KUSWALI NA KUOMBA DUA KWENYE MAKABURI YA MAWALII

Miongoni mwa mambo ambayo Mawahabi wanayapigia kelele katika vitabu vyao na sehemu nyingine ni kuswali na kuomba dua kwenye makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu, pia kuwasha taa katika sehemu hizo.

Muanzilishi wa Uwahabi anasema katika moja ya risala zake iitwayo "Ziyaratul-Qubur " kama ifuatavyo:

"Hakuna Imamu yeyote miongoni mwa Maimamu waliyotangulia aliyetaja kwamba, kuswali makaburini na kwenye maziyara ni jambo la Sunna, na wala kuswali na kuomba katika sehemu hizo kuwa ni bora, bali Maimamu wote wameafikiana kuwa, kuswali misikitini na majumbani ndiyo bora kuliko kuswali kwenye makaburi ya Mawalii na Wachamungu".[98]

Na vile vile yamekuja maelezo yanayonasibishwa kuwa ni jawabu lililotolewa na wanachuoni wa Madina kama ifuatavyo:

"Ama kukielekea chumba alichozikwa Mtume wakati wa kuomba dua, kilicho bora ni kulizuwia tendo hili, kama inavyoeleweka katika vitabu vya Madhehebu vinavyotegemewa, kwani upande uliyo bora kuelekewa ni upande wa Qibla".

Jambo hili limevuka mpaka, kutoka kwenye kiwango cha wao Mawahabi kulizuwiya, mpaka kwenye kiwango cha kuwa ni shirki, kiasi kwamba leo hii wanalizingatia kuwa ni shirki na kila alitendaye kuwa ni mushriki.

Bila shaka ni kwamba, kuswali kwa ajili ya huyo mwenye kaburi na kumuabudia au kumfanya yeye ndiyo Qibla katika swala itakuwa ni shiriki moja kwa moja.

Lakini ifahamike kwamba, hapa duniani hakuna Muislamu anayefanya namna hii kwenye makaburi ya Mitume na Mawalii, na hakuna anayemuabudia aliyezikwa hapo au kumuelekea katika sala.

Kwa hiyo basi fikra hii ya kuwepo shirki ni uzushi na ni tuhuma zinazopandikizwa na Mawahabi.

Hakika lengo la Waislamu kuswali na kuomba dua kwenye makaburi ya Mawalii ni kutaka kupata baraka za sehemu hizo ambazo zimehifadhi vipenzi miongoni mwa vipenzi ya Mwenyezi Mungu.

Waislamu wanaitakidi kuwa mahali hapo pana daraja kubwa kwa sababu pameuhifadhi mwili wa mtu mtakatifu miongoni mwa watu watakatifu wa Mwenyezi Mungu.

Hivyo basi, kuswali na kuomba dua sehemu hiyo kunampa thawabu nyingi mwenye kutenda hayo.

Kuna swali ambalo niwajibu lijibiwe nalo ni hili:

Je, kuwazika Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika sehemu fulani huwa kunaifanya sehemu hiyo ipate aina fulani ya heshima au hapana?

Iwapo itathibiti kuwa "ndiyo" kwa mujibu wa dalili za Qur'an na hadithi, basi kuswali na kuomba dua kwenye makaburi ya viongozi wa Uislamu ni jambo mustahabu na linazo thawabu nyingi.

Hata kama pengine lisithibiti jambo hili (kama tulivyotangulia kusema) haiwezekani kuharamisha kuswali na kuomba dua mahali hapo bali patajaaliwa kuwa ni kama sehemu nyingine tu ambazo inafaa kuswali na kuomba dua japokuwa hapana aina yoyote ya ubora.

Hebu tuyaelekeze mazungumzo yetu kwenye maudhui yenyewe ambayo ni Je, maziyara na kaburi ya Mawalii yanaoutukufu na heshima maalum?

Na Je kuna ushahidi ndani ya Qur'an na hadithi kuhusu jambo hili.

Jawabu liko kama ifaatavyo:

1. Kisa cha As-Habul-Kahfi ambacho tumetangulia kueleza kwamba, waumini na watu wa tauhidi walisema kuhusu namna ya kuyafanya mazishi ya hao As-Habul-Kahfi .

