HIJJA - MSIMU WA IBADA NA NI MKUTANO WA KISIASA

Mwenyezi Mungu ameifanya al-Kaaba kuwa ni nyumba tukufu na ni wasila wa kusimamisha amani miongoni mwa watu, na akaifanya Hijja kuwa ni msimu wa ibada na ni fursa ya Waislamu kutoka kila upande kukutana na kufahamiana, na pia wafahamishane mambo muhimu ya Dini yao na kuzichunguza hali zao.

Basi mambo haya baada ya Ibada ni miongoni mwa uthibitisho dhahiri wa kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

"Na ili washuhudie manufaa yao"

Qur'an, 22:28

Basi ni manufaa yepi makubwa baada ya ibada kuliko Waislamu kukutana mahala pamoja ambapo wameacha kila hisia ya dhati na jamii na mipaka ya kitaifa na kimataifa na rangi, bali Waislamu wote hufunikwa na kivuli cha Dini na kupambwa na hisiya za upendo pia moyo wa udugu wa kweli?

Na ni mas-ala gani muhimu kuliko Waislamu kufahamishana hatari na matatizo yaliyowazunguka, na wakaeleweshana namna ya kuyatatua kwa pamoja na kwa nguvu moja na azma ya pamoja ili kuyaondoa au kupunguza uzito wake?

Na Je, Ni tatizo gani kubwa zaidi linalowakandamiza Waislamu leo hii kuliko tatizo la ukoloni wenye aina tofauti ambao umezikalia nchi za Waislamu kijeshi, au kuzitawala kisiasa au kizipiga vita kitaaluma na kisha kuupora uchumi wa Waislamu na kueneza fitna miongoni mwao na kuwauwa watoto wao na kuwaharibu (kitabia) vijana wa Kiislamu, na, na, na, na......!!!

Je, siyo kwamba Hijja ndiyo mahali bora pa kutangazia uchungu wa Waislamu wote dhidi ya ukoloni huu mbaya unaongozwa na Amerika na Urusi?

Na kama Waislamu wenye kudhulumiwa na kutawaliwa katika nchi zao hawawezi kutangaza uchungu wao na chuki yao dhidi ya wakoloni wakiwa ndani ya kitovu cha nchi zao kwa kuwa tu kuna serikali zinazotumiwa kuwaziba vinywa na kunyamazisha sauti zao, basi Hijja haiwi ndiyo fursa inayofaa mno kutangaza uchungu wao na chuki zao bega kwa bega, Waislamu wote wakiwa katika ibada unyenyekevu na kutubia (kwa Mwenyezi Mungu)?

Je, kuwapinga mabeberu ambao kuwatii hukmu zao na kukubaliana nao na pia kuwategemea ni miongoni mwa shirki katika twa'a ya Mwenyezi Mungu?

Je, kuwapinga mabeberu siyo miongoni mwa aina dhahiri mno za tauhidi ambayo Mwenyezi Mungu ameifanya Hijja iwe ndiyo kielelezo chake na uthibitisho wa ukweli wake?

Na kwa hakika leo hii Waislamu wameutambua ukweli huu pamoja na kukua kwa harakati za Kiislamu na kuongezeka kwa jamii ya Kiislamu.

Waislamu wamekwisha tambua kwamba Hijja ndipo mahali panapofaa na ni fursa inayofaa kuwaunganisha Waislamu na kuwazindua, kisha kawatambulisha ukweli wa matukio ya kusikitisha ambayo yanatendwa na maadui wa Uislamu, (ambao ni) Amerika, Urusi, Ufaransa, Uingereza na wengineo miongoni mwa tawala za kikoloni na kibeberu.

Kwa hakika Waislamu wamekwisha fahamu kwamba, Hijja ndiyo fursa nzuri ya kutangaza uchungu wa Waislamu bega kwa bega kutokana na ukoloni muovu pamoja na kufanya ibada na kutubu kwa kufuata kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Ili washuhudie manufaa yao na wamtaje Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 22:28

Kauli hii (ya Mwenyezi Mungu) inaashiria falsafa ya Hijja inayochanganya ibada na siyasa na malengo yake ya kidunia na akhera.

Na kwa ajili hii ndiyo maana kumekuweko mshikamano mkubwa wa kisiasa ambao Waislamu wameuanzisha katika siku za Hijja kwa miaka kadhaa wakiongozwa na Waislamu wa Iran.

Lakini kwa huzuni kubwa tunakuta baadhi ya watu wanaodai kuwa na elimu na wanakalia vyeo vya uenezaji wa Uislamu, wanapinga kwa nguvu harakati hizi tukufu, na wanapinga hatua hizi zenye athari (nzuri) ambazo hazilengi ila kuwakomboa wenye kunyimwa na kudhulumiwa (haki zao) (pia harakati hizi zinalenga) kuutokomeza ukoloni na utumwa.

(Watu hao wapingao wanapinga) hali ya kuwa kila sika wanasikia habari za mauaji na uchinjaji wa mamilioni ya vijana wa umma wa Kiislamu huko India, Palestina, Lebanon na Afghanistan, Eritrea na katika mipaka ya Iraq na Iran na kwingineko. Na mauaji hayo moja kwa moja yanatokana na sababu zinazosababishwa na ukoloni.

Watu hawa badala ya kuunganisha sauti zao na sauti za Waislamu wengine wanaopinga matendo ya ukoloni ambao kwa uovu wake unapokonya haki za Uislamu na Waislamu, tunawakuta wananyanyua sauti zao upande wa ukoloni dhidi ya Waislamu, na wanapinga chuki na hasira za Waislamu dhidi ya ukoloni mamboleo wa Kimarekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa ambao mikono yao imelowana kwa damu ya Waislamu na majumba yao yamejengwa kwa mafuvu ya watoto wa Kiislamu.

Cha ajabu zaidi kuliko hili, ni kule kushikilia kwao kuharamisha hatua hizi tukufu (za kupinga wakokoni kwenye Hijja) kwa kutumia kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema; "Hapana kusema maneno machafu wala kufanya vitendo vichafu wala asibishane katika Hijja."

Qur'an, 2:197

Huyo ni Sheikh Abdallah al-Khayyat ambaye ni Imam na ni Khatibu wa msikiti Mtukufu wa Maka. Yeye ameona kuwa, kuyaeleza matatizo ya kisiasa ya Waislamu katika msimu wa Hijja ni kutoka nje ya lengo la Hijja, na akatoa dalili ya madai yake kwa kutumia kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema: "Basi yeyote aliyekusudia kufanya Hijja, asiseme maneno machafu wala kufanya vitendo vichafu, wala asibishane katika hiyo Hijja."

Qur'an, 2:197

Na akasema tena Sheikh Khayyat, "Na kama alivyoikusudia Mtume [s] Ibada ya Hijja pale aliposema, "Yeyote mwenye kuhiji na akawa hakusema maneno machafu wala hakutenda matendo machafu hurejea kama siku aliyozaliwa na mama yake". Anaendelea kusema Sheikh Abdallah al-Khayyat, "Ama wito wa Iran ya Khomein ambao anataka kuigeuza Hijja kuwa ni matangazo ya kisiasa na maandamano ya kudai (haki) na kupinga Serikali, mambo hayo hayakubaliki namna yafanyikavyo na pia madhumuni yake, kwani yanapingana na mafunzo ya Dini yetu tukufu na yanatoka nje ya maana yake na misingi yake bora, kwa kuwa yanavunja moja ya nguzo miongoni mwa nguzo (za Dini)."

"Ndani yake mna uvunjaji wa heshima ya vitu vitukufu vya Mwenyezi Mungu na kuna kiburi dhidi ya mambo matukufu ya Mwenyezi Mungu na pia kwenda kinyume cha mwelekeo alioelekeza Mwenyezi Mungu."

"Anaendelea kusema: "Bila shaka mwito wa Iran ya Khomein unaeneza fitna na kubomoa umoja na kubadilisha upendo kuwa chuki na kuzigeuza sehemu takatifu kuwa nyanja za kutangaza mambo ya siasa na kueneza miito isiyokuwa na maana. Hapana Muislamu yeyote ulimwenguni isipokuwa anapinga wito huu, kwani ndani yake kuna mambo yanayopinga Uislamu na kuvunja heshima ya alama za Kiislamu. Na Hijja haiwezekani kuwa isipokuwa ni mkutano wa kiroho na ni mkusanyiko wa kila mwaka ambao Waislamu toka kila shemu za mbali hukusanyika".[234]

Bila shaka yaliyomo ndani ya khutba hii (iliyotangulia) ndiyo maneno ambayo tunayasikia (kila mara) kutoka kwa watu wanaoajiriwa na Suudiya, kila mwaka tunayasikia, na katika kila hotuba na kila muhutubiaji (anayasema), basi wao hawakiuki zaidi ya kusoma aya hiyohiyo na kufuata vile alivyosoma khatibu huyo maneno ambayo ni matupu.

Na sisi hapa hatutamkabili Sheikh isipokuwa kwa njia aliyotuamuru Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema, "Jadiliana nao kwa njia iliyo njema", hivyo basi tunaifafanua maana ya aya hiyo na kuiweka wazi ili makusudio yake yaeleweke na watu wote wajue kwamba maandamano ya kisiasa na kutangaza kujitenga na makafiri na kuyatokomeza matendo yao yanayoupinga Uislamu na Waislamu, na kuwaita Waislamu kwenye umoja ambao ndiyo nguzo ya maandamano aliyoyaamrisha Imam Khomeini siyo uthibitisho wa mabishano yaliyotajwa katika aya hiyo.

Hebu iangalie tafsiri ya aya hiyo na ufafanuzi wa makusudio yaliyomo.

Amesema Mwenyezi Mungu, "Hijja ni miezi maalum, basi yeyote anayekusudia kufanya Hijja katika miezi hiyo, asiseme maneno machafu wala asifanye matendo machafu na wala asibishane katika Hijja".

Qur'an, 2:197

1. Bila shaka kukaririka kwa tamko la "Hijja" mara tatu katika aya hii, imeweka neno dhahiri badala ya dhamiri, hata hivyo hapa ni ufupisho kwani makusudio ya Hijja ya kwanza ni kutaja "wakati wa kufanya Hijja" na ile ya pili ina maana ya "tendo lenyewe la Hijja" na ile ya tatu inakusudia wakati na mahala pa kufanyia Hijja", na Iau siyo kudhihirisha (tamko la) Hijja ingekuwa hapana budi kuleta "It-Nab Ghair lazim" (Ufafanuzi usiyo wa lazima).

Amesema ndani ya tafsiri aI-Manar ya Rashid Ridhaa:

"Bila shaka miongoni mwa "Balaghatul-Iijaz" katika aya hii ni kule kuweka dhahiri mahala pa kuweka dhamiri kwa kuitaja Hijja mara tutu, ya kwanza ikiwa na maana ya kipindi cha Hijja kama wasemavyo "Baridi ni miezi miwili", na ya pili maana yake ni ile Hijja yenyewe ambayo ni Ibada, na ya tutu makusanya kipindi cha kutekeleza na mahala pake ambapo ni ardhi tukufu ya msikiti wa Maka nasehemu zinazofuatia kama vile Arafa".[235]

2. Makusudio ya kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Yeyote anayekusudia kufanya Hijja katika miezi hiyo" Yami ameilazimisha nafsi yake kuanza Hijja kwa nia ya makusuduio ya ndani (ya moyo) na kuhirimia kwa kutenda dhahiri na kuitikia kwa kutamka labbaika.[236]

3. Iliyo Mash-huri ni kwamba maana ya neno "Ar-Rafathu" ni "kuingilia", imepokewa kwa Abdallah bin Omar na Tauus na Atwa'a na wengineo kuwa, "Ar-Rafathu" ni kutusemesha mwanamke kwa maneno machafu au uchafu kwa jumla, na imesemwa vinginevyo pia.[237]

4. Na wamelifasiri neno "Fusuuq" kuwa ni maasi yote, amesema Ibn Zaidi na Malik "Al-Fusuuq" ni kuchinja kwa ajili ya masanamu, na Adhahak amesema "Al-Fusuuq" ni kuitana (kuaibishana) kwa majina mabaya, na amesema Ibn Omar, "Al-Fusuuq" ni "Kutukana".

Na kauli ya mwanzo ndiyo sahihi zaidi kwani inakusanya kauli zote.

Na imepokewa kwa Mtume [s] kwamba amesema, "Atakayehiji ikawa hakusema maneno machafu wala kufanya matendo mabaya hurejea kama siku aliyozaliwa na mama yake". "Na Hijja iliyotekelezwa vyema haina malipo isipokuwa pepo". Amepokea hadithi hizi Muslim na wengineo.

5. "Jidala" katika maana ya kilugha ni mabishano, uhasama na ugomvi.

Na uhasama umeitwa kuwa ni mjadala kwa kuwa kila mmoja hutaka kumgeuza mwenziwe kutoka kwenye rai yake.

La muhimu mahala hapa ni kuifasiri kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo kuwa, "Na asibishane katika Hijja" na pia kubainisha makusudio yake. (Kauli hii ya Mwenyezi Mungu) kwa watu wanaoajiriwa na Suudiya wanaifanya kuwa ndiyo dalili ya kuharamisha maandamano na utoaji wa hotuba za kisiasa na miito ya umoja na kudhihirisha kujitenga na makafiri na wanafiki.

Wala hakiwezi kubainika kiwango cha dalili ya aya hii kama waionavyo watu hawa, isipokuwa ni kunakili maoni ya uwezekano wa namna ya kuifasiri aya hii kama yalivyotajwa na wafasiri wakubwa kama ifuatavyo:

A. Maoni aliyoyataja Qadhi al-Baidhawi na ar-Razi naye ameegama kwa Baidhawi, kwa kuichukulia kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "La Rafatha Wala Fusuqa Fil-Hajji Wala Jidalafil Haji" kuwa ni "Khabar" maelezo ambayo maana yake ni kwamba, "Hijja haiwezi kuthibiti (ikitendwa) pamoja na mojawapo ya mipaka hii, bali itaharibika kwa kuwa ni kama kufanya kinyume chake, na mambo hayo yanazuwia kusihi kwa Hijja.

Kwa hiyo basi matamko hayo matatu ni lazima yachukulike kuwa ni yenye kuharibu Hijja na muradi wake ni vitendo vinavyoharibu Hijja na yanawajibisha kulipa Qadha mwakani iwapo Hijja hii ilikuwa ni wajibu.

Basi "Ar-Rafathu" hufasirika kwa maana ya "Kuingilia" na "Al-Fusuqu" kwa maana ya "Kuzini" kwa sababu vitendo hivi vinaharibu Hijja, na jidala huchukuliwa kwa maana ya kuitilia Hijja juu ya kuwa kwake ni wajibu na kusihi kwake kisheria na kuwa kwake ni tendo linalokubaliana na akili.[238]

Kwa kifupi, bila shaka kilicho dhahiri ni kule kuwepo kinyume kati ya mambo haya na Hijja ambayo Mwenyezi Mungu ameamuru mwanzoni na kwa msingi huo basi, kama ambavyo haiwezekani kuchukulia neno "Fusuqu" katika maana ya lugha kwani siyo kila "Fusuqu" huharibu Hijja kama vile uongo na kuteta, vile vile haiwezekani kuchukulia neno "Jidala" katika maana ya kila ubishi kwani siyo kila ubishi unaharibu Hijja, bali muradi wake ni mabishano maalum ambayo hayawezi kukusanyika pamoja na Hijja kama vile kutia shaka uwajibu wa Hijja na kusihi kwake kisheria na kuona kuwa ni upuuzi kule kutufu jiwe, udongo na ubao - al-Kaaba.

Maana hii ndiyo aliyoichagua Qadhi (al-Baidhawi) na akaiunga mkono Ar-Razi katika tafsiri yake, na (maana hii) ndiyo chaguo la wanachuoni wengi ndani ya sentensi nyingi (zilizokuja namna hii) kama vile:

"La Salata ila Bifatihatil-Kitabi"
Yaani, hakuna Sala ila kwa (kusoma) "Suratil-Fatiha". Au "La Salata ila Bitahurin" Yaani, hakuna Sala ila kwa Tahara."

Na makusudio yake ni kukanusha kusihi (kwa Sala) bila ya vitu hivyo viwili, na kwamba kuthibiti kwa Sala kumetegemea vitu hivyo, kama ambavyo makusudio ya aya ile vile vile ni kukanusha kusihi kwa Hijja (ikitendwa) pamoja na mambo hayo matatu.

Basi iwapo uwezekano huo utasihi, haitafaa kuitolea dalili kwa namna waionayo hawa (wanaofadhiliwa na Suudiya) kwa kuharamisha kila majadiliano ikiwa ni pamoja na maandamano, kwani makusudio ya aya ni kubainisha uharamu wa majadiliano ambayo hayaafikiani na kusihi kwa Hijja, na makusidio (ya aya) siyokubainisha uharamu wa kila mjadala japokuwa unaafikiana na usahihi wa Hijja. Hata kama tukikubali kwamba Jidala na maandamano juu ya kuyakadiria ni haramu lakini haiharibu Hijja.

