TAUHIDI KATIKA IBADA

Msingi wa wito wa Manabii [a] siku zote umekuwa ni kulingania kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake na siyo kumuabudu mwingine peke yake, au kumshirikisha na Mwenyezi Mungu. Na msingi wa hukmu za mbinguni tangu mwanzo wa kutumwa ujumbe wa Manabii ilikuwa ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kukata mizizi ya shirki.

Ukweli halisi ulivyo ni kwamba, lengo la kutumwa kwa Manabii ni kulingania (watu) kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake, na kupiga vita ushirikina wa aina zote na khususan kupinga shirki katika ibada.

Qur'an Tukufu inaashiria ukweli huu wazi wazi na inasema:

"Na bila shaka tulimpeleka Mjumbe kwa kila umma (akawambie umma wake) muabuduni Mwenyezi Mungu na muyaepuke masanamu.

Qur'an, 16:36

Na hatukumtuma kabla yako Mjumbe yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hakuna apasiwaye kuabudiwa ila mimi, basi niabuduni."

Qur'an, 21:25

Qur'an imeizingatia ibada ya Mwenyezi Mungu kuwa ni jambo linalokusanya na kushirikisha sheria zote za mbinguni na inasema:

"Waambie, Enyi mliopewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu njooni katika neno lililo sawa baina yetu na baina yenu, ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu na wala tusimshirikishe na chochote."

Qur 'an, 3:64

Tauhidi katika ibada ni msingi imara kwa Waislamu wote, na hapana yeyote aipingaye Tauhidi au kuwa na tofauti ndani yake miongoni mwa vikundi vyote vya Kiislamu, ijapokuwa Mutazilah mtazamo wao juu ya Tauhid ya matendo ya Mwenyezi Mungu unatofauti, na vile vile Ashaira nao wanayo tofauti juu ya Tauhid katika sifa za Mwenyezi Mungu, lakini madhehebu zote za Kiislamu zinaafikiana kuhusu Tauhid ndani ya ibada na hakuna nafasi ya kupinga hilo.

Kama kutakuwa na khitilafu, basi ikhtilafu hiyo haiko katika msingi wa Tauhidi ya ibada bali iko katika Misdaaq za Tauhidi ya Ibada.

Hii inamaanisha kwamba, baadhi ya Waislamu wanaona kuwa baadhi ya matendo ni ibada na Waislamu wengine wanaona kuwa (matendo hayo) ni Takrima na Taadhima tu na siyo ibada.

Na kwa mujibu wa Istilahi ya Elimu ya "Mantik" Tofauti kama hii iko ndani ya 'As-Sughraa" ambayo ni Je, kitendo hiki ni ibada au hapana? Wakati ambapo hakuna tofauti katika 'Al-Kubraa" ambayo ni je, inafaa kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu au hapana? Na hii wameafikiana (Waislamu wote) kwamba haijuzu kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Kwa maneno mengine (Tunaweza kusema) tofauti iliyopo inatokana na Mawahabi kuyazingatia matendo fulani kuwa ni ibada wakati ambapo wasiokuwa wao miongoni mwa Waislamu ulimwenguni kote hawayazingatii kamwe matendo hayo kuwa ni ibada.

Hapana budi tuifafanue maana ya "Ibada" kwa mujibu wa lugha na vile vile kwa mjibu wa Qur'an, na hapo ndipo yatakapofahamika matawi ambayo ndani yake imekuja tofauti kuyahusu mwenyewe kwa dhati yake, na ndipo utakapotudhihirikia uhakika na ukweli wa ibada.

TAARIFU KAMILI YA MAANA YA IBADA

Bila shaka maana na Maf-humu ya Ibada iko wazi katika lugha ya Kiarabu, na lau tutakwa hatuwezi kuiarifisha "Ibada" kwa Taarifu ya kimantik kwa kutumia neon moja, basi ni kama mbingu na ardhi ambazo zina maana mbili zilizowazi, wakati ambapo wengi katika sisi hawawezi kutoa taarifu kamili kwa kutumia neon moja lakini hali hii haizuwii kujengeka maana ya ardhi na mbingu katika akili zetu tunapoyasikia matamko hayo.

Bila shaka basi, maana ya Ibada ni kama maana ya ardhi na mbingu ambayo inafahamika kwetu sote, pamoja na kutokuweza kuziarifisha mbingu na ardhi kwa taarifu ya kimantiki:

Kwa hiyo basi "Ibada" na "Kutukuza" na "Kuheshimu" na "Kukirimu" ni matamko mbali mbali yenye matawi yanayofahamika, na kuyachambua ni jambo rahisi tena jepesi.

Kwa hakika mtu ambaye anampenda yeyote yule kwa mapenzi ya kweli kabisa, utamuona akibusu kutaza nyumba ya mpenzi wake na kunusa mavazi yake na kuyakumbatia kifuani, na atapokufa (mpenzi wake huyu) atalibusu kaburi lake na udongo wa kaburi hilo....

Pamoja na matendo yote haya, hapana yeyote atakayeona kuwa matendo yake huyu mwenye kupenda ni ibada amfanyiayo yule mpenzi wake.

Hali hii ni kama ile ya watu kukimbilia kwena kuona miili ya viongozi iliyomo ndani ya majeneza, au kuona kumbukumbu zao na majumba walioyokuwa wakiishi na kusimama dakika chache kuonyesha huzuni kwa ajili ya rohozao yote haya hayazingatiwi kuwa ni ibada katika Taifa lolote miongoni mwa mataifa ulimwenguni, japokuwa mapenzi yao na unyenyekevu wao kwa wato hao uko katika kiwango cha unyenyekevu wa waumini kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Hivyo basi, watu wenye maarifa na wachambuzi wa mambo ndiyo ambao wanaweza kupambanua baina ya kuheshimu na ibada.

Ewe msomaji mtukufu iwapo tutataka kutoa taarifu ya ibada kimantik, basi ibada itakuwa na taarifu za aina tatu na zote hizi zitalenga maana moja.

Ama Mawahabi wao wamechagua Taarifu mbili nyingine na wakazitegemea, lakini zinaupungufu hazikukamilika. Katika maelezo yafuatayo tunazileta hizo Taarifu zao ili tuzijadili.

TAARIFU MBILI PUNGUFU KUHUSU IBADA

Ibada ni kunyenyekea na kudhalilika.

Ndani ya vitabu vya lugha Taarifu ya ibada imekuja kwa maana ya kunyenyekea na kudhalilika. Na maana hii imekuja katika Qur'an tukufu lakini Taarifu hii ya Ibada haitoi maana ya ibada kwa undani, na hiyo ni kwa sababu zifuatazo:

Ikiwa ibada inakubaliana katika maana na kuwa ni kunyenyekea na kudhalilika, basi haitawezekana kwa mtu yeyote kumzingatia kuwa anampwekesha Mwenyezi Mungu, kwani mtu kwa maumbile yake humnyenyekea Mwalimu wake na mtoto naye huwanyenyekea wazazi wake wawili na kila mpenzi kwa ampendaye.

Bila shaka Qur'an Takufu inamuamuru mtu adhalilike kwa wazazi wawili inasema:

"Na wainamishie Bawa Ia udhalili kwa kuwaonea huruma na useme, Mola wangu wahurumie (wazazi) wangu kama walivyonihurumia mimi nilipokuwa mdogo".

Qur'an, 17:24

Basi iwapo unyenyekevu na udhalili maana yake ni kumfanyia ibada uliyemdhalilikia, basi italazimu kumhukumu ukafiri yeyote anayelea wazazi wake wawili na kinyume chake itakuwa ni lazima kumhukumu kuwa ni mtu wa Tauhidi yule anayewatelekeza wazazi wake na kutowafanyia wema.

B: Ibada ni ukomo wa kunyenyekea. Baadhi ya wafasiri walijaribu kuitengeneza na kuirekesbisha Taarifu ya ibada ya kilugha pale walipogundua kuwa inaupungufu wakasema:

"Ibada ni ukomo wa kunyenyekea kwa yule ambaye utukufu wake na ukamilifu wake unafahamika."

Taarifu hii inashirikiana na ile ya kwanza katika upungufu na utata.

Mwenyezi Mungu anawaamuru Malaika wamsujudie Adam anasema:

"Na kumbuka tulipowaambia Malaika, msujudieni Adam, wakasujudu wote isipokuwa Iblisi".

Qur'an, 2:34

Bila shaka kusujudu ndiyo ukomo wa kadhalilika na kunyenyekea kwa yule unayemsujudia, basi ikiwa maana ya ibada ni ukomo wa kunyenyekea italazimu kuwakufurisha Malaika waliotekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, na Iblisi kwa kupinga kwake amri ya Mwenyezi Mungu atakuwa ndiyo mwenye imani.

Hakika ndugu wa Nabii Yusuf na wazazi wake Nabii Yusuf wote walimsujudia Yusuf kama asemavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Na waliporomoka wote kumsujudia, (Naye Yusuf) akasema: Ewe Baba yangu hii ndiyo Tafsiri ya ndoto yangu ya zamani bila shaka Mwenyezi Mungu ameithibitisha".

