SEHEMU YA KWANZA

(1) UWAHHABI : ASILI NA KUENEA KWAKE

Katika zama za utawala wa Uthmaniyyah (Ottoman Empire), tawala zote ambazo zilikuwapo katika bara la Uarabu, kila jimbo lilikuwa na maofisa waliokuwa wameteuliwa kutoka serikali kuu. Baadaye, kila mkoa isipokuwa Hijaz ilikuwa mikononi mwa wale walioweza kuzinyakua na kuwa tawala za Kifalme.

Imani za Mawahhabi zilizoenezwa na Muhammad ibn ‘Abd al - Wahhab zilikuwa zimeshabadilika kuwa katika sura za kisiasa katika kipindi kifupi katika mwaka 1150 A.H.( 1737) na zilienea Bara zima la Arabia. Baadaye, kwa amri za Khalifa wa Istanbul, Muhammad ‘Ali Pasha, Gavana wa Misri, aliikomboa Arabia kwa msaada wa majeshi ya Misri.

‘Abd al-‘Aziz ibn Muhammad, aliyewaamini Mawahhabi, alitangaza vita kwa mara ya kwanza katika 1205 A.H. (1791) dhidi ya amir wa Makkah, Sharif Ghalib Effendi. Wao walikuwa wamekwisha eneza Uwahhabi kisirisiri hadi hapo. Wao waliwaua na kuwatesa Waislamu wengi mno, kuwachukua wanawake na watoto wao mateka na kuzipora mali zao zote.

Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab alitokana na kabila la Bani Tamim. Alizaliwa katika kijiji cha Uyaina karibu na mji wa Huraimila huko katika jangwa la Najd, mwaka 1111 A.H.(1699) na kufa 1206 A.H.( 1792). Hapo awali alikuwa na nia ya kufanya biashara, hivyo alisafiri hadi Basra, Baghdad, Iran, India na Damascus, ambako kote huko alijipatia sifa la jina kama Sheikh wa Najdi kwa sababu za ujanja na tabia yake.Yeye aliona na kujifunza mambo mengi katika sehemu hizi na hivyo akawa na hamu ya kuwa kiongozi mkubwa. Hivyo ili kutaka kutimiza hamu yake hiyo ilimbidi abuni njia moja iliyokuwa tofauti na njia zinginezo ili aweza kutimiza malengo yake, na kwa kujitayarisha kwa hayo, alianza kuhudhuria mihadhara ya maulamaa wa Kihanbali waliokuwapo katika Mji Mtukufu wa Madinah na baadaye huko Damascus kwa kipindi fulani. Wakati aliporejea Najd, alianza kuandika makala juu ya maudhui ya dini kwa ajili ya wanakijiji wake.Katika kuandika makala hayo,yeye alikuwa akiongezea fikara zake alizokuwa amezipata kutoka makundi ya bid’a ya Mu’tazila na wengineo. Wanakijiji wengi waliokuwa masikini majahili, hususan wakazi wa Dar’iyya na chifu wao jahili, Muhammad ibn Sa’ud, walikuwa wakimfuata Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab. Waarabu walikuwa wakiheshimu mno ukabila na kwa kuwa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab alikuwa si kutoka kabila maarufu, basi alimtumia Muhammad ibn Sa’ud kama chombo kwa kuutangaza fitna yake mpya aliyokuwa ameiita Uwahhabi. Yeye alijitambulisha kama Qadhi (mkuu wa mambo ya dini ) na Muhammad ibn Sa’ud kama Hakim (mtawala). Kwa hila zake alikwishafanya mabadiliko katika katiba yao kuwa wao hawatarithiwa na mtu yeyote yule isipokuwa watoto wao tu.

Katika mwaka 1306 (1888) wakati ambapo kitabu kiitwacho Mir’at al-Haramain kilipoandikwa, kiongozi wa Najd alikuwa ‘Abdullah ibn Faysal, kutokea kizazi cha Muhammad ibn Sa’ud, na Qadhi pia alikuwa ametokana na kizazi cha Muhammad ibn ‘Abd al-Wahhab.

