KUWAOMBA MSAADA MAWALII WA MWENYEZI MUNGU

Je, inafaa kuwaita Mawalii wa Mwenyezi Mungu kuwaomba msaada wakati wa shida na matatizo?

Mas-ala haya ni miongoni mwa Mas-ala ambayo kuna tofauti ndani yake baina ya Waislamu na Mawahabi.

Kuwaomba msaada Manabii na Mawalii wa Mwenyezi Mungu, na pia kuwaita kwa majina yao wakati wa shida, matatizo na mambo ya hatari ni sunna iliyojengeka miongoni mwa Waislamu.

Basi, ni sawa sawa kuwaomba msaada huo kwenye makaburi yao matukufu au sehemu nyingine yoyote ile na wala hawaoni ubaya wowote katika kuomba msaada wa aina hii wala siyo shirki na wala si kinyume cha dini.

Wakati Mawahabi wanalipinga jambo hili kwa bidii zote, Waislamu hawaoni ubaya wa kulitenda wala siyo shirki ndani ya uombaji huu wala siyo kinyume cha dini.

Mawahabi hawa kila wafanyapo upinzani wao dhidi ya mas-ala haya wanatumia baadhi ya aya za Qur'an ambazo kamwe hazina uhusiano wowote na mas-ala haya, isipokuwa lengo lao ni kuuchanganya uovu wao huo na haki.

Aya wazitumiazo ni kama hii ifuatayo:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na kwa hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 72:18.

Ewe msomaji mpendwa, ili uweze kuzifahamu aya za Qur'an ambazo Mawahabi wanazitolea ushahidi kutilia nguvu maoni yao ya kipekee, tunazileta hapa aya hizo kwa ajili ya kufanya utafiti na uchunguzi ili uweze kufahamu tafsiri yake sahihi "Insha-Allah".

Na kwa hiyo basi sisi tunawajibu kwa Qur'an hii hii ambayo wao wanadai kuwa ndiyo wanayoitolea ushahidi kabla ya kitu kingine chochote.

Baadhi ya aya hizo tunazitaja kama ifuatavyo:

"Kwake ndiko yaliko (maitikio ya) maombi ya haki, na wale wawaombao asiyekuwa yeye hawatawaitikia kwa chochote".

Qur'an, 13:14

"Na wale mnaowaita badala yake, hawawezi kukusaidieni wala hawawezi kujisaidia nafsi zao".

Qur'an, 7:197

"Na wale mnaowaita kinyume chake, hawamiliki japo utando wa kokwa ya tende."

Qur'an, 35:13

"Na wale mnaowaita kinyume cha Mwenyezi Mungu (wao) ni waja kama ninyi".

Qur'an, 7:194

"Waambie, waiteni wale mnaodai (kuwa ni Miungu) kinyume chake (Mwenyezi Mungu) hawawezi kukuondoleeni matatizo wala kubadilisha (chochote).

Qur'an, 17:56

"Hao wanaowaita wao (wenyewe) wanatafuta (njia) ya ukaribiano na Mola wao".

Qur'an, 17:57

"Wala usikiite (chochote) kinyume cha Mwenyezi Mungu, ambacho hakikunufaishi wala kukudhuru".

Qur'an, 10:106

"Kama mkiwaomba (masanamu hao) hawasikii wito wenu:

Qur'an, 35:14

"Ni nani mpotevu mkubwa kuliko yule anayemuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ambaye hatamjibu mpaka siku ya Qiyama?"

Qur'an, 46:5

Kwa kutumia aya hizi, Mawahabi wanazitolea ushahidi kuharamisha kuomba msaada kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu na pia kuwaita baada ya kufa kwao, na (wanasema) kwamba, kufanya hivyo ni kuwaabudia Mawalii hao na ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Wanasema Mawahabi, "Kama mtu atasema kwenye kaburi la Mtume [s] au akawa sehemu nyingine akasema, "Ewe Muhammad". Basi atakuwa amemuabudu (Mtume) kwa wito huu alio mwita na dua hii.

