nyoyo zenu kwa  huruma, uwema na kuwapenda waliochini yenu. Na kamwe musitendee kama wanyama walafi na waroho, kujifanya kama munawalea kwa kuwatenga, kwani wao wapo wa aina mbili: ama wao ni nduguzo katika imani au wapo sawa katika kuumbwa. Wao wanapotoka bila ya kujua na kasoro zinawaghalibu, wanakosa makosa ama kwa makusudi au bila kukusudia.  Kwa hivyo nawe pia uwasamehe  kwa kutegemea naye Allah swt atakusamehe, kwani wewe umekuwa na uwezo dhidi yao, na Yule aliyekuchagua wewe yu juu yako, na Allah swt  yupo juu ya yule aliyekuweka katika wadhifa huu.” [13]

 

3.  Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. :

Kusikitika baada ya kutoa msamaha ni afadhali ya kufurahi baada ya kuadhibu.” [14] 

 

4.  Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika  Hadith ‘Arbain, ananakili Marehemu Deilami:

“Siku ya Qiyama, mpiga mbiu atasimama na kusema: ‘Yeyote aliye na malipo yake kwa Allah swt basi asimame.’  Lakini hakuna watakao simama isipokuwa wale tu ambao walikuwa ni wasamehevu.  Anaendelea kusema ‘Je hao hawakusikiaga ahadi iliyokuwa imetolewa na Allah swt :

Surah Ash-Shuura  ( 42 ) Ayah ya 40 [15]

‘… lakini anayesamehe na kusahihisha; ujira wake uko kwa Allah ….’

 

Baadhi ya mifano ya misamaha iliyokuwa imetolewa na Mtume Muhammad s.a.w.w. na Maimamu a.s.

 

Moja ya utambulisho wa viongozi wa Kidini ni kwamba wao pamoja na kuwa ni watangazaji wa Dini kwa watu, wao walikuwa, kwa hakika ni wahuishaji wa Dini.

 

Wao walikuwa ni mifano ya mema yote ambayo wao walikuwa wakiwalingania watu.  Katika maneno mengine, kwa hakika viongozi wetu ndio mifano hai na halisi wa Islam.  Hivyo ni wajibu wetu sisi kuainisha maisha yetu ya kidunia na kiroho pamoja nao.  Ama wale ambao hazijui habari na taarifa za viongozi wao wa Kidini, sisi tunajaribu kuwaleteeni mifano michache kwa kutumai kuwa mifano hizi zitatusaidia katika kurekebisha maisha yetu na kuwa fundisho kwetu sote.

 

Mfano wa msamaha wa Mtume Muhammad s.a.w.w.

Yapo matukio mengi mno ambapo Mtume Muhammad s.a.w.w. ametoa misamaha, lakini tutazungmzia  mojawapo juu ya kuikomboa Makka.  Baada ya kupokea Utume, Mtume Muhammad s.a.w.w. aliishi Makkah kwa muda wa miaka kumi na mitatu (13 ). Katika kipindi hiki cha miaka kumi na mitatu, Mtume Muhammad s.a.w.w. alistahimili mateso na maumivu mbalimbali na vile vile alivumilia shutuma za uongo kutoa wakazi wa Makkah na mapagani wa Qoreish. Wao hata walithubutu kumwita Mtume Muhammad s.a.w.w. kuwa ni mtu mwehu.  Wao walimshambulia kwa mawe na kumtupia mchanga usoni mwake hadi Mtume Muhammad s.a.w.w. akatamka:“Hakuna Mtume aliyeteseka kiasi hiki kama vile nilivyoteseka mimi.” Mapagani wa Qoreysh hata walithubutu kupanga njama za kutaka kumwua Mtume Muhammad s.a.w.w.. Lakini Allah swt alimjulisha Mtume Muhammad s.a.w.w. kuhusu njama hiyo na hapo ndipo Mtume Muhammad s.a.w.w. alipomwambia Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.  alale juu ya kitanda chake na hivyo Mtume Muhammad s.a.w.w. aliondoka Makkah kuelekea Madina wakati wa usiku. Yeye alisimama mahala ambapo mji wa Makkah ulikuwa ukionekana kwa uwazi na akasema kwa sauti ya masikitiko, “ Ewe nyumbani kwangu ! Allah swt anaelewa vyema kuwa ninakupenda. Iwapo wakazi wako wasingalipanga njama hizi za kunitoa nje,  basi mimi kamwe nisingalikuacha kwa kuuchagua mji mwingine. Mimi ninahuzunika kwa kutengana nawe.” [16]

 

Baada ya kusafiri masafa marefu, Mtume Muhammad s.a.w.w. alianza kuishi katika mji mtukufu wa Madinah, mji ambao ndio ukawa wa kuuhubiri Uislamu.  Hapo Madina, vile wakazi wake walikuwa wakimbughudhi Mtume Muhammad s.a.w.w..  Wao walipigana na Mtume Muhammad s.a.w.w. kiasi cha vita ishirini na nane ( 28 ). Wao walimwua baba mkubwa wa Mtume Muhammad s.a.w.w. katika vita vya Uhud, wakatoa maini yake na kumpatia Hinda, mke wake Abu Sufyan, kama zawadi naye aliila maini ikiwa bado mbichi kabisa.  Wao pia waliziharibu sehemu za mwili wake na kuzivaa shingoni. Wao waliijaza moyo mlaini wa Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa huzuni na masikitiko na majonzi makubwa kwa kifo cha baba yake mkubwa.

