VIBARAKA WA BANI UMAYYA

Lile agizo la Muawia kupitia kwa magavana wake ya kuwa: "Wasiache kumtukana Ali na kumkashifu, na kumhurumia Uthman na kumuombea msamaha, na kuwatia aibu watu wa Ali na kuwatenga mbali......."

Agizo hilo limefika mbali sana na sumu yake inaendelea mpaka leo hii.

Hapa tutataja baadhi ya Makada wa Muawia ambao wako katika mstari wa mbele wa usimamiaji wa siasa hiyo.

(1) ABU HURAIRA

Haijapata kutokea katika zama za Ujahili, au hata katika zama za Uislam, kuwa mtu ye yote ametiliwa shaka kujua jina lake na jima la baba yake isipokuwa Abu Huraira.

Wamekhitilafiana jina la baba yake na jina lake kwa kauli thelathini.

Taz: Al'Isaba J. 7 Uk. 199
Usudul Ghaba J.5 Uk. 315

Abu Huraira anasema: "Hatukuweza kusema chochote juu ya Hadithi za Mtume mpaka alipokufa Umar lbn Khattab, tukiogopa bakora".

Taz: Al'bidayatu Wannihaya J.8 Uk. 210

Sayyid Muhammad Rashid Ridha amesema: "Laiti Umar angebakia mpaka kufa Abu Huraira, zisingetufikia Hadithi nyingi namna hii".

Abu Huraira anasema: "Laiti nitakusimulieni Hadithi za Mtume nilizonazo Wallah mtanipiga mawe"

"Laiti nitakuelezeni ninayoyajua, Wallahi watu watanitukana waseme Abu Huraira mwenda wazimu".

"Hakika Mwenyezi Mungu ameamini katika Wahyi wake watatu:

Jibril, Mtume Muhammad na Muawiya".

Taz: Mustadrakul Hakim J.3 Uk 509
Tabaqatul Kubra J.4 Uk. 7
Shaikhul Mudhira Uk. 230

Abu Huraira ameifanyia marekebisho Aya ya 214 katika Sura ya 26. Iliposhuka Aya hii kama inavyoonyesha Tarikh Mtume (s.a.w.) alitoa tamko: Hakika huyu (Ali) ni ndugu yangu na wasii wangu na Khalifa wangu kwenu, basi msikilizeni na mumtii".

Tazama vitabu vya Tarikh na vitabu vya Tafsiri utayaona. Lakini kwa bahati mbaya sana, Abu Huraira ameikata Hadithi hii akaondoa na kupachika maneno yake, kama hivi: Enyi Makuraishi! Mimi sitakufaeni chochote kwa Mwenyezi Mungu, enyi kizazi cha Abdul Manaf mimi sitakufaeni cho chote kwa Mwenyezi Munge, ewe mwanangu Fatima, niombe unachotaka katika mali yangu, mimi sitakufaa cho chote kwa Mwenyezi Mungu".

Taz: Sahih Bukhari J. 4 Uk. 7

La ajabu zaidi mbali ya kuzua uongo huu, Aya hii imeshuka katika mwaka wa tatu wa Utume, wakati huo Abu Huraira ni kafiri yuko Yemeni hana habari na Uislamu.

Vile vile Tarikh inaonyesha kuwa: Wakati ikishuka Aya hii, ilikuwa ni mwaka wa tatu wa kupewa Utume Mtume Muhammad (s.a.w.), wakati ambao Mwana Fatima bint Muhammad hajazaliwa bado!! Kwa sababu Tarikh inaonyesha kuwa: Mwana Fatima (a.s.) amezaliwa mwaka wa tano baada ya kupewa Utume Mtume Muhammad (s.a.w.).

Kwa hiyo Abu Huraira siyo mwongo tu, bali ni mwendawazimu kama asemavyo mwenyewe.

Ndiyo maana unaweza kuona baadhi ya vitabu vya Tafsir au vya Tarikh ikifikia kutajwa madhumuni ya tukio hili huandikwa: "Hakika huyu ni ndugu yangu na kadha wa kadha, basi msikilizeni na mumtii"

(2) IBN KATHIR

Jina lake ni: Ismail bin Umar bin Kathir Addamashqi.