Wahabi aitwaye As-San-Ani anasema: "Bila shaka Mwenyezi Mungu ameiita dua kuwa ni ibada pale aliposema, "Niombeni nitakuitikieni, kwa hakika wale wanaopinga ibada yangu...." Basi yeyote atakayeliita jina la Mtume fulani au Mcha mungu fulani kwa kutaka kitu fulani (kwa Nabii au Mchamungu huyo) au akasema (Ewe Nabii) niombee kwa Mwenyezi Mungu katika shida yangu au akasema, nakuomba uniombee kwa Mwenyezi Mungu katika shida yangu, au akasema, (Ewe Nabii) nilipie deni langu, niponye ugonjwa wangu na mengineyo mfano wa haya, basi atakuwa amemuomba Nabii huyo au Mchamungu huyo wakati dua ni Ibada, na zaidi ya hapo (dua) ndiyo roho ya ibada, hivyo amemuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na amekuwa mshirikina, kwani tauhidi haitimii isipokuwa kwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika uungu kwa kuitakidi kuwa hakuna muumba wala mwenye kutoa riziki isipokuwa yeye, na pia kumpwekesha katika ibada kwa kutokumuabudu asiyekuwa yeye japo kwa baadhi ya ibada, na wale waabuduo sanamu walikuwa washirikina kwa kutompwekesha Mwenyezi Mungu katika ibada."[232]

Jibu Lake: Miongoni mwa mambo yasiyokuwa na shaka ndani yake ni kwamba, tamko "Dua" katika lugha ya Kiarabu maana yake ni wito, na huenda pia likatumika kwa maana ya ibada, isipokuwa tu haiwezekani kwa namna yoyote ile matamko ya dua na ibada kuwa na maana moja.

Haiwezekani kusema kuwa "Kila dua ni Ibada" kutokana na sababu zifuatazo:

1. Bila shaka Qur'an imelitumia tamko la dua mahala pengi na haiwekani kusema kuwa makusudio yake yalikuwa ni ibada, kwa mfano:

Mwenyezi Mungu anasema: "(Nuhu) akasema, Ee Mola wangu hakika nimewalingania (yaani Daawtu) watu wangu usiku na mchana".

Qur'an: Nuh: Aya ya 5

Hivi kweli inakubalika kusema kwamba Nabii Nuh [a] kwa maneno yake hayo alikusudia kwamba yeye amewaabudu watu wake usika na mchana?

Hebu soma kauli ya Mwenyezi Mungu akimnukuu Ibilisi atapokuwa akiwaambia wenye dhambi siku ya Qiyama:

"Wala sikuwa na mamlaka juu yenu (ya kukulazimisheni mnifuate) isipokuwa nilikwiteni (yaani Daawtukum) nanyi mkaniitikia".

Qur'an, 14:22

Je, kuna yeyote atakayepelekea (mawazo yake) kwamba, maana ya wito (yaani dua) wa shetani kwa watu wenye dhambi unamaanisha kuwa shetani aliwaabudu wata hao? Pamoja na hali hii tunafahamu kwamba, kama ibada ikithibitika basi ibada hiyo itatoka kwa watu hao wenye madhambi kumuabudia shetani na siyo shetani kuwaabudia wao.

Ndani ya aya hizi mbili na zingine zinazofanana na hizi, tamko "Aad-Daawah" limekuja siyo kwa maana ya ibada, kwa ajili hiyo basi haiwezekani kusema kuwa dua na ibada ni matamko mawili yenye maana moja, wala haiwezekani kusema kwamba yeyote mwenye kumuita mmoja wa Manabii au Mawalii basi atakuwa kamuabudia na amemshirikisha Mwenyezi Mungu hapana sivyo kabisa, kwani mwito na dua yana maana pana zaidi kuliko ibada na mengineyo.