Baba yake mzazi wa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab, ‘Abd al-Wahhab, ambaye alikuwa ni mcha Mungu, ‘alim halisi katika Madina, ndugu yake Sulaiman ibn ‘Abd al-Wahhab na waalimu wake walikuwa wamekwisha tambua kutoka maneno, matendo, ishara na mawazo yake, ambayo mara kwa mara alikuwa akidhihirisha katika sura ya maswali alipokuwa mwanafunzi huko Madina, kuwa atakuwa mpotofu ambaye ataidhuru mno Islam kwa undani katika kipindi kifupi kijacho. Wao wote kwa pamoja walimuasa na kumnasihi aache mawazo yke hayo ya upotoshi na vile vile walikuwa wakiwashauri Waislamu wote kwa ujumla wasimfuate na wajiepushe na Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab. Lakini katika muda mfupi tu walikumbana na jambo walilokuwa nalo khofu, na yeye alianza kueneza uzushi wake huo kidhahiri kwa jina la Uwahhabi. Kwa ajili ya kuwapotosha majahili na wapumbavu, yey alijitokeza kwa mawazo ya kurekebisha na kuzua mambo ambayo hayakubaliani na vitabu vya maulamaa wa Islam. Yeye alithubutu kwa kishindo kuwatuhumu Waislamu wa Ahl as-Sunnah wal Jama’a kuwa ni makafiri. Yeye alikuwa akiamini kuwa ni shirk kumwomba Allah swt kwa kupitia Mtume Muhammad s.a.w.w. au Mitume mingine a.s. au ma-Awliya’’ na kuzuru makaburi.

Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab alikuwa akimwona mtu yeyote yule anayesali na kuomba karibu na kaburi kuwa ni Mushrik. Yeye alisisitiza kuwa Waislamu wasemao kuwa mtu fulani au kitu fulani mbali na Allah swt kimefanya hivi au vile,kwa mfano, kwa kusema kuwa dawa fulani na fulani zimeponyesha au mimi nimeweza kupata kile nilichokuwa nikihitaji kwa kupitia Wasila wa Mtume Muhammad s.a.w.w. au au mawali fulani fulani basi hao wote ni Mushrik. Ingawaje waraka wa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab hazikuwa chochote isipokuwa ni uongo na fitina tu, lakini majahili hawakuweza kutofautisha baina ya ukweli na uongo, wale wasiokuwa na kazi, wazururaji, majahili, wenye kuvizia bahati na wenye nyoyo ngumu walizipokea mawazo yake na kujiweka bega kwa bega pamoja naye na kuamini wale Waislamu waliokuwa katika njia sahihi kuwa wote kwa pamoj ni makafiri.

Wakati Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab alipowaomba ruhusa watawala wa Dar’iyya kutaka kueneza imani zake za uzushi kwa kupitia utawala wao, wao walimpokea kwa mikono miwili kwa matumaini ya kupanua eneo la utawala na kuzidi kwa nguvu zao. Wao walijitolea kwa hali na mali kueneza imani hizo kila mahala. Wao hata walithubutu kutangaza vita dhidi ya wale wote waliokuwa wakimkataa na kumpinga. Watu Mahayawani na wateka nyara wa jangwani walikuwa wakishindana katika kujiunga na jeshi la Muhammad ibn Sa’ud wakati pale iliposemwa kuwa ni halali kumwua na kupora mali za Waislamu. Katika mwaka 1143 ( 1730 ), Muhammad ibn Sa’ud pamoja na Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab wakishirikiana kwa pamoja walifikia maafikiano kuwa wale wote ambao hawata kubalia Uwahhabi, basi watakuwa ni makafiri na Mushrik, na hivyo ilikuwa ni halali kwao kuwaua na kutaifisha mali yao yote, na walitangaza rasmi amri hiyo miaka saba iliyofuatia. Hapo ndipo Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab alipoanza kutunga uzushi wa ijtihad pale alipokuwa na umri wa miaka thelathini na miwili na aliitangaza kidhahiri pale alipokuwa na umri wa miaka arobaini.

