KUTABARUKU KWA ATHARI ZA MAWALLI WA MWENYEZI MUNGU NA KUOMBA UPONYO

Mawahabi wanaitikadi kwamba kutaka baraka kwenye Athari za Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Mawahabi pia wanamuona kuwa ni mshirkina mtu ambaye ataibusu mihrabu ya Mtume [s] na mimbari yake, japo hatafanya hivyo kwa nia ya ibada, isipokuwa ni kwa ajili tu ya mapenzi yake kwa Mtume [s] ndiyo maana katabaruku na kutaka uponyo kwenye Athari zake.

Kukataza kutabaruku kwa athari za Mtume [s] na kulibusu kaburi lake na mimbari yake tukufu ni katika mambo ambayo Mawahabi wametilia nguvu kuyapinga dhidi ya Waislamu, na wamekuwa wakitumia makundi ya askari wa kigaidi waliopewa jina la waamrishaji mema na kukataza maovu, na wamewasambaza (askari) hao katika Msikiti wa Mtume [s] ili wazuwiye kulibusu kaburi lake tukufu na mimbari yake tukufu, pamoja na mihrab ya Msikiti wa Mtume [s].

Mawahabi hawa wanawahujumu mahujaji hapo Madina kwa kila aina ya mateso na kuwazuwiya kutabaruku na kulibusu kaburi la Mtume [s] na utawaona kila mara wameshika fimbo, na mikononi mwao mna nyaya ngumu tayari kumshambulia kila Hujaj atakayethubutu kutabaruku au kulibusu kaburi la Mtume [s].

Na kutokana na hali hii basi, mara kwa mara wamekuwa wakimwaga damu za mahujaji wasio na makosa na kuudhalilisha utu wao katika Msikiti wa Mtume [s], kwa madai kwamba kutabaruku na kulibusu kaburi ni kumuabudu huyo aliyezikwa hapo.

Kwa hakika watu hawa hawaujuwi Uislamu, na wamekosea kufahamu maana ya Ibada na Maf-humu yake, na kwa sababu hii basi wamepotea njia na wanatangatanga ndani ya upotevu. Wamekuwa wanaona eti kila anapoheshimiwa mtu aliyekwisha kufa ni kumuabudu mtu huyo, pamoja na kufahamu kwamba kubusu kaburi tukufu na kutabaruku kwa athari za Utume siyo kwa ajili nyingine isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Waislami hawamtukuzi Mtume Mtukufu wala hawatabaruku kwa athari zake ila ni kwa kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni Nabii wake mteule ambaye Mwenyezi Mungu amemtukuza kuliko Manabii wote na viumbe wote.

Basi na ifahamike kwamba kila wanapoheshimiwa na kutukuzwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu tendo hilo (kwa asili) ni kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Na hauthibitiki ukweli wa Tauhidi ila pale kila kitu kitakapotendwa kiwe ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na katika njia yake, na hapo ndipo itakapokuwa kila kitu kinaanzia kwa Mwenyezi Mungu na kila kitu kinaishia kwake.

Tutazungumzia maana ya Ibada katika sehemu ifuatayo kwa undani, ama sasa hivi utafiti wetu utahusu kutabaruku kwa athari za Mawalii, na utafiti huu tutalazimika kuulekeza kwenye kipimo cha Qur'an na Sunna ya Mtume [s] ili haki iweze kubainika.

MTAZAMO WA QUR'AN JUU YA KUTABARUKU

Katika Qur'an tunatosheka na aya moja tu, nayo ni ile inayomnukuu Nabii Yusuf [a] akisema:

"Nendeni na kanzu yangu hii mukaiweke usoni kwa baba yangu (macho yake yatarudi) ataona".

Qur'an, 12.93.

Nabii Yusuf aliituma kanzu yake kwenda kwa baba yake na akawaambia ndugu zake "Nendeni na kanzu yangu hii na muiweke usoni kwa baba yangu ili macho yake yarudi apate kuona.

Mwenyezi Mungu anasema:

"Na alipokuja mtoaji habari njema, aliiweka kanzu ile usoni kwake na macho yalirudi akaona".

Qur'an, 12:96.

Aya hii iko wazi kutoa ruhusa ya kutabaruku kwa athari za Manabii na Mawalii kiasi kwamba hata Nabii anatabaruku kwa Nabii mwenziwe kama hivi Nabii Yaqub [a] anatabaruku kwa kanzu ya Nabii Yusuf [a].

