KUMUAPIA ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU MTUKUFU

Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa mambo ambayo Mawahabi wana uchungu nayo sana na ni katika mas-ala ambayo wao wanayakemea na kuyapigia kelele kwa kutumia kalamu zao potofu.

Mwandishi wa Kiwahabi aitwaye As-San-Ani, yeye kwa mawazo yake anaona kuwa kumuapia asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni shirki!![218]

Vile vile mtunzi wa Kitabu kiitwacho 'Al-Hadiyyatus-Saniyya, yeye kwa mawazo yake anaona kuwa (kumuapia asiyekuwa Mwenyezi Mungu) ni shirki ndogo.[219]

DALILI ZINAZORUHUSU KUMUAPIA
ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU

Dalili Ya Kwanza: Bila shaka Qur'an ndicho kile kizito kikubwa na ndicho kiongozi cha juu na ndiyo kiigizo hai kwa kila Muislamu. Ndani yake utaona viapo vingi katika mahali pengi vya kumuapia asiyekuwa Mwenyezi Mungu kiasi kwamba kuvitaja kwa uchambuzi kutapelekea kurefusha uchambuzi wa maudhui hii.

Kwa mfano: Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat As-Shamsi peke yake ameapa kwa vitu vinane vikiwa ni miongoni mwa viumbe vyake.

Vitu hivyo ni: Jua, Mwanga wa Jua, Mwezi, Mchana, Usiku, Mbingu, Ardhi na nafsi ya mtu.

Qur'an, 91:1-7.

Kama ambavyo Mwenyezi Mungu katika Surat "An-Naziat" ameapia vitu vitatu, na akaapa kwa vitu viwili katika Surat "Al-Mursalat" na pia vimekuja viapo kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika Surat "At-Tariq", "Al-Qalam" "Al-Asr", na "Al-Balad".

Qur'an, 79:1-3 na 77:1-3.

Hebu angalia mifano ya aya za kiapo cha kumuapia asiyekuwa Mwenyezi Mungu ndani ya Sura zingine (zaidi ya tulizozitaja hapo juu).

"Naapa kwa (Miti Ya) Tini na Zaituni, na kwa Mlima Sinai, na kwa Mji huu wenye Amani".

Qur'an, 95.1-3.

"Naapa kwa usiku ufunikapo, na kwa mchana uangazapo".

Qur'an, 96:1-2.

"Naapa kwa Al-Fajri, na kwa masiku kumi, na kwa Shafaa na Witri na kwa usiku unapopita".

Qur'an, 89:1-4.

"Naapa kwa Mlima, na kwa Kitabu kilichoandikwa katika karatasi ya ngozi kikakunjuliwa, na kwa nyumba inayozuriwa, na kwa sakafu (mbingu) iliyonyanyuliwa, na kwa bahari zilizojazwa (maji).

Qur'an, 52:1-6.

"Naapa kwa uhai wako, bila shaka wao wako katika upofu wanahangaika".

Qur'an, 15:72.

Basi ni vipi itafaa kuhukumu kwamba kuapia kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni shirki na ni haramu, hali ya kuwa kuna aya nyingi za Qur'an zimelitaja jambo hilo?

Ikiwa mtu atasema, "Kiapo hiki kinamuhusu Mwenyezi Mungu peke yake".

Jawabu: Sivyo kabisa, bila shaka Qur'an ni Kitabu cha muongozo kwa watu, na watu wanakichukulia kuwa ni kiigizo cha kufuata, basi lau ingekuwa aina hii ya kiapo ni haramu kwa waja wa Mwenyezi Mungu, Qur'an ingelazimika kuhadharisha kwamba kiapo hiki ni miongoni mwa mambo yanayomuhusu Mwenyezi Mungu.

Na ilipokuwa tahadhari hii haikutajwa, basi imekuwa ni dalili ya kutokuhusika kwa kiapo hiki kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Wako baadhi ya watu miongoni mwa wale wasiojua malengo ya Qur'an wanasema kwamba "Inawezekana kuwa jambo litokalo kwa Mwenyezi Mungu likawa zuri, na jambo hilo hilo likafanywa na mwingine likawa baya".