Amesema: "Ama yale wanayohadaika nayo wajinga wengi wa Kishia na watoa visa wapumbavu, yakuwa Ali ameusiwa Ukhalifa, ni uongo.........."

Taz: Al'bidayatu Wannihaya J.7 Uk. 226

Wajinga na wapumbavu, watoa visa vya uongo, kuwa Ali ni wasii na khalifa wa Mtume (s.a.w.) ni hawa:

(a) Imam Ali bin Abii Talib (a.s.)

b) Abu Ayyub Al'Ansar (a.s.)

(c) Abu Said Al'khudury (a.s.)

(d) Abu Dharri Al'ghifari (a.s.)

Na wengine wengi katika Masahaba wakubwa wa Mtume (s.a.w.).

Je! Masahaba hawa tuliowataja hapa ni wapumbavu, wajinga wenye kutoa visa vya uongo.

(3) IBNI HAZMI

Jina lake ni: Abu Muhammad Ali bin Ahmad bin Said bin Hazmi. Amesema: "Hakuna hitilafu kwa ye yote katika umma kuwa, Abdur Rahman bin Muljam hakumuua Ali ila alifanya jitihada akidhani anafanya sawa, na ndiyo maana Imran bin Hattan amesema: Ewe dharba ya mcha Mungu, hakuikusudia ila apate radhi ya Mwenyezi Mungu. Mimi naikumbuka siku hiyo, basi najua atapata malipo makubwa kwa Mwenyezi Mungu"

Taz: Al'MuhalIa J. 10 Uk. 484

Ibn Hazmi anasema: Abul'A'dia Yasir bin Sab'i Assalmi (aliyemuua Ammar bin Yasir) ni mtu aliyejitahidi akakosea, atapata malipo ya kujitahidi. Lakini huyu si sawa na waliomuua Uthman, kwa sababu watu hao hawana nafasi ya kujitahidi kumuua".

Taz: Al'Fisal J. 4 Uk. 161

(4) IBN TAYMIYYA

Jina lake ni: Abul Abbas Ahmad bin Abdul Halim bin Abdus Salami bin Abdullah Muhammad bin Alkhudhar bin Muhammad bin Alkhudhar bin Ali bin Abdullah bin Taymiyya.

Amesema: "Mambo mengi yaliyofanywa na Masahaba wakubwa yanasamehewa, na mahala pake huwekwa katika nafasi ya "JITIHADA" ambayo mwenye kupata hulipwa thawabu mbili na mwenye kukosa hulipwa thawabu moja.

Taz: Minhaj Sunna J. 3 Uk. 19/261

(5) IBN HAJAR

Jina lake ni: AInnad ibn Muhammad bin Muhammad bin Ali bin Mahmuud bin Ahmad bin Ahmad bin Al'Asqalan.

Amesema: "Wamekhitilafiana kusema: Alayhis salamu kumwambia mtu mwingine asiyekuwa Mtume (s.a.w.). Ingawa wamekubaliana kuwa ni sharia kwa Mwislamu kumsalimu; Assalamu Alaykum. Kwa kuwa jambo hili linatumiwa sana na Mashia, vyema sasa kuliacha, bali kuacha ni sunna na kulitumia ni bid'a.

Taz: Fat'hul Bari J. 11 Uk. 142

(6) AL'GHAZALY

Jina lake ni: Abu Hamid Muhammad bin Muhammad bin Muhammad Al'ghazaly. Amesema "Inakatazwa kwa kiongozi wa dini na mwingine yeyote kusoma matukio ya mauwaji ya Husein na kuyasimulia. (Haifai kutajwa) yaliyopita kati ya Masahaba, na kuwakosoa makosa yao kwa sababu wao ni viongozi wa dini na yaliyotokea kati yao huchukuliwa kwa nia nzuri, na pengine hayo yametendeka kwa makosa katika kujitahidi na wala si kwa kutaka ukubwa.

Taz: Ruhul Bayan J. 4 Uk. 142

Hawa ni baadhi ya Makada wachache wa Muawia, ambao wake katika mstari wa kwanza kufuta - ikiwezekana - athari za Ahlul Bait (a.s.).