Na ni wazi kabisa kwamba kuponya kunatoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yeye ndiye mtendaji halisi, isipokuwa kutabaruku kwa kanzu ya Nabii kumekuwa ni wasila wa kuponya kama tunavyotumia dawa kuwa ni wasila wa kupona kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Ewe msomaji ingekuwaje kama kutabaruku kwa Nabii Yaqub kwa kanzu ya mwanawe Yusuf kungelitokea mbele ya watu wa Najdi na wafuasi wa Muhammad Ibn Abdul-Wahab, wangelihukumu namna gani jambo hili?

Je, wangehukumu kuwa ni kafiri au mshirikina au mwenye dhambi? Wakati yeye ni Nabii na ni maasum?

Kutabaruku kwa Waislamu kwenye kaburi la Mtume [s] na makaburi ya watu wa nyumba yake na pia athari zao hakuna tofauti na kutabaruku alikotabaruku Nabii Yaqub [a] kwa kanzu ya mwanawe Yusuf [a].

KUTABARUKU NA SERA YA WAISLAMU

Mtazamo wa haraka katika sera ya Waislamu kuanzia kwa Masahaba mpaka leo, unatuonyesha wazi sunna inayofuatwa kuhusu kutabaruku kwa Mtume [s] yeye mwenyewe na athari zake tukufu katika kpindi chote cha historia ya Uislamu.

Na katika maelezo yafuatayo tutaeleza mifano michache inayohusu kutabaruku:

  1. Bibi Fatma Az-Zahra ambaye ndiye mwanamke bora ulimwenguni na ni binti ya Mtume [s], alifika kwenye kaburi la baba yake na akachukua gao Ia udongo wa kaburi akawa anaunusa na kulia huku akisema:
  2. "Mtu aliyenusa udongo wa kaburi la Ahmad, halaumiwi iwapo hatanusa mafuta mazuri ya ghaliya."

    Yamenipata milele masaibu ambayo lau yangeliupata mchana ungegeuka na kuwa usiku. Wameitaja Qadhiya hii wanahistoria wengi miongoni mwao ni As-Samhudi.[151]

    Kwa hakika kitendo hiki cha Bibi Fatma Az-Zahra ambaye ni maasum kinajulisha kwamba kutabaruku kwenye kaburi la Mtume [s] ni jambo linalofaa na pia kutabaruku kwa udongo wa kaburi lake.

  3. Bilal ambaye alikuwa ni muadhini wa Mtume [s] alipata kuishi Shamu katika kipindi cha utawala wa Omar Ibn Khattab. Siku moja alimuona Mtume [s] katika ndoto anamwambia:
  4. "Ewe Bilal mbona umenitupa kiasi hiki, je haujakufikia wakati

    wa kunizuru ewe Bilal?"

    Basi Bilal alizindukana usingizini akiwa na huzuni na khofu nyingi na alipanda kipando chake kuelekea Madina na akafika kwenye kaburi la Mtume [s] akawa analia pale kaburini huku anausugua uso wake kwenye kaburi, mara Hasan [a] na Husein [a] wakafika, Bilal akawakumbatia na kuwabusu....[152]

  5. Ibn Hajar anasema:
  6. "Kila mtoto aliyezaliwa katika zama za uhai wa Mtume [s] huhukumiwa kwamba alimuona Mtume [s], na hii ni kwa sababu Ansar wote walikuwa wakiwaleta watoto wao kwa Mtume [s] kwa ajili ya Tahnik[153] na kupata baraka kiasi kwamba imesemwa kuwa: Wakati Makka ilipotekwa na (Waislamu), watu wa Makka wakawa wanakuja kwa Mtume [s] wakiwa na watoto wao ili awaguse vichwa vyao na awaombee baraka".[154]

    Na kuhusu jambo la kutabaruku, mwandishi wa kitabu kiitwacho, "Tabar-rukus Sahabah" amesema: "Hapana shaka kwamba athari za Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (ambaye ni) mbora kuliko viumbe wote na mbora kuliko mitume wote, kuwepo kwake ni jambo lenye kuthibiti na ni mashuhuri mno. Basi kwa hiyo athari hizo ndiyo bora kutabaruku kwazo, na idadi kubwa ya Masahaba wameziona na wakaafikiana kutabaruku kwazo na kuzipa umuhimu wa kuzikusanya nao Masahaba ndiyo watu waongofu na ni kiigizo kizuri, kwani walitabaruku kwa nywele zake na maji aliyotawadhia na jasho lake na nguo zake na pia kuugusa mwili wake na mengineyo yanayofahamika katika athari zake tukufu ambazo zimesihi khabari zake toka kwa watu wema.[155]