2. Maana ya dua katika aya walizotolea ushahidi Mawahabi haina mama ya wito tu, bali ni wito ambao uko katika maana ya ibada, kwa kuwa aya zote hizi zilishuka kuwahusu wafanyao ibada ya masanamu, ambao walikuwa wakiyaitakidi masanamu yao kuwa ni mungu wadogo waliopewa jukumu Ia (kusimamia) baadhi ya mambo ya ulimwengu, na miungu hao wanaouwezo wa kuendesha (mambo ya ulimwengu).

Zaidi ya hapo ni kwamba, dua na mwito kwa masanamu haya sawa sawa kama yatakuwa ni miungu wakubwa au wadogo, kuitakidi kuwa yanamiliki uwezo wa kushufaiya na maghfira ni kuyaabudu na ni shirki.

Dalili iliyo wazi mno juu ya kwamba waabudu sanamu walikuwa wakiyaita masanamu yao kwa kuitakidi kuwa hayo ni miungu ni hii kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Haikuwafaa kitu miungu waliyokuwa wakiita kinyume cha Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 11:101

Kwa hiyo basi aya zilizotajwa (Na Mawahabi) hazina kabisa uhusiano kati yake na mas-ala haya, kwa kuwa mas-ala haya yanachunguza juu ya uwezekano wa mtu kumuomba msaada mtu mwingine bila ya kumuitakidi kuwa ni mungu wala kumuitakidi kuwa na uwezo wa kujitegemea na kumiliki uendeshaji wa mambo ya ulimwengu wala dunia wala akhera isipokuwa (anaombwa msaada huo hali ya) kuzingatiwa kuwa ni mja mwema mwenye cheo mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Utume au Uimamu, na Mwenyezi Mungu ameahidi kukubali maombi ya mja huyu mwema kwa amuombeaye kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Lau wao waliopojidhulumu nafsi zao wangekujia na wakamuomba Mwenyezi Mungu msamaha, na Mtume naye akawaombea msamaha, wangemkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kukubali toba Mwenye huruma".

Qur'an, 4:64

3. Bila shaka aya zilizotolewa na Mawahabi kama ushahidi zinaonyesha kuwa Makusudio ya neno "Dua" yanamaanisha maana ya "Ibada" nasiyo kinyume cha hivyo.

Hebu fanya mazingatio ya kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

"Na Mola wenu anasema, niombeni nitakujibuni, kwa hakika wale wanaojivuna kufanya ibada yangu, bila shaka wataingia motoni wadhalilike."

Qur'an, 40:60

Bila shaka Mwenyezi Mungu amelitaja jambo la "Ud-uuni" kisha akalifuatisha tamko la Ibada yangu, "ibaadati" jambo ambalo linajulisha wazi kwamba, makusudio ya "Niombeni (Ud-uuni)" katika aya hii ni ibada ya Mwenyezi Mungu na (kunatakiwa) kuacha ibada isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu, na hii inaonyesha kuwa washirikina walikuwa wakijivuna kufanya dua na ibada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu."

Mjukuu wa Mtume [s], al-Imam Zainul-Abidin [a] anasema katika moja ya dua zake:

"Dua ya (kukuomba) wewe umeiita kuwa ni ibada, na kuiacha umekuita ni kujivuna na umeonya kwa kuiacha (kutasababisha) kuingia motoni katika hali ya kudhalilika."[233]

Katika Qur'an kuna aya mbili zilizokuja zikiwa na maana moja, mojawapo limetumika tamko 'Al-Ibadah" na ya pili limetumika tamko 'Ad-Daawa".

Aya ya kwanza Mwenyezi Mungu Anasema:

"Waambie, Mnawabudu wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao hawamiliki dhara wala manufaa"?

Qur'an, 5:76

Ya pili kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Waambie, Je, tumuombe asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ambaye hatatunufaisha wala kutudhuru"?