B. Kutenganisha kati ya mambo haya matatu kwa kuyachukulia yale mawili ya mwanzo kuwa ni katazo, japokuwa itakuwa ni kwa kulihalifu dhahiri ya tamko yaani "La Tar-Fathuu Wala Tufsiquu" (msitoe maneno machafu wala vitendo vichafu) na kulichukulia lile jambo la tatu kuwa ni "Khabari" yaani, hapana mjadala wala kwenda kinyume ndani ya wakati wa Hija na sehemu ya (kufanyikia) Hijja, kwa msingi huu basi, makusudio itakuwa, "Hapana mjadala wala kwenda kinyume ndani ya kipindi cha Hijja na mahali panapofanyikia Hijja, na maana hii ndiyo ambayo ameishikilia Ibn Jariri at-Tabari ndani ya Tafsiri yake.[239]

Na ameitaja pia Az-Zamakh-Shari:[240]

Na wote wawili wametoa ushahidi kwa namna mbili:

Ya Kwanza: Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu [s] amesema: "Yeyote atakaye Hiji kwa ajili ya Mwenyezi Mungu akawa hakusema maneno machafu wala kufanya matendo mabaya hurejea katika hali yake kama siku aliyozaliwa na mama yake". Na wala (Mtume) hakusema "Wala hakufanya mjadala".

Kwa msingi huu kuna dalili kwamba yale mambo mawili ya mwanzo yana maana ya makatazo ya kusema machafu na kutenda mabaya, wala hakuna katazo kwa lile la tatu, vinginevyo lingefuatishwa kwa hayo mawili kwa namna ya katazo, isipokuwa (hili la tutu) lina maana ya kutoa khabari na kukanusha kuwepo mjadala na kubishana katika kipindi cha Hijja na mahali pa Hijja.

Kwa hiyo kutokana na pande hizi mbili (yaani mahala na wakati) inajulikana wazi kuwa hapastahiki kutiliwa mashaka wala wasi wasi.

Ya Pili: Hakika Maquraishi walikuwa wakiwakhalifu Waarabu wengine, wao husimama Mash-Aril-Haram na Waarabu wengine husimama Arafah, na walikuwa mwaka mwingine wakiiwahisha Hijja na mwaka mwingine wakiichelewsha na hiyo ndiyo "An-Nasii". Basi Hijja ikarejeshwa kwenye wakati mmoja na Wuquuf ikarudishwa Arafah, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu akaeleza kwamba "Hakika tofauti imeondoka katika Hijja" na Mwenyezi Mungu akaieleza "An-Nasii" kuwa ni kuzidi katika kufru, inawapotosha waliokufuru wanahalalisha mwaka fulani na wanaiharamisha mwaka mwingine.

Naam, Hijja ilirejea kwenye wakati wake na mahala pake katika Hijja ya kuaga, Mtume [s] alisema, "Bila shaka wakati umerejea kama ulivyokuwa siku iliyoumbwa mbingu na ardhi". Naye Qur-tubi amesema maana yake ni kuwa, "Suala Ia Hijja limerejea kama lilivyokuwa, yaani limerejea kwenye siku yake na wakati wake".

Na amesema Mtume [s] alipohiji yakuwa "Chukueni Ibada zenu kutoka kwangu" akabainisha visimamo vya Hijja na mahala pake.[241]

Basi kama tukikubali maana hii kauli ya Mwenyezi Mungu haitakuwa na mafungamano yoyote na maoni ya huyu khatibu al-Khayyat, kwani kauli hiyo haina maana ya katazo ili iwe Taklifu II-zami inayokusanya aina yoyote ya mjadala, isipokuwa hiyo ni jumla Khabariyah na hii khabari inaeleza mambo ya kimaumbile.

Kwa hakika baada ya matendo ya Mtume [s] na kuweka kwake mipaka ya visimamo na Mash-Ari na kuithibitisha katika mwezi maalum, Hijja imekuwa kama jua la mchana, basi haiwezi kukurubiwa na shaka kuhusu wakati wake na mahali pake, basi maneno haya yana uhusiano gani wa kuharamisha mjadala na kuharamisha maandamano ya kisiasa hata kama tutasema kwamba maandamano ya kisiasa yanaingia katika maana ya mjadala.

Amesema Ibn Jariri:

Kauli zinazostaajabisha mno kwangu mimi kuhusu jambo hilo, iwapo litakuwa kama nilivyoeleza kwamba, kisomo cha atakayesoma, "Falaa Rafathun Wala Fusuqun Wala Jidala FilHaj" kwa kuitia Raf-u Rafathu na Fusuqu na kuzitia Tan-win zote hizo mbili, na kuitia Fataha jidala bila ya Tan-wini, kisomo ambacho ni cha watu wa Basra na watu wengi wa Maka akiwemo Abdallah bin Kathiri, na Ibn Amri bin Al-Ula.[242]

Na bila shaka yamerufaishwa matamko mawili ya mwanzo na likanasibishwa la tatu kwa kuyachukulia yale matamko mawili ya mwanzo kwa maana ya makatazo, na ikawa kama kwamba pamesemwa kwa mkazo pasiwepo maneno machafu na wala matendo mabaya, na la tatu kwa maana ya kueleza kukanushwa kwa mjadala ikawa kama kwamba pamesemwa, hapana shaka wala kutofautiana katika Hijja, yaani ndani ya kipindi chake na mahali pake.

Ya Tatu: Ni kauli iliyoteuliwa na wafasiri wengi, nayo ni kuichukua nafyi (kanusho) na kulipeleka kwenye makatazo, na lengo liwe ni kukataza mambo yote matatu, na katika kipindi hiki (ifanywapo namna hii) ndipo anapokanganyika mtoaji wa dalili, kwa kuwa dhahiri ya aya inakataza mjadala wowote ule ikiwa ni pamoja na maandamano ya kisiasa.

Lakini ni lazima kwa mtu anayetaka kupata ukweli atulizane kidogo ili yambainike mambo mawili:

1. Jidala, inagawika kwenye haramu, mubaha na mustahabbu sasa basi kilichokatazwa ni jidala (mjadala) wa aina yeyote au ni ule unaohusu sehemu ya kwanza (yaani mjadala ulio haramu) na kama mjadala huo utakuwa haramu katika nyakati zingine basi haipingiki kuwa ni haramu katika Hijja vile vile na inakuwa mkazo zaidi uharamu wake katika Hijja.

2. Bila shaka maandamano ya kisiasa na kutoa hotuba na kuwazindua Waislamu kutokana na kujisahau kwao, na kudhihirisha kujitenga na maadui zao wa mashariki na magharibi, Je, hayo ni katika aina za "Jidala" na ndiyo milango yake au hayana kabisa mahusiano nayo?

Hebu angalia ufafanuzi wa mambo mawili:

Bila shaka makusudio ya "Jidala" Ni kubishana ambako ni lazima kuepukwa katika Hijja na kwingineko, lakini katika Hijja ndiyo muhimu zaidi kuepuka.

Amesema Zamakhshari:

"Wala Jidala, Yaani hapana mabishano na marafiki na watumishi wa wenye kuajiriwa, na imeamuriwa kujiepusha na ubishani na ni wajibu kujiepusha nao kwa hali yoyote ile, kwani katika Hijja ni kubaya nino (kubishana) kama vile kuvaa nguo ya hariri katika Sala na kujitingisha tingisha wakati wa kusoma Qur'an."[243]

Na amesema ndani ya Tafsir Al-Manaar kwamba, "Al-Jidalu, ni kubishana na kukhasimiana (kugombana) basi yote haya yaliyokatazwa yanakuwa ni mafunzo ya ulimi (namna ya kuzungumza) na ni wajibu kwa mtu anapokuwa katika ibada na mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, awe mwenye ukamilifu wa adabu na mazingira bora".[244]

Al-Jas-Sas amesema:

Al-Jidal ni Mabishano, na Ibn Abbas amesema, Al-Jidal ni kumjadili mwenzio mpaka ukamkasirisha, kisha akasema, hakika aliyehirimia amekatazwa kutukana na kubishana katika miezi ya Hijja na katika miezi mingine, na amekatazwa matendo mabaya japokuwa matendo hayo ni haramu hata kabla ya kuhirimia, basi Mwenyezi Mungu ameyataja uharamu wake wakati wa kuhirimia ili kuonyesha ubaya zaidi kutokana na utukufu wa Ih-ram, na hasa kwa kuwa kufanya maasi katika hali ya kuwa ndani ya Ih-ram kuna adhabu kubwa zaidi kuliko katika wakati mwingine.[245]

Na kinachoweka bayana zaidi ni kule kuikutanisha "Jidala" na "Fusuqu" kwani kunaonyesha kuwa, mambo haya mawili yanatokana na asili moja ya jinsi moja, basi haifai kukusanya jidala kwa ujumla, (yaani) Jidala Mubaha au Mustahabu katika sheria.

Na ndani ya sheria ya Kiislamu kuna aina za majadiliano mbayo ni Mubaha na zaidi ya hapo kuna ambayo ni mustahabbu na aya ile haihusiki nayo.

Ama Jidala (majadiliano) ambayo ni Mubah miongoni mwake ni yale yaliyokuja katika kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

"Bila shaka Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya mwanamke ambaye anajadiliana nawe kuhusu mumewe, na anashitakia mbele ya Mwenyezi Mungu"

Qur'an, 58:1

Lau litawafika jambo kama hili katika Hijja haliwezi kuwa haramu si kwa msemaji wala kwa msikilizaji. Kinachojulisha hapa ni kwamba, makusudio ya Jidala ni majadiliano na mabishano yaliyokatazwa ambayo ni lazima kujiepusha nayo, nao wameyafasiri majadiliano ndani ya aya hiyo kuwa ni mambo yote yasiyotokana na mjadala na ubishi uliokatazwa.

Amesema Ar-Razi: "Wafasiri wametaja namna nyingi kuhusu mahali hapa:

1. Mjadala unaohofiwa kuleta matusi na kukadhibishana na kupeana sifa ya ujinga.

2. Amesema Muhammad bin Kaab Al-Quradhi, "Hakika Maquraish walikuwa wakikusanyika Mina na kuambizana, "Hijja yetu imetimia" Na wengine husema, "Sisi yetu ndiyo iliyotimia", Basi Mwenyezi Mungu akawakataza kufanya hivyo".

3. Malik amesema katika Muwatta, "Jidala katika Hijja, (maana yake) ni kwamba Maquraishi walikuwa wakifanya wuqufu kwenye Mash-Aril-Haram katika Muzd-alifa Mahala paitwapo Qaza na wengine hufanya wuquf Arafa, na walikuwa wakibishana hawa husema "Sisi ni sahihi zaidi" Na hawa nao husema "Sisi ndiyo sahihi zaidi", Mwenyezi Mungu akasema, "Kila umma tumeujalia ibada wanayoishika, basi wasishindane nawe katika jambo hili, walinganie watu kwa Mola wako, bila shaka wewe uko katika uongofu ulio sawa kabisa, na kama wakiendelea kukujadili basi waambie Mwenyezi Mungu anayajua yote mnayoyatenda".

Qur'an, 22:67-68

Malik amesema haya ndiyo majadiliano (yaliyoharamishwa katika aya hii).

4. Amesema Qasim bin Muhammad "Majadiliano katika Hijja ni wengine kusema, "Hijja nileo" na wengine weseme, "Hijja ni kesho" na hiyo ni kwa kuwa walikuwa wameamrishwa kuweka hesabu ya miezi kwa kuonekana mwezi.

5. Amesema Al-Qaffaal: "Katazo linaingia kutokana na mambo ambayo walimjadili Mtume [s] alipowaamuru kubadilisha Hijja na kufanya Umra tamatui wakaona vibaya kufanya hivyo, na wakasema, Je, tutakwenda Mina hali yakuwa tupu zetu zinadondosha manii? Mtume [s] akasema, kama ningelijuwa mwanzoni kitu nilichoamuriwa sasa hivi nisingeleta pamoja nami wanyama wa kuchinja, na ningelifanya umra tamatui, basi baada yake wakuacha mjadala.

6. Amesema Abdur-Rahman bin Zaid:

"Mabishano yao katika Hijja ni kwa sababu ya kuhitilafiana kwao kuhusu nani kati yao ambaye Hijja inafanana nmo na Hijja ya Nabii Ibrahim [a]?

7. Wao walikuwa wakitofautiana katika miaka, wakaambiwa hapana kujadiliana kuhusu wakati wa Hijja kwani nyakati zimerejea kama ilivyokuwa wakati wa Ibrahim [a].

Basi huu ni mkusanyiko wa yale waliyoyasema wafasiri katika mlango huu.[246]

Mifano hii inajulisha kuwa makusidio ya majadiliano ndani ya aya hiyo, ni majadiliano yaliyokatazwa sawa yakiwa yamekatazwa katazo Ia kuharamisha au katazo la karaha.

Na imekuja katika kitabu kiitwacho Al-Fiqhi Alal Madhahibil-Arbaa, kwamba "Ni haramu kutoka katika taa (kumtii) Mwenyezi Mungu tendo lolote la haramu japo litakuwa tendo hilo limeharamishwa mahala pasipokuwa pa Hijja, isipokuwa kunatiwa mkazo zaidi katika tendo hilo wakati wa Hijja, na ni haramu kugombana na marafiki na watumishi na mfano wa hao kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema, "Yeyote atakayekusudia Hijja, basi asiseme maneno machafu, wala asitende matendo mabaya wala asijadiliane katika Hijja", na Jidala (maana yake) ni kukhasimiana.[247]

Na kwa msingi huu basi, majadiliano ambayo ni Mubah na kupingana bila ya kuzusha ghadhabu kwa mwingine ni kama majadiliano yaliyokuja katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema, "Bila shaka Mwenyezi Mungu ameisikia kauli ya mwanamke anayejadiliana nawe kuhusu mumewe na anashitakia kwa Mwenyezi Mungu". Majadiliano hayo yako nje ya mtiririko wa aya hiyo, na lau yule mwanamke anayeshitakia angekuwa katika hali ya Ihram na angelipeleka mashitaka yake kwa Mtume [s] na kutaka haki yake toka kwa mumewe, hiyo isingehesabiwa kuwa ni majadiliano haramu na kugombana kuliko kuchukiwa bali itahesabiwa kuwa huyu anafuta haki kwa njia iliyo sahihi.

Wafasiri wamesimulia kwamba, kuna mwanamke wa Kiansari ambaye baada ya mumewe kumfanyia dhihari alikwenda kwa Mtume [s] akasema, "Hakika mume wangu aliniowa nikiwa bado kijana tena najitosha kwa mali na jamaa, alipokwisha kula mali yangu na kuumaliza ujana wangu na jamaa zangu kutawanyika na umri wangu kuwa mkubwa amenifanyia dhihari...." Na mengine aliyoyataja.

Ikiwa Jidala iliyo Mubaha iko nje ya aya hiyo basi mjadala ambao ni mustahabbu unayo haki zaidi kutoka kuliko hii, na kwa nini isiwe hivyo wakati Mwenyezi Mungu amemuamuru Mtume wake katika kitabu chake kufanya mjadala uliyo Mandub.

Lau wakati wa Hijja yatatolewa Mas-ala ya Kifiq-hi au Akida au Tafsiri na kila mmoja akatowa Maoni yake na mwingine akamjadili kwa njia nzuri, basi haitakuwa haramu jambo hilo, bali litakuwa ni kutekeleza kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema, "Waite watu katika njia ya Mola wako kwa hekima na Mawaidha mema na ujadiliane nao kwa namna iliyo nzuri".

Qur'an, 16:125

Na lau utatokea uchambuzi katika mahema ya Arafah kuhusu Mas-ala ya Kifiqhi au Akida kisha mmoja wa Waislamu akashika msimamo wake maalum na kutetea itikadi yake kwa dalili na hoja, bila ya kuonyesha uhasama au ubishi au jeuri, hapana shaka kwamba jambo hilo linafaa, na wala halitahesabiwa kuwa ni kuingia kwenye mjadala uliokatazwa na aya hiyo.

Maelezo yote yaliyotangulia ndiyo msimamo ulivyo kwa Ahli-Sunna, ama kwa upande wa msimamo wa watu wa nyumba ya Mtume [s] ambao wako sambamba na Qur'an na ni wenza wa Qur'an kwa mujibu wa kauli ya Mtume [s], wao wanafasiri

"Jidala" iliyotajwa katika aya kuwa ni kauli ya mtu atakaposema La Wallah, Wallah (Nime....) Na (akasema) Balaa Wallah..... Ikiwa ataapa viapo vitatu vya kweli mfululizo basi huyo amefanya "Jidala" na anawajibika achinje, na akiapa kiapo kimoja cha uongo (Pia) atakuwa kafanya "Jidala" na anawajibika kuchinja.[248]

Basi uko wapi uharamu wa kuharamisha kila aina ya "Jidala" wanaoudai watu hawa? Na kilicho haramu kwa mujibu wa riwaya zao ni mabishano "Jidala" Maalum kama ulivyokwisha fahamu (hapo kabla).

