KUMUAPA MWENYEZI MUNGU KWA HAKI YA MAWALII

Miongoni mwa nukta wanazotofautiana Waislamu na Mawahabi ni kwamba, Mawahabi wanadai kuwa, ni haramu kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii, na pia kuapia kisichokuwa Mwenyezi Mungu.

Wakati mwingine Mawahabi wanaona kuwa viapo hivi viwili ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika Ibada. Katika maelezo yafuatayo tutaisherehesha kwa urefu maudhui hii ili kupata hukmu sahihi ya kisheria.

KUMUAPA MWENYE MUNGU KWA HAKI YA MAWALII

Bila shaka Qur'an inawasifu baadhi ya waja wa Mwenyezi Munga inaposema:

"Wafanyao subira na wasemao kweli na watifu na watoao sadaka na wale wanaoomba msamaha saa zilizo kabla ya alfajiri".

Qur'an, 3:17.

Basi lau mtu atasimama katikati ya usiku akasali kwa ajili ya Mola wake rakaa nyingi, kisha akanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu huko akisema:

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kwa haki ya wanaokutaka msamaha wakati wa karibu ya al-fajiri, unisamehe dhambi zangu". Itakuwaje basi kauli yake hii tuione kuwa ni shirki katika Ibada?

Bila shaka shirki katika Ibada maana yake ni "Kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, au ni kumzingatia asiyekuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni Mungu na ndiyo chanzo cha matendo ya Kiungu".

Ama mahala hapa (tunapopazungumzia) yule mtu anayeswali anamuelekea Mwenyezi Mungu na haombi chochote (kwa mwingine) isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu. Basi iwapo tendo hili ni haramu, hapana budi kuwe kuna sababu nyingine isiyokuwa shirki.

Sisi hapa (nia yetu) tunataka kuwaelekeza Mawahabi wafahamu kwamba, Qur'an Tukufu imetaja kipimo na kanuni ili kufafanua na kupambanua baina ya mshirkina katika Ibada na yule mwenye Tauhidi, na kwa kipimo hiki imeweka kizuwizi mbele ya kila tafsiri itayofasiriwa kwa maoni (binafsi) juu ya maana ya "mshirikina."

Kipimo hiki ni kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Na anapotajwa Mwenyezi Mungu peke yake, nyoyo za wale wasioamini Akhera huchukia, na wanapotajwa wale wasiokuwa Mwenyezi Mungu basi wao hufurahi".

Qur'an, 39:45.

Na katika aya nyingine Qur'an inawataja waovu ambao ni wale wafanyao shirki inasema:

"Bila shaka wao walipokuwa wakiambiwa "Hakuna aabudiwaye kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, walikuwa wakipinga na husema je, sisi tuiache Miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu."

Qur'an, 37:35-36.

Kwa hiyo basi kwa mujibu wa aya mbili hizi mushrik (mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu) ni yule ambaye huchukia moyo wake atajwapo Mwenyezi Mungu peke yake, na hufurahi watajwapo Miungu batili, au hupinga upweke wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Baada ya kipimo hiki cha Qur'an tunajiuliza, "Hivi yule mtu asimamaye katikati ya usiku na akamaliza saa nyingi akifanya Ibada na kuomba na akaswali mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi na unyenyekevu na akamuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii wake wema na akamuomba Mwenyezi Mungu kupitia kwa waja wake wema..... hivi kweli mtu huyu atakuwa mushrik kwa amali yake hii?!

Basi ni kwa namna gani amepinga utajo wa Mwenyezi Mungu na ni vipi amekataa kukiri upweke wa Mwenyezi Mungu Mtukufu (hata aitwe ni mushrik)?!!!

Ni kwa nini basi waandishi wa Kiwahabi wanategemea misingi ya kabuni na dalili dhaifu kuliko hata nyumba ya buibui, kisha wanawatuhumu Waislamu kuwa wanafanya shirki halafu wao wakajiona kuwa peke yao ndiyo taifa teule la Mwenyezi Mungu?!

Vipi itafaa wawazingatie asilima 99% ya Waislamu kawa ni washirikina na wao wawaone Mawahabi toka Najdi kuwa ndiyo peke yao ni watu wa Tauhidi pamoja na kuyazingatia (maelezo) ya kipimo cha Qur'an?