As-Sayyid Ahmad ibn Zaini Dahlan, Mufti wa Makkah, akielezea katika somo la Al-fitnat al-Wahhabiyya (kitabu cha Al-Futuhat al-Islamiyya) kuhusu imani za Uwahhabi na dhuluma na maafa zinazowapata Waislamu kutoka kwa Mawahhabi. Yeye anaandika: “Ili kutaka kuwadanganya ma’ulamaa wa Ahl as-Sunnah katika miji ya Makkah na Madinah, wao waliwatuma watu wao katika miji hizo, lakini watu wao walishindwa kujibu maswali ya Maulamaa wa Kiislamu. Imekuwa dhahiri kuwa wao kwa hakika walikuwa ni wazushi majahili. Kulipitishwa sharia ikiwasema kuwa ni makafiri na kuenezwa kila mahala. Shariff Mas’ud ibn Sai’d, Amir wa Makkah, aliamrisha kuwa Mawahhabi watiwe mahabusu. Baadhi ya Mawahhabi walikimbilia Dar’iyya na kuelezea yale yaliyowapata.”

Maulamaa wa Hijaz, wanaotokana na Madhehebu yote manne, akiwemo Sulaiman ndugu yake Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab na waalimu wake waliokuwa wamemfundisha, walivisoma vitabu vya Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab na wakatayarisha katika sura ya vitabu majibu ya maandiko yake, yenye kuleta utenganishi na kuidhuru Islam, kwa ajili ya kuwatanabahisha Waislamu, wajitahadhari na kujitenga na upotoshi wa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab.

Kwa hakika vitabu hivi havikuweza kusaidia zaidi na badala yake ziliongeza hasira na chuki za Mawahhabi dhidi ya Waislamu na kumzuzua zaidi Muhammad ibn Sa'ud awashambulie Waislamu na kusababisha umwagikaji mwingi wa damu. Yeye alitokana na kabila la Bani Hanifa, kabila ambalo alitokamo mzushi wa Utume Musailamat al-Kadh-dhab. Muhammad ibn Sa'ud alikufa katika mwaka 1178 (1765), na hivyo kwa mujibu wa katiba waliyokuwa wametunga, mwanake ‘Abd al-‘Aziz alimrithi. ‘Abd al-‘Aziz aliuawa kwa kupigwa kisu tumboni, katika msikiti wa Dar’iyya katika mwaka 1217 (1803). Na hapo mtoto wake Sa’ud ibn ‘Abd al-‘Aziz ndiye aliyekuwa chifu wa Mawahhabi. Hawa wote watatu walijitolea kimabavu kama kwamba walikuwa wakishindana, katika kumwaga damu ya Waislamu ili waweze kuwadanganya na kuwapotosha Waarabu na kueneza Uwahhabi.

Mawahhabi wanadai kuwa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab alikuwa akihubiri mawazo yake kwa ajili ya kujipatia utukufu katika imani yake katika upweke wa Allah swt na kuwakomboa Waislamu wasitumbukie katika Shirk. Wao wanadai kuwa Waislamu wamekuwa wakitenda dhambi la Shirk kwa karne sita mfululizo na hivyo yeye alikuja kuirejesha upya dini ya Waislamu. Yeye anazitoa Ayah za Qur’an Tukufu nambari 5 ya Surah al-Ahqaf, Ayah 106 surah Yunus, Ayah 14 sura al-Ra’d ili kwamba Waislamu wote wakubaliane na mawazo yake. Hata hivyo, zipo Ayah nyingi kama hizo, na Maulamaa wanasema kuwa hizo Ayah zimekuwa zikiwazungumzia makafiri waliokuwa wakiabudu miungu na masanamu au waliokuwa washirikina.

Kwa mujibu wa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab, Mwislamu anakuwa Mushrik pale anapoomba kwa Mtume Muhammad s.a.w.w. , au kwa Mtume a.s. mwingine, au wali au mcha Mungu karibu na kaburi au mbali kutoka hapo, yaani, iwapo anapomwomba msaada wa kutokana na shida aliyonayo, au anapoomba kutetewa mbele ya Allah swt kwa kutaja jina lake au anapotaka kuzuru kaburi lake. Allah swt anatuambia kuhusu makafiri wanaoabudu miungu na masanamu katika Ayah ya tatu ya surah al-Zumar, lakini Mawahhabi wanaonyesha Ayah hii kama ndio waraka wa kuhalalisha utumiaji wao wa neno la Mushrik kwa ajili ya Waislamu waombao kwa kuwaweka Mitume a.s. au Mawalii kama ndio watu walio baina yao na Allah swt. Wao wanasema kuwa hata Mushrik waliokuwa wakiabudu miungu pia awaikuwa wakijua kuwa vyote vilikuwa vimeumbwa na Allah swt. Wao wanasema kuwa Allah swt amebainisha: Na kama ukiwauliza, Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akalitiisha jua na mwezi?” Bila shaka watasema, Allah (Surah Ankabut, ayah ya 61na Sura Zukhruf, Aya ya 87 ). Wao wanadai kuwa hao Mushrik walikuwa hivyo makafiri Mushrik si kwa sababu walikuwa wakiamini hivyo bali wao walizungumza kama ilivyosemwa katika Ayah ya 3 ya Surah az-Zumar: Wale wanaofanya marafiki na wale mbali na Allah wanasema, “Wao wanatusaidia kutufikisha karibu (ya Allah swt) kwa kututetea mbele Allah’” Wao wanadai kuwa Waislamu wanaoomba katika makaburi ya Mitume, ma-Awliya’ kwa utetezi na misaada basi wanakuwa Mushrik kwa kusema hivyo.