Hebu tukadirie kwamba aya inakusanya majadiliano ya aina zote, yale yaliyo haramishwa katika wakati usio wa Hijja na yale ya Mubaha na Mandubu yote hata kama tutakubali hivyo basi makusudio ni mjadala baina ya Haji na Haji mwingine.

Ama mjadala wa Haji na watu walioko katika haram (ya Maka), na ama yale maandamano yanayofanywa na Mahuhjaji wa Kiislamu na kutangaza kujitenga kwao na makafiri na kukemea matendo yao ya uadui kwa Waislamu na Uislamu, na (ama) kuwaita Waislamu kwenye umoja miongoni mwao ili kuzikabili hatari na ushindani, yote hayo asilani hakuna cho chote cha mabishano. Hapana chochote katika mkusanyiko huo isipokuwa ni (kuonyesha) umoja wa Waislamu na hapana yeyote miongoni mwa makafiri na wanafiki anayekabiliana nao (wakati huo kwenye Hijja) mpaka (Eti) isababishe kuzuka kwa majadiliano kati ya pande mbili hizo.

Hebu angalia, hivi je, inahesabiwa kuwa kitendo alichokifanya Imam Ali [a] alipowasomea makafiri aya zilizoko katika Surat Al-Baraat katika msimu wa Hijja kwa amri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (kitendo hicho kinaitwa) kuwa ni majadiliano? "Jidala Fil-Hajj"? Au ni tangazo la Mwenyezi Mungu na Mtume wake kujitenga na makafiri na washirikina? Na iko wapi basi tofauti kati ya misimamo hii miwili?

Bila shaka maandamano wanayoyafanya Waislamu wanaokwenda Kuhiji wakati wa Hijja kwa amri ya Imam Khomeni "Mwenyezi Mungu amrehemu" si kwa maana nyingine ila ni kutekeleza kwa vitendo na kuyathibitisha maelekezo yaliyokuja katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema, "(Waislamu) ni wakakamavu dhidi ya makafiri na ni wenye kuhurumiana wao kwa wao".

Qur'an, 48:29

Naam, bila shaka watawala wa Suudiya ndiyo wanaoleta mazingira ya Jidala iliyokatazwa kwa kuwa wao ndiyo wanaowazuwiya Waislamu kutangaza chuki zao dhidi ya makafiri, na kuonyesha chuki zao kwa matendo yao maovu. Kuwa wanawazuia Waislamu wasitekeleze wajibu wao wa Kiislamu, na wanawalazimisha Waislamu wasiwahoji (watawala hao) na kuwajadili, basi watawala wa Suudiya ndiyo mjadala na ndiyo sababu ya jidala (mabishano).

Basi Iau ingetolewa fursa ya Mahujaji wote wakaafikiana juu ya umuhimu wa kushirikiana katika maandamano haya yanayopinga matendo ya makafiri na uovu wa Walahidi, haitakuwepo tofauti miongoni mwa Mahujaji (kuhusu jambo hili) isipokuwa kile wanachokichochea watawala wa kizazi cha Suud.

Mwisho tunamuuliza Khayyaat: Yeye anasema katika Khutba yake kuwa "Hijja ni mkutano wa kila mwaka ambao Waislamu hukusanyika kutoka sehemu mbali mbali". Basi ikiwa Hijja ni kama adaivyo yeye, Je, ni Mas-ala gani miongoni mwa Mas-ala yanayopasa kutolewa katika mkutano huu?

Je, inapasa kuzungumza maneno madogo madogo kama vile ukaraha wa kula kitunguu maji na kitunguu thaum kwa mtu atakaye kuingia msikitini au kuzungumzia kukosha nyayo na viatu kutokana na udongo na jasho kama ambavyo tumekuwa tukisikia mara nyingi (maneno hayo) toka kwa Makhatibu wa msikiti mtukufu wa Makka katika siku za Hijja na katika Sala za Jamaa, kama kwamba hakuna mambo mengine ya Kiislamu (yanayopaswa kuzungumzwa) isipokuwa haya.

Utakapo kubainikia ewe msomaji ubatili wa yale aliyoyasema Khayyat, na pia ubatili wa ushahidi wake, bali kutokuwepo kwa maungamano ya aya (aliyoitowa) na Qadhiya hii (ya maandamano kwenye Hijja) basi inapasa tuwe na msimamo wa pamoja juu ya (kuifahamu) falsafa (Hekima) ya Hijja ya kweli kwa namna ya uchambuzi kwa mujibu wa aya za Qur'an na hadithi tukufu na pia matukio ya kihistoria na sera za waliotangulia.

Na sasa hebu tazama maelezo haya yafuatayo kwa ujumla:

NINI LENGO LA HIJJA?

Kwanza Hijja ni Ibada:

Hapana shaka kwamba jambo la kwanza ambalo Hijja inalilenga na ndiyo makusudio muhimu ya ibada zake, ni kuzidisha kumuelekeza mja kwa Mwenyezi Mungu na kumfanya kuwa mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na kuimarisha uhusiano kwake na kuiingiza kwa ndani zaidi imani katika moyo wake na kuithibitisha itikadi ndani ya dhamiri yake juu ya upweke wa Mwenyezi Mungu.

Kwa kifupi tunaweza kusema kwamba lengo muhimu la Hijja ni ibada na ni kwa kuanzia kuhirimia kwa ajili ya umra na kutufu al-Kaaba tukufu kisha kuswali na kwenda baina ya Safa na Marwa na kupunguza nywele, na kisha Ihramu ya pili ni kwa ajili ya Hijja na kusimama Arafah na kwenda Muz-dalifa na kusimama hapo, kisha kwenda Mina na kulala usiku kadhaa na kupiga Jamarat, kisha kuchinja ngamia au (ng'ombe, mbuzi au kondoo) halafu kunyoa kisha kutufu aI-Kaaba Tukufu na kumalizia kufanya Saayi baina ya Safa na Marwa pamoja na kufanya yanayoambatana nayo miongoni mwa dua na dhikri na kujizuwiya na yaliyoharamisha yanayohusika nayo, yote haya ni kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hiyo ni ibada iliyo katika ubora wa aina yake, na ni kuonyesha utumwa (mbele ya Mwenyezi Mungu) katika daraja iliyo juu ya ibada. Na kwa hakika ni (kuonyesha) unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika namna zilizo bora mno.

Ni ibada inayoonyesha udhalili (wa waja) mbele ya Mwenyezi Mungu kwa undani wa aina yake. Hivyo basi Hijja ni ibada inayokusanya kila misingi inayodhihirisha utumwa (mbele ya

Mwenyezi Mungu, na (pia inadhihirisha) kila aina za unyenyekevu na utii kwa Mola Mtukufu, (miongoni mwake) ni kutosheka na dunia na kuyapuuza ma-tamanio na kujitolea kwa mali na kudhalilika na kufanya dhikri, na Tah-lili na Tasbihi, Tahmidi na Takbira na kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika kumtii na kumuomba msaada na kutoka kwenye uzio wa mapendekezo ya kimaada na kujisahaulisha kwa muda (furaha ya) mali mtoto mke na jamaa kwa ajili ya kuitumikia dini ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili yake Mwenyezi Mungu na kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kufuata hukmu ya Mwenyezi Mungu, na kutekeleza matakwa ya Mwenyezi Mungu, na kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu pekee asiye na mshirika.

Bila shaka Hijja ni ibada, lakini je, lengo la Hijja linaishia kwenye matendo haya matukufu ya ibada tu? (au kuna zaidi)?

Na Je, hivi Hijja ilifaradhishwa kwa Waislamu wote wanaume na wanawake, wazee na vijana na kila aina ya rangi (za watu) na jinsi (zao) ili watekeleze maamrisho yanayofungamana na uhusiano (wao) na Mola wao tu bila wajibu huu mtukufu (wa Hijja) kuwa na lengo la (maisha) ya kijamii na bila mafungamano yoyote na masuala ya maisha yao na mambo yao?

Na Je, hivi hata tendo dogo la kiibada ndani ya Uislamu huwa halina lengo la kijamli kiasi kwamba ibada hii kubwa ya Hijja ikose lengo hilo (la kijamii)?

Na faradhi hii kubwa yenye vigawanyo na misingi mingi na yenye muundo wa kijamii kama swala ya Ijumaa (Iwe haina lengo lolote ndani yake)?

Bila shaka aya za Qur'an na Sunna tukufu na sera za waliotangulia na kauli za wanachuoni zote zinaungana (kutambulisha) kwamba lengo la Hijja haliishii na kukoma katika hali ya kuwa ni jambo la ibada peke yake na unyenyekevu auonyeshao mja katika maisha yake ya kijamii, (Bali) makusudio yake ndiyo makusudio ya ibada zingine miongoni mwa faradhi za Kiislamu kama vile Swala, Saumu, Zaka, Jihadi na nyinginezo ambazo hazihusiani tu na mambo ya kuabudu peke yake, bali zinajumuisha malengo ya Kijamii na mambo ya kisiasa katika maisha ya Waislamu (kuanzia) mmoja mmoja na (hadi kufikia ngazi ya) Taifa.

Na jambo hili (kwa maana iliyoelezwa) linaungwa mkono na akili iliyosalimika na kutiwa nguvu na fikra sahihi.

Bila shaka Uislamu ni dini yenye kuenea (kila upande) yaani ina muongozo wa kiibada, kisiasa, kiuchumi na kijamii, nayo iko kinyume na Uyahudi na Ukristo wa leo na kanuni zilizowekwa na watu, na haukuwa Uislamu ila ni mkusanyiko uliopangika wa itikadi na kauni na mafunzo yanayohusu kila upande wa maisha, bali ni kila sehemu ya dini hii ni mchanganyiko uliyowekwa kimahesabu kutokana na malengo mbali mbali na ni mpango uliowekwa kwa usawa kwa mtu mmoja mmoja, jamii, ibada, siasa, uchumi, afya, dunia na akhera.

Zaidi ya hayo ibada katika fikra ya dini hii, mipaka yake inatanuka mpaka inakusanya maisha yote na kuyaenea matendo yote ya watu kama yatatendwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haikomei kwenye mambo ya ibada yaliyo mashuhuri kama vile Sala, Zaka na Hijja, bali inakusanya kila tendo ambalo kwalo kuna mafanikio ya maisha na kufaulu kwa watu.

Na kwa ajili hii Mtume Mtukufu [s] amesema kumwambia Abu Dharri: "Uwe na nia njema kwa kila kitu (ukitendacho) hata katika usingizi"[249]

Kwa hiyo basi, Hijja kama tunavyoibainisha kutoka katika Qur'an na Sunna na sera za waliotangulia, na kauli za wanachuoni wahakiki, (lengo lake) halikomei kwenye kuwa yenyewe ni msimu wa ibada kwa utambuzi uliozoeleka kwa watu wengi bali kwa upande mwingine ni mkutano wa kisiasa wa ulimwengu na ni mkusanyiko wa kijamii kwa jumla unaowapa Waislamu wanaokuja kutoka kila pande za miji fursa ya kufahamiana, kuzoweyana, kukutana na kunufaishana wao kwa wao na kubadilishana mambo yao na kutatua matatizo yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii wakiwa mahala pa amani na utukufu na upendo.

Na haya ndiyo tunayotaka kuyaonyesha na kuyatolea ushahidi katika kurasa hizi chache pamoja na kuwa tunakiri ya kwamba Mas-ala haya (ya Hijja, na kuyasoma malengo ya Hijja ya kiibada na kisiasa na kijamii ni (somo) pana mno kuliko hili somo (tutakalolieleza) kwa ufupi.

Kwa hiyo basi tunataraji kawa yatakayokuja katika mlango huu ni dalili tu siyo zaidi, na ni wajibu wa Waislamu wote na mahujaji kwa upande wao wajaribu kufahamu mafunzo zaidi katika nyanja hii, nayo ni kwa kuifanyia mazingatio faradhi hii na ibada zake na kuzitilia maanani aya za Qur'an na hadithi Tukufu katika njia hii.

MAKUSUDIO YA HIJJA KIJAMII NA
KISIASA NDANI YA QUR'AN

Qur'an Tukufu imeitaja Hijja mahala pengi ya kuwa ndani yake mna mambo yenye manufaa kwa watu na inayo maslaha yao, pale Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema:

"Watangazie watu habari ya Hijja, watakujia watu kwa miguu na (wengine) wakiwa juu ya mnyama aliyekonda kutokana na machofu ya njiani, wakija kutoka njia ya mbali, ili washuhudie manufaa yao na kulitaja jina Ia Mwenyezi Mungu katika siku zinazojulikana - Juu ya yale aliyowaruzuku, nao ni wanyama wenye miguu minne, na kuleni katika wanyama hao na mumlishe mwenye shida aliye fakiri. Kisha wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao na waizunguke nyumba ya kale (Al-Kaaba). Namna hii iwe, na anayevitukuza vitu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu basi (kufanya) hivyo ni kheri yake Mwenyewe mbele ya Mola wake, na mumehalalishiwa wanyama isipokuwa wale mnaosomewa humu (katika Qur'an kuwa wasiliwe), basi jiepusheni na uchafu wa masanamu na jiepusheni na usemi wa uongo, Mkhalisike kwa Mwenyezi Mungu bila kumshirikisha na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo kumtupa mbali. Namna hivi, yeyote anayeziheshimu alama za (Dini ya) Mwenyezi, basi hilo ni jambo katika utawa wa nyoyo. Katika (wanyama) mnaowapeleka Makka

kuchinjwa) mnayo (ruhusa kutumia) manufaa (yake) mpaka muda maalumu, kisha mahala pa kuchinjwa kwake ni (karibu na) ile nyumba kongwe".

Qur'an, 22:27-33

Kuna mambo matatu ya kuzingatia ndani ya aya ya pili miongoni mwa aya hizi:

Kwanza: Manufaa yamewekwa upande wa kumtaja Mwenyezi Mungu na ndani yake inafahamisha kwamba Hijja inayo malengo mawili:

Moja wapo ni la Kiibada na linachukua nafasi ya kumtaja Mwenyezi Mungu, lengo jingine siyo Ia kiibada kwa maana iliyozoweleka nalo linachukua mahala pa manufaa.

Pili: Kuyatanguliza manufaa juu ya kumtaja Mwenyezi Mungu jambo linaloshika nafasi ya kiibada.

Tatu: Kuyafanya manufaa yasiwe na ufupisho uliofungika bali yawe yenye kuingia katika nyanja nyingi, kwani Mwenyezi Mungu hakusema kuwa ni manufaa ya kiuchumi tu peke yake, jambo ambalo linafahamisha kwamba manufaa haya yanakusanya manufaa ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na mengineyo.