 

Wakati Mtume Muhammad s.a.w.w. alipoona hali hiyo ya kusikitisha ya baba mkubwa wake, alisema : “Kwa kiapo cha Allah swt ! Mimi kamwe sijawahi kusimama mahala kama hivi ambavyo imenikasirisha kiasi hiki. Iwapo Allah swt atanijaalia ushindi juu ya Maqoreish hawa, basi nami nitawatendea watu sabini miongoni mwao kwa kulipiza kisasi cha babangu mkubwa Bwana Hamza.”  Papo hapo Malaika Jibraili a.s. alimteremkia  akiwa pamoja na Ayah hii : [17]

Sura An-Nahl (16) Ayah ya 126

Na mkilipiza, basi lipizeni sawa na vile mlivyoonewa, na kama mkisubiri basi hiyo itakuwa bora kabisa kwa wafanyao subira’.

 

Baada ya ufunuo wa Ayah hiyo, Mtume Muhammad s.a.w.w. alisema : “mimi nitakuwa mwenye subira.” [18]

 

Mtume Muhammad s.a.w.w. ajitayarisha kuelekea Makkah

 

Baada ya kuvumilia maumivu yote haya pamoja yalimsibu, hatimaye Allah swt  alimwahidi Mtume Muhammad s.a.w.w.  “Allah ambaye amekufaradhishia Qur’an juu yako Atakurejesha Makkah siku moja.”

 

Katika mwaka wa nane ( 8 ) baada ya Hijrah,  Mtume Muhammad s.a.w.w. aliwaamuru wale wote waliokuwa Wamesilimu kujitayarisha kwa ajili ya vita vitakatifu.  Kiasi cha wapiganaji elfu kumi na mbili, chini ya amri za Mtume Muhammad s.a.w.w. waliondoka kuelekea Makkah siku ya kumi ya mwezi mtukufu wa Ramadhaan. [19]

 

Wakati huo, Amu yake Mtume Muhammad s.a.w.w. aliyeitwa ‘Abbas, ambaye alikuwa amehamia Makkah kutoka Madina pamoja na familia yake, alikutana na jeshi la mtoto wa ndugu yake, yaani Mtume Muhammad s.a.w.w., mahala panapoitwa Zul-Halifa. Kwa kumwona Amu yake, Mtume Muhammad s.a.w.w. alifurahishwa mno na kwa kujawa  matumaini alisema : “ Uhamisho wako huu ndio wa mwisho kwa kuhama kama vile ulivyo Utume wangu ndio mwisho wa wote.”

 

Hapo ndipo alimwamrisha ‘Abbas aitume familia yake kwenda Madina na yeye mwenyewe kuungana na Mtume Muhammad s.a.w.w. katika msafara wake huo.

 

Msafara mrefu ulipitwa kwa wepesi na haraka hadi hapo Wailsamu walipofika kiasi cha Km 25 kufika Mjini Makkah.  ‘Abbas alifikiri kuwa iwapo yeye ataweza kufika Makkah kabla ya jeshi la Waislamu hawajaingia humo, basi ataweza kuwashawishi Maqoreish kujisalimisha na hivyo ataweza kuzuia umagikwaji wa damu yaani vita havitatokea.  Kwa madhumuni haya, yeye aliondoka na usafiri wa Mtume Muhammad s.a.w.w. na alikimbia haraka kuelekea Makkah, na alipofika mahala paitwapo Arak karibu na Makkah, yeye alisikia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya Abu Sufyan na Badil ibn Wurqa.

 

‘Abbas alimwita Abu Sufyan ambaye kwa kumtambua alimwambia : “Wazazi wangu wawe fidia juu yako ewe ‘Abbas ! Je kumetokea nini kwamba umewahi kurudi kwa haraka ?”

 

‘Abbas alimjibu, “ Kwa sasa hivi Mtume Muhammad s.a.w.w. akiongozana na jeshi la Waislamu wapatao elfu kumi na mbili, hapo wanakaribia Makkah. Wewe ( Abu Sufyan ) hauna chaguo lingine lolote isipokuwa kuambatana nami ili ukamwone (Mtume Muhammad s.a.w.w. ) ili nikuombee msamaha ili uweze kuyanusuru maisha yako.  Ni lazima utambue kuwa kikosi cha mbele kinaongozwa na ‘Umar ibn Khattab, na iwapo  ataweza kukushika, basi hatasita kukuua papo hapo”  Kwa maneno hayo ‘Abbas alimshtua mno Abu Sfyan na akampakia katika usafiri wake na kumleta mbele ya Mtume Muhammad s.a.w.w. . Hapo ‘Abbas alisema: “Ewe Mtume wa Allah swt, mimi nimemhurumia na kumwachia maisha ya Abu Sufyan. “ Hapo Mtume Muhammad s.a.w.w. alimjibu: “Mwambie asilimu ili aweze kuufaidi uhifadhi kamili.”

 

Ndipo Mtume Muhammad s.a.w.w. alipomgeukia Abu Sufyan na kumwambia: “ Je utawafanya nini miungu iitwayo Lat  na Habal ?”  Kabla ya Abu Sufyan kujibu chochote, ‘Umar ibn Khattab alijiingiza na kusema, “Wewe lazima uyaangamize kwa machukizo mno.”  Abu Sufyan kwa kumwelekea ‘Umar alimjibu, “Laana ziwe juu yako ! Je kwa nini unatumia lugha ya kashfa na huku uniniingilia mimi nikizungumza na ndugu yangu huyu  (Mtume Muhammad s.a.w.w. ) ?” Kwa hayo ‘Umar alizidiwa na ghadhabu. Lakini Mtume Muhammad s.a.w.w. alimtuliza.  Haya yote pia yalimshtua na kumwogopesha huyo Abu Sufyan.

