KUADHIMISHA KUZALIWA KWA MAWALII WA MWENYEZI MUNGU NA KUFA KWAO

Je, kuadhimisha uzawa na vifo vya Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni Bid'a?

Hakika Mawahabi wao wanadai kuwa, kufanya maadhimisho hayo ni haramu.... kwa madai yao haya, wanaonyesha wazi chuki na uadui walionao dhidi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu na viongozi wa Uislamu, hasa pale wanapozuwia kufanyika mikusanyiko ya kusherekekea kuzaliwa kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu na ile ya kuomboleza vifo vyao.

Wahabi mmoja ambaye ni Rais wa kikundi cha "AnsarusSunnatil-Muhammadiya" aitwaye "Muhammad Hamid Faqii", katika hashiya yake juu ya kitabu kiitwacho AI-Fat-hul-majid anasema:

"Kumbukumbu zilizojaa katika Miji (ya Kiislamu) kwa nia ya kuwakumbuka Mawalii (wa Mwenyezi Mungu) yote hayo ni miongoni mwa aina za kuwafanyia ibada Mawalii hao na kuwatukuza".[141]

Ukweli ulivyo ni kwamba, sababu ya msingi ya upotovu wa Kiwahabi katika mambo haya ni kuwa, wao Mawahabi mpaka sasa hawajaifahamu maana ya "Tauhidi, shiriki na ibada".

Na kwa sababu hii basi, wao wanachukulia kila aina ya kuwaheshimu Mawalii wa Mwenyezi Mungu kuwa ni kuwafanyia ibada na ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika utaona kwamba, mtunzi huyo wa Kiwahabi amefanya mambo bila kuwa na muelekeo hali ambayo imemfanya achanganye baina ya maneno mawili "Ibada" na "Kutukuza".

Yeye ameyataja maneno haya kuwa kila moja lina maana sawa na ya lile lingine, akidhani kwamba maana ya maneno haya mawili ni moja.

Ama kwa upande wetu sisi, baadaye tutazungumzia neno "Ibada" na maf-humu yake katika mlango ujao, na tutatoa uthibitisho kwamba, siyo kabisa kila wanapotukuzwa na kuheshimiwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, basi hiyo iwe ni kuwafanyia ibada.

Sasa hivi hebu mazungumzo tuyaelekeze upande wa ruhusa ya kuyaheshimu (Maadhimisho ya) uzawa na kufa kwa Mawalii hao kwa mujibu wa muongozo wa Qur'an tukufu.

Katika mambo ambayo hayana shaka ndani yake ni kuwa, Qur'an Tukufu imewataja Manabii wengi kwa maneno ya kuwasifa na kuwatukuza na kuwaheshimu.

Kwa mfano:

1. Qur'an inasema kumhusu Nabii Zakariyya na Yahya na wengine kama ifuatavyo:

"Bila shaka wao (Manabii) walikuwa wepesi wa kufanya mema, na wakituomba kwa shauku na khofu na walikuwa wakitunyenyekea".

Qur'an, 21:90.

Basi iwapo kutafanywa Mah-fali ya kuwatukuza manabii hawa, kisha akasimama mzungumzaji akazungumzia habari zao kama zilivyokuja katika Qu'ran kwa maneno ya kuwasifu na akawataja kva utukufu na heshima...basi je, kufanya hivyo atakuwa kafanya kosa?

Ilivyo sawa ni kwamba atakuwa ameifuata Qur'an!

2. Qur'an inasema tena kuhusu watu wa nyumba ya Mtume [s]:

"Na huwalisha chakula katika mahaba yake, masikini, mayatima na wafungwa...

Qur'an, 76:8.

