LENGO LA KITABU HIKI

Katika kitabu lilki tumejaribu kuchukua Masail ya msingi ambayo kuna hitilafu ndani yake baina ya Mawahabi na Madh-hebu mengine ya Kiislamu, na kuyatolea hukumu kwa mujibu wa Qur'an Tukufu na Sunna Tukufu ili tufahamu rai ya Uislamu katika Masail hayo.

Na kitabu hiki siyo pekee ambacho tulichoandika kuhusu maudhui hizi, bali kimetanguliwa na vitabu vitatu na kila kimoja miongoni mwa hivyo kimebeba jukumu Ia kuchunguza na kuhakiki baadhi ya Masail haya, na vitabu hivyo ni:

1. Mafahimul-Qur'an: Na ndani yake kuna uchunguzi mpana juu ya Tauhidi katika ibada ndani ya juzuu ya kwanza ya kitabu hicho kutoka ukurasa wa 378 hadi 528, nayo ni mkusanyiko wa mihadhara iliyotolewa katika hauza ya elmu katika mji mtakatifu wa Qum, na akaiandika kwa kalamu Sheikh Jaafar al-Hadi na ikachapishwa nchini Iran na Lebanon.

2. At-Tawasul-Bil-Auliya: Ni uchunguzi unaohusu kujuzu kutawassal kwa Maimamu watakatifu (Amani iwashukie) na kutawassal kwa Mawalii wema wa Mwenyezi Mungu, na mas-ala haya ni miongoni mwa mas-ala muhimu ambayo Mawahabi wanaeneza Shub-ha (Utata) juu yake.

3. At-Tauhid Wash-Shirki Fil-Qur'anil-Karimu: Kwa hakika (ndani ya Kitabu hiki) nimejaribu kujihusisha na Mas-ail ya Tauhidi na shirki, na nimelitatua tatizo hili ambalo limekishughulisha kikundi hiki cha Mawahabi kwa muda wote wa karne mbili na nusu, na kimechapishwa katika nchi nyingi za ulimwengu.

Na mihadhara hii (iliyomo kitabuni humu) ni uchunguzi wa mara ya nne ambao tunautoa kwa ulimwengu wa Kiislamu, na tunawaita Mawahabi walioko Riyadhi na katika Haram mbili Tukufu na waandishi walioajiriwa na Mawahabi ambao wanaandika kwa Maslahi yao, waikubali haki wala usiwadanganye upinzani wa kijinga na wazinyenyekee dalili, na iwapo hawatakubali isipokuwa (kuendelea na) uadui na kupinga haki, basi sisi tunawapa changa moto ya kukijibu kitabu hiki kwa jawabu madhubuti linalokubalika, linalotegemea mantiki na siyo (jibu la) udanganyifu na uzushi.

Na, Mawahabi wanalazimika kuwaacha huru Waislamu katika Haram mbili tukufu watende mambo yao matukufu ya dini, na wasiwakabili kwa uovu ndani ya Haram ya amani ya Mwenyezi Mungu na waache propaganda za Kiwahabi ambazo haziongezi chochote ndani ya Waislamu isipokuwa utengano, fitna na bughudha. "Bila shaka huu ni ukumbusho, basi yeyote atakaye na aishike njia kwenda kwa Mola wake".

Jaafar Subhani
Chuo cha Elimu - Qum Tukufu
26 / Mfunguo Mosi /1406 A.H.