    Yanatosheleza maelezo aliyoyataja Muslim katika Sahih yake kuhusu kutabaruku aliposema:

    "Hakika Mtume [s] alikuwa akiletewa watoto naye huwafanyia tahnik.[156]

  7. Masahaba walikuwa wakitabaruku kwa maji ya udhu aliyotawadha na aliyokoga Mtume [s]:

    Bukhari amopokea hadithi isemayo: "Mtume [s] alitutokea katika kipindi cha jua kali, akaletewa maji ya kutawadha na akatawadha, basi watu wakawa wanachukua maji ya udhu atawadhayo Mtume [s] wanajipangusia".[157]

    Kuhusu jambo hilo kuna riwaya nyingi zilizojaa katika vitabu vya hadithi.

  8. Masahaba walikuwa wakitabaruku kwa nywele za Mtume [s] kama alivyopokea Anas kwamba:
  9. "Mtume [s] aliponyoa kichwa chake, Abu Tal-ha alikuwa ni mtu wa kwanza kuchukuwa nywele za Mtume ([s]).[158]

    Anas anaposema "Abu Tal-ha ndiyo mtu wa kwanza kuchukua nywele za Mtume [s]" inaonyesha wazi kuwa Masahaba walishindana katika kutabaruku kwa nywele za Mtume [s] lakini Abu Tal-ha alikuwa wa kwanza kuzichukua.

    Na imepokewa tena kwamba: "Mtume [s] alifika Mina akaenda kwenye Jamrah akalipiga, kisha akaenda kwenye makazi yake hapo Mina, kisha akamwambia kinyozi, "ninyowe," na akaashiria upande wa kulia kisha kushoto kisha akaendelea kuwapa watu (nywele zake)".[159]

  10. Masahaba vile vile walikuwa wakitabaruku kwa chombo alichokuwa amenyewea Mtume [s]:

    Abu Bar-da amesema: "Abdullah bin Salaam aliniambia, "Je, nisikunyweshe kwenye chombo alichonywea Mtume?"[160]

    Riwaya hii inaonyesha kwamba, Abdallah bin Salaam alikuwa amekihifadhi chombo hicho kwa kuwa kilikuwa kimepata baraka kwa sababu mjumbe wa Mwenyezi Mungu alinywea chombo hicho.

  11. Pia Masahaba walikuwa wakitabaruku kwa mikono yake Mitukufu:
  12. "Imepokewa toka kwa Abu Juhaifah amesema, "Mtume alitoka katika siku yenye joto kali akaenda mpaka Bat-haa akatawadha kisha akaswali Adhuhuri rakaa mbili na Al-asr rakaa mbili.... watu wakasimama wakaishika mikono yake wakawa wanajipangusia nyuso zao.

    Anasema Abu Juhaifah, "Nikauchukua mkono wake nikauweka usoni kwangu, basi niliuona ubaridi mno kuliko theluji na una harufu nzuri kuliko miski".[161]

  13. Pia wakitabaruku kwenye mimbari yake tukufu:

    Imepokewa toka kwa Ibrahim bin Abdur-Rahman bin Abdil-Qari kwamba yeye alimuona Ibn Omar ameweka mkono wake kwenye Mimbar mahala ambapo Mtume [s] alikuwa akikaa, kisha akauweka nikono wake usoni kwake.[162]

  14. Vile vile walikuwa wakitaka uponyo kwenye kaburi lake tukufu:

    Imepokewa toka kwa Imam Ali [a] kwamba yeye amesema, "Kuna bedui alikuja kwetu baada ya kuwa tumemzika Mtume [s] kiasi cha siku tatu zimepita, akajitupa kwenye kaburi Ia Mtume [s], akajipaka kichwani udongo wa kaburi Ia Mtume [s] na akasema, ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ulisema tukasikia usemi wako na uliyapokea toka kwa Mwenyezi Mungu, nasi tulipokea toka kwako na miongoni mwa yale ulioteremshiwa na Mwenyezi Mungu ilikuwa, lau wao watazidhulumu nafsi zao wangekujia... nami nimedhulumu (nafsi yangu) na nimekujia unitakie msamaha". Basi palisemwa kutoka kaburini "Hakika umesamehewa."[163]

Kwa kifupi, iwapo mtu atavirjea vitabu vya historia (As-sihah na As-Sunan na Masanid) ataona ni jinsi gani Masahaba na Tabiina walivyokuwa wakitabaruku kwa kila kitu ambacho kinamafungamano na Mtume [s], na walikuwa wakitaka kuponywa kwenye kaburi lake kwa kuweka mashavu yao juu ya kaburi na kuunusa udongo wa mahali hapo na kulia kwenye kaburi la Mtume [s].

