KUWAWEKEA NADHIRI WATU WALIOKUFA

Kabla ya kueleza chochote, tunataja kwanza "Taarifu" ya "Nadhiri".

Maana ya nadhiri ni mtu kuilazimisha nafsi yake kutenda kitu maalum iwapo makusudio yake yatatimia au haja yake ikikubaliwa, na atasema wakati awekapo nadhiri, kwa mfano: "Ni wajibu juu yangu iwapo nitapasi mtihani nitahitimisha Qur'an kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."

Hii ndiyo nadhiri ya kisheria, na ni lazima iwekwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu.

Ikiwa muweka nadhiri atasema: "Nimeweka nadhiri kwa ajili ya mtu fulani, basi usemi wake huo utachukuliwa kuwa ni "majazi", na maana yake itakuwa "Nimeweka nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na thawabu za nadhiri hii ni kwa ajili ya Fulani."

THAWABU ZA NADHIRI

Thawabu za nadhiri zimegawanyika mafungu matatu:

1. Thawabu zake ziwe kwa mwenye kuweka nadhiri

2. Thawabu zake ziwe kwa mtu mwingine aliye hai

3. Thawabu zake ziwe kwa mtu mwingine aliye kufa.

Kwa hiyo muweka nadhiri anaweza kuzihusisha thawabu za nadhiri yake kwake mwenyewe au kwa mtu mwingine aliye hai mmoja au zaidi au kwa mtu aliye kufa mmoja au zaidi. Mafungu yote haya matatu yanafaa na ni lazima kwa yule anayeweka nadhiri kuitimiza nadhiri yake pindi atakapokuwa ametimiziwa haja yake.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amemsifu Imam Ali, Bibi Fatma, Hasan na Husein [a] (kwa kutekeleza nadhiri) aliposema: "Wanatimiza nadhiri."

Qur'an, 76:7

Ewe msomaji, nadhiri ni suna maarufu kwa Waislamu wote ulimwenguni kote, na hasa katika miji ambayo kuna makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu na waja wake wema.

Na ilizoweleka kwa muda mrefu miongoni mwa Waislamu kuweka nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuzitoa zawadi thawabu zake kwa mmoja wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu na waja wake wema, mpaka lilipokuja lile gonjwa baya la kansa (fitna na unafiki wa Ibn Taimiyya) akadai kuwa nadhiri ni haramu na kuwashambulia Waislamu hasa Mashia ambao nadhiri imezoweleka kwao zaidi ya Waislamu wengine kutokana na kuweko kwa makaburi mengi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika miji yao, basi kwa hilo (Ibn Taimiyya) akawatuhumu kuwa wanafanya shirki na upotevu na akasema:

"Yeyote mwenye kuweka nadhiri ya kitu chochote kwa ajili ya Mtume au mwingine miongoni mwa Manabii na Mawalii katika watu waliokufa, au akachinja kichinjo, basi atakuwa kama washirikina ambao huchinja kwa ajili ya masanamu yao na kuyawekea nadhiri masanamu hayo, basi mtu huyo atakuwa anaabudu kisichokuwa Mwenyezi Mungu kwa hiyo atakuwa ni kafiri."[133]

Baadaye tena akaja Muhammad ibn Abdul-Wahab baada ya kupita karne tatu hivi, akaanza kuipiga kelele kama za huyo aliyemtangulia na kuhuisha bid'a na uzuishi wake.

Kwa bahati mbaya sana wawili hawa hawakufahamu au walijifanya hawafahamu kwamba, kipimo cha ujumla ni makusudio na nia ya moyoni kwani "matendo ni kwa niya".

Na kama itahukumiwa kuwa, eti kiasi cha matendo yanavyoonekana ndiyo dalili ya nia ilivyo basi matendo mengi ya Ibada za Hija yanafanana na matendo ya wale waabuduo sanamu kwa yanavyoonekana, kwani wao walikuwa wakitufu kuzunguuka masanamu yao na wakiyabusu, nasi tunatufu kuzunguuka Al-Kaaba tukufu na tunaibusu Hajarul-as-wad, na tunachinja na kufanya Taqarub huko Mina siku ya Idi Al-adh-haa.