"Tuwajangee msikiti juu yao"[99]

Hapa utaona kuwa, lengo lililowafanya waumini hao kujenga msikiti mahali walipozikwa As-Habul-Kahfi si jingine bali ni kwa ajili wapate kutekeleza faradhi zao ndani ya msikiti huo.[100]

Waumini hao walikuwa wakifikiri kuwa: Mahali hapa pamekuwa patukufu na panaheshimika kwa sababu panahifadhi miili ya watu miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu waliowachamungu, kwa hiyo hapana budi kutabaruku napo kwa kupafanya kuwa ni msikiti kwa ajili ya swala na ibada za Mwenyezi Mungu ili kupata thawabu nyingi zaidi.

Qur'an inalitaja jambo hili lililofanywa na Waumini hao bila ya kuwakemea wala kuwakosoa bali imenyamaza kabisa. Na lau tendo lao hili lingekuwa liko kinyume cha sheria au ni miongoni mwa mambo ya upuuzi yasiyofaa, Qur'an isingewanyamazia, bali ingewakemea kama ilivyo kawaida ya Qur'an kutokunyamazia itikadi batili.

2. Qur'an tukufu inawaamuru mahujaji wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu waswali kwenye "Maqam Ibrahim [a] nalo ni jiwe ambalo Nabii Ibrahim [a] alisimama juu yake alipokuwa akijenga Al-Kaaba.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema

"Pafanye mahali alipokuwa akisimama Ibrahim pawe pa kusalia".

Qur 'an, 2:125.

Yeyote anayeisoma aya hii atafahamu wazi kabisa kwamba swala iliwajibika mahala hapo siyo kwa jingine bali ni kwa sababu ya Maqam Ibrahimu (jiwe aliposimama Nabii Ibrahim) na kwamba lilejiwe ndilo lilisababisha mahala hapo papate utukufu na heshima hiyo. Na utawaona Waislamu kwa mamilioni wanapafanya kuwa ni mahali pa kusalia na kuomba dua.

Kama mambo yako namna hii kuhusu mahali tu aliposimama Nabii Ibrahimu, je haitapasa hali iwe ni kama hiyo kuhusu sehemu walizolala watu wa Mwenyezi Mungu na viongozi wa Uislamu?

Je, haitakuwa swala inayoswaliwa katika makaburi yao ni bora kuliko swala inayoswaliwa sehemu nyinginezo?

Ni kweli kwamba aya hii imeshuka kuhusu kusimama kwa Nabii Ibrahimu mahala pale, lakini je hivi haiwezekani tukatoa kutokana na aya hii hukmu inayoenea?

Khalifa Mansoor Al-Abbasi (Ad-Dawaaniqi) alimuuliza Imam Malik Bin Anas (Imam wa Madhehebu ya Malik) walipokuwa ndani ya Msikiti wa Mtume [s] akasema:

"Ewe baba Abdillahi nielekee Qibla ndiyo niombe au nimuelekee Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

Malik akasema: "Kwa nini wampa kisogo Mtume hali ya kuwa yeye ni wasila wako na ndiye wasila wa baba yako Adam [a] siku ya Kiyama? Iliyopo muelekee na umuombe, Mwenyezi Mungu atakukubalia maombi yako."[101]

Mazungumzo haya yanatufahamisha kwamba dua kwenye kaburi la Mtume [s] ilikuwa haina mushkeli wowote, pia kwamba suali la Mansur kumuuliza Malik ilikuwa ni kutaka kupata nguvu ya kufanya maombi kwa kuelekea Qibla au kwenye kaburi la Mtume [s], naye Imam Malik anatoa fatwa kwamba kuelekea kaburi Ia Mtume [s] katika dua ni kama kuelekea Qibla.

3. Lau tutayarejea maelezo ya safari ya Miiraji, ukweli ungelijitokeza wazi wazi kwa namna nyingi zaidi.

Kuna maelezo yasemayo kwamba Mtume [s] katika safari hiyo alishuka "Madina" na kwenye "Mlima wa Sinai" na Baiti Allaham" na aliswali katika sehemu hizo.

