TUKIO LA KARATASI

Waandishi wa tarikh na Hadithi wamelieleza tukio la Karatasi kama hivi:

"Mtume (s.a.w.) alipokuwa mgonjwa mahtuti, watu wengi walikusanyika ndani ya nyumba ya Mtume akiwamo Umar Ibn Khattab. Mtume (s.a.w.) aliwaambia kuwa: "Nileteeni Karatasi niwaandikieni maandiko hamtapotea baada yake." Umar akasema: Mtume anaweweseka! Mtume akawaambia: "Niondokeeni" wakaondoka.

Katika kauli nyingine inasema: Umar alimwambia Mtume baada ya kuagiza karatasi: "Mtume yamemzidi maradhi inakutosheni Quran mliyo nayo".

Kauli ya kwanza na ya pili utazipata katika:

Sahih Bukhar Kitabul Ilmi
Sahih Bukhar Kitabul Tibb
Sahih Bukhar Kitabun Nabi ila Kisra
Sahih Bukhar Babu Karahiyatul Khilaf
Sahih Bukhar Babu Jawaizil wafdi
Sahih Muslim Babu Tarikil Wasia
Tarikhut Tabari J.2 Uk. 436
Sharhush Shifaa J.2 Uk. 353

Mwenyezi Mungu anasema: "Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake) hayakuwa haya ila ni Wahyi uliofunuliwa." 53:3-4

Amesema Abdallah bin Amri: "Nilikuwa nikiandika kila kitu ninachokisikia kwa Mtume Muhammad (s.a.w.) ili nikihifadhi, Makuraishi wakanikataza wakanambia: Wewe unaandika kila kitu unachokisikia kwa Mtume!? Na Mtume ni binadamu, anazungumza (wakati mwingine) katika hali ya ghadhabu. Basi nikajizuia kuandika, nikamjulisha hayo Mtume (s.a.w.). Akasema Mtume, "Andika, na muape ambae nafsi yangu imo katika milki yake, mimi sisemi isipokuwa haki tupu".

Taz: Tafsir Ibni Kathir J.4 Uk. 264
Tafsir Maraghi J.27 Uk. 45

Somo hili linatufundisha kuwa: Wakati wote Mtume (s.a.w.) anaposema, huwa ni Wahyi. Sawa sawa awe katika furaha kubwa au katika ghadhabu, na awe katika maradhi au afya.

Sasa: kwa nini Umar kuzuia usiandikwe Wahyi na nini hukumu ya mtu kama huyu?

Sikiliza, Mwenyezi Mungu anasema: "Atakaempinga Mtume baada ya kudhihirikiwa muongozo, na kufuata njia isiyokuwa ya waumini, tutamgeuza alikogeukia mwenyewe, na tutamwingiza katika moto wa Jahannamu." 4:115.