KUTAWAS-SAL KWA MAWALII WA MWENYEZI MUNGU

Mas-ala ya kutawasal Kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu na wapenzi wake ni mas-ala yanayofahamika miongoni mwa Waislamu ulimwenguni kote, na zimekuja hadithi nyingi kuruhusu jambo hili na kulipendekeza.

Kwa hiyo kutawas-sal siyo jambo geni bali ni jambo Ia kidini lililofahamika miongoni mwa Waislamu tangu mwanzoni mwa kuja Uislamu mpaka leo hii, na wala humkuti Muislamu anayelipinga.

Kwa muda wote wa karne kumi na nne tangu kuja Uislamu, hapana yeyote aliyelipinga jambo hili isipokuwa Ibn Taymiyyah na wanafunzi wake katika karne ya nane Hijiriya.

Na baada ya karne mbili akaja Muhammad bin Abdil-Wahab, ambaye yeye wakati mwingine akaona kuwa kutawas-sal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni Bid'a na wakati mwingine akaona kuwa eti ni kuwaabudu Mawalii hao.

Hapana shaka yoyote kwamba kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni shiriki na ni haramu.

Sisi sasa hivi hapa hatufanyi uchunguzi juu ya neon Ibada na uhakika wake ingawa jambo hili ni muhimu sana, lakini tutalizungumzia kwa ufafanuzi katika mahali pake maalum, kwa kuwa sasa hivi tunashughulika na kutawas-sal kwa Mawalii.

Hivyo basi tunasema: Fahamu (ewe msomaji) kwamba, kutawas-sal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kuna namna mbili:

  1. Kutawas-sal kwa Mawalii wao wenyewe nafsi zao kama vile tukisema:
  2. "Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nintawas-sal kwako kwa Mtume wako Muhammad [s] nikubalie haja yangu".

  3. Kutawas-sal kwa cheo cha Mawalii na utukufu waliyonao mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama vile tukisema:
  4. "Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi ninatawas-sal kwako kwa utukufu wa Muhammad na heshima yake na haki yake unikubalie haja yamgu."

Kwa upande wa Mawahabi, wao wanaziharamisha namna zote mbili, wakati ambapo hadithi tukufu za Mtume [s] na sera ya Waislamu vinashuhudia kinyume cha madai ya Kiwahabi na pia vinatilia mkazo kuwa namna zote mbili zinafaa.

Hivi sasa tunataja baadhi ya hadithi hizo moja baada ya nyingine, kisha tutaleta maelezo juu ya sera ya Waislamu, na hapo ndipo itakapoyeyuka na kupotea kauli ya mwenye kuharamisha tawas-sul na kuwa eti ni Bid'a.

HADITHI TUKUFU ZA MTUME [s]

Hadithi zinazojulisha kuwa kutawa-sal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu kunafaa ni nyingi mno, na zinapatikana katika vitabu vya Historia na hadithi.

Katika maelezo yafuatayo tunataja sehemu yake tu:

HADITHI YA KWANZA

Imepokewa toka kwa Uthman bin Hunaif kwamba amesema:

"Mtu mmoja kipofu alikuja kwa Mtume [s] akasema:

"Niombee kwa Mwenyezi Mungu aniponye (upofu)".

Mtume akamwambia, "Ukipenda nitaomba na ukipenda uvumilie na ndiyo bora".

Yule mtu akamwambia Mtume: "Muombe Mwenyezi Mungu (aniponye").

Basi Mtume [s] akamuamuru kipofu yule atawadhe vizuri na aswali rakaa mbili na aombe kwa kutumia Dua hii.

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako Mtume wa Rehma, Ewe Muhammad hakika mimi naelekea kwa Mola wangu kupitia kwako katika haja yangu ili ikubaliwe, ewe Mwenyezi Mungu mfanye Muhammad kuwa muombezi wangu."

Ibn Hunaif anasema:"Basi Wallahi, tulikuwa hatujatawanyika tukiendelea kuzungumza mpaka aliingia kwetu kama kwamba hakuwa na ugonjwa (upofu)".

MAELEZO JUU YA SANAD YA HADITHI HII

Hakuna ubishi katika kusihi kwa Sanad ya hadithi hii, kwani hata huyo Imam wa Mawahabi "Ibn Taimiyyah" ameihesabu kuwa ni hadithi sahihi na akasema kuwa, makusudio ya "Abu Jaafar" jina linalopatikana katika Sanad ya Hadithi hi ni 'Abu Jaafar Al-Khatmi" na huyu Bwana ni mpokezi anayetegemewa. Imekuja katika Musnad ya Imam Ahmad (Abu Jaafar Al-Khatmi). Amma ndani ya Sunan Ibn Majah imekuja (Abu Jaafar) tu.

Mwandishi wa Kiwahabi katika zama hizi aitwaye Ar-Rifai ambaye wakati wote anajaribu kuzifanya dhaifu hadithi zinazohusu Tawas-sul anasema kuhusu hadithi hii tuliyoitaja hapo kabla:

"Hapana shaka kwamba hadithi hii ni sahihi na ni mashuhuri na imethibiti bila wasiwasi wala mashaka (kwamba) macho ya kipofu yule yalirudi (akawa anaona) kwa sababu ya Dua ya Mtume [s]."[110]

Na anasema tena:

"Hadithi hii wameileta An-Nasai na Al-Baihaqi, At-Tabran na At-Tirmidhi na AI-Hakim wao wametaja "Allhumma Shaf-Fihu Fihi" badala ya "Allahumma Shaf-Fihu Fiy-ya."[111]

Mufti wa Makka Zaini Dahlan anasema:

"Bukhari na Ibn Majah na Al-Hakim (ndani ya Mustadrak yake) pamoja na Jalalud-Dinis-Suyuti (katika Jaami' yake) wameitaja hadithi hii na Sanad zake ni sahihi.

Na sisi tunaitaja hadithi hii kutoka katika rejea zifuatazo:

1. Sunan Ibn Majah, Juzuu ya kwanza, uk. 441 ikiwa ni hadithi na 1385, kimehakikiwa na Muhammad Fuad Abdul-Baqii, toleo la Dar-Ihyail-Kutubil-Arabiyya.

Naye Ibn Majah anaeleza kutoka kwa Abu Is-Haqa kwamba yeye amesema:

"Hadithi hii ni sahihi."

Kisha akasema:

"Na ameipokea Tirmidhi katika kitabu "Abuwa-bul-ad-iyya" akasema, Hadithi hii ni ya kweli na ni sahihi gharib.