Ni jambo la kipumbavu kabisa kwa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab kuwasema Waislamu wanakuwa makafiri na Mushrik kwa Ayah hiyo. Kwa sababu, makafiri wanawaambudu masanamu ili kwamba ni masanamu hayo tu ndiyo yatakayowasaidia kuwatetea wao; wao wanamwacha Allah swt na badala yake wanakluwa na imani moja tu ya kuwaomba miungu na masanamu hiyo kuwa watetezi wao. Lakini ni uhakika uliyo bayana kuwa Waislamu kamwe hawawabudu Mitume a.s. au Ma-Awliya’ lakini wanayo imani kuwa kila kitu kinatoka kwa Allah swt. Sisi tunapenda kuwa hao ma-Awliya’ wawe ni Wasila wetu. Makafiri wanaamini kuwa miungu na masanamu yao inawaombea chochote kile wakitakacho na kumfanya Allah swt kuwatimizia chochote kile wakitakacho.

Wakati ambapo, Waislamu wanaomba msaada wa Awliya’ ambao wanawajua kuwa hao ndio watumwa wapenzi wa Allah swt, kwa sababu Allah swt ameahidi katika Qur’an tukufu kuwa Yeye atawaruhusu waja wake wapenzi kuwatetea na atakubali utetezi wao na Sala na kwa sababu Waislamu wanaamini ubashiri mzuri katika Qur’an. Kamwe huwezi kulinganisha baina ya kafiri anayeabudu miungu na masanamu na Waislamu wakiomba msaada wa Awliya’. Waislamu na Makafiri wote ni binadamu kwa miili, na wanafanana kwa kuonekana, lakini Waislamu ni marafiki wa Allah swt na watakuwa Peponi kwa milele wakati ambapo Makafiri ni maadui wakubwa wa Allah swt na watakuwapo kwa milele katika Motoni. Kujionesha kwao hakumaanishi kuwa watabakia vivyo hivyo daima. Wale wanaowaabudu masanamu na miungu ambao ndio maadui wakubwa wa Allah swt, yatawafikisha hadi kuingia Jahannam. Lakini wale wanaowafanya marafiki wa Allah swt kuwa marafiki wao, basi Allah swt atawabariki na kuwarehemu. Ipo Hadith isemayo: Rehema za Allah swt zinateremka pale waja wake wapenzi wanapotajwa, nayo pia inatuonyesha kuwa Allah swt ataonyesha rehema zake na misamaha yake pale Mitume a.s. na Awliya’ wanapoombwa.

Waislamu wote kwa pamoja wanatambua waziwazi kuwa Mitume a.s. na Awliya' si watu wa kuabudiwa na wala si washiriki wa Allah swt. Waislamu wanatambua vile vile kuwa wapo waja wa Allah swt ambao hawastahili kuombwa na papo hapo wapo waja wengineo ambao maombi yao hukubaliwa Kwake. Katika surah Maidah, Ayah ya 35 tunaambiwa: “Tafuteni Wasila wa kunifikia Mimi” Allah swt anamaanisha kuwa Yeye atakubalia ibada za waja wake halisi na kuwapatia kile wakiombacho. Tunapata Hadith sharif iliyonakiliwa na al-Bukhari, Muslim na katika Kunuz ad-daqaiq, isemayo: “Kwa hakika, wapo wacha Mungu halisi wa Allah swt ambapo Yeye anawaumbia kile walacho kiapo; kamwe hawasingizii.” Waislamu wanawachukulia Awliya' kama Wasila na kutegemea maombi na msaada wao kwa sababu wao wanaamini Ayah na hadith za hapo juu.