Amesema Al-Mar-hum Al-Imam Sheikh Muhammad Shaltut ambaye alikuwa Sheikh wa Chuo Kikuu cha Az-Har, kuhusu tafsiri ya aya hii kama ifuatavyo:

"Manufaa ambayo Hijja imefanywa kuwa ndiyo njia ya kuyashuhudia na kuyapata - nayo ndiyo yaliyotajwa mwanzo kuhusu hekima za Hijja, ni manufaa ya ujumla bila ya sharti, hayakufungiwa kwa aina moja pasina aina nyingine, wala upande mmoja bila upande mwingine, nayo kwa ujumla wake yanakusanya kila kinachomnufaisha mtu mmoja na jamii na kutengeneza mambo yao, kwani kuitakasa nafsi na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu ni manufaa na kushauriana kuweka mipango ya Elimu na Taaluma na kuungana kuimarisha Da'awa na kufanya juhudi kuutangaza Uislamu na hukmu zake bora ni manufaa, na kuandaa mikakati ili kuimarisha heshima ya Uislamu kutokana na ukandamizaji na unyonge ni manufaa, na hali kama hii manufaa yake ni mengi na yana aina nyingi kutegemeana na hali zinavyolazimu na nyakati zinavyotambulisha na mitazamo kati ya watu na watu".[250]

Na amesema tena: "Nayo Hijja kwa kuzingatia utukufu wake ndani ya Uislamu na lengo lake lililokusudiwa kwa mtu binafsi na jamii, bila shaka wanaikubali watu wa elimu na watu wanaohusika na mafunzo na taalauma pia wanaohusika na uendeshaji wa mambo na idara na wale wanaohusika na mali na uchumi na watu wa sheria na dini na wale wanaohusika na mambo ya vita na jihadi. Ukweli ni kwamba (ilipasa) wakaishuhudia watu wa aina mbali mbali wenye fikra na watatuzi wa matatizo (tofauti tofauti ya kijamii n.k.), wachunguzi na wenye juhudi (ya kutafuta amani) na wenye imani ya kweli na malengo ya kisiasa ambayo Waislamu wanawajibika kuyakusudia (yawe ni msimamo wao) katika maisha yao, inafaa waielekee Hijja watu wote hawa na Makka iko tayari kuwapokea na kuwaunganisha kwenye neno la Mwenyezi Mungu pembezoni mwa nyumba ya Mwenyezi Mungu, utawaona wakitambuana (kufahamiana huyu katoka wapi na ninani anafanya nini huko aliko) na wanashauriana na kusaidiana, hatimaye hurejea makwao hali ya kuwa ni umma mmoja (kitu kimoja) na nyoyo zilizoshikamana na mawazo na fikra za aina moja".[251]

Kwa hiyo ukweli ulivyo ni kwamba, aya hizi za Hijja zinaendelea mpaka zinamalizika na kuungana na kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Bila shaka Mwenyezi Mungu huwakinga wale walioamini, kwa hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini asiyeshukuru, wameruhusiwa (kupingana) wale wanaopigwa hiyo ni kwa sababu wamedhulumiwa, na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuwasaidia wale waliotolewa majumbani mwao pasipo haki ila kwa sababu wamesema kuwa, Mwenyezi Mungu ndiye Mola wetu, na kama Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangelivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyingine za ibada na misikiti ambamo jina la Mwenyezi Mungu hutajwa kwa wingi, na bila shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayesaidia Dini yake, hakika Mwenyezi Mungu nimwenye nguvu na ni mwenye kushinda".

Qur'an, 22:38-40

Mtiririko huu haukuja kwa bahati tu bila kutegemea, haiwezekani kwa aya za Qur'an zipangike kwa mpangilio huu bila ya kuwepo mahusiano baina yake.

Bila shaka mshikamano na mfumo wa namna ya aya hizi zilivyokuja kwa aina hii, kunaonyesha kuwepo maungamano yenye nguvu kati ya Hijja na matendo ya kisiasa.

Nasi hatukusudii kusema kuwa Hijja igeuke na kuwa uwanja wa mapigano, lakini kinachofahamika ndani ya mtiririko huo ni kuwa Hijja iwe ni hatua ya maandalizi ya mwelekeo (huo).

Kwa hakika kinachowezekana kukipata na kufaidika nacho katika mtiririko huu ambao umekusanya baina ya aya zinazohusu Hijja na Jihadi na kupinga dhulma, na kuwemo msaada wa Mwenyezi Mungu kwa wanaodhulumiwa inajulisha kwamba Hijja ni mahala bora pa Waislamu kujiandaa kiroho na kinafsi kukabilina na dhulma na wanaodhulumu, na kupinga ukandamizaji na wakandamizaji na pia kupinga ukoloni na wakoloni.

Bila shaka Hijja ni fursa nuzuri kwa Waislamu wanaokusanyika huko kutoka miji mbali mbali, kuonyesha nguvu waliyonayo na umoja wao, na watangaze msimamo wao wa umoja kisiasa na wawatamkie maadui mafunzo ambayo hawatayasahau pamoja nakuwa tendo hili haliishii kwenye Hijja tu kwani upinzani dhidi ya dhulma na wanaodhulumu na kutangaza chuki zao dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu ni jambo ambalo halina mipaka ya nyakati wala mahali.

Ndiyo maana wafasiri wametafsiri "Manufaa" kuwa ni mambo yanayojumlisha mambo ya dunia na dini.

lbn Jaririt-Tabari, baada ya kunakili kwake kauli nyingi kuhusu tafsiri ya "manufaa" ameandika kama ifuatavyo:

"Na kauli bora miongoni mwa kauli iliyo sawa, ni kauli ya yule aliyesema: Akikusudia hilo (yaani) "Ili washuhudie manufaa

yao" ni miongoni mwa matendo anayoyaridhia Mwenyezi Mungu na biashara, na hiyo ni kwamba Mwenyezi Mungu ameyajumlisha manufaa yao yote yanayoshuhudiwa na kipindi cha Hijja na huiletea Makka katika siku za msimu huo manufaa ya dunia na akhera na hakuhusisha kitu fulani miongoni mwa manufaa yao kwa kupitia riwaya yoyote au akili, basi manufaa hayo ni ya jumla."[252]

Kisha Qur'an imeieleza AI-Kaaba Tukufu kuwa imefanywa iwe ni Qiyam (Kisimamo) kwa ajili ya watu pale iliposema:

"Mwenyezi Mungu ameifanya Al-Kaaba nyumbaTukufu kuwa ni kisimamo kwa ajili ya watu.

Qur'an, 5:97

Na ndani ya Qur'an tamko "Qiyam" limekuja kuhusu mahali pale pale Mwenyezi Mungu anaposema,

"Wala musiwape wapumbavu mali zenu ambazo Mwenyezi Mungu amezijaalia kuwa ni Qiyam kwenu.

Qur'an, 4:5

Na hii inafahamisha namna ya kufanana baina ya Hijja na mali, kama ambavyo uchumi na mali vinaendesha maisha ya watu na kulinda maslahi ya umma na Kiislamu. Basi hivyo hivyo Hijja nayo ndivyo ilivyo, na hii ikiwa na maana kwamba mkusanyiko wa mambo yaliyomo ndani ya Hijja hauishii kwenye ibada na kuabudu peke yake na kuneynyekea tu, bali unayo nafasi pana kiasi cha kujumlisha kila kitu chenye mafungamano na maslahi ya Waislamu miongoni mwa mambo yanayoendesha maisha yao na mazingira yao.

Na kitu chochote kinachoendesha maisha yao (kitu hicho) ni bora kuliko matendo ya kisiasa ambayo yanalengo Ia kupinga ukoloni na utumwa na kunyonywa na kuthibitisha uhuru wao katika kila nyanja, na kuwazindua Waislamu kutokana na kuendelea kwa mambo yanayowazunguka ikiwemo njama na vitimbi na hatimaye kuwaelekeza kushika msimamo mmoja na kumpiga adui na kumzuia.

Kisha ikiwa haifai kuwapa mali watu wapumbavu ambao hawajui jinsi ya kuitumia kwa kukosa kwao kuwa na upeo wa maarifa au upungufu wa akili zao, basi haifai kabisa kwa njia ambayo inastahiki mno kuachwa Hijja ikawa mikononi mwa watu wasiotambua utukufu wake na uzito wake na umuhimu wake katika maisha ya umma wa Kiislamu.

Hebu tazama waliyoyasema baadhi ya wafasiri kuhusu aya hii:

Amesema Ibn Jaririt-Tabari: Mwenyezi Mungu anasema:

"Mwenyezi Mungu ameifanya Al-Kaaba nyumbaTukufu kuwa ni yenye kuwatengenezea mambo yao watu ambao hawana cha kuwatengenezea mambo yao kutokana na kiongozi ambaye anamzuwia mwenye nguvu dhidi ya mnyonge na muovu miongoni mwao dhidi ya mwema na dhalim dhidi ya anayedhulumiwa na akaifanya kuwa ndiyo utambulisho wa dini yao na maslahi ya mambo yao.[253]

Na ndani ya Tafsirul-Manar amesema kama ifuatavyo:

"Bila shaka (Mwenyezi Mungu) ameifanya Kaaba kuwa ni kisimamo kwa watu kuhusu mambo ya dini yao na ni yenye kurekebisha nyendo zao, na ni yenye kuzitakasa nafsi zao kwa yale aliyoyafaradhisha kwao katika Hijja, ambayo ni miongoni mwa nguzo kubwa za dini, kwani hiyo ni ibada ya kiroho na kimali na kijamii".

Na amesema tena: "Hakika uwekaji wa Mwenyezi Mungu wa mambo haya (Yaani Ibada za Hijja) ni kuweka kulikohusisha maumbile na sheria kwa pamoja na uwekaji huu unajumlisha kusimamia na kuyathibitisha maslahi ya dini yao na dunia yao".[254]

Na lau tutayafumbia macho yote hayo basi Je, ni kweli itawezekana kuifumbia macho sura ya Bara'ah ambayo inatangaza wazi msimamo wa kisiasa kuwahusu washirikina, ilishuka (Sura hii) ili isomwe ndani ya siku za Hijja nalo ni tendo la kisiasa bila ya shaka yoyote.

Basi hebu na tuisikilize Qur'an Tukufu inasema:

"(Hili ni) tangazo la kujitoa katika dhima, litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina (Makafiri) - (waambieni) basi tembeeni katika nchi kwa miezi minne na mtambue kwamba ninyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwadhalilisha makafiri. Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwenda kwa watu kuwajulisha siku ya Hijja kubwa kwamba, Mwenyezi Mungu yu mbali na washirikina na pia Mtume wake (yu mbali nao) basi kama mkitubu ndiyo kheri kwenu na mkikengeuka basi jueni kwamba ninyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na wapashe waliokufuru habari ya adhabu iumizayo:

Qur'an, 9:1-3. Na zinazofuatia.

Na Mtume Mtukufu [s] alimuamrisha Imam Ali [a] alifikishe onyo hili na tangazo hili kwa washirikina ndani ya siku za Hijja, basi Imam Ali akafanya hivyo na liii ni kwa ushahidi wa wana tafsiri wote na wanahistoria na wanahadithi wote.

Ndani ya tafsiri ya Tabari kuna hadithi yenye Isnad kama ifuatavyo:

"Ilipofika siku ya kuchinja (siku ya kumi mfunguo Tatu) Ali bin Abi Talib (R.A.) alisimama akawatangazia watu kile alichoamuriwa na Mtume na Mwenyezi Mungu [s] akasema:

"Enyi watu nimeamuriwa mambo manne:

(1) Asiikurubie nyumba hii baada ya mwaka huu mshirikina yeyote.

(2) Na wala asitufu uchi yeyote.

(3) Na haitaingia peponi isipokuwa nafsi iliyosilimu.

(4) Na atimize ahadi yake kila aliye na ahadi.

Katika Riwaya nynigine imesema: "Na yeyote aliye na ahadi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu [s] basi na aitimize kwa muda wake.[255]

Na ukipenda unaweza kusema kwamba kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema: "(Hili ni) tangazo la kujitoa katika dhimma, litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina". Na kauli yake aliposema: "Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwenda kwa watu kuwajulisha siku ya Hijja kubwa kwamba Mwenyezi Mungu yu mbali na washirikina na pia Mtume wake (yu mbali nao)", bila shaka kujitenga kulikotajwa ndani ya aya hizi mbili hakuhusiani tu na washirikina wa Kiquraishi au washirikina wa Bara Arabu peke yao bali kujitenga kulikokusudiwa ndani ya aya hizo mbili ni tangazo la Kiungu linalokusanya washirikina wa ulimwengu mzima, waliokuwepo katika zama zake Mtume [s] na baada ya hao mpaka siku ya Kiyama.

Qur'an Tukufu inafunza umma wa Kiislamu na kufafanua daraja yao ya kidini na inawalazimisha kujibari (kujitenga) na washirikina wote katika zama zote, na kwa sababu hiyo lau wageni wa Mwenyezi Mungu wote watajibari kutokana na walahidi na washirikina wanao wakandamiza, basi watakuwa wametekeleza wajibu wao kwa pamoja.

Na huenda ikafikiriwa kwamba, kujibari na kuwapinga (washirikina) kulikokuja katika aya hizi, kunahusika na zama aliyoishi Mtume [s] wala haikuvuka baada ya hapo, kwa hakika hiyo ni kauli isiyo na dalili, nayo ni mfano wakauli ya watu waovu ambao wanataka kuuhusisha ujumbe wa Mtume [s] na mwongozo wa Qur'an Tukufu katika zama maalum pasina zama zingine.

Nami sifikiri kwamba Muislamu aliye huru atakuwa na shaka kwamba, wakomunisti na wanaowaunga ni wabaya mno kuliko washirikina ambao ufunuo wa Mwenyezi Mungu umewajibisha kujitenga nao, kama ambavyo sifikirii mtu mwenye insafu atakuwa na shaka kwamba shetani mkubwa (Amerika) ni mbaya mno na ni mwenye madhara mno kuliko washirikina. Kama ambavyo imekuja ndani ya vitabu ya pande mbili (Sunni na Shia) kwamba Hisham Ibn Abdil-Malik alihiji katika zama za Ukhalifa wa Baba yake na akatufu, kisha akataka aibusu "Hajar-al-Aswad, "lakini hakuweza kutokana na msongamano (wa watu) basi akatengenezewa mimbar na akakaa juu yake, mara akaja Ali bin Husein [a] akiwa amevaa Ihram, akiwa ni mwenye uso mzuri kuliko watu wote na mwenye harufu nzuri na kwenye paji lake la uso kuna athari ya Sijda inaonekana kama koti la kondoo, akaanza kutufu Al-Kaaba na anapofika kwenye Hajar al-Aswad watu humpisha ili aibusu kwa kumheshimu na kumtukuza, basi jambo hilo likamchukiza Hisham, na mtu mmoja katika watu wa Sham akamuuliza Hisham "Ni nani mtu huyu ambaye watu wamemuheshimu kwa heshima hii na wamempisha kwenye Hajar al-Aswad?

Hisham akasema: "Simjui", Alijibu hivyo ili tu watu wa Shamu wasije wakampenda Imam Ali bin Husein.

Basi Farazdaq aliyekuwepo hapo akasema: "Lakini mimi namjua". Yule mtu wa Shamu akamwambia "Ni nani huyu Ewe Abu Faras"? Farazdaq akasoma Qasida, nasi tunataja hapa sehemu ya beti zake.

"Huyu ndiyo yule ambaye Makka inatambua sauti ya nyayo zake, nayo Al-Kaaba na nje ya Makka na Haramu ya Makka zote zinamtambua. Huyu ni mwana wa mmbora wa waja wa Mwenyezi Mungu wote. Huyu ndiye mcha Mungu mtakasifu mwenye tahara na ni bendera ya uongofu. Huyu ndiye ambaye mzazi wake ni Ahmad mteule, Mola wangu amsalie mpaka siku ya Qiyama".

(Aliendelea) mpaka akasema:

"Babu yake ni miongoni mwa Quraishi katika nasaba yake ni Muhammad kisha Ali ambaye ni bendera ya viongozi mashahidi wake ni vita vya Badri na pango la mlima wa Uhdi na vita vya Khandaq na wote walijulikana siku ya Fat-hi Makka, na Khaybar na Hunayn zinamshuhudia na siku ya Quraydha".[256]

Namna hivi ndivyo mshairi huyu mkubwa wa Kiislamu anavyomkabili khalifa huyo mjeuri kwanjia ya kaswida hii ya kishujaa na anamuarifisha Imam wa haki kutoka katika kizazi cha mtume katika mkabala wenye changamoto la kisiasa.

Jambo ambalo linajulisha kwamba jambo hili ni sheria (kufanyika) katika msimu wa Hijja na kujuzu kwake ni kutokana na kutopingwa na Mwislamu yeyote siyo zama hizo wala baada ya hapo.

Na kwa maneno mengine tunaweza kusema kwamba, mshairi huyo analazimika kufanya munadhara huo wa kisiasa wenye nguvu iii amtambulishe Imam mbele ya mkusanyiko wa Mahujaji waliofika kwenye nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, kwa kumzingatia kuwa ndiyo mrithi wa haki wa kizazi cha mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s], na tukio hili linatupatia dalili iliyo wazi kwamba, tendo la kisiasa katika msimu wa Hijja linazingatiwa kwa mujibu wa kanuni na sheria, na hiyo ni kwa sababu hakuna kizuwizi au uharamu wa kutekeleza matendo kama haya, sawa sawa ni katika siku hizo, au miaka iliyofuatia siku hizo.

MALENGO YA HIJJA YA KIJAMII NA
KISIASA KATIKA SUNNAH

Kwa hakika Sunna na sera tukufu ya Mtume na kitu kingine kinachoashiria kwamba, Mtume [s] alifanya matendo ya kisiasa katika Hijja, na zaidi ya hapo kuna hadithi zinazofidisha kwamba Hijja ni aina ya jihadi pale Mtume [s] aliposema:

"Jihadi iliyo bora ni Hijja".[257]

Na kauli yake Mtume [s] isemayo: "Hijja ni Jihadi"

Na pia kauli yake Mtume [s]: "Hijja ni Jihadi ya kila mnyonge"

Hadithi hizi mbili za mwisho zinapatikana katika: Sunan lbn Majah: Al-Manasik, na Sunan an-Nasai: Al-Haj, Na Musnad ya Ahmad bin Hanbal.