2. Musnad Ahmad bin Hanbal, Juzuu ya nne uk. 138, "kutoka kwa Athuman bin Hunaif" chapa ya "Maktabul-islami, Muasasah dari-Saadir/Beirut, na ameipokea hadithi hii kwa njia tutu.

3. Mustad-ra kus-sahihain ya Al-Hakim An-Nishapuri, Juzuu ya kwanza, uk. 313, chapa ya Haidar-abad/India.

Amesema baada ya kuitaja hadithi hi:

"Hadithi hii ni sahihi kwa sharti ya Bukhari na Muslim lakini hawakuiandika".

4. Al-Jamius-Saghiru cha As-Suyuti, uk. 59, kutoka kwa Tirmidhi na Al-Hakim.

5. Tal-khisul-Mustad-rak cha Adh-dhahabi-alivefariki mwaka 748 A.H., kilichochapishwa katika Hashiya ya AI-Mustad-rak.

6. At-Tajul-Jamii, Juzuu ya kwanza, uk. 286, nacho ni kitabu kilichokusanya hadithi zilizomo katika sihahi tano isipokuwa sahih ya Ibn Majah.

Baada ya haya hakuna haja ya majadiliano kuhusu Sanad ya Hadithi hii au kuitia dosari.

Ama maelekezo yake na mafunzo yaliyomo, lau utamuonyesha hadithi hii mtu anayefahamu vyema lugha ya Kiarabu tena mwenye akili safi na akajiepusha na chuki za Kiwahabi na kuchanganya kwao mambo kuhusu tawa-suli kisha umuulize: "Ni kitu gani Mtume [s] alimuamuru kipofu yule akifanye wakati akiomba dua ile"?

Kwa haraka tu jibu lake litakuwa: "Mtume [s] alimfundisha namna atakayo tawas-sal kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake Mtume wa Rehma na namna Mwenyezi Mungu atakavyokubali maombi yake".

Maana hii ndiyo inayofahamika moja kwa moja kutokana na maneno yaliyomo katika hadithi iliyotajwa.

Ndani ya maelezo yafuatayo tunaigawa hadithi hii katika mafungu ili kuongeza ufafanuzi.

FUNGU LA KWANZA

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi ninakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako."

Neno "Mtume wako"linauhusiano na maneno mawili yaliyokuja kabla ya neno hili.

Maneno hayo ni: "Ninakuomba na ninaelekea kwako".

Kwa maneno yaliyo wazi tutasema kama ifuatavyo:

Kipofu yule anamuomba Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume [s] kama ambavyo anaelekea kwa Mwenyezi Mungu kwa kupitia heshima na utukufa wa Mtume [s] na wasila wake.

Kinachokusudiwa kwa neno "Mtume" siyo dua yake bali ni ile dhati yake tukufu. Ama anayesema kwamba neno dua limekadiriwa kabla ya neno Mtume na maana ya (As-aluka Binabiyyika) ni ninakuomba kwa dua ya Mtume wako, basi kusema hivyo ni madai bila ya dalili na ni kinyume cha maana iliyo dhahiri.

Na sababu ya madai hayo yaliyo kinyume na dalili ni kuwa, yeye haitakidi kutawasal kwa dhati ya Mtume [s] ndiyo maana akalazimika na akakadiria kusema kwamba neno dua hapa limekadiriwa ili tu kwa njia hii apate kuitakasa itikadi yake ya kupinga kutawasal kwa Mtume mwenyewe.

FUNGU LA PILl

"Muhammad Nabii wa Rehma".

Ili iweze kufahamika vyema kwamba makusudio katika Dua hiyo, ni kumuomba Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume na dhati yake na heshima yake, basi imekuja jumla baada ya neno "Mtume wako" isemayo "Muhammad Nabii wa Rehma", ili ifafanue lengo wazi wazi.

FUNGU LA TATU

Sentensi isemayo "Ewe Muhammad, hakika mimi naelekea kwa Mwenyezi Mungu kupitia kwako", inajulisha kwamba kipofu yule alimfanya Mtume mwenyewe kuwa ndiyo wasila wa maombi yake, siyo dua ya Mtume [s] yaani yeye alitawassal kwa dhati ya Mtume siyo kwa dua ya Mtume.

FUNGU LA NNE

Na aliposema: "Mfanye Muhammad awe muombezi wangu", alikuwa na maana ya kusema kuwa:

"Ewe Mola mfanye Muhammad [s] awe ndiye muombezi wangu na ukubali uombezi wake kwangu, katika haki yangu."

Ewe msomaji mpenzi bila shaka imekudhihirikia kwamba nukta muhimu katika dua yote ni dhati ya Mtume [s] na shakhsiyya yake tukufu, na katika dua hii hakuna utajo wa dua ya Mtume asilan. Na kila atayedai kuwa kipofu yule alitawassal kwa dua ya Mtume na wala hakutawassal kwa dhati ya Mtume wala shakhsiyya yake, huyu atakuwa amejifanya kutoyaelewa maneno ya hadithi hii yaliyo wazi na amejifanya kutoifahamu hadithi hii.

Nawe msomaji lau utaifanyia mazingatio kauli ya muombaji aliposema:

"Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba na ninaelekea kwako kupitia kwa Mtume wako, Mtume wa Rehma" na aliposema tena muombaji huyo:

"Ewe Muhammad hakika mimi naelekea kwa Mola wangu kupitia kwako", itakudhihirikia wazi wazi kwamba, lengo linalokusudiwa ni nafsi ya Mtume awe ndiyo wasila kupitishia maombi ya muombaji.

Na lau lengo ingekuwa ni dua ya Mtume ndiyo wasila ingelazimika kusema:

"Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba kwa (kupitia) dua ya Mtume".

Baada ya haya tuliyoyaeleza hivi punde hakuna mush-keli unaobakia miongoni mwa mish-keli aliyoitaja yule mwandishi wa Kiwahabi katika Kitabu kiitwacho "At-Tawas-Sul Ilaaz HaqiqatitTawas-sul". Mish-keli hiyo tumeitaja pamoja na majibu yake ndani ya kitabu chetu kiitwacho "At-Tawas-sul" kuanzia ukurasa wa 147 mpaka 153 na unaweza kurejea ukaona.