 

Mtume Muhammad s.a.w.w. aliwaamuru Waislamu wamweke Abu Bufyan katika hema la ‘Abbas kwa usiku ule. Kulipokucha, Bilal alitoa adhaan. Abu Sufyan aliuliza “Je ni mwito wa nini huo ?” Bwana ‘Abbas alimjibu “Hii ni adhaan inayotolewa na Bilal wa Habashi ambaye ndiye Muaddhin wa Mtume Muhammad s.a.w.w. ,  inayotuita kusali sala ya alfajiri.”  Abu Sufyan alikuwa akiyatazama matukio yote kwa mshangao mkubwa: Mtume Muhammad s.a.w.w. alijitayarisha kufanya wudhuu na hakuna hata tone moja la maji lililodondoka chini kwani Masahaba walikuwa wakizidaka matone yote ya maji yaliyokuwa yakidondoka na kujipaka usoni na vichwani mwao.

 

Kwa mshangao mkubwa Abu Sufyan alisema: “Mimi ninayaangalia mambo kwa makini kabisa ambayo hata hatukayaona kwa Qaisari na Kasra.”  Kwa kuogopea maisha yake, yeye aliitamka kalimah na kusilimu.

 

‘Abbas amwombea Abu Sufyan mapendeleo

 

Ili kuufanya ukombozi wa Makkah kuwa wa urahisi, ‘Abbas alimwomba Mtume Muhammad s.a.w.w. ampatie upendeleo fulani Abu Sufyan katika ukombozi na ushindi huu. Alisema : “Ewe Mtume wa Allah swt ! Iwapo utaonelea kuwa ni ushauri, basi tafadhali sana umpe upendeleo fulani Abu Sufyan ili  yeye asiwe na hisia ya kudharauliwa miongoni mwa Maqoreish na hivyo asithubutu kutunga hila za aina yoyote ile dhidi ya Waislamu.”  Mtume Muhammad s.a.w.w. alisema : “Yeyote yule atakayeingia katika nyumba ya Abu Sufyan atasalimika na vile vile na yeyote atakaye salimisha silaha zake pia atasalimika, atakayeingia nyumbani mwake, na kujifungia mlango basi atakuwa pia amesalimika. Na yeyote atakayeingia ndani ya Masjid –al-Haram pia atakuwa amepewa hifadhi na amesalimika.”

 

Tunapenda kuwatahadharisha wasomaji wetu kuwa msamaha huu aliopewa Abu Sufyan ulikuwa umepigiwa mahesabu sawasawa hivyo wasije wakafikiria vinginevyo.  Ingawaje tunatambua waziwazi kuwa hakuna kabila lililomtesa na kumuudhi Mtume Muhammad s.a.w.w. pamoja na wafuasi wake kama Abu Sufyan na kabila lake. Hayo yote Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa akiyakumbuka na kuyatambua vyema kabisa na hivyo alitumia busara hiyo ya kuwasalimisha wale wote watakaoingia nyumbani kwake ili kuepukana na upinzani na umagikwaji wa damu wa watu wasio na hatia hivyo ukombozi na ushindi wa Makkah uwe bila kumwagika damu. Na hivyo Abu Sufyan aliridhika na mbinu hiyo ya Mtume Muhammad s.a.w.w.

 

Abu Sufyan atangaza kuingia kwa Mtume Muhammad s.a.w.w. huko Makkah

 

Abu Sufyan aliingia Makkah akiwa amechanganyikiwa na kubabaika. Wakazi wa Makkah walishangazwa mno kwa vitendo vya Abu Sufyan , bila ya kujua kile kilichotokea.

 

Kwa ufadhaisho mkubwa akisema hofu yake, Abu Sufyan alisema: “Ole wenu!, Mtume Muhammad s.a.w.w. yupo karibu kuingia Makkah dakika yoyote ile kuanzia sasa pamoja jeshi lake kubwa sana, hivyo mutambue kuwa yeyote yule atakaye ingia nyumbani kwangu atasalimika na vile vile yeyote yule atakayeingia katika Masjid al-Haram pia atanusurika na kusalimika.”  Watu walimkimbilia na kumkemea mno Abu Sufyan. Na mke wake, Hind, alithubutu kumpiga kibao usoni mwake na kusema kwa sauti : “ Kiuweni hiki kizee kichaa na kipumbavu.”

 

Hatimaye, Mtume Muhammad s.a.w.w. aliingia katika ardhi ya nyumbani kwake, ambapo kutoka kwake kulimhuzunisha mno. Allah swt alimwamrisha kutohuzunika kwani itafika siku moja ambapo atakapomrejesha nyumbani akiwa mshindi na mwenye heshima. Ahadi ya Allah swt ikawa kweli. Jeshi la Waislamu lilifika Hajoon na kaburi la Bi. Khadija. Mtume Muhammad s.a.w.w. alitawadha na kutimiza faradhi za Dini  katika hema lake na akiutoa upanga wake, alimpanda farasi wake na kuelekea Al-Ka’abah huku akisoma Sura al-Fateh ya Qur’an Tukufu :

 

Surah  Fat-h   (48 ) Ayah 1-2

‘ Bila shaka tumekwishakupa kushinda kuliko dhahiri. Kwamba Allah  alinde kwa ajili yako (dhidi) ya yale yaliyopita kabla ya (wafuasi wako) kasoro zako na yale yanayokuja …’ [20]