Jawabu la madai haya liko wazi, kwani kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu lau ingekuwa ni shirki na ni kumshabihisha kwa Mwenyezi Mungu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi ni kwa nini shirki hii hii (ndogo au kubwa) imetoka kwake Mwenyezi Mungu? Je, Hivi inasihi kwa Mwenyezi Mungu yeye mwenyewe kujiwekea mshirika na akamkataza mwingine kufanya shirki kama hii?

Dalili Ya Pili: Mtume [s] aliapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika mahala pengi.

Miongoni mwake ni:

1. Muslim katika Sahihi yake amepokea (hadithi ifuatayo).

Kuna mtu fulani alikuja kwa Mtume [s] akasema, "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ni sadaka gani yenye malipo makubwa"? Mtume akasema, "Amma naapa kwa baba yako, wewe ni lazima utapewa khabari yake nayo ni kwamba wewe unatoa sadaka wakati wewe ni mzima na unaipenda mali, unaogopa ufakiri na unatarajia kuendelea kuishi."[220]

2. Muslim amepokea tena (hadithi ifuatayo):

"Kuna mtu fulani kutoka Najdi, alikuja kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] akitaka kuufahamu Uislamu, Mtume [s] akasema: "Ni Kusali Sala tano kila siku."

Yule mtu akasema; Je, kuna wajibu juu yangu zaidi ya Sala tano? Mtume akasema: Hapana, isipokuwa ukitaka kufanya Sunna na ufunge mwezi wa Ramadhani".

Yule mtu akasema: Ninawajibu mwingine juu yangu zaidi ya huu?

Mtume akasema: "Hapana, isipokuwa ukifunga Sunna na Mtume akamtajia mtu huyo Zaka".

Yule mtu akasema: "Kuna wajibu juu yangu zaidi ya huu"?

Mtume akasema: "Hapana, isipokuwa ukitaka kufanya Sunna".

Yule mtu aliondoka huku akisema, "Namuapa Mwenyezi Mungu sintazidisha zaidi ya hivi (nilivyofundishwa) wala sintapunguza."

Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] akasema, "Naapa kwa Baba yake, kama anasema kweli, basi amefaulu". Au alisema, "Naapa kwa Baba yake, kama anasema kweli ataingia Peponi."[221]

3. Hadithi hii (Tuliyoitaja) imekuja pia katika Musnad ya Ahmad bin Hanbal na mwishoni mwa hadithi hii katika Musnad ya Ahmad imekuja kwamba Mtume [s]. alimwambia yule mtu, "Naapa kwa maisha yangu, ikiwa utaamrisha mema na kukataza maovu ni bora kuliko kukaa kimya".[222]

Na kuna hadithi nyingine ambazo nafasi ya kitabu haitoshelezi kuzitaja.[223]

Naye Amirul-Mu'miniina Ali Ibn Abi Talib [a] ambaye anazingatiwa kuwa ni mfano ulio wazi wa malezi ya Kiislamu na uongozi mtukufu, aliapia nafsi yake tukufu zaidi ya mara moja katika khutba zake na barua zake na maneno yake.[224]

Vile vile Bwana Abubakr bin Abi Qahafah aliapa kwa baba wa mtu aliyekuwa akizungumza naye.[225]

KUAPA KWA ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU KATIKA MADHEHEBU MANNE

Kabla hatujaleta dalili za Mawahabi zinazoharamisha kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ni bora tukaleta fat-wa za Maimamu wa madhehebu manne kuhusu mas-ala haya.

Kwa ufafanuzi zaidi unaweza kurejea kitabu kiitwacho "Al-Fiq-hu Alal-Madhahibil-Ar-Baa", mlango wa kiapo Juz. 1, uk. 75 Chapa ya Misri.

Ama Madh-hebu ya Kihanafi, wao wanasema kwamba, "Kuapia baba na uhai kama vile mtu akasema, "Naapa kwa baba yako, au akasema, naapa kwa uhai wako" na mfano wa viapo hivi, jambo hili ni karaha (makruhu).