Zaidi ya hapo, walikuwa pia wakitabaruku kwa fimbo ya Mtume [s] na mavazi yake na kuswali sehemu alizokuwa akiswali au alimopita.

Na masimulizi yanayozungumzia jambo la kutabaruku ni mengi mno na haiwezekani kwa mtu mwenye akili kusema eti masimulizi haya ni ya kutungwa tu.

Basi yatakuwaje ni ya kutunga wakati Bukhari na Muslim pamoja na wanachuoni wengine wa hadithi wameyapokea? Isitoshe hali hii, bali wanachuoni wawili wakubwa wamesimamia ukusanyaji wa riwaya hizi na kuzifafanua pamoja na kutaja rejea zake.

Wa kwanza ni, Al-Ustadh Sheikh Muhammad Tahir Makki katika kitabu chake kiitwacho "Tabar-rukus-Sahabah Bia'thari Rasulillah".

Wa pili ni, Al-Ustadh Sheikh Ali Ahmadi katika kitabu chake madhubuti kiitwacho "At-Tabar-ruk". Yeye amefafanua kwa undani habari zote zilizokuja kuhusu Tabar-ruk; na kitabu hiki kinahesabiwa kuwa bora cha zama hizi.

Basi watasemaje Mawahabi juu ya hadithi hizi ambazo ni mutawatiri kimatamko na kimaana?

Na ni upi msimamo wao kutokana na ukweli huu ulio wazi?

Basi ni za nini kelele hizi wazipigazo dhidi ya kutabaruku kwenye kaburi la Mtume [s] jambo ambalo Masahaba na Tabiina wamekuwa wakilifanya bila ubaya wowote wala kulipinga au kuliharamisha, wakati hatuoni popote kwamba Mtume au Masahaba wake waliharamisha jambo hili.

Na ni kwa nini Mawahabi hawawaachi Waislamu walibusu kaburi la Mtume [s] na wapate baraka zake na waonyeshe hisiya zao na mapenzi yao kwa Mtume [s]?

Je, Mawahabi hawajuwi kuwa, kukataza kutabaruku kwenye kaburi la Mtume na athari zake ilikuwa tabia na kazi ya Bani Ummayya hasa Mar-wani aliyelaaniwa na Mtume [s]?

Hebu soma mapokezi aliyoyapokea Al-Hakim ndani ya Mustad-rak yake kutoka kwa Dawuud bin Salih amesema:

"Sika moja Mar-wan alikuja akamkuta mtu ameweka uso wake juu ya kaburi (la Mtume [s]) akamshika shingoni kisha akamwambia, "Je unafahamu unachokifanya"?

Kumbe mtu yule alikuwa Abu Ayyubul-Ansari, akamjibu, "Ndiyo mimi sikulijia jiwe hapa nimemjia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu".

Nimemsikia mjumbe wa Mwenyezi [s] akisema:

"Msiililie dini (msiihuzunikie) kama watawala wake ni watu wanaostahiki lakini ililieni dini watakapoitawalia wasiostahiki".[164]

Mar-hum Sheikh Al-Amini amesema:

"Hadithi hii inatufahamisha kwamba kuzuwiya kutawas-sal kwenye makaburi matakatifu ni miongoni mwa Bid'a za Banu Ummayya na upotevu wao tangu zama za Masahaba na hakuna hata sikio moja kabisa lililopata kumsikia Sahaba akipinga tawas-sul hiyo isipokuwa Mar-wan mdhalimu aliyetokana na kizazi cha Umayya".

Ni kweli "Ng'ombe huilinda pua yake kwa pembe zake". Ni kweli pia kwamba "Kwa kisingizio cha kumtafuta njiwa, muwindaji hula tende (za shamba la mitende aliloingia).