 

Wapiganaji wa Kiislamu huku wakiwa wamemzingira Mtume Muhammad s.a.w.w. na wakisoma dhikiri , waliingia katika Masjid al- Haram.  Wakati kazi ya kuvunja masanamu ya miungu ya mapagani ilipoanza, Mtume Muhammad s.a.w.w. aliisoma Ayah ifuatayo :

 

Surah Bani- Israil (17 ) Ayah 81

Na sema : ‘Ukweli umefika; na uongo umetoweka; Kwa hakika uongo ndio wenye kutoweka.[21]

 

Wakati Mtume Muhammad s.a.w.w. akiisoma Ayah hii alikuwa akiinyooshea vidole sanamu hizo zilizokuwa zikianguka chini moja baada ya nyingine huku zikivunjika na kuwa mavumbi.  Baadhi ya masanamu yalibakia mazima katika sehemu za juu ya Al-Ka’abah ambapo palikuwa hapafikiki kwa mikono, basi Mtume Muhammad s.a.w.w. alimwambia Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ampande mabegani mwake Mtume s.a.w.w. na ayavunje masanamu. Hivyo Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alipanda mabegani mwa Mtume Muhammad s.a.w.w. na kuyabomoa masanamu ya miungu ya mapagani Qoreish, yote kwa pamoja.

 

Mtume Muhammad s.a.w.w. atangaza msamaha wa ujumla kwa wote

 

Baada ya kuitakasisha  Al-Ka’aba Tukufu kutoka ushirikina wa kila aina na kubomolewa kwa masanamu ya miungu ya mapagani, Mtume Muhammad s.a.w.w. aliweka mikono yake katika viambaza vya mlango wa Al-Ka’aba tukufu, huku akielekeza uso wake penye watu, alisema: “Sasa nini ? Je mwafikiriaje ?”  Wao walijibu: “Sisi twasema baraka na wala si kitu kingine, kwani wewe ni ndugu yetu mkarimu na ni mwana wa mkarimu; zaidi ya hayo wewe umekuwa mshindi juu yetu. “

 

Mtume Muhammad s.a.w.w. alivutiwa kwa huruma na machozi yalidondoka kutoka machoni mwake. Yeye alisema: “Mimi nitayazungumza yale ambayo ndugu yangu Mtume Yusuf a.s. aliyasema,

Surah  Yusuf  (12 ) Ayah 92

… ‘Hakuna lawama juu yenu leo; Allah atakusameheni, naye ni Mwenye rehema zaidi kuliko wanaorehemu.[22]

 

Hapo ndipo aliposema: “Nendeni ! Nyinyi nyote ni watu walioachiwa huru !”

 

Kwa hakika mtu ambaye aliinuliwa kama ndiyo dalili za Allah swt za Rehema kwa ulimwengu mzima, amechukua hatua kubwa wa moyo mpana wenye huruma kwa kuwasamehe wakazi wa Makkah kwa unyanyasaji, ubaguzi, udhia, mateso na makosa ya kila aina waliyomfanyia. Yeye, Mtume Muhammad s.a.w.w. aliwasamehe wote kwa pamoja akiwemo Hinda, mke wake Abu Sufyan , ambaye aliyatafuna maini majichi ya baba mkubwa wa Mtume Muhammad s.a.w.w.  katika vita vya Uhud na alitunga katika kamba viungo vitakatifu vyake na kuvivaa shingoni.

 

Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. alimsamehe mtumwa wa Kihabeshi, Wahshi, ambaye ndiye aliyekuwa amemwua Bwana Hamza, babake mkubwa wa Mtume Muhammad s.a.w.w. . Alimsamehe wakati ambapo alikuwa na uwezo kamili wa kumwadhibu na kulipiza kisasi. Kwa hakika hii ndiyo iliyokuwa kanuni ya mtu ambaye alikuwa akiwaambia watu wote kuwa huruma ipo imefungamana katika tabia tatu:

 

1.  Kumsamehe yule aliyekutendea yasivyo sahihi.

2.  Kudumisha mshikamano wa udugu pamoja na jamaa ambaye ameuvunja

     uhusiano pamoja nawe.

3.  Kumsamehe yule ambaye amekudhulumu au kukunyima haki yako.

 

Qur’an tukufu inawatakata Wailsamu waigize tabia na mwnenendo kama Mtume Muhammad s.a.w.w. na ndiye awe kiigizo chao :

Surah  Ahzab (33 ) Ayah 21

‘ Kwa hakika mnao mfano mwema kwa Mtume wa Allah, …’ [23]

 

Kwa mujibu wa Ayah hiyo, iwapo sisi tutapenda kuwa Waislamu wema, basi itatubidi kuzifuata tabia na mienendo yote ya Mtume Muhammad s.a.w.w. .

 

Mfano wa Msamaha uliotolewa na Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.

 

Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alikuwa ni mtu mwenye subira, uvumilivu na  usamehevu wa hali ya juu kabisa.  Tukielewa vile alivyowatendea  maadui wake itatosheleza kuelezea usamehevu wa huyu mrithi wa Mtume Muhammad s.a.w.w.  kwa ajili ya wafuasi wake.