Ingawaje wapo baadhi ya makafiri wanaowaabudu masanamu wakidai kuwa ingawaje masanamu wao si waumbaji lakini Allah swt tu ndiye muumba, hivyo wao wanaamini kuwa masanamu wao wanastahili kuabudiwa kwa sababu masanamu hao wananao uwezo wa kumfanya allah swt awatimizie kile wakiombacho. Wao wanawashirikisha masanamu wao pamoja na Allah swt. Iwapo mtu yeyote atakayemwomba yeyote yule ambaye ameshirikishwa na Allah swt kwa ajili ya maombi yake basi huyo mtu atakuwa kafiri. Lakini yule asemaye kuwa: “Kwa hakika maombi yangu hayatakubaliwa kwa amri yake. Yeye ni sababu tu. Allah swt anawapenda wale ambao wanaojiimarisha katika njia Yake. Ni yeye anaumba kwa matokeo ya sababu. Mimi namwomba msaada huyu mtu kwa sababu ya kuwa imara katika njia ya Allah swt, lakini nategemea maombi yangu kukubaliwa na Allah swt. Mtume Muhammad s.a.w.w. alikuwa ni mja wake mpenzi na mimi ninazifuata Sunnah zake katika utiifu Wake,” basi atapata thawabu. Iwapo maombi yake yatakubaliwa basi atamshukuru Allah swt; na kama sivyo, basi itabidi aridhike kwa amri ya Allah swt. Kuabudu masanamu na miungu kwa Makafiri si sawa na vile Waislamu wawaombavyo Awliya' kwa maombi, utetezi na misaada. Hakuna mtu mwenye akili timamu ambaye atasema kuwa makundi mawili haya yako sawa bali atasema kuwa makundi haya mawili yapo tofauti kabisa. Hakuna muumba isipokuwa Allah swt pekee.

Mushrik na Makafiri, hata hivyo, huwachukulia masanamu wao kuwa ni ilah ( miungu ) au ma’bud ( anayestahili kuabudiwa ) na huwa wanawaabudu ingawaje wao wanatambua waziwazi kuwa masanamu kamwe hawawezi kuwaumbia chochote. Baadhi yao wanakuwa mushrik kwa kuwachukulia masanamu wao kuwa ni ilah ambapo wengine kwa kuwaabudu au kuwachukulia kama ma’abud. Watu hao sio Mushrik kwa sababu wanasema kuwa masanamu yao itawatetea na kuwafanya karibu zaidi ya Allah swt, bali wao ni Mushrik kwa sababu wao wanawachukulia kama ma’bud na kwa sababu wanawaabudu.

Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, “Utafika wakati ambapo Ayah zilizoteremshwa kuhusu Makafiri zitatumika dhidi ya Waislamu.” na “Ninayo khofu sana kuwa watu watakuja kuzitumia Ayah za Qur’an kwa matumizi ambayo Allah swt hazikubalii.” Hadith hizi mbili zinadalilisha kuwa watu wasio na dini watatokezea na kuzibandika Waislamu Ayah zile zilizoteremshiwa Makafiri na hivyo kuichezea Qur’an.

Waislamu wanazuru makaburi ya wale, wanaowaamini kuwa wanapendwa na Allah swt. Wao wanamwomba Allah swt kwa kuwapitia waja wake wanaopendwa naye. Mtume Muhammad s.a.w.w. pamoja na ma-Sahaba watukufu pia walifanya hivyo na sisi pia tumeambiwa kufanya hivyo.

Mtume Muhammad s.a.w.w. baada ya kumlaza kaburini mama yake na Imam Ali a.s. Fatimah bint Asad na aliomba: “Ewe Mola wangu ! Mrehemu Mama Fatima bint Asad ! Mrehemu mno kwa mapenzi ya Mtume Wako na Mitume waliyokuwa wamenitangulia mimi !”