HADITHI YA PILl

KUTAWAS-SAL KWA HAKI YA WAOMBAJI

Amepokea Atiya Al-aufi kutoka kwa Abu Said Al-Khudri kwamba Mtume [s] amesema: "Yeyote atakayetoka nyumbani mwake kwenda kuswali akasema: Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kwa haki ya wanaokuomba, na ninakuomba kwa haki ya mwendo wangu huu kwani mimi sikutoka kwa maringo na majivuno, wala kujionyesha wala kutaka sifa, nimetoka kwa kuogopa ghadhabu zako na kutafata radhi zako, basi ninakuomba unilinde kutokana na moto na unisamehe madhambi yangu, kwani hapana anayesamehe madhambi isipokuwa wewe.
[112]

(Atakayesema hivi) Mwenyezi Mungu atamuelekea mtu huyo kwa dhati yake na watamtakia msamaha malaika sabini elfu."

Hadithi hii iko wazi mno katika maana yake na inajulisha kwamba mtu anayo ruhusa ya kutawas-sal kwa heshima ya Mawalii na daraja walizonazo na cheo chao mbele ya Mwenyezi Mungu. Basi na awafanye Mawalii hawa kuwa ndiyo wenye kukaa kati na kuwa waombezi, ili haja zake zikubaliwe na dua zake zipokelewe.

HADITHI YA TATU

KUTAWAS-SAL KWA HAKI
YA MTUME MTUKUFU [S]

Nabii Adam [a] yalipomtokea mambo ambayo ilivyokuwa ni bora yasimtokee, naye akarejea kwa Mwenyezi Mungu kutokana na hayo yaliyomtokea, alipokea maneno kutoka kwa Mola wake kama Qur'an Tukufu inavyoonyesha:

"Kisha Adam akapokea maneno kutoka kwa Mola wake, na Mola wake akakubali toba yake hakika yeye ni mwingi wa kupokea (toba) na ni mwingi wa huruma."
[113]

Qur'an, 2:37.

Wafasiri wa Qur'an na wataalam wa hadithi wamefafanua na kutoa rai zao na mtazamo wao kuhusu aya hii na maana yake, na wamefanya hivyo kutokana na kutegemea kwao baadhi ya hadithi ili kupata maana ya aya hii.

Yafuatayo ni maelezo ambayo ndani yake tutataja hadithi hizo ili tuone matokeo ambayo tunaweza kuyapata baada ya kuzitaja hizo hadithi.

At-Tabrani katika Al-muujamus-Saghir na Al-Hakim katika Mustadrak yake, na Abunuaim Al-Isfahani katika Hil-yatulAuliyai, Baidhawi naye katika Dalailun-nubuwat, na Ibn Asakir Ad-Dimishqi katika Tarikh yake, As-Suyuti naye ndani ya Tafsirud-duril Manthur, Al-A'lusiy yeye katika Tafsiri Ruhul-maan wote hawa wametoa mapokezi kutoka kwa Umar bin Al-Khatab naye kutoka kwa Mtume [s] kwamba Mtume amesema:

"Wakati Adam alipokosea lile alilolikosea, alinyanyua kichwa chake juu akasema, Nakuomba (Ewe Mwenyezi Mungu) kwa haki ya Muhammad unisamehe, Mwenyezi Mungu akampelekea wahi Adam (akamwambia) huyu Muhammad ni nani? Adam akasema:

Limetukuka Jina Lako (Ewe Mwenyezi Mungu), wakati nilipokuwa nimeumbwa nilinyanyua kichwa changu, kuiangalia arshi yako, basi niliona maandishi (yasemayo) hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na Muhammad ni mjumbe wa Allah nikasema, bila shaka hapana kiumbe Mtukufu mbele yako kuliko yule ambaye umeliweka jina lake pamoja na jina lako, Mwenyezi Mungu akampelekea Adam wahi (akamwambia) huyo ndiyo Nabii wa mwisho katika kizazi chako, na lau si yeye nisingekuumba wewe."[114]

Akinakili toka kwa At-Tabrani na Abunuaim na AI-Bayhaqi na matni ya hadithi imenakiliwa kutoka kwa Ad-durul-Manthoor.

MAONI YETU JUU YA HADITHI HII

Kinyume cha mazowea tuliyonayo kuwatambulisha watu hao au nafsi hizo. Qur'an inazungumzia nafsi au watu kwa kutumia neno "AL-KALIMAH" kinyume cha matumizi yetu ya kawaida kuhusti neno hili.

Kwa mfano Mwenyezi Mungu anasema:

(a) "Mwenyezi Mungu anakupa bishara njema ya Yahya mwenye kumsadikisha neno atokaye kwa Mwenyezi Mungu.

Qur'an, 3:39

(b) Kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: "Ewe Mariam, Mwenyezi Mungu anakupa bishara njema ya neno atokaye kwake jina lake ni Masih Isa mwana wa Mariam".

Qur'an, 3:45.

(c) "Hakika Masih Isa mwana wa Mariam ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu na ni neno lake."

Qur'an, 4:171

(d) Kauli ya Mwenyezi Mungu:

"Waambie lau kama bahari ingekuwa ndiyo wino kwa (kuandikia) maneno ya Mola wangu, basi bahari ingekwisha."

Qur'an, 18:109.

 

(e) Kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:

"Na bahari hii (ikafanywa wino) na bahari nyingine saba (zikaongezwa), maneno ya Mwenyezi Mungu yasingelikwisha."

Qur'an, 31:27.

Tukiziangalia aya hizi inawezekana kabisa kusema kwamba:

Makusudio ya "Kalimaat" yaani katika ile aya isemayo "Akapokea Adam kutoka kwa Mola wake maneno" makusudio yake ni dhati tukufu yenye heshima ambayo kwayo Nabii Adam alitawas-sal kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Na katika hadithi iliyotangulia utaliona jina la Muhammad [s] tu ndiyo lililotajwa.

Ama katika hadithi zilizoko katika madheheb ya haki (Shia) utaona hadithi hii imepokewa kwa sura inayokubaliana na aya tukufu ya Qur'an, pia utaikuta imepokewa kwa namna mbili.

Wakati mwingine neno "Kalimaat" limefasiriwa kwa maana ya majina ya watukufu watano [a], na wakati mwingine limefasiriwa kwa sura zao zenye nuru.

Hebu itazame hadithi ifuatayo: "Hakika Adam aliona kwenye arshi pameandikwa majina matukufu yenye heshima akauliza, majina hayo (ni ya kina nani)? Akaambiwa, haya ni majina ya viumbe watukufu mno kwa daraja mbele ya Mwenyezi Mungu, kuliko viumbe wote na majina hayo ni, Muhammad, Ali, Fatma, Hasan na Husein. Basi Adam [a] akatawas-sal kwa Mola wake kupitia kwao ili kukubaliwa toba yake na kunyanyuliwa daraja yake.[115] Na baadhi ya hadithi zinajulisha kwamba Adam [a] aliona Sura za nuru za watukufu watano, basi akatawas-sal kwazo baada ya kuziona. (Kwa ufafanuzi zaidi tazama Tafsir AI-Burhan, juz. 1, uk. 87, Hadith na 13, 15, na 16.)