Nao Mashafii wao wanasema kwamba; "Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa si kwa itikadi ya shirki, basi jambo hili ni makruhu."

Ama madhehebu ya Kimaliki, wao wanasema, "Bila shaka kuapia vitu vitukufu na vyenye heshima, kama Nabii na Al-Kaaba, kuna kauli mbili, haramu na karaha." Lakini iliyo mashuhuri baina yao (wenye Madhehebu ya Malik) ni haramu.

Na kwa upande wa Madh-hebu ya Hanbal wao wanasema kwamba, kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu na sifa zake ni haramu hata kama kiapo hicho kitakuwa ni kuapia Manabii au mmoja wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu.

Hizi ndizo fat-wa za Maimamu wa madh-hebu manne.

Nasi sasa hivi hatuko katika msimamo wa kujadiliana na wale wasemao kuwa ni Haramu (kuapa kwa asiye Mwenyezi Mungu). (Tunachoweza kusema) ni kwamba fat-wa zao ni jitihada yao dhidi ya nassi ya Qur'an na Sunna ya Mtume [s] na sera ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kadhalika wanachuoni wa madhehebu haya wameufunga mlango wa Ijtihadi kwao wao kwa hiyo wakajikuta wamelazimika kufuata maoni ya wale Maimamu wanne peke yao.

Sisi hatuyaamini maneno waliyonasibishiwa Maimamu hao juu ya mas-ala haya, kwani AI-Qastalani amesema kuwa, "Imam Malik bin Anas alikuwa akisema kuwa ni karaha kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu".[226]

Pia kuwanasibishia Madh-hebu ya Hanbal kuwa wanasema ni haramu haikuthibiti vile vile kwa sababu, Ibn Qud-damah anaeleza katika kitabu kiitwacho "Al-Mughni" alichokiandika ili kuihuisha Fiqhi ya Kihanbal anasema, "Ahmad bin Hanbal ametoa fat-wa kuwa inafaa kuapia kwa Mtume [s], na kwamba kiapo kinathibiti kwa kuwa Mtume ni moja ya nguzo mbili za shahada.

Na amesema Ahmad bin Hanbal: "Lau (Mtu) ataapa kwa kumuapia Mtume, kiapo chake kitathibiti na kama hatatekeleza kiapo chake basi itamlazimu kutoa kafara".

Pamoja na kauli zilizo tangulia, haiwezi kuthibitika moja kwa moja kuwa Maimamu wa madhehebu haya manne wametoa Fat-wa kuharamisha kuapia kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ewe msomaji mpendwa, baada ya kuzichunguza fat-wa za Maimamu wa madh-hebu manne, sasa tunahamia kwenye kutaja hadithi mbili ambazo Mawahabi wamezishikilia katika kuharamisha kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Na kwa kutumia hadithi hizo, Mawahabi wamemwaga damu ya watu wasiyokuwa na makosa na kuwashambulia mimilioni ya Waislamu kwa kuwakufurisha.

Kwa hakika Mawahabi waliushambulia mara mbili mji mtakatifu wa Karbala, moja ya mashambulizi hayo lilikuwa mwaka 1216 A.H. na jingine mwaka 1259 A.H., na hawakumhurumia mdogo wala mkubwa kiasi kwamba waliwauwa Waislamu elfu sita katika muda wa siku tatu tu, na walipora kila kitu cha thamani kubwa kichokuwa katika Haram Tukufu ya Imam Husein, na tendo lao hili ni la kufuata nyayo za matendo yaliyofanywa na majeshi ya Yazid Ibn Muawiyah wakati yalipoushambulia mji wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s]. Lakini ni kwa nini? Ni kwa nini basi kufanya mashambulizi haya yenye chuki?

Sababu yake ni kuwa, Waislamu hawa walikuwa wakimuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya watoto wa Mtume [s] na wakiwapenda.

