MWITO WA KUFANYIKA KONGAMANO LA KIISLAMU

Kwa hakika ni muhimu sana kufanyika kongamano la Kiislamu ambalo ndani yake yatatatuliwa Masail yenye Khitilafu kwa mujibu wa muongozo wa kielimu na Mantiq na dalili, kwani wakati huu wa sasa ziko khitilafu kubwa mbili ambazo ni Uwahabi na madhehebu mengine ya Kiislamu juu ya Tauhidi na shirki, basi Je, kwa lengo la kukurubiana pande hizi mbili si inafaa kufanya mkutano wa kielimu ambao Masail haya yataaridhiwa katika meza ya uchunguzi na uhakiki kwa lengo Ia kuondoa batili na kuithibitisha haki, kwani huenda ikachomoza nuru ya kuonyesha njia kwa wanaobabaika?

Inabidi kongamano hili lifanyike kwa msingi wa kutatua tatizo na siyo propaganda tu, na lisichukuliwe kama vile ni jambo Ia propaganda ya Serikali fulani.

Na ili jambo hili lipate kukamilika kama inavyotakiwa, inapasa kuchunga sharti zifuatazo:

1. Mwito huo utolewe kwa wanafikra wa Kiislamu kutoka katika Madhehebu mbali mbali za Kiislamu ambao wanawakilisha Madhehebu hayo na wanafahamika khasa kuwa wao ni wanachuoni na ni wafikra wa dhehebu hilo (wanaloliwakilisha), na wasipelekewe mwito huu wanachuoni wa Pilato wa Saudia peke yao ambao wanapatikana India, Pakistani na Misri iliyodhulumiwa.

2. Na zaidi ya wawakilishi wa Madhehebu manne, ni lazima mwito huu utolewe kwa wanachuoni na wanafikra wa Shia Ithna-Asheriyyah na dhehebu la Zaydiyyah ili mkutano huo unenekane kwa muono wa pamoja na ujumla wa Waislamu wote.

3. Ni lazima utolewe uhuru kamili kwa wajumbe wa mkutano ili kila mmoja miongoni mwao aweze kujadili juu ya Masail yatakayokuwa yamearidhiwa kwenye uwanja (wa majadiliano), na awe na haki ya kuzitetea kwa uhuru fikra zake na itikadi zake, pia kongamano hilo lijiepushe na kila kitu kinachoharibu heshima ya wajumbe wake, miongoni mwa maneno ya matusi na dharau ambayo leo hii yameenea katika miji ya Saudia.

4. Na ni lazima idara inayoendesha kongamano isifungamane na upande wowote, na bora zaidi iwe imeundwa kutokana na Madh-hebu tofauti tofauti yanayoshiriki kwenye kongamano.

5. Utafiti wote unaofanyika kwenye kongamano usambazwe (kama ulivyo) bila ya mabadiliko yoyote ndani yake na utumwe kwenye vituo (vyuo) vya Elimu ulimwenguni ili wanaopenda kujua matokeo ya kongamano hilo wausome. Aina hii ya kongamano na kwa kuchunga sharti hizi, tunataraji Masail mengi mbali mbali yatatatuliwa, na kile kiini cha mafahamiano kitathibitika na maelewano baina ya Waislamu yatapatikana.