MWANDISHI WA KITABU HIKI

Jina langu ni OMAR JUMAA MAYUNGA. Nimezaliwa mwaka 1947 Mkoa wa Tabora katika Wilaya ya Igunga Tarafa ya Simbo.

Mwaka 1957 baba yangu alianza kunisomesha Quran Tukufu, ilipofika mwaka 1959 nilianza masomo ya Kizungu katika Shule ya Msingi ya Simbo hadi mwaka 1962 nilipokaa nyumbani kuendelea na masomo ya Qur'an.

Mwaka 1968 baba yangu alinipeleka mjini Tabora kusoma kwa Sheikh Mzee Fereji Farahani (Mwenyezi Mungu amrehemu) mpaka mwaka 1972 nilipokwenda Mombasa kujiunga na Madrasa ya Tahdhib Muslim School ambayo iliongozwa na Almarhum Al'ustadh Alwy Qasim. Kwa kipindi nilichosoma katika Madrasa hii, siwezi kusahau ukarimu niliopata nikiwa ugenini. Kwanza kabisa Sheikh Muhamad Amran Bushir, ambaye yeye ndiye aliyenipokea kwa mara ya kwanza nyumbani kwake. Akanikirimu kwa ukarimu mkubwa, akanifanyia mambo yote na watoto wake. Pili; Ustadh AIwy Qasimu aliyenipenda sana, akanisomesha kwa juhudi kubwa. Ustadh Alwy alinipatia vitabu vingi mbali mbali na akanisomesha kwa undani zaidi vitabu vya ibn Taymiyya, Ibn Qayyim Aljawziyya, na vya Muhammad Abdulwahabi. Tatu; Maulamaa Sheikh Abdallah Saleh Alfarsy na Sheikh Muhammad Kasim Mazrui, ambao walikuwa machifu Kadhi wa Kenya. Kila mmoja alinisaidia sana kunipa maarifa na mwongozo mwema. Nilibaki katika Madrasa hii mpaka alipofariki Ustadh kwa ajali ya gari.

Mwaka 1975 nilikwenda kusoma Ujiji - Kigoma, kwa Sheikh Khalfani Muhammad Kiumbe hadi 1976.

Nikiwa Ujiji, Almarhum Mzee Husein Taufik Msanga alinihudumia kwakunipa kila masaada kwa muda wote nilioutumia katika masomo.

Mwaka 1976 nilikwenda kusoma Iringa kwa Sheikh Harith Khelef Khamis. Sheikh Harith kwa mapenzi yake makubwa juu yangu alinisomesha masomo mengi yenye maana sana. Nikiwa Iringa. Al'marhum Mzee Hasan Souf Imam wa Msikiti Mkuu wa Iringa, alinipokea akanipa chumba.

Nilipata miada mingi mbalimbali kwa; Mzee Ali Fundi, Mzee Muhammad Bunnu, Mzee Muhammad Mbarak. Mpenzi wa roho yangu niliyeshikamana naye wakati mwingi, Al-haji Saburi Goha Momba ambave hatimaye alinioza binti yake.

Mwaka 1978 niliajiriwa katika Chuo cha Kiislamu- Chang'ombe, Dar es Salaam.

Mwaka 1980 Sheikh Abdallah Idd Chaurembo (Mwenyezi Mungu amrehemu) alinitaka niasisi "Madrasatu Ahli Sunnatu Waljamah" katika Msikiti wa Mtoro. Nilisomesha miezi mitatu nikaandika barua ya kujiuzulu ya tarehe 2J.5.1980 kwa nia ya kuasisi Madrasa yangu binafsi.

Mwaka 1982 niliandika kitabu: "Jawabu la wazi kwa wateteao bid'a" kilichochapishwa Dar es Salaam tarehe 27.1J.1982. Kitabu hiki kilitetea msimamo wa Kiwahabi, na kabla ya hapo niliandika Makala mbali mbali kwa mujibu wa matukio yaliyotokea kati yangu na baadhi ya Masheikh. Aidha mwaka 1982 nilikwenda mara nyingi Bujumbura, huko nilitoa mihadhara mingi mikubwa katika Msikiti wa Bwiza.

Mihadhara hiyo niliielekeza Bujumbura tokea mwaka 1982 hadi 1985. Kisha nilielekeza mihadhara hiyo mjini Lusaka - Zambia. Mwaka 1985 vile vile nilikwenda Saudi Arabia katika Ofisi ya Muslim World League mara tatu, kwa lengo la kupanua mawasiliano baina ya Madrasa yangu na taasisi mbali mbali za Kimataifa.