Ukweli ulivyo ni kwamba Banu Ummayya na hasa Mar-wan, wanayo chuki dhidi ya Mtume [s] tangu siku ile Mtume [s] alipokuwa hakubakisha heshima yoyote ya Banu Ummayya, ila aliivunja wala cheo chochote ila alikiharibu na wala nguzo yao yoyote isipokuwa aliivunja na hayo yametokea kutokana na maneno makali ya Mtume [s] kuhusu Bani Ummayya ile siku ya Badri alipowapiga. Mtume [s] hasemi lolote kwa matamanio ya nafsi yake ila ni wahyi aliyopewa (aliyemfundisha Bwana Mtume ndiye mwenye nguvu zote) kwani imepokewa hadithi sahihi kuwa Mtume [s] amesema, "Itakapofika idadi ya Banu Ummayya watu arobaini watawafanya waja wa Mwenyezi Mungu kuwa ni watumwa, na mali ya Mwenyezi Mungu wataipora na kuifanya knwa ni mali yao na watakitumia vibaya kitabu cha Mwenyezi Mungu".[165]

Umeona jibu la Abu Ayyubul-Ansari kwa Mar-wan pale alipomuuliza unafanya nini? Akawa amejibu, sikujia jiwe bali nimemjia mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Hapa tunamuona Abu Ayyubul-Ansari anaeleza kwamba:

"Makusudio ya kutawas-sal na kutabaruku ni kwa Mtume [s] ambaye tunaitakidi kuwa hapana tofauti baina ya kuwa yu hai au amekufa katika suala hili, lakini udongo na jiwe havina umuhimu wowote, isipokuwa udongo na jiwe vilivyopo kwenye kaburi la Mtume [s] vimepata heshima na utukufu kwa sababu ya Mtume [s].

Ewe msomaji mpendwa, Bukhari ambaye kitabu chake kinazingatiwa na Masunni kuwa ndiyo kitabu sahihi mno kuliko vingine, yeye ameweka mlango aliouita "Babu Ma-dhukira Min Dir-in-nabi wa asahu wa Saifahu wa qadahahu wa khatamahu wa mas-ta-amalal-khulafan baadahu.

Yaani mlango unaozungumzia habari za deraya ya Mtume, panga lake na fimbo yake, kikombe chake, pete yake na vitu walivyovitumia makhalifa waliokuja baada yake katika vitu ambavyo havikugawanywa na nywele zake, na viatu vyake na vyombo vyake ambavyo Masahaba wa Mtume na wengineo walikuwa wakitabaruku kwa vitu hivyo baada ya kufa Mtume [s]. [166]

Kama Mawahabi watazifuatilia hadithi hizi nyingi zaidi ya mia hawatakuwa na njia isipokuwa kukubali ukweli na kukiri iwapo tu watakuwa miongoni mwa wale wanaosikiliza maneno na kufuata yaliyo bora, vinginevyo: "Siku ya Hukumu imewekewa wakati maalum".

[151] (1) Wafaul-wafa cha As-samhudi, juz. 2, uk. 444 (2) Sul-hul-ikh-wan cha Al-Khalidi, uk. 57 na wengine.

[152] Usudul-ghabah cha Ibnil Athir, juz. 1, uk. 28.

[153] Tahnik: Maana yake ni kuweka asali kwenye dole gumba na kumrambisha mtoto ndani ya kinywa sehemu ya juu.

[154] Al-Isabah, juz. 3, uk. 63.

[155] Tabar-rukus Sahabah, uk. 5.

[156] Sahih Muslim, juz. 3, uk 1691.

[157] Sahih Bukhari, juz. 1, uk. 59, Fat-hul-bari, juz. 1, uk. 256.

[158] Sahih Bukhari, juz. 1, uk. 54.

[159] Sahih Muslim, juz. 3, uk. 947.

[160] (1) Sahih Bukhari, juz. 7, uk. 147 (2) Fat-hul Bari, juz. 10, uk. 85.

[161] Sahih Bukhari, juz. 4, uk. 188.

[162] AI-tabaqatul-kubra, juz. 1, sehemu ya pili, uk. 13.

[163] Kanzul-Ummal, juz. 2, uk. 248, Wafaul Wafa, juz. 2, uk. 1361.

[164] Mustad-rak Al-Hakim, juz. 4, uk. 515.

[165] Al-Ghadir, juz. 5 uk. 129-130

[166] Sahih Bukhari, juz. 4, uk. 82, kilichochapishwa mwaka 1314 A.H.