DALILI ZA MAWAHABI ZA KUHARAMISHA KUOMBA SHAFAA

Tumetaja ndani ya mlango uliopita dalili zinazoruhusu kuomba Shafaa, zikiwemo hadithi mbali mbali na aya za Qur'an.

Sasa hivi umefika wakati wa kutaja dalili za Mawahabi ambazo wanadai kwamba zinaharamisha Shafaa, zikiwemo hadithi mbali mbali na aya za Qur'an.

Huu ndiyo ule wakati muafaka wa kutaja zile dalili za Mawahabi ambazo wanadai kwamba zinaharamisha Shafaa na kuzijadili (ili Mwenyezi Mungu aithibitishe haki kwa maneno yake). Mawahabi wametolea ushahidi mambo kadhaa katika kuharamisha Shafaa, nasi tunayataja kama ifuatavyo:

1) WANASEMA: "KUOMBA SHAFAA NI
KUMSHIRIKISHA MWENYEZI MUNGU".

Wanachokikusudia Mawahabi katika shirki ni ile shirki ndani ya Ibada, kiasi wanadai kwamba kuomba kwa huyo anayeshufaiya ni kumuabudu.

Katika mlango uliopita tumeeleza kwa upana maana ya Ibada na tumetaja kwamba, ombi Ia mtu kuomba Shafaa litakuwa Ibada tu ikiwa litatolewa na muombaji haliya kuwa anaitakidi kuwa huyo mwenye kuombwa Shafaa ni Mola au ni Mungu au yeye ndiye asili ya kupatikana matendo ya Mwenyezi Mungu, na kwamba muombeaji huyo ndiyo msimamizi halisi wa mambo ya ulimwengu na anasimamia yote ambayo (kwa asili na ukweli) yanarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu (kuwa ndiyo muumba wa mambo hayo).

Hakika (ilivyo ni kwamba) mtu anayeomba Shafaa kwa waombeaji ambao Mwenyezi Mungu amewapa idhini ya kuombea, huwa anaitakidi kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu waliokaribu naye na ni watukufu na wenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hapana itikadi ya kuwa wao ni Miungu au eti wao ndio asili ya matendo ya Mwenyezi Mungu, na hakuna itikadi ya kuwa eti uombezi huo au msamaha wa Mwenyezi Mungu umetegemezewa kwao moja kwa moja bila ya kuhitajia idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hakuna kabisa itikadi za aina hiyo, kwani waombeaji hao wema huwa wanaombea kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kumuombea anayestahiki hiyo Shafaa na hii ni kwa sababu ya kuwepo maungamano yao ya kiroho ambayo hayakatiki.

Ukweli unaojitokeza ni kwamba, lau kama kuomba shafaa kwa mtu aliyekufa maana yake itakuwa ni kumuabudu, basi kuomba Shafaa kwa mtu aliye hai pia itakuwa ni kumuabudu.

Katika mlango uliotangulia tumetaja kwamba Qur'an inawataka Waislamu waende kwa Mtume [s] na wamuombe awaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu, hivyo basi ombi hili kwa Mtume [s] ni kuomba Shafaa katika zama za uhai wake na haiwezekani tendo hili la kumuomba Mtume Shafaa liwe ni shirki katika wakati fulani na wakati mwingine liwe ni tendo la tauhidi ya Mwenyezi Mungu. Kama ambavyo tumetaja pia katika mlango wa kuomba msaada kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kwamba, "Iwapo kuomba Shafaa kwa Walii mwema, hakutakuwa kwa kumuitakidia Uungu Walii huyo, basi Shafaa hiyo haitazingatiwa kuwa ni shiriki kabisa.

Kwa mfano Mwenyezi Mungu anasema: "Peke yako tu tunakuomba msaada".

Qur'an, 1:5.

Hapa ina maana kwamba msaada ni jambo linalomuhusu yeye Mwenyezi Mungu peke yake.