Mtu mmoja kipofu alimwomba Mtume Muhammad s.a.w.w. amwombee duaa ili apone upofu wake. Mtume Muhammad s.a.w.w. alimwambia aombe hivi: “Ewe Mola wangu! Kwa hakika mimi ninakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako Mtume wa Rehma, Ewe Muhammad! Kwa hakika mimi naelekea kwa Mola wangu kupitia kwako katika haja yangu ili ikubaliwe, ewe Mola wangu ! Mfanye Muhammad kuwa muombezi wangu.”

Mtume Adam a.s. aliomba: “Ewe Mola wangu! Naomba nisamehe kwa mapenzi ya mwanangu Mohammad s.a.w.w.!” wakati alipoteremka katika kisiwa cha Serandib (Ceylon) baada ya kula tunda la mti alilokuwa amepigiwa marufuku na Allah swt. Na Allah swt alibainisha: “Ewe Adam ! Mimi ningalikuwa nimekubali utetezi wako iwapo ungekuwa umeomba msamaha kupitia Muhammad kwa ajili ya viumbe vyote vilivyopo duniani na mbinguni.”

Umar alimchukua ‘Abbas (r.a.) kwa ajili ya kuomba mvua kwa nia ya kumchukua kama Wasila, na maombi yake yalikubaliwa.

Katika historia kuna matukio na habari nyingi zielezeazo ruhusa kuzuru makaburi na kuhusu kuwataja watu waliokwisha kufa kuwafanya Wasila katika kuomba duaa.

Muhammad ibn Sulaiman Effendi anadondoa kuwa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab alikuwa mwovu na aliyepotoka na kwamba alikuwa na tabia ya kutumia Ayah za Qur’an na Hadith visivyotakiwa. Yeye ameandika:“Ewe Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab! Usiwatukane Waislamu ! Mimi ninakushauri kwa kiapo cha Allah swt. Mwambie ukweli yeyote yule asemaye kuwa kuna muumba mwingine mbali na Allah swt! Msahihishe huyo kwa kumtolea uthibitisho ulio sahihi! Wasilamu kamwe hawawezi kuitwa Makafiri! Wewe pia u Mwislamu pia. Inawezekana ukamwita mtu mmoja kuwa ni Kafiri kuliko kuwaita mamilioni. Kwa hakika ni dhahiri kuwa yeyote yule ajitoaye nje ya jumuiya yake basi anaangukia hatarini. Katika surah an-Nisa, Ayah ya 115 tunaambiwa: “Na atakayemwasi Mtume baada ya kumdhihirikia uwongofu na akafuata njia isiyokuwa ya Waislamu, tutamgeuza alikogeukia mwenyewe na tutamwingiza katika Jahannam; napo ni pahali pabaya kabisa pa mtu kurudia.” Kwa hakika Ayah hii inawasema wale waliojitoa katika madhehebu ya Kiislamu.

Zipo Hadith nyingi mno zinazoelezea kuwa imeruhusiwa kuzuru makaburi. Ma-Sahaba walikuwa wakiizuru kaburi ya Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa mara nyingi mno kwa ajili ya kutaka kupata baraka, na kumeandikwa makala na vitabu vingi mno juu ya baraka za kuzuru hapo.

Kamwe haidhuru kuomba kwa kupitia Mawali’ (Wasila), kuomba kwa kutaja majina yao. Ni imani potofu kuamini kuwa mtu atajwaye atakuwa akimwathiri mwombaji na atamfanyia chochote kile atakacho na atakuwa akijua mambo asiyoyajua.Waislamu kamwe wasituhumiwe kwa mambo kama hayo kwani wao hawaamini hivyo. Waislamu wanaomba kwa kupitia waja wake wapenzi wa Allah swt wawe kama watetezi wao, wawaombee wao. Sifa ya kuumba kile kiombaccchwo ni kwa ajili ya Allah swt tu peke yake na wala hakuna mwingine. Allah swt anawataka waja wake wamwombe Yeye kama vile alivyoamrisha katika Surah al-Maidah, Ayah 27: Allah huwakubalia (ibada,duaa n.k.) wale awapendao. Watu waliokufa hawatakiwi kutimiza kile walichoombwa bali wanakuwa ni watu wa kati kwa Allah swt kuwatimizia kile walichomuomba Allah swt kutimiziwa. Hairuhusiwi kuwaomba wafu kitu chochote na Waislamu hawafanyi hivyo. Inaruhusiwa kuwataka wawe watu wa kati katika kutimiziwa maombi yao. maneno Istighatha, Istishfa’ na tawassul vyote hivyo vinamaanisha kuomba kwa Wasila .