Na kauli yake Mtume [s] alipokuwa akiwajibu wanawake walipomtaka waende katika Jihadi akasema: "Jihadi yenu ni Hijja"

Na katika baadhi ya hadithi Mtume [s] amelinganisha Hijja na Jihadi kinyume cha faradhi zingine hakuzilinganisha nayo, aliposema: "Mwenye kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na mwenye kuhiji na mwenye kufanya umra niwageni wa Mwenyezi Mungu aliowaita".[258]

Na hadithi hii inaonyesha kupatikana kwa maungamano na wajihi wa kufanana katika athari na malengo baina ya faradhi hizi mbili na ukitaka unaweza kusema:

"Hakika hadithi hii inaonyesha kwamba Hijja si mujaradi wa ibada kwa maana inayoelekeweka, bali ni tendo linalofanana na jihadi yaani ni ibada na ni tendo Ia kisiasa, basi Hijja ni msimu wa tendo la kisiasa kama ambavyo ni msimu wa ibada na unyenyekevu na kumuelekea Mwenyezi Mungu kwa kumuabudu."

Kisha ni kwamba, sera inatusimulia kuwa Mtume Mtukufu [s] alihutubu mahala pawili (yaani) Arafah na Mina na akatangaza katika hotuba yake misimamo na hukumu muhimu za Kiislamu, za kiuchumi, kisiasa na za kijamii, hapa tunataja sehemu ya hotuba hiyo:

Katika Sunan At-Tirmidhi: Imepokewa toka kwa Jabir ndani ya mlango wa Hijja ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] amesema: Ilipofika siku ya Tarwiyyah (siku ya nane ya mfunguo Tatu) na wakaelekea Mina na wakasoma Tal-Biya ya Hijja, Mtume [s] pia alikusudia na akasali Mina Adhuhuri na Alasiri na Magharibi, na I'sha na Asubuhi, kisha akakaa kidogo mpaka jua likachomoza na akaamuru khema lake lililotengenezwa kwa manyoya lisimikwe Namirah, Mtume akaenda mpaka Arafat akakuta hema lake limesimikwa, akateremka mpaka jua likapanda juu, akaamuru ngamia wake aletwe, na akaletwa basi akapanda mpaka akafika Bat-Nul-Wadi na akawahutubia watu akasema:

1) Bila shaka Damu yenu na mali zenu ni vitu vyenye heshima juu yenu, kama ilivyo na heshima siku yenu hii ya leo katika mwezi wenu katika mji wenu huu.

2) Fahamuni ya kwamba kila kitu katika mambo ya kijahiliya kiko chini ya nyayo zangu hizi (yaani vimebatilishwa).

3) Na Damu za wakati wa Jahiliyah zimeondolewa, na damu ya kwanza ninayoiondoa ni ya Rabia Ibn Al-Harith (Ibn Ammi ya Mtume, alikuwa amepelekwa kulelewa katika Bani Saad watu wa kabila la Huzail wakamuua)

4) Na riba ya Jahiliyah imeondolewa na riba ya kwanza ninayoindoa ni riba ya Abbas Ibn Abdil-Muttalib, hii imeondolewa yote.

5) Hakika kila Muislamu ni ndugu wa Muislamu na kwamba Waislamu wote ni ndugu, basi hakiwi halali chochote kwa mtu kutoka kwa nduguye isipokuwa kile alichompa kwa moyo safi.

6) Vitu vitatu moyo wa Muislamu usifanye hadaa juu ya vitu hivyo: Kufanya ikhlasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu katika matendo, kuwa na moyo safi kwa Maimamu wa haki na kushikamana na jamaa ya waumini.

7) Katika Uislamu watu wote ni sawa, watu wote wanatokana na Adam na Hawa hapana ubora kwa Muarabu juu ya asiyekuwa Muarabu isipokuwa kwa kumcha Mwenyezi Mungu.

8) Bila shaka Muislamu nduguye ni Muislamu, asimdanganye nduguye wala asimfanyie khiyana wala asimtete wala damu yake haiwi halali kwake wala kitu chake chochote hakiwi halali kwake isipokuwa kwa radhi ya nafsi yake.

9) Msije mkarudia kuwa makafiri wenye kupotea baada yangu, baadhi yenu wasiwakandamize wengine.

10) Kwa hakika ninyi mutaulizwa, basi aliyepo na amfikishie asiyekuwepo.

Kisha Mtume [s] aliwashuhudisha mara tatu mambo aliyoyabalighisha, nao masahaba wakashuhudia kwake juu ya hayo.[259]

Na bila shaka mapokezi sahihi yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume [s] miongoni mwa dua na dhikri zinazohusu Hijja, mambo ambayo yameshikamana na maana za kisiasa pamoja na maana za Tauhidi.

Ni ushahidi bora juu ya kuwa Hijja ni msimu unaonasibu (unaostahiki) kwa Waislamu kudhihirisha msimamo wao kwa maadui wa Mwenyezi Mungu na Uislamu na pindi tutakapofahamu kuwa ni mustahabu kuzikariri dua hizi wakati wa ibada kwa mfano dua ifuatayo:

"Lailaha-illa-llah Wahdahu la Sharika Lahu Lahul Mulku Walahul-Hamdu Yuhyi Wayumitu Wahuwa Ala kulli shain Qadir."

Lailah illa-llah Wahdahu Wahdahu Anjaza Waadahu Wanasara Abdahu Wahazamal-Ah-Zaba Wahdah.[260]

Haya ni pamoja na ishara zinazopatika katika Manasikul Haj.

Kila ibada iliyomo ndani ya ibada hizi inaashiria kwenye jambo la kijamii na kisiasa na kiakhlaq (Muenendo) zaidi ya kuwa kwake ni ibada na ni kutii japokuwa hatuwezi kujua kwa ukamilifu kila mama zilizomo katika Ibada hizi.

Wanachuoni wengi wa Kiislamu na wanafikra wa Kiislamu wameyaashiria mambo yanayoelekezwa na ibada hizi, miongoni mwake yamo mambo ya kiroho, kiuchumi, kijamii na kisiasa, nasi tunamfupishia msomaji mtukufu ili kufanya mukhtasari.

Kwa hiyo kuna zaidi ya mambo ambayo yanajulisha kuwa Mtume [s] aliyachanganya matendo ya kiibada na matendo ya kisiasa katika Hijja.

Ndani ya Bukhari, imepokewa kwa Said bin Jubair kutoka kwa Ibn Abbas amesema:

"Pindi Mtume ([s] alipofika katika mwaka aliopewa amani (mwaka wa saba Hijiriya) akasema, ongezeni mwendo (katika Saayi)". Mtume alifanya hivyo iii awaonyeshe washirikina nguvu za Waislamu.

Ibn AI-Athir amesema ndani ya An-Nihayah, Mtume aliwaamuru Masahaba wake kuongeza mwendo katika Tawafu wakati wa umrah ya Qadhaa (mwaka wa saba Hijiriya) ili kuwaonyesha washirikina nguvu za Waislamu, kwa sababu washirikina walikuwa wakisema, "Limewadhoofisha joto la Madina" na ni sunna katika baadhi ya tawafu tu. Na pindi Uislamu ulipoimarika na kupata nguvu, Umar akasema, "Kuna haja gani sasa hivi kuongeza mwendo, yaani kutufu kwa aina ile, au kuacha wazi mabega, na Mwenyezi Mungu amekwisha yasawazisha mambo ya Waislamu na ameifukuza kufru na makafiri".

Ibn al-Athir amesema tena:

"Muradi wa Umar kusema, Ramalani, maana yake ni tawafu pekee iliyosuniwa kwa ajili ya kuwaonyesha makafiri".

Na hii inaashiria kuwa inajuzu kuziunganisha ibada za Hijja kwenye makusudio ya kisiasa na malengo yake ya Jihadi, kwa mfano kuwakhofisha maadui kama vile kuwaogopesha maadui na kupinga matendo yao na kuziangamiza njama zao na kuiumbua mipango yao.

Kisha Je, hivi Mtume [s] kuzichagua Suratut-Tauhid "Qul-Huwallahu Ahad" na Suratul-Kafiruna katika Sala ya kutufu na kuzipendekeza zisomwe na muislamu anayehiji wakati kuna Sura nyingine na aya nyingine ambazo zinazo maana na malengo ya kiakhlaq na mafunzo zaidi na kushuhudia kwamba Hijja ni mkusanyiko wa Kiislamu wa ulimwengu na kwamba mkutano huu ni wakati mzuri wa kutangaza msimamo uliyo wazi dhidi ya nguvu za kufru na ubeberu kama ambavyo inajulisha hivyo (kwa mapokezi yasemayo) kwamba Umar Ibn Khattab pindi akipiga Takbira na kulibusu jiwe alikuwa akisema: "Bismillahi Wallahu Akbaru ala Mahadana, Lailaha illa llahu la Sharika lahu Amaantu Billahi Wakafartu Bittaghuti"[261]

Maana ya maneno hayo: "Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa juu ya aliyotuongoza, hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu asiye na mshirika, nimemuamini Mwenyezi Mungu na nimeyakufuru mataghuti". Kisha ni kwamba Imam Jaafar bin Muhammad As-Sadiq [a] amesema katika kubainisha falsafa ya Hijja kama ifuatavyo:

"Bila shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaumba viumbe si kwa ajili yoyote isipokuwa alitaka na akafanya, akawaumba mpaka ulipofika muda fulani akawaamuru na kuwakataza, kuhusu mambo ambayo yatakuwa ni miongoni mwa mambo ya utiifu katika dini na maslahi yao miongoni mwa mambo ya dunia yao, basi akafanya ndani yake mkusanyiko wa (watu) kutoka mashariki mpaka magharibi ili wafahamiane.... Na ili athari za mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] zitambulike na habari zake nazo zijulikane zisije zikasahaulika, na lau kila watu wangelitegemea miji yao na yaliyomo basi wangeangamia na miji ingeharibika na mapato na faida vingeanguka na khabari zingepotea na wasingefahamu chochote, basi hiyo ndiyo sababu (ya kuweko kwa) Hijja".[262]

Na vile vile imepokewa toka kwake Imam Jaafar As-Sadiq [a] amesema:

"Hapana uwanja wowote unaopendwa mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko Mas-aa (Mahala pa Saayi baina ya Safa na Marwa) kwani mahala hapo hudhalilika kila mwenye nguvu.[263]

MALENGO YA HIJJA YA KISIASA NA YA
KIJAMII KATIKA SERA YA SALAFU

Bila shaka historia inatusimulia kwamba Salafus-Salih hawakufupizika na matendo ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na ibada tu katika Hijja, bali munasaba huu wa Hijja waliutumia kwa ajili ya matendo ya kisiasa kuwa ni sehemu ya asili katika faradhi hii na siyo kitu chenye kuzidi juu yake au kilicho nje yake.

Basi huyu hapa Imam Husein Ibn Ali ambaye ni mjukuu wa Mtume [s] anatoa hoja cihidi ya mtawala jeuri miongoni mwa watawala wa zama zake hapo Mina katika kipindi cha Hijja.

Hakika Imam [a] aliwakusanya Bani Hashim wanaume na wanawake na wafuasi wao wenye kuhiji na wale wasiohiji na Ansari ambao ni wafuasi wake na watu wa nyumba yake, kisha hakumwacha yeyote miongoni mwa Masahaba wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] na watoto wao na (Tabiina) na Maansari waliokuwa mashuhuri kwa uchamungu na ibada.

Basi wakakusanyika hapo Mina zaidi ya watu elfu moja na wengi wao walikuwa Tabiina na watoto wa Masahaba, na Imam Husein [a] akatoka kwenye hema lake akasimama kuhutubia, akamhimidi Mwenyezi Mungu na akamtukuza kisha akasema:

"Amma baad, kwa hakika ujeuri huu tumefanyiwa sisi jambo ambalo nyote munalijua, mumeliona, mumelishuhudia na limekufikieni, nami kwa hakika nataka kuwaulizeni vitu fulani basi iwapo nitakuwa mkweli nisadikisheni, na nikiwa muongo, basi nikadhibisheni, sikilizeni usemi wangu na mufiche kauli yangu kisha murudi kwenye miji yenu na makabila yenu, yeyote mutayemuamini na mukawa na imani naye mwiteni (mumjulishe) yale muyajuayo kwani mimi naogopa haki hii itafutwa na kutoweka na Mwenyezi Mungu ndiyo mwenye kutimiza nuru yake japokuwa makafiri watachukia.[264]

Basi Imam Husein [a] hakukiacha chochote alichokiteremsha Mwenyezi Mungu ndani ya Qur'an kuhusu Ahlul Bait ila alikisema..... Na alisema: "Nakuombeni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, mukirudi msimulieni yeyote munayemuamini".

Kisha alishuka na watu wakatawanyika. Naye Uthmani lbn Affan anaiandikia miji yote ya Kilslamu zama za ukhalifa wake barua ambayo ndani yake alisema kama ifuatavyo:

"Hakika mimi ninawalazimisha magavana wangu wanifikie katika kila msimu (wa Hijja) na kwa hakika umma umepewa madaraka ya kuamrisha mema na kukataza maovu, basi hapana chochote kitakachodaiwa dhidi yangu au dhidi ya magavana wangu ila nitampa anayestahiki, na sina mimi wala magavana wangu haki upande wa raia isipokuwa imeachwa kwao, na kwa hakika watu wa Madina wameniletea mashitaka kwamba kuna watu wanashutumu na kupiga (wenzao) basi yeyote mwenye kudai chochote katika hayo na aje kwenye msimu (wa Hijja) achukue haki yake ikiwa ni kutoka kwangu au kwa magavana wangu au msamehe kwa hakika Mwenyezi Mungu anawalipa wenye kusamehe.[265]

Bali hata wasiokuwa Waislamu walipata fursa ya kuaridhi mashtaka yao kwa Khalifa katika Hijja, basi Khalifa husimama kuwapatanisha ndani ya kipindi cha Hijja na siyo baada ya kipindi hicho, basi sote tunakijua kisa cha mtoto wa Kimisri aliyefanya mashindano na mtoto wa Amri bin Aas (gavana wa Misri) na yule Mmisri akashinda, mtoto wa Amri akampiga yule mtoto wa Kimisri, basi baba wa mtoto wa Kimisri akaeleza mashtaka yake kwa Umar, Umar akamchukulia kisasi katika msimu wa Hijja mbele ya macho na masikio ya maelfu ya mahujaji kisha akamwambia Liwali Amri lbn Al-Aas mbele ya ushuhuda wa mkusanyiko mkubwa:

"Ewe Amri ni lini mumewafanya watu kuwa watumwa na hali ya kuwa mama zao waliwazaa wakiwa huru".[266]

Na hapa inafaa tuashirie mambo aliyoyaandika mwandishi wa Kiislamu wa zama hizi muheshimiwa Dr. Yusuf Al-Qar-dhawi katika kitabu chake muhimu kuitwacho, 'Al-lbadatu-fil-Islam", kuhusu lengo hili.

"Makhalifa walitambua umuhimu wa msimu huu wa kiulimwengu, wakaufanya kuwa ndiyo nafasi ya kukutana baina yao na wanachi wanaokuja kutoka masafa ya mbali, na baina yao na magavana wao kutoka katika miji, basi yeyote miongoni mwa watu mwenye kudhulumiwa au mwenye mashitaka na ayalete kwa Khalifa mwenyewe bila ya wasita wowote wala kizuwizi, na huko wananchi wamkabili gavana mbele ya Khalifa bila ya woga wala kificho, basi hapo husaidiwa mnyonge na haki kupewa aliyedhulumiwa na haki kurejeshwa kwa mwenyewe hata kama haki hii ni ya gavana au Khalifa."

Basi iwapo Hijja ni msimu wa kuibainisha dhulma na malalamiko yatendwayo na watawala na wasimamizi wa Kiislamu, je, haiwi ni bora zaidi kujulisha ndani yake malalamiko kwa wakoloni na wafuasi wao na watumishi wao na kuwasaidia Waislamu dhidi yao?

Na Je, inajuzu kumlalamikia mtawala Muislamu anapovuka mipaka yake lakini haijuzu kumlalamikia mkoloni dhalimu mvamizi aliyetoka nje na hali yakuwa anafanya maovu na mauaji?

MALENGO YA HIJJA YA KISIASA NA KIJAMII
KATIKA KAULI ZA WANACHUONI

Kwa hakika wanachuoni na wanafikra wengi wa Kiislamu wameandika umuhimu wa Hijja kisiasa na kijamii na wakazingatia kuwa ni msimu bora na fursa nzuri kwa Waislamu kuonyesha nguvu yao, mshikamano wao, muamko wao na umoja wao kwa kauli na matendo na kwa dhahiri na hisia.