Qur'an, 12:100

Ndoto aliyoiashiria Nabii Yusuf katika Aya hii, hi ile iliyoko katika kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

"(Kumbuka) Yusuf aliopomwambia Baba yake, Ewe baba yangu hakika nimeona (ndotoni) nyota kumi na moja na jua na mwezi vinanisujudia"

Qur'an, 12:4

Ni hakika (isiyopingika) kwamba Waislamu wote kwa kufuata mwendo wa Mtume [s] huwa wanalibusu "Hajarul-As-wad". Jiwe jensi lililoko kwenye kona ya Kaaba Tukufu na pia hutaka baraka kwenye jiwe hilo.

Kitendo kile kile hufanywa na waabuduo sanamu kwenye masanamu yao jambo ambalo moja kwa moja ni shirki, lakini tendo la Waislamu kwenye Hajarul-As-wad ni tendo la Tauhidi bila shaka yoyote.

Kwa hiyo, maana ya ibada siyo ukomo wa kunyenyekea na kudhalilika ingawaje (kunyenyekea na kudhalilika) hakika ni miongoni mwa nguzo za Ibada lakini siyo kwamba hizo ndiyo nguzo pekee za ibada. Hivyo basi, hapana budi pasemwe kuwa, Ibada maana yake ni kunyenyekea na kudhalilika kunakoambatanishwa na itikadi maalum, kitu ambacho kitaifanya ibada iwe imeundika katika misingi miwili.

1. Kunyenyekea na kudhalilika.

2. Itikadi maalum.

Na hii itikadi maalum ndiyo ambayo inaweka msimamo wa kufafanua Qadhiya ya ibada, kwani kunyenyekea japo si sana, ikiwa kutaambatanishwa na itikadi maalum, basi itakuwa ibada.

Kwa hakika "Itikadi Maalum" ndiyo inayokivalisha kitendo vazi Ia Ibada, na bila itikadi hiyo maalum ibada haithibitiki japo itadhihirika katika hali ya Ibada.

Na sasa baada ya kuwa tumethibitisha ubatili wa Taarifu mbili ambazo Mawahabi wamezitegemea, na umedhihiri upungufu wake na udhaifu wake, umefika wakati wa kuzungumzia zile Taarifu tatu.

Sasa suali ni je, ni nini hiyo "Itikadi maalum" ambayo inaitenganisha ibada na visivyokuwa ibada?

Jawabu lake: Kwa hakika ukweli na usahihi, hapa ndipo mahali pa uchambuzi na uhakiki, na jawabu lake litaonekana ndani ya Taarifu tatu zifuatazo:

Taarifu ya Kwanza: Ibada ni kunyenyekea kimatendo au kimatamko, ambako kunatoka ndani ya itikadi ya mtu kwa ajili ya Uluhiyyah (Uungu).

Nini maana ya Uluhiyyah nukta hii ni muhimu sana kwa hiyo ni lazima kuieleza.

Jibu: "Uluhiyyah" ni tamko litakanalo na neno "Al-Ilahu" na hilo neno "Al-Ilahu" ndiyo Allah kwa tamko la nakira, (naye ndiyo muumba mtukufu).

Na ilivyokuwa neno "Al-llahu" hupata likafasiriwa kwa maana ya mwenye kuabudiwa, basi tafsiri hiyo hiyo ni tafsiri ya kulazimiana, yaani Uluhiyyah unalazimu kuabudiwa siyo kwamba Ilahu maana yake ni mwenye kuabudiwa.

Bila shaka watu wanaoitakidi Ilahu vile vile wanaitakidi kuwepo ulazima wa kumuabudia, sawa sawa ikiwa ni Ilahu wa haki kama alivyo Mwenyezi Mungu au akawa siyo wa haki kama illvyo miungu isiyokuwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo neno Al-Ilahu hufasiriwa kwa maana ya chenye kuabudiwa kutokana na hali hii tu basi.

Dalili iliyowazi kuhusu taarifu hii ni Aya za Qur'an zilizokuja kuzungumzia nyanja hii.

Katika mazingatio ndani ya aya hizo inatudhihirikia kwamba "Ibada" na matendo na maneno yanayotokana na Itikadi za Uungu, na kwamba Itikadi hii inapokosekana, basi maana ya Ibada haithibitiki, na ndiyo maana utaiona Qur'an wakati inapoamuru ibada ya Mwenyezi Mungu, basi haraka sana hutoa maelekezo kwamba, hapana mungu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Kwa mfano isema:

"Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu ninyi hamna Mungu ila yeye."

Madhumuni ya aya hii yamekuja katika sehemu tisa ndani ya Qur'an au zaidi, nawe msomaji mpendwa unaweza kuzirjea aya hizi katika Surat A'araf aya ya 65, 73 na 58. Pia Surat Huud aya ya 5, 61 na 84, vile vile Surat Anbiyyah aya ya 25, kadhalika Surat Muuminnuna aya ya 23 na 32 na Surat Taha aya ya 14.

Ibada zote hizi zinajulisha kwamba, ibada ni kule kunyenyekea na kudhalilika kunakotokana na itikadi ya kuitakidi Uluhiyyah na bila itikadi hii tendo hilo halitaitwa Ibada.

Hebu angalia aya zaidi zinazojulisha makusudio hayo.

Anasema Mwenyezi Mungu:

"Hakika wao walipokuwa wakiambiwa, hapana Mungu (Mwingine) ila Mwenyezi Mungu wao Hupinga."

Qur'an, As-Safaat:35

Ni kwa nini walikuwa wakipinga? Ni kwa sababu wanaitakidi waungu wasio Mwenyezi Mungu na wanawaabudu.

Na anasema Mwenyezi Mungu:

"Au wanaye Mungu mwingine asiye Mwenyezi Mungu, ametakasika Mwenyezi Mungu kutokana na hao washirikina hao wanaowashirikisha."

Qur'an, 52:43

Qur'an inawazingatia watu hawa kuwa ni washirikina kwa kuwa wanaitakidi uungu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Anasema tena Mwenyezi Mungu: "Wale ambao wanafanya pamoja na Mwenyezi Mungu; Mungu Mwingine basi hivi karibuni watajua."

Qur'an , 15:96

"Na wale ambao hawamuombi mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu .....

Qur'an, 25:68

Na miongoni mwa aya zinazojulisha kwamba maombi ya Washirikina yalikuwa yakiambatana na itikadi ya uungu kwa masanamu yao ni hizi zifuatazo:

"Waliwafanya waungu wengine badala ya Mwenyezi Mungu ili wawe wenye nguvu."

Qur'an, 19:81

"Je, ninyi mnashuhudia kwamba kuna waungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu."

Qur'an, 6:19

"Na (kumbukeni) Ibrahimu alipomwambia Baba yake Azar. 'Unawafanya Masanamu kuwa ni waungu.'"

Qur'an, 6:74

Mazingatio katika aya zinazozungumzia shirki yawatu wanaoabudu sanamu yatatudhihirishia ukweli huu, nao ni kuwa ushirikina wa watu hawa umekuja kwa sababu ya kuitakidi kwao uungu wa masanamu yao waliyokuwa wakiyaabudu, na kwamba masanamu hayo ni miungu wadogo ambao Mungu mkubwa amewapa baadhi ya mambo yanayomstahiki, basi (masanamu hayo) yameumbwa na wakati huo huo yanaabudiwa. Na kwa ajili hii basi walikuwa wakiikataa Tauhidi.

Qur'an inasema: "Hii ni kwa sababu mlikuwa akitajwa Mwenyezi Mungu peke yake mnakanusha, na akishirikishwa mnaamini, basi (leo) hukumu ni yake Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye mkuu."

Qur'an, 40:12

Na kwa ajili hii mfasiri mkubwa mar-hum Ayatullah Sheikh Muhammad Jawad Al-Balaghi ametoa Taarifu nzuri ya "Ibada" katika tafsiri yake madhubuti iitwayo Aalaur-Rahman anasema:

"Ibada: Ni hisia ya unyenyekevu wanayoifanya kwa ajili ya yule wanayemfikiria kuwa ni Mungu wake ili atimize haki yake makususi ya uungu.[167]

Bila shaka marehemu Al-Balaghi ametoa mtazamo wake wa kielimu kutokana na ufahamu wa kimaumbile juu ya neno "Ibada" katika msingi wa tamko, ndipo ilipokuja Taarifu hii inayokubaliana na aya za Qur'an.

Taarifu ya Pili ya Ibada: Hakika Ibada ni kunyenyekea mbele ya yule ambaye (Mwenye kunyenyekea) humzingatia kuwa ndiyo Rabbi (Mola).

Na tunaweza kuiarifisha ibada kama ifuatavyo; Ibada ni kunyenyekea kimatendo au kimaneno kwa yule anayeitakidiwa kuwa Mola basi kuabudiwa kunalazimiana na kuwa Mola na ikiwa mtu atajiona yeye mwenyewe kuwa ni mja kwa yule anayemuitakidi kuwa ni Mola wake kwa kuumba; sawa sawa Mola huyo akiwa ni kwa hakika au hapana, na akamnyenyekea pamoja na itikadi hii basi atakuwa amemuabudia.