2. Na tunaporejea vitabu vya historia na hadithi inatudhihirikia kwamba, Qadhiya ya Adam kutawas-sal kwa Mtume Muhammad [s] lilikuwa ni jambo mashuhuri miongoni mwa watu, ndiyo manna utamkuta Imam Malik bin Anas (Imam wa Madhehebu ya Malik) anasema kumwambia Mansur Ad-Dawaniq katika Msikiti wa Mtume [s] : "Mtume ni wasila wako na ni wasila wa Baba yako Adam".

Nao washairi wa Kiislamu wameuonyesha ukweli huu katika mashairi yao.

Mmoja wa washairi hao anasema: "Kwa Mtume [s] Mwenyezi Mungu alikubali maombi ya Adam na aliokolewa Nuhu ndani ya Safina."[116]

Mwingine naye anasema: Ni watu ambao kwao lilisameheka kosa la Adam, nao ndiyo wasila na nyota zing'aazo.[117]

HADITHI YA NNE

MTUME KUTAWAS-SAL KWA HAKI YAKE NA HAKI YA MANABII WALIOMTANGULIA

"Alipofariki Bibi Fatma binti Asad, Mtume alinigia mahala alipofia Mama huyo, akakaa upande wa kichwa chake akasema:

"Mwenyezi Mungu akurehemu ewe mama yangu baada ya mama yangu. Kisha Mtume akamwita Usama bin Zaid, na Abu Ayyubul-Ansari na Omar bin AI-Khatab na kijana fulani mweusi ili wakachimbe kaburi.

Wakachimba kaburi hilo, na walipofikia kuchimba mwanandani, Mtume [s] akaichimba mwanandani hiyo yeye mwenyewe kwa mkono wake na kuutoa mchanga. Alipomaliza, akaingia kwenye mwanadani kisha akalala ndani yake na akasema:

"Mwenyezi Mungu ndiye anayehuisha na kufisha, na yeye yu hai wala hatokufa. Ewe Mwenyezi Mungu msamehe mama yangu Fatma binti Asad na uyapanue makazi yake kwa haki ya Mtume wako na Manabii ambao wamepita kabla yangu". Mtungaji wa kitabu kiitwacho "Khulasatul-kalam" amesema:

Hadithi hii imepokewa na, Tabrani katika kitabu kiitwacho, Almuujamul-Kabir na Almuujamul-Ausat, na ameipokea Ibn Hiban na Al-Hakim na wamesema kuwa ni hadithi sahihi.[118]

Naye Sayyid Ahmad Zaini Dah-lan ameandika katika kitabu kiitwacho "Ad-Durarus-Saniyya Fiir-radd Alal-Wahabiyya" kama ifuatavyo:

"Amepokea Ibn Abi Shaiba kutoka kwa Jabir (kama tulivyoitaja hadithi hii, na vile vile ameipokea hivyo hivyo Abdul-Bari kutoka kwa lbn Abbas, na ameipokea Abu Nuaim katika kitabu "Hil-yatul-auliyai" kutoka kwa Anas, na yote haya ameyataja Alhafidh Jalalud-dinis-Suyuti katika kitabu "Al-jamiul-Kabir"[119]

Ama sisi tumetaja hadithi hii kutoka kwenye rejea mbili, moja inaambatana na maudhui haya tunayozungumzia ambayo yanahusu dua, na ya pili haihusiani na maudhui haya.

Rejea hizo ni:

(1) Hil-yatul-auliyai ya Abu Nuaim AI-Isfahani, juzuu ya tatu, uk. 121.

(2) Wafaul Wafa ya As-Samhudi, juzuu ya tatu, uk. 899.

HADITIII YA TANO

KUTAWAS-SAL KWA MTUME MWENYEWE

Wanachuoni wengi wa hadithi wamepokea kwamba, bedui mmoja aliingia kwa Mtume [s] akasema: Kwa hakika tumekujia hali ya kuwa wanyama na wanaadamu wote hawana hata sauti kwa ajili ya njaa."

Kisha akasema Ushairi huu:

"Tumekujia (Ewe Mtume) hali ya kuwa maziwa ya mwanamke kijana yanatoka damu (badala ya maziwa, kwa sababu ya njaa) na kwa hakika mama mwenye mtoto naye hamjali mwanawe na hatuna cho chote kinacholiwa na watu isipokuwa hanzal (matunda machungu) na Il-hizi,[120]. Na wala hatuna pengine pa kukimbilia isipokuwa kwako. Basi watu wakimbilie wapi? Hakuna, isipokuwa waende kwa Mtume".

Basi Mtume [s] alisimama huku nguo zake zinakokota chini mpaka akapanda kwenye Mimbar na kunyanyua mikono yake akasema, ewe Mwenyezi Mungu tupe mvua nyingi kabla Mtume hajateremsha mikono yake, basi mbingu ilinyesha mvua, kisha Mtume akasema: "Mwenyezi Mungu amlishe Abu Talib huko peponi. Lau angekuwa hai angelifurahi sana basi nani atatusomea maneno yake?"

Akasimama Ali bin Abi Talib [a] akasema, ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu kama kwamba unakusudia maneno yake haya yafuatayo:

"Na mwenye nuru ambaye huombwa mvua kwa uso wake yeye ndiye tegemeo la mayatima na yeye ndiyo mlinzi wa wajane. Wanamzunguka wenye matatizo miongoni mwa kizazi cha Hashim, basi kwake yeye wao wanapata neema nyingi na raha".

Mtume [s] akasema "Naam".

Imam Ali [a] alisoma beti nyingi za Qasida ile na huku Mtume anamuombea Magh-fira Abu Talib hali yeye akiwa kasimama kwenye Mimbar.

Baadaye mtu mmoja miongoni mwa Bani Kinanah akawa anasoma Qasida akasema, "(Ewe Mwenyezi Mungu) unastahiki shukurani, na shukurani hizi zatoka kwa mwenye kushukuru. Kwa hakika tumepata mvua kupitia kwenye uso wa Mtume mwenyewe".

Mimi nasema, "Rejea zilizotaja Qadhia hii ni nyingi mno, nasi tumeitaja Qadhia hii kutokana na rejea zifuatazo:

(1) Umdatul-qarii fii shar-hil Bukhari, juzuu ya saba, uk. 31 utunzi wa Badru-din Mahmud bin Ahmad Al-ain aliyefariki mwaka 855 A.H, chapa ya Idaratut-Taba-atil-Muniriyya.