Sasa basi, iwapo watakusanyika wafuasi wa Amirul Muuminina Ali bin Abi Talib [a] katika kumbukumbu ya siku tukufu aliyozaliwa, na kisha mzungumzaji wao (kwenye mkusanyiko huo) akasema "Kwa hakika Imam huyu yeye ni miongoni mwa hao watu waliotoa chakula chao kumpa masikini, yatima na mfungwa). Je! Hi itakuwa na maana kwamba wamemuabudia?

Kwa hiyo basi, hali ni hiyo hiyo katika munasaba wa (maadhimisho ya kumbukumbu ya) kuzaliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu [s].

Tunapofanya sherehe kubwa siku ya kuzaliwa kwa Mtume [s] na tukazizungumzia aya za Qur'an ambazo zimemsifu Mtume [s] au tukazitafsiri aya hizo kutoka katika lugha ya Kiarabu na kuziweka katika lugha nyingine - kutegemeana na hafla yenyewe ilivyo, au tukataja maana ya aya hizo katika mfumo wa kishairi au mfano wake, basi ni kwa nini kwa kitendo hiki tuwe ni waasi wa dini ya Mwenyezi Mungu?

Kwa hakika Mawahabi, wao ni maadui wa heshima na utukufu wa Manabii, na Mawalii na uadui wao wanauvalisha vazi la (kutetea) dini na wanasema: "Hakika kuwatukuza na kuwaheshimu Manabii na Mawalii ni Bid'a", ili wawazuwiye Waislamu kufanya maadhimisho haya.

Ewe msomaji mpendwa: Hakika maudhui wanayoipinga na kuikemea Mawahabi kwa kupitia madai yao batili, ni ile ya kufanya hafla kwa ajili ya kumbukumbu za Mawalii wa Mwenyezi Mungu.

Mawahabi wanadai kwamba, kwa kuwa sherehe hizo zinafanywa kwa Jina Ia Uislamu, basi hapana budi Uislamu uzikubali kwa N-nass maalum au ya jumla vinginevyo zitakuwa ni bid'a na ni haramu.

Jawabu la madai haya liko wazi mno, kwani aya nyingi za Qur'an zinazotufanya tuone umuhimu wa kumheshimu na kumtukuza Mtume [s] zinatosha kuruhusu na kwamba mahfali hizi na maadhimisho haya, hayafanywi isipokuwa ni kwa ajili tu ya kuwaheshimu Manabii na Mawalii (wa Mwenyezi Mungu).

Basi lengo la maadhimisho haya na mahfali hizi ambazo Mataifa yote ulimwenguni yanaziadhimisha, siyo jingine bali ni kuwapa heshima na daraja watu mashuhuri, kadhalika maadhimisho haya siku zote yamekuwa yakifanywa na Mataifa yote ya Kiislamu ukiondoa tu kikundi hiki kipotofu cha kutoka Najdi (Mawahabi).

Lau ingekuwa kitendo hiki ni bid'a na ni jambo jipya linalokwenda kinyume na sheria ya Kiislamu, basi wanachuoni wa Kiislamu katika nchi zote za Kiislamu wao wenyewe wasingefanya mahfali haya wala wasingeshiriki kutoa hotuba na kusoma visomo mbali mbali ambavyo huzidisha mazingatio na furaha kwenye mahfali hizo.

QUR'AN NA KUWATUKUZA MANABII NA MAWALII:

Hivi sasa tunataja baadhi ya ushahidi kutoka katika Qur'an unaoruhusu kuwatukuza Manabii na Mawalii kama ifuatavyo:

Aya ya Kwanza: Qur'an inawaunga mkono watu walionitukuza Mtume [s] na inasema: "Basi wale ambao wamemuamini yeye (Mtume [s]) na wakamheshimu na kumsaidia na wakaifuata nuru iliyoteremshwa pamoja na (Qur'an) hao ndiyo wenye kufaulu.[142]

Kwa hakika maneno yaliyokuja katika aya hii ni haya yafuatayo:

1. Amanu Bih.. Waliomuamini

2. Az-Zaruhu.... Wamemheshimu

3. Nasaruhu.... Wamemsaidia

4. It-tabaun-nura... Wameifuata nuru.

Je, hivi kuna yeyote awezaye kusema kuwa maneno haya na sifa hizi zinahusika tu (kutumika) katika zama zile (alizoishi) Mtume [s]?