Na katika Qur'an Tukufu kuna aya zinazofahamisha kuwa ibada ni miongoni mwa mambo ya umola yaani "Ar-rububiyyah".

Hebu ziangalie baadhi ya hizo aya:

"Naye Masihi alisema, Enyi wana wa Israeli, mwabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu".

Qur'an, 5:72

"Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na ni Mola wenu. Basi muabuduni hii ndiyo njia iliyonyooka"

Qur'an 3.51

Na aya nyinginezo zaidi ya hizi. Na kuna aya nyingine zinazoizingatia Ibada kuwa ni miongoni mwa mambo ya muumba kama ilivyo katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema:

"Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu, hakuna anayeabudiwa kwa haki ila yeye muumba wa kila kitu, basi muabuduni."

Qur'an 6:102

Ni maana ya neno (Ar-Rabbu)? Neno Rabbu hutumika katika lugha ya Kiarabu kwa yule aliyetegemezewa uangalizi wa kitu fulani na yakaachwa mikononi mwake matokeo au ukomo wa kitu hicho.

Basi iwapo neno hili litatumika kwa mtu anayemiliki nyumba na au anayemiliki ngamia au mlezi wa mtoto na mkulima na wengineo, basi hiyo ni kwa sababu wanamiliki kuendesha kitu hicho na kusimamia majukumu yake.

Nasi tunapomzingatia Mwenyezi Mungu kuwa ni "Ar- Rabbu" ni kwa sababu mambo yetu na mwisho wetu kama vile mauti, uhai, rizki, afya na uwekaji wa sheria pia msamaha na mambo mengineyo, yote yako mikononi mwake Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Sasa basi Iau kuna mtu ataitakidi kwamba, moja katika mambo haya au yote, Mwenyezi Mungu amempa mtu fulani (Ayasimamie), basi maana ya itikadi hii ni kwamba kumzingatia huyo mtu kuwa ni "Rabbu" na kumuamini Rabbi huyu na kumnyenyekea itakuwa ni kumuabudia.

Kwa maneno mengine tunasema, "Bila shaka ibada inatokana na hisiya za mtu kujiona kuwa yeye ni mja (mtumwa) na hii ndiyo hakika ya ubudiyah, ni ni mtu kuizingatia nafsi yake kuwa amemilikiwa na yuko juu yake aliyemmiliki, kuwepo kwake na kifo chake na uhai na rizki yake na mengineyo.

Au kwa uchache akamfanya huyo aliye juu yake kuwa ni mwenye kumiliki uwezo wa kusamehe:

(1) Mwenyezi Mungu Anasema: Nani anayesamehe madhambi isipokuwa ni Mwenyezi Mungu; 3:135

(2) Mwenyezi Mungu Anasema: Waambie Shafaa ni ya Mwenyezi Mungu; Az-zumar: 44

(3) Mwenyezi Mungu Anasema: Waliwafanya Makasisi wao na watawa wao kuwa ni Mola badala ya Mwenyezi Mungu, 9:31

Na Shafaa, na kumuwekea Kanuni (za maisha yake) na wajibu mwingineo, basi kwa ajili hiyo atakuwa amemfanya kuwa ni "RABBU" mlezi wake.

Kwa hiyo yeyote ambaye atakayeamini na kuitakidi katika nafsi yake (kama tulivyoeleza hapo kabla) na akaifasiri itikadi hiyo kwa maneno na matendo, basi hapana shaka kwamba anamuabudu huyo aliyemzingatia kuwa ni "Rabbu".

TAARIFU YA TATU YA IBADA

Hapa tunaweza kutoa Taarifu hii ya tatu ya ibada inayopatikana kutokana na maumbile na nguvu ya nafsi.

Tunasema: "Ibada ni kumnyenyekea yule ambaye tunamzingatia kuwa Mungu na ndiyo asili ya matendo ya kiungu".

Hapana shaka kwamba matendo ambayo yanahusiana na ulimwengu, kama vile kusimamia uendeshaji wa ulimwengu na kuhuisha na kufisha na kugawa rizki baina ya viumbe na kusamehe madhambi yote haya yanamuhusu Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Nawe (msomaji) lau utazizingatia vyema aya za Qur'an zinazozungumzia maelezo tuliyotangulia kuyataja, katika Aya ya 35 Surat Al- Qasa, Aya ya 60 mpaka Aya ya 64 Surat An-Namli Aya ya 5 na ya 6 Sura Az-Zummar. Utaona kwamba Qur'an inasisitiza kwa nguvu sana kuwa matendo haya yanamuhusu Mwenyezi Mungu tu na wala hayamuhusu mwingine asiyekuwa yeye.

Hii ni kwa upande mmoja, ama kwa upande wa pili:

Sote tunafahamu kwamba ulimwengu wa viumbe ni ulimwengu uliopangwa vyema kabisa, na hakiwezi kutokea kitu isipokuwa sababu ya kutokea kwake itarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Qur'an Tukufu inaonyesha (ukweli) wa jambo hili.

Mwenyezi Mungu anasema: "Na ni yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye anayehuisha na kufisha, na mabadiliko ya usiku na mchana yamo katika milki yake."

Qur'an, 23:80

Katika mahala pengine Mwenyezi Mungu anasema kwamba miongoni mwa Malaika wapo wanaosimamia utoaji wa Roho.

Nayo ni kauli yake isemayo: "Hata pale mmoja wenu anapofikiwa na mauti wajumbe wetu humfisha."

Qur'an, 6:61

Kwa kuijengea hali hii, inawezekana kuzikusanya aya hizi mbili na tukasema kama ifuatavyo:

"Bila shaka hizi sababu zinazosababisha pia matendo ya ulimwenguni, kama yatakuwa ni ya kimaumbile ya kawaida au kimaana kama vile Malaika, basi iwe iwavyo yanathibitika kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu naye ndiye mtendaji halisi."

Kwa maneno mengine ni kwamba, kitendo cha watendaji hawa wawili (Mwenyezi Mungu na Malaika) ni kitendo kimoja tu na si vitendo viwili lakini mtendaji wa kwanza anafanya kwa uwe wake na yule wa pili anamfuatia yule wa kwanza (kutekeleza maamrisho yake).

Maana hii ni miongoni mwa maarifa ya juu katika Qur'an ambayo hufahamika kwa kuzirejea aya za Qur'an zinazozungumzia matendo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Sasa basi ikiwa mtu ataitakidi kwamba Mwenyezi Mungu amewapa baadhi ya viumbe wake kama vile, Malaika na Mawalii matendo yake ya kuruzuku, na kuhuisha na yasiyokuwa hayo, na akaammi pia kuwa viumbe hao ndiyo wanaoendesha mambo ya ulimwengu na kuyasimamia mambo yake na akaona kuwa Mwenyezi Mungu hahusiki tena kwenye matendo hayo kiasi kwamba itikadi hiyo ikampelekea kuwanyenyekea viumbe hawa, basi hapana shaka yoyote kwamba unyenyekevu wake huu ni ibada na tendo hili ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa maneno mengine tunasema:

"Lau mtu ataitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ameukabidhi ustahiki wa kutekeleza matendo kwa Malaika na Mawalii, na Mwenyezi Mungu akawa amebaki hana ustahiki wote wote (katika matendo hayo) na hao Malaika na Mawalii wanayafanya matendo hayo bila kumtegemea Mwenyezi Mungu na bila idhini yake, basi mtu huyu aliyeitakidi itikadi hii, hakika amemfanyia Mwenyezi Mungu mshirika na amemfananisha (Na viumbe vyake).

Hapana shaka kwamba itikadi kama hii ndiyo kuishirikisha dhati ya Mwenyezi Mungu na kutawas-sal na kunyenyekea kunakotokana na itikadi hii ni ibada kama ilivyokuja katika Qur'an Tukufu.

Anasema Mwenyezi Mungu:

"Na miongoni mwa watu wako wanaofanya waungu badala ya Mwenyezi Mungu, na wanawapenda kama (anavyostahiki) kupendwa Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 2:165

Kwa hakika chochote chenye kuwa na kuwepo hakiwezi kuwa mfano wa Mwenyezi Mungu au mshiriki isipokuwa kitakapokuwa na uwezo wa kuuendesha ulimwengu kwa matakwa yake binafsi bila ya matakwa ya Mwenyezi Mungu lakini hakuna yeyote mwenye uweza huo. Bali kila kilichopo ni chenye kunyenyekea mbele ya matakwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kitake au kisitake basi kwa hiyo hakiwezi kuwa mshirika wa Mwenyezi Mungu bali kitakuwa kitiifu kwake kutenda kama atakavyo yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ukweli halisi in kuwa, washirikina walikuwa wakiitakidi kwamba, masanamu yao waliyokuwa wakiyaabudu yanajitegemea katika kunendesha ulimwengu huu na pia katika mambo ya uungu.