Baadaye Mwenyezi Mungu anasema: "Tafuteni msaada kwa kusubiri na kuswali".

Qur'an, 2:45.

Basi je mtu anaweza kusema kwamba kutafuta msaada kwa kusubiri ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu?

Moja kwa moja jibu lake ni hapana, kwani kutaka msaada kulikoharamishwa ni kule kutakakoambatanishwa na itikadi ya uungu wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, jambo ambalo hakuna anayeliamini miongoni mwa Waislamu.

2) WASHIRIKINA NA UOMBEZI WA MASANAMU

Baada ya kuibatilisha dalili ya kwanza ya Mawahabi inayoharamisha kuomba Shafaa kwa Mawalii, sasa ni wakati mwingine na kuibatilisha dalili ya pili ambayo ni: "Mwenyezi Mungu aliwazingatia wanaoabudu masanamu kuwa ni washirikina kwa kuwa wao walikuwa wakiomba Shafaa kwa masanamu yao, na walikuwa wakilia mbele ya masanamu hayo na kuyaomba uwakala kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Wanaabudu visivyokuwa Mwenyezi Mungu, vitu ambavyo haviwezi kuwadhuru wala kuwanufaisha, na (walipoulizwa kwa nini wanaviabudu) husema hawa ni waombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 10:18.

Na kwa msingi huu basi, kumuomba Shafaa asiyekuwa Mwenyezi Mungu kwa ujumla kutafahamika kuwa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ni kumuabudu muombezi huyo.

JAWABU LA MADAI HAYO

Kwanza:
Katika aya hii hakuna kabisa dalili yoyote iliyopo wanayoidhani Mawahabi kuwa inawaunga, kwani Qur'an kwa mujibu wa aya hii inapowaona watu hao kuwa ni washirikina siyo kwa ajili ya kuomba Shafaa kwa masanamu bali ni kwa sababu ya wao kuyaabudu Ibada ambayo imewapelekea wayaombe Shafaa vile vile. Na kama ingekuwa kile kiasi cha kutaka Shafaa kwa masanamu ni kuyaabudu jambo ambalo lingewajibisha shirki, kusingekuwa na haja yoyote kwa Mwenyezi Mungu kusema "na wanasema kuwa hawa ni waombezi wetu" bali kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo "Wanayaabudu" ingetosha kuwahusisha watu hao na ushirikina, lakini kuongezeka kwa sentensi ile ya pili baada ya ile ya kwanza ni dalili ya kwamba vitu hivyo viwili ni tofauti na pia kwamba maudhui ya kuabudia masanamu ni tofauti na maudhui ya kutaka Shafaa kwa hayo masanamu.

Kwa hakika kuyaabudu Masanamu ni dalili ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, ama kuomba Shafaa kwa jiwe au ubao ni dalili ya ujinga na kukosa akili, pia ni kutokuwa na busara.

Zaidi ya hapo aya hii tuliyoitaja hapo kabla haijulishi kwamba kutaka Shafaa kwa masanamu ni kuyaabudu, basi vipi itawezekana kuzingatia kuwa kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni dalili ya kuwaabudu Mawalii hao?

Kwa hiyo aya hii haina mafungamano kabisa na maudhui ya Shafaa.

Pili: Hebu tukadirie (kama mjadala) kwamba sababu ya shirki kwa watu hao waliotajwa ndani ya aya ni kule kuomba kwao Shafaa kwa masanamu, lakini ieleweke pia kwamba baina ya hao washirikina kuomba kwao Shafaa kwa masanamu na Waislamu kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, kuna tofauti kubwa na kuna utengano mfano wa masafa yaliyopo baina ya mbingu na ardhi, hasa kwa kuwa washirikina hao walikuwa wakiamini kuwa, masanamu hayo yanaimiliki hiyo Shafaa na msamaha kama kwamba Mwenyezi Mungu hahusiki kabisa katika mambo hayo mawili, na waliyaona hayo masanamu ndiyo yenye uamuzi wote wa kusamehe na kushufaiya.