Basi huyu hapa Al-Allamah Muhammad Farid Waj-di anaiandika ndani ya Dairatul-Maarif yake Maddah ya Hijja anasema:

"Amma hekima ya kufaradhishwa Hijja kwa Waislamu, hakuna nafasi ya kueleza katika kitabu hiki, lakini kitu ambacho ni wazi kuhusu Hijja ni kwamba lau wenye mamlaka ndani ya Waislamu wangetaka kuitumia Hijja katika kuleta umoja wa Kiislamu basi wangefaulu. Kwani hukusanyika kwa mamilioni ya watu katika uwanja mmoja kutoka miji mbali mbali ya ulimwengu na kuzielekeza nyoyo zao na masikio yao mahala hapo penye kukhofisha kwa kila linalotolewa kwani huwajibisha kuwaathiri wote kwa roho moja na hasa watakapolinganiwa mambo ambayo ndani yake mna kheri zao, basi pindi wataporudi kwenye nchi zao na wakatawanyika kwenye miji yao watayatangaza mambo waliyojifunza kwa ndugu zao, na watakuwa kwao ni kama wajumbe wa mkutano mkuu uliohusisha jinsi zote na zama zote, ambapo wajumbe wake hukutana kila mwaka mara moja, basi ni athari iliyoje unayoikadiria kwa tukio hilo tukufu katika maisha ya umma huu mkubwa, na ni matokeo gani bora unayoyatarajia kutokana nalo pindi umma huu utakapozindukana kutoka katika usingizi wake. Basi Hijja itakuwa miongoni mwa nyenzo zake kubwa, na unafahamu ya kwamba mataifa ya nje yanayozikalia baadhi ya nchi za Kiislamu yanawazuia raia zake kufanya Hijja, kwani mabadiliko ya maisha lau yataenea (yataingia) ndani ya mataifa hayo. Hakuna chochote kitakachoweza kuyazuwia, na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye amri siku zote.[267]

Na imekuja ndani ya kitabu kiitwacho: "Ad-Dinu Wal-Hajj Alal-Madhahibil-Arba" kama ifuatavyo:

"Hijja ni njia ya mafahamiano, mshikamano, usawa na kuimarisha mahusiano na ushirikiano na maungamano baina ya mataifa ya Kiislamu. Basi nyoyo zao hushikamana na tamko lao kuwa moja na kutenda kitu kitakachotengeneza hali yao na kurekebisha dosari katika mambo yao".

Na ameandika ustadhi mtukufu Muhammad Mubarak ambaye ni mshauri katika chuo kikuu ya Mfalme Abdul-Aziz, amesema (katika maandiko yake): "Madhumuni ya Ibada peke yake bila kuunganisha na kitu chote iko wazi katika Hajji lakini kaiunganisha pamoja na maana nzuri ya kijamii, kwani Hijja ni mkutano wa ulimwengu (ambao) hukusanyika washiriki katika uwanja mmoja kwa ajili ya ibada ya Mungu mmoja. Pamoja na hayo ibada hii siyo kwamba imejitenga na maisha (ya kila siku) bali imeshikana nayo kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema ndani ya kitabu chake kitukufu, "Ili washuhudie manufaa yao na kutaja jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalum" (Qur'an, 22:28), basi kushuhudia manufaa yao ni maana pana, inawezekana kukusanya maslahi mbali mbali ya Waislamu".

Kwa hiyo iwapo tendo la kisiasa linajuzu ndani ya Hijja, kama ulivyokwisha tambua kutokana na Qur'an na Sunna na sera ya Salaf na kauli za wanachuoni watukufu bali Hijja ni fursa inayofaa kuwakhofisha maadui na kuwatisha na kuzitokomeza njama zao, basi ni adui gani aliyedhidi yenu kuliko Amerika ambayo inafanya njama dhidi ya Uislamu na Waislamu siku zote na inapora mali zao na kuiba Petroli yao?

Na Je, Ni adui gani aliye dhidi yetu kuliko Israel ambayo imepora ardhi yetu na kuwafukuza wananchi wetu na ikawaua na inaendelea kuwaua watoto wa Kipalestina na kuhalalisha mauaji yao na kuvunja utu wao?

Na ni adui yupi aliye dhidi yetu kuliko Urusi ambayo inayoufanyia uadui Uislamu na Waislamu katika itikadi na katika kila kitu na inaikalia ardhi yetu ndani ya Afghanistan na kuwaua vijana wake na kuibomoa miji yake na inaendelea (kufanya hayo)?

Na Je, ni adui gani aliye dhidi yetu kuliko Uingereza ambayo imeunda dola ya Israel na ikafanya njama na inaendelea kufanya njama dhidi yetu kwa mujibu wa chuki za jadi za vita ya msalaba.

Na ni adui gani aliye dhidi yetu kuliko Ufaransa ambayo imeua malaki ya wanachi wetu Waislamu katika Algeria, na bado inaendeleza mauaji na njama huku na huko katika miji ya Waislamu?

Na ni kwa nini tunatofautisha baina ya Marekani na Urusi na wote hao mila yao ni moja katika kuipinga dini yetu na kufanya njama mbaya dhidi yetu na kuyaua mataifa yetu na kupora utajiri wake?

Na ni kwa nini tunaiacha fursa ya Hijja Tukufu na mkusanyiko wa pekee wa mamilioni (ya Waislamu), mkusanyiko ambao unakusanya nchi 40 za Kiislamu upotee bure bila ya kuutumia kuwaamsha Waislamu na kuwafanya wajitolee kupinga maovu ya (watu wa) magharibi na mashariki dhidi yetu. Na Je, hivi sisi tunazijua hukmu za Hijja zaidi kuliko Mtume [s] na Salaf wema

waliokuja baada yake ambao katika Hijja walikuwa wakichanganya baina ya ibada na matendo ya kisiasa?

Na ni kwa nini hatutoi nafasi katika Makka, Madina, Arafat, na Mina kwa Wapalestina, Philipine, Iraq, Iran, Afghanistan, Africa, Lebanon na Eritrea na kwingineko wanakodhulumiwa wabainishe dhuluma (wanazotendewa) na wawaamshe Waislamu juu ya yale wanayokabiliana nayo miongoni mwa dhulma na ukandamizaji na mauaji na jinai za kikoloni na wafuasi wao na watumishi wao?

Na ni kwa nini hatutoi fursa katika Hijja ili wanafikra wa Kiislamu kutoka kila nchi na sehemu zote wajadili matatizo ya Waislamu na watafiti ufumbuzi wa pamoja wa taabu wanazozipata toka kwa mabeberu?

Kwa nini watawala wa Makka na Madina hawatoi nafasi kufanyika mikutano ya Jumuiya ili kuwajulisha Waislamu undani wa ukoloni wa Kimarekani, Kirusi, Kiingereza, na Kifaransa na malengo yao ya kishetani na wafahamishe matendo wanayotenda wavamizi hawa kutoka nje, ikiwa ni pamoja na kupora na kuiba na kuua na ukandamizaji.

Mpaka lini Hijja itatengwa na athari zake za kijamii na kisiasa chini ya mapendekezo ya watu kutoka nje?

Na ni mpaka lini idadi hii kubwa ya Waislamu kutoka kila sehemu ya ulimwengu (itaendelea) kukusanyika kisha kutawanyika bila ya ndugu huyu kumtambua nduguye na bila ya ndugu huyu kuyajua matatizo na matarajio ya nduguye? Na ni hadi lini (Tutaendelea) kuipoteza fursa hii kubwa ambayo Uislamu umeiandaa kwa ajili ya umma huu?

Na iwapo Hijja itatupita (tukakosa kuitumia) basi ni wapi pengine itakapowezekana kuupata mkusanyiko huu mkubwa na idadi kubwa, na kongamano hili la waumini lililojiandaa kutenda na kuitika wito wowote wa Kiislamu unaowataka kupigana jihadi na kuwahimiza kuwa na muamko?

Na ni vipi watawala wa Hijazi wanakubali waipoteze fursa hii kubwa na wanawazuia Waislamu kunufaika nayo kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu (Na washuhudie manufaa yao)?

Bali ni vipi Waislamu wenyewe wanaruhusu kuiacha fursa ya Hijja ipotee bure bila ya kuitumikisha katika njia ya mambo yao yanayowahusu na kutatua matatizo yao?

UCHAMBUZI WA MWISHO

Hapa zimebakia sehemu mbili muhimu za uchunguzi tutazionyesha katika sehemu hii ya mwisho, nazo ni kama ifuatavyo:

A). Kumlilia maiti kabla ya kuzika au baada ya kuzika.

B). Kudhifia tamko la "Abdi" kwa mja.

Basi huenda mtu asiyejua hukmu za sheria akadhani kuwa, sheria zimeyaharamisha mambo hayo, na sasa hivi tunabainisha hukmu zake kwa mujibu wa kitabu (Qur'an) na sunnah na tunasema:

Kwanza: Kumlilia maiti:

Jicho na moyo havilaumiwi pindi mtu anaposimama juu ya kaburi la Mtume wake na Maimamu wa nyumba ya Mtume [a] na Masahaba wema R.A. (Jicho halilaumiwi) kutoa machozi (na moyo) kuhuzunika, ili kuonyesha kilichomo ndani (ya nafsi) katika upendo, kutawalisha, mapenzi, huruma na shauku, na kwa hakika jambo hili linafuatana na maumbile ya kibinaadamu na wala sheria ya Mwenyezi Mungu hailipingi.

Amma maumbile (yalivyo) ni kwamba:

Huzuni na kuathirika hulazimiana na huruma ya kiutu pindi mtu anapojaribiwa kwa msiba wa mtu ampendaye miongoni mwa wapenzi wake au mtoto wake na ndugu zake, na yeyote asiyekuwa na hisia hii huhesabiwa kuwa ni wa pekee katika maumbile ya kiutu, na wala simuoni yeyote ulimwenguni anayekanusha ukweli huu kwa nguvu zake zote.

Ama Sheria: Inatosha (kulieleza) hilo kufuatia kilio cha Mtume Mtume [s] na Masahaba na watu waliowafuatia kwa wema kuwalilia maiti wao.

Basi huyu hapa mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] anamlilia mwanawe mpenzi "Ibrahim" na anasema: "Jicho linatoa machozi na moyo unahuzunika, na wala hatusemi (chochote) isipokuwa kile anachokiridhia Mola wetu, nasi kwako Ewe Ibrahim ni wenye kuhuzunika:[268]

Wanasira na wanahistoria wamepokea kwamba wakati Ibrahim mtoto wa Mtume alipokuwa katika 'Sakratul-maut' Mtume [s] alikuja akamkuta migunni mwa mama yake, akamchukua na kumweka miguuni mwake akasema:

"Ewe Ibrahim hakika sisi hatuwezi kukutosheleza kitu kwa Mwenyezi Mungu". Kisha macho yake yakatiririka machozi na akasema: "Hakika sisi kwako wewe ni wenye kuhuzunika Ewe Ibrahim, jicho linalia na moyo unahuzunika na wala hatusemi kitakachomchukiza Mola, na lau lisingekuwa ni jambo la haki na ahadi ya kweli basi tungelikuhuzunikia huzuni kubwa mno kuliko hii".

Na pindi Abdur-Rahman bin Auf alipomwambia Mtume kwamba; "Je, Hukutukataza kulia"?

Mtume alijibu kwa kusema: "Hapana, lakini nilichokataza ni sauti mbili za ujinga na sauti mbili zingine: Sauti wakati wa msiba, na kilio cha kishetani na sauti ya ngoma, na kilio changu hiki ni huruma, na asiyekuwa na huruma hahurumiwi".[269]

Na kilio hiki cha Mtume [s] hakikuwa ni cha kwanza na cha mwisho wakati akijaribiwa kwa misiba ya wapenzi wake, bali alikuwa akamlilia mwanawe "Tahir" na husema:

"Jicho linatoa machozi, na machozi hayazuiliki, na moyo unahuzunika na wala hatumuasi Mwenyezi Mungu"[270]

Na Al-Allama AI-Amini ndani ya kitabu chake kikubwa kiitwacho 'Al-Ghadir," amekusanya mahali pengi ambapo Mtume [s] na Masahaba na Tabiina waliwalilia maiti wao na wapenzi wao pindi walipofariki na hapa tunanakili ibara ya mwanachuoni huyu mtafiti:

Huyu hapa Mtume [s] wakati Hamza R.A. alipouawa, kisha Safiyah binti Abdil-Muttalib R.A akaja akimtafuta Hamza, Maansari wakamzuia, basi Mtume [s] akasema "mwacheni". Akakaa mbele yake, ikawa Safiyah anapolia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu naye hulia, na anapozidisha kulia kwa uchungu, Mtume [s] naye hulia kwa uchungu. Naye Bibi Fatmah alipokuwa akilia Mtume [s] naye hulia na kusema: "Sintapata msiba kama wako kamwe".[271]

Na pindi Mjumbe wa Mwenyezi Mungu aliporudi toka Uhdi, wanawake wa Kiansari waliwalilia mashahidi wao, basi sauti zao zikamfikia Mtume [s] akasema:

"Lakini Hamza hana wakumlilia" Basi Maansari wakarudi na wakawaambia wanawake wao "Msimlilie yeyote mpaka muanze kumlilia Hamza", basi desturi hiyo kwa Maansari imebakia mpaka leo hawamlili mtu ila kwanza humlilia Hamza.[272]

Na huyu (tena) ni Mtume [s] anawapa watu wa Madina habari ya shahada ya Jaafar na Zaid bin Harith na Abdallah bin Ruwah na hali macho yake yanatiririka machozi.[273]

Na hapa Mtume [s] alilizuru kaburi la mama yake na akalia na akawaliza waliokuwa pamoja naye.

Pia Mtume [s] anambusu Uthman bin Madh-un akiwa ni maiti na machozi yake (Mtume) yanatiririka usoni.[274]

Vile vile Mtume [s] anamlilia mtoto wa mmoja wa mabinti zake na Ubbadah Ibn Samit akamwambia "Nini hiki Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?"

Mtume Akasema:

"Ni huruma aliyoiweke Mwenyezi Mungu ndani ya wanaadamu, na kwa hakika Mwenyezi Mungu anawahurumia wenye huruma miongoni mwa waja wake".[275]

Naye Bibi mkweli aliyetakasika, (Fatmah binti Muhammad [s] anamlilia baba yake na anasema:

"Ewe baba yangu uko karibu mno na Mola wako, Ewe baba yangu umemwitika Mola aliyekuita, Ewe baba yangu tunakuomboleza kwa Jibril, Ewe baba yangu makazi yako ni pepo ya Firdaus".[276]

Na vile vile Bibi Fatmah [a] alisimama kwenye kaburi tukufu Ia Baba yake na akachukua gao la udongo wa kaburi akauweka (karibu na macho) na akalia na kusoma shairi akasema:

"Ana lawama gain mtu atakayenusa udongo wa kaburi la Ahmad [s] iwapo hatanusa ghaliya[277] milele. Nimefikwa na msiba ambayo lau ungeufika mchana ungegeuka na kuwa usiku.

Na huyu hapa Abu Bakr Ibn Abi Qahafah anamlilia mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] na kumuomboleza kwa kusema:

"Ewe Jicho lia usichoke, ni haki kumlilia Bwana".

Na amesema tena:

"Wanamlilia yule ambaye mbingu inamlilia na ni yule ambaye ardhi imemlilia na watu wamehuzunika mno".

Na anasema: "Ewe Jicho lia kwa machozi mengi yanayotiririka, na usichoke kutoa machozi kila wakati na kulia".

Naye Ar-wi binti Abdul-Muttalib anamlilia Mtume [s] na kumuomboleza kwa kusema:

"Fahamu Ewe Jicho! Ole wako nipoze kwa machozi yako muda wote nitaobakia, na unipe ushujaa. Fahamu Ewe jicho, Ole wako jitokeze kwenye nuru ya miji na unipoze."

Na Atikah binti Abdul-Muttalib anamuomboleza Mtume [s] na anasema:

"Enyi macho yangu! lieni sana siku zote na mutoe machozi, mtiririshe machozi bila udhuru.

Ewe Jicho lia kwa machozi yasiyokatika. Ewe Jicho lia kwa machozi sana kwa ajili ya Mtume mwenye nuru aliyechaguliwa kuliko viumbe wengine wa Mwenyezi Mungu".

Naye Safiyah binti Abdul-Muttalib, anamlilia Mtume na kumuomboleza kwa kusema:

"Ewe Fatma lia pamoja na wenzako wala usichoke mpaka nyota zichomoze, Mtume ni mwenye kuliliwa na anastahiki kuliliwa, Yeye ndiye Mtukufu na Bwana aliye mzuri". Na pia anasema: "Enyi macho yangu lieni kwa machozi mfululizo. Enyi macho yangu lieni na mtiririshe machozi kwa huzuni nyingi".

Na huyu hapa Hind bint Al-Harith Ibn Abdil-Muttalib anamlilia Mtume na anasema:

"Ewe Jicho lia kwa machozi na uyatirirshe kama yanavyoshuka maji ya mvua yakatiririka".