Kamwe haiwezekani kabisa!!! (Kudai namna hiyo).

Ilipokuwa hakuna kabisa uwezekano huo, basi neno "Az-zaruhu" ambalo maana yake ni kutukuza na kuheshimu,[143] litakuwa linaenea katika zama za uhai wa Mtume [s] na baada ya kufa kwake. Basi Mwenyezi Mungu anataka kipenzi chake mteule (Mtume Muhammad [s]) awe ni mwenye kutukuzwa na kuheshimiwa siku zote.

Sisi tunajiuliza: Je, kufanya mahfali siku ya kuzaliwa Mtume [s] na siku aliyotangaza utume wake na kusoma khutba na Qasida siyo utekelezaji ulio wazi wa kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema "Az-zaruhu" yaani wamemheshimu?

Ni ajabu kwamba Mawahabi hawa wanawapa heshima kubwa zaidi viongozi wao na watawala wao, na sisi tunapofanya chini ya heshima hiyo kwa Mtume [s] au kwa mimbari yake au Mihrabu yake wao hudai kuwa ni bida'a na ni shirki.

Kwa hakika Mawahabi kwa itikadi yao hii kavu (isiyo hai) wanaharibu heshima ya Uislamu mbele ya mtazamo wa ulimwengu kwa jumla, na wanasababisha Uislamu ueleweke kuwa ni dini isiyokuwa na hisia za kiutu na haina maono ya kiuanadamu na ina upungufu wa kila aina katika kuheshimu na kutukuza na inapinga kuwaheshimu wakubwa zake na viongozi wake.

Mawahabi wanaufanya Uislamu uonekane kuwa na upungufu wa kila aina katika (suala zima la) kuwaheshimu na kuwatukuza viongozi wake na kwamba Uislamu unapinga mambo hayo.

Na kwa sababu hii basi Mawahabi wanawafanya watu wawe na chuki na Uislamu na kuwaacha wakiupinga na kuuchukia.

Yote haya wayafanyayo ni kinyume kabisa na Uislamu ambao, Mwenyezi Mungu ameufanya kuwa ni dini nyepesi yenye ukarimu inayokubaliana na maumbile ya watu, na inakwenda sambamba na huruma za kiutu, na pia kwa uzuri wake inawavutia watu mbali mbali kuikubali.

Aya ya Pili: Kikundi cha Mawahabi ambacho kinapinga kila namna ya maombolezo na kuwalilia mashahidi waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu, kinasemaje juu ya mambo yaliyompata Nabii Yaqub [a]? Lau Nabii huyu Mtukufu angekuwa hai anaishi miongoni mwa watu wa "Najdi" na wafuasi wa Muhammad bin Abdul-Wahabi, wangelimhukumu vipi Nabii huyu?

Kwa hakika Nabii Yaqub [a], alikuwa akilia usiku na mchana kwa kutengana na mwanawe Yusuf [a]., na alikuwa akiomboleza na kutaka kujua habari zake na kutaja jina lake mpaka "Macho yake yakawa meupe kutokana na huzuni naye alikuwa amejawa na huzuni."[144]

Nabii Yaqub alikuwa akikabiliwa na kila aina ya misiba na macho kuwa meupe na huzuni ya moyo na machungu ya kutengana na mwanawe, lakini hakumsahau mwanawe, bali alikuwa akizidi kuwa na hamu kwa mwanawe kila muda wa kukutana naye ulivyokaribia, kiasi cha kuweza kunusa harufu ya Yusuf [a] kutoka masafa ya mbali. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema akimnukuu Nabii Yaqub [a]: "Hakika mimi nahisi harufu ya Yusuf, lau msingekuwa mnaitakidi kuwa nimeharibikiwa na akili (ningenisadiki)".[145]

Basi yatakuwaje mapenzi haya na kudhihirisha uhusiano wenye nguvu katika uhai wa huyu mwenye kupendwa (Yusuf [a] kuwa ni tendo linalofaa na linaafikiana na Tauhidi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu - lakini mapenzi hayo hayo na tangazo la uhusiano huo huo ugeuke kuwa bid'a, tena haramu baada ya kufa kwake?!!!