Na katika zama za Jahiliya (kabla kuja Uislamu) kulikuwa na ushirikina wa namna mbali mbali na ushirikina wa daraja ya chini kabisa ilikuwa ni itikadi ya Mayahudi na Wakristo kwamba mapadri na Makasisi wao wanayo madaraka ya uwekaji wa kanuni na sheria kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Waliwafanya wanachuoni wao na watawa wao kuwa ni waungu wao kinyume cha Mwenyezi Mungu".

Qur 'an, 2:31

Kadhalika washirikina walikuwa wakiitakidi kwamba, ustahiki wa Shafaa na Maghfira (mambo ambayo yanamstahiki Mwenyezi Mungu tu) vimekabidhiwa kwa Masanamu yao wanayoyaabudu, na masanamu hayo yanafanya mambo hayo yenyewe kikamilifu kwa kujitegemea katika ustahiki huo.

Na kwa ajili hii utaona aya nyingi za Qur'an zinazozungumzia Shafaa zinasisitiza kwamba Shafaa haithibitiki ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu asemavyo ndani ya Qur'an:

"Na ni nani huyo awezaye kushufaiya (kuombea) mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa idhini yake."

Qur 'an, 2:255

Na lau washirikina wangekuwa wanaitakidi kwamba, masanamu yao waliyokuwa wakiyaabudu yanauwezo wa kushufaiya kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, basi usingeona Qur'an inakanusha moja kwa moja Shafaa bila ya idhini ya Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya wanafalsafa wa Kiyunani walikuwa wamejenga ndani ya fikra zao Miungu wengi kwa kila jambo miongoni mwa mambo ya ulimwenguni. (Kwa mfano) mvua ina Mungu wake, mimea ina mungu wake, mtu ana Mungu wake na mambo mengine (kila moja lina mungu wake).

Na walikuwa wakidai kwamba utendaji wa kuendesha mambo ya ulimwengu ambao unamuhusu Mwenyezi Mungu peke yake, umekabidhiwa kwa miungu hawa.

Na katika zama za Jahiliya, baadhi ya Waarabu walikuwa wakiabudu Malaika na nyota zitembeazo na zile zisizotembea hali ya kuwa wakidhani kwamba usimamizi wa mambo ya ulimwengu na watu umekabidhiwa kwa vitu hivyo, navyo ndivyo vinavyotenda kikamilifu kwa kujitegemea na hiyari kamili, na kuwa Mwenyezi Mungu ameuzuliwa na hana uwezo wowote juu ya mambo haya kabisa (ametakasika Mwenyezi Mungu na fikra hizi sana sana).[168]

Na kwa hiyo basi kila aina ya unyenyekevu utaofanywa kwa Malaika na nyota utazingatiwa kuwa ni ibada kwa kuwa unatokana na itikadi hii yenye makosa.

Kuna baadhi ya Waarabu wengine wa zama za Jahiliyyah, hawakuyaitakidi masanamu yaliyochongwa kwa miti na madini kuwa ni Miungu na kwamba ndiyo yaliyowaumba wala kusimamia mambo ya ulimwengu na watu, bali wao walikuwa wakiyaamini kuwa yanao uwezo wa kuwaombea na walikuwa wakisema: "Masanamu haya ni waombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu".[169]

Na kwa msingi wa mtazamo huu batili, walikuwa wakiyaabudu Masanamu haya kwa lengo la kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na walikuwa wakisema wamasema:

"Sisi hatuyaabudu (Masanamu) isipokuwa kwa ajili ya kutukurubisha kwa Mwenyezi Mungu."

Qur 'an, 39:3

Kwa kifupi tunasema: "Bila shaka tendo lolote litokanalo na itikadi hii na likajulisha kufuata na kunyenyekea basi ni ibada, na kinyume chake ni kuwa tendo lolote ambalo halikutegemezewa itikadi kama hii haliwezi kuzingatiwa kuwa ni ibada wala shirki."

Lau mtu atanyenyekea mbele ya mtu na akamuheshimu na kumtukuza bila ya kuamini itikadi kama hii, basi tendo hili halitachukuliwa kuwa ni shirki wala ibada hata kama tendo hilo litakakadiriwa kuwa ni haramu.

Kwa mfano: Haitazingatiwa kuwa ni ibada sijda ya mpenzi kwa mpenzi wake, wala mwenye kuamriwa kumsujudia aliyemuamuru na mke kumsujudia mume pamoja na kwamba Sijda kumsujudia asiye Mwenyezi Mungu ni haramu kisheria, kwani Sijda ni Makhsusi kwa Mwenyezi Mungu peke yake wala hairuhisiwi kwa yeyote yule kafanyiwa japo itakuwa ni kwa sura ya dhahiri isiyokuwa na itikaadi isipokuwa kama Mwenyezi Mungu ataamuru kufanywa kwa sijida hiyo (kwa asiye Mwenyezi Mungu).

NATIJA YA UTAFITI

Mpaka hapa kwa namna fulani tunaweza kufafanua uhakika wa Ibada na sasa ni lazima tueleze kwa kifupi matokeo ya utafiti huu na tunasema:

Lau mtu atawanyenyekea watu wengine bila ya kumzingatia mmoja wapo kuwa ni Mungu au Rabbu au kuwa ni asili inayojitegemea kwa kutenda matendo ya Mwenyezi Mungu, bali amewaheshimu tu kwa kuwa wao ni: "Waja waliotukuzwa hawamtangulii Mwenyezi Mungu kwa neno (Lake asemalo) nao wanatenda amri zake" - Qur'an, 21:26. Basi mtu huyo tendo lake hili la kunyenyekea haliwi ila kuwaheshimu na kuwatukuza, wala hakuna uhusiano wowote wa tendo hili na ibada kamwe.

Bila shaka Mwenyezi Mungu amewataja baadhi ya waja wake kwa utajo mwema na amewasifu kwa namna inayoamsha raghba (hamu) ya kila mtu awatukuze na kuwaheshimu.

Miongoni mwa utajo huo ni kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema:

"Bila shaka Mwenyezi Mungu alimchagua Adam na Nuh na kizazi cha Ibrahim na kizazi cha lmran juu ya walimwengu wote."

Qur'an, 3:32

Vile vile Qur'an inabainisha kwamba Mwenyezi Mungu alimchagua Nabii Ibrahim kwa ajili ya Uimamu anasema:

"(Mwenyezi Mungu) akasema bila shaka ninakufanya uwe lmamu kwa ajili ya watu.

Qur'an, 2:124

Pia Mwenyezi Mungu katika Qur'an amewataja kwa utajo mwema Manabii Nuh, Ibrahim, Dawood, Seleiman, Musa, Isa na Muhammad, (Rehma za Mwenyezi Mungu ziwashukie wote).

Na amewasifu kwa sifa tukufu kiasi kwamba kila sifa moja peke yake inatosha kuuvuta moyo na kuleta mapenzi ndani ya nafsi za watu. Na utaiona Qur'an Tukufu inatangaza ubora wa kizazi cha Mtume Muhammad [s] katika aya nyingi.

Miongoni mwa aya hizo ni hizi zifuatazo:

"Bila shaka Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu Enyi watu wa nyumba (ya Mtume) na akutakaseni sana sana."

Qur'an, 33:33

"Waambie sikutakeni malipo yoyote juu ya utume wangu isipokuwa muwapende Al-Qurbaa".

Qur'an 42:23

Na huwalisha chakula katika mahaba ya Mwenyezi Mungu, masikini, yatima na mateka hali ya kuwa wenyewe wanakipenda (chakula hicho) (nao husema moyoni mwao) tunakulisheni kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu (tu) hatutaki kwenu malipo wala shukurani, hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na taabu, basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha na atawalipa mabustani ya pepo na (nguo) za hariri kwa sababu ya kusubiri (kwao)... mpaka mwisho wa Surat hii ya 76.[170]

Basi lan watu wangesimama upande wa Mawalii hawa watukufu kwa matendo ambayo yanakubalika ikiwa ni pamoja na kuwatukuza na kuwaheshimu, sawa sawa katika zama za uhai wa Mawalii hao au baada ya kufa kwao, bila ya kuwaitakidi kuwa wao ni miungu na ni vyanzo vinavyojitegemea kwa matendo yanayomstahiki Mwenyezi Mungu, basi hapana mtu yeyote ambaye angeyaona matendo haya kuwa ni ibada wala anayeyasimamia asingeonekana kuwa ni mshirikina, bali kinyume chake angewaona kuwa ni watu wenyc mafanikio wanaoheshimu Mawalii wa Mwenyezi Mungu na kudumisha utajo wao na kuwafanya Mawalii hao kuwa ni kiigizo (chema) kwa watu hao.

Bila shaka kuwatukuza Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni kutukuza vitambulisho vya Mwenyezi Mungu kama ilivyokwisha onyeshwa hapo kabla, na kwamba Uislamu unavitukuza vitambulisho vya Mwenyezi Mungu.

