Muujiza

Hali ya hewa ilikuwa shwari wakati wa kushambuliwa kwa mji wa Ta’if. Kulikuwa hakuna upepo. Kulitokea kwa tufani kali baada ya waporaji kuondoka, na ilichukua majani (kurasa) yote ya Qur’an Tukufu pamoja na vitabu vinginevyo na baadaye kutulia. Baada ya kutulia, hapakuwapo na hata karatasi moja iliyobakia juu ya ardhi ya mji wa Ta’if. Hakuna ajuaye zimepeperushwa kwenda wapi.

Chini ya jua kali, maiti zote za mashahidi zilioza vibaya sana katika kipindi cha siku kumi na sita. Hali ya hewa kuzunguka mji huo ilikuwa yenye kunuka na kuharibu hewa. Waislamu walimwomba, walilia kilio na kumbembeleza Ibn Shakban awaruhusu kuwazika majamaa zao. Hatimaye aliwakubalia, na hivyo walichimba mashimo mawili makubwa, wakatumbukiza katika mashimo hayo maiti zilizooza za wazazi, mababu, jamaa na watoto wao na kuwafukia kwa udongo. Hakuna maiti hata moja iliyoweza kutambuliwa; baadhi ya miili hiyo ilikuwa imebakia miili nusu au robo tu kwani ndege na wanyama pori walikuwa wamesambaza vipande vya miili hiyo huku na huko.Wao walikuwa wameruhusiwa kuvikusanya vipande hivyo vilivyokuwa vimezagaa huku na huko kwa sababu harufu mbaya ya maozo ilikuwa ikiwabughudhi sana hao Mawahhabi. Kwa hakika Waislamu walikuwa hawana lingine la kufanya isipokuwa ni kutafuta na kuokota vipande vya miili ya watu wao na kuzizika katika mashimo hayo mawili.

Kwa hakika tendo hili la kinyama la Mawahhabi la kuacha maiti za Mashahidi zibakie bila kuzikwa hadi kuoza zilikuwa ni hatua ya kulipiza kisasi. Hapa chini ninawaleteeni mashairi juu ya hayo:

‘Italeta harufu ya manukato, musisikitike enyi mlioanguka,

Nyumba haijengwi kabla ya kubomoka.’

Hali ya mashahidi (Allah swt awarehemu ) mbele ya Allah swt inaongezeka wakati miili yao inapoachwa kuoza na kuliwa na ndege na wanyama pori.

Maharamia hao waliteketeza kabisa makaburi za ma-Sahaba, Awliya' na Maulamaa baada ya kuwaua Waislamu wa Ta’if na kugawana mali waliyokuwa wamepora. Wao hata walithubutu kulichimba kaburi la ‘Abdullah ibn ‘Abbas, Sahaba mpenzi wa Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa ajili ya kutaka kuchoma moto mifupa yake, lakini waliogopa pale waliponusa harufu ya manukato iliyokuwa ikitokea kaburini wakati walipokuwa wamepiga kwa mara ya kwanza kwa sululu. Wao walisema: “Kuna shetani mkubwa kaburini humu. Hivyo inatubidi kulilipua kaburi hili na mabaruti kuliko kupoteza wakkati wetu katika kulichimba.” Ingawaje wao walijaribu kwa jitihada zao zote kwa kujaribu kulilipua kaburi hilo kwa kuweka unga mwingi wa baruti, lakini halikulipuka na hivyo waliondoka kwa mshangao. Kaburi hilo liliachwa sawa na ardhi kwa muda wa miaka kadhaa, na hapo baadaye, Sayyid Yasin Effendi aliweka uzio mzuri sana na kulihifadhi kaburi hilo lisisahaulike.

Mahramia hao hao wamekuwa wakijaribu mara nyingi mno kufumua makaburi ya Sayyid ‘Abd al-Hadi Effendi pamoja na Maulamaa wengi, lakini wamekuwa wakizuiwa kufanikiwa katika nia zao mbaya kwa karama (miujiza) tofauti tofauti katika kila kaburi. Walipoona kuwa wao hawafanikiwi katika uovu wao huo, hatimaye waliamua kuacha kuendelea na hamu yao ya kufumua makaburi.

‘Uthman al-Mudayiqi na Ibn Shakban vile vile walitoa amri za kubomolewa kwa Misikiti pamoja na Vyuo (Madrassah) viende sambamba na kubomolewa kwa makaburi. Yasin Effendi, mwanachuoni wa Ahl as-Sunna aliwauliza: “Je ni kwa nini munataka kubomoa hata Misikiti ambayo imejengwa kwa ajili ya kufanyia ibada za Allah swt na kusali sala za Jama’a? Iwapo nyinyi mwataka kuubomoa Msikiti huu kwa ajili ya kaburi la ‘Abdullah ibn ‘Abbas (r.a) lipo hapa, basi ninawaambieni kuwa kaburi lake liko nje ya Msikiti huu mkubwa. Hivyo, si muhimu kuubomoa Msikiti huu” Kwa maneno hayo, Uthman al-Mudayiqi na Ibn Shakban hawakuwa na jibu lolote. Lakini, Matu, mzindiqi miongoni mwao, alitoa kauli ya kashfa: “Chochote kile chenye kushukiwa na kutuhumiwa ni lazima kiteketezwe.” Kwa hayo Yasin Effendi aliuliza: “Je kuna chochote kile kinachoshukiwa kuhusu Misikiti?” na mhalifu huyo hakuweza kujibu chochote. Baada ya ukimya mrefu, ‘Uthman al-Mudayiqi alisema; “Mimi sikubaliani na nyote wawili,” na aliamrisha, “Msibomoe Msikiti, teketezeni makaburi !.”