Inavyoeleweka ni kwamba, kutengana na mtu umpendaye kwa kufariki kwake, ni jambo linalouacha moyo ukiungua kwa majonzi na huzuni na machungu mengi kuliko kutengana naye hali akiwa yu hai.

Basi leo iwapo waumini watakusanyika (ambao wanafanana na Yaqub [a] katika kuhuzunika kwake) wakaomboleza kifo cha Walii fulani miongoni mwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu (kama vile Maimamu watukufu ambao kutokana na matatizo yaliyowapata wanafanana na Yusuf bali misiba yao ni mikubwa kuliko ule wa Yusuf) wakafanya kumbukumbu za Walii huyo mwema, kwa hotuba na Qasida, pia wakairejea sera yake na tabia zake tukufu na mambo yake mengine mazuri, kisha wakalia machozi ya mapenzi na huruma juu yake... Je, maana ya matendo yao haya ni kwamba watakuwa wamemuabudu Walii huyo?!!!

(Kuitakidi kuwa wamemuabudu Walii huyo) ni uchache wa kufikiri na uchambuzi wa mambo pia ni uchache wa maarifa na kufahamu!!!)

Aya Ya Tatu: Mwenyezi Mungu anasema: "Waambie sikutakeni malipo yoyote (juu ya kuwaleteeni Uislamu) isipokuwa muwapende Al-Qurbaa".[146]

Miongoni mwa mambo yasiyo na shaka ndani yake ni kwamba, kuwapenda Al-Qurbaa ni moja ya mambo ya faradhi kidini, faradhi ambayo Qur'an imelitolea ushahidi wa wazi mno jambo hili.

Sasa basi, iwapo mtu atataka kuutekeleza wajibu huu (wa kuwapenda Al-Qurbaa) baada ya kupita karne kumi na nne, basi atafanya nini katika hali kama hii?!!!

Je, siyo kwamba anachotakiwa ni kufurahi kwa yale yaliyowafurahisha na ahuzunike kwa yale yaliyowahuzunisha?!!!

TAN-BIH:

Zimekuja hadithi nyingi kutoka kwa Mtume [s] kwamba, maana ya Al-Qur-baa ni watu wa nyumba ya Mtume [s].

Basi iwapo mtu ataadhimisha hafla maalum kwa ajili ya mmoja wa watu hao watukufu, akamsifu Mtukufu huyo na kuyaeleza maisha yake yaliyoambatana na mema na sifa zake njema, pia namna alivyojitolea (katika dini) na akaeleza matatizo na misiba iliyompata Mtukufu huyo... basi je atakuwa kafanya kitendo cha haramu? Au atakuwa amehuisha utajo wa Mtukufu huyo na kumtekelezea yale Mawadda (mapenzi) yaliyowajibishwa (katika aya iliyotajwa hapo kabla)?

Na lau mtu yeyote katika kuzidisha upendo kwa hao Al-qurbaa atamtafuta yeyote mwenye nasaba na hao Al-qurbaa na akaja kuzuru makaburi yao, na akasimamisha visomo kwenye makaburi hayo. Je, watu wenye akili na utambuzi wa dini hawataona kuwa mtu huyo anatekeleza faradhi ya kuwapenda Al-Qur-baa?

Labda Mawahabi watuambie kuwa: "Ni wajibu kuyaficha moyoni na kutoyadhihirisha kwa namna yoyote ile mapenzi (kwa Al-Qurbaa)...."