Hadithi ya Kwanza: Hakika mjumbe wa Mwenyezi Mungu alimsikia Omar akisema, "Namuapa baba yangu". Mtume akamwambia, "Hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni kuapa kwa baba zenu, basi kama kuna yeyote mwenye kuapa na amuape Mwenyezi Mungu au anyamaze (asiape)".[227]

Jawabu:
Kwanza, huenda katazo la kuwaapa wazazi (wao) lilikuja kwa sababu wazee hao wengi wao walikuwa ni washirikina waliokuwa wakiabudu masanamu, kwa hiyo hawana ubora wala utukufu kiasi cha kuweza yeyote yule kuwaapia.

Na bila shaka kuna hadithi imekuja kutoka kwa Mtume [s] kwamba: "Musiapie kwa wazee wenu wala kwa masanamu".[228]

Na imepokelewa vile vile kwamba: "Musiapie kwa Baba zenu wala mama zenu wala kwa miungu."
[229]

Pili: Makusudio ya katazo la kuapa kwa baba, (Mtume alipokataza kuapa kwa baba makusudio yake) ilikuwa ni kile kiapo ambacho kinatumika katika hukumu ya kesi ili kuondoa kutokuelewana na uhasama kwani wanachuoni wa Uislamu wanaafikiana kwamba, kiapo ambacho kinatumika kwa ajili ya kuondosha kutoelewana na ugomvi ni kuapa kwa Mwenyezi Mungu na sifa zake, ama kiapo kingine hiki hakiingii mahala hapa. Pamoja na kuwepo kwa Qarina hizi zilizowazi..... Basi vipi itawezekana kusema kwamba Mtume [s] alikataza kuapia kwa vitu vitakatifu kama vile Al-Kaaba na Qur'an na Mawalii wa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa tunafahamu kwamba katazo lilikuwa linahusu mahali maalum na Mtume mwenyewe alikuwa akiapia vitu visivyokuwa Mwenyezi Mungu?

Hadithi ya Pili: Ibn Omar aliijiwa na mtu mmoja akamwambia, "Je, Niapie Al-Kaaba"? Ibnu Omar akamwambia yule mtu, "Hapana (usiapie Al-Kaaba) lakini apa kwa Mola wa al-Kaaba, kwani Omar alikuwa akiapa kwa baba yake na Mtume akamwambia, usiapie kwa baba yako kwani yeyote mwenye kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu bila shaka atakuwa amefanya shirki".[230]

Jibu La Kwanza: Bila shaka hadithi hii imefungamana na mambo matatu:

1. Mtu aliyekuja kwa Ibn Omar akasema niape kwa al-Kaaba? Akamjibu kwa kusema, hapana, lakini apa kwa Mola wa Al-Kaaba.

2. Omar bin Khatab alikuwa akiapa kwa baba yake, Mtume [s] akamkataza kufanya hivyo.

3. Mtume [s]. alibaimsha ubaya wa kufanya hivyo kuta kusema "Yeyote atayeapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu atakuwa kafanya shirki".

Kiapo chenye uhakika katika hadithi hiyo kama yalivyokuja maneno ya Mtume [s] ni kuwa, iwapo kinachoapiwa siyo katika vitu vitakatifu kama vile kafiri na sanamu.

Lakini Ibn Omar alifanya Ij-tihadi kwa kusema kuwa, kauli ya Mtume isemayo "Yeyote mwenye kuapa kwa asiye Mwenyezi Mungu atakuwa kafanya shirki" ambayo aliisema kutokana na kuapiwa kwa mshirkina ambaye ni Khattab mzazi wa Omar, Ibn Omar alijitahidi (kutoa maoni yake) kuwa eti kauli hiyo ya Mtume inakusanya pia kuapa kwa vitu vitakatifu, kama vile al-Kaaba, hali ya kuwa anafahamu kuwa maneno ya Mtume [s] yalikuja kutokana na kiapo cha kumuapia mshirkina kama tulivyofafanua wakati tukiichambua ile hadithi iliyotangulia.

Kwa hiyo basi maneno ya Mtume [s] yalikuwa katika kanuni maalumu aliyoiweka kwamba, ikiwa kinachoapiwa ni kitu kisichokuwa kitakatifu.

Lakini Ibn Omar alifanya Ij-tihadi akayafanya maneno ya Mtume kuwa yanakusanya zaidi ya maana hiyo. Na Ij-tihad yake hiyo ni hoja juu yake mwenyewe na siyo juu ya mwingine.