Allah swt ndiye pekee muumbaji na ni desturi Yake kumfanya mja wake kuwa Wasila au sababu ya kuumbwa kwa kitu kingine. Yeyote yule atakaye Allah swt aumbe jambo basi achukue Wasila ambacho ndiccho kitakachokuwa Wasila wa kuumbwa kitu hicho. Mitume yote imekuwa ikitumia Wasila katika masuala yao.

Allah swt anasifia mno matendo ya kutawassuli na vile vile Mitume a.s. pia wametuamrisha hivyo. Matukio ya kila siku pia yandalilisha umuhimu wake na inambidi mtu ang’angie ili aweze kufanikiwa katika kutimiziwa haja zake. Ni muhimu kutambua kuwa Allah swt tu ndiye afanyaye hizo sababu kuwa sababu za vitu, na huziumba baada ya mtu kuzishikilia kwa madhubuti sababu. Mtu yule anayeamini anaweza kusema: “Nimejipatia kitu hiki kwa kutokana na sababu hiyo.” Sentenso hii haimaanishi kuwa hiyo sababu ndiyo iliyoumba kitu hicho, bali inamaanisha kuwa Allah swt amekiumba kitu hicho kwa kupitia sababu. Kwa mfano, sentenso, “dawa nilizozitumia zimeniponya”; “ Mgoonjwa wangu amepona baada ya mimi kuchukua nadhiri ya Sayyidat Fatimah”; “Supu imenikinaisha,” na “maji yametuliza kiu changu,” vyote hapo vinamaanisha sababu hizo kuwa ni Wasila. Ni muhimu kutambua kuwa Mwislamu asemaye kauli kama hizi huwa anaamini hivyo. Wale wanaoamini hivyo kamwe hawawezi kuitwa Makafiri. Mawahhabi nao pia wanasema kuwa inaruhusiwa kuoma kitu kutoka wale walio karibu na hai. Wao wanaomba mmoja kwa mwinginw na hata kuwaomba maofisa wa serikali kwa mambo mengi.; hata kuthubutu kusema kuwa wanawaomba kuwatimizia maombi yao. Kwao ni shirk kuwaomba waliolkufa au waliombali, bali si shirk kuwaomba walio hai. Hata hivyi iwe wazi kuwa Maulamaa wa Dini hii wanasema kuwa si shirk kwa sababu wa pili hayupo na hakuna tofauti baina yao. Kila Mwislamu anaamini kuwa kile kilicho faradhi ni faradhi na kile kilicho haraamu ni haraamu tu. Na vile vile ni imani yetu ya msingi kuwa Allah swt ndiye muumba pekee na afanyake kwa kudura zake na wala hakuna mwingine anayeumba wala mwenye uwezo kama Allah swt. Iwapo Mwislamu atasema, “Mimi sitasali,” basi itaeleweka kuwa yeye hatasali wakati huo au katika mahala hapo, au kwa sababu amekwisha kusali.Si haki kwa mtu yeyote kumtuhumu kuwa yeye hatasali kamwe.Kwa sababu, kuwa kwake Mwislamu itawazuia wengine wasimwite kafir au Mushrik. Hakuna mtu yeyeote mwenye haki kumwita Mwislamu ati ni kafiri au Mushrik kwa sababu amezuru makaburi, awaombaye waliokufa kwa msaada na utetezi au asemaye “Maombi yangu kadhaa wa kadhaa yakubaliwe,” au “Ewe Rasulullah! Tafadhali naomba unitetetee mimi !” Kuwapo kwake Mwislamu kunadalilisha kuwa maneno na matendo yake yote yapo kwa mujibu wa imani iliyokubaliwa, halali na nia.

