WANACHUONI WA KIWAHABI WANAJIPENDEKEZA KWA WATAWALA

Tunaona kwamba wanachuoni wa Kiwahabi nchini Saudia na sehemu zingine wanajipendekeza kwa watawala na Makhalifa wajeuri, wanajaribu kuyatakasa matendo ya dhulma ya watawala hao na msimamo wao wakijeuri, na wanajitahidi kutoa kibali cha kisheria kwa kila kinachotokana na watawala wao na wenye mamlaka juu yao (mtawala huyo) awe mwema au muovu.

Na hilo siyo jambo la ajabu (kwao) kwani wao (Mawahabi) ndiyo wanaoona kuwa kusali nyuma ya kila Imam mwema au muovu sala inasihi, na kuwaombea wema viongozi wa Waislamu ni faradhi, na kuwapinga wanapopotoka ni haramu.[5]

Wanaichukuliaje kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu [s] kama alivyoinakili toka kwake mjukuu wake Husein bin Ali [a] "Abu-Shuhadaa" pale aliposema:

"Enyi watu, hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu [s] amesema; mtu yeyote atakayemuona mtawala muovu anayehalalisha haramu ya Mwenyezi Mungu, mwenye kutengua ahadi ya Mwenyezi Mungu, mwenye kwenda kinyume cha Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, anawatendea uovu na uadui waja wa Mwenyezi Mungu, kisha mtu huyo akaacha kumkataza kwa kitendo au kauli, basi Mwenyezi Mungu atakuwa na haki ya kumuingiza motoni mtu huyo." [6]

Hebu niambie kweli, ni ipi baina ya kauli mbili na ni ipi baina ya njia mbili inayotokana na Uislamu halisi na inaonyesha picha ya nadharia ya Uislamu halisi?

Mwenyezi Mungu amesema:

"Wala msiwategemee (mkawa pamoja nao) wale wanaodhulumu usije kukupateni moto."

Qur'an, 11:113.

[5] Maqa'latul-Islamiyyin uk 322 (na hii ni Itikadi ya As-habul-hadith na ibn Taiymiyyah na wafuasi wake katika kundi hili.)

[6] Tarikh at-Tabari Juz. 4 Uk. 304 (matukio ya mwaka wa sitini na moja).