Bila shaka hapo kabla tumefafanua ya kwamba, Mtume [s] alikuwa akiapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu mara nyingi tu.

Basi inapasa tuichukue kauli yake isemayo; "Yeyote mwenye kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu atakuwa kafanya shirki" iwe kwa maana ya kuapia kwa mshirikina na mfano wake, na siyo kwa maana ya kuapia vitu vitukufu kama vile Qur'an na al Kaaba na Mtume.

Na hii itakuja kutokana na dalili kwamba Mtume aliweka kanuni hii wakati Omar alipoapa kwa baba yake ambaye ni mshirikina. Ibn Omar alipoieneza hadithi hii na kuingiza kuapa kwa asiyekuwa mshirikina hiyo in ij-tihadi yake mwenyewe bila ya dalili. (Pengine) utauliza: Ni kwa nini Mtume [s] aliona kuwa kuapia kwa mshirikina ni shirki?

Jawabu Lake: Ni kwamba, kuapa kwa mshirikina ni miongoni mwa aina za kumpa nguvu mshirkina na kumtukuza na kuithibitisha dini yake na itikadi yake potofu.

Kwa kifupi sisi tunaikubali asili ya hadithi lakini hatukubali Ij-tihad ya Ibn Omar kutokana na yeye kwenda kinyume na Sunna ya Mtume [s] na sera ya Masahaba.

Kanuni iliyotajwa ndani ya hadithi ya Mtume Mtukufu [s] inahusu kile alichokiapia Omar, wala haikusanyi kamwe vitu vitukufu vya Kiislamu.

Na ama kuapia Al-Kaaba na Qur'an na Manabii na Mawalii mahala pasipokuwa na kesi na hukumu zake jambo hilo liko nje ya kanuni hiyo ya ujumla, na siyo shirki wala haramu.

Jawabu la Pili: Hapa kuna Jawabu jingine lililo wazi zaidi kuliko lile la kwanza, nalo ni lifuatalo):

Bila shaka kauli ya Mtume [s] aliposema: "Yeyote atakayeapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu basi atakuwa kafanya shiriki". Inaashira kiapo maalum tu nacho ni kuapia masanamu kama vile lata na uzza (miungu iliyokuwa ikiabudiwa na Maquraishi) wala hakimuingizi mtu mshirikina licha ya vitu vitukufu.

Jawabu hili, linaungwa mkono na hadithi aliyoipokea An-Nasai ndani ya Sunan yake kwamba, Mtume [s] amesema:

"Yeyote atakayeapa akasema katika kiapo chake, Naapa kwa Lata na Uzza, basi mtu huyu na (Atoe Shahada) aseme; "La illaha Ila-llahu."[231]

Pia hadithi aliyoipokea ndani ya kitabu hicho hicho kwamba Mtume [s] amesema: "Msiape kwa baba zenu wala mama zenu wala kwa miungu".

Bila shaka hadithi ya kwanza inajulisha kuwa, itikadi za Kijahiliya zilikuwa zimeacha mabaki yake katika baadhi ya nafsi za watu, basi wakawa huapia Masanamu yao waliyokuwa wakiyaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu, ndipo Mtume [s] akawaamuru kusema "La illaha ila llahu" ili kuondosha mabaki hayo ya itikadi za Kijahiliyya.

Na yale mapokezi yaliyopokelewa na Imam wa Mahanbali yanafahamisha kuwa kauli yake Mtume [s] isemayo, "Yeyote atakayeapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu basi atakuwa kafanya shirki". Hadithi iko peke yake tu.

Baadaye akaja huyu Ibn Omar akaingiza Ij-tihadi yake binafsi kwamba, kiapo (kilichotajwa katika hadithi) kinakusanya kiapo cha kumuapia baba na vitu vitakatifu.

Lakini (kwa mujibu wa hadithi hiyo) kuapia kwa wazazi na vitu vitakatifu havikuwemo ndani ya hadithi hiyo, na aliyeviingiza humo ni Ibn Omar.