Imani potofu na maandiko ya Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab yatavunjika na kukanushwa katika misingi yake kwa nguvu za ufahamu na uamuzi kwa kutokana na maelezo yafuatayo. Katika kuongezea, kwa hakika kumeandikwa vitabu vingi mno kwa kuthibitisha kuwa Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab alikuwa ni mtu aliyepotoka, amewatukana Waislamu na amefanya njama zake zote za kuungamiza Uislamu undani mwake. Sayyid ‘Abd ar-Rahma (r.a.), Mufti wa Zabid, Yemen, ameandika kuwa itatosheleza kabisa kuandika Hadith ifuatayo ili kumthibitishia yeye kuwa alikuwa amepotoka: “Baadhi ya watu watatokezea Mashariki mwa bara la Arabia. Wao watasooma Qur’an tukufu. Lakini Qur’an tukufu haitawashuka kooni mwao. Wao wataiacha Islam kama vile mshale unavyouacha upinde. Wao wananyoa nyuso zao.” Nyuso zao kunyolewa inamaanisha waziwazi kuwa ni wale watu ambao wanasemwa kupotoka ni wafuasi wao. Hakuna haja ya kupekua vitabu vingine baada ya kuisoma Hadith hii. Imeamriwa katika kitabu cha Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab kuwa wafuasi wake wanyoe ngozi ya kichwa pamoja na nywele na pembeni za uso. Amri kama hii haipatikani katika madhehebu zote sabili na mbili za Kiislamu.

MWANAMKE AMNYAMAZISHA IBN ‘ABD AL-WAHHAB

Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab vile vile aliwatolea wanawake amri ya kunyoa nywele zao zote. Alitokezea mwanamke mmoja, kwa ujasiri akamwambia: “Nywele ni pambo muhimu kwa mwanamke kama vile ilivyo ndevu kwa ajili ya mwanamme. Je amri hii inataka kuwafanya wanaadamu wajinyime opambo walilojaaliwa na Allah swt ?” Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab hakuweza kumjibu mwanamke huyo.

Ingawaje kuwa mambo maovu mengi katika imani potofu za Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab, zipo imani tatu kuu:

1. Yeye amefundisha kuwa matendo yanafanya sehemu ya imani na yeyote yule anayepuuzia faradhi (kwa mfano, hajatimiza sala mara moja kwa sababu ya uvivu au hajatoa Zaka kwa muda wa mwaka mmoja kwa sababu ya ubahili, ilhali anajua kuwa sala na zaka vyote hivyo ni faradhi) basi atageuka kuwa kafiri, na lazima auawe na mali yake yote igawiwe miongoni mwa Mawahhabi.

2. Wao wanaamini kuwa ni tendo la shirk kuwafanya Wasila Mitume a.s. na Awliya'’ na kuomba kwa kupitia wao kwa ajili ya kutimizika haja yake au kuwa katika hali ya amani dhidi ya khofu. Wao wanasema kuwa ni haramu kabisa kukisoma kitabu cha sala kiitwacho Dala’il al-Khairat.

3. Wao wanasema kuwa ni ushirikina kwa kujenga misikiti karibu na makaburi ya watu wema, kuwasha taa au vibatari katika misikiti hiyo kwa ajili ya wale wafanyao ibada au kwa kutoa misaada kutoa nadhiri ya kuchinja mnyama kwa ajili ya watu waliokufa. Kwao kila mojawapo la tendo hilo ni katika sura ya ‘ibada ya mtu sambamba na Allah swt.

Makaburi yote ya Ahl al-Bayt a.s.,Masahaba wote, ma Awliya'’ na Mashahidi yaliteketezwa isipokuwa lile la Mtume Muhammad s.a.w.w. wakati Sa’us ibn ‘Abd al-Aziz alipoishambulia Makkah na Madinah.Makburi hayakuweza kutambuliwa. Ingawaje wao wamejaribu hila zao za kutaka kuteketeza kaburi la Mtume Muhammad s.a.w.w., kwani wale waliokuwa wameinua mapanga na mashoka, waligeuka kuwa wehu au walipooza miili yao, na hivyo hawakuthubutu kutenda maovu yao hayo. Wao walipoishika Madinah,Ibn Sa’ud aliwakusanya Waislamu na akiwa tuhumu alisema:“Dini yenu kwa sasa imekamilshwa na Mawahhabi na Allah swt ameridhika nanyi. Wazazi wenu walikuwa makafiri na mushrik. Kamwe musiifuate dini yao! Waambieni watu wote kuwa wao walikuwa ni makafiri. Imeharamishwa kusiomama mbele ya kaburi la Mtume Muhammad s.a.w.w. na kuomba. Nyie munaweza kusema: “As-salaamu ‘ala Muhammad” wakati mpitapo katika msikiti. Hamuruhusiwi kuomba utetezi wake mbele ya Allah swt.”