Basi je tumekufuru na tumemshirikisha Mwenyezi Mungu katika kutekeleza Ibada hizi?!!!

Kwa hiyo, kipimo ni nia ya moyoni na wala haifai kabisa kuhukumu na kutoa fatwa kwa kiasi cha matendo kama yanavyoonekana. Kwa hiyo kila anayeweka nadhiri kwa mmoja wa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, hakuna anachokikusudia moyoni mwake isipokuwa ni nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuzitoa zawadi thawabu za nadhiri hiyo kwa Walii huyo na wala siyo kinyume chake.

Na kwa bahati nzuri ni kwamba, wanachuoni na wanafikra wa Kishia na Kisunni wameupinga uzushi na upotevu wa Ibn Taimiyyah na waliyo kama yeye.

Hebu msikilize Al-Khalidi akimpinga Ibn Taimiyyah anasema:

"Hakika mas-ala ya nadhiri yatatazamwa kwa mujibu wa nia ya mwenye kuweka nadhiri na kwamba matendo yanategemea nia ya mtendaji, basi kama mwenye nadhiri atamkusudia maiti mwenyewe kuwa ndiyo anamuwekea nadhiri na kujikurubisha kwa maiti huyo, nadhiri hiyo haitafaa kabisa. Na ikiwa nia yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukfu na kuwanufaisha walio hai kwa namna fulani, na thawabu zake apate yule aliyemuwekea nadhiri hiyo sawa sawa akibainisha aina ya manufaa hayo au asibainishe, na kukawa kuna kitu kitakachoendelea kutumika katika mazingira ya watu au ndugu wa maiti au mfano wa hayo, basi katika hali hii ni lazima nadhiri hiyo itimizwe."[134]

Kisha akaeleza mambo waliyoyaweka wazi wanachuoni wa zama zake na waliokuwa karibu ya zama zake juu ya mas-ala haya.

Naye Al-Azzami katika kitabu chake kiitwacho "Fur-qanul-Qur'an amesema:

"Na yoyote atakayefahamu hali ya wanaofanya jambo hilo (nadhiri) miongoni mwa Waislamu, atawakuta katika kuchinja wanakochinja na nadhiri waziwekazo hawawakusudii maiti miongoni mwa Manabii na Mitume isipokuwa wanachokusudia ni kutoa sadaka kwa niaba yao na thawabu ziwaendee wao, nao wanafahamu kwamba Ij-mai ya Masunni imekubaliana kwamba sadaka itolewayo na watu walio hai, huwanufaisha waliokufa na inawafikia, na hadithi zilizotaja jambo hili ni sahihi tena mashuhuri."

Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyosihi na kupokelewa toka kwa Sa'ad, kwamba yeye alimuuliza Mtume [s] akasema:

"Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, hakika mama yangu amefariki na ninafahamu kwamba lau angeishi zaidi ya hapa angetoa sadaka, basi je kama nitatoa sadaka kwa niaba yake itamnufaisha?"

Mtume [s] akasema: "Ndiyo". Sa'ad akauliza: "Ni sadaka ipi yenye manufaa makubwa zidi ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?"

Mtume [s] akasema "Maji".

Basi Sa'ad akachimba kisima na akasema: "Kisima hiki (thawabu zake) ni kwa ajili ya mama wa Sa'ad".[135]

Amekosea sana Muhammad Ibn Abdul-Wahab pale alipodai kwamba, Muislamu atakaposema "Sadaka hii Linnabi (kwa ajili ya Mtume) au Lil- Walii (kwa ajili ya Walii)" eti lamu iliyopo hapa ni ile ile lamu iliyopo kwenye kauli yetu tusemapo "Nadhartu Lillah" yaani nimeweka nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na maana yake ni kuonyesha lengo Ia nadhiri. Lakini maoni haya si sahihi kwa sababu kama sadaka hii itatumika kwa maslahi ya Nabii wakati wa uhai wake na baada ya kifo chake (basi nadhiri itakuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, lakini matumizi yake ni kwa ajili ya maslahi ya Nabii).