Inafaa kusema, zama alizoishi Mtume [s] na baada yake, zilikuwa na mabadiliko ya itikadi na fikra, basi zama hizi zinashuhudia kukubaliwa kwa Uislamu na mataifa mbali mbali na watu wa aina tofauti, na ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema:

"Na utawaona watu wanaingia katika dini ya Mwenyezi Mungu makundi kwa makundi".[147]

Uislamu ulikuwa ukiwalea wote wanaosilimu na kutosheka na shahada mbili tu hapo mwanzoni, na wao walikuwa wakibakia katika utamaduni wao na desturi zao.

Na wala Mtume [s] na waliokuja baada yake hawakuweka usimamizi juu ya ada ya watu hao na desturi zao na wala hawakuyataka makabila yote kuwa na desturi moja ya kiutamaduni (bali Mjumbe wa Mwenyezi Mungu aliwaacha wakaendelea na desturi na mila hizo ambazo haziendi kinyume na sheria ya Mwenyezi Mungu.)

Kwa hakika kuwaheshimu watu wakubwa na kufanya mikutanao ya maombolezo ya kutaja vifo vyao, na kukusanyika kwenye makaburi yao, pia kudhihirisha upendo kwa ajili yao, yote hayo yalikuwa na bado yanaendelea kuwa ni mambo yanayotendeka katika mataifa yote ulimwenguni.

Na katika zama zetu za leo, utawaona watu wa Mataifa ya Mashariki na Magharibi wanasimama muda wa saa nyingi wakisubiri kwenda kuzuru miili iliyohifadhiwa ya viongozi wao na pia makaburi ya viongozi wao waliopita hapo zamani, na huwa wanababujikwa na machozi kutokana na hisia za kujiona kuwa karibu na miili ya viongozi hao, kisha tendo hili wanalizingatia kuwa ni moja katika namna za kuwaheshimu na kuwatakuza.

Haijapata kupokewa habari kwamba Mtume [s] alikuwa akichunguza mila na desturi za watu kwanza ndipo awakubalie kusilimu, bali alikuwa akitosheka kwa shahada mbili walizokuwa wakizitoa.

Basi lau mila na desturi hizi za (kuheshimu uzawa na kuomboleza vifo vya viongozi wao) zingekuwa haramu na ni aina ya kuwaabudu watu hao bila shaka Mtume [s] angeliwapa sharti ya wao kujitenga na kila aina ya mila na desturi walizonazo ndipo waingie katika Uislamu, lakini Mtume [s] hakufanya hivyo.

Aya ya Nne: Nabii Isa [a] alimuomba Mola wake amteremshie chakula kutoka mbinguni na aifanye siku ya kushuka chakula hicho kuwa ni sikukuu kwake yeye Nabii Isa [a] na wafuasi wake.

Ikimnukuu Nabii Isa [a], Qur'an Tukufu inasema: "Ewe Mola wetu tuteremshie chakula kutoka mbinguni kiwe ni sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu (nao ni sisi) na wa mwisho wetu na kiwe ni ishara itokayo kwako na uturuzuku kwani wewe ndiye mbora wa wanaoruzuku".[148]

Basi je ndugu msomaji, unafikiria kwamba dhati ya Mtume Muhammad [s] ilikuwa na daraja ya chini kuliko kile chakula ambacho Nabii Isa [a] aliifanya siku ya kushuka kwake kuwa ni sikukuu? Ikiwa siku hiyo imefanywa kuwa ni sikukuu kwa sababu ya kuwa chakula hicho ni alama na ishara za Mwenyezi Mungu na muujiza uliotoka mbinguni, basi je hakuwa Nabii wa Uislamu ni alama na ishara kubwa itokayo kwa Mwenyezi Mungu na ni muujiza wa milele?