(2) Shar-hu Nah-jul-Balaghah cha Ibn Abil-Hadid, juz. 14, uk. 80.

(3) As-siratul-Halabiyya, juz. ya 3, uk 263.

(4) Al-hujat Ala dhahib ila tak-fiiri Abi-Talib, utunzi wa Shamsuddin Abi Ali Fakhar bin Maad aliyefariki mwaka 630,chapa ya Najaf katika Maktaba ya Alawiyya, uk 79.

(5) Siratu Zaini Dah-lan, kilichochapishwa katika Hamish Sirat Al-halab-iyyah, juzuu 1, uk. 81.

HADITHI YA SITA

VILE VILE INAHUSU KUTAWAS-SAL KWA MTUME

Imepokewa kwamba, Sawad bin Qarib alimsomea Mtume [s] Qasida yake ambayo ndani yake alitawas-sal kwake Mtume [s] akasema: "Nashuhudia kwamba hapana Mola isipokuwa Allah, na kwamba wewe ndiwe mwenye kuaminiwa kuhusu mambo ya kila asiyekuwepo. Nawe ndiye uliye karibu mno kama wasila kwa Mwenyezi Mungu kuliko Mitume wengine ewe mwana wa watukufu walio wema. Tuamrishe (tutende) yale yanayokufikia ewe mbora wa Mitume, japo yatukuwa mazito, na uwe muombezi wangu siku ambayo maombezi yeyote hatamnufaisha Sawad bin Qarib japo kwa sehemu ndogo.[121]

Ewe msomaji mpenzi, mpaka sasa tumetaja kiasi cha kutosha cha hadithi zilizopokelewa kuhusu Tawas-sul, na tumetegemea vitabu vya hadithi na historia vya Kisunni.

Ama kutawas-sal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa mapokezi ya watu wa nyumba ya Mtume [s] katika vitabu vya kishia jambo hili liko wazi mno na limethibiti barabara kiasi ambacho limekuja kwa njia ya dua vile vile.

Sote tunawajibika kujiuliza:

"Je tunalazimika kuchukua maarifa ya Kiislamu na hukumu za sheria kutoka kwa "Ibn Taimiyyah" na "Muhammad Ibn Abdul Wahab" na wengineo mfano wa watu kama hawa, au tuchukue maarifa ya Kiislamu na hukumu za sheria toka kwa watu wa kizazi cha Mtume [s] ambao Mtume amewataja katika hadithi "Thaqalan" (vizito viwili) kwamba wao ndio kile kizito kidogo cha pili na kwamba wao ni sawa na Qur'an?

Kwa hakika kila Muislamu mwenye akili safi ataamua na kuona ulazima wa kuchukua mafunzo hayo toka kwa watu wa kizazi cha Mtume [s] ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na kuwatakasa mno.

MIFANO VA DUA ZA TAWAS-SUL

Ama dua ambazo zimekuja na ndani yake kuna kutawas-sal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, na zimetapakaa katika Sahifatul-Alawiyyah[122], na dua ya Arafah[123], na Sahifatus-Sajjadiyyah[124] na vitabu vinginevyo ni nyingi mno, tunataja mifano ya dua hizo kama ifuatavyo:

1. Imam Ali [a] katika dua yake anasema:

Kwa haki ya Muhammad na Aali Muhammad iliyo juu yako, (Ewe Mwenyezi Mungu) na kwa haki yako tukutu juu yao (nakuomba) uwape rehma kwa sababu wewe ndiwe unayestahiki na unipe mimi kilicho bora mno ya vile ulivyowapa waombaji miongoni mwa waja wako waliopita katika waumini na unipe kilicho bora mno ya vile utakavyowapa waja wako waliosalia miongoni mwa waumini.

2. Na anasema bwana wa mashahidi AI-Imam Husein bin Ali [a] katika dua yake ya Arafah:

"Ewe Mwenyezi Mungu tunaelekea kwako jioni hii ambayo umeifaradhisha na kuitukuza kwa haki ya Muhammad Mtume wako, mjumbe wako na mteule wako katika viumbe vyako".

  • Na anasema Al-Imam Zaynul-Abidiina katika dua yake inayohusu kuandama kwa Mwezi wa Ramadhan:
  • "Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba kwa haki ya Mwezi huu na kwa haki ya wale wataofanya Ibada ndani yake tangu mwanzo hadi mwisho, miongoni mwa Malaika uliyemkurubisha au Nabii uliyemtuma, an mja mwema uliyempenda".
    [125]

    MWENENDO WA WAISLAMU KATIKA TAWAS-SUL

    Sera ya Waislamu katika zama za uhai wa Mtume [s] na baada ya kufa kwake inakubaliana na kutawas-sal kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu na kuomba uombezi kupitia vyeo vyao na heshima zao mbele ya Mwenyezi Mungu.

    Ifuatayo ni mifano ya sera hiyo ya Waislamu.

    1. Ibn Al-Athir mwana historia mashuhuri aliyefariki mwaka 630 anaandika hivi:

    "Omar bin Al-Khatab aliomba mvua kupina kwa Abbas katika mwaka wa ukame ulipozidi, basi Mwenyezi Mungu akawateremshia mvua na kwa dua hiyo ardhi ikaota mimea, Omar akasema: "Wallahi huu ni wasila kwa Mwenyezi Mungu na hii ni daraja mbele yake".

    Naye Hassan alisema:

    "Imamu aliomba baada ya ukame kutufikia mfululizo. Basi Mawingu yakanyesha kwa kipaji cha Abbas. Ni Ammi ya Mtume na ndugu wa mzazi wake ambaye amemrithisha Mtume heshima hiyo, watu wengine hawakuipata. Kwake yeye Mola ameihuyisha ardhi na sasa imekuwa ya kijani kibichi kila sehemu baada ya kuwa kame".

    Na baada ya watu kuwa wamepata mvua hii wakawa wanajipangusia kwa Abbas na kumwambia, pongezi ewe uliyezinywesha maji haram mbiIi (Maka na Madina).[126]

    Kufanya mazingatio kwenye tukio hili la kihistoria ambalo sehemu yake fulani ameitaja pia Bukhari katika sahihi yake, kunatia nguvu kusema kwamba miongoni mwa aina za wasila ni kutawas-sal kwa watu wenye vyeo na heshima mbele ya Mwenyezi Mungu, na ni kitu ambacho matokeo yake ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na pia kumtukuza muombaji na yule mwenye kutawas-sal.