Na kwa muelekeo huu anasema Al-Azzami baada ya kukitaja kisa cha Sa'ad:

"Lamu iliyoko kwenye "Hadhihi Liumi Sa'ad" ni lamu inayoonyesha upande ilikoelekezwa thawabu ya sadaka hii, wala haionyeshi kwamba mama wa Sa'ad ni mwenye kuabudiwa na mwanawe, na maana hii ndiyo inayokusudiwa na Waislamu, hivyo wao ni wafuasi wa Sa'ad na wala siyo wenye kuabudu sanamu.

Na lamu hiyo ni kama iliyoko katika kauli yake Mwenyezi Mungu aliposema: "In-namas-sadaqatu Lil-fiqarai" yaani sadaka ni kwa ajili ya mafakiri (wenye kuhitajia), na siyo kama lamu iliyoko kwenye kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema "Rabbi Innii Nadhartu Laka Mafii Bat-ni Muhar-ran" yaani, "Mola wangu nimeweka nadhiri kwako aliyemo tumboni mwangu awe wa kukutumikia"- Qur'an, 3;35.

Aukauli ya msemaji asemapo, "Salaitu Lillahi wa Nadhartu Lillahi", yaani nimeswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na nimeweka nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Atakapochinja mchinjaji kwa ajili ya Nabii au Walii au akaweka nadhiri ya kitu kwa ajili yake, hapo huwa hakusudii ila kumtolea sadaka hiyo na kumpa thawabu za sadaka hiyo.

Na hapo itakuwa ni zawadi toka kwa walio hai kuwapa waliokufa jambo ambalo linakubalika kisheria na lina thawabu.

Mas-ala haya yanadhri yameelezwa kwa urefu katika vitabu vya Fiq-hi na vile vilivyoandikwa kumpinga Bwana huyo (Ibn Taimiyya) na wale wote wanaomfuata".[136]

Bila shaka ewe msomaji imekudhihirikia kwamba inafaa kuweka nadhiri kwa ajili ya manabii na Mawalii bila ya kuwepo mchanganyiko wa shirki katika suala hili, hupata thawabu kwa tendo hilo anayeweka nadhiri iwapo nadhiri hiyo ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kile kinachowekewa nadhiri kikachinjwa kwa jina Ia Mwenyezi Mungu.

Mtu asemapo nimechinja kwa ajili ya Mtume haina maana kuwa kachinja kwa ajili yake bali ana maana ya zile thawabu za kuchinja ndiyo za Mtume, ni sawa na kusema nimemchinja kuwa ajili ya mgeni ambayo itamaanisha manufaa ya kilichochinjwa yatamrejea mgeni, kwani yeye ndiye sababu ya kupatikana kichinjo hicho.

Kuliweka wazi zaidi jambo hili tunataja hadithi iliyopokelewa kwa Thabiti bin Adh-haak amesema:

"Mtu fulani aliweka nadhiri katika zama za Mtume [s] kuchinja ngamia mahala paitwapo "Buwanah" baadaye alikuja kwa Mtume [s] akamweleza, Mtume [s] akasema: Je, hapo Buwanah kulikuwa na sanamu anayeabudiwa miongoni mwa masanamu ya Kijahiliya?"

Wakasema: "Hapana".

Mtume [s] akauliza, "Je, kulikuwepo na sikukuu miongoni mwa sikukuu zao?"

Wakasema: "Hapana". Mtume [s] akamwambia muulizaji, "Timiza nadhiri yako, kwani nadhiri haitimizwi katika kumuasi Mwenyezi Mungu, wala kitu asichokimiliki mwanadamu".[137]

Na imepokewa tena kama ifuatavyo:

Kuna mwanamke fulani alifika kwa Mtume [s] akasema:

"Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu mimi niliweka nadhiri kuchinja mahala fulani ambapo watu wa zama za Jahiliyya walikuwa wakichinja..."

