UWAHHABI Asili na kuenea kwake( Uchambuzi wa kihistoria )

Kimekusanywa na kutarjumiwa na : AMIRALY M. H. DATOO

MANENO MACHACHE

KWA JINA LA ALLAH SWT MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

Natoa shukurani zangu kwa Allah swt, Mtume Muhammad s.a.w.w. pamoja na Ahli Bayt tukufu ya nyumba yake a.s. kwa kunijaalia uwezo wa kukikusanya na kukitarjumu kitabu hiki.

Allah swt amewatuma Mitume a.s. kuja kutuongoza na kutuletea maamrusgo Yake ili tusihangaike kwa kutapa huku na huko tukitafuta kipi ni kweli na sahihi. Lakini wapo watu wenye uchu wa kujitakia dunia kwa hali yoyote ile, hivyo wanawasahau Mitume a.s. na ujumbe waliokuwa wametuletea katika miaka yote hiyo. Kwa tamaa na uroho wao wanachafua dunia na desturi za amani.Wanawatesa na kuwateketeza watu bila ya kujali kuwa wao wafanyavyo si haki.

Mtume s.a.w.w. alisema kuwa, “Ummah wangu utagawanyika katika makundi sabini na tatu, ni kundi moja tu litakaloingia Peponi.” Hivyo makundi sabini na mbili , kama zilivyobainishwa, zitaingia Motoni kwa sababu za itikadi zao potofu, na kwa hakika hayo yamshakwisha tokea. Makundi haya sabini na mawili si makundi ya makafiri kwa kutojua ilimu sahihi ya Qur’an na Hadith, lakini wataingizwa Motoni kwa sababu wao wamediriki kuubadilisha Uislamu.Na hao wanaitwa ahl al-bid’a au -dalala , wakaidi. Wakaidi, kwa sababu wao ni Waislamu, na hapo mbeleni watatolewa kutoka Jahannam na kupelekwa Peponi. Mbali na hao, wapo wale ambao ni Waislamu lakini wanakuwa katika jitihada za kuubadilisha kwa ilimu yao potofu na kipeo chao kidogo, hivyo wanatoka nje ya Uislam. Kwa hakika hao watabakia Motoni kwa milele. Nao ni Zindiq na wachafuzi.

Leo, watu waitwao la-madhhabi wanatumia mamilioni ya madola kwa kueneza imani zao potofu katika kila nchi humu duniani. Ni jambo lakusikitisha mno kuona kuwa hawa waroho wa mapesa wamekuwa wakivutiwa mno katika imani zao potofu na za kufitini, huku nyuma wakiachia hazina kubwa waliyoachiwa na Ahl al-Bayt a.s. ya Nyumba ya Mtume Muhammad s.a.w.w. na Maulamaa wa Ahl-as-Sunna. Hao Mawahhabi wamejaribu kwa jitihada zao zote kuwadanganya Waislamu kuwa vitabu vya Maulamaa wao vinawapotosha. Wao wametayarisha vitabu na propaganda zao dhidi ya Islam halisi iliyokuja kwetu kutokea Mtume Muhammad s.a.w.w.,kwa maandiko ya Mawahhabi yaliyojaa upotofu na vitisho na ulghai.

Kwa hakika Muhammad ibn 'Abd al-Wahhab na kizazi chake wamekuwa wakitoa imani zao potofu kwa kuchapa vitabu ambavyo vimekuwa vikiwapotosha Waislamu kwani walikuwa wakizitumia Ayah za Qur’an tukufu dhidi ya Waislamu wenyewe. Wao hata walithubutu kuwaita Wailsamu kuwa ni Makafiri kwa kuelezea kiuongo Ayah na Hadith. Na jambo hili ndilo limenifanya mimi nijiandae kukitoa kitabu hiki ambacho kitafichua uasili wao.

Kijitabu hiki kilicho mikononi mwenu ni sehemu moja ya kitabu kamili juu ya Mawahhabi. Sehemu hii inazungumzia vile Mawahhabi walivyotokezea, vile walivyo enea vile majahili na makatili waliojiingiza katika Uwahhabi ili kujipatia mali na cheo wamewateketeza na kuwaua Waislamu na kuzipora mali zao.

Vile vile ninakitayarisha kitabu kingine ambacho kitazungumzia imani za Mawahhabi na kuzichambua moja baada ya pili ili Waislamu wajue waziwazi kuwa wao wanadanganywa juu juu tu. Vitabu vingi vimeandikwa juu ya Mawahhabi, lakini kuna haja ya kutoboa mambo yao ili uasili wao ujulikane.

Hivi karibuni rafiki yangu mmoja Msunni, ambaye alikuwa akitoa mihadhara dhidi ya wauaji wa Imam Hussain a.s. huko Karbala, Iraq, nimesikia amejiunga na Mawahhabi hawa. Hivyo natumai atakapoisoma habari zilizoandikwa humu, labda atajifikiria.

Jambo la pili, nimebishana na rafiki yangu mmoja ambaye ni shabiki mkubwa wa mpira. Mimi nilimwambia kuwa katika siku atakazokuwa yeye akiangali mechi za footbal za Kombe la dunia 1998,Ufaransa,mimi nitakitayarisha kitabu kimoja.Hivyo tuone yule anayeupoteza muda na yule anayeutumia muda kwa ajili ya manufaa ya wengine.

Tunamwomba Allah swt awasaidie Waislamu wasiteleze kutumbukia katika mitego ya Mawahhabi.