 

Marwan Hakam, Abdullah ibn Zubair na ‘Amr ibn al-As na akiwemo ‘Aisha, mmoja wa wake wa Mtume Muhammad s.a.w.w.  waliwahadaa watu wa Basra na kuwafitini na kuwachochea mpaka wakaanza vita dhidi ya Islam ambayo ilikuwa na kiongozi wao Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.. Ili kuulinda,kuihami  na kuunusuru Uislamu, Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. ilimbidi apigane vita dhidi yao.  Kwa kutokana na msaada wa Allah swt, Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. aliwashinda maadui zake na kuwachukua mateka wale wote waliokuwa wamekuja kupigana dhidi yake.  Hapo Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. aliwaachia huru wote kwa pamoja bila ya kulipiza kisasi kwa makosa yao yenye kuaibisha. Kwa taadhima na heshima zote, Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alimkalisha mwanamke (‘Aisha ) aliyekuja kupigana naye juu ya ngamia hadi Madina. Vile vile alitoa msamaha kwa watu wote waliokuwa wamehadaiwa na majeshi ya maadui wake, wote ambao waliwatolea mapanga ‘Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. na wananyumba yake, pamoja na kuwabughudhi, kuwaudhi na kuwadhuru yeye na wafuasi wake. Vile vile Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. hakukubali kuwa maadui wake wateswe kwa hali yoyote ile wala watoto na mali zao pia zisiharibiwe.

 

Vile vile, katika vita vya Siffin, Muawiyah ibn Abu Sufyan alimfungia maji Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. pamoja jeshi lake lote kutoka kianzio chake hivyo wote walibanwa na kiu kikali. Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alitoa hotuba kali na kilichofuatia ni kwamba jeshi lake liliwaghalibu na kuwashinda maadui wao na kumfukuza Muawiyah kwenda jangwani.  Wafuasi wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.  walisema: “Sasa ni zamu yetu sisi  kuwafungia maji hawa maadui wetu ili nao pia wafe kwa kiu na hivyo ndivyo kutamaanisha mwisho wa vita pamoja nao.”  Kwa kuona jazba yao, Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.alisema : “Kwa kiapo cha Allah swt !  Mimi kamwe sitafanya jambo kama hilo. Mimi ninaona kuwa upanga wangu unatosheleza kufikia malengo yetu.”  Na kwa hayo aliwaamrisha kuwafungulia  mtiririko wa maji hadi jeshi la Muawiyah bin Abi Sufyan , ili nao pia waweze kujisaidia kwa hayo.”

 

Mtu amwota Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika ndoto.

 

Ndugu zetu Masunni katika vitabu vyao baadhi ya Wanazuoni wameelezea tukio moja  kama lifuatavyo :

“Mmoja wa  mtegemewa Sunni alisema : “Mimi nimemwota Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. katika usingizi wangu na kusema : ‘Ewe Kiongozi wa Waumini ! Nyinyi mulipoikomboa Makkah, muliifanya nyumba ya Abu Sufyan kuwa ni nyumba yenye amani kwa mkazi yeyote wa Makkah atakayekuwa ameingia ndani humo na vile vile mulitangaza kuwa nyumba yake ilikuwa ina usalama, lakini huko Karbala, wao waliwaua kwa kikatili watoto wenu na hawakuacha juhudi zozote za kuwadhulumu na kuwatesa. Je ni vipi hivyo ?”  Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. alimjibu: “Je wewe haujazisoma beti alizozitunga mwana wa Saifi ?”  Mimi nilimjibu: “La.”  Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. akasema : “Wakati utakapoamka, basi utazisikia kutoka kinywani mwake mwenyewe.”  Basi mtu huyo akasema: “Wakati nilipoamka, mimi niliharakisha kwenda nyumbani kwa mwana wa Saifi iliyokuwa ikijulikana kama Haiis u-Bait na kumwelezea kuhusu ndoto yangu hiyo.  Punde alipoisikia, alipiga mayowe na kuangua kilio, na akasema : “ Kwa kiapo cha Allah swt !  Mimi nimezitunga beti hizi  usiku wa kuamkia leo. Mimi bado sijamsomea mtu yeyote yule na Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. anakuamrisha wewe uzisikie.”  Hapo ndipo alipomsomea beti zote ambazo zilikuwa zikizungumzia: “Wakati sisi tulipoupata ushindi, sisi tuliufanya msamaha ndiyo biashara, lakini nyinyi mulipokuwa washindi, nyinyi  muliigeuza ardhi ya Abtah ikageuka kuwa nyekundu kwa ajili ya umwagikaji wa damu. Nyinyi mulihalalisha uuwaji wa mateka wenu, wakati sisi kwa miaka mingi tumekuwa tukiwaachia huru mateka wote.  Tofauti hii inatosheleza baina yako na mimi, kwa mfano wa ulivyo mti ndivyo yatakavyokuwa matunda yake.”

 

 

Mfano wa msamaha uliotolewa na Al-Imam Zaynul ‘Aabediin a.s.

 

Baada ya kipindi cha miaka ishirini na moja ya udikteta wa Abdul Malik ibn Marwan,alifariki  katika mwaka 86  baada ya Hijriyyah na mwanake alitawazwa aliyeita Walid.  Ili kupunguza lawama na shutuma za watu, Walid alianza kurekebisha muundo mzima wa ukhalifa [24]   na namna ya kuwatendea watu.  Yeye alikuwa na kusudi la kuzishinda nyoyo na ridhaa za watu  wa Madina ambao ulikuwa mmoja wa miji miwili iliyo mitukufu ya Waislamu., na kitovu cha wafuasi, ambao waliokuwapo wakiishi Masahaba wa Mtume Muhammad s.a.w.w. , na watu wa hukumu na Ahadith.  Kwa sababu hizi ndipo Walid alipomfukuza Hisham ibn Ismail Makhzuni, babamkwe wa Abdulmalik ibn Marwan ambaye alikuwa akitawala kama gavana wa Madina na alikuwa akiwakandamiza na kuwaonea watu na kuanguka kwake kulikuwa kukipendwa na watu.