    Je, ni maelezo gani yaliyo wazi kuliko kauli ya Omar aliposema "Wallahi huu ndiyo wasila kwa Mwenyezi Mungu na daraja mbele yake".

    2. Al-Qastalimy aliyefariki mwaka 923 A.H. anasema:

    "Hakika Omar alipoomba mvua kwa wasila wa Abbas alisema, "Enyi watu hakika Mtume alikuwa akimuona Abbas kuwa ana haki kwake kama ile aionayo mtoto kwa mzazi wake, basi mfuateni Mtume kwa amii yake na mumfanye Abbas kuwa ni wasila kwa Mwenyezi Mungu". Katika maelezo haya kuna ufafanuzi wa kusihi tawas-sul, na kwa maelezo haya pia inavunjika kabisa kauli ya mwenye kuzuwiya Tawasul kwa watu walio hai na wafu na pia inavunjika kauli ya anayezuwiya kutawas-sal kwa mtu asiye Mtume."
    [127]

    3. Hapo kabla tumetaja kwamba "Mansur Al-Ab-basi Ad-dawaniqi" alimuuliza Malik bin Anas, Imam wa Madhehebu ya Malik, namna ya kumzuru Mtume [s] na namna ya kutawas-sal kwake..... naye akamwambia Malik:

    "Ewe Abu Abdillah nielekee Qibla niombe au nimuelekee mjumbe wa Mwenyezi Mungu?" Malik akasema: "Kwa nini unampa kisogo Mtume wakati yeye ndiyo wasila wako na wasila wa baba yako Adam kwa Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama? Ilivyo sawa muelekee na umuombe akuombee na Mwenyezi Mungu atakubali maombi yako, kwani Mwenyezi Mungu anasema: Na lau wao wakizidhulumu nafsi zao...[128]

    4. Beti hizi mbili zifuatazo amezitaja lbn Hajar Al-Haithami kutoka katika shairi la Imam Shafii - Imam wa Madhehebu ya Kishafii.

    "Kizazi cha Mtume, wao ni njia yanga na wao ni wasila wangu kwa Mwenyezi Mungu, kwao wao kesho nataraji kupewa kitabu changu kwa mkono wa kulia."[129]

    Baada ya maelezo yote yaliyotangulia miongoni mwa dalili na hoja na ushahidi inawezekana kusema kwamba Manabii na watu mashuhuri wa dini wao ndio ule wasila alioukusudia Mwenyezi Mungu aliposema:

    "Enyi mlioamini, mcheni Mwenyezi Mungu na mtafute wasila kwake."

    Qur'an, 5:35.

    Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ameamuru kuwafanya wao kuwa ni wasila wa kumfikia yeye Mwenyezi Mungu.

    Na hapana shaka kwamba, wasila haukuishia kwenye kutekeleza mambo ya faradhi na kujiepusha na mambo ya haramu peke yake, bali unakwenda mbele zaidi na kukusanya matendo ya Sunna ambayo ndani yake mna kutawas-sal kwa Mawalii.

    Je, yawezekana kusema kwamba wanachuoni na wahakiki walikosea kuifahamu maana ya "wasila"? Pamoja na kufahamika kuwa wao ndio marejeo katika hukmu za sheria nao ndio walohifadhi hadithi na ni miongoni mwa wasomi wa Kiislamu ambao huashiriwa kwa kutolewa mifano yao?

    Hakika watu wanaojitokeza kukosoa ukweli huu na dalili hizi na wakawa wanatafiti huku na huko kujaribu kugeuza kila hadithi na dalili, wao wanafanana na hakimu ambaye hukimbilia kuhukumu bila ya kuwa na ushahidi anaoutegemea.

    Bukhari anapokea hadithi katika Sahihi yake isemayo:

    "Hakika Omar bin Khatab alikuwa kila wanapopatwa na ukame huomba mvua kwa Abbas bin Abdil-Muttalib (r.a.) na kisha husema, "Ewe Mwenyezi Mungu tulikuwa tukitawas-sal kwako kupitia kwa Mtume wetu na ukitupa mvua, basi sasa tunatawas-sal kwako kwa ammi ya Mtume wetu basi tupe mvua." Bukhar anasema, "Basi hupewa Mvua."
    [130]

    Hakuna majadiliano juu ya kusihi kwa hadithi hii kiasi kwamba hata huyo Ar-rifai ambaye ni mwandishi wa Kiwahabi anayepinga hadithi mutawatiri za kutawas-sal kwa njia yoyote ile, lakini amekiri kwamba hadithi hii imesihi akasema:

    "Hakika hadithi hii ni sahihi na kama ruhusa hii itakuwa imesihi kisheria, basi sisi tutakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuikubali na kutenda kwa mujibu wa hadithi hiyo".

    Kutokana na kufahamika maelezo waliyoyataja yaliyopokelewa toka kwa Omar bin Khatab kuhusu kutawas-sal kwa Abbas na kwamba yeye aliapa kwa Mwenyezi Mungu akasema, "Wallahi huu ndiyo wasila kwa Mwenyezi Mungu na daraja mbele yake", inadhihiri katika hadithi hii kuwa ukweli wa wasila ni kutawas-sal kwa Abbas yeye mwenyewe an ni kwa heshima yake na jaha yake mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na siyo kutawas-sal kwa dua ya Abbas.

    Kwa hali hii, amepokea Muhammad Bin Nuuman Al-Maliki aliyefariki mwaka 683 A.H. ndani ya kitabu chake kiitwacho "Misbahud-dhalami fil-mustaghiithina bikhairil-anam" namna ya kutawas-sal alikotawas-sal Omar kwa Abbas akasema:

    "Ewe Mwenyezi Mungu tunakuomba mvua kupitia kwa ammi ya Mtume wako, na tunataka kwako msaada kupitia kwake kwa ndevu zake nyeupe, basi wakapewa mvua" na kwa matokeo haya Abbas bin Ut-ba bin Abi-Lahab anasema:

    "Kupitia kwa ammi yangu Mwenyezi Mungu aliinywesha Hijazi na watu wake, wakati Omar alipoomba kupitia kwenye ndevu zake nyeupe".[131]

    Naye Hassan alisema
    : "Mvua ilinyesha kwa kipaji cha Abbas".

    Na amesema Ibn Hajar Al-Al-as-qalani, "Abbas aliomba kwa Mwenyezi Mungu kwa kusema....Watu walikuelekea kupitia kwangu kutokana na daraja yangu kwa Mtume wako".

