UIMAM

Msimamo wa Aya zilizokuja juu ya uongozi ukisoma yalioandikwa katika vitabu mbali mbali na Hadithi zilizothibiti, na tarikh inayoonyesha katika jambo hili, utapata mambo makuu matatu ambayo yanaonyesha kuwa: Uimam/Ukhalifa lazima uteuliwe na Mwenyezi Mungu. Na kwa upande wa pili utaona kuwa Nyimati zilizopita zilifuata uongozi uliochaguliwa na Mwenyezi Mungu, wala jambo hilo halikuachiwa watu wenyewe kwa njia ya kuchaguwana.

Jambo la kwanza lililoongoza baina ya Mtume waliopita ilikuwa ni kusalimu amri na kufuata uongozi wa Mwenyezi Mungu, na kila alipoondoka Mtume aliweka atakaeshika nafasi yake.

Wengi wao waliorithi kazi zoa walikuwa Manabii, hata hivyo baadhi yao hawakuwa Manabii bali walikuwa Mawasii tu.

Jambo la pili: Uongozi katika nyimati zilizopita ulipatikana kwa njia ya kurithi baina ya vizazi katika koo za Mitume kama tunavyosoma katika Aya zifuatazo:

  1. "Hakika Mwenyezi Mungu alimchagua Adam na Nuh na Kizazi cha Ibrahim na Kizazi cha Imrani juu ya walimwengu wote. Ni kizazi cha wao kwa wao, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua" 3:33-34
  2. "Na tulimpa Isihaqa na Yaaquubu na tukaweka katika Kizazi chake Unabii na Kitabu , na tukampa ujira wake katika dunia. Nae katika akhera kwa hakika atakuwa miongoni mwa watu wema." 29:27
  3. "Na hakika tulimpeleka Nuhu na Ibrahim na tukauweka katika kizazi chao Unabii na kitabu." 57:26
  4. Mwenyezi Mungu alimweka Ibrahim kuwa Imam (Kiongozi wa watu). Ibrahim alimuomba Mola wake awape nafasi hiyo vile vile katika kizazi chake. Mwenyezi Mungu hakumkemea wala kumgombeza, ila alimwambia ya kuwa: "Haiwafakii ahadi yangu (Unabii and Uimam) watu madhalimu." 2:124

Nabii Musa (a.s.) alipoomba kwa Mwenyezi Mungu ndugu yake Haruna awe msaidizi wake katika uongozi, Mwenyezi Mungu hakumkasirikia wala kumkatalia ombi hilo.

"Na unijaalie waziri katika jamaa zangu, Haruna ndugu yangu. Uniimarishe kwake nguvu zangu, na umshirikishe katika kazi yangu. Ili tukutukuze sana, na tukutaje kwa wingi. Hakika wewe unatuona, akasema hakika umepewa maombi yako ewe Musa" 20:29-36. Musa alimweka Haruna kuwa Khalifa wake alipoondoka, kama Quran inavyosema:

"Na tulimwahidi Musa siku thelathini na tukatimiza kwa kumi ikatimia miadi ya Mola wake siku arobaini. Na Musa akamwambia ndugu yake Haruna: Shika mahala pangu katika watu wangu na usuluhishe wala usifuate njia ya waharibifu." 7:142

Katika Aya hizi tumeona nafasi ya Uongozi unavyoendelea kati ya Kizazi na Kizazi baina ya koo za Manabii.

Mtiririko huu ikiwa umejengeka kwa Wahyi katika nyimati zilizopita katika suala la Khilafa, basi kubadili utaratibu huo katika Islam lazima ipatikane dalili na ufafanuzi.

Jambo la tatu: Kumbukumbu za tarikh ya Mitume inaonyesha waziwazi kuwa: Kila alipoondoka Mtume aliweka mtu wa kushika mahala pake, na hapa tutaonyesha kwa ufupi:

Wakati iliposhuka Aya 214 katika Sura ya Ash'Shuaraa, Mtukufu

Mtume (s.a.w.) alisema:

"Enyi Bani Abdil Muttalib! Hakika mimi wallahi simjui kijana yeyote katika Waarabu, aliyewaletea watu jambo bora kabisa kuliko nililokuleteeni mimi. Hakika mimi nimekuleteeni kheri ya dunia na ya akhera, Mwenyezi Mungu ameniamrisha nikuiteni kwake, basi nani kati yenu atakaenisaidia jambo hili ili awe ndugu yangu na wasii wangu na Khalifa wangu kwenu?

Watu wote wakanyamaza, nikasema (Ali) na mimi ni mdogo wao kwa umri mng'avu wao wa macho, mkubwa wao wa tumbo, mnene wa miundi, mimi ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu nitakuwa waziri wako. Pale pale akanishika shingo yangu, kisha akasema: Hakika huyu ni ndugu yangu, na wasii wangu, na Khalifa wangu kwenu, basi msikilizeni na mtiini".