Mtume [s] alikuwa akilishika na kulibusu "Hajarul-Aswad" pamoja na yeye kufahamu wazi kwamba hilo ni jiwe tu. Na sisi pia tunamfuata Mtume [s] kwa tendo lake hilo, tunalibusu Hajarul Aswad na tunatufu nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo si kitu ila mkusanyiko wa mawe na udongo, na tunakimbia baina ya Safa na Marwah na si kitu ila vilima viwili.

Hii ni (kana kwamba) tunatenda matendo yale yale yaliyokuwa yakitendwa na waabuduo sanamu kwa masamu yao, lakini hapana kabisa mtu yeyote ambaye imepata kumpitia katika fikra zake kwamba sisi tunaabudu udongo na mawe.

Basi Je, ni kwa nini? Ni kwa sababu mawe hayo hayadhuru wala kunufaisha.

Ama tungetekeleza Ibada hizi hali ya kuwa tunaitakidi kuwa mawe haya na vilima hivi ni miungu na ndiyo chanzo cha athari za uungu, basi tungekuwa miongoni mwa wanaoabudu sanamu.

Na kwa msingi huu, bila shaka kuubusu mkono wa Nabii au Imam au Mwalimu au wazazi wawili na pia kuibusu Qur'an na vitabu vya dini kama vile "Nahjul-Balagha" na kubusu Zariha na kila kile chenyc kuhusiana na waja wema wa Mwenyezi Mungu, hakuna kinachokusudiwa ila ni heshima na kuwatukuza, na kawatukuza wao si kitu kingine ila kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ndani ya Qur'an imekuja (Habari) ya Malaika kumsujudia Adam [a] na pia ndugu wa Nabii Yusuf kumsujudia Yusuf [a], lakini hapana yeyote iliyempitia katika akili (yake) kwamba kusujudu (kwao hawa) ilikuwa ni kumuabudia Adam au Yusuf na hiyo ni kwa sababu hao waliomsujudia Adam na Yusuf hawakuwaitakidi wawili hao kuwa ni miungu na hawakuwazingatia kuwa wao ndiyo asili ya matendo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, bali jambo hilo lilikuwa ni heshima na utukufu na siyo ibada kama inavyoonekana.

Bila shaka Mawahabi wakati wanapokutana na aya hizi, wanagongana nazo, kwani utawaona wanachunguza huku na huko ili kuzikwepa na kuzificha na husema; "hakika kusujudu kwa watu hao ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu kwa hiyo haiwezi kuzingatiwa kuwa ni ibada."

Ni sawa kwamba yote hayo na hata kusujudu kwa ndugu wa Yusuf [a] kulikuwa ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu au radhi yake, lakini kitu ambacho Mawahabi wanajisahaulisha na kujifanya hawakijuwi ni ule ukweli wa tendo lenyewe Ia Sajdah siyo ibada na ndiyo maana Mwenyezi Mungu akaliamrisha.

Na lau Sajdah ingekuwa ni ibada kwa anayesujudiwa, Mwenyezi Mungu asingeliamrisha kabisa, kwani amri haiwezi kuitoa ibada kwenye uhakika wake na wala haiwezi kuifanya shiriki kuwa Tauhidi.

Mwenyezi Mungu anasema: "Waambie, bila shaka Mwenyezi Mungu haamrishi maovu, Je, Mwasema juu ya Mwenyezi Mungu mambo msiyoyajua?"

Qur'an, 7:28

Kifupi ni kuwa, uhakika wa tendo lolote lazima uwe siyo wa kiibada kabla haijatolewa amwi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuliamrisha tendo hilo ili (itakapotoka amri) ipate kuihusisha ibada (kwenye tendo hilo) na wala hakuna namna yoyote ya amri itakayokuja kulitengua tendo hilo kutoka kwenye hukmu ya Ibada.

Bila shaka kujitakasa ambako Mawahabi wanategemea, kitu ambacho muda mrefu tumekuwa tukisikia toka kwa Masheikhe zao huko Maka na Madina, kunajulisha ukaidi walionao juu ya kufahamu maarifa ya Qur'an na kukosa kwao kuelewa kuwa "Ibada" inao uhakika wa pekee unaojitegemea na hupata ikatokeza amri kuamrisha ibada na wakati mwingine katazo kukataza.

Hii ina maana kwamba, kitu ambacho kwa dhati yake ni ibada, Mwenyezi Mungu hukiamrisha au kukikataza, kama vile Sala na Saumu ambazo Mwenyezi Mungu amewaamrisha watu "Mukalafu" kazitekeleza na amemkataza (kufanya ibada hizo) mwanamke mwenye hedhi, ati kama vile kufunga siku ya Idi al-Fitri na Adh-haa ambazo Mwenyezi Mungu amewakataza watu wote "Wasifunge".

Basi kama kusujudu kwa Malaika kumsujudia Adam [a] na ndugu wa Yusuf [a] na wazazi wake wawili kumsujudia Yusufu [a] ni kuwafanyia Ibada, basi ile amri ya kuamrishwa kwao kusujudu, hakuitoi sijda katika uhakika wa kuwa ni ibada bali hapana budi tuseme kuwa kuitakidi Uungu ndiko kutakakokiharamisha kitendo hicho na kukifanya kuwa ni ibada, au kuitakidi kuwa yule anayenyenyekewa ndiyo asili (chanzo) cha matendo ya Mwenyezi Mungu. Vipi tutapata msimamo?

Ewe msomaji mpendwa inapasa ufahamu kuwa, kuondosha tofauti iliyopo kati ya Waislamu na Mawahabi ndani ya mambo mengi (wanayohitalifiana) inategemea kupata ufumbuzi wa maana ya ibada. Ikiwa haikubainishwa maana ya ibada kwa taarifu ya kimantiki, na ikawa hakuna maelewano na uadilifu katika pande mbili, basi hakuna faida ya kutafiti na kujadiliana.

Kwa maelezo haya basi, hana budi mtu mwenye kutafuta ukweli afanye kila njia ya kuchunguza maudhui hii kwa undani na asihadaike na taarifu za kilugha zilizopungufu kuweza kutatua na kufafanua.

Rejea iliyo bora atakayoirejea ni aya za Qur'an, hiyo ndiyo dalili inayoongoza (kufahamu) maudhui hii na kila maudhui.

Na miongoni mwa mambo yanayohuzunisha ni kwamba, waandishi na watunzi wa Kiwahabi na walioandika kuwajibu Mawahabi, wamefanya utafiti na uchunguzi kwa urefu katika nukta zingine na wala hawakuitilia maanani nukta hii muhimu (ya Ibada) kwa kuisherehesha na kuithibitisha.

Basi Mawahabi wanasema, "Matendo mengi muyafanyayo Enyi Waislamu kumhusu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu [s] na Maimamu wa nyumba yake ni kumuabudia, na hali hiyo inalazimu kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada."

Kwa hiyo basi inabidi Waislamu walete ufafanuzi na maelezo ya kina kuhusu ibada ili kuiondoa dalili yao ya upuuzi. Kwa hakika Mawahabi wanayaona mambo mengi wayatendayo Waislamu kwa maiti kuwa ni kumuabudia.

Kwa mfano:

1). Kuomba Shafaa kwa Mtume [s] na watu wema.

2). Kuomba uponyo kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu.

3). Kuomba kutekelezewa haja toka kwa viongozi wa Dini.

4). Kumheshimu na kumtukuza mwenye kaburi.

5). Kutaka msaada kwa Mtume [s] na wengineo.

Basi wao (Mawahabi) wanasema, "Hakika Shafaa ni katika matendo ya Mwenyezi Mungu na vile vile kuponya ni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuomba mojawapo ya mawili haya kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu kunapelekea kumuabudu huyo (aombwaye).

NI KIPI KITENDO CHA MWENYEZI MUNGU?

Katika kitabu hiki kidogo tunatanguliza uchunguzi juu ya matendo ya Mwenyezi Mungu na maana yake ili maudhui hii ipate kufahamika na tunasema: "Ikiwa ambaye anasimamaia Shafaa na kuponya kwa uwezo wake mwenyewe na kwa kutaka kwake hali ya kujitegemea bila ya kuipata haki ya Shafaa kutoka kwa yeyote yule na bila ya kutegemea uwezo wa aliye juu zaidi kuliko yeye kiuwezo) basi haya ni miongoni mwa matendo ya Mwenyezi Mungu yanayomuhusu peke yake.

Na kuomba Shafaa kwa yeyote yule hali ya kaitakidi (kama tulivyosema hivi punde) maana yake ni kuamini Urabbi na Uungu wa huyo anayeombwa.

Ama ikiwa kuomba Shafaa na uponyo kumesalimika kutokana na itikadi hii, na mtu akaomba Shafaa kwa mtu anayemuitakidi kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu, pia anatenda kwa msaada na uwezo wa Mwenyezi Mungu na idhini yake, basi Shafaa hii na uponyo huu havilazimiani na itikadi ya Uungu na siyo kuomba tendo la Mwenyezi Mungu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu."