Na je, Mwenyezi Mungu amewapa uwakala Mawahabi wa kuifasiri maana ya shirki kama wapendavyo na waamue kwamba kundi hili ni washirikina wa kundi hili ni la watu wa Tauhidi? Ukweli ulivyo ni kwamba, "Mwenyezi Mungu ameweka kifuniko kwenye nyoyo zao basi wao hawafahamu (kitu)".

AMIRUL-MU'MINIINA (ALl [a]) NA KUMUAPA MWENYEZI MUNGU KWA HAKI YA MAWALII

Tunaangalia kumuapa Mwenyezi Mungu kama ilivyo katika dua za Mawalii wake watukufu.

Kwa mfano: Amirul-Mu'miniina Imam Ali [a] anasema katika maombi yake baada ya Sala ya usiku:

"Ewe Mwenyezi Mungu mimi ninakuomba kwa heshima ya yule aliyejilinda kwako kutokana na adhabu yako na akazitumainia nguvu zako na akajikinga kwa kivuli chako na akashikamana na kamba yako na hakutegemea ila kwako".[204]

Na anasema tena Imam Ali [a] katika dua aliyomfundisha Sahaba wake mmoja. "Na kwa haki ya wanaokuomba na wale wanaonyenyekea kwako na wanajilinda kwako na wanaodhalilika mbele yako na kwa haki ya kila mja mwenye kukuabudia katika kila sehemu ya nchi kavu au baharini au mbugani au mlimani, nakuomba maombi ya mtu mwenye shida mno...[205]

Hivi kuna kitu gani kingine kisichokuwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu ndani ya maombi haya yanayoihimiza roho na kuipeleka kwenye Ibada na kudhalilika mbele ya Mwenyezi Mungu.... Je, kuna matokeo mengine yasiyokuwa ya kuimarisha kumpwekesha Mwenyezi Mungu na (kuonyesha kuwa) hakuna mlinzi ila yeye, na kudhihirisha upendo kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu na wapenzi wake, jambo ambalo linaonyesha kuwa ni kumuelekea Mwenyezi Mungu katika wakati ule ule?"

Na kwa mantiki hii basi, tuhuma ya ukafiri na shirki inayotangazwa na Mawahabi (juu ya jambo hili) kuliko kitu kingine chochote ni lazima ikome.

Na inafaa kuyasoma maudhui haya kwa njia ya mantiki na dalili.

Kwa ajili hii ndiyo maana utawaona baadhi ya Mawahabi waadilifu japo kidogo wametatua suala la "kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii", na wanasema kwamba jambo hili ni haramu au makruhu, kinyume cha huyu 'As-san-ani" Wahabi aliyekosa uadilifu ambaye ameyasoza mas-ala haya kwenye shirki.

Na sasa basi baada ya kubainika msingi wa mazungumzo ni lazima kusoma maudhui ndani ya eneo la uharamu na karaha na kisha kubainisha dalili iliyo wazi juu ya kusihi kwa jambo hili na kufaa kwake.

Kwa hiyo tunasema:

KUTHIBITI KWA KIAPO HIKI NDANI YA UISLAMU

Qadhiya ya kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii imekuja katika hadithi nyingi mutawatiri baadhi yake zimepokewa kwa Mtume [s] na nyingine zimepokewa toka kwa Maimamu wa nyumba ya Mtume [s].

Na kwa mujibu wa hadithi hizi haiwezekani kabisa kusema kwamba ni haramu au karaha kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii.

Hebu tazama mifano ya hadithi hizo:

1. Hapo kabla imetangulia ishara kwamba, Mtume [s] alimfundisha kipofu aliyekuja kwa Mtume akimuomba Mtume [s] amuombee Mwenyezi Mungu ili macho yake yarudi.

Mtume alimfundisha kipofu yule aseme! "Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba na ninaelekea kwako kwa haki ya Mtume wako Muhammad Mtume wa Rehma".[206]

2. Abu Said Al-khudri amepokea toka kwa Mtume [s] dua hii ifuatayo:

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi ninakuomba kwa haki yawanaokuomba na ninakuomba kwa haki ya mwendo wangu huu".[207]

3. Naye Nabii Adam [a] alitubia kwa Mwenyezi Mungu akasema:

"Nakuomba kuta haki ya Muhammad unisamehe".[208]

4. Baada ya Mtume [s] kwisha kumzika Bibi Fatma binti Asad ambaye ni mama wa Imam Ali [a], Mtume alimuombea dua mama huyu akasema:

"Msamehe mama yangu Fatma binti Asad na uyakunjue makazi yake kwa haki ya Mtume wako na Manabii waliopita kabla yangu.[209]

Dua hizi japokuwa hazina lile tamko lenyewe la kiapo, lakini madhumuni yake ni kiapo kwa kuwepo herufi ya "BAA" ambayo ni ya kiapo katika hadithi zote, kwani muombaji asemapo ALLAHUMMA INNII AS-ALUKA BIHAQQIS-SAILIINA ALAIKA" maana yake ni, ninakuapa kwa haki yao.