Basi ukweli uko wazi kusema kwamba kuomba Shafaa kwa namna hii itakuwa ni kuyaabudu masanamu hayo kwa kuwa Shafaa hii imeambatanishwa na itikadi ya uungu kwa masanamu hayo na vile vile yenyewe kufanywa ndiyo chimbuko la matendo ambayo ni ya Mwenyezi Mungu katika hali ya kuendesha ulimwengu.

Kwa hiyo basi Mwislamu huwa anaomba Shafaa na dua kwa huyo mwenye kushufaiya hali ya kumuitakidi kwamba yeye ni mja aliyekurubishwa kwa Mwenyezi Mungu na ni mja mwenye heshima na utukufu aliyepewa ruhusa ya kuombea toka kwa Mwenyezi Mungu.

Ewe msomaji, hivi kudai kwamba hakuna tofauti baina ya Shafaa hizi mbili (iliyofanywa na washirikina kwa masanamu yao na ile ifanywayo na Waislamu kwa Mitume na Mawalii) ni kupingana na akili na mantiki na ni kuacha uadilifu? Je, huoni tofauti iliyopo kati ya mambo haya mawili kama unavyoweza kuona tofauti baina ya kiza Ia usika na mwangaza wa mchana?

3). KUTAKA HAJA KWA ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU NI HARAMU

Baada ya kuivunja dalili ya pili ya Mawahabi inayoharamisha kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, sasa inakuja dalili yao ya tutu. Nayo ni ile inayokataza kumuomba na kumtaka haja asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kudai kwamba kuomba Shafaa kwa Mawalii ni namna ya kutaka haja, basi jambo hili ni haramu kwani Qur'an inaeleza wazi wazi kama ifuatavyo:

Mwenyezi Mungu amesema, "Msimuombe yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 72:18.

Kuikusanya kauli inayoharamisha kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kauli inayothibitisha kupatikana uombezi wa Mawalii nikumuomba Mwenyezi Mungu awaamuru Mawalii wake wamuombee mwanadamu.

Na dalili ya kwamba kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni kumuabudu huyo anayeombwa ni kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Niombeni nitakubali maombi yenu, hakika wale wajivunao kufanya Ibada yangu wataingia Jahanamu wadhalilike."

Qur'an, 40:60.

Pindi tukiifanyia mazingatio aya hii tutaiona imeanza kwa tamko la 'Ad-dawat" kwa maana ya maombi, na imemalizikia kwa tamko la "Ibada". Basi hali hii inatuonyesha kwamba, Maf-humu ya maneno haya mawili ni moja.

Imepokewa kwa Mtume [s] amesema: "Dua ndiyo kiini cha Ibada".[201]

Jawabu Letu: Kwanza Tunasema: Siyo kweli kwamba makusudio ya kuharamisha kumuomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika aya iliyotajwa ni kuharamisha maombi kwa ujumla, lakini makusudio yaliyopo kwenye aya hiyo ni kuharamisha "kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu". Ushahidi wa jambo hili uko mwanzoni mwa aya aliposema Mwenyezi Mungu, "Na kwa hakika misikiti yote ni ya Mwenyezi Mungu basi msimuombe (msimuabudu) yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu". Kwa hiyo basi mkusanyiko uliomo katika aya unajulisha kwamba dua iliyoharamishwa ni ile inayochanganywa na Ibada na kuitakidi uungu wa huyo anayeombwa na pia kuitakidi uwezo wake wa kuamua katika mambo ya viumbe na ulimwengu.

Ukweli ulivyo ni kwamba, itikadi kama hii haipo miongoni mwa Waislamu ambao huomba Shafaa kwa mawalii wa Mwenyezi Mungu.