Na Hind binti Athatha anamuomboleza Mtume anasema:

"Ewe Jicho lia usichoke kwa hakika nimepata khabari ya mauti ya yule umpendaye (Mtume [s])".

Na huyu hapa Atika binti Zaid anamuomboleza Mtume na anasema:

"Na sasa vipando vyake vinatingisha moyo na kwa hakika alikuwa akivipanda yule ambaye ni pambo lake. Na vipando hivyo vimekuwa vinamlilia Bwana wake na macho yake yanatiririsha machozi".

Naye Ummu Ayman anamuomboleza Mtume kwa kusema:

"Ewe Jicho langu lia kwa sababu huzuni yangu itakuwa Shifaa, basi lia sana kwa machozi mengi mpaka ifike hukumu ya Mwenyezi Mungu ya kheri".

Na huyu hapa Shangazi ya Jabir bin Abdallah alikuja siku ya Uhdi akimlilia nduguye Abdallah Ibn Amr, na Jabir amesema:

"Nikawa nalia na watu wakawa wananikataza na mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] hanikatazi, basi mjumbe wa Mwenyezi Mungu akasema: "Lieni kwa ajili yake hata musipolia, Wallah Malaika hawakuacha kumfunika kwa mbawa zao mpaka mumemzika."[278]

Naam, imepokewa toka kwa Umar lbn Khattab na Abdallah Ibn Umar kwamba Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] amesema:

"Hakika mauti huadhibiwa kwa kilio cha watu wake".

Mimi nasema: Dhahiri ya hadithi hii iko kinyume na matendo ya Khalifa (mwenyewe) aliyotenda mahala pengi palipothibitishwa na historia.

Miongoni mwake ni kwamba, yeye alimlilia Nuuman Ibn Muqrin Al-Muzani pindi ilipomfikia habari ya kifo chake, basi akatoka akawajulisha watu akiwa juu ya mimbar na akaweka mkono wake juu ya kichwa chake akalia.[279]

Na miongoni mwake ni kulia kwake yeye na Abu Bakr wakimlilia Saad Ibn Muan mpaka Aisha akasema:

"Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake hakika mimi nilikuwa na tambua sauti ya kilio cha Abu Bakr na sauti ya kilio cha Umar, wakati mimi nikiwa chumbani mwangu."[280]

Na miongoni mwake ni kilio chake juu ya nduguye Zayd Ibn Khattab, na huyu (Zayd) alifuatana na mtu fulani katika Bani Adiy Ibn Kaab, basi yule mtu akarudi Madina na alipomuona macho yake yakatiririka machozi akasema: "Wewe umemuacha Zayd hali ya kuwa ni maiti nawe umekuja kwangu".[281]

Basi kulia kwa Khalifa ambako kumekaririka kunatuongoza kwamba, makusudio ya hadithi hata kama Sanadi yake itasihi yana maana nyingine, itakuwaje (hali hii)? Na dhahiri ya hadithi lau tutaiamini inakwenda kinyume cha Qur'an, na hapa nakusudia kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo, "Wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine".

Qur'an, 35:18.

Basi kuna maana gani ya kumuadhibu maiti kutokana na watu wengine kumlilia!!

Shafii amesema: Na hadithi aliyoipokea Aisha toka kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] (Itatajwa baadaye) inaaminika kwamba ni hadithi iliyosemwa na Mtume [s] (Kuliko hadithi zilizotajwa na Umar na Abdallah) na dalili yetu ni Qur'an na Sunnah. Na iwapo itasemwa iko wapi dalili ya Qur'an, patasemwa, ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo "Wala Hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine" na ile isemayo: "Na kwamba hatapata mtu isipokuwa yale aliyoyafanya"

Qur'an, 53:39.

Na kauli yake isemayo: "Basi anayefanya wema (hata) wa kiasi cha mdudu chungu atauona na anayefanya uovu (hata) wa kiasi cha mdudu chungu atauona".

Qur'an, 99: 7-8

Na kauli yake isemayo: "Ili kila nafsi ilipwe kwa yale iliyoyafanya"

Qur'an, 20:15.

Na iwapo itasemwa iko wapi dalili ya Sunnah? Patasemwa, "Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alimwambia mtu fulani "Huyu ni mwanao"? Akasema "Ndiyo" "Hakika yeye hatafanya makosa kwa ajili yako, wala hutafanya makosa kwa ajili yake". Basi Mtume akamjulisha kama alivyomjulisha Mwenyezi Mungu kwamba kila kosa Ia mtu ni lake mwenyewe kama ambavyo amali yake siyo ya mwingine wala dhidi yake.[282]

Ufahamisho wa hadithi: Yote tuliyonakili yanatujulisha kwamba makusudio ya hadithi inayosema kwamba, "Hakika maiti anaadhibiwa kwa kumlilia walio hai" (Kama Sanadi yake itasihi) sicho kinachofahamika kutokana na dhahir yake, na hadithi ilikuwa na qarina kujulisha maana yake lakini zilianguka wakati wa kunakili.

Na kwa ajili hiyo baadhi ya watu wamedhania kuwa ni haramu kumlilia maiti kwa kutegemea hadithi hii hali ya kuwa wameghafilika na lengo Ia hadithi na maana yake.

Amepokea Umrah, kwamba yeye alimsikia Aisha R.A. wakati alipoambiwa kwamba Abdallah Ibn Umar anasema: Maiti huadhibiwa kwa ajili ya kilio cha walio hai, basi Aisha R.A. akasema:

"Amma yeye hajasema uongo (kwa makusudi) lakini amekosea au amesahau, hakika mjumbe wa Mwenyezi Mungu alipita kwenye mazishi ya Myahudi ambaye jamaa zake walikuwa wanamlilia akasema: "Hakika wao wanamlilia naye anaadhibiwa kaburini mwake."[283]

Na imepokewa toka kwa Ur-wa naye toka kwa Abdallah bin Umar amesema: "Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] hakika maiti huadhibiwa kwa ajili ya kilio cha watu wake juu yake basi Ur-wa akamtajia Aisha hadithi hii akasema hali akimkusudia Ibn Umari:

"Kwa hakika Mtume [s] alipita kwenye kaburi la Myahudi akasema, hakika mwenye kaburi hili anaadhibiwa na hali ya kuwa watu wake wanamlilia kisha akasoma, "Na wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine".[284]

Huu ndiyo ufahamisho wa hadithi na maana yake na hawezi kutia shaka katika kusihi maana hii mtu mwenye utambuzi na maarifa ya Qur'an na hadithi.

Na kuna Riwaya nyingine zinazojulisha kwamba Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] alimkemea Umar kutokana na kuwakataza kwake wanawake waliokuwa wakiwalilia maiti.

Imepokewa toka kwa Ibn Abbas amesema:

"Alipofariki Zainab binti ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] Mtume [s] alisema, mfuatishieni kwa Salaf wetu mwema (aliyetangulia) Uthman Ibn Madh-un, basi wanawake wakalia, Umar akawa anawapiga kwa fimbo yake, mjumbe wa Mwenyezi Mungu akaushika mkono wake akasema, tulia Ewe Umar, waache walie na Ole wenu! na maombolezo ya shetani". Hadi akasema. Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikaa ukingoni mwa kaburi na Fatmah akiwa pembeni mwake analia, basi Mtume [s] akawa anayapangusa macho ya Fatmah kwa nguo yake kwa kumuonea huruma".[285]

Na Al-Bayhaqi ameandika ndani ya Sunan Al-Kubra hadithi kama hiyo kuhusu kufariki kwa Ruqaiyyah binti ya mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Na mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] alisema:

"Wacha Ewe Umar" Kisha akasema: "Ole wenu! na maomboleza ya shetani, kwani chochote kiwacho kutoka jichoni na moyoni ni miongoni mwa huruma na kiwacho kutoka ulimini na mkononi kinatokana na shetani".[286]

Na katika Riwaya nyingine:

Mjumbe wa Mwenyezi Mungu akasema: "Ewe Umar waache kwani jicho linalia na moyo unapata huzuni na ni hivi punde tu msiba umetufika".[287]

Hiki ndicho tulichokinakili kutoka katika riwaya nyingi, kitamjulisha msomaji Mtukufu hukmu ya Kiislamu katika Mas-ala ya kumlilia maiti sawa sawa maiti akiwa ni jamaa na ni kipenzi au akawa ni rafiki mpenzi, basi iwapo itajuzu kuwalilia hao basi kumlilia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] na watu wa nyumba yake waliotakasika na Masahaba wake wema ni awla kujuzu.

Kwa nini isiwe na hali yakuwa riwaya nyingi zimekuja kuhusu jambo hili kutoka kwa makundi mawili Shia na Sunni zinazohusu kumlilia Mtume [s] na misiba ya watu wa nyumba yake, hatukulenga kuzitaja kwa, kufupisha maelezo na atakae kufahamu arejee kitabu kiitwacho, "Siratuna Wa Sunnatuna Siratun-Nabiyyi Wa Sunnatuh" cha mwanachuoni mkubwa Sheikh Abdul-Husain Al-Amini R.A. Japokuwa tuliyoyataja katika kurasa hizi yanaambatana na yale aliyoyahakiki mwanachoni huyo katika mlango huu (Mwenyezi Mungu amrehemu).

Pili: Kudhifia tamko la "Abdi" (lenye maana ya mja au mtumwa) kwa kiumbe:

Kwa hakika imekuwa ni jambo mashuhuri kwa wapenzi wa Ahlul Bayt [a] kuwaita watoto wao (majina ya) "Abdur-Rasul" na "Abduali" na "Abdul-Husein".... na mfano kama huo, yaani kudhifia neno "Abdi" kwenye majina ya (Ahlul-Bayt) [a].

Na kuita majina (kwa namna hii) kumezusha wasi wasi ndani ya baadhi ya makundi na hasa Mawahabi, hali yakuwa wanadai kwamba kuita jina (namna) hii ni aina ya shirki na wala hakuafikiani na misingi ya Tauhidi. Na kuna kikao huko Syria kilichotukutanisha mimi na Sheikh Nasirudin Al-Abani ambaye ni msahihishaji na ni mhakiki na baadhi ya vitabu vya hadithi, basi niliiona kwake chuki kubwa kutamkwa jina la Abdul-Husein, na hali hiyo (Ilitokea) pale yalipokuja mazungumzo kumhusu Al-Allamah AI-Hujjah As-Sayyid Abdul-Husein Sharafud-din Al-Amili ambaye ndiye mwandishi wa Al-Murajaat (Mwenyezi Mungu aitakase roho yake).

Na kwa ajili ya kuondoa utata mbele ya ukweli, sisi tunasimama kutatua Mas-ala haya kwa mtazamo wa Qur'an na Sunna, na tunasema: "Ubudiyyah, hutumika na kukusudiwa kutokana nayo (maana zifuatazo):

Kwanza: Maana inayokabili uungu, nalo kwa maana hii linajulisha kwamba mtu huyo au watu wote ni milki ya Mwenyezi Mungu katika asili ya kuumbwa, na mwenye kumiliki ni yeye Mwenyezi Mungu, nawe unafahamu kwamba mtu ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu na ndiye Bwana wake, na chanzo cha mambo haya mawili ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyemuumba baada ya kuwa hakuwepo naye ndiye mwenye kumpa kila kitu kinachomuhusu.

Kwa hiyo basi Ubudiyyah kwa maana hii ni asili ya kila kilichopo, na ni asili ya kila kitu na kamwe hakiepukani na maana hiyo inayokusudiwa na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukafu isemayo:

"Hapana yeyote aliyeko mbinguni na ardhini ispokuwa atafika kwa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehma hali ya kuwa ni mtumwa "Abdi".

Quran, 19:93.

Kama ambavyo kauli ya masihi (Isa bin Mariyam) [a] inavyoashiria akasema:

"Hakika mimi ni Abdullahi (Mtumwa wa Mwenyezi Mungu) amenipa kitabu na amenifanya kuwa ni Nabii".

Qur'an, 19:30. Na aya nyinginezo.

Na Idhafa ya Abdi kwa maana hii haiwezekani ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

Pili: Ubudiyyah hutumika na kukusudiwa kutokana nayo utiifu au maana inayokaribiana na hiyo, na kwa hakika wameifafanua maana hii waandishi wa kamusi za lugha.

Amesema ndani ya "Lisanul-Arabi": At-Taabudu (Maana yake ni) At-Tanasuku (kufanya ibada.), Al-Ibada (maana yake) "At-Taa" (utufii).

Na amesema ndani ya "Al- Qamusul-Muhit":

"Wal-Abdiyah, Wal-Ubudiyyah, Wal-Ubudah, Wal Ibadah, (Maana yake ni) At-Taa (yaani utiifu)".

Na kwa msingi huu basi, makusudio ya "Abdur-Rasuli, Abdu Ali na.... "Ni Mwenye kumtii Mtume na mwenye kumtii Ali. Na "Makusudio haya" yako wazi, basi kwa nini isiwe hivyo na Mwenyezi Mungu ametuamuru kuwatii wao akasema: "Mtiini Mwenyezi Mungu na mumtii Mtume na wenye mamlaka miongoni mwenu".

Qur'an, 4:59.

Basi Qur'an imetambulisha kuwa Mtume ni mwenye kutiiwa na Waislamu ni wenye kutii, na halaumiwi mtu kuidhihirisha maana hii kwa kuwaita wanawe na awapendao (kwa majina hayo).

Naam, ndani ya hadithi ya Abu Hurairah (imesemwa) "Asiseme mmoja wenu kumwambia aliyemmiliki "Abdii" Wa "Amatti" Yaani mtumwa wangu na mjakazi wangu, na aseme kijana wangu" (Lakini) Ibnul Athir ndani ya kitabu chake kiitwacho, "An Nihayah" ameitolea dosari hadithi hii kwa kauli yake aliposema:

"Hadithi hii ni kwa maana ya kupinga kuwafanyia ujeuri juu yao na kuwanasibishia utumwa kwa maana ile ya kwanza. Kwani mwenye kustahiki hilo ni Mwenyezi Mungu Mtukufu naye ndiyo mlezi wa waja wote".[288]

Na hadithi hii kwa dhahiri yake inakwenda kinyume na Qur'an Tukufu, vipi itakuwa wakati yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliyewanasibishia "Ubudiyyah" kwa watu wanaowamiliki.

Akasema Mwenyezi Mungu: "Waozeni wajane miongoni mwenu na waliowema katika watumwa wenu (Ibadikum) na wajakazi wenu (Imaikum) na wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha katika fadhila zake na Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa mwenye kujua".

Qur'an, 24:32

Utaona kwamba Mwenyezi Mungu anaunasibisha Ubudiyah (utumwa) na Imaiyah (Ujakazi) kwa wale wanaowamiliki, na lau ndani ya Taabiri (Hii) kungekuwa na kitu fulani (kinachoonyesha) kiburi kwa mtumwa, basi Mwenyezi Mungu asingelitumia Taabiri hii.

Kisha ni kwamba msingi wa Shubha hii ni kuwa, wenye kuwa na mushkeli (wa jambo hili) hawatofautishi baina Ubudiyyah Tak-winiyyah Al-haqiqiyyah ambayo haiepukani na mtu tangu mwanzo wa kupatikana kwake mpaka kwenye siku zake za mwisho, na baina ya milki yenye kajitokeza (isiyokuwa ya asili) kwa mtu kufuatia hali na masharti (yanayohusika) basi hapo bwana huwa mtumwa na mtumwa huwa bwana na hakimu. Hii ndiyo Fiqh ya Kiislamu inayojulisha kuwafanya mateka wa vita wanaume na wanawake kuwa watumwa. Amesema Ibn Quddamah ndani ya Kitabu chake kiitwacho, "Al-Mugni": "Pindi Imam anapowateka mateka, basi anahiyarishwa, akiona kuwa (inafaa) kuwaua (atawaua), na akiona awasamehe bila ya badali (ya kiti chochote atawasamehe), na akiona atawaachia kwa (badali ya) mali atakayoichukua toka kwao (atawaachia) na akiona (inafaa) atakubali fidia. Na akiona kuwa inafaa kuwafanya watumwa ni bora, (basi atafanya analoona kuwa linafaa kati ya hayo)".

Kwa hiyo ndani ya vitabu vya Fiqhi kuna mlango mpana unaohusu hukmu za watumwa na wajakazi, hivyo wanazo hukmu maalum anazifahamu yule aliye mtaalamu wa Fiqhi ya Kiislamu. Basi hulitumia tamko Ia "Maula" kwa yule Bwana anayewamiliki watumwa kwa kuwateka (vitani) au kwa kuwanunua, kama ambavyo hulitumia tamko la "Abdi" na "Amah" (mtumwa na mjakazi) juu ya mateka ambao hakimu ameona kuwa inafaa kuwafanya mateka, na hapana mwanachuoni yeyote miongoni mwa Mafaqihi aliyeona ubaya wa kutumia jina hili mtumwa au mjakazi.