Basi ole wao na wameangamia wale wanaokubali kuifanya sikukuu siku kiliposhuka chakula hicho toka mbinguni (ambacho hakikuwa na athari isipokuwa kushibisha matumbo yenye njaa) lakini watu hao hao wanaipuuza siku iliyoshuka Qur'an kwa Mtume [s], na pia wanaipuuza siku tukufu aliyotumwa Mtume [s] na zaidi ya kupuuza kwao wanaona kuwa kuadhimisha siku hiyo ni uzushi na ni haramu.

Aya ya Tano: Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tumeutukuza utajo wako".[149]

Hakika kufanya vikao na maadhimisho, ni miongoni mwa kutukuza utajo (wa Mtume [s]) na Waislamu wanapoadhimisha uzawa wa Mtume [s] na siku ya kumbukumbu ya kupewa kwake utume pamoja na maadhimisho mengine ya kidini hakuna kitu kingine wanachokikusudia isipokuwa kutukuza utajo wa Mtume [s] na watu watukufu wa nyumbani kwake. (Amani ya Mwenyezi Mungu iwashukie).

Basi je ni kwa nini hatufuati muongozo wa Qur'an? Je, Qur'an siyo muongozo wetu na kigizo chetu tunachotakiwa kufuata?

Kwa hiyo basi, haifai kabisa kwa mtu yeyote kusema kwamba: "Kuutukuza utajo wa Mtume [s] ni jambo linalomhusu Mwenyezi Mungu tu na kwamba mwingine hahusiki". Kwani kusema namna hii ni kama kusema kwamba kumsaidia Mtume [s] kunamhusu Mwenyezi Mungu peke yake wala haifai kwa yeyote miongoni mwa Waislamu kumsaidia Mtume [s] kwa sababu Mwenyezi Mungu amesema: "Na akusaidie Mwenyezi Mungu kwa msaada wenye nguvu."

Qur'an, 68:3

Kwa hakika lengo la aya kama hizi ni kuwataka Waislamu wamsaidie Mtume [s] na kudumisha utajo wa (sifa zake) na kulihuusha jina lake na sera zake.

MANENO NA MATENDO VA MAWAHABI YANAPINGANA

Ajabu waliyonayo Mawahabi ni kama ifuatavyo:

Ni vipi wanaharamisha hafla ya utajo na uzawa mtukufu wa Mtume [s], Mtume ambaye ndiye aliyewapa wanaadamu wote zawadi kubwa kuliko zote tena ya kudumu (nayo ni Uislamu) na tena Mawahabi kwao wao wanaona kumheshimu Mtume [s] na kuadhimisha uzawa wake ni shirki, lakini wao hao hao ndiyo wanaofanya maadhimisho makubwa kwa ajili ya watu wao na viongozi wao, na wanatoa mamilioni ya Riali (pesa za Kisaudia) ili kufanya maadhimisho haya na ili kuonyesha heshima kwa utumishi wa hao viongozi wao?

Hebu litazame toleo la 102 la jarida la Al-Faisal, (Jarida ambalo uchapishwaji wake ni wa hali ya juu na wa pekee nchini Saudi Arabia) limekusanya kwa urefu maelezo yanayohusu maadhimisho (yao) makubwa ambayo yalifanywa na utawala wa mabavu wa Wasaudiyya kuadhimisha kurejea kwa "Amiri Sul-taan" kutoka katika safari ya anga ndani ya rocket iitwayo "Discovery".

Toleo hili pia limekusanya picha nyingi zinazoonyesha gharama kubwa zilizotumika katika sherehe hizo na limechapisha hotuba na nyimbo zilizoimbwa katika sherehe hizo, isitoshe (limechapisha) sifa zilizosomwa kwenye maadhimisho hayo kuwasifu wafalme wa kizazi cha Saudi kwa jumla na kwa amiri kwake pekee, sifa ambazo zilikuwa ni za kuvuka mipaka mno.