Qur'an, 6:71

Pia Mwenyezi Mungu Anasema:

"Na wale muwaombao hawamilki japo utando wa kokwa ya tende".

Qur'an, 35:13

Ndani ya aya hii imekuja kwa tamko "Mnaomba," yaani "Tad 'uuna" na humo mna dalili iliyo wazi kabisa kwamba, ombi hili 'Ad Daawah" ni la kuwaomba masanamu, na hiyo ndiyo iliyokuwa itikadi ya washirikina, wakiitakidi kuwa masanamu ni Miungu inayodhuru na kunufaisha kinyume cha Mwenyezi Mungu na ndiyo maana Mwenyezi Mungu akawakosoa kwa kuwaambia kuwa (Masanamu) hayo "Hayamiliki japo utando wa kokwa ya tende."

Maana kama hii imekuja katika aya inayofanana kwa tamko la "Ta'abuduna" kama ilivyo kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

"Bila shaka hao mnaowaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu hawana mamlaka ya riziki zenu".

Qur'an, 29:17

Na ndani ya aya nyingine yamekuja maneno mawili yenye kulingana kwa maana moja.

Mwenyezi Mungu anasema: "Waambie, Mimi nimekatazwa kuwaabudu wale mnaowaita kinyume cha Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 6:56

Na karibu na maana ya aya hii ni aya ya 66 Sura ya 40.

Ewe msomaji mpendwa nakutarajia kuwa utairejea al-Mujamul-Mufahras Li alfaadhil-Qur'an il-Karim katika madda ya "Abada, ameabudu" na "Daa, ameomba" ili upate kuona kwa macho yako ni namna gani tamko la ibada lilivyokuja katika aya fulani na pia tamko la "Ad daawat" na "Ad duaa" yalivyokuja katika aya nyingine. Utaona kuwa matamko hayo katika namna hizo mbili yamekuja kwa maana na madhumuni ya namna moja yaani ibada, jambo ambalo ni dalili iliyo wazi kuonyesha kuwa makusudio ya "Ad Daawat" na "Ad Duaa" katika aya hizi ni ibada na kwamba aya hizi hazihusiki na mwito peke yake.

Basi utakapozifanyia mazingatio aya ambazo zimeambatana na tamko "Ad Duaa" na "Ad Daawat" kwa maana ya ibada, utaona kuwa aya hizo zinazungumzia mapambano kati ya imani na kufru, na pia baina ya ibada ya Mwenyezi Mungu, Tauhidi, imani ya uungu wake dhidi ya ibada ya masanamu na itikadi za (kuyapa) uwezo wa kumiliki riziki, maghfira, shafaa, kunufaisha na kudhuru.

Hivyo basi, Mawahabi kutoa ushahidi kwa aya hizi ili kuharamisha kuwaita Manabii na Mawalii na kutaka kwao msaada, ni jambo linalopelekea kushangaza na kustaajabisha hasa inapoonekana kuwa aya walizotolea ushahidi hazina uhusiano wowote na mas-ala haya.

Kifupi tu, kwa yale yaliyothibiti ndani ya utafiti huu ni kuwa: Kauli yako utaposema, "Yaa Ali" hali ya kuwa unakusudia kumsemesha Khalifa wa Mtume [s] au ukasema, "Ya Husain" au "Ya Zahraa" au ukataja jina jingine la mmoja miongoni mwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu waliotakasika hakuna tatizo kabisa kwa kusema hivyo, bali ni namna ya kuomba msaada kwao, Mwenyezi Mungu awateremshie Rehma wote.

Basi jambo hili ni zuri linalofaa kufanywa, na humsaidia mtu kujinasua toka kwenye matatizo na shida na kumuokoa kutokana na maangamizi na kisha kumpa faraja.

[232] Kashful-Irtiyabi: uk. 274, ikiwa ni makala toka ndani ya kitabu Tanzihul-iitikad cha As-San-Ani.

[233] As-Sahifatus-Sajjadiyyah, dua ya 45.