    Ewe msomaji mpendwa; imekudhihirikia wazi kwamba kutawas-sal hapa tunakokuelezea hapa kulikuwa ni kutawas-sal kwa dhati ya Abbas na heshima yake.

    Wanachuoni wa fani ya Balagha wamesema:

    "Taaliqul-hukmi Bil-was-fi Mush-irun bil-illiyyat."

    Maana yake: "Hukumu inapolazimiana na sifa huwa inajulisha kwamba sababu ya kupatikana hukumu hiyo ni sifa ile.

    Kwa mfano Qur'an tukufu inasema:

    "Na ni juu ya mtu ambaye kwa sababu yake amezaliwa mtoto (yaani baba) rizki ya hao kina mama".

    Qur'an, 2:233.

    Maana yake ni kwamba mwanamke aliyemzalia mume mtoto, basi ni wajibu kwa mume kusimamia matumizi ya mwanamke huyo. Hukumu iliyopo hapa ni ule wajibu wa kutoa matumizi, na sifa ni yule mtoto aliyezaliwa na mwanamke.

    Hebu tazama mfano mwingine:

    "Kama mzazi atamwambia mwanawe "Muheshimu mwanachuoni" hakuna sababu nyingine isipokuwa ni elumi yake na ubora alionao.

    Kwa msingi huu tulioueleza sasa hivi unaikuta kauli ya Omar anaposema:

    "Sisi tunatawas-sal kwako kupitia kwa ammi ya Mtume wako".

    Ndani ya kauli hii kunabainika sababu ya katawas-sal kwa Abbas kinyume na mtu mwingine, na hiyo ni kwa sababu ya kuwa kwake ni ammi ya Mtume [s].

    Naye Abbas mwenyewe alisema: "Kwa heshima niliyo nayo kwa Mtume wako".

    Kwa ufupi baada ya yote yaliyotangulia inawezekana kusema kwa yakini kamili kwamba, "Bila shaka Waislamu toka hapo mwanzo wa kuja Uislamu walikuwa wakitawas-sal kupitia kwa watu wema na watukufu".

    6. USHAIRI WA SAFIYYAH AKIOMBOLEZA KIFO CHA MTUME [S]

    Bibi Safiyyah binti Abdil-Muttalib (Shangazi ya Mtume) alisoma Qasida baada ya kufariki Mtume [s] kuomboleza kifo chake, na sehemu ya Qasida hiyo ni hii ifuatayo:

    "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu wewe ndiyo matumaini yetu, uIikuwa mwema wetu na wala hukuwa mnyanyasaji, na ulikuwa mwema mpole ewe Mtume wetu, basi leo na akulilie yeyote mwenye kulia".[132]

    Kitika kipande hiki cha shairi ambacho kilisomwa mbele ya masikio ya Masahaba, nao wanahistoria wakakisajili tunapata faida ya mambo mawili:

    Kwanza: Kuzisemesha roho na hasa kumsemesha Mtume baada ya kufa ni jambo lililokuwa linafaa na likitumika tangu hapo mwanzo, na bibi Safiyyah anaposema: "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu" kusema hivi haikuwa ni usemi wa kipuuzi na mchezo tu, au ni shirki kama wanavyodai Mawahabi wapotovu.

    Pili: Bibi Safiyyah aliposema, "Wewe ndiyo matumaini yetu" inajulisha kwamba Bwana Mtume [s] ndiye matarajio na matumaini ya jamii ya Kiislamu katika nyakati zote na kila hali na wala hauwezi kukatika au kumalizika uhusiano wake na jamii hiyo hata baada ya kufariki kwake.

    BAADHI YA MAANDIKO YALIYOANDIKWA
    KUHUSU TAWAS-SUL

    Inafaa tuashirie baadhi ya vitabu vinavyotegemewa vilivyoandikwa na wanachuoni wa Kisunni kuhusu kutawas-sal kwa Mtume Mtukufu [s], na pia kuvirjea vitabu hivi kutayaweka wazi maoni ya wanachuoni wa Kiislamu juu ya kutawas-sal kwa Manabii na Mawalii, na kutia nguvu kwamba kutawas-sal tangu hapo mwanzo lilikuwa ni jambo linalotendeka na ni sunna iliyokuwa ikifuatwa na Waislamu sika zote kinyume cha wanavyodai Mawahabi.

    1. Kitabu kiitwacho, Al-Wafau fii Fadhailil-Mustafa, cha lbn Al-Jauzi aliyefariki mwaka 597 A.H. Yeye alitenga mlango maalumu katika kitabu chake hiki utakaozungumzia kutawas-sal kwa Mtume [s] na mlango mwingine uliohusu kuomba uponyo kwenye kaburi lake tukufu.

    2. Mis-bahud-dhalami fil-mustaghithina Bikhairil-anam, kilichotungwa na Muhammad bin Nuuman Al-Maliki, aliyefariki mwaka 673 A.H., na As-Samhudi amenakili nakala nyingi kuweka kwenye kitabu chake kiitwacho Wafaul Wafa kutoka ndani ya kitabu hiki cha Muhammad bin Nuuman Al-Maliki Babul-tawas-sul Binnabi [s].

    3. Al-Bayan Wal-Ikhtisar cha ibn Dawud Al-Maliki As-Shadhili.

    Ndani ya kitabu hiki ametaja khabari za wanachuoni na watu wema kutawas-sal kwa Mtume [s] nyakati walizokuwa wakipatwa na matatizo.

    4. Shifaus-siqami cha Taqiyuddin as-Subaki aliyefariki mwaka 756 A.H., yeye amezungumzia vizuri kutawas-sal kwa Mtume kwa njia ya Tah-liiili kuanzia uk. 120 mpaka 133.

    5. Wafaul Wafai liakhbari Daril-Mustafa cha As-sayyid Nurudin As-Samhudi aliyefariki mwaka 911 A.H. Yeye ameitafiti tawas-sul kwa upana sana ndani ya juzuu ya pili kutoka uk. 413 mpaka 419.

    6. Al-Mawahibal-laduniyyah cha Abul-abbas AI-Qastalani aliyefariki mwaka 932 A.H.

    7. Shar-hul-mawahibil-laduniyyah cha Az-Zirqani Al-Maliki Al-Misri aliyefariki mwaka 1122 A.H., ndani ya Juzuu ya Nane uk. 317 amezungumzia tawas-sul.

    8. Sul-hul-ikh-wan cha Al-Khalidi Al-Bagh-dadi aliyefariki mwaka 1299, pia anayo risala maulum inayozungumzia ruhusa ya kutawas-sal kwa Mtume [s], akimpinga katika risala hiyo Al-Alusi, na risala hiyo ilichapishwa mwaka 1306 A.H.