Qur'an Tukufu inasema ikimnukuu Nabii Isa [a]:

"Na ninaponya vipofu na wenye mbaranga, na ninafufua wafu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 3:49

Na ufafanuzi kama huu unakuja pia ndani ya munasaba wa kuomba kukidhiwa haja toka kwa mmoja wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu au kumuomba msaada.

Basi kutaka kukidhiwa haja na Walii huyo kuna namna mbili:

1). Kumuomba mja pamoja na kuitakidi kuwa anao uwezo wa kujitegemea Mwenyewe, hii itakuwa ni Ibada.

2). Kumuomba mja hali ya kuitakidi kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na nguvu zake zinatoka kwa Mwenyezi mungu, basi hali hii haihusiani kabisa na ibada.

Kwa Hakika ufafanuzi huu siyo tu ndiyo ukomo wa kutenganisha baina ya ibada na kisichokuwa ibada kwa munasaba wa matendo haya, bali ni kanuni ya ujumla inayotenganisha baina ya Shirki na Tauhidi katika kila vinavyo athiri na sababu.

Bila shaka kuitakidi athari (matokeo) ya 'Asprini' (kwa mfano) katika kutuliza maumivu, na kuitakidi kuwa ikiwa athari hiyo inatokana na uwezo wake wa kujitegemea na kwamba hakuna mafungamano na uwezo uliyo juu zaidi ambaye ni Mwenyezi Mungu, basi maana yake ni kuitakidi Uungu wa hiyo 'Asprini'.

Ama kuitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeyaweka matokeo haya na athari hii ndani ya Asprini na pia dawa hii si lolote ila ni sababu ya kutuliza maumivu na vile vile haiwezi kutuliza maumivu isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, bila shaka itikadi ya namna hii inatokana na Tauhidi yenyewe khasa, kwani hapana mwenye kuathiri ila yeye Mwenyezi Mungu.

Na kwa sababu hii tumesema kwamba "Kuondosha tofauti mbali mbali kunaegemezewa kwenye ufafanuzi wa maana ya Ibada na kuitakasa Tauhidi kutokana na shirki na matendo ya Mwenyezi Mungu kutokana na mengineyo na kuutakasa uungu kutokana na Ubudiyyah.

Na hapo kabla imeonyeshwa kuwa Waarabu wa zama za Jahiliyya walikuwa wakiitakidi itikadi hii yenye makosa, kwamba Masanamu (hayo hayo) ndiyo yaliyokuwa yanaendesha baadhi ya mambo ulimwenguni kwa kujitegemea na yalikuwa yakimiliki Shafaa na mambo mengineyo.

Itikadi hii ndiyo iliyowafanya wawe washirikina.

Kwa hiyo, iwapo utataka ufafanuzi wa kielimu juu ya maudhui hii rejea vitabu hvi viwili vifuatavyo vilivyoandikwa na Mwandishi wa kitabu hiki.

1). Maalimut-Tauhidi Fil-Qur-'anil-Karim.
2). At-Tauhidu Was-Shirku Fil-Qur-anil-Karim.

MAMBO YA AL-QUDHAI AL-MISRI

Baada ya kuwa nimeyahariri (maelezo yaliyotangulia) na kubainisha ufafanuzi wa ibada niliyaangalia kwa makini maneno ya mmoja wa wachunguzi miongoni mwa wanachuoni wa chuo cha Az-har, yaani Ustadh Sheikh Salamah Al-Qudhai Al-Izami As-Shafii ambaye ndiye Mwandishi wa kitabu kiitwacho "Fur-Qanul Qur'an Baina Sifatil-Khaliq Wa Sifatil-Ak-Waan.[171]

Yeye amesema: Mwenyezi Mungu aing'arishe hoja yake:

(Sasa tutazame maana ya Ibada kisheria, na ninataraji mahala hapa patatoa uzinduzi uliyo bora, kwa hakika kosa lililomo ni kuteleza kukubwa na ni kosa kubwa ambalo zilimwagwa damu (za watu) zisizoidadi ya kudhibitiwa na heshima za watu zilizovunjwa hazina hesabu, na jamii zikatenganishwa mahala ambapo Mwenyezi Mungu ameamuru ziunganishwe Mwenyezi Mungu atulinde kutokana na makosa na fitna hasa hasa fitna za Shubuhati - basi fahamu kwamba wao yaani Mawahabi waliifasiri ibada kuwa ni "Kufanya unyenyekevu ulio katika daraja ya juu sana", na wakakusudia ndani ya tafsiri hiyo maana ya kilugha tu. Ama maana ya kisheria inatoa maana iliyo finyu kuliko hii (ya kilugha) kama itakavyodhihiri kwa mchunguzi mwenye kuvumilia katika utafiti iwapo ataangalia kila mahali ambapo neno ibada limekuja katika sheria, kwani maana yake ni "kufanya unyenyekevu wa hali ya juu kwa moyo kwa kuitakidi Uungu wa anayenyenyekewa, au kwa mwili pamoja na itikadi hiyo.

Basi ikiwa itikadi hii itakuwa haipo, unyenyekevu wa dhahiri alioufanya (Mwenye kunyenyekea) hauwezi kuwa ni ibada kisheria, ikiwa kanyenyekea sana au kidogo na kwa namna yoyote hata kama ni kusujudu na hata kama hakuamini Rububiya kwa yule anayemnyenyekea lakini akaamini kuwa anazo khususiyah fulani za Rububiyah, basi hii pia itakuwa ni ibada. Kwa mfano kama ataitakidi kwamba huyo mwenye kunyenyekewa anajitegemea katika kunufaisha au kudhuru na kama vile kupitisha matakwa yake japokuwa kwa njia ya Shafaa kumshufaia huyo mwenye kumuabudia mbele ya Mola ambaye ni mkuu kuliko huyu mwenye kuabudiwa.

Kwa hakika washirikana walikufuru kwa sababu ya kuyasujudia masanamu yao na kuyaomba na mambo mengineyo miongoni mwa aina za unyenyekevu kwa sababu ya sharti hii kwani washirikina waliitakidi umola wa hayo wanayoyanyenyekea au wakayahusisha na khususiyyat za Rububiyah kama utakavyokujia ufafanuzi wake.

Na haiwezekani kusema kwamba kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu bila itikadi hii ni ibada kisheria ukiachilia mbali aina zingine za unyenyekevu ambazo ni duni kuliko Sijda. Na kama tutasema, Sijda hii ni Ibada itakuwa ni kufru, na chochote kilicho kufru hakitofautiani kutokana na tofauti ya sheria wala amri ya Mwenyezi Mungu kwa kitu hicho wala Mwenyezi haamrishi kitu kama hicho:

"Waambie Mwenyezi Mungu haamrishi mambo mabaya"

Qur'an, 7:28

"Na wala haridhii kufru kwa waja wake."

Qur'an, 39:7

Na haya yako wazi (yanaeleweka) kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

Na (sasa) hebu msikilize Mwenyezi Mungu Mtukufu alipowaambia Malaika:

"Msujudieni Adam, wakasujudu wote isipokuwa Ibilisi alikataa na akapinga"

Qur'an, 2:34

Na alisema Iblisi: "Mimi ni bora kuliko yeye":

Qur'an, 7: 12

"Na alisema tena: Je, Nimsujudie Uliyemuumba kwa Udongo?"

Qur 'an, 17:61

Na kusema kwamba Adam alikuwa ndiyo Qibla (cha Malaika walipamuriwa kumsujudia) ni usemi ambao haukubaliwi na ukweli na pia uchunguzi (wa jambo hili) katika kuifahamu aya inavyopasa kuifahamu unapinga kauli hiyo.

Na kama fahamu zako zitashindwa kulifahamu jambo hili, basi huyu hapa Nabii Yaqub na mkewe na watoto wao kumi na mmoja ambao Mwenyezi Mungu amesema kuhusu wao, "Wakaporomoka kumsujudia". Hapa inamaana walimsujudia Yusuf [a].

Qur'an, 12:100

Mwanachuoni Al-Hafidh Ibn Kathir amesema katika Tafsiri ya aya hii, "Walimsujudia (Yusuf) wazazi wake wawili na ndugu zake na walikuwa watu kumi na moja, na tendo lao hili lilikuwa ni desturi inayokubalika kufanywa katika sheria zao wanapomsalimia mkubwa humsujudia.

Na desturi hii ilikuwa imeruhusiwa tangu kwa Nabii Adam [a] hadi kwenye sheria ya Nabii Isa [a], kisha iliharamishwa katika mila hii ya Kiislamu na kuifanya Sijda ni makhsusi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na haya ndiyo madhumuni ya kauli ya Qatada (juu ya Qadhiya hii na wengineo). Na kuna mapokezi katika hadithi kwamba: "Muadhi alifika Shamu akawakuta watu wa huko wakiwasujudia Maaskofu wao, naye aliporudi (Madina) akamsujudia Mtume [s], Mtume akasema "Nini hiki (ukifanyacho) Ewe Muadhi"?