Mwaka 1986 nilikwenda Mombasa - Kenya huko nilikutana na Sheikh Abdillah Nasir: Nilipata nafasi ya kuzungumza naye mambo mengi kuhusu msimamo wa dini. Jambo lililojitokeza zaidi katika mazungumzo yetu ni Usunni na Ushia, na ilipohitajika kupata vitabu vya Kishia ndipo aliponikutanisha na Sheikh Ali Muhammad Jaafar, Kiongozi wa Bilal Muslim Mission ya Kenya. Naye alinipatia vitabu "Aslus Shia wausuluha, Al-murajaatu, Fadhailu Lkhamsa."

Niliporudi Dar es Salaam nilivisoma kwa makini na kufuatilia vitabu vya Kisunni vilivyoonyeshwa humo. Na nilikuwa karibu sana na Mwanachuo wa Kishia hapa Dar es Salaam Maulana Sayyid Saeed Akthar Rizvi. Nilikuwa na nukta kadhaa zilizonikera dhidi ya Shia, kwa hivyo nilimuomba Maulana Rizvi anipatie wakati wa kutosha ili tuzijadili hizo nukta. Mbali na shughuli zake nyingi alizokuwa nazo, Maulana alinipatia siku mbili kwa wiki.

Baadhi ya nukta tulizozichambua ni:- Tahriful Qur'an, Imamah, Taqiyya, na Mut'a. Sayyid Saeed Akthar Rizvi mbali na kunijibu nukta hizi, lakini pia amenifundisha na kunionyesha mengi sana yaliyomo katika vitabu vya Kisunni. Kisha alinipa kitabu "AIghadir" akaninyesha yaliyomo humo, na Kisha tulifuatilia baadhi ya nukta zilizotajwa katika "Aighadir" kwa vitabu vya Kisunni. Kwa utafiti huu wa pamoja katika vitabu vya kutegemeka vya Kisunni, ambavyo ndivyo vimenifanya kuwa Shia lthnaasheri. Baadhi ya vitabu hivyo ni:- Sahihi Bukhari, Sahihi Muslim, Tarikhut Tabari, Tarikh Ibn Athir, Mizanul Itidal na Tafsir nyingi za Quran, nimeamua kuwa:- "Mimi ni Shia Ithna-asheri, nitafuata sheria na kanuni zake katika uhai wangu na baadaye Insha-Allah".

Tarehe J.9.1986 nilialikwa na Bilal Muslim Mission ya Kenya, katika Majlis ya kukumbuka mauaji ya Imam Husein (a.s.).

Tarehe 8.9.1986 mimi nilisoma Majlis katika ukumbi wa Huseiniyya Mombasa. Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kupanda katika Mimbari na kusoma habari za watukufu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.).

Tarehe 20.1J.1987 nilialikwa kuhudhuria Mkutano mjini Tehran-Iran, mkutano ambao ulizungumzia mauaji ya kinyama walio fanyiwa ndugu zetu Mahujaji na askari wa Kisaudi katika Haram ya Makka. Katika Mkutano huo mimi nilipata nafasi ya kuhutubia kwa kulaani kitendo cha kinyama cha mauaji ambayo askari wa Kisaudi waliwauwa Mahujaji wasio na hatia.

Mwaka 1987 nilifasiri Dua Kumayl kilichochapishwa Mombasa - Kenya Mwaka 1989, Tarehe 24.10.1989 niliandika kitabu:- "Mut'a ndoa sahihi" kilichochapishwa Dar es Salaam tarehe 8.3.1990.

Tarehe 8.7.1990 nilialikwa kuhudhuria sherehe ya Imam Ali (a.s.) mjini London. Sherehe ambayo mwaka 1410 Hijiria ilikuwa inatimia karne kumi na nne tokea Imam Ali (a.s.) atangazwe na mtume (s.a.w.) hadharani katika bonde la Khum. Nilibahatika kuchaguliwa na kamati ya maandalizi ya Mkutano huu kuwa mmoja wa watakaohutubia katika hafla hii.

Tarehe 13.7.1990 katika majira ya jioni, nilihutubia katika ukumbi wa Hotel ya Ramada mjini London. Katika hafla hii kuna zawadi maalum ilitengwa kwa ajili ya wale watakaofanya vizuri.

Mimi nilibahatika kutunikiwa saa yaa mkono yenye nembo ya ujumbe maalum wa lile agizo la Mtume (s.a.w.) juu ya Imam Ali (a.s) siku ya Ghadir Khum, kuwa yeye Imam Ali (a.s.) ni Kiongozi wa Waumini baada yake aliposema:

"Ambaye mimi ni kiongozi wake, basi huyu Ali ni kiongozi wake".