5. Bwana wa mashahidi Imam Hussein bin Ali [a] anasema alipokuwa akiomba:

"Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba kwa haki ya maneno yako, na kwa mafungamano ya enzi yako, na kwa haki ya wakaazi wa mbingu zako na ardhi yako na Manabii wako na Mitume wako, unikubalie (maombi yangu) kwani nimefikwa na jambo zito, basi nakuomba umpe rehma Muhammad na kizazi cha Muhammad na uyawepesishe mambo yangu".

Na utakapoiangalia Sahifatu as-Sajadiyah iliyopokelewa toka kwa Imam wa nne katika Maimamu wa nyumba ya Mtume aitwaye Imam Zainul-abidina [a] humo utaona viapo vingi sana, na hii ndiyo dalili iliyo bora mno inayoonyesha kusihi kwa aina hii ya kutawassal.....

Hebu angalia mifano ifuatayo:

6. Imam Zainul-abidina [a] anasema ndani ya dua yake siku ya Arafa "(Ewe Mola) kwa haki ya yule uliyemchagua miongoni mwa viumbe wako, na kwa haki ya yule uliyemteua kwa ajili yako, na kwa haki yake uliyemchagua kutoka miongoni mwa viumbe wako, na uliyemteua kwa ajili ya shani yako, na kwa haki ya yule ambaye umeunganisha kumtii yeye ndiyo kukutii wewe na ni yule ambaye umeunganisha kufanyiwa yeye uadui ni kufanyiwa wewe uadui.[210]

7. Na wakati Imam Jaafar as-Saadiq alipozuru kaburi Ia Imam Ali [a] ambaye ni babu yake, mwishoni mwa ziyara yake aliomba akasema: "Ewe Mwenyezi Mungu nikubalie maombi yangu na upokee sifa ninazokutukuza, na unikutanishe na Mawalii wangu, kwa haki ya Muhammad na Ali na Fatma na Hasan na Husein."[211]

Ewe msomaji Mtukufu, aina ya dua kama hizi zilizoshikamana na kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii wake zimekuja kwa wingi mno kutoka kwa Maimamu wa nyumba ya Mtume [s], wenye ismah, na wala nafasi haitoshi kutaja zaidi ya tulizotangulia kuzitaja. Na dua zote hizi zinajulisha juu ya ruhusa ya kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii wake wema

DALILI ZA MAWAHABI JUU YA KUHARAMISHA

Mawahabi wametaja baadhi ya dalili za kuharamisha kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki ya Mawalii wake.

Dalili hizo ni dhaifu hazifai kutolea hoja wala kutiliwa maanani. Na sasa tunazitaja sambamba na kuzijibu katika maelezo yafuatayo:

Dalili ya Kwanza:

Mawahabi wanasema: "Wanachuoni wa Kiislamu wameafikiana kwamba, kumuapa Mwenyezi Mungu kwa haki za viumbe wake ni haramu."[212]

Jawabu Lake: Maana ya Ij-mai ni kuafikiana wanachuoni wa Kiislamu katika zama moja au zama zote juu ya hukmu fulani miongoni mwa hukmu za kisheria. Hii ndiyo Ij-mai, nayo ni hoja ya kisheria kwa Masunni kwa sababu kuafikiana kwa wanachuoni juu ya hukumu fulani ni hoja kwao na ni hoja ya kisheria kwa Mashia kwa kuwa inadhihirisha kuwafikiana na maoni ya Imam aliye Maasum ambaye huwa anaishi miongoni mwa watu, ima akawa haonekani machoni pao au akawa yu waonekana.

Sasa hivi hebu tuone je, Ij-mai ya wanachuoni ilithibiti kuharamisha mas-ala haya au hapana? Sisi kwa sasa tunayaacha kwanza maoni ya wanachuoni wa Kishia na yale ya wanachuoni wa Kisunni kuhusu mas-ala haya, na tunatosheka na kutaja fat-wa za Maimamu wa madh-hebu manne kisha tunajiuliza; je maimamu wa madh-hebu manne wanayofat-wa inayoharamisha jambo hili?