Muadhi akasema: "Mimi nimewaona (Huko Shamu) wanawasujudia Maaskofu wao, nawe unastahiki mno mimi nikusujudie." Mtume akasema: Lau ningekuwa mwenye kumuamrisha yeyote kumsujudia mwingine, basi ningemuamuru mke amsujudie mumewe kutokana na haki kubwa aliyonayo kwake."

Na katika hadithi nyingine inasemwa kwamba: "Salmaan alikutana na Mtume [s] katika baadhi ya njia za Madina, na huyu Salmaan alikuwa kasilimu hivi karibuni, basi akamsujudia Mtume [s], Mtume akasema, "Ewe Salmaan usinisujudie bali msujudie (Mwenyezi Mungu) aliye hai ambaye hatakufa".

Lengo katika maelezo haya ni kuonyesha kuwa (Desturi ya kusujudia wakubwa) ilikuwa ikiruhusiwa katika sheria zao, (mwisho wa kauli ya Ibn Kathir).

Naye Imam Abu Jaafar (At-Tabari) katika tafsiri yake amesema mfano wa maelezo haya. Bila shaka umekwisha fahamu kwamba (Kitendo) kilicho cha kufru hakitofautiani kwa kutofautiani sheria, wala Mwenyezi Mungu hakiamrishi kuwa kitendwe wakati fulani miongoni mwa nyakati, basi kusujudu kwa Malaika kumsujudia Adam wala sijda aliyosujudiwa Yusuf [a] hazikuwa ni kufru kwa kuwa waliosujudu hawakuwa wameitakidi itikadi ya mambo ambayo yanamuhusu Mwenyezi Mungu peke yake wakati walipowasujudia hao waliosujudiwa, bali Malaika waliposujudu (kumsujudia Adam) kwao ilikuwa ni ibada kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaamuru kufanya hivyo waliomsujudia Yusuf kwao ilikuwa ni maamkizi yaliyoruhusiwa, na ruhusa hiyo ilifutwa katika sheria yetu (ya Kiislamu). Na wanachuoni wamehukumu kuwa, ni kufuru kwa yeyote mwenye kusujudia jua, au mwezi au sanamu, kwa kuwa kufanya hivyo ni alama za kufru ambayo ni kupinga mafunzo ya msingi katika dini kama ambavyo wamehukumu kuwa, mwenye kutamka shahada mbili ni muumini kwa hivyo ndizo dalili za imani, na imani ni kitu cha moyoni. Wamehukumu hivi sio kwa kuwa eti kile kitendo cha kwanza yaani kusujudia mwezi na jua kwa dhati yake ndiyo kufru na kile cha pili (kutamka shahada mbili) ndiyo imani. Ikiwa kuna uzito wa kufahamu maelezo haya ambayo siyo mazito kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hebu iangalie nafsi yako mwenyewe, huenda heshima na adabu uliyonayo kwa baba yako ikakuzuwia kukaa au kulala mbele yake, hivyo ukawa umesimama au kuketi kiasi saa moja au zaidi, na (kufanya hivi) haitakuwa ni ibada uliyomfanyia. Kwa nini basi?

Hii ni kwa sababu tendo lako hili halikuambatana na itikadi ya mambo ambayo ni maalum kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na utaposimama kiasi cha kusoma Sura Al-Fatihah, na ukakaa kiasi cha kusoma Tashahudi kwa kiasi cha dakika moja au mbili hivi, na ikahesabiwa kuwa umefanya ibada kwa huyo uliyemsalia. Siri ya kuwa matendo haya ni ibada, ni kule kunyenyekea kwako kulikofanyika ndani ya kisimamo chako na kukaa kwako kulikoambatana na itikadi ya Uungu wa yule uliyemnyenyekea ambaye ni Mwenyezi Mungu.

Na (kwa mfano) unamwita kiongozi wako katika kazi au amiri wako ili akusaidie dhidi ya mtu aliyekudhulumu, au akusaidie kutokana na shida iliyokufika na hali wewe hukuitakidi kuwa huyo umwitaye ana uwezo wake wa kujitegemea kuleta manufaa au kuondosha madhara lakini tu Mwenyezi Mungu amemfanya awe ndiyo sababu ya kupitishia mambo ya kawaida mikononi mwake kwa yale ayapendayo yeye Mwenyezi Mungu.

(Basi kuomba kwako msaada kwa kiongozi wako au amiri wako) haiwezi kuwa ni ibada kwa yule uliyemuomba kama tulivyokwisha eleza.

Lakini iwapo utamwita (akusaidie) hali ya kuwa unaitakidi kwamba yeye ndiye anayenufaisha kwa dhati yake au kudhuru au kupitisha maamuzi bila kupingwa kwa ombi hilo, itakuwa wewe ni mwenye kumuabudia yeye, na kwa ibada hii umemshirikisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kuwa umeitakidi ndani ya tendo hilo mambo yanayomuhusu Mwenyezi Mungu, kwani bila shaka kujitegemea kwa dhati, kuleta manufaa au kuondoa madhara na kupitisha maamuzi bila kipingamizi ni katika matendo makhususi ya Mwenyezi Mungu.

Na washirkina walikufuru kwa kuyasujudia masanamu na mfano wake kwa sababu ya kuyaitakidi masanamu hayo kuwa na uwezo wa dhati wa kujitegemea kunufaisha au kudhuru na kupitisha maamuzi bila kuyatenganisha na Mwenyezi Mungu japo kwa njia ya uombezi mbele yake kwani wao wanamuitakidi Mwenyezi Mungu kuwa ndiyo Mungu mkubwa na vile wanavyo viabudia ni waungu chini ya Uungu wa Mwenyezi Mungu, na kwa sababu ya uungu walionao imebidi wapitishe maamuzi wao na Mwenyezi Mungu bila kipingamizi.

Aya nyingi za Qur'an zinajulisha kama tulivyoeleza na kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Ni nani huyu ambaye ni mlinzi wenu atakayekusaidieni pasipo (Mwenyezi Mungu) mwingi wa Rehma, hawako makafiri ila katika kudanganyika".

Qur'an, 67:20

Na kauli yake nyingine aliposema: "Je, wanao Miungu wanaowalinda badala yetu, hawawezi kujisaidia wenyewe na wala hawatahifadhiwa katokana nasi."

Qur'an, 21:43

Na Istif-hami iliyoko katika aya hizi mbili ni ya makemeo kwanjia yakuwalaumu katokana na yale waliyoitakidi. Pia Mwenyezi Mungu amesimulia habari za watu wa Nabii Huud [a] walipomwambia: "Hatusemi ila ni kuwa baadhi ya Miungu yetu imekwisha kukutia katika balaa".

Qur'an, 11:54

Naye Nabii Huud alipowaambia: "Basi nyote nifanyieni hila (kunidhuru) na musinicheleweshe".

Qur'an, 11:55-56

Nyingine ni kauli yake Mwenyezi Mungu atakayosema kuwalaumu washirikina siku ya Qiyama kutokana na itikadi walizoziitakidi kwa masanamu ikiwa ni pamoja na kuamini kuwa yana uwezo wa kunufaisha na kupitisha maamuzi kama yapendavyo:

"Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, Je, wanaweza kukusaidieni au kujisaidia wenyewe?

Qur'an, 26:92-93

Nao washirkina watasema hali wakiwa motoni wakizozana na kuwaambia hao waliowaitakidi kuwa ni Miungu na wanazo khususiya za kiungu:

"Wallahi bila shaka tulikuwa katika upotofu uliodhahiri, tulipokufanyeni sawa na Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote".

Qur'an, 26:97-98

Hebu angalia kulinganisha walikokiri (washirikina) kiasi kwamba muongo anasema kweli na muovu naye anajuta wakati majuto yake hayamsaidii kita.

Bila shaka kulinganisha kulikotajwa ikiwa ni kwa ajili ya kuthibitisha kitu katika sifa za Uungu, basi hilo ndilo lengo na kutokana na hali hii ndipo unapatikana ushirikina wao na kufru yao, kwani sifa za Mwenyezi Mungu zinawajibisha upweke kwa maana ya kutokuwa na mfano wake kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kama ilivyotangulia kuelezwa.

Na kama kulinganisha huko ni katika kustahiki kwake ibada, basi italazimu kuitakidi ushirika katika yale ambayo ndani yake kuna ustahiki wa ibada, na huo ustahiki ni sifa za Uungu au baadhi ya sifa hizo, na ikiwa (kulinganisha) ni katika nafsi ya ibada yenyewe basi kitendo hicho hakifanywi na mtu mwenye akili ila kwa yule anayeitakidi kustahiki huyo mwenye kuabudiwa kama vile anavyostahiki Mola wa ulimwengu.

Basi ni vipi itakanushwa itikadi yao ya Uungu kwa miungu yao hali ya kuwa waliifanya kuwa niwashirika wa Mwenyezi Mungu na wakaipenda kwa mapenzi anayostahiki kupendwa Mwenyezi Mungu kama alivyosema yeye Mwenyezi Munga akieleza habari zao:

"Na miongoni mwa watu kuna wanaowafanya miungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu, wanawapenda kwa mapenzi anayostahiki kupendwa Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 2:165

Na neno "Andaad" lililotumika kwenye Aya hiyo hapo juu ni uwingi wa "Nidd" na maana yake ni kama walivyosema wataalam wa tafsiri na lugha.