Pili: Kwa hakika kinachoharamishwa ndani ya aya hiyo nakukatazwa ni kumuabudu Mwenyezi Mungu pamoja na mwingine na kumfanya huyo kuwa yeye ni sawa na Mwenyezi Mungu katika dua (Ibada), kama inavyojulisha sentensi iliyoko kwenye aya isemayo "pamoja na Mwenyezi Mungu" yaani sawa naye.

Basi iko haja ifahamike kwamba, mtu anapomuomba Mtume [s]. anyenyekee kwa Mwenyezi Mungu kumuombea mtu huyo ili shida yake itatuliwe au asamehewe makosa yake haina maana kwamba mtu huyu atakuwa amemuomba (yaani amemuabudu) Mwenyezi Mungu pamoja na mwingine bali maombi haya ukweli wake ni kumuomba yeye Mwenyezi Mungu peke yake.

Na ikiwa ziko baadhi ya aya za Qur'an zinazofahamisha kuwa, kutaka haja kwa masanamu ni ushirikina, hiyo ni kwa sababu watu hao walikuwa wakiamini masanamu hayo kuwa ni Miungu wadogo wenye kumiliki kikamilifu maamuzi ya matendo ya Mwenyezi Mungu yote au sehemu yake, na ndiyo maana utaiona Qur'an inaikosoa fikra hii potofu.

Qur'an inasema: "Na wale muwaombao kinyume cha Mwenyezi Mungu hawawezi kukusaidieni wala kujisaidia wenyewe nafsi zao"- Qur'an, 7:197. Pia Qur'an inasema: "Bila shaka hao muwaombao kinyume cha Mwenyezi Mungu ni viumbe kama ninyi". Qur'an, 7:194.

Kwa kufupisha maelezo ni kwamba, washirikina walikuwa wakiamini kuwa masanamu hayo ni miungu wadogo na kwamba matendo ya Mwenyezi Mungu yameegemezwa kwao moja kwa moja, lakini kuomba Shafaa na dua kwa mtu ambaye Mwenyezi Mungu amempa cheo hiki na haki hii hatuamini kwamba wao ni Miungu wadogo au matendo ya Mwenyezi Mungu yameegezwa kwao, basi kuna tofauti kubwa baina ya itikadi ya washirikina na itikadi ya utukufu wa walii mwema na mwenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu na kutaka kwake msaada mbele ya Mwenyezi Mungu. Je, Mawahabi hawana uadilifu wala hawatazami vitu kama vilivyo? Je, hawana akili kabisa?

Tatu: Kwa hakika neno 'Ad-dawah" lina maana pana kiasi kwamba wakati mwingine hutumika kimajazi kwa maana ya "Ibada" kama ambavyo (Mawahabi) walivyolitolea ushahidi katika aya ya 60 sura ya 7 tuliokwisha itaja hapo kabla, na pia katika hadithi ambayo tumeitaja huko nyuma.

Lakini tunajua wazi kwamba matumizi haya ya kimajazi hayatoshi kuwa ni ushahidi wa kufasiri maana ya dua kuwa ni ibada kila wakati, au ushahidi wa madai kwamba kuomba haja kwa yeyote ni ushirikina.

4). SHAFAA NI HAKI INAYOMUHUSU MWENYEZI MUNGU TU

Ewe msomaji mpendwa, tumeibatilisha dalili ya tatu ya Mawahabi na sasa tunaitaja dalili yao ya nne ambayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Au ndiyo wamejifanyia waombezi mbele ya Mwenyezi Mungu, waambie: Ijapokuwa hawana mamlaka juu ya kitu chochote wala hawatambui lolote? Waambie uombezi wote uko katika milki ya Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 39:43-44.

Makusudio ya kutolea ushahidi aya hii, ni kubainisha kwamba Shafaa ni jambo linalomuhusu Mwenyezi Mungu tu, kwa hiyo basi kuna maana gani kutaka Shafaa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu?