    9. Kanzul-matalib cha AI-Adawi AI-Hamzawi aliyefariki mwaka 1303 A.H.

    10. Fur-qanul-Qur-an cha Al-Azzami As-Shafi al-Qudhai kitabu hiki kilichapishwa pamoja na kitabu kiitwacho Al-as-mau Wassifat cha Al-Baihaqi chenye kurasa 140.

    Ewe msomaji mpendwa kuvirejea vitabu hivi na hasa vile vilivyozungumzia tawas-sul kwa ufafanuzi (kitabu Sul-hul-Ikhwan na Fur-qanul-Qur'an viko katika mstari wa mbele) kunaithibitisha sera ya Waislamu katika zama zote na nchi zote kuwa wao hutawas-sal kwa Mtume [s] na kunadhihirisha kupotea kwa Ibn Taimiyyah na wanafunzi wake na ubovu wa maoni yao na itikadi yao mbovu.

    Mwisho: Kwa kumalizia sehemu hii tunasema: Qur'an tukufu imeweka wazi kuwa kutawas-sal kupitia kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni jambo linalofaa, bali inahimiza kutawas-sal pale iliposema:

    "Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu na mtafute wasila kwake na piganeni katika njia yake ili mpate kufanikiwa".

    Qur'an, 5:35.

    Aya hii inahimiza kutafuta wasila katika nyanja zote kwa jumla. Swali linakuja, "Wasila ni kita gani?"

    Jawabu: Aya tukufu ya Qur'an haikutaja wasila kuwa ni kitu gani. Bila shaka kutekeleza faradhi za dini ni miongoni mwa (wasila) za mafanikio na uokovu, lakini hapana shaka vile vile kwamba wasila hauishii kwenye mambo hayo peke yake, bali kufuatana na mwenendo wa Waislamu kwa muda mrefu katika historia, miongoni mwa wasila ni kutawas-sal kupitia kwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu na wacha Mungu na kwamba wasila huu ni miongoni mwa mafanikio na kukubaliwa mahitajio na matumaini.

    Jambo hili liko wazi ndani ya maelezo tuliyoyaeleza katika maneno ya Imam wa Kimalik alipozungumza na Mansuri AI-Abbasi. Na kutawa-sal kwa Omar bin Khataab kwa Abbas ili wapate mvua na mengineyo.

    "Hakika haya ni mawaidha atakaye na ashike njia aende kwao Mola wake".

    [110] At-Tawas-sul Ilaa Haqiqatit-Tawas-sul, uk. 158

    [111] At-Tawas-sul Ilaa Haqiqatit-Tawas-sul, uk. 158.

    [112] Sunan Ibn Majah, juz. 1, uk. 256. Hadith namba 778.

    [113] 4. Maelezo:Imethibiti kwamba, lile katazo lililoko katika kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: 'Msiukurubie mti huu" ni katazo la kutoa muongozo na siyo katazo Ia kuharamisha litokalo kwa Mola. Na katazo la muongozo liko katika mahala pa nasaha na mawaidha, na kulikhalifu katazo hili hakuwajibishi adhabu, wala haliondoshi isma kwa namna yoyote ile. Basi huwajibisha Taathira kwenye dhati ya kitendo, k.m., Lau tabibu atamkataza mgonjwa wa mafua kutumia vitu vichachu, kisha mgonjwa akakhalifu, basi tendo lake la kukhalifu litaakisi athari ya kimaumbile ambayo ni kuzidi kwa mafua na ugonjwa. Na ndani ya Qur'an Tukufu ziko aya nyingi zinazojulisha kwamba, katazo alilokatazwa Adam kuukurubia mti ule lilikuwa ni katazo la kutoa muongozo na hapana athari kwa kukhalifu katazo hili isipokuwa ni matokeo ya kimaumbile kwa kukhalifu huko. Unaweza kurejea aya ya 118 na 119 katika Surah Taha.

    [114] (1) Mustadrakus-Sahihain, juz. 2, uk. 615.(2) Ruhul-Maani, juz. 1, uk. 217.(3) Ad-durul-Manthoor, juz. 1, uk. 59.

    [115] (1) Maj-maul-bayan Juz. 1 uk 89 Chapa ya Lebanon (2) Tafsirul-bur-han Juz. 1, uk 86-88 hadithi namba 2, 5, 11, 12, 14 na 27.

    [116] Kashful-irtiyab, uk. 307. Ameinakili kutoka katika Mawahib, na shairi hili ni la Ibn Jabir.

    [117] Kashful-irtiyab, uk. 308. Na Shairi hili ni la Al-wasiti.

    [118] Kashful-irtijab, uk. 312 amenakili toka Khulasatul-kalaam.

    [119] Ad-durarus-Saniyya,uk. 8

    [120] Il-hizi ni kitu ywalichokuwa wakikitumia katika miaka ya njaa na kilikuwa kikitengenezwa kutokana na mcanganyiko wa damu na manyoya ya ngamia kisha hukikaanga kwa moto na kukila. Taz: Annihayah fi Gharibi-lhadith cha Ibn Athir al-Jazari chapa ya Beirut, juz. 3, uk 293.

    [121] Ad-duraru Saiyyah, uk. 27 utunzi wa Zaini Dah-lan, At-tawas-sul Ilahaqiqati-tawas-sul, uk 300.

    [122] Ni mkusanyiko unaokusanuya baadhi ya dua za Imam Ali, Amirul-Muuminina [a] alizikusanya Sheikh Abdulla As-Samahiji.

    [123] Ni dua ya Imam Husein [a] katika Arafaat siku ya Arafah.

    [124] Ni baadhi ya dua za Imam Zaynul Abidiina.

    [125] Sahifatus-Sajjadiyah dua namba 44.

    [126] Usudul-ghabah fii maarifat-S-Sahaba, juz. 3, uk 111, chapa ya Misri.

    [127] Kitabul-Mawahibil-laduniyyah: Chapa ya Misri.

    [128] Wafaul Wafa, juz. 2, uk. 1376

    [129] As-sawaiqul-muh-riqah cha Ibn Hajar, uk. 178

    [130] Sahih Bukhari, babu salatul-istiqai, juz. 2, uk. 32.

    [131] Wafa-ul Wafa, juz. 3, uk. 375. Amenakili toka katika Mis-bahud-Halam.

    [132] (1) Dhakhairul-uqbaa cha Al-hafidh Al-Muhibbu At-Tabari, uk. 252.(2) Maj-mauz-zawaid, juz. 9, uk. 36.