Ewe msomaji, nakuapia kwa Mwenyezi Mungu kwamba, hivi kweli Amiri (wa Kisaudiya) ambaye hakufanya chochote katika safari hiyo isipokuwa aliwafuata wageni wa kimagharibi kwenda

hiyo safari ya anga za juu ambayo iliandaliwa na Wamarekani, anastahiki kuheshimiwa na kutukuzwa na kutolewa mali nyingi na kupiga mizinga bila faida yoyote?

Na eti asistahiki heshima na utukufu huo Mtume [s] ambaye amewakusanya watu katika ukamilifu wa kiroho na amewatoa watu kwenye giza na kuwapelekea kwenye nuru na akawaonyesha ubora wa utu wao na akawaepusha na kila aina za unyonge na upotevu.

Hivi kweli haistahiki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu [s] kudumishwa utajo Mtukufu wa kuzaliwa kwake na kutajwa katika kuadhimisha uzao huo, sifa zake na kazi zake alizozifanya, ikiwemo utumishi wake kwa umma wake na jihadi alizopigana na ukarimu wa Mtume [s] na mengineyo, ili tu kizazi kijacho kifahamu kuwepo na kuendelea kwa matendo na kazi za Nabii huyu Mtukufu? Pia kizazi hicho kijacho kiweze kufahamu namna mbali mbali za matatizo yaliyomkuta Bwana Mtume [s] na jinsi alivyoyakabili akiwa na lengo la kuwaongoa watu.

Na hayafanywi maadhimisho haya na heshima hizi pamoja na kueneza msimamo bora wa Mtume [s] isipokuwa ni kwa lengo Ia kuhimiza kumuiga na kumfuata Mtume [s] na kuhifadhi kumbukumbu zake.

Basi ni kwa nini isifae kumsifu Mtume [s] na kusomwa qasida zinazohusu ubora na utukufu wake, ila eti ifae kukisifu kizazi cha Wasaudiya na maamiri waovu ambao si chochote bali ni madhara na balaa kwa jamii na umma?

Ni kwa kiasi gani basi maneno na matendo ya Mawahabi yanapingana?

Kwa nini Mawahabi wanazuwia kufanyika kwa maadhimisho ya kuzaliwa Mtume Mtukufu kwa hoja ya kuwa eti jambo hili halikuja katika sheria ya Kiislamu, lakim wao hao hao wanafanya sherehe kubwa kwa ajili ya watu wao wa Kisiasa?

Mwenyezi Mungu anasema: "Wanapokutana na walioamini husema: "Tumeamini' na wanapokuwa peke yao kwa mashetani wao husema: "Hakika sisi tu pamoja nanyi tunawacheza shere tu, Mwenyezi Mungu atawalipa shere yao na kuwaacha katika upotofu wao wakitangatanga ovyo".

Qur'an, 2:14-15.

Bila shaka waislamu tangu hapo zamani wamekuwa wakifanya sherehe za kuzaliwa Mtume [s]:

Anasema "Ad-diyar Bakri"

"Waislamu wanaendelea kufanya sherehe katika mwezi aliozaliwa Mtume [s] na kupika vyakula pamoja na kutoa sadaka katika siku za mwezi huo, pia hufurahi na wanafanya kheri nyingi na kusoma Maulidi ya Mtume [s] na huonekana mambo mengi mazuri kwao kutokana na ukarimu wa (Mwezi huu).[150]

[141] Al-Fat-hul-majid, uk. 154.

[142] Qur'an, 7:157

[143] Kitabu Mufradatil-Qur'an cha Ar-Raghib katika mada ya Az-Zara.

[144] Qur'an, 12:84.

[145] Qur'an, 12:94.

[146] Qur'an 42:23.

[147] Qur'an, 11 0:3.

[148] Qur'an, 5.114.

[149] Qur'an, 94:4

[150] Tarikh Al-Khamis, juz. 1, uk 223.