Ama kauli ya Mwenyezi Mungu akiwazungumzia washirikina akasema: "Na ukiwauliza ni nani aliyewaumba, bila shaka watasema, ni Mwenyezi Mungu".

Qur'an, 43:87

Kauli hii na nyinginezo mfano wa hii maana yake siyo kwamba wao (washirikina) hawauthibitishi uungu wa miungu yao na yale mambo maalum yanayohusu uungu, bali maana yake ni kwamba, wanapohojiwa hukiri kutokana na ukweli ambao Mwenyezi Mungu ameziumbia nafsi (kumtambua). Lakini ni kwa kiasi gani wao hurejea haraka katika itikadi zao za waungu wa uongo kwa miungu yao, hurudi na katumbukia humo kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika aya nyingine.

"Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu kisha wanazikanusha na wengi wao ni makafiri".

Qur'an, 16:83

Na kauli nyingine ya Mwenyezi Mungu akizungumzia kikundi miongoni mwao:

"Kila wakirudishwa katika fitna, huangushwa humo".

Qur'an, 4:91

Kurudishwa katika fitna na kuangushwa humo siyo jambo la ajabu kutokea kwa wale walioyafanya matamanio yao kuwa miungu yao, nawe msomaji utawaona hao wenye matamanio hayo iwapo utamjadili katika Bid'a zake, atakusikiliza kwa makini na atakinaika (atatosheka) wakati wa majadiliano na atakiri kuwa amekwenda kinyume cha haki na ataonyesha dalili za uadilifu (katika majadiliano na matokeo yake). Kinapomalizika kikao cha mjadala hurudi kule kwenye mazoea ya matamanio na kurudia Bid'a yake kama kwamba hapakuwa na mjadala baina yako na yeye (isipokawa waliorehemewa na Mwenyezi Mungu).

Na hali kama hii tumeiona mara nyingi kwa wale tuliokutana nao miongoni mwa wanaofuata matamanio. Tunamuomba Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake atupe mafanikio.

Pamoja na yote haya, lau itakubalika kwamba (washirikina) hawakuitakidi kwa miungu yao kuwa na uwezo wa kuumba, kuruzuku wala kuendesha mambo, lakini wanaitakidi ndani ya miungu hiyo mambo yasiyokuwa hayo ambayo yanahusu mas-ala ya uungu nao ni wajibu wa kupitisha maamuzi wayatakayo.

Basi wao wanaona kuwa shafaa ya masanamu hayo inakubaliwa moja kwa moja hairudishwi na haitegemei idhini ya Mwenyezi Mungu. "Ametakasika sana Mwenyezi Mungu na yale wayasemayo wajinga."

Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'an akijibu madai yao haya:

"Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake (Mwenyezi Mungu) bila idhiniyake?

Qur'an, 2:255

Amesema Qadhi Nasirudin Al-Baidawi katika tafsiri ya aya hiyo, "Ni ubainifu wa utukufu wa mambo yake, na hiyo ni kwa sababu hakuna anayeungana naye au kumkurubia awezaye kutoa akitakacho iwe kwa shafaa au kunyenyekea, basi itakuwaje iwezekane kwa njia ya kumpinga": Hivyo basi iangalie kauli ya Baidawi aliposema; "Awezaye kutoa akitakacho ikiwa ni kwa Shafaa" utakuta ni dhahiri kuwa inahusu wajibu wa matakwa yake yakubalike kwanza kwa Mwenyezi Mungu na wajibu wa kupitisha maamuzi ni miongoni mwa mambo yanayohusu uungu kama inavyofahamika.

Na aina hii ya Shafaa ni Shafaa ya shirki ambayo Qur'an imeibatilisha, kwani kuiamini Shafaa ya aina hii ni kufru kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Au ndiyo wamejifanyia waombezi kinyume cha Mwenyezi Mungu?"

Qur'an, 39:43

Na kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

"Waambie, ni nani ambaye anaweza kukulindeni kutokana na Mwenyezi Mungu kama akikutakieni ubaya au (nani anayeweza kuzuwiya Rehma yake) kama akikutakieni Rehma?"

Qur'an, 33:27

Ama Shafaa ambayo wanaiitakidi watu wa Tauhidi na ndiyo iliyoletwa na Qur'an na Sunna, yenyewe iko mbali na itikadi ya Shafaa inayoitakidiwa na washirikina kama ulivyo umbali wa imani na kufru na umbali wa mwangaza na kiza.

Na Shafaa ya watu wa Tauhidi ni maombi ya mwenye kushufaiya kumuombea mwenye kushufaiwa, na Mwenyezi Mungu kwa fadhila zake humkubalia amtakaye na hiyo ndiyo maana ya Istith-nai katika kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Isipokuwa kwa idnini yake".

Na maana ya idhini hapa ni kuridhia kama alivyosema kwenye aya nyingine: "Wala hawamuombei yeyote ila yule aliyeridhiwa (na Mwenyezi Mungu).

Qur'an, 21:28

Na nyingine tena: "Na wako Malaika wangapi mbinguni ambao uombezi wao hautafaa chochote isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia".

Qur'an, 53:26

Na kwa maelezo haya inakubainikia tofauti baina ya yale iliyoyathibitisha Qur'an katika Shafaa na yale iliyoyakanusha (ambayo hayana idhini yake na radhi yake.) Mwenyezi Mungu ni mkubwa, hakifanyiki kitu katika ufalme wake ila yeye atake.

Ama Shafaa kwa idhini yake na radhi yake inayotokana na waja wake wema walio wateule kuwaombea wenye kuasi katika watu wa Tauhidi inafaa, na limethibiti hilo kwa njia ya mutawatir wala hapana kizuizi ndani yake na kuitakidi hivyo ni katika mambo ya dini, kwani jambo hili liko katika mlango wa Dua, naye Mwenyezi Mungu huwakubalia waaminio na wakatenda mema na huwazidishia fadhila zake.

Tunataraji itakuwa imeeleweka kwako msomaji (Insha-Allah) nini maana ya ibada kisheria, na wakati huo huo utakuwa umefahamu kuwa siyo ibada ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu pale Mwislamu anapotaka wasila kwa Mwenyezi Mungu.[172]

Basi haya yalikuwa ndiyo maneno yaliyoandikwa na Al Allamah Al-Qudhai, nasi tumeyaleta kutokana na faida nyingi zilizomo, na bila shaka tumeifafanua hali yake, ni juu yako ewe msomaji muadilifu kufanya uchunguzi.

[167] Tafsiri Alaul-Qur'an, juz. 1, uk 57.

[168] Al-Milal Wanihal cha Shahirstani, juz. 2, chapa ya Misri uk. 244-247

a href=#n169 name=r169>[169] Qur'an, 10:18.

[170] Qur'an, 76:8-12

[171] Ni miongoni mwa vitabu bora kilichotungwa katika zama za hivi karibuni, na mtunzi huyu pamoja na mwenziwe aitwaye Al- Ustadhi Muhammad Zahid AI-Kauthari AI-Misri ambaye ni mwanachuoni wa hadithi na muhakiki, ni miongoni mwa Wanachouni ambao walisimama kupinga uzushi wa Kiyahudi unaomshabihisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumfanyia mwili na upande na mahali. Kwa hakika uzushi huu ulianza kupata nguvu mwanzoni mwa Qarne ya nane kutoka mkononi mwa Sheikh wa Bid'a na upotofu aliyekuwa akiitwa: "Ahmad Abdil-Halim Ibn Taimiyyah AI-Jarrani na baada yake kupitia mkononi mwa mwanafunzi wake lbn Al-Qayyim, na baada ya wawili hao, kupitia kwa yule aliyekunywa makombo yao yaani Sheikh Muhammad Ibn Abdil-Wahab. Basi huyo mwanachuoni wa mwanzo alisimama akatunga Kitabu chake kiitwacho, "Fur-Qanul-Qur'ani akapinga uzushi huu (wa Ibn Taimiyyah na wenzake) na mwingineo miongoni mwake ikiwa ni kuzuwia (watu) kutawassal na kuomba msaada na kutaka shafaa kwa yule ambaye Mwenyezi Mungu amemjaalia kuwa mwenye kusaidia kwa idhini yake na mwenye kushufaiya kwa amri yake Mwenyezi Mungu, kama ambavyo yule mwanachuoni wa pili alisimama kwa kusambaza kitabu kiitwacho "Al-Asmau Was-sifatu" cha Al-Hafidh Abubakr Al-Bayhaqi ikiwa ni pamoja na kukihakiki na kukiwekea ufafanuzi wa utangulizi wenye manufaa, na vitabu hivi viwili vilichapishwa Misri Mwaka 1358 A.H. katika mjaladi mmoja. Basi Mwenyezi Mungu awalipe juhudi zao najuhudi za msambazaji wa vitabu vya haki.

[172] Fur-qanul-Qur'an, uk. 111-115