 

Hisham ibn Ismail alikuwa amewakandamiza, kuwatesa, kuwanyanyasa na kuwakashifu mno wakazi wa Madina.  Hisham alikuwa amemchapa viboko sitini Sai’d ibn Musayyib, mwelezaji mashuhuri wa Hadith za Mtume Muhammad s.a.w.w.  na mtu ambaye alikuwa akiheshimiwa mno na wakazi wa Madina. Na alichapwa viboko hivyo kwa sababu ya kukataa kula bai’a (kiapo cha kumkubalia kuwa yu kiongozi halali wa Umma wa Kiislamu ) yake. Na baadaye alimvalisha nguo zisizo za heshima, akamkalisha juu ya ngamia na kumzungusha mjini kote.  Hisham alikuwa amewatendea makosa makubwa wananyumba ya Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. , hususan Al-Imam Zaynul ‘Aabediin a.s. , kiongozi na Chifu wa Alawiyya (wafuasi wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. )  kuliko watu wowote.

 

Walid alimfukuza Hisham kutoka wadhifa wake huo.na kumweka ndugu wa kijamaa aliyekuwa bado yu kijana, ‘Umar ibn abdul –‘Aziz, ambaye alikuwa akijulikana kwa nia zake njema na uhaki, kama ndiye gavana mpya wa Madina.  Ili kuondoa masikitiko na chuki zilizokuwamo katika vifua vya watu, ‘Umar aliwaamuru watu wake wamweke Hisham ibn Isma’il Makhzuni mbele ya nyumba ya Marwan Hakam.  Yeye alisema kuwa yeyote yule aliyemsikia au kumwona Hisham akitenda maovu, basi aje na kujilipizia kisasi.  Kwa kuyasikia hayo, watu walimiminika hapo na kwa kutumia lugha zilizojaa kashfa walikuwa wakimtukana na kumlaani Hisham ibn Isma’il.

 

Hisham ibn Isma’il alikuwa akisubiri wakati Al-Imam Zaynul ‘Aabediin a.s. pamoja na wafuasi wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. watakapokuja kutaka kulipiza kisasi chao, basi hakuna kitu kingine isipokuwa ni kuuawa tu kwa mateso, udhalilisho na laana alizokuwa akiwaelekezea hao watukufu wa nyumba ya Mtume Muhammad s.a.w.w. na wafuasi wao.  Kumbe mambo hayakuwa hivyo !  Al-Imam Zaynul ‘Aabediin a.s. aliwaambia wafuasi wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s.:

“Si desturi yetu kuwapiga mateke walioanguka na kulipiza kisasi wakati adui wetu amekwisha. Badala yake, sisi tunayo desturi ya kuwasaidia wale walioanguka.”

 

Wakati Al-Imam Zaynul ‘Aabediin a.s. akiwa ameambatana pamoja na umati mkubwa wa wafuasi wa Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. walipomwelekea Hisham ibn Isma’il, akapooza kabisa akijua kuwa mauti yake imemfikia dakika yoyote ile. Kumbe kinyume na vile alivyokuwa amedhania, Al-Imam Zaynul ‘Aabediin a.s. akasema kwa sauti ya kupaaza : “Amani iwe juu yako” na akapeana naye mkono na kumhurumia, kama vile ilivyodesturi ya kawaida ya wanapokutana Waislamu wawili.  Al-Imam Zaynul ‘Aabediin a.s. akamwambia : “Iwapo utahitaji msaada wangu, basi nipo tayari kukusaidia.” [25]

 

 Kwa hakika haya ndiyo iliyokuwa baadhi ya mifano kuhusu uwema, ukarimu, ukuu, ututkufu na misamaha ya viongozi wa Islam.  Mifano hii ni lazima iigwe na wafuasi wa Dini ya Islam.

 

SWALI : USAMEHEVU NA ADHABU YA VIBOKO

 

Tumeona kuwa Islam inasisitiza mno ‘usamehevu’ sasa kwa nini bado adhabu ya ‘kuchapa viboko bado ipo ?’

 

Bila shaka msomaji wa kijitabu hiki atakuwa amejionea kuwa Ayah za Qur’an Tukufu pamoja na Ahadith Tukufu zinasisitiza mno usamehevu, na hivyo inapinga adhabu za kuchapwa viboko.

 

Jibu na maelezo ni kwamba, ni lazima isemwe kuwa usamehevu umesisitizwa mno katika Islam kama ndiyo haki ya msingi ya kila Mwislamu, yaani mtu yeyote kwa ajili ya ridhaa za  Allah swt na ambaye anamwamini Allah swt, Mtume Muhammad s.a.w.w.,na mitume a.s. yote na siku ya Qiyama awahurumie na kuwasamehe wale waliomkandamiza na kuzikanyaga haki zake. Yeye kamwe asifikirie kulipiza kisasi., ili kwamba chuki na uadui utatokomezwa ulimwenguni kote na Allah swt atamlipa mema humu duniani na Akhera mtu atendaye hayo .

 

Hadi kule kunapohusika haki za jamii , msamaha utasababisha kukithiri kwa maovu na kudhihiri kwa machafuzi. Wakati huo,  usalama wa kijamii utaharibika na watu waovu hawataacha kudhulumu mali, maisha na heshima za watu. Kwa sababu hizi, Ndipo Dini ya Islamu imewekea ulazima kutekelezwa kwa adhabu za kutubisha kuliko kusamehe.