Jibril alimwambia Mtume [s]:

"Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu unazifahamu sehemu ulizoswali? Hakika umeswali katika "Taiibah". Na hapo ndipo utapohamia, na umeswali kwenye "Mlima Sinai" mahali ambapo Mwenyezi Mungu alimsemesha Mussa na pia umeswali katika Bait Allaham (Bait-lehem)" mahali alipozaliwa Issa [a]." [102]

Hadithi hii inafahamisha kwamba, inapendekezwa kuswali katika sehemu ambazo zimeguswa na Manabii, na kwamba sehemu hizo zimepata heshima na utukufu kwa sababu ya Nabii huyo.

4. Bibi Hajir "Mama wa Ismail bin Ibrahim" alifikia daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa sababu ya subira na kuvumilia taabu katika njia ya Mwenezi Mungu mambo ambayo yalisababisha Mwenyezi Mungu apafanye mahali alipokanyaga Mama huyu, kuwa ni mahali pa ibada na akawajibisha Mahujaji wa nyumba yake tukufu waende kama alivyokwenda Bibi Hajir baina va Milima miwili ya "Safaa na Marwaa", jambo ambalo Ibn Al-Qayyim ambaye ni mwanafunzi wa Ibn Taimiyya analikubali.[103]

Sisi tunajiuliza, ikiwa uvumilivu wa Bibi Hajir kuyavumilia matatizo na taabu katika njia ya Mwenyezi Mungu kumesababisha kupapatia utukufu mahala zilipo kanyaga nyayo zake, na Mwenyezi Mungu akawajibisha kwa Waisiamu kuwa wamuabudu yeye Mwenyezi Mungu katika sehemu hiyo kwa kuenda baina ya Safaa na Marwaa, basi ni kwa nini kaburi la Mtume [s] lisiwe ni lenye baraka na utukufu wakati Mtume [s] alivumilia aina nyingi za matatizo na misiba na kero kwa ajili ya kuitengeneza jamii na kuiongoza?

5. Iwapo kuswali makaburini ni haramu katika sheria ya Kiislamu, basi ni kwa nini Bibi Aisha aliishi umri wake wote huku akiswali katika nyumba yake ambayo ndani yake mna kaburi la Mtume [s]?

Kama tutakubali kwamba hadithi ifuatayo ni sahihi yaani Mtume amesema:

"Mwenyezi Mungu awalaani Mayahudi na Wakristo, wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni Misikiti".[104]

Basi maana yake ni kwamba wao walikuwa wakiwaabudu Mitume wao na wakisujudu juu ya makaburi ya Manabii hao au kuyafanya makaburi hayo kuwa ndiyo kibla yao.

Na mambo haya mawili ni kinyume cha sheria tukufu ya Kiislamu. Lakini Mawahabi huitumia hadithi hii kuharamisha kuswali kwenye makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu. Basi lau dalili ya hadithi hii ingekuwa sahihi, ni kwa nini basi Bibi Aisha ambaye ni mpokezi wa hadithi hii alimaliza karibu muda wa miaka hamsini ya umri wake akiswali na kufanya ibada ndani ya chumba ambacho amezikwa Mtume [s].

6. Lau kaburi la Mtume [s] lisingekuwa na heshima na utukufu, ni kwa nini basi Abubakar na Omar walikazania wazikwe karibu na kaburi la Mtume [s]?

Hivyo basi hadithi hii inauhusiano gani na mwenendo wa Waislamu unaoruhusu kuswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa kuelekea Qibla lakini karibu ya kaburi la Mtume [s] ili kupata ubora na thawabu nyingi?

7. Bibi Fatm az-Zah-Raa [a] alikuwa akizuru kaburi Ia Ammi yake Hamza kila siku ya ljumaa au kila wiki mara mbili, na alikuwa akilia na kuswali kwenye kaburi lake.