Jawabu Lake: Mwenyezi Mungu aliposema kwamba "Uombezi wote uko katika milki ya Mwenyezi Mungu" siyo maana yake kwamba Shafaa ni jambo linalo muhusu yeye Mwenyezi Mungu na hakuna mwingine mwenye haki ya kuombea. Na hii ni kwa sababu, hapana shaka kabisa kwamba, Mwenyezi Mungu hamuombei mtu fulani kwa (Mola) mwingine, bali maana iliyokusudiwa hapo ni kuwa, yeye Mwenyezi Mungu ndiye mwenye asili ya mamlaka ya Shafaa wala siyo masanamu, na hiyo ni kwa kuwa muombezi (mwenye kushufaiya) ni lazima kwanza awe na akili na utambuzi, na aweze huko kuombea kwa upande wa pili, kitu ambacho masanamu yamekosa sifa hizi mbili:

Na kwa ajili hii Mwenyezi Mungu amesema:

Kwanza: "Waambie japokuwa hawana mamlaka juu ya kitu cho chote"?

Pili: "Wala hawatambui lolote?" Kwa hiyo aya inasisitiza kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiyo mwenye mamlaka ya Shafaa siyo masanamu, na pia kwamba Mwenyezi Mungu humpa jambo hili (la Shafaa) mtu ambaye zimetimia sifa zinazostahiki kuwaombea waja wa Mwenyezi Mungu.

Hivyo basi aya hii haina uhusiano na maudhui tunayoyazungumzia, hasa inapozingatiwa kwamba Waislamu wanaamini kuwa, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye mamlaka ya Shafaa na wala siyo Mawalii wake, kadhalika Waislamu wanaamini kwamba yeyote ambaye Mwenyezi Mungu amempa ruhusa ya kuombea, basi anao uwezo wa kuombea kinyume cha mtu ambaye hakupewa ruhusa hiyo.

Hali hii ya kushufaiya ndiyo ile ile ambayo Waislamu wanayoitakidi kwa kutegemea aya za Qur'an na hadithi kwamba, Mwenyezi Mungu amempa idhini Mtume [s] yeye na watu wa nyumba yake [a] ya kuombea, nasi kwa sababu hiyo basi tunaomba Shafaa yao.

Kwa hiyo Ewe msomaji imekudhihirikia kutokuwepo uhusiano baina ya aya hizo na uchunguzi huu na kutokuwepo uhusiano bania ya hadithi waliyoitaja na uchunguzi huu.

5). UPUUZI WA KUTAKA SHAFAA KWA MAITI

Dalili ya mwisho ya Mawahabi juu ya kuharamisha Shafaa kwa Mawalii inasema kwamba:

"Kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika maisha haya (ya duniani) ni sawa na kuomba haja kwa maiti asiyesikia".

Mawahabi wametolea ushahidi madai yao haya kwa aya mbili zifuatazo:

Kwanza: "Kwa hakika huwezi kuwasikilizisha wafu mwito - wala kuwasikilizisha viziwi wanapogeuka wanakwenda zao".

Qur'an, 27:80.

Makusudio ya kutolea ushahidi wa aya hii ni kwamba, Qur'an Tukufu imewafananisha washirikina na maiti na aya hii inamwambia Mtume [s] kwamba yeye hawezi kuwafahamisha washirikina hawa kwani wao nikama maiti hawasikii, kwa hiyo lau maiti wangekuwa wanao uwezo wa kusema na kusikia basi isingefaa washirikina kufananishwa na maiti.

Pili: "Bila shaka Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye na wewe huwezi kuwasikilizisha waliomo makaburini".

Qur'an, 35:22.

Kutolea ushahidi aya hii ni sawa na ushahidi uliotolewa katika aya iliyotangulia kwa kutokuwepo uwezekano kwa maiti kusikia na kusema.

Kwa hiyo basi kuwaomba (maiti) Shafaa ni kama kukiomba Shafaa kitu kisicho uhai, kama vile mawe n.k.