 

1.  Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. “Kutekelezwa kwa adhabu moja ya kutubisha juu ya ardhi inatakisha kuliko kunyesha kwa mvua juu ya ardhi hii kwa mfululizo wa siku arobaini.” [26]

 

 2.  Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. “Allah swt hakubakiza chochote kile ambacho waja Wake watakihitaji hadi Siku ya Qiyama, isipokuwa vyote vipo katika kitabu kitakatifu cha Qur’an na ambayo yote yamefikishwa kwa Mtume Muhammad s.a.w.w.. Yeye amewekea mipaka kwa kila kitu, na kuweka uthibitisho kwa ajili yake.  Kwa wale watakaopita mipaka yake, Allah swt ameainisha adhabu za kutubu za Kidini.” [27]

 

Maneno matukufu haya ya Al-Imam a.s. yanatutuonyesha waziwazi kabisa kuwa adhabu za Kidini zimeruhusiwa katika Islam ili kuepeukana na ukandamizwaji wa wadhalimu; zaidi ya hayo,  vile vile inabakiza duniani haki sawa kwa wote; kutokomeza uchafuzi wa aina yoyote ile, na kuzifanya jamii zote ziishi kwa amani na upendo  chini ya nuru ya haki za Islam na kudumisha na kulinda  heshima na thamani ya mtu  dhidi ya walafi na waovu wa kila zama katika kila hali na sura mbalimbali.  Katika Sharia za Kiislamu, iwapo kutakuwa na mashahidi watatu katika kutoa ushahidi dhidi ya mtu aliyezini bila ya kuwapo na shahidi wa nne, basi mashahidi wote watatu wataadhibiwa kwa kuchafua heshima ya mtu.

 

Islam inataka pamoja na kumwadhibu mtuhumiwa iweze kulinda heshima za watu, wanawake, wanaume, masikini na matajiri.

 

Masharti yenye nguvu kwa ajili ya kuimarisha ‘adhabu za kidini’

 

Islam imeweka kanuni kali kabisa za kuthibitisha dhambi.  Iwapo masharti haya yatafuatwa zilivyowekwa kwa usahihi basi mahakimu hawataweza kufanya makosa hata kwa asilimia moja katika maamuzi yao hivyo inamaanisha kuwa hakuna hata mtu mmoja atakayedhulumiwa  hata kwa makosa. Miongoni mwa masharti haya, mtu huyo lazima astahili kuwa na sifa za hakimu. Swala hili limezungumziwa kwa undani zaidi na maulamaa katika kitabu kiitwacho Qadhaa ( hukumu ). Swala lingine linalostahili liwe ni ahadi na uaminifu. Swala hili limezungumziwa katika vitabu vya ushahidi Kwa hakika kijitabu hiki kidogo hakina nafasi ya kuyaleta yote hata hivyo tunawaleteeni machache tu kuhusu kuthibitisha kwa dhambi inavyoweza kutokea katika njia mbili kama zifuatazo:

 

1.  Kwa maelezo ya shahidi:

Iwapo mashahidi waadilifu watatoa ushahidi dhidi ya mtu mbele ya mahakimu wa Kidini, kwa mfano, iwapo wote watatoa kauli kuwa fulani bin fulani ni mhalifu basi inambidi hakimu huyo atekeleza adhabu za Kidini mara moja  baada ya kupata vithibitisho sahihi.  Hakimu hawezi kumsamehe baada ya kuthibitika kwa kosa lake hata kama atapendelea yeye mwenyewe au ataombwa na watu isipokuwa pale tu mhalifu mwenye atakapokiri na kutubu kwa uhalifu wake na kuomba msamaha na kula kiapo cha kutokutenda wala kurudia madhambi. Katika kesi hii,  mali yote iliyopatikana itarudishwa kwa mwenyewe; na hivyo hao hawatamkata mkono huyo mhalifu. [28]

 

2.. Kwa kukiri kwa mhalifu:

Hii inamaanisha kuwa iwapo mhalifu akiwapo mbele ya hakimu na akikiri makosa yake, mfano, kwa kusema : “Mimi nimezini na hivyo naomba kuadhibiwa kisheria”  na iwapo kwa mujibu wa masharti ya uthibitisho ikakamilika, basi  hakim Sharah anayo haki kamili ya kumwadhibu kwa mujibu wa adhabu zilizowekwa na Islam au kumsamehe kwa misingi kuwa huyo mtu ametubu kwa kweli na amekiri na kwamba hatarudia kutenda maovu. [29]

 

Tukio la kihistoria

 

Moja ya mienendo katika zama za upagani ilikuwa ni kutokuwa imara, kutokuwa na nguvu na watu dhaifu walikuwa daima wakiadhibiwa wakati matajiri na wenye urafiki walikuwa hawafikiwi na sharia. Wao kamwe walikuwa hawaadhibiwi kwa matendo yao yaliyokuwa yakiiaibisha jamii, Baada ya Mtume Muhammad s.a.w.w. kutangaza Utume, kikundi cha aina hii kiliendelea kuwapo katika dola ya Kislamu.

 

Siku moja, mwanamke mmoja aliyekuwa akitambulikana sana na kujulikana miongoni mwa makabila ya Kiarabu, alitenda kosa la uizi.  Mtume Muhammad s.a.w.w. aliwaamuru  watu wake wamkate mkono wake hadi vidole vinne. Kwa kuwa yule mwanamke alikuwa akitambulikana, kikundi cha watu kilimwendea Mtume Muhammad s.a.w.w. kumwombea msamaha.