Akili, na maandiko, pamoja na matukio ya tarikh, vyote vinaonyesha kwa pamoja kuwa: Msingi wa asili katika hukumu ni maamuzi ya Mwenyezi Mungu tu peke yake, na yeye ndiye anayemtawalisha amtakae katika waja wake.

Tukio la Ghadir Khum ni tangazo muhimu Ia uongozi mkuu, lililokamilisha dini na neema na radhi ya Mola. Tarehe kumi na nane mfungo tatu Mtukufu Mtume (s.a.w.) alipokuwa akirejea Madina kutoka Makka katika mwaka wa kumi baada ya kumaliza ibada ya Hija alifika mahali katika bonde la Khum akiwa na Waislam zaidi ya laki moja. Mwenyezi Mungu akateremsha Aya: "Ewe Mjumbe fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hutafanya, basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu, hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu wanaokufuru" 5:67

Baada ya kushuka Aya hii, Mtume (s.a.w.) alimshika mkono Imam Ali (a.s.) akasema:- "Ambaye mimi natawalia mambo yake, basi huyu Ali ni mtawala wake. Ee Mola! Muunge atakae muunga, na mfanyie uadui atakae mfanyia uadui".

Ilipokamilika hutuba ya Mtume (s.a.w.) Masahaba walianza kutoa kiapo cha utiifu kwa Imam Ali (a.s.) kama tunavyomnukuu hapa Umar bin Khattab:- "Hongera ewe mwana wa Abu Twalib sasa umekuwa kiongozi wangu na kiongozi wa Waislamu wote".

Taz; Tarikhu Dhahbi J.2 Uk. 197
Tariku Baghdad J.8 Uk. 290
Tarikhu Ibn Asakir J.2 Uk. 45
Al Isaba J.1 Uk. 305
Tafsirul Kabir J.12 Uk. 49
Addurrul Manthur J.5 Uk. 182
Ansabul Ashraf J.2 Uk. 315
Albidayatu Wannihaya J.7 Uk. 359

Hata hivyo, wako baadhi ya Masahaba waliopinga kitendo hiki cha kutoa kiapo cha utiifu kwa Imam Ali (a.s.)

Baada ya Masahaba kutoa kiapo cha utiifu kwa Imam Ali (a.s.) Harithi bin Nuuman Al'fahri, alimkabili Mtume (s.a.w.) akamwambia: Ewe Muhammad! umetuamrisha kushuhudia kuwa hapana apasae kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu na wewe ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, tumekubali. Umetuamrisha kusali mara tano kila siku, tumekubali. Umetuamrisha kutoazaka katika mali yetu, tumekubali. Umetuamrisha kufunga mwezi wa Ramadhani kila mwaka, tumekubali. Umetuamrisha Kuhiji AI'kaaba, tumekubali.

Kisha hukutosheka yote haya mpaka umempandisha mtoto wa ammi yako juu ya shingo zetu! Hili ni wazo lako au ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu?" Mtume (s.a.w.) akajibu:- "Wallahi, hapana apasae kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu, hili si langu isipokuwa ni Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu". Harithi akaondoka zake na huku akisema: "Ee Mola! ikiwa haya anayosema Muhammad ni kweli, basi tuteremshie mvua ya mawe au tuletee adhabu nyingine kali". Naam, pale pale alipokuwa, Mwenyezi Mungu akamdondoshea kijiwe kikagonga utosini kikatokezea kwenye tundu ya nyuma akafa papo hapo.

Mwenyezi Mungu akateremsha Aya ya kwanza na ya pili katika Suratul Ma'ariji: "Muombaji aliomba juu ya adhabu itakayotokea, kwa makafiri hapana awezae kuzuia"

Taz: Tafsirul Qurtubi J.18 Uk. 278

Tukio la Ghadir Khum ni ujumbe muhimu sana kwa Waislamu, na kila anayeshuhudia: "LAA ILAHA ILLA LLAHU MUHAMMADUN RASULULLAH"

Lazima vile vile atoe kiapo cha utiifu kwa uongozi wa Ahlul Bait (a.s.). Kwa sababu tarikh inaonyesha kuwa Masahaba waliokataa kutoa kiapo chao kwa Imam Ali, Mwenyezi Mungu aliwaadhibu. Katika hao walioadhibiwa ni huyu Harithi bin Nuumani Al'fahri, kama ulivyoona kisa chake hapo juu. Pia tarikh inaonyesha kuwa Sahaba Zaid bin Ar'qam alipotengua kiapo chake cha utiifu kwa Ahlul Bait, alipofuka macho yake mara moja.

Taz: Manaqibul Imam Ali Uk. 23