Iwapo walitoa fat-wa kuharamisha, basi tunachokitaraji ni watutajie Nassi ya fat-wa hiyo pamoja na kitabu ambacho fat-wa hiyo imo pia nambari ya ukurasa ilipo. Bila shaka vitabu vya Fiqhi na hadithi vya wanachuoni wa Kisunni havikulizungumzia kabisa jambo hili ili tuweze kuufahamu mtazamo wao katika qadhiya hii.

Kwa hiyo basi iko wapi hiyo Ij-mai na maafikiano anayoyadai mtunzi wa kitabu kiitwacho "Al-hadiyatus-saniyyah"?!!

Hapana shaka kwamba mtu pekee ambaye mtunzi huyu alinakili kutoka kwake uharamu wa jambo hili ni mtu "Maj-hul" asiyefahamika hali yake, asiye na utajo wowote anayeitwa "Al-izzu bin Abdis-salaam", basi je vitabu vyote vya wanachuoni wa Kiislamu vimo ndani ya maandiko yaliyomo katika kitabu kiitwacho Al-hadiyatus-saniyyah? Na je, wanachuoni wote wa Kiislamu wamo ndani ya huyu Al-izzu bin Abdus-salaam?

Ukweli ulivyo ni kwamba yeye mwenyewe mtunzi wa kitabu hiki "Al-hadiyyatus-saniyyah" amesema ndani ya kitabu hiki kwamba, Abu Hanifa na mwanafunzi wake aliyekuwa akiitwa Abu Yusuf wametoa fat-wa kwamba ni karaha kuapa kwa haki ya viumbe lakini hawakuharamisha.

Baada ya hapo, je ina nafasi gani fat-wa ya mtu fulani mbele ya hadithi sahihi zilizopokelewa toka kwa Mtume [s] na Maimamu watukufu toka katika kizazi cha Mtume [s] ambao wanachuoni wa Kisunni wamekubaliana kuwa (Maimamu hao ndiyo kile kizito kidogo baada ya Qur'an na maneno yao ni hoja ya kisheria).

Hadithi ya vizito viwili ni Mutawatiri toka kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] na wameitaja wana sihahi na sunan na wanahadithi na wanahistoria, na hawezi kuipinga isipokuwa mjinga na hadithi yenyewe ni hii: Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s]:

"Hakika ninakuachieni vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Kizazi changu watu wa nyumba yangu, ambavyo nikishikamana navyo hamtapotea baada yangu milele; na kwamba viwili hivyo havitaachana mpaka vinifikie kwenye haudh, basi angalieni ni vipi mtanifuata katika viwili hivyo."

Zaidi ya hapo maelezo aliyoyataja mtunzi huyo toka kwa Abu Hanifa hayakuthibiti. Kwa kifupi tunasema, "Hakuna dalili yoyote ile ya Ij-mai juu ya mas-ala haya moja kwa moja."

Dalili Ya Pili: Baada ya kuibatilisha dalili ya kwanza ya Mawahabi na kubainisha kutokusihi kwa dalili hiyo, sasa tunataja dalili yao ya pili nayo ni kauli ya mmoja wao anasema: "Kwa hakika kuomba kwa haki ya viumbe haifai, kwani viumbe hawana haki juu ya Muumba."[213]

Jawabu Lake: Bila shaka kutoa ushahidi kama huu ni ijtihadi dhidi "Nassi" iliyo wazi, basi lau viumbe wasingekuwa na haki yoyote katika dhimma ya Muumba mtukufu, ni kwa nini basi Nabii Adam [a] na Mtume Muhammad [s] walimuapa Mwenyezi Mungu kwa haki hizi (za viumbe) na walimuomba Mwenyezi Mungu kwa sababu ya haki hizi kama ilivyokuja katika hadithi zilizotangulia?!!

Zaidi ya hapo, wanasemaje watu hawa (Mawahabi) juu ya aya za Qur'an ambazo zinathibitisha haki za waja wema wa Mwenyezi Mungu juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu."[214]

Pia watasemaje jun ya hadithi tukufu zinazothibitisha haki hizo?

Soma aya zifuatazo:

  1. "Na ni haki juu yetu kuwanusuru wenye kuamini"
  2. Qur'an, 30:47.

  3. "Hii ndiyo ahadi na haki juu ya Mwenyezi Mungu ndani ya Taurati na Injili".
  4. Qur'an, 9:111.