 

Mtume Muhammad s.a.w.w. alisema : “Tofauti baina ya Waislamu na jamii zingine ni kwamba watu wote ni sawa mbele ya Shariah za Allah swt.  Islam haitofautishi baina ya tajiri na masikini, au baina ya mwenye nguvu na mnyonge.  Kwa kiapo cha Allah swt ! Lau Fatima binti ya Mtume Muhammad s.a.w.w. angalikuwa amefanya uizi, basi Mtume Muhammad s.a.w.w. angalimkata mkono wake pia.” [30] 

 

 

                                       TAMATI  WALHAMDULILLAH

 

VITABU VILIVYOKUSANYWA NA KUTARJUMIWA NA

AMIRALY  M. H.  DATOO  - P.O. Box  838 - BUKOBA TANZANIA

                            e-mail : datooam@hotmail.com

 

1.    TAJWID ILIYORAHISISHWA

2.    BWANA ABU TALIB a.s. MADHULUMU WA HISTORIA

3.    FADHAIL ZA IMAM ALI IBN ABI TALIB a.s.

4.    HUKUMU ZILIZOTOLEWA NA IMAM ALI IBN ABI TALIB a.s.

5.    UHARAMISHO WA KAMARI KATIKA ISLAM

6.    UHARAMISHO WA VILEO KATIKA ISLAM

7.    UHARAMISHO WA ULAWITI KATIKA ISLAM

8.    UHARAMISHO WA KUSEMA UONGO KATIKA ISLAM

9.    UHARAMISHO WA RIBA’ KATIKA ISLAM

10. MSAFARA WA IMAM HUSAYN IBN ALI a.s. MADINA – KARBALA

11. DALILI ZA QIYAMA NA KUDHIHIRI KWA IMAM MAHDI a.s.

12. KITABU CHA TAJWID

13. NDOA KATIKA ISLAM

14. MAKALA MCHANGANYIKO  No. 1

15. MAKALA MCHANGANYIKO  No. 2

16. KESI YA FADAK

17. UWAHHABI – ASILI NA KUENEA KWAKE

18. TAWBA

19. TADHWIN AL-HADITH

20. HEKAYA ZA BAHLUL

21. SHADA LA MAUA KUTOKA BUSTANI YA AHADITH

22. TAFSIRI YA JUZUU’ ‘AMMA

23. HIARI NA SHURUTISHO KATIKA ISLAM

24. WAANDISHI MASHIA KATIKA SAHIH NA SUNAN ZA AHL SUNNA

25.  USINGIZI NA NDOTO

26. MAJINA KWA AJILI YA WATOTO WAISLAMU

27. USAMEHEVU KATIKA ISLAM

28. QURBAA - MAPENZI YA WANANYUMBA YA MTUME S.A.W.W.

 

 

 



[1] Tuhaf ul-Qaul , uk.26

[2] Chuo cha Wananyumba ya Mtume Muhammad s.a.w.w. , j.1, uk. 13

[3] Safinat ul-Bihar, j. 1, uk. 549

[4]  Chuo cha Wananyumba ya Mtume Muhammad s.a.w.w. , j.1, uk. 11

[5] Nahjul Balaghah, uk. 266

[6] Nahjul Balaghah, uk. 142

[7] Nahjul Balaghah, uk. 103

[8]  Safinat ul- Bahar, j.2, uk. 207

[9] Al-Quran, Sura ‘Aaraf, Ayah 199 - 200

[10] Al-Quran, Sura Ali Imran, Ayah 134

[11] Al-Quran, Sura Ali Imran, Ayah 159

[12] Al-Mizan al - ‘i’tidal, j.8, uk. 402,

[13] Nahjul Balaghah, uk. 94

[14] Safinat ul- Bahar, j.2, uk. 207

[15] Safinat ul- Bahar, j.2, uk. 208

[16]  Muntahi al-A’mal, j.1, uk. 85

[17] Al-Quran, Sura Nahl, Ayah 126

[18] Muntahi al-A’mal, j.1, uk. 62

[19]  Maisha ya ibn Hisham, j.2, uk. 46 - 47

[20] Surah  Fath (48 ) Ayah 1-2

[21] Surah  Bani-Israil (17 ) Ayah 81

[22] Surah  Yusuf (12 ) Ayah 92

[23] Surah   Ahzab (33 ) Ayah 21

[24]  Ukhalifa hapa haumaanishi Ukhalifa baada ya Mtume Muhammad s.a.w.w.

   kwa misingi ya Din na Imani  kwa sababu hapa utawala wa kisiasa tu ndio

   unaomaanishwa. Hivyo msamaji mtukufu unaombwa kusoma Makala:na

   vitabu vinvyozungumzia maudhui haya ndipo utakapoweza kujua ukweli wa

    ukhalifa kwa undani. Hebu tujiulize : Je inawezekana kwetu sisi tukaanza kubadilisha miundo ya

    ukhalifa iwapo ni wa Allah swt au ni wa watu ?

[25]  Dastan – Rastan, uk. 255

[26] Hudud Wasail, uk.308

[27] Hudud Wasail, uk.311

[28] Mabani Takmilih al-Minhaj, j.1, uk. 185, swali nambari 148

[29] Mabani Takmilih al-Minhaj, j.1, uk. 176, swali nambari 140

[30] Islam na Fikara za kibinadamu, uk. 670


 

The .HTML version of this book is taken from
www.al-islam.org and ebooked by www.ShiaLibrary.com and www.islamkutuphanesi.com . May Allah be pleased with all.