Ile hadithi aliyoipokea Imam wa Madh-hebu ya Hanbal ni hii ifuatayo:

Imepokewa kutoka kwa Ibn Omar amesema, Baba yangu alikuwa akiapa, Mtume akamkataza akasema; "Yeyote atakayeapa kwa asiye Mwenyezi Mungu basi atakuwa kafanya shirki".

Bila shaka unaiona hadithi ya Mtume [s] imepwekeka kutokana na maneno ya Ibn Omar na haikuja na Waw ya Atfu au Fau ya Tafrigh, bali amesema; "Fanahahun-Nabiyyu" (Yaani Mtume akamkataza) akasema: ...... Jambo ambalo linajulisha kwamba hadithi hii ilitoka katika wakati mwingine na haikuwa na nyongeza yoyote.

Ewe msomaji mpendwa mukhtasari wa maelezo yaliyomo ndani ya mlango huu tulioeleza uko kama ifuatavyo:

1. Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu hapana kizuwizi chochote kishera, na kiapo hicho kimeanzia kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya Qur'an Tukufu na Mtume wa Mwenyezi Mungu [s] na pia Khalifa wa Mtume Amirul-Mu'minina Ali [a] na Waislamu.

2. Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu si sahihi (Lakini hutusemi haijuzu), si sahihi katika hukumu na kesi, bali ni lazima kumuapa Mwenyezi Mungu au kuapa kwa moja ya sifa zake ambazo ndizo dhati yake tukufu, na hili limethibiti kwa dalili maalum wala halina uhusiano katika uchunguzi huu.

Bila shaka hadithi mbili ambazo Mawahabi wapotofu wamezitolea dalili juu ya kuharamisha kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, hazina uhusiano na kile ambacho sisi tunakizungumzia yaani kuapa kwa vitu vitukufu vya Kiislamu kama Qur'an, al-Kaaba, Manabii, Maimamu na Mawalii, bali hadithi hizo zinahusu kuapia mambo yasiyokuwa matukufu kama vile wazazi washirikina na masanamu yaliyokuwa yakiabudiwa zama za jahiliya.

Namna hi kwa maelezo haya kile kifuniko cha Uislamu walichokivunja Mawahabi wapotovu kinaondoka, kifuniko ambacho hukivalisha ule mtazamo wao wa kipekee na fikra zao potofu.

Sifa zote njema Anastahiki Mwenyezi Mungu.

[218] Tat-Hirul-Iitiqad cha As-Sanani, uk. 14

[219] Al-Hadiyyatus-Saniyyah, uk. 25

[220] Sahihi Muslim, Juz. 3, Kitabul-zakat.

[221] Sahih Muslim, Juz. 1, babu Mahuwal-Islam, uk.32

[222] Musnad Ahmad, Juz. 5, uk. 225

[223] Musnad Ahmad, Juz. 5, uk. 212, Sunan Ibn Majah, Juz. 4, uk. 995 na Juz. 1, uk. 255 ili kupata maelezo kwa urefu zaidi.

[224] Nah-Jul-Balagha Hashiya ya Muhammad Abdoh, Khutba Na. 22, 25, 56, 85, 161, 168, 182, 187, na Barua Na. 6, 9 na 54.

[225] Kitabul-Muwataa cha Malik Bin Anas Imam wa Madh-hebu ya Malik chenye Sherehe ya Zir-Qani, Juz. 4, uk. 159.

[226] Ir-Shadis-Saari, Juz. 9, uk. 358.

[227] Sunan Ibn Majah Juz. 1, uk. 277, na Sunan Atir-midhi, Juz. 4 uk. 109 n.k.

[228] Sunan An-Nasai Juz. 7, uk. 7, Sunan Ibn Majah, Juz. 1, uk. 278

[229] Sunan An-Nasai Juz. 7, uk. 9

[230] As-Sunanul-Kubraa cha Al-Baihaqi Juz. 10, uk. 29, na hadithi kama hii iko katika Musnad Ahmad bin Hanbal, Juz. 2, uk. 69.

[231] Sunan An-Nasai Juz. 7, uk 8.