Al-Baihaqi anasema: Fatma [r.a.] alikuwa akilizuru kaburi la Ammi yake Hamza kila ljumaa na kisha huswali hapo na kulia."[105]

Bibi Fatma huyu ndiye yule ambaye zimepokelewa kwa Mtume hadithi sahihi zisemazo kwamba:

"Radhi ya Fatma ndiyo radhi ya Mwenyezi Mungu na mjumbe wake, na ghadhabu ya Fatma ndiyo ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na mjumbe wake."[106]

Ewe msomaji mpendwa, dalili zote hizi ukiongeza na mwenendo wa Waislamu wa kuswali na kuomba dua katika sehemu walizozikwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu, na wapenzi wake vinatia nguvu kuwa, kuswali na kuomba dua kwenye makaburi haya kuna thawabu nyingi na ubora mkubwa, na kwamba lengo ni kupata baraka zilizopo katika sehemu hizo na ni kutekeleza faradhi mahala hapo kwa kutaraji kukubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Lau tutakadiria kwamba hakuna dalili katika Qur'an na hadithi inayoonyesha ubora na heshima ya sehemu hizo na pia kwamba hakuna ubora wowote kuswali na kuomba dua mahala hapo, hata hivyo ni kwa nini iwe haramu kuswalia katika sehemu hizo?

Na ni kwa nini basi sehemu hizi haziingii ndani ya kanuni ya Kiislamu yenye kuenea, ambayo inaizingatia ardhi yote kuwa ni mahali pa kufanyia ibada ya Mwenyezi Mungu kama alivyosema Mtume [s]:

"Ardhi yote imefanywa kuwa ni msikiti na ni safi kwa ajili yangu."[107]

KUWASHA TAA MAKABURINI

Kuwasha taa kwenye makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu, jambo ambalo mawahabi wanadai kuwa ni haramu, halina umuhimu mkubwa kwa kuwa dalili pekee waitumiayo ni ile hadithi aliyoitaja An-Nasai kutoka kwa Ibn Abbas kwamba, "Mtume [s] amewalaani wanawake wanaozuru makaburi na wanaoyafanya kuwa ni misikiti na wale wanaayawasha taa".[108]

Hadithi hii na nyinginezo mfano wa hii zinahusika tu kama kuwasha taa huko kutakuwa ni kupoteza na kufuja mali au kutasababisha kujifananisha kwa baadhi ya nyumati na mataifa na dini batili, kama alivyolionyesha jambo hilo Al-Allamah as-Sindi katika sherehe ya hadithi hii aliposema:

"Na katazo hilo ni kwa kuwa (kuwasha taa) husababisha kupoteza mali bila manufaa".[109]

Ama kama lengo litakuwa ni kuwasha taa kwa ajili ya kusoma Qur'an, kuomba, kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, kuswali na mengineyo katika mambo mustahabbu na wajibu pamoja na manufaa yanayo kubalika kisheria, basi haya yote hayana matatizo kabisa,

"Saidianeni katika mema na uchamungu".

(Qur'an, 5:2).

Basi vipi itakuwa haramu?

Ilivyo ndivyo ni kwamba, kuwasha taa makaburini ni jambo mustahabbu kisheria na linapendeza kiakili.

[98] Ziyaratul-Qubur uk. 159-160.

[99] Qur'an. 18:21.

[100] Tafsiri Al-Kas-Shaaf anasema Az-Zamakhshari wakati akifasiri aya hizo: "Waislamu wanaswali katika Msikiti huo na kupata baraka za mahali hapo." Al-Nishapuri naye anasema hivi hivi: Waislamu wanaswali katika msikiti huo na kupata baraka za mahali hapo.

[101] Wafa-ul Wafai, juz. 4, uk. 1376

[102] Al-Khasaisul-Kubra cha As-Suyuti.

[103] Kitabu-Jalail-Af-Haami. Fis-salat Was-Salaam Ala Khairil-Anam cha Ibnul-Qayyim, uk. 228.

[104] Sunan An-Nasai, juz. 4, uk. 96. Chapa ya Beirut.

[105] 1. As-Sunan Lil-Baihaqi, juz. 4, uk. 78.2. Mustadrak As-Sahihain Lil-Hakim, juz. 1, uk 377.

[106] Sahihi Bukhari, juz. 5, Babu Manaqib Qarabat Rasulillahi uk. 21.

[107] Sahih Bukhari, juz. 1, uk. 91, Musnad ibn Hanbal, juz. 2, uk. 222 na vinginevyo.

[108] Sunan An-Nasai, juz. 3, uk. 77.

[109] As-Sunan An-Nasai. juz. 3, uk. 77, chapa ya Misri. Na juz. 4, uk. 95, chapa ya Beirut, Sharh Jamiu Saghir, juz. 2, uk. 198.