  5. "Namna hii, ni haki juu yetu kuwaokoa walioamini".
  6. Qur'an, 10:103.

  7. "Kukubali toba ni juu ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wale wanaofanya uovu kwa ujinga".

Qur'an, 4:17.

Kwa kuongezea juu ya aya zilizotangulia kuna hadithi nyingi zinazohusu jambo hili, na hebu ona mifano ifuatayo:

1) "Ni haki juu ya Mwenyezi Mungu kumsaidia aliyeowa kwa kutaka kujizuwiya na mambo aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu".[215]

2) Mtume [s] amesema, "Watu wa aina tatu ni haki juu ya Mwenyezi Mungu kuwasaidia, mpiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu, na Mtumwa mwenye kutaka kujikomboa na mwenye kuoawa kwa kutaka kujizuwiya kutenda maovu".[216]

3) "Je, unafahamu ni ipi haki ya waja waliyonayo juu ya Mwenyezi Mungu"?[217]

Naam,.... inaeleweka wazi kwamba hakuna yeyote ambaye kwa dhati yake anayo haki juu ya Mwenyezi Mungu, hata kama atamuabudu Mwenyezi Mungu kwa muda wa karne nyingi hali ya kumkhofu na kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, kwani kila alichonacho mja, kimetoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hakuna alichokitoa mja yeye mwenyewe kwa nafsi yake katika njia ya Mwenyezi Mungu eti ili astahiki kwa dhati yake kupewa thawabu.

Basi tunauliza, nini maana ya "haki".

Jawabu: Hakika makusudio ya haki katika Ibara hizi, ni malipo, na daraja ambavyo Mwenyezi Mungu huwapa waja wake wanapomtii na kumfuata yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, na haya yote ni ziyada na ubora na umuhimu autoao Mwenyezi Mungu (kwa waja wake), na hii inaonyesha upole (huruma) na utukufu wake.

Basi haki hii ambayo kwayo tunamuapa Mwenyezi Mungu ni haki aliyoiweka yeye Mwenyezi Mungu juu yake siyo kwamba mja anayo haki juu ya Mwenyezi Mungu, na maana hii imeelekezwa katika baadhi ya hadithi tukufu za Mtume [s].

Na hii ni kama karadha anayowakopa Mwenyezi Mungu waja wake aliposema, "Nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu kopesho zuri."

Qur'an, 2:245.

Kwa hakika utendaji huu wa Mola na kutoa haki kwa waja wake unatokana na huruma yake Mwenyezi Mungu na uangalizi wake mkubwa kwa waja wake wema kiasi cha kujiona dhati yake tukufu kuwa ni yenye kudaiwa na waja wake na anawaona waja wake kuwa ndiyo wenye haki juu yake. Na ndani ya hali hii (iliyopo baina ya Mwenyezi Mungu na waja wake) inahamasisha na kutia nguvu ya kumtii Mwenyezi Mungu jambo ambalo liko wazi.

[204] As-sahifatul-alawiyya, uk. 370

[205] Al-sahifatul-alawiyya, uk. 51

[206] (1) Sunan Ibn Majah,Juz.1, uk 441(2) Mustad'rak sahihain, Juz. 1, Uk 313.(3)Musnad Ahmad Juz. 4, uk. 138 n.k

[207] (1) Sunan lbn Majah Juz. 1, uk. 261.(2) Musnad Ahmad Juz. 3, hadithi ya 21

[208] (1) Sunan Ibn Majah, Juz. 1, uk 441.(2) Mustadrak sahihain, Juz. 1, uk. 313 (3)Musnad Ahmad, Juz. 4, uk. 138 n.k.

[209] Al-fusulul-muhimmah, uk. 31 cha Ibn Sab-baagh al-Maliki aliyefariki mwaka 855 A.H.

[210] Al-Sahifatus Sajadiyah, dua ya 47

[211] Ziyaratu Aminil-lahi Al-maarufah

[212] Kashful-ir-tiyabi, uk. 32, imenakiliwa toka 'Al-hadiyyatus-saniyyah".

[213] Kashful-ir-tiyabi akinakili kwa al-Qaduuri.

[214] Mawahabi wanatumia rai zao na maoni yao kupinga aya za Qur'an na hadithi za Mtume [s].

[215] Al-Jamius-saghiru cha Suyutiyy, Juz. 2, uk. 33

[216] Sunan ibn Majah, Juz. 2, uk. 84

[217] An-nihayah cha Ibn Athir katika Maddah (Haq).