Mtume [s] akasema, Je, hapo kulikuwepo na wathan (kitu chochote kinachoabudiwa)?

Yule mama akasema: "Hapana". Mtume [s] akamwambia: "Timiza nadhiri yako"[138]

Na imepokewa toka kwa Maimuna binti Kardam kwamba, baba yake alimwambia Mtume [s]:

"Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu mimi nimeweka nadhiri, iwapo atazaliwa kwangu mtoto wa kiume, nitachinja kiasi cha mbuzi fulani kwenye kilele cha Buwanah".

Anasema mpokeaji aliyepokea toka kwa Maimuna, sikumbuki isipokuwa yeye alisema hamsini. Basi Mtume [s] akasema, "Je, kuna chochote katika wathan?" Akajibu, "Hapana".

Mtume [s] akasema: "Tekeleza nadhiri yako uliyoiweka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu".[139]

Bila shaka ewe msomaji umeona jinsi ambavyo Mtume [s] amekariri suali la kuwepo masanamu mahali pa kuchinjia?

Hii ni dalili kwamba nadhiri iliyo haramu ni ile ya kukusudia masanamu, kitu ambacho ilikuwa ndiyo desturi ya watu wa Jahiliyya kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu,... "Na kilichochinjwa mahali panapofanyiwa Ibada ya masanamu... hilo kwenu ni dhambi".

Qur'an, 5:3

Na kila atakayetazama kwa makini hali za watu wanaozuru sehemu tukufu na makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu, atafahamu vizuri kwamba watu hao huweka nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na radhi yake na huchinja vichinjo vyao kwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa nia ya kumnufaisha mwenye kaburi kwa thawabu za nadhiri hiyo na kuwanufaisha mafakiri kwa nyama ya hicho kilichochinjwa.

Kwa kumalizia sehemu hii tunataja neno la Al-Khalidi alilolisema baada ya kutaja yale aliyoyapokea Abu Dawud katika Sunan yake.

Amesema Al-Khalidi:

"Ama Makhawarij kutolea kwao dalili hadithi hii kuwa eti haifai kuweka nadhiri mahala walipozikwa manabii na watu wema kwa madai kwamba manabii hao na watu hao wema ni masanamu (Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kauli kama hizi) na nisherehe miongoni mwa sherehe za Kijahiliya, madai yao yote ni miongoni mwa upotevu wao na uzushi wao na ujeuri wao dhidi ya manabii wa Mwenyezi Mungu na Mawalii wake kiasi cha kuwaita kuwa ni masanamu, na kwa kweli inaonyesha wazi dharau kubwa hasa kwa Mitume [a].

Hakika yeyote atakayewadharau japo iwe kwa kinaya atakufuru na toba yake haikubaliwi katika baadhi ya kauli za Maulamaa.

Na watu hawa (makhawariji) ambao Mwenyezi Mungu amewatenga kwa sababu ya ujinga wao wanasema eti kutawas-sal kwa Mitume ni kuwaabudu na wanawaita ni masanamu, hawawaidhiki (hawasikii) watu hawa kwa ujinga wao na upotevu walio nao.

Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi.[140]

[133] Fur-qanul-Qur'an cha Al-Azzami uk. 132 (amemnukuu Ibn Taimiyya)

[134] Sul-hul-ikh-wan cha Al-Khalidi, uk. 102 na kuendelea

[135] Fur-qanul-Qur'an, uk. 133.

[136] Fur-qanul-Qur'an, uk 133.

[137] Sunan Abu Dawud, juz. 2, uk 80.

[138] Sunan Abu Dawud, juz. 2, uk. 81.

[139] Sunan Abu Dawud, juz. 2, uk. 81.

[140] Sul-hul-ikh-wan cha AI-khalidi, uk. 109.