Na miongoni mwa mambo yanayostaajabisha ni kauli ya Muhammad Abdul-Wahabi isemayo kuwa: "Yeyote mwenye kumwambia mtu fulani, Maulana au Sayyidina basi mtu huyo ni kafiri".[289] Wakati ambapo Qur'an Tukufu inalitumia tamko la Sayyid kwa mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Mwenyezi Mungu amesema: "....Mwenye kusadikisha kwa neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu na atakayaekuwa "Sayyid" (Bwana) na mtawa".

Qur'an, 3:39.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na akairarua kanzu yake kwa nyuma na akawakuta Sayyid wake mlangoni".

Qur'an, 12:25.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na watasema Mola wetu hakika tuliwatii Masayyid wetu na wakubwa zetu basi wao wametupoteza njia".

Qur'an, 33:67.

Zaidi ya hayo kuna riwaya nyingi Mutawatiri (zimekuja) katika matumizi ya "Sayyid" kwa Mtume na kwa Hasan na Husein[290] [a] kiasi kwamba hapana yeyote mwenye kutia shaka katika kusihi kwake. Na kwa hakika Abubakr alimuomboleza Mtume Mtukufu kwa beti ambazo mwanzoni mwake (alisema:).

"Ewe Jicho lia wala usichoke na haki ya kumlilia iko juu ya Sayyid, Mlilieni yule ambaye alikuwa mlinzi wetu kwenye mabalaa, na sasa amezikwa kaburini".

Naam, Suyuti ameleta (masimulizi) ndani ya Al-Jamius-Saghir toka kwa Daylami ndani ya Musnad ya Al-Fir-Dausi toka kwa Ali [a] kwamba: "As-Sayyid ni Mwenyezi Mungu".

Kama alivyoleta (masimulizi) AI-Azizi ndani ya Sharhul-Jamii As-Saghir kutoka Musnad ya Abi Dawood kwamba, ulikuja ujumbe wa Bani Amir kwa Mtume [s] wakasema: "Wewe ni Sayyid wetu", Mtume akasema, "Sayyid ni Mwenyezi Mungu".

Basi lau hadithi hizi mbili zitasihi itabidi zichukuliwe kwenye maana ya hakika ya "As-Sayyid" yaani "Mwenye kumiliki na muumba" kwani As-Sayyid kwa maana hii inamuhusu Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa nini isisihi wakati Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alilitumia neno Sayyid kwa Saad Ibn Maadh R.A. Tabari amesimulia kama ifuatavyo: "Alipotokea Saad, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] alisema: "Simameni kwa ajili ya Sayyid Yenu"[291]

Makatazo haya yaliyokuja hapa kuhusu neno Sayyid yatachukuliwa kwa makusudio ya maana inayokanusha Tauhidi ya Mwenyezi Mungu pindi ikitumika kwa maana ya mwenye kumiliki na kuamba.

Naapa kwamba, ukweli uko wazi hauhitaji maelezo marefu, itakuwaje hali hii wakati ambapo maneno ya Waarabu na Mtume na Masahaba na Tabiina na Maimamu wa nyumba ya Mtume na Mafaqihi wa umma, yamejaa kwa matumizi ya maneno haya kuhusu asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na hapana yeyote aliyeona ubaya wa kayatumia kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na waliyachunguza mas-ala haya kwa upana na mtazamo wa undani na hawakuwatia Waislamu katika dhiki na shida na walifahamu kwamba sheria ya Kiislamu ni nyepesi inafuata makusudio na malengo siyo dhahiri (yake) na matamko (yalivyo).

Basi Mawahabi ni kama Makhawariji, waliyadhiki mambo juu ya nafsi zao na juu ya Waislamu kwa vitu ambavyo Mwenyezi Mungu hakuviwekea vikwazo na makundi mawili haya yanaafikiana katika Mas-ala mengi bega kwa bega.

Khitamuhu Misk:

Ewe msomaji mpendwa, sasa hivi umefika wakati wakuhitimisha uchambuzi huu mpana kuhusu itikadi za Kiwahabi na misingi yake na malengo yake kwa neno fupi lenye manufaa kwa jamii ya Kiislamu kwa jumla, na kwa vijana wa Kiislamu wenye ghera kwa upande wao.

Bila shaka Uislamu umejengwa juu ya maneno mawili:

Kalimatul-Tauhid
na Tauhid-ul-Kalimah, basi ni wajibu juu ya umma wa Kiislamu kuulinda umoja wa kalima na mshikamano wa udugu, kama ambavyo ni wajibu juu ya umma kuihifadhi Kalimatul-Tauhid kwani viwili hivyo ni matawi mawili yanayotokana na asili moja.

Basi kama ambavyo Qur'an na Sunna vimehimiza juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu kwa dhati na kwa vitendo na ibada, basi ndivyo hivyo hivyo vimehimiza kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu na vimekemea mafarakano: "Shikamaneno katika kamba ya Mwenyezi Mungu na wala musifarakane". Qur'an, 3:84.

Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na atakayemuasi Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu na akafuata njia ya wasiokuwa waumini, tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza

ndani ya Jahannam na hayo ni marejeo mabaya".

Qur'an, 4:115.

Na amesema Imam Ali [a] "Basi shikamaneni na Jamaa kubwa kwani mkono (msaada) wa Mwenyezi Mungu uko pamoja na wengi, na Ole wenu na mafarakano kwani hakika wenye kukhalifa miongoni mwa watu ni (kundi la) shetani kama ambavyo wenye kujitenga miongoni mwa kondoo ni kwa ajili ya mbwa mwitu, basi fahamuni ya kwamba mwenye kulingania kwenye utengano huu muueni japokuwa atakuwa chini ya kilemba changu hiki."[292]

Basi iwapo Tauhidul-Kalimah iko katika daraja hii ya juu, basi itakuwaje hali ya mtu anayevunja mshikamano wa Waislamu na kueneza ndani yao utengano na kubomoa umoja wao na kuyavuruga maafikiano yao kwa kupandikiza mbegu ya mashaka ndani ya mambo ambayo umma wa Kiislamu ulikuwa ukiafikiana kabla (hata) ya kuzaliwa (huyu) aliyepandikiza mashaka yaani Ibn Taymiyyah na aliyeimwagilia mbegu hiyo yaani Ibn Abdul-Wahab.

Ewe msomaji mpendwa: Kwa hakika yote tuliyokueleza ndani ya kurasa hizi ni kwa mujibu wa Qur'an Tukufu na Sunna ya Mtume Mtukufu [s] na ni matokeo ya kile ambacho umma wa Kiislamu umekubaliana kwa karne zote. Basi lina thamani gani neno au maneno yanayopinga kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake [s] na kile ambacho umma umekubaliana?

Ni jambo zito kwa umma wa Kiislamu ukiongozwa na Wanachuoni wake na wanafikia wake kupatikana ndani ya Makka na mahala paliposhuka wahyi watu wanaoukufurisha umma wote wa Kisunni na Kishia na wala hawamvui miongoni mwao isipokuwa watu wachache toka miji ya Najd.

Na kwa hakika wakubwa watukufu wa umma wa Kiislamu walikwishahadharisha hatari ya msimamo huo na madhara ya fikra za kishetani ambazo alizipandikiza Sheikh Ibn Taymiyyah mpaka Al-Hafidh Ibn Hajar amesema ndani ya kitabu chake kiitwacho, "Al-Fatawa AI-Hadithiyyah" kumuhusu Ibn Taymiyyah kama ifuatavyo:

"Ibn Taimiyya ni mja ambaye Mwenyezi Mungu amemdhalilisha, na amemuacha apotee naakampofua na kumfanya kiziwi, na wameyabainisha mambo haya yakawa wazi Maimamu ambao walieleza ufisadi wa hali yake na uongo wa kauli zake, na mwenye kutaka (kujua) ni juu yake kutalii (kusoma) maneno ya Imam Al-Muj-Tahid Abul-Hasan As-Subaki ambaye Uimamu wake na utukufu wake na kufikia kwake daraja ya Ij-Tihadi kumekubaliwa na wote na pia asome maneno ya) mwanawe (aliyekuwa akiitwa) At-Taaj na Sheikh Al-Imam Al-Izz miongoni mwa jamaa na watu wa zama zao miongoni mwa Mashafii na Malik na Mahanafii, na huyu Ibn Taymiyyah hakuishia kuwapinga Masufi wa zama zake bali amewataaradhi watu kama vile Umar Ibn Khataab na Ali Ibn Abi Talib R.A. Kilichopo ni kwamba maneno yake hayana maana na ni yakutupwa njiani. Na inaitakidiwa kwamba yeye ni mzushi mpotovu mwenye kupotosha amevuka mpaka, Mwenyezi Mungu amlipe kwa mujibu wa uadilifu wake".[293]

Na tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie "Miongoni mwa wenye kusikiliza maneno na wakafuata mema yake".

Rehma na Amani Zimshukie Bwana wetu Muhammad Mwisho wa Mitume na Aali Zake wema waliotakasika na Sahaba Zake Wema Watukufu.

Na Maombi yetu ya mwisho ni kuwa kila sifa njema zinamstahaki Mwenyezi Mungu Mola wa Walimwengu.

Jaafar Sub-Hani,
Qum Takatifu,
Siku ya Idi ya Ghadir,
18 Mfunguo Tatu 1406.

[234] Jarida la Rabitat al-Alami al-Islami la mwaka wa kumi na moja toleo la kumi na mbili.

[235] Al-Manar, Juz. 2, uk. 228.

[236] Tafsiri Al- Qurtubi, Juz. 2, uk. 406.

[237] (1) Tafsiri aI-Kashaaf ya Zama Ukhshari, Juz. 1, uk. 264. (2) Tafsiri Qur-Tubi, Juz. 2, uk. 406.

[238] Mafatihul-Ghaib, Juz. 2, uk. 175, Naye pia amenakili kwa Qadhi al-Baidhawi.

[239] Tafsir at-Tabari, Juz. 2, uk. 162.

[240] Tafsir al-Kash-Shaaf, Juz. 1, uk. 264

[241] Tafsir Qurtubi Juz. 2, uk. 410.

[242] Tafsir Ibn Jariri Juz. 2, uk. 161

[243] Al-Kashaafa Juz. 1, uk. 263.

[244] AI-Manaar, Juz. 2, uk. 227-228.

[245] Ah-kamul-Qur'an ya Al-Jasas, Juz. 1, uk. 308.

[246] Tafsir ya Imam Fakhrur-Razi, Juz. 1, uk. 175.

[247] Al-Fiq-Hu Alal-Madhahibil-Ar-Baa, Juz. 1, uk. 524.

[248] Nurut-Thaqalain, Juz. 1, uk. 162, pia tazama vitabu vya hadithi k.m. Al-Wasail n.k.

[249] Madinatul-Balagha Fi Khutabin-Nabi Wa Kutubihi Wamawaidhihi, Juz. 1, uk. 469.

[250] Tafsir Tabari, Juz. 17, uk. 108.

[251] Tafsir Tabari, Juz. 7, uk. 49.

[252] Tafsir Tabari, Juz. 17, uk. 108

[253] Tafsir Tabari, Juz. 7, uk. 49.

[254] Tafsir-ul-Manar cha Sayyid Rashid Rida, Juz. 7, uk 119.

[255] Tafsir Tabari, Juz. 10, uk. 47.

[256] Al-Alhani, Juz. 21, uk. 376, Chapa ya Beirut, na Manaqib ya Ibn Shah-Rashud, Juz. 4, uk. 169, na Qadhiya hii imenakiliwa katika vitabu vingi vya Tarikh na vya Adab, kwa mfano, "Al-Bayan Wat-Tabyin, na Al-Iqdu al-Farid na Matalibus-Suul na Tadh-Kiratul-Khawas, na Nurul-Absar.

[257] Bukhar: Jihad.

[258] Sunan lbn Majah: Al-Manasik na Sunan An-Nasai: Al-Haj na Jihad

[259] Khutba hizi mbili tulizozichanganya hapa zimekuja ndani ya Sahihi Muslim katika hadithi inayozungumzia Hija ya Mtume na pia zimekuja ndani ya Sunan ya Abu Dawood na Sira ya Ibn Hisham na vitabu vinginevyo.

[260] Bukhar: Umrah, na Muslim: Al-Hajj, na Dawuud: Al-Manasik, na At-Tirmidhi Al-Hajj na Ibn Majah: Al-Manasiki, na Al-Muwattaa cha Malik: Al-Hajj, na Musnad Ahmad.

[261] Tarikh Makkah, Juz. 1, uk. 339 chapa ya Makkatul-Mukarramah ya mwaka 1385 A.H.

[262] Biharul An-War, Juz. 99, uk. 33 imenakiliwa toka Ilalis-Sharaii ya Saduq.

[263] Biharul-An-War, Juz. 99, uk. 49.

[264] Al-Ihtijaj cha Attabrasi, uk. 19 na kitabu cha Sulaim Ibn Qays uk. 183.

[265] AI-Ibadah Fil-Islam cha Dr. Qar-Dhawi.

[266] Rejea tuliyoitaja hapo nyuma, na vile vile kitabu kiitwacho, "Madha khasira Al-Alam Al-Islami cha Abul-Aala Al-Maududi akinakili kutoka Tarikh ya Ibn Al-Jauzi.

[267] Dairatul-Marif, Juz. 3, uk. 350.

[268] Abu Dawood, Juz. 3, uk. 58, Sunan Ibn Majah, Juz 1, uk. 482

[269] Siratul-Halabiya, Juz. 3, uk. 348.

[270] Maj-Mauz-Zawaid ya Al-Haithami, Juz. 3, uk. 8.

[271] Imtau ya Al-Maqrizi, uk. 154.

[272] Majmauz-Zawaid, Juz. 6, uk. 120.

[273] Sahih Bukhar, Kitabul-Manaqib Fii Alaamatin-Nubuwwah Al- Islam. (2) Sunan Al-Bayhqi, Juz. 4, uk. 70.

[274] Sunan Abi Dawood, Juz. 2, uk. 63, Suna Ibn Majah, Juz. 1, uk. 445.

[275] Sunan Abi Dawood, Juz. 2, uk. 58, Sunan Ibn Majah, Juz. 1, uk. 481.

[276] Sahih Bukhar, Babu Maradhin-Nabi Wawafatih Musnad Abi Dawood, Juz. 2, uk. 197. "Sunan An-Nasai, Juz. 4, uk. 13, Mustadrak Al-Hakim, Juz. 3, uk. 163, Tarikh AI-Khatib, Juz. 6, uk. 262.

[277] Al-Ghadir, Juz. 5, uk. 147.

[278] Al-Istiab: Tarjuma ya Abdallah, Juz. 1, uk. 368, Al-Ghadir, Juz. 3, uk. 165-167.

[279] AI-Istiab katika Tarjuma ya Nuuman, Juz. 1, uk. 297, Al-Iqd Al-Farid cha Ibn Abdi Rabih Al- Undulus, Juz. 3, uk. 235.

[280] Tarikh Tabari, Juz. 2, Uk. 253.

[281] Iq-dul-Far, Juz. 3, uk. 235.

[282] Ikhtilaful-Hadithi katika Hashiya ya kitabu Al-ummu cha Shafii, Juz. 7, uk. 267.

[283] Sahih Bukhar mlango wa 32 katika milango ya Jeneza, Juz. 2, uk. 80, Ikhtilaful-Hadith cha Shafii, Juz. 7, uk. 266, Al-Muwatta cha Malik, Juz. 1, uk. 96, Sahih Muslim Juz. 1, uk. 344, Sunan Nasai, Juz. 4, uk. 17, Sunan Bayhaqi, Juz. 4, uk. 72.

[284] Sunan Abi Dawood, Juz. 2, uk. 59, Sunan Nasai, Juz. 2, uk. 17.

[285] Musnad Ahmad, Juz. 1, uk. 235-237. Mustadrak ya Al-Hakim, Juz. 1, uk. 191. Na amesema Adhahabi ndani ya Tal-Khisul-Mustadrak: Sanad yake ni nzuri.

[286] As-Sunan Al-Kubra, Juz. 4, uk. 70.

[287] Umdatul-Qarii, Juz. 4, uk. 87.

[288] An-Nihayah cha Ibnul-Athir, Juz. 3, uk. 170.

[289] Kashful-Irtiyabi cha Sayyid Muhsin al-Amin: Amenakili toka katika Khul-Satul-Kalam.

[290] Kinachokusudiwa ni ile hadithi isemayo Hasan na Husain ni Masayyid wa vijana wa peponi.

[291] Tabari, Juz. 2, uk. 249.

[292] Nahjul-Balagha Khutba Na. 123.

[293] Al-Fatawa Al-Hadithiyyah, uk. 86.