Jawabu Letu: Bila shaka Mawahabi wamelifanya suala la shirki kuwa ndiyo ngao yao kila wanapoyakosoa madhehebu mbali mbali ya Kiislamu na kuwatuhumu Waislamu kwa ukafiri nyuma ya pazia la kutetea Tauhidi ya Mwenyezi Mungu na kuihusisha kwake Ibada.

Lakini Mawahabi walipotolea ushahidi aya hizi wamebadilisha usulubu wao wakang'ang'ania usemi wao kuwa "kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni jambo la upuuzi wala halina faida, kwa kuwa Mawalii hao wamekwisha kufa".

Mawahabi hawa ambao Qur'an hawaifahamu vilivyo, wamejisahaulisha na kupuuza hata zile hoja za kiakili na sheria ambazo zinathibitisha kuwa hai kwa Mawalii hata baada ya kufa.

Wanafalsafa wa Kiislamu wamethibitisha kwamba, baada ya roho kujitenga na mwili na kutoutegemea, yenyewe hubakia milele na kuishi maisha yanayohusiana na roho na ufahamu wa kiroho.

Wanafalsafa wanaomuitakidi Mwenyezi Mungu wametaja dalili kumi za kiakili kuhusu jambo hili, kiasi kwamba hazikuacha nafasi ya mashaka na wasi wasi ndani yake kwa kila mtu muadilifu na mwenye akili. Zaidi ya hizo dalili za kiakili, Qur'an ambayo ni kitabu cha Mwenyezi Mungu imetangaza wazi wazi kuwepo kwa uhai baada ya kufa, pia ziko hadithi nyingi za Mtukufu Mtume [s] kuhusu jambo hili.

Ili kuthibitisha unaweza kurejea katika Qur'an aya zifuatazo:

1) Aya 169-170 Sura ya 3

2) " 41 " 4.

3) " 45 " 33.

4) " 100 " " 23.

5). " 46 " " 40.

Zote hizi zinathibitisha juu ya kuwepo uhai baada ya kifo. Basi ina hali gani hoja yenu dhaifu enyi Mawahabi? Na Je, zinamaanisha nini basi aya hizo mbili?

Jawabu Lake: Bila shaka aya hizo mbili zinamaanisha kwamba, miili iliyolala makaburini haina uwezo wowote wakufahamu kitu, jambo ambalo linakubalika moja kwa moja, kwani mwili unapotengana na roho kinachobakia ni kitu (kiwiliwili) kisicho na fahamu wala akili.

Lakini lazima ieleweke kwamba nukta muhimu tunayozungumzia hapa ni kwamba, wale ambao sisi tunawasemesha na kuwaomba Shafaa kama ambavyo Qur'an inasisitiza "siyo kiwiliwili kilichozikwa katika udongo bali ni roho takatifu zilizo hai ndani ya miili ya Bar-zakh katika ulimwengu wa Bar-zakh."

Hivyo basi, ilivyokuwa hakuna uwezekano wa miili iliyozikwa ardhini kufahamu cho chote, hali hii haimaanishi kwamba roho takatifu za miili hiyo ambazo ni hai na zinaruzukiwa huko kwenye ulimwengu wa Bar-zakh eti nazo haziwezi kufahamu kitu.

Na ifahamike pia kwamba, salamu, maamkizi na ziyara (zifanywazo na Waislamu kwa Mawalii) ni kwa ajili ya roho zenye nuru zinazobakia milele na ndizo zinazoombwa Shafaa.

Na pengine utajiuliza, ni kwa nini Waislamu wanayazuru Makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu?

Jawabu: Ni kwa sababu ya mambo yafuatayo:

1. Zimekuja hadithi mutawatiri za Mtukufu Mtume [s] zinazohimiza kuzuru makaburi ya Mawalii, na katika mstari wa mbele wa hao katika umuhimu, ni Mtume [s] na watu wa nyumba yake watakatifu (amani ya Mwenyezi Mungu iwashukie), na kuna thawabu nyingi na radhi za Mwenyezi Mungu katika ziyara za makaburi hayo, nasi hapo kabla tumetaja baadhi ya hadithi zilizohimiza kuhyazuru wakati tulipokuwa tukizungumzia kuhusu kumzuru Mtume [s].

2. Kuyazuru makaburi yao huwa kunaijenga hali ya kuwepo kwao (miongoni mwetu) na kuziandaa nafsi zetu kuwasiliana na roho zao tukufu, na hali zao za kiroho na wakati tunapowatolea salamu huwa tunajihisi kama kwamba tunaongea nao hali ya kuwa wanatusikiliza, kama ilivyokuja katika moja ya ziyara iliyowekwa na hao maasumin.

"Nashuhudia kwamba wewe unashuhudia kisimamo changu na unayasikia maneno yangu, na kwamba wewe ni hai mbele ya Mola wako unaruzukiwa, basi muombe Mola wako ambaye ndiye Mola wangu anikubalie haja yangu.[202]

Kadhalika yemekuja mapokezi yasemayo:

"Ewe Mwenyezi Mungu...Mimi nafahamu pia kwamba, Mtume wako na Makhalifa wako [a] wako hai mbele yako wanaruzukiwa, wanakiona kisimamo changu na wanasikia maneno yangu na wanajibu salamu yangu na wewe Mola wangu umeweka kizuwizi kwangu mimi kutoyasikia maneno yao (lakini) umefungua mlango wa fahamu zangu ili nipate utamu wa kuwazungumzisha".

3. Kuna hadithi tukufu chungu uzima zinazobainisha kwamba miili ya Manabii na Mawalii na wengineo pia hubakia katika udongo hali ya kuhifadhika bila ya kuharibika kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Jambo hili linayo masimulizi mengi na matukio mengi ambayo nafasi hairuhusu kuyaeleza.

Tunatosheka kuashiria tukio lililotajwa na wanahistoria kwamba, Waislamu walichimba mifereji ya maji katika ardhi ya Uhdi huko Madina, miaka hamsini baada ya tukio la vita vya Uhdi.

Walipokuwa wakichimba wakafukua miili iliyovuja damu ikiwa mizima kabisa kama kwamba imezikwa sasa hivi, kiasi hata sanda zake hazijaharibika.

Habari za tukio hili zilipofika mjini Madina, watu walitoka mbio wakiwemo Masahaba na wengineo hata kina mama pia walitoka kwenda kushuhudia na waliitambua miili ya maiti hao kwa majina yao na majina ya wazazi wao na kwamba miili hiyo ilikuwa ya mashahidi wa Uhdi.

Miili hiyo ilibakia katika hali ya usalama ikazishinda zama na mchanga (kutoiharibu) kwa idhini ya Mwenyezi Mungu muweza.

Ikiwa miili ya mashahidi hawa imeweza kubakia katika hali hii, basi vipi mwili wa Mtume [s] na Maimamu watukufu wa kizazi cha Mtume?

Hapana shaka miili yao itabakia katika hifadhi dhidi ya kila aina ya uharibufu hasa kwa kuwa miili hiyo inao utukufu mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Vile vile sehemu ambayo umezikwa mwili wa mmoja wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, inapata utukufu kwa ajili ya Walii huyo, hivyo basi kufika mahali hapo patukufu huwa panamsababishia mtu kupata rehma na baraka za Mwenyezi Mungu.

Mpaka hapa ewe msomaji, imekudhihirikia kwamba, dalili wazitumiazo Mawahabi kuharamisha kuomba Shafaa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni dalili dhaifu, na ukweli ni ule ambao Waislamu wanautenda kwa kufuata Qur'an na hadithi tukufu za Mtume [s].

[201] Safinatul-bihar mada inayohusu dua.

[202] Kitabu Ud-datid-daai, cha Ibn Fahd AI-hilli, imepokewa toka kwa